Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Edward Olelekaita Kisau (2 total)

MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Nakushukuru, kwa kuwa swali lililoulizwa linafanana kabisa na matatizo na changamoto tunayopata kama Wilaya ya Kiteto, hususan Hospitali ya Wilaya, tuna upungufu wa mashine ya x-ray, jenereta ni mbovu, majengo, gari la kubeba wagonjwa, vitanda na mashine ya usingizi. Ni lini sasa Serikali itapeleka vifaa hivi katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Kiteto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya utoaji wa huduma za afya yakiwemo majengo, vifaatiba, x-ray, ultra sound na vifaa tiba vingine ni vifaa ambavyo vimepewa kipaumbele katika vituo vyetu vya huduma ili kuweza kufikisha huduma bora kwa wananchi na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimeeleza jinsi ambavyo Serikali imetenga fedha kiasi cha takribani bilioni 33.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali zetu 67 za Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali ni kuhakikisha tunaendelea kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba katika vituo vyetu vyote ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Kiteto.
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, nini kauli ya Serikali kwa vijana waliomaliza mafunzo ya JKT na wameshiriki katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa nchi yetu lakini sasa wamerudi nyumbani bila ajira?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ni mara kadhaa amekuja tumezungumza juu ya hatma ya vijana na inaonyesha namna anavyowajali vijana wake. Kwa hiyo, nampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema nafasi hizi za mafunzo ya vijana wetu zina nia nzuri, kwanza ya kuwafanya vijana ambao tunawafundisha kuwaunda ili kuwa na umoja wa kitaifa. Hiyo haipingiki kwa sababu tunavyokuwa tunawafundisha kule hatuna siasa, hatuna maneno mengi, tunawaunda wakae vizuri. Pia tunawaunda kuwa viongozi, wanaweza kuwa viongozi kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uongozi katika biashara na mambo mbalimbali ya ujasiriamali. Pia tunawafundisha kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na ubunifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa vijana ambao wamepata nafasi ya kupata mafunzo haya pamoja na kupata stadi za kazi, tunawaandaa hawa vijana kwenda kujitegemea. Pia upande wa Serikali ziko fursa kadhaa ambazo Waheshimiwa Wabunge tunazifahamu ni za kuwafanya vijana hawa waweze kuchangamkia fursa ambazo zipo kwa maana ya kupata mitaji na kadhalika. Mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge tukiwaunganisha hawa vijana kwa skill ambazo wamezipata katika mafunzo yetu tutawafanya waweze kujitegemea na kutoa mchango mkubwa sana kwenye taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe Wabunge pale ambapo vijana wetu hawana taarifa hizi za fursa ambazo Wabunge tunazifahamu, tutumie nafasi hiyo kuwaunganisha vijana hawa, wawe kwenye makundi au binafsi ili Serikali iweze kuwasaidia vijana hawa na lengo ambalo limewekwa kwa ajili ya kuwasaidia vijana wetu liweze kutimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumejipanga vizuri na Waheshimiwa Wabunge niwakaribishe pale ambapo labda wanaweza wasiwe na uelewa wa kutosha niko tayari kuwaweka vizuri ili tuweze kuwasaidia vijana wetu kadri tutakavyokuwa tumejipanga. Ahsante sana.