Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Geophrey Mizengo Pinda (2 total)

MHE. ZAINAB A. KATIMBA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha baadhi ya Sheria kandamizi kwa Wanawake ili ziendane na wakati?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu nasimama mbele ya Bunge lako kwa mara ya kwanza. Pia niwashukuru wananchi wa Kavuu kwa kunidhinisha kuwa Mbunge wao. Vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniona nafaa kuwakilisha Wizara hii ya Katiba na Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Mkoa wa Kigoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kabla ya kujibu swali la msingi, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa Serikali haina sheria kandamizi. Sheria zote zinazotumika nchini zilitungwa na Bunge lako Tukufu ambalo halijawahi kutunga sheria kandamizi. Aidha, Serikali kwa kuzingatia mahitaji ya wakati na watu wake, imekuwa ikiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali ili kuziboresha sheria hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na wakati tulionao na mahitaji ya sasa, Serikali imeanzisha mchakato wa kuzipitia baadhi ya sheria ili ziweze kufanyiwa marekebisho kuendana na wakati. Hivi sasa, Serikali kupitia Wizara imeandaa Muswada wa Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Ndoa utakaowasilishwa katika Bunge lako Tukufu ili kuiboresha, kwa lengo la kulinda makundi ya wanufaika na sheria hii. Aidha, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mirathi na Sheria za Kimila. Hatua hizo zikikamilika, Muswada wa Mapendekezo ya kuzirekebisha sheria hizo utawasilishwa kwenye Bunge lako Tukufu ili Wabunge wapate nafasi nzuri ya kujadiliana na kuyapitisha marekebisho hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ipo katika mabadiliko makubwa ya kuhakikisha kunafanyika maboresho makubwa ya sheria zetu ikiwemo kuzitafsiri kwa Kiswahili lakini pia kuweka vipengele kwenye sheria hizo vya kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili jambo ambalo litaleta tija kubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Tunawaomba Wabunge kuunga mkono juhudi za Serikali katika eneo hili kwa lengo la kuimarisha utawala wa sheria na upatikanaji wa haki nchini.
MHE. ALMAS A. MAIGE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Uyui?
NAIBU WAZIRI YA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ni mara ya kwanza kusimama hapa baada ya uteuzi, nipende tu kutumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini vilevile kumshukuru Mama yangu Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria nipende kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama ya Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya uhaba na uchakavu wa majengo na miundombinu ya Mahakama. Katika maeneo mengi Mahakama imekuwa ikitumia majengo ya kuazima kutoka taasisi nyingine na kupangisha ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, katika baadhi ya Wilaya wananchi wamekuwa wakipata huduma za Mahakama ya Wilaya katika Wilaya za jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Tabora Wilaya tatu; Uyui, Kaliua na Sikonge hazikuwa na Mahakama. Hivyo, wananchi wa Wilaya hizo wamekuwa wakipata huduma katika Wilaya za jirani ambapo Wilaya ya Uyui na Sikonge wanahudumiwa na Wilaya ya Tabora na Wilaya ya Kaliua wanapata huduma za Mahakama Wilayani Urambo. Mwaka 2020 Mahakama ilianzisha Mahakama ya Wilaya za Uyui na Kaliua katika Majengo ya Ofisi za Wakuu wa Wilaya ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, utatuzi wa changamoto hii ya majengo inafanyika kwa awamu kadiri bajeti inavyoturuhusu. Katika mipango yake, Mahakama ya Wilaya ya Uyui itajengwa mwaka wa fedha 2022/2023 kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Mahakama ya Wilaya ya Kaliua itajengwa mwaka wa fedha 2021/2022 na tayari zabuni imetangazwa. Vilevile Mahakama inaendelea kukamilisha ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Sikonge, pamoja na ukarabati mkubwa wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora.