Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Geophrey Mizengo Pinda (3 total)

MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Aidha, nina swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama vile Serikali ilivyoona umuhimu wa kuanzisha Mahakama kwa mfano za Kazi (Labor Courts) au Mahakama za Mafisadi (Economic Crimes Courts) au Commercial Courts (Mahakama ya Biashara) kwa ajili tu ya kutengeneza mazingira wezeshi ya kiuchumi lakini pia ya uwekezaji. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuanzisha Divisheni ya Familia (Family Division) katika Mahakama itakayoshughulika na masuala ya ndoa, talaka na mirathi ili kuharakisha mashauri haya na kuwaondolea wanyonge adha wanayopata ya kuchelewa kwa mashauri haya katika mfumo wa kawaida wa mahakama na hasa ukizingatia wanyonge hao ni wajane? Sisi tunajua kuna legal maxim ambayo inasema justice delayed is justice denied (haki iliyocheleweshwa ni sawasawa na haki iliyonyimwa). (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zainab, Mbunge Viti Maalum kutoka Kigoma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wake ni mzuri sana na chombo hiki ndiyo chombo chenye kazi ya kutunga sharia kwani sheria zote zinatungwa hapa Bungeni. Tusema tu tumepokea wazo lake na tutalipitisha katika mamlaka mbalimbali za kuangalia ile modality ya kuanzisha chombo kama hiki ili tuweze sasa kufikia maamuzi halisi. Naamini Bunge lako Tukufu litapata nafasi ya kupitia na kutoa maoni mbalimbali juu ya muundo utakaowezesha kutoa haki kwa makundi husika. Ahsante.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri kwamba na matumaini kwamba tutajengewa Mahakama yetu mwaka 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini je, kwa kipindi hiki ambacho Mahakama ya Wilaya ya Uyui iko ndani ya chumba kidogo sana katika jengo lile la DC. Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta jengo kubwa ili kutatua tatizo hilo la jengo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa vile yako majengo ya Mahakama ya awali ya Mwanzo ya Upuge yametelekezwa na ni makubwa yana nyumba za wafanyakazi na sasa kuna umeme wa REA, lakini pia kuna maji ya Ziwa Victoria na barabara nzuri; je, Serikali haioni ni busara kuanza kutumia majengo yale ya Mahakama ya Mwanzo ya Upuge kwa shughuli za Mahakama ya Wilaya ya Uyui?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria nipende kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maige kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hili la kutumia chumba kidogo hili tutalifanyia kazi haraka sana, nadhani mamlaka zinanisikia huko ni muhimu kuanza kufanya tafiti ili kujua tunaweza tukapata chumba wapi kikubwa ambacho kinaweza kikatoa huduma hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hii Mahakama ya Mwanzo Upuge nitaifuatilia kwa karibu kuona inaanza kazi mara moja kwa sababu kwanza, tunasema tunaupungufu wa vyumba halafu kumbe kuna nyumba zingine zimekaa hazifanyi kazi, kwa hiyo nadhani hili tumelichukua na tutalichukulia hatua haraka sana, ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kuniona na mimi niulize swali la nyongeza kwa Wizara hii yetu ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Mahakama ya Wilaya ya Uyui ni sawasawa na tatizo lililoko pale kwetu Wilaya ya Busega na kesi za Mahakama ya Wilaya zimekuwa zikienda kusikilizwa Wilaya jirani ya Bariadi.

Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kutumia jengo lililopo la Mahakama ya Mwanzo ili litumike kusikiliza kesi za Mahakama ya Wilaya, lakini hivyo hivyo ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa…

NAIBU SPIKA: Swali ni moja Mheshimiwa, swali la nyongeza ni moja.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba Waziri wa Katiba na Sheria nipende kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutumia jengo la Mahakama ya Mwanzo inategemea sana sifa ya hilo jengo kwa sababu vingine ni vyumba vidogo ambavyo haviwezi kuhimili huduma ambazo zinatakiwa kutolewa kwenye ngazi ya Wilaya, lakini tutalichukua na kulifanyia utafiti ili kuona kama hiyo Mahakama ya Mwanzo ina sifa zinazostahili kuwa kwenye kiwango cha matumizi ya Wilaya na tukijiridhisha huduma itaanzishwa mara moja kwenye eneo husika, ahsante.