Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kasalali Emmanuel Mageni (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na afya njema na kuniwezesha kufika hapa nilipofika. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza kwenye Bunge hili, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Sumve kwa ushindi mkubwa waliokipatia Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi uliopita. Nikishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kunipitisha na kunisimamia na kuhakikisha nashinda kwa kishindo katika uchaguzi uliopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika hoja iliyoko Mezani. Katika Nchi ya Tanzania, baada ya mimi kuangalia hizi hotuba, hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kulifungua Bunge na nimepitia hotuba ya mwaka 2015 aliyoitoa wakati akilifunga Bunge la Kumi na Moja, nimeona kwamba Nchi yetu ya Tanzania inayo bahati kubwa. Tumempata Rais ambaye anayo maono, tumempata Rais ambaye ana nia ya dhati ya kulitumikia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa la Tanzania ni moja ya mataifa machache yenye bahati ya kuwapata viongozi wa aina ya Dkt. John Pombe Magufuli. Ukiangalia mipango yote na namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga na ilivyokuwa imejipanga katika kipindi cha kwanza na ilivyojipanga katika kipindi cha pili, unayaona matumaini ya Tanzania itakayokuwa ni nchi yenye uchumi mkubwa. Kwa hiyo ninayo sababu ya msingi ya kujivunia kwamba Watanzania tunaye Rais mwema, mwenye maono na ambaye anataka kutuvusha, anataka twende sehemu ambayo wote tumekuwa tukitamani kufika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengi yamefanywa na Serikali yetu, tunaweza tukazungumza hapa lakini muda usitoshe. Nitajaribu kuzungumza machache ambayo yamefanyika na kushauri nini tufanye vizuri zaidi. Serikali ya Awamu ya Tano katika jambo kubwa ambalo imelifanya ambalo dunia nzima inaona na tunajivunia ni kuhakikisha inasimamia vizuri uzembe, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imeweka utaratibu kuanzia Mheshimiwa Rais akisimama, ukiwaona Mawaziri wake wamesimama, wote wanakemea namna yoyote ya uzembe, namna yoyote ya ubadhirifu na ufisadi wa mali za umma. Serikali ya Awamu ya Tano imefanya vizuri sana kwenye jambo hilo; majizi, mafisadi wameshughulikiwa vizuri na kila namna ambayo Serikali imeona inaweza kufanya kuhakikisha mali zetu, mapato yetu tunayoyakusanya yanakuwa salama, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya vizuri sana na matunda tumeyaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye ukusanyaji wa mapato kupitia TRA na halmashauri zetu, tumefika kiwango cha kuongeza mapato ya mwezi kutoka bilioni 800 mpaka mwezi uliopita tumeweka rekodi ya kukusanya trilioni mbili, mwezi Desemba; Serikali imefanya vizuri sana kwenye hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yapo mambo ambayo yanahitaji kuangaliwa kwa undani zaidi. Katika kusimamia ubadhirifu wa mali za umma na matumizi mabaya ya fedha za Serikali, Serikali yetu katika kiwango cha Kitaifa, katika taasisi zilizoko karibu na Serikali kama maeneo ya bandari na maeneo mengine tumefanya vizuri sana. Hata hivyo, kwenye maeneo ya chini, kama kwenye Halmashauri za Wilaya kazi kubwa inahitajika kufanyika. Fedha nyingi za matumizi zinazopelekwa kwenye Halmashauri zetu hazitumiki inavyotakiwa. Bado kuna miradi hewa, kuna usimamizi mbovu wa fedha na fedha nyingi zinapotea. Hata viwango vya majengo na miradi inayosimamiwa na Halmashauri zetu hazijafikia viwango vinavyotakiwa. Kwa hiyo, Wizara husika, ambayo ni TAMISEMI, wanatakiwa kuziangalia Halmashauri kwa jicho la pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya vizuri sana kwenye sekta ya kilimo kufufua ushirika na mambo mengine, lakini bado kuna mambo ya kufanya kwenye ushirika. Naweza nikakupa mfano, katika Wilaya yetu ya Kwimba kuna shida kubwa sana sasa hivi inaendelea. Kuna mazao ambayo Serikali imeyaweka kusimamiwa na ushirika ambayo kiuhalisia hayakupaswa kusimamiwa na ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna zao la choroko na mazao mengine kama ufuta, yamewekwa kwenye ushirika lakini mazao haya siyo kama mazao mengine yaliyoko kwenye ushirika kama pamba. Mazao haya ni ya chakula, ni mazao ambayo uuzaji na usimamizi wake unapaswa uwe wa kawaida na usitegemee AMCOS na ushirika. Katika Wilaya Kwimba, moja ya jambo ambalo linatutesa sasa hivi ni mazao yetu ya choroko kupelekwa kwenye ushirika na tunalazimishwa mazao ambayo ni ya chakula, mazao ambayo sisi muda wote tunayategemea, tukitaka kuuziana ni lazima twende kwenye AMCOS.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiombe Serikali kwamba umefika wakati wa kuangalia ushirika wetu. Tumeuimarisha ushirika, unafanya vizuri lakini tunauongezea majukumu ambayo ni magumu kuyafanya. Moja ya jukumu ambalo ushirika unapata shida kulifanya ni hili la ununuzi wa choroko, dengu na mazao mengine ambayo ni mazao yetu ya chakula na biashara, kuna wakati tunahitaji kuyatumia kama mazao ya chakula. Mimi siwezi kuhitaji kununua choroko ikabidi niende kununua AMCOS, nitanunua kwa mtu mwenye choroko. Naomba sana katika suala hili Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ione namna ya kuhakikisha mazao yaliyoongezwa kwenye ushirika yanarudishwa, tunaanza kuyanunua kwa njia zetu za kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naomba niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima lakini pia nitumie fursa hii kutoa pole kwa Watanzania na mimi mwenyewe kufuatia kifo cha Rais wetu wa Awamu ya Tano Rais wetu aliyekuwa amejikita kwenye kuhakikisha anatuletea maendeleo ya kweli Watanzania Hayati Dkt John Pombe Magufuli tunamuombea huko aliko apate pumziko jema na sisi tulioko huku tuendelee kuchapa kazi ili kutimiza malengo waliyonayo Watanzania na matumaini waliyonayo na Serikali yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan na Makamu wake na Serikali yote na niwakaribishe katika kuchapa kazi sisi tupo tutaungana nao na tutawaunga mkono kuhakikisha kazi ina kwenda ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika mpango wa bajeti ambao umewasilishwa leo Bungeni hapa. Ukiangalia Mpango huu unaona yapo matumaini ndiyo maana naanza kwa kuunga mkono lakini yapo mambo ya kuzingatia ambayo nilitaka tuyazungumze kidogo kwenye Bunge lako.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu mambo ya vijijini kwasababu ni moja ya Wabunge wenye Majimbo ya vijijini, huko vijijini asilimia kubwa ya watu ni wakulima na sekta ya kilimo imekuwa ni uti wa mgongo wa Taifa letu lakini sisi kule kijijini ndiyo Maisha yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia Bunge lako niiombe Serikali katika sekta ya kilimo mnatakiwa sasa ifike tuanze kuwekeza katika kuboresha sekta hii kuanzia kwenye uzalishaji. Kumekuwa na utaratibu ambao umekuwa ukinishtua nadhani kwenye kikao kilichopita nilisema wakulima wakati tunazalisha mazao yetu Serikali imekuwa ikikaa kimya ikituangalia inapofika wakati wa kuvuna mazao yetu unaanza kuona vitu vinaitwa AMCOS unaanza kuona vitu vinaitwa Stakabadhi Ghalani, unaanza kuona usimamizi ambao si rafiki kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo la Sumve tunalima mazao ya jamii ya kunde hizi choroko na dengu ni mazao ambayo sisi wakulima tunayalima kwa nguvu zetu wenyewe hatujawahi kuona mbegu kutoka Serikalini, hatujawahi kuona dawa kutoka Serikalini, hatujawahi kuona Afisa Ugani kutoka Serikalini lakini inapofika wakati wa kuyauza unaanza kuona kuna watu wanaitwa AMCOS, kuna watu wanaitwa Ushirika wanakuja kusimamia mazao ambayo tumeyalima sisi wenyewe kwa nguvu zetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi wanaleta utaratibu wa hovyo utaratibu ambao hautusaidii bei zimeshuka sasa hivi ukienda kwenye maeneo ambayo yanalima hizi choroko na dengu tunakaribia kuanza kuuza choroko soko lake limeporomoka kwa wakulima. Wakulima wameshindwa kabisa kufaidika kwa hiyo, naomba Serikali muwekeze zaidi kwenye uzalishaji kabla hamjaamua kuwekeza kwenye kutupangia namna ya kuuza mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni lazima mliangalie kwa undani hamuwezi kuweka mazao yote kwenye kapu moja zao kama choroko na dengu huwezi kulifananisha na korosho. Dengu sisi na choroko Wasukuma ni zao la chakula na biashara kuna mtu anahitaji kwenda kununua dengu sokoni akapike atumie lakini wewe umemwambia ili aziuze lazima apeleke AMCOS.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu amezungumza hapa Mheshimiwa Tabasamu kuhusu zao la pamba, ni Mbunge ninayetoka kwenye jimbo la wakulima wa pamba. Wilaya ya Kwimba ni moja ya wilaya ambazo zinazalisha pamba kwa wingi kuliko zote kwenye Mkoa wa Mwanza zao la pamba niwaambie kabisa Serikali mmeshiriki kuliua na mnaendelea kushiriki kupitia namna ambavyo mnasimamia masoko yake. Wakulima wengi wa Tanzania tunalima hatujui hata kama tunapata faida au hasara huwa tunalima tu lakini ukifanya hesabu asilimia kubwa tunapata hasara. Lakini bado Serikali kwenye kusimamia bei za mazao bado haijaonekana kwamba tuko serious kwasababu tunapeleka watu kwenda kusimamia vitu wasivyovijua.

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la pamba asilimia kubwa linasimamiwa na watu wasiolijua na limeingiliwa amesema Mheshimiwa Tabasamu hapa hawa siyo wawekezaji ni mabeberu ni watu ambao wanakwenda kumdidimiza mkulima. Kwa hiyo, ni lazima Serikali muangalie Mheshimiwa Waziri wa Fedha muone namna ambavyo mtalifufua zao la pamba kwasababu tunataka viwanda, viwanda vinatoka wapi kama mazao tunayaua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini huko vijijini kwetu ambako ndiko tunakozalisha mazao haya ya chakula ambayo watu wa mjini wanatumia lakini ndiko nguvu kazi nyingi iko kule, bado tunazo changamoto za miundombinu. Katika mpango wa bajeti nimeona tunazungumza kuhusu miundombinu mikubwa mikubwa kama reli ya kati tunazungumza madaraja lakini pia sisi kule site vijijini kuna miundombinu ya kwetu ya kawaida kabisa mabarabara ya vijijini kupitia TARURA bado hali vijijini si nzuri barabara za Dar es Salaam zisipopitika utaona watu wamepiga picha zimeonekana kwenye mitandao Serikali imeenda kurekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini barabara za Sumve asilimia kubwa hazipitiki vijijini kuna kata zingine kama Kata ya Mwabomba ikinyesha mvua ikakukuta uko kule kama una pikipiki unaacha unatembea kwa mguu. Kwa hiyo, bado kabisa tunatakiwa tuwekeze pesa kwenye miundombinu ya vijijini ili wakulima wetu waweze kusafiri waweze kusafirisha mazao lakini pia ipo miundombinu ya kimkakati ambayo inawezekana hatujaiona sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ambayo imekuwa ikiongelewa sana tangu mimi nimekuwa chaguzi zote za Chama cha Mapinduzi za vyama vingi imekuwa ikitajwa barabara yenye urefu wa kilometa 71 inayotokea Hungumarwa kupita Ngudu kwenda mpaka Magu. Barabara hii ni barabara ya kimkakati ambayo imesahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mpango huu pia nimeiona imezungumzwa lakini imezungumzwa katika ile stori ya kutenga pesa na mipango ya baadaye. Lakini imeanza kuzungumzwa niko darasa la tatu. Sasa barabara hizi za kimkakati kwasababu barabara hii ikijengwa kwa kiwango cha lami inapunguza umbali wa mtu anayesafiri kutokea Shinyanga kwenda nchi Jirani ya Kenya au Mkoa wa Mara au Wilaya ya Magu kwa kilometa zaidi ya 83. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ukiijenga unakuwa umeokoa uchumi tunaposema kukuza uchumi barabara za kimkakati ndiyo hizi. Hii ni barabara ambayo inaweza ikafungua mbali na kufungua wilaya ya Kwimba kuongeza mapato kuongeza mzunguko kwasababu Wilaya ya Kwimba ni wilaya pekee ambayo kwenye Mkoa wa Mwanza haijui maana ya lami kwenye Makao Makuu yake kwa hiyo, barabara hii ikipita itafungua uchumi wa Wilaya ya Kwimba. Lakini siyo tu uchumi wa Wilaya ya Kwimba itafungua uchumi wa kanda ya Ziwa na uchumi wa Taifa kwasababu tunahitaji mizigo inayopelekwa nchi jirani ya Kenya iende kwa urahisi zaidi, tunapunguza uhai lakini tunafungua uchumi wa wilaya husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika mpango huu wa kiuchumi; Mpango Mkakati wa Maendeleo ambao tumeletewa leo, ni lazima tuangalie pia maeneo ya vijijini. Sisi tunaotoka vijijini, bado tumesahaulika. Hii miundombinu yote tunayoisema inazungumza mambo mengi ya mjini, lakini sisi ambao wakati mwingine hata mawasiliano ya simu siyo mazuri, hatuzungumzwi humu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kupitia Bunge lako, Wizara na Serikali katika Mpango wao huu wahakikishe wanazingatia maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)