Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Soud Mohammed Jumah (1 total)

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Ahsante sana Mheshimiwa Spika kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu kwamba mifuko hii ya Adaptation Fund pamoja ile ya LDCF yaani Least Developed Country Fund hutengewa fedha maalum na Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi kupitia hii mifuko na fedha hizi hutakiwa zitumike katika muda maalum na ni fungu maalum, na kutokana na utaratibu ambao unaendelea katika Serikali au katika Wizara zetu imekuwa ikichukua muda mrefu sana kutayarisha maandiko na kuweza kuyawasilisha na mpaka kupata hizi fedha.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba, fedha hizi ambazo zinakuwa zinatengwa kwa ajili ya Tanzania zinaombwa kwa haraka na kuweza kupatikana katika muda muafaka ili kupunguza hatari ya kuweza kuja kuzikosa hizi fedha au kuzipoteza?

Mheshimiwa Spika, swali namba mbili, je, kuna utaratibu gani wa uwiano wa fedha hizi kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS,
MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, kumekuwa na, kwa namna moja au nyingine ucheleweshaji wa fedha hizi, lakini tunaendelea kuimarisha utaratibu wa mawasiliano. Fedha hizi kwanza lazima mradi uandikwe, lakini vilevile tunashiriki na wenzetu wa Wizara ya Fedha ambao wana taratibu zao, tunahitaji tax exemption katika jambo hili. Kwa hiyo, lazima wataalam wetu wapitie kwanza halafu kisha wamshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha namna bora ya kuweza kuruhusu mradi uweze kuendelea. Wakati mwingine unalazimika kwenda site, hiyo ndio inasababisha muda unakuwa mrefu kidogo, lakini tunaahidi mbele ya Bunge lako tukufu kwamba tutachukua hatua za haraka na miradi hii itakuwa haichukui muda mwingi sana kutekelezwa, ili tuweze kupata fedha hizo ambazo ni manufaa makubwa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili ambacho Mheshimiwa Mbunge anataka kujua ni kwamba kuna uwiano. Hii miradi kama nilivyotaja katika miradi mitano mradi ukiibuliwa kule upande wa Zanzibar kiasi hicho cha fedha mradi utatekelezwa fedha zinapelekwa bila kuwa na mgawo, kwa hiyo, hapa kazi kubwa ni kujiimarisha, kuandaa watu wetu, wataalam wetu, waandae maandiko ya kutosha fedha zinapatikana. Sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais ni ku- facilitate na kuratibu mambo haya yaweze kufanyika kwa haraka zaidi. Ahsante sana.