Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe (447 total)

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika Wilaya ya Mvomero ipo miradi ya maji iliyo chini ya Wizara katika maeneo ya Tarafa za Mgeta, Mlali, Turiani na Mvomero na kwa kuwa miradi hiyo imeanza, lakini bado haijakamilika na kwa kuwa Serikali imeshatumia mamilioni ya fedha. Je, Serikali sasa iko tayari kuleta fedha zilizobaki ili miradi ikamilike katika maeneo hayo na wananchi wapate maji safi na salama Wilayani Mvomero?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, jana kwenye jibu la msingi la matatizo ya maji nilieleza katika awamu ya kwanza ya programu ya maji iliyoanza mwaka 2007 na imeishia mwaka 2012 tulikuwa na miradi 1,855.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi iliyokamilika ni miradi 1,143 na miradi inayoendelea ni miradi 454 ambapo katika hii miradi inayoendelea ipo miradi katika Jimbo la Mheshimiwa Saddiq, sasa hivi mwezi Januari tunaanza progamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kwa hiyo, katika mpango huu nimhakikishie Mheshimiwa Saddiq kwamba fedha itatolewa kuhakikisha miradi hii inakamilika.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Waziri, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa skimu ambazo amezitaja zinapita nje ya Vijiji vya Langoni A, Langoni B, Mkundyambaro na Mkundyamtae, je, Serikali haioni sasa kwamba kuna umuhimu wa kipekee wa kuwapa wananchi wa vijiji hivyo bwawa la kuhifadhia maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne tarehe 10 Julai, 2014, alipita katika Kata ya Mng‟aro na akatoa ahadi kuboresha miundombinu ya maji ambayo ni chakavu toka mwaka 1972. Upembuzi yakinifu umefanyika, gharama ya ukarabati ni shilingi 157,200,050/=Mheshimiwa Mwenyekiti, . Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutimiza agizo hilo la Rais? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rashid Shangazi, tangu niteuliwe kuwa Naibu Waziri ameshakuja ofisini mara nne kwa ajili ya kufuatilia miundombinu ya umwagiliaji pamoja na maji ya kunywa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, swali (a) kwamba Serikali inafanya upembuzi wa awali ili kuweza kubaini maeneo mengine yanayoweza kujengwa mabwawa. Kwa sababu hiyo, kwenye utafiti huo utahusisha pia vijiji ambavyo Mheshimiwa Shangazi amevitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne ya kukarabati miundombinu ambayo imefanya kazi kwa muda mrefu na inaelekea kupunguza ufanisi wake. Mheshimiwa Rais aliahidi kutoa shilingi milioni 152 kwa ajili ya ukarabati huo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi hiyo tumeipokea na tutaifanyia kazi.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niishukuru sana Serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuleta hizi fedha haraka na kujua umuhimu wa wananchi wa Chemba na Kondoa kutokana na tatizo hili la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ningeomba hizi shilingi milioni 600 anazosema Mheshimiwa Waziri, ziliingia akaunti ya DAWASCO Dodoma toka Januari mwaka jana, mpaka leo hiyo fedha haijaingia katika Halmashauri ya Kondoa. Je, yuko tayari sasa, kusukuma ili fedha hii iingie kati ya leo na kesho?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ucheleweshwaji wa miradi mingi ya maji umechangiwa sana na flow ya fedha kutoka Hazina kwenda kwenye Halmashauri. Je, Wizara sasa iko tayari kupeleka fedha hizi haraka ili miradi mingi nchini iweze kukamilika hasa hii ya maji ambayo wakandarasi wengi wameanza kutishia sasa kwenda Mahakamani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata taarifa kwamba hizo fedha zimekwama Mamlaka ya Maji Dodoma (DUWASA). Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafuatilia kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa Kondoa, lakini ndiyo umekuwa utaratibu kwamba fedha zikitolewa kwanza zinaanzia DUWASA, baadaye ndiyo zinakwenda huko kwenye kazi.
Hoja ya pili ya Mheshimiwa Mbunge, sasa hivi tunaingia katika awamu ya pili ya programu ya maji. Miradi mingi haikukamilika kwa sababu ya matatizo ya kifedha, lakini sasa tunaanza programu ya pili na hii programu ya pili tayari tunaanza kupata pesa na Serikali itatenga fedha ili kuhakikisha miradi yote iliyokuwa inaendelea inakamilika na miradi ambayo ilikuwa haijaanza inaanza. Pia tunatarajia kuwa na miradi mipya kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuhakikisha tunapunguza hili tatizo la maji.
MHE. DUA W. NKURUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri na yanayotia moyo kwa wananchi wangu wa Nanyumbu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Nanyumbu tulikuwa na bahati mbaya ya gari la Programu ya Maji kupata ajali, gari ambalo sasa haliwezi kutumika kabisa.
Je, Mheshimiwa Waziri ana mpango gani sasa kuipatia Wilaya ya Nanyumbu gari ili wataalam waweze kutoa huduma hizo kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ingawa swali hili limepata majibu kidogo hafifu kutoka kwa Mheshimiwa Nkamia, lakini nataka pia tuna tatizo la wakandarasi kuzidai Halmashauri pesa za maji za Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini hasa tutawalipa hawa Wakandarasi ili kuondokana na kero ya mgogoro kati ya Halmashauri na Wakandarasi hao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la gari ambalo limeharibika, tutaliangalia na tutakapopata fedha tutalifanyia matengenezo na kama matengenezo yatashindikana, basi tutafanya utaratibu wa kununua gari lingine jipya ili wananchi wa Mangaka waendelee kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kabisa kwamba kuna miradi mingi ambayo imechelewa kukamilika kwa sababu ya fedha zinazoitwa fedha za Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matatizo ya kifedha katika nchi ambayo yamesababisha miradi mingi ya maji isikamilike. Hata hivyo, tunamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia sasa fedha zinaanza kutolewa ambazo zitahakikisha kwamba miradi yote ambayo ilikuwa haijakamilika, inakamilika pamoja na miradi ya Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Suala la Arumeru Magharibi linafanana sana na tatizo ambalo lipo Mikumi, je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa kero ya maji katika Kata ya Mikumi, Ruaha, Uleling’ombe na maeneo ya Tindiga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri katika majibu yake ametoa taarifa kwamba tunaingia katika progamu ya pili kupitia sera ya mwaka 2002 ya kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2020 asilimia 85 ya Watanzania wote watakuwa wanapata maji katika vijiji na asilimia 95 katika miji.
Mheshimiwa Mbunge, kwa upande wa Jimbo lako la Mikumi na Kata zake, tutahakikisha kwamba tunazipa kipaumbele kuhakikisha zinapata maji katika hii progamu ya pili. Na ninakuomba sana baada ya Bunge hili tuwasiliane ili tuweze kupata taarifa iliyo nzuri zaidi tuanze utekelezaji.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la Arumeru Mashariki linafanana kabisa na tatizo la maji la Lushoto.
Je, ni lini Serikali itaondoa adha hii kwa wananchi wa Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Wilaya ya Lushoto mlalo wake wa ardhi ni mzuri kuruhusu ujenzi wa mabwawa. Tumeweka mpango wa kujenga mabwawa katika awamu hii ya programu ya pili ambayo yatasaidia kwenye irrigation pamoja na kuhakikisha kwamba tunapata maji ya kunywa kwa wananchi wa Jimbo lake.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, jina langu naitwa Mussa Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ilianzisha mpango wa maji safi na salama vijijini katika mradi uliofadhiliwa na World Bank na mradi ule umekwama. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha katika Halmashauri ya Jiji la Tanga ili kuondoa kero ya maji katika Kata za Mabokweni, Chongoleani, Kilale na Marungu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilianzisha mradi wa vijiji 10 kupitia progamu ya Benki ya Dunia na mradi huo ungali unaendelea. Katika mradi huo tulikuwa na miradi 1,855 kama nilivyotoa taarifa ya awali kwamba katika miradi hiyo miradi 1,143 imekamilika na miradi 454 inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo la fedha ndiyo lililofanya hii miradi isikamilike kwa wakati lakini nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika eneo lako la Tanga kufuatia juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukusanya fedha, fedha zimeanza kutoka na nikupe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba wiki iliyopita tumeletewa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kuendelea kulipa miradi hiyo mingi ambayo ilikuwa imesimama na siyo Tanga tu, ni karibu Mikoa yote miradi ilikuwa imesimama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nikuhakikishie kwamba Serikali inatoa fedha kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ili katika progamu ya pili tuanze kuweka tena miradi mingine. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya maji yaliyoko Hydom yanafanana kabisa na matatizo ya maji yaliyoko katika Mkoa wangu wa Arusha hasa Longido na Monduli. Kwa kuwa Monduli walikuwa na mabwawa matatu ambayo yamepasuka na sasa hivi wananchi wa Monduli wana tabu kubwa sana ya maji, wana-share maji na mifugo. Kwa kuwa kuna maji yanamwagika Engaruka na Mto wa Mbu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuwasaidia wananchi hawa wa Monduli kwa kuyatumia maji yale kuliko yanavyomwagika bure? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru ametupa taarifa kuna mabwawa ambayo yamepasuka katika Jimbo la Mbulu. Naomba kuchukua nafasi hii kuagiza Mkoa wa Arusha wakatembelee eneo hilo na waipe taarifa Wizara ili hatua mahsusi ziweze kuchukuliwa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa miradi hii haijakamilika na wananchi sasa hivi wanapata adha ya kutopata maji hasa katika miji niliyoisema na vijiji vyake, je, Serikali itahakikisha vipi leo hii itapeleka pesa kule ili wananchi wapate maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na adha ya maji katika maeneo yetu, yuko mwananchi mmoja amechimba maji na kuyapata katika Mji wa Hydom. Je, kwa nini Serikali isiweze kupata maji katika maeneo yale na kuweka hela nyingi namna hii? Waziri yuko tayari kufuatana na mimi akaone jinsi ambavyo wananchi wanapata adha katika mji wa Hydom na maeneo mengine ya Mbulu Vijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Massay yeye mwenyewe tayari anafahamu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inafanya juhudi kubwa sana kukusanya pesa. Sasa hivi pesa zimeanza kupatikana kwa hiyo wakati wowote ule fedha zitaanza kutumwa kwenda kukamilisha miradi ambayo haijakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza katika maswali yaliyopita kwamba tumekuwa na miradi ya maji 1,855, miradi 1,143 tayari imeshakamilika na iliyobaki ni 454 ambayo tunatarajia tuipatie pesa ili iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, muuliza swali amedai kwamba kuna mwananchi ambaye amepata maji lakini haku-specify kwamba huyo mtu aliyapata hayo maji kwa shilingi ngapi? Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna miradi inayoendelea katika wilaya yake. Kuna Mradi wa Tumati, Hasha, Mungay, Hydom, Moringa na Dongobesh. Miradi hii ikikamilika, naimani kabisa kwamba matatizo ya maji katika eneo lake yatakuwa yamekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kibali cha Mheshimiwa Spika, nitakuwa tayari kufuatana naye ili kwenda kuona tatizo lilivyo kwenye Jimbo lake.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Pale Musoma Mjini tumekuwa na tatizo la maji kwa muda mrefu na bahati nzuri tumepata mradi ambao tulitegemea toka mwaka jana ungekuwa umekamilika na watu wameanza kupata maji. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba mradi huo umekamilika kama ilivyokuwa ahadi yake ya toka mwaka jana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeanza kupata fedha, kwa hiyo, wakati wowote ule tutatuma fedha na kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha tutakuwa tumekamilisha mradi huo.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, licha ya kuongeza ujazo wa mita za maji katika Manispaa ya Morogoro bado kuna sehemu za Lukobe, Kihonda, Kilakala, Folkland, SUA, Mbuyuni na sehemu zingine ambazo hawapati maji. Je, kwa nini hawapati maji wakati wote?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Manispaa ya Morogoro inakua na watu wanaongezeka. Licha ya mradi wa Milenia wa Halmashauri ambao umepita, je, kuna mkakati gani wa kubuni mradi mwingine wa maji kusudi maji yaweze kutosheleza Manispaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Maji ya mwaka 2002 imeainisha kuhakikisha kwamba nchi yetu ifikapo mwaka 2025 watu wote watakuwa wamepata maji safi na salama. Hiyo itakuwa ni pamoja na wananchi wote wa maeneo ya Morogoro. Maeneo aliyoyataja kwa sasa hivi tunaanza programu ya pili ambayo imeanza Januari, 2016 ya kuendeleza miradi ya maji katika nchi yetu. Katika programu hiyo, tutaendeleza utafutaji wa maji katika Mkoa na Mji wa Morogoro kwa maeneo ambayo yamebaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kweli kabisa kwamba Mkoa wa Morogoro unapanuka na nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mikakati tuliyonayo, tutahakikisha kwamba maeneo yote na wakazi wote wa Mkoa wa Morogoro na Mji wa Morogoro hasa wanapata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu aliyoyatoa, pamoja na majibu mazuri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Kwanza nakubaliana kabisa na Serikali kwamba jawabu la haraka la matatizo ya Urambo kuhusu maji ni Mto Ugalla, kwa sababu ni kilomita 30 tu kutoka Usoke. Ninaamini kwamba tumefanya hivyo kwa sababu ya suala la quick win ili wananchi wapate maji haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, katika kipindi tulichopita, katika maandalizi ya kupata maji kutoka Ugalla lilikuja tatizo la mazingira kwamba kuna wanyama, sijui kuna msitu; naomba Serikali itoe kauli, tusije tukafika katikati wakaanza tena masuala ya wanyama na misitu wakati sisi tunapata shida ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni vizuri kweli miradi miwili hii ikaenda pamoja kwa sababu kwanza Mto Malagarasi unategemea hayo maji kutoka Ugalla ambayo ndiyo yanatoka Urambo. Kwa hiyo, nashukuru Serikali hivyo, lakini je, Waziri yuko tayari kwenda na mimi uko akajionee mwenyewe uharaka wa kupata maji katika Mji wa Urambo na Usoke? Lini twende naye tufuatane wote wawili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sera ya Maji ya mwaka 2002 inaendelea kutekeleza Mpango wa Sekta ya Maji nchi nzima ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wanaoishi vijijini wanapata maji safi na salama. Kama alivyoongea Mheshimiwa Waziri, ni kwamba tunatarajia ifikapo mwaka 2025 asilimia 100 ya wananchi wanaoishi vijijini na wale wanaoishi mijini waweze kupata maji.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea na usanifu wa mradi wa kutoka Malagarasi, kupeleka maji hadi Tabora ili kuhakikisha kwamba vijiji vingi vinapata maji hayo. Katika usadifu huo unaoendelea, pia kuna sehemu ambayo itatafiti uwezekano wa kuchota maji, kuweka mradi wa maji kutoka Mto Ugalla na kupeleka Wilaya ya Urambo ambayo itahusisha pia kupeleka maji katika Kata ya Usoke.

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta kwamba nitakuwa tayari kuambatana naye kwenda kuangalia tatizo la maji katika Mji wa Urambo.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa hapa Bungeni tumekuwa tukipitisha fedha nyingi sana kwa ajili ya kwenda kutatua matatizo ya maji kule vijijini ikiwemo Mkoa wa Singida, lakini yamekuwa ni mazoea kwamba ma-engineer wanakwenda kuchimba maji maeneo ambapo hakuna maji ya kutosha na hivyo fedha nyingi kupotea.
Je, Serikali ni lini itakuja kutuletea idadi ya fedha ambazo zimepotezwa kwa sababu ya ma-engineer kwenda kuchimba maji kwenye maeneo ambayo hakuna maji matokeo yake wananchi wanaendelea kuteseka na adha za maji? Ni lini Serikali itatuletea figures hizo? Asante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji chini ya ardhi ni gumu sana na tuchukulie mfano Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Tabora ulifanyiwa study na Wajapani na waka-confirm kwamba chini kuna maji, lakini wamekwenda kuchimba maji yamekosekana kutokana na mfumo wenyewe wa miamba chini ya ardhi. Kwa sasa Wizara ya Maji imetengeneza utaratibu mpya kwamba, study ya maji pamoja na uchimbaji utafanywa na mtu mmoja. Kitu tulichokiona ni kwamba, study inafanywa na Mhandisi Mshauri, anayekuja kuchimba ni mwingine na unakuta tunapoteza pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kitu tulichokifanya sasa hivi kwamba, pale tutakapotoa fedha kwa ajili ya kuchimba visima tunatafuta Mkandarasi mmoja na huyo huyo ndiyo anafanya study. Ili akifanya study akichimba kama maji hayakupatikana basi pesa hatutamlipa na kuhakikisha kwamba huo upotevu wa pesa unakuwa haupatikani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye hoja ya pili, tutafanya tafiti na tutatoa taarifa kwenye Bunge hili kuona ni fedha kiasi gani ambazo zimepotea baada ya huo utaratibu wa kuchimba visima na maji hayapatikani.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Maji ni uhai, ningependa kuiuliza Serikali, kwa sababu iko ahadi ya kupeleka maji katika maeneo ya Sumve, Malya, Mwagini kupitia Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria, ningependa Serikali iniambie ni lini hasa mradi huo mkubwa ambao utanufaisha zaidi ya vijiji 40, utaanza kwa sababu ni ahadi ya muda mrefu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imeahidi kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka maeneo ya Sumve na maeneo mengine. Naomba nimhakikishie tu kwamba ahadi hiyo ipo pale pale na nitakapoleta bajeti yangu nitaeleza hilo jibu la lini kazi hiyo itaanza.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali ya nyongeza mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, katika bajeti ya mwaka 2014/2015, Serikali ilitenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuwawezesha Mamlaka ya Usambazaji wa Maji (MANAWASA) waweze kusambaza maji ya kutosha katika Vijiji vya Jimbo la Masasi. Pia bajeti hiyo hiyo na kiwango hicho hicho cha fedha kilitengwa 2015/2016 na fedha hizo mpaka sasa hazijatoka. Ni lini Serikali sasa itapeleka fedha hizi ili kusudi wananchi waweze kupata huduma hii ya msingi na ni ya lazima?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba kufahamu, ni lini Serikali itapunguza gharama kubwa za maunganisho ya maji kwa wananchi ambao kimsingi hawamudu gharama hizo na tayari Naibu Waziri alipotembelea Jimbo la Masasi tulimdokeza? Asante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza amesema Serikali ilitenga shilingi bilioni moja mwaka wa fedha uliopita na mwaka wa fedha tulionao, ni kweli, fedha hii ilitengwa lakini kutokana na makusanyo ya Serikali kutokuwa mazuri, basi fedha hii haikupelekwa kwenye mradi. Hata hivyo, kwa sasa Serikali imeanza kukusanya mapato vizuri na ninyi wenyewe Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, kwa hiyo, sasa tutaanza kupeleka fedha ili shughuli iliyotarajiwa kufanyika kutokana na hii fedha iweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, gharama za maunganisho, ni kweli nilipokwenda kule nilikuta kuna malalamiko ya gharama za maunganisho. Nilielekeza mamlaka ya MANAWASA waweze kupitia gharama hiyo pamoja Bodi na waweze kuja na gharama ambayo itakuwa ni rafiki kwa watumiaji wa maji. Nashukuru wameniletea taarifa kwamba maelekezo yote niliyowapa wameanza kuyafanyia kazi.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kwenye majibu yake ya msingi amesema kwamba Mkoa wa Pwani ulikuwa na wananchi wachache, lakini kwa kuwa Mkoa wa Pwani sasa hivi una ongezeko kubwa la wananchi. Je, haoni kama ni wakati muafaka kwa Mkoa wa Pwani kuwa na Mamlaka yake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na majibu yote ya Mheshimiwa Waziri, haoni kwamba kunatakiwa kuwepo na mpango wa kati kabla ya mpango huu ambao anasema kuna upembuzi ili kuondoa maji machafu katika Mkoa wa Pwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nilisema kwamba wakati Mamlaka ya DAWASA inaanzishwa, Miji ya Bagamoyo na Kibaha haikuwa na watu wengi. Kwa sasa nakiri kabisa kwamba ni miji ambayo imekomaa ina watu wa kutosha.
Mheshimiwa Mbunge, kupitia Sera ya Maji na Sheria ya Maji Na.12 ya mwaka 2009 unaweza kumwomba Mheshimiwa Waziri mwenye mamlaka akaidhinisha uanzishwaji wa Mamlaka katika Mji wa Kibaha. Ijulikane kwamba au utambue kwamba Mamlaka zinazoanzishwa zinatakiwa kujitegemea. Kwa hali hiyo, italazimika ziwe na chanzo chake cha maji. Kwa hiyo, unapoleta hilo ombi ni vyema mkatafakari na kujiweka sawa.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu suala la huduma ya majitaka kwamba kuwe na mpango wa kati wakati tunaendelea kusanifu uondoaji wa majitaka kwa Miji ya Bagamoyo na Kibaha, mpango wa kati upo. Tunaweza tukajenga mfumo wa mtandao wa majitaka lakini mpango wa kati ni kujenga septic tanks kwa kila nyumba ambazo zinasaidia kuondoa majitaka kwa kipindi cha kati.
MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majawabu mazuri ya Naibu Waziri wa Maji, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, Mradi wa Kalinzi huu ni mwaka wa tatu mfululizo zinawekwa fedha kwenye bajeti hazijawahi kuja, naomba leo Waziri alieleze Bunge lako, sasa fedha zilizotengwa mwaka huu zitakuja ili mradi huu uweze kutekelezwa?
Swali la pili, tunalo tatizo kubwa sana la mazingira, vijiji vyote alivyovitaja vinategemea kupata maji kwenye mito na ikifika kiangazi karibu yote inakauka, kwa hiyo tatizo linarudi kuwa palepale. Sasa, Serikali haioni imefika wakati kutumia maji ya Lake Tanganyika ili yaweze kuchukuliwa ili kupeleka maji kwenye vijiji vyote hivi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa inatenga fedha kila mwaka kama alivyosema, lakini kutokana na matatizo ya upatikanaji wa fedha, na sisi sote ni mashahidi, uchumi umekumba dunia yote, kwa hiyo hali ya upatikanaji wa fedha ulikuwa kidogo mgumu. Lakini kwa sasa baada ya kuanza Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inakusanya fedha vizuri nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa fedha itapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, na pili kwenye Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Maji ambayo tunashirikiana na wadau, mwezi Januari mwaka huu tayari tumeanza Programu ya Pili na tuna ahadi za kutosha za kupatiwa fedha kutoka kwa wadau tunaoshirikiana nao.
Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huo sasa utatekelezwa na utafiti umeshakamilika kama nilivyojibu kwenye swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili ni kweli kwamba kipindi cha kiangazi maeneo mengi ya Jimbo lako, mito ile inayotiririsha maji inakauka. Lakini pia wewe mwenyewe ni shahidi kwamba sasa hivi kuna mradi mkubwa wa maji ambao tunajenga Mji wa Kigoma na tunachukua maji kutoka Ziwa Tanganyika na mpango huo kwa sasa Wizara ya Maji inataka kutumia vyanzo vyote vya maji ambavyo viko karibu na miji ambayo imepata bahati ya kuwa karibu na vyanzo vizuri vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo tumeanza mradi wa maji Mjini Kigoma, na kadri jinsi tutakavyokuwa tunakwenda, yale maeneo ambayo hayatakuwa na chanzo kizuri cha maji tutaendelea kutumia maji ya Lake Tanganyika kufika mpaka kwenye maeneo yenu.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali fupi la nyongeza.
Wilaya ya Ilemela ilikuwa ina mradi ambao ulikuwa unatakiwa kukamilika mwaka 2014, mradi huu ambao ulitakiwa kuwanufaisha Kata za Wilaya ya Ilemela ikiwepo Kata ya Kayenze, Sangabuye, Shibula, Monze na Buswelu ambayo ni Kata Mama ya Wilaya ya Ilemela.
Je, ni lini mradi wa tenki hili la kutoa maji Wilaya ya Ilemela utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi umekuwepo Wilaya ya Ilemela na ulishindwa kukamilika. Tulipata matatizo kidogo baada ya kuanza Programu ya Sekta ya Maji Awamu ya Kwanza iliyoanza mwaka 2007, programu ilizinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, lakini kwa sababu fedha nyingi tulikuwa tunapata za wafadhili, ule mchakato wa manunuzi, kwa mfano mwaka 2007 ndiyo programu ilianza, lakini kuja kupata no objection ya kuanza kusanifu tuliipata Disemba mwaka 2009, utekelezaji wa miradi ukaanza mwaka 2012. Kwa hiyo, hicho ndiyo kitu ambacho kilifanya miradi mingi isikamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunatoa ahadi kwamba miradi yote ambayo haikukamilika tunaanza nayo tukamilishe ndiyo tunaingia kwenye miradi mipya. Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba Kata zako zote za Wilaya ya Ilemela katika Programu ya Pili ya Mpango wa Maji itafikiwa na itakamilika.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza, naomba Mheshimiwa Waziri jina langu amelitamka vibaya naitwa Saed siyo Sadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na tatizo la mtambo wa Ruvu kupatiwa ufumbuzi lakini tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa kubwa hasa katika Jimbo la Ubungo, Kibamba, Segerea, Kigamboni, Ukonga, na hata Temeke.
(a) Mheshimiwa Waziri tatizo hili linatokana kwa kiasi kikubwa na uchakavu wa miundombinu hasa yale mabomba yanayosambaza maji katika majumba. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kukarabati miundombinu ya maji katika Jiji la Dar es Salaam?
(b) Kwa kuwa, majibu ya Mheshimiwa Waziri yamekuwa ya jumla, kwamba mtambo umekamilika, majaribio yameanza, ukarabati unafanyika, Mheshimiwa Waziri anaweza akataja kwa majina mitaa ambayo mradi huu wa maji utafanyika katika kipindi hiki cha haraka?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba msamaha nimetamka Sadi kumbe ni Saed, basi nitafanya marekebisho Mheshimiwa Kubenea.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini maswali ya Mheshimiwa Kubenea mawili ni kwamba, Serikali kupitia Wizara ya Maji inao mpango mkubwa sana wa kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa ukarabati na upanuzi wa mfumo wa kusambaza maji safi katika Jiji la Dar es Salaam, unaohusisha maeneo ya Tegeta-Mpiji, Mpiji-Bagamoyo na Mbezi-Kiluvya. Mradi huu unagharimu dola za Marekani milioni 23.927 na ujenzi unatarajiwa kukamilika tarehe 21/4/2017. Mradi huu utakapokamilika maeneo yatakayopatiwa maji ni pamoja na Mji wa Bagamoyo na vitongoji vyake, eneo la uwekezaji la Bagamoyo EPZ, Mpiji, Bunju, Mabwepande, Boko, Mbweni, Tegeta, Ununio, Wazo, Salasala, Kizundi, Matosa, Mbezi Juu, Goba, Changanyikeni, Makongo, Kiluvya, Kibamba, Mbezi Msakuzi, Makabe, Marambamawili na Msigani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali kwa kutambua kwamba kuna maeneo mengi ambayo hayatofikiwa kwa haraka na mtandao wa mabomba ya maji, imefanya utaratibu wa kuchimba visima 51, katika hivyo visima 51 visima 24 vimekamilika, na maeneo ambayo tayari yameanza kupata huduma hiyo ni pamoja na Mavurunza A, Kilungule A na B, King’ongo I, King’ongo III, Sandali, Mpogo, Mwemberadu, Mburahati, Kipunguni, FFU, Ukonga, Mongo la Ndege, Segerea, Chanika na Yombo, Saranga na Saranga II. Chang’ombe A, Ununio, Chang’ombe Toroli, Keko Magurumbasi na Keko Mwanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Mheshimiwa Kubenea uwe na uhakika matarajio yetu ni kwamba, ikifika mwaka 2017 maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam yatakuwa tayari yameshapatiwa maji.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tumekuwa tunapata taarifa za Serikali juu ya kuanza kwa mradi huu kila mwaka na hata mwaka 2014 tulipata taarifa hiyo, je, Serikali inaweza kutuambia katika bajeti hii ya mwaka 2016/2017 imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya kuanza kwa mradi huo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ilikuwa ni ahadi ya Makamu wa Rais kutupatia maji ya Ziwa Victoria katika maeneo ya Choma na Tarafa ya Simbo na iliombwa kwa madhumuni ya kuwa, moja tunakwenda kupata Wilaya mpya, lakini pili katika maeneo hayo tuna hospitali ya rufaa ya Nkinga ambayo inahudumia karibu mikoa mitano, je, Serikali haijaona haja ya kupeleka maji katika maeneo hayo yaliyoombwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa ujenzi wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda maeneo ya Nzega, Tabora na Igunga ulianza mwaka 2012 na inatarajiwa sasa katika mwaka mpya wa fedha unaokuja 2016/2017 taratibu zile za manunuzi zitakuwa zimekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri mradi huu unafadhiliwa na tayari mfadhili amesha-commit dola milioni 268.35. Kwa hiyo, uhakika wa fedha tunao. Kama nilivyojibu katika hoja ya msingi kwamba sasa hivi tumeshamaliza kutambua Makandarasi na tumepeleka kwa mfadhili Benki ya India kwa jili ya kupata no objection ili tuweze kuendelea na hatua nyingine ili ifikapo mwezi Julai mwaka huu tuwe tumeanza kazi ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli taarifa ipo, kwamba Mheshimiwa Makamu wa Rais aliahidi kupeleka maji Manonga, lakini kama nilivyosema kwamba mchakato huu ulianza mwaka 2012 na tukaanza kufanya usanifu na kipindi hicho wakati tunatengeneza memorandum tulikubaliana kwamba kwa maana ya mradi huu utakwenda kilomita 12 kila upande wa bomba litakapopita lile bomba kuu. Kwa hiyo, ahadi imekuja wakati taratibu hii iko nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, huu siyo mwisho, ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais tunayo, kwa hiyo, asubiri tuanze ujenzi. Wakati wa ujenzi tutaangalia tutakachofanya ili kuhakikisha kwamba, tunatimiza ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
(a) Naomba anieleze ni tatizo gani linalofanya Mji huu usipate maji ya kutosha na ya uhakika wakati vyanzo vya maji vipo?
(b) Pia ni lini wananchi hawa walioteseka kwa muda mrefu hasa wanawake watapata maji safi na salama? Nataka time frame, ni lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni matatizo gani yanafanya wananchi hawa wasipate maji. Ni kweli kabisa kwa bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge ni shahidi, katika Mikoa na Wilaya ambayo nilitembelea ni pamoja na Wilaya ya Nanyamba. Maeneo yale yana vyanzo vikubwa vya maji vya Mitema na Mkunya. Tatizo ni kwamba huko nyuma tulikotoka upatikanaji wa fedha ulikuwa kidogo siyo mzuri na kwa sababu tumekuwa tunaishi kwa kutegemea wafadhili vile vile. Hilo ndilo ambalo limefanya miradi ile isiweze kukamilika na kutoa maji yale yanayotakiwa kwa matumizi ya wananchi wa Nanyamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameuliza ni lini. Sasa hivi tumeingia kwenye program ya pili ya maendeleo ya maji ambayo tunatarajia Serikali inatenga fedha na tunaanza kutenga fedha kuanzia mwaka ujao wa fedha, pia wafadhili wametuahidi na kuna juhudi kubwa ambayo inafanywa na Serikali kupitia Waziri wa Fedha, lakini na Mwanasheria wa Serikali pia ambapo tunaongea na wafadhili waweze kutupatia pesa ili tuweze kukamilisha hii miradi ya Mito ya Mitema na Nanyamba ambayo itahakikisha kwamba vyanzo vya Mitema na Mkunya ili tuweze kuhakikisha maji yanapatikana kwa hizi Wilaya za Nanyamba pamoja na Tandahimba.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, anajua kwamba Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria unaanzia katika Kitongoji cha Ihelele, Kijiji cha Nyahumango. Cha kusikitisha Mheshimiwa Waziri, sina tatizo na maji kwenda Nzega, kwenda Kahama au sehemu nyingine, pale kwenye chanzo cha maji Ihelele penye matanki makubwa kuna kituo kimoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, hivi ungekuwa wewe ndiyo mwenye Jimbo hilo na una Waziri ungejisikiaje?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ningekuwa sijafanya ziara ningeshtuka sana, lakini kwa sababu sijawahi kwenda kwenye eneo hilo nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitaenda nikaone kwa nini vijiji ambavyo vinazungukwa na matenki makubwa ya maji havipati maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa ziara yangu Mkoa wa Mtwara, nilikwenda eneo la Mbwinji. Eneo la Mbwinji lina matanki makubwa sana ya maji ndiyo chanzo cha maji, kitu cha ajabu nilikuta wananchi wanaokaa lile eneo hawapati maji. Nilivyojaribu kuuliza ikaonekana kwamba maji pale yakishachotwa lazima yapelekwe Masasi kwenda kufanyiwa sasa utibabu, kuwekewa dawa ili yaweze kuwa safi kwa ajili ya matumizi ya binadamu, ndiyo baadaye sasa yaweze kusambazwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipofika pale niliagiza na sasa hivi wananchi wa maeneo yale tayari wanapata maji. Sasa sielewi hilo eneo analozungumza Mheshimiwa Mbunge, linaweza likawa na tabia ya kufanana na hiyo kwamba, hapo ndipo wanapochota maji, wanaweka kwenye matenki halafu baadaye yanakwenda kwenye mtambo wa kutibu maji. Sasa, japo sijafika lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili suala nitalifuatilia na nitamjibu kabla hatujamaliza Bunge hili.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Joseph Lusinde, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza Miradi ya Maji ya Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri, Halmashauri ya Chamwino inatekeleza miradi kwenye vijiji saba ambapo miradi katika Vijiji vitano vya Mvumi Makulu, Itiso, Mvumi Mission, Chamuhumba na Membe imekamilika na wananchi wapatao 49,000 wanapata huduma ya maji. Mradi wa Wilunze unaendelea kutekelezwa na upo asilimia 60.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi wa maji katika Kijiji cha Manzase umefikia asilimia 40. Kazi zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji, ujenzi wa nyumba ya mashine na ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 80,000. Gharama ya ujenzi wa mradi ni shilingi milioni 355, ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 71 kimeshapelekwa kwenye Halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Serikali itaendelea kupeleka fedha ili kukamilisha mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji katika Kijiji cha Chinoje ni kati ya miradi iliyokosa chanzo cha maji wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Program ya Maendeleo ya Maji. Utafiti wa chanzo kingine cha maji unafanyika na ujenzi wa mradi utafanyika katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Manzase wanakabiliwa na kero kubwa ya maji na Mkandarasi hayupo kwenye eneo la Site, je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kufika Manzase kwenda kuonana na wananchi na kuwahakikishia mwenyewe kwamba kweli mradi ule utakamilika?
Swali la pili, kwa kuwa Mradi wa World Bank, maeneo mengi maji yalipochimbwa vijijini hayakupatikana na wananchi wanaendelea kukabiliwa na shida kubwa ya maji. Serikali ina mpango gani wa kukamilisha miradi ya maji au Je, wananchi waendelee kusuburi tena, hawana mpango wowote Serikali mpaka Benki ya Dunia itusaidie tena? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Manzase, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi ni kweli Mkandarasi alikimbia na tayari tumeshafanya ufuatiliaji ni kwa nini alikimbia, tumemwagiza katika muda wa siku kumi arudi eneo la mradi, kama hatarudi basi tumeshapanga kuchukua hatua nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huo utakamilika kabla ya nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha tunaouanza mwezi Julai. Pia sina tatizo kwa ruhusa ya Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa sababu hapa ni Dodoma sina tatizo Mheshimiwa Mbunge, tunaweza kwenda huko tukawaambia wananchi ni lini huo mradi utakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Mheshimiwa ameuliza kwamba kuna miradi mingi ya World Bank ambayo ilifanyiwa kazi, lakini kuna maeneo ambayo maji hayakupatikana. Je ni lini sasa miradi hii itakamilishwa au tusubiri tena World bank?
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na Program ya kwanza ya Maendeleo ya Maji ambayo ilikwisha mwezi Desemba mwaka 2015, sasa tunaingia katika program ya pili. Maeneo yote yale tulikuwa tumeyapanga kwamba tunachimba maji, lakini katika kuchimba maji hayakupatikana, maeneo hayo mengi tumeshayafanyia utafiti, tumepata vyanzo vingine vya maji, kwa hiyo kuanzia bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja 2016/2017, tutahakikisha kwamba maeneo hayo tunatekeleza hiyo miradi ili wananchi waweze kupata maji.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kuanza kunipatia maji
katika vijiji vyangu vya Udadai, Ngiresi na Sokontuu. Swali langu ni kwamba, kumekuwa na tatizo kubwa la wizi wa maji maeneo mbalimbali nchini. Mfano, katika Jiji la Arusha asilimia 40 ya maji yanaibiwa; je, Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo hili kubwa la wizi wa maji. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali tayari imefanikiwa kupata fedha zaidi ya dola milioni 210 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika Jiji la Arusha. Mradi huo unaanza kutekelezwa katika mwaka fedha wa 2016/2017, utakuwa ni mradi wa miaka mitatu baada ya mradi huo kukamilika, Jiji la Arusha litapata maji asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Jiji la Arusha lina upungufu mkubwa wa maji lakini juhudi mbalimbali zinafanyika katika hiki kipindi kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia kuhusu upotevu wa maji, ni kweli upotevu wa maji upo kwa sababu miundombinu ambayo ipo ni ya zamani, kwa hiyo maji yanavuja na pili, hiyo element ya wizi nayo ipo. Mamlaka ya Maji ya Arusha inaendelea kufanya juhudi kupunguza upotevu wa maji na katika mradi unaokuja iko item ya kutekeleza hiyo kuhakikisha kwamba tunapunguza upotevu wa maji na tunatarajia kwamba upotevu utapungua mpaka kufika asilimia 30.
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini katika miradi miwili aliyosema imekamilika, mradi wa Nandembo na Nalasi tarehe 22 Julai, 2014, Rais wa Awamu ya Nne alifungua miradi ile, lakini cha kusikitisha hadi leo maji hayatoki katika miradi yote miwili. Je, yuko tayari kufuatana na mimi kwenda kuangalia miradi ile kama alivyosema imekamilika wakati maji hayatoki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mradi wa Mbesa umesimama kwa takribani kwa mwaka mmoja na nusu na vifaa viko pale, vina-hang hovyo bila usimamizi wowote. Je, ni lini Serikali itapeleka mkandarasi mwingine ili aweze kumalizia mradi ule?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, miradi miwili niliyoitaja amesema kwamba miradi hiyo haitoi maji. Nitafanya mawasiliano na Mkurugenzi wa Halmashauri husika ili aweze kutupatia maelezo kwa nini miradi hiyo haitoi maji ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakamilisha pale ambapo pamepungua kuhakikisha hiyo miradi inatoa maji. Pia kwa ridhaa yako, ridhaa ya Mheshimiwa Spika na Waziri wangu wa Maji na Umwagiliaji, hatuna matatizo kabisa, tukimaliza Bunge tunaweza tukaambatana naye ili kwenda kuangalia utekelezaji wa hii miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza kuhusu mradi wa Mbeso. Mradi huu ulikosa chanzo cha maji lakini kama mnavyofahamu Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tumeanza Programu ya Pili ya Maendeleo ya Maji ambayo imeanza Januari, 2016, baada ya kukamilisha programu ya kwanza. Ile miradi yote tuliyoi-earmark kwenye Programu ya Kwanza ambayo ilianza mwaka 2007 na haikukamilika ndiyo tutaanza nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika bajeti ambayo itasomwa na Mheshimiwa Waziri mwezi huu kwanza tunalenga kukamilisha miradi ambayo tulianza na haikukamilika na miradi ambayo pengine haikuanza lakini ilikuwa imependekezwa itekelezwe katika Programu ya Kwaza tutahakikisha kwamba miradi hii tunaikamilisha kabla hatujaenda kwenye miradi mipya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii miradi yote 11 katika Programu ya Pili tutahakikisha kwamba inakamilika kabla hatujaingia kwenye miradi mingine.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo kubwa sana la maji Wilayani Misungwi kwenye Kata za Mbarika, Nyangomango na Iyerere ambako chanzo cha maji cha Ziwa Viktoria kinapita maji yaendayo Shinyanga na Kahama. Je, ni lini Serikali itapitisha maji kwenye vijiji hivi ambavyo vinayaona maji tu yanapita, lakini wao hawana maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilikamilisha mradi wa kutoa maji Ziwa Viktoria kupeleka Shinyanga. Katika bajeti inayokuja ambayo Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji ataisoma, tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha upelekaji wa maji kwenye vijiji ambavyo vimepitiwa na hilo bomba kuu lakini havikuweza kupatiwa maji katika hiyo Programu ya Kwanza. Hii itakwenda sambamba na huu mradi ambao unaanza Shinyanga kuelekea Wilaya za Nzega na Mkoa wa Tabora na kwenda Igunga. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi, tunalifahamu hilo, sehemu zote ambazo hazijapatiwa maji kupitia mradi huo tutahakikisha kwamba tunaongeza vijiji ikiwemo vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge umevitaja.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduma ni lango kuu la nchi za Kusini na Kati mwa Afrika na kwa sababu Mheshimiwa Waziri amenihakikishia kwamba mradi mkubwa wa maji utajengwa kwenye Mji wa Tunduma lakini kuna mradi ambao ulijengwa mwaka 1973, mradi wa maji wa kutega kwenye Kijiji cha Ukwire ambapo ulikuwa unahudumia Kata za Mpemba, Katete na Chapwa na sasa hivi mradi ule hautoi maji ya kutosha. Ni lini Serikali itakwenda kukamilisha mradi ule wa Mpemba ambao unalisha kata tatu katika Mji wa Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mji wa Tunduma tayari study imeshafanyika kwa ajili ya kuweka mradi mkubwa wa maji. Tuna mfadhili ambaye ameshajitokeza, tunaongea naye, Serikali bado inafanya mazungumzo na yeye kwa sababu alikuwa amekuja na masharti ambayo yanaweza yasiwe na manufaa kwa upande wa wananchi wa Tunduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba moja, tunaweza tukapitia mradi huo mkubwa unaokuja, lakini pili ni kwamba mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano inahakikisha kwamba inakarabati miradi yote iliyokuwa imejengwa hapo awali ili kuondoa upungufu ukiwemo mabomba ya maji ambayo yamechakaa, mitambo ambayo imechakaa na vilevile kuongeza huduma kwa sababu kila kunapokucha watu wanaongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika programu hiyo tutahakikisha kwamba, hayo maeneo Mheshimiwa Mbunge ambayo anayataja nayo tumeyapitia ili kurudisha upatikanaji wa maji ambao umepungua kwa sasa na hasa kwa kuzingatia kwamba Mji wa Tunduma unapanuka sana. Nafikiri upunguaji huo wa upatikanaji wa maji ni kutokana na kwamba watu wameongezeka katika Mji wa Tunduma.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuwa inatekeleza mradi wa program ya maji kwa vijiji kumi kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na kuna baadhi ya Halmashauri hawakufanikiwa kupata hata anagalau vijiji vitano. Je, Serikali iko tayari sasa kutuletea taarifa ya kina ikionesha Halmashauri moja baada ya nyingine na taarifa hiyo ikionesha ni miradi mingapi imefanikiwa kwa kila Halmashauri ili tuweze kujua?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, tulianza Programu ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji mwaka 2006 na tumemaliza Awamu ya Kwanza mwaka 2015. Sasa hivi tumeanza Programu ya Pili ambayo imeanza mwezi Januari, 2015, kwa hiyo tunaendelea.
Mheshimiwa Spika, iko miradi ambayo hatukuikamilisha kwenye Programu ya Kwanza. Bajeti ambayo tumeitenga mwaka 2016/2017, itaanza kwanza kukamilisha ile miradi ambayo ilikuwa inaendelea, haijakamilika, lakini pili itaendelea na ile miradi ambayo imekuwa earmarked kwenye Programu ya Kwanza. Kwa hiyo, tutaingia mikataba na kuikamilisha, hiyo ndiyo Sera yetu tunaendelea namna hiyo, ikiwa ni pamoja na Jimbo la Mheshimiwa Mbunge. Pamoja na hilo ni kwamba tunayo orodha ya Wilaya zote, kwa hiyo, kama utahitaji upatiwe tutakapokuwa tumesoma bajeti Mheshimiwa Mbunge tutakupatia hiyo orodha.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo la usambazaji wa maji linalokabili mradi wa Mbwinji, Nachingwea, linafanana na tatizo la usambazaji wa maji wa mradi wa Makonde hususan chanzo cha maji Mitema. Kwa hiyo, nataka niulize, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati mkubwa ili Miji inayonufaika na mradi ule; Nanyamba, Kitangari na Tandahimba wapate maji ya kutosha.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili siyo swali dogo, ni swali kubwa la Mheshimiwa Chikota kuhusu mradi wa Mitema kupitia Mamlaka ya Maji ya Makonde.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Mheshimiwa Chikota unawahisha shughuli na wakati unajua kwamba mradi ule tumeutengea zaidi ya Dola milioni 84, mradi wa Makonde, fedha ambayo inapatikana kutoka Serikali ya India. Nikuhakikishie tu kwamba wakati wowote, inawezekana kwenye mwezi wa Saba au wa Nane fedha hiyo itakuwa imeshaidhinishwa na utekelezaji wa mradi wa Makonde na pamoja na vyanzo vya Makonde na Mitema vitafanyiwa kazi nzuri kukarabati ule mfumo wote wa maji tuhakikishe kwamba wananchi wa maeneo ambayo yako chini ya Makonde wanapata maji safi na salama.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Serikali katika kutatua upatikanaji wa maji hasa kwenye maeneo kame vijijini, imekuwa ikihamasisha kujenga miundombinu ya uvunaji wa maji kwa kutumia mapaa ya nyumba za Serikali, Asasi za Umma na nyumba za watu binafsi; na pia imekuwa ikitoa miongozi katika Halmashauri kutunga Sheria ndogo kwa ajili ya uvunaji wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimekuwa nikishuhudia uvunaji huu wa maji ya mvua katika paa, ukivunwa kwenye mabati yaliyopakwa rangi. Naomba niambiwe kama kuna matatizo yoyote yanayopatikana kutokana na maji yaliyovunwa toka kwenye mabati yaliyopakwa rangi.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Komanya, ameelezea vizuri kabisa kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba Halmashauri zinaweka Sheria ndogo ndogo na zinapitisha michoro kwenye ujenzi wa nyumba kuhakikisha kwamba kila nyumba inakuwa na kisima cha kuvuna maji kutoka kwenye mapaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la msingi ni kuhusu yale mabati yenye rangi. Mheshimiwa Mbunge nakushukuru kwa swali lako zuri. Rangi ikipakwa, baada ya siku 90 process ile ya oxidation inaondoa kabisa kemikali katika rangi,
kwa hiyo, baada ya miezi mitatu hata ukivuna yale maji yanakuwa hayana madhara ya aina yoyote. Kwa hiyo, wala hakuna wasiwasi wowote.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, hiyo elimu wale waopaka hizo rangi wanapewa kweli? Kama mvua ikinyesha kabla ya miezi mitatu!
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nielekeze Wakurugenzi kwamba wasimamie, kwasababu nchi yetu imegawanywa na katika mgawanyo huo, utawala uko katika Halmashauri na Halmashauri ina wataalam wote. Kwa hiyo, Wahandisi wote walio katika Halmashauri wasimamie suala hili la upakaji rangi kwenye mabati. Ni kweli upakaji rangi umekuwa unafanyika kwa jinsi mtu anavyopata hela yeye mwenyewe, lakini naomba kupitia Halmashauri, basi elimu itolewe kwamba rangi nayo ina sumu ila baada ya muda fulani ile sumu inaondoka. Kwa hiyo, elimu hii itolewe kwa wananchi pale ambapo wananchi wanataka kupaka rangi katika maeneo yao. Utaratatibu ndivyo ulivyo kwamba unapotaka kufanya ukarabati wa aina yoyote kwenye nyumba ni vyema uombe kibali ili uwe na usimamizi unaofaa.
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Sika, Mji wa Mkwajuni ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Songwe hatuna maji kabisa, hivi ninavyoongea ule Mji unakua, watu wanahamia kwa wingi sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura na kwa haraka tuweze kupata maji katika ule Mji ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya na Mkuu wa Wilaya atakuja hivi karibuni pamoja na Wakurugenzi na Watumishi wengine wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumeelekeza kupitia bajeti hii tuliyonayo kwamba tumetenga fedha katika Halmashauri ili Halmashauri zile ziweze kutekeleza miradi ya maji katika maeneo yao, lakini pia tumeelekeza kwamba Halmashauri zifanye utafiti wa kujenga mabwawa na wakishafanya utafiti walete taarifa Wizara ya Maji ili tuangalie katika mwaka wa fedha utakaofuata, tuweze kutoa fedha za kujenga mabwawa kuhakikisha kwamba miji yetu hii inakuwa na uhakika wa kupata maji, lakini kwa sasa Mheshimiwa Mbunge, ile fedha tuliyoitenga katika Halmashauri yako, naomba sana ushirikiane na Halmashauri ili ile fedha itumike katika kuhakikisha kwamba kwasababu ile Wilaya ni mpya, maji na upungufu utakaokuwa umejitokeza, basi naomba sana tuwasiliane.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:
Swali la kwanza, kwa sababu mradi huu unagusa Wilaya zaidi ya tatu, Wilaya ya Nachingwea, Wilaya ya Ruangwa pamoja na Wilaya ya Masasi, kiasi cha pesa ambacho kimetengwa ni shilingi bilioni moja. Mheshimiwa Waziri anaweza kuwa tayari kunitajia ni vijiji gani ambavyo vitaanza katika awamu hii ambayo imetengewa bilioni moja, hasa vile vinavyogusa Wilaya ya Nachingwea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningependa kujua, mwezi Februari mwaka huu Mheshimiwa Naibu Waziri tulifuatana mimi na yeye ndani ya Wilaya ya Nachingwea kwenda kukagua miradi ya maji ya Chiola, Nampemba pamoja na maeneo ya Mkoka. Miradi ile bado haijakamilika na yako mambo ambayo yamefanyika ambayo siyo mazuri, alituahidi ataleta wataalamu kwa ajili ya kuja kufanya uchunguzi ili tuweze kuchukua hatua za kisheria kwa hujuma iliyofanyika kwenye miradi ile.
Je, Mheshimiwa Waziri anatoa jibu gani kwa Wananchi wa maeneo haya ambayo nimeyataja ambao wanasubiri majibu yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa naibu Spika, swali la kwanza, ameuliza katika hii shilingi bilioni moja tuliyoitenga ni vijiji gani katika Wilaya ya Nachingwea ambavyo vitahudumiwa na hii fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji ambavyo vilikosa maji katika awamu iliyopita ikiwemo Kitandi Nakalonji, Mkotokuyana, tutahakikisha kwamba hivi vijiji katika hii fedha ambayo imetengwa mwaka wa fedha huu tunaouanza tarehe Mosi Julai, tuhakikishe kwamba vijiji hivi pia vinapitiwa. Pia, Mheshimiwa Mbunge atusaidie kuwasiliana na mamlaka ya maji safi MANAWASA ili wakasaidine pia kupanga vijiji vingine zaidi ambavyo vinaweza vikapitiwa na fedha hizi kupitia huu mradi wa maji wa Mbwinji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kweli nilitembelea Masasi Mkoa wa Mtwara na kwenda kujionea hii miradi ukiwemo mradi wa Chiola ambao nilikuta utekelezaji wake kidogo ulikuwa na mtatizo, baada ya kurudi niliwasilisha taarifa niliyoikuta kwa Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri tayarai alishatoa maelekezo kwa uongozi wa Wizara ili kuunda timu kwenda kuangalia nini kilichojitokeza katika ule mradi na kuhakikisha kwamba uboreshaji unafanyika ili wananchi wa Chiola waweze kupata huduma ya mamji safi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tumeelekeza kwamba miradi ile ambayo haikukamilika katika awamu ya kwanza, basi Halmashauri kwenye fedha tulizotenga katika Wilaya zihakikishe kwamba zinakamilisha ile miradi ambayo haikukamilika kabla hatujaingia kwenye miradi mipya.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Matatizo yaliyoko Kasulu na yale yaliyoko Bukombe yanafanana kwa kiasi kikubwa na kwa sehemu kubwa yanatokana na ucheleweshwaji wa upelekaji wa fedha za miradi ya maji. Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Bukombe juu ya maombi ya fedha, shilingi milioni 96 ambazo zimeombwa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji iliyoanzishwa? Ahsante.
MHE. NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dotto Biteko, umeomba shilingi milioni 96 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika Vijiji vya Ibambilo, Bukombe na Ikuzi. Katika bajeti ambayo tumeitenga kwenye Halmashauri, naomba sana Mheshimiwa Biteko kwamba tufanye ushirikiano na Halmashauri kuhakikisha kwamba tunatekeleza kwanza ile miradi iliyokuwa inaendelea, tukikamilisha ndiyo tunakwenda kwenye miradi mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama fedha haitatosha kama tulivyotoa ahadi katika Bunge hili, basi usisite, tufanye mawasiliano ili kuhakikisha kwamba mwaka wa fedha utaofuata tunaendelea kutenga fedha tena kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika. Nitoe taarifa kama ilivyotolewa na Mheshimiwa Waziri kwamba kwa kweli tunashukuru kwamba fedha inatolewa na juzi tena Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametupatia shilingi bilioni 15. Kwa hiyo, maeneo yote yale ambayo yalikuwa hayajakamilika, tunaendelea kuyakamilisha.
Butiama linafanana sana na swali lililoulizwa hapo nyuma; nataka kujua, kwanini maji kutoka Mgangu kwenda Butiama hayajafika, sasa ni kipindi kama miaka 20. Itatokea lini maji yafike pale Butiama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tunakamilisha usanifu wa mradi wa Mgango Kyabakari na tumeshaomba fedha kutoka Benki ya Maendeleo KFW kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, mradi huo utakapokuwa umekamilika utapita kwenye vijiji vingi. Mradi huu tunaukarabati; kwasababu ni mradi ambao upo, tunafanya ukarabati kuhakikisha kwamba tunasambaza maji maeneo mengi na tunaongeza chanzo cha upatikanaji wa maji.
Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu tunao tayari kwenye andiko na tukishamaliza usanifu, wakati wowote tunaanza kusambaza maji na tutarudi nyuma zaidi, tutaenda mpaka vijiji vya Byaiku Musoma, tutapitisha maji kule. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, mradi huu tunao.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba niulize swali moja la nyongeza. Mradi unaokusudiwa kujengwa au kukamilishwa Mbinga ni mradi mkubwa; na fedha zilizoainishwa ambazo zinatafutwa, Dola milioni 11.86 ni nyingi, zinaweza zisikamilike kwa wakati:-
Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kutengeneza mpanga wa dharura kwa kukarabati miundombinu ya maji ulioko sasa ili watu wa maeneo ya Frasto, Kipika, Masumuni, Lusonga, Mbambi, Bethlehemu, Luiko na Misheni waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimwambie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali tayari imeendelea na ujenzi wa miradi ya vijiji 10 katika Jimbo la Mbinga ambapo mpaka sasa kuna mradi mmoja wa Kigonsela ambao umekamilika na watu wanapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuna miradi ambayo inaendelea ikiwepo Kingirikiti, Mkako, Kihongo, na Litoha. Pia katika bajeti ya mwaka wa fedha tunaoanza tarehe moja mwezi wa saba, tumetenga shilingi bilioni 1.7 ambazo yeye mwenye Mheshimiwa Mbunge akirishikiana na Halmashauri yake, basi watapanga kuangalia vipaumbele maeneo yale ambayo ameyataja ili yaweze kupata huduma ya maji.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo hayajaweza kutia matumaini makubwa, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitenga fedha kwa bajeti ya 2015/2016 kwa ajili ya miradi ya kipaumbele na ya kilio cha muda mrefu cha wananchi hususani mradi wa maji katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Haydom ambayo inatumikia mikoa zaidi ya minne ikiwepo Manyara, Singida, Simiyu na kwingineko na ambayo hadi leo haijakamilika kutokana na kukosa fedha lakini pia ikiwepo na bwawa la maji la Dongobeshi ambacho ni kilio cha muda mrefu. Hata Mheshimiwa Rais alipopita wakati wa kampeni walimpa mabango na ni kilio cha muda mrefu kweli kweli na sasa mkandarasi ameacha hiyo kazi kwa sababu pia hajalipwa fedha zake. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu miradi hii ya kipaumbele cha wananchi na kilio cha muda mrefu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, miradi ya maendeleo ambayo inatengewa fedha kwa kipindi kilichopita huwa zile fedha zinakwenda kwenye dharura nyingine ambazo zinapangwa na Serikali kuliko fedha kwenda kwenye miradi iliyokusudiwa kama ilivyoidhinishwa na Bunge. Je, Serikali ina mikakati gani sasa kwa bajeti ya 2016/2017 kuhakikisha kwamba fedha zote zinakwenda kwenye miradi yenye kilio cha muda mrefu cha wananchi kuliko kwenda kwenye miradi ya dharura kama ambavyo ilikwenda kwenye miradi ya maabara kipindi kilichopita?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji ya Dongobeshi pamoja na bwawa la Dongobeshi, ni kweli kwamba miradi hii ilitambuliwa katika programu ya kwanza ya maendeleo ya sekta ya maji ambayo ilianza mwaka 2006/2007 na imekamilika mwaka 2015. Ilianza kutekelezwa na iko katika hatua mbalimbali lakini kutokana na matatizo kidogo ya fedha basi miradi hiyo haikukamilika kwa wakati. Tayari tumeshaanza kupeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo ya Dongobeshi na katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha na tumeelekeza kwamba kwanza lazima tukamilishe miradi ambayo ilikuwa inaendelea ndiyo tuanze miradi mingine mipya. Kwa hiyo, tutahakikisha tunashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba tunakamilisha miradi hii na hasa ule ambao utakuwa unapeleka maji kwenye Hospitali Teule ya Dongobeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli kabisa kuna miradi mingi ya kipaumbele ambayo ilishindwa kupelekewa fedha katika awamu iliyopita lakini Mheshimiwa Mbunge wewe mwenyewe ni shahidi kwamba mwaka 2015 Serikali ilikuwa na majukumu mengi sana na yalikuwa ni majukumu yale ya muhimu kama vile suala la uchaguzi, kulikuwa na suala la kutengeneza Katiba, hivi vitu ni vya muhimu, ndiyo uhai wa nchi kwa hiyo fedha ilipelekwa kwenye maeneo haya. Nikuhakikishie kwamba kwa sasa majukumu hayo yameshakamilika na tayari tumeongeza ukusanyaji wa fedha. Kwa hiyo, miradi yote ambayo ilikuwa imeainishwa na kupewa kipaumbele tutahakikisha kwamba inakamilishwa.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mji wa Korogwe unapitiwa na Mto Pangani katikati ya mji, je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kwa kuutumia mto ule kuwapatia watu wananchi wa Mji wa Korogwe maji hasa ikizingatiwa kwamba wana shida ya maji, wanaangalia mto lakini maji hawayapati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatekeleza mradi wa HTM na tayari tumeshaahidiwa fedha kwa wafadhili na usanifu wa mradi huo umekamilika. Bahati nzuri ni kwamba usanifu huo utachukua maji kutoka Mto pangani tena karibu kabisa na eneo la Korogwe.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nakuahidi kwamba wakati tunachukua maji kutoka katika Mto wa Pangani hatuwezi kuacha kupeleka maji sehemu yenye chanzo. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba eneo la Korogwe pia litapatiwa maji kutokana na huo mradi wa HTM.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini napenda kujua, kwa sababu maendeleo hayana utengemano yaani ni maendeleo kwa jumla bila kujali mipaka na itikadi ya kisiasa, miradi hii inakwenda kwa wananchi wote. Baada ya kutandaza mabomba mpaka maeneo ya Kishapu, je, mradi huu mnaweza kuupeleka mbele zaidi hadi vijiji vya Mwamashindike mpaka Lalago wakapata maji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wilaya ya Maswa nayo inasubiri Mradi wa Maji ya Ziwa Viktoria ambao utakuja katika phase two ya ule mradi wa maji kutoka Lamadi. Je, Wizara ina mpango gani kuwasaidia wananchi ambao hawana maji hivi sasa kwa kutumia mabwawa yaliyopo katika Wilaya ya Maswa kwa mfano Bwawa la Sola, Nyangugwana, Mwantonja kwa kuyasafisha na kuyafanya kuwa chanzo cha maji katika Wilaya ya Maswa ili wananchi waweze kupata maji kwa sasa wakati wanasubiri mradi wa Ziwa Viktoria ukamilike? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stephen Nyongo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, mwenyewe amesema kwamba miradi hii haina mipaka ndiyo maana tunatoa maji kutoka Ziwa Viktoria Mwanza yanakuja Shinyanga yatafika mpaka Tabora yatakuja mpaka Singida. Kwa hali hiyo, vijiji alivyovitaja kama ile pressure itaweza kufika tutaweza kuvifikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, amezungumzia kuhusu Wilaya ya Maswa ambayo itafikiwa na awamu ya pili ya mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria lakini kwa hatua za dharura, tufanye nini kwenye mabwawa? Tumetenga fedha kwenye halmashauri zote, zihakikishe kwamba zinapeleka fedha hizo kwenye miradi ya kipaumbele ambayo itahakikisha kwamba wananchi wanapata maji kwa uharaka.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuiuliza Serikali, hii miradi yote ya mwaka 2015/2016 ambayo tunaendelea nayo ambayo fedha zake hazijaenda kwa mfano Babati Vijijini na zimebaki siku kumi, je, kipindi hiki cha bajeti cha 2017 mbali na hii pesa iliyotengwa, hii ya nyuma yote tutapatiwa ili ile miradi ambayo haijatekelezwa itekelezwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Jitu Soni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kushukuru Ofisi ya Wizara ya Fedha wamefanya kazi nzuri, wamekusanya fedha na wanatupatia na hata wiki iliyopita walitupatia zaidi ya shilingi bilioni 15. Katika Bunge hili nimekuwa nikiagiza kwamba Waheshimiwa Wabunge wawaambie Wakurugenzi wa Halmashauri yeyote aliye na hati mkononi ailete ili tuweze kulipa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jitu Soni kama kuna certificate, sijui kwa siku hizi zilizobaki itawahi kwa sababu tarehe 26 ni mwisho, inabidi tuwe tumeshamaliza kulipa lakini hata hivyo wala usiwe na wasiwasi hata ukichelewa kama certificate ipo naomba ije ili tuweze kulipa. Nikuhakikishie kwamba miradi yote ambayo ilikuwa haijakamilika Mheshimiwa Jitu Soni tutahakikisha kwamba tunaikamilisha.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Mpanda Vijijini lina miradi miwili ya umwagiliaji. Mradi wa kwanza ni ule wa Karema ambao Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo lakini bado haujakamilika na mradi wa pili ni ule wa Mwamapuli ambao unamwagilia vijiji vya Kabage. Miradi yote hiyo haijaweza kukamilika kwa wakati. Je, ni lini Serikali inaweza kukamilisha miradi hiyo ili iweze kuwasaidia wananchi ili kutopata hasara kwa fedha za Serikali ambazo zimeshatumika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumzia kuhusu miradi ya umwagiliaji, ni kweli kabisa kwamba kumekuwa na miradi ya umwagiliaji katika eneo hilo lakini baadhi ya miradi hiyo ilipata matatizo kidogo na tumeagiza kuifanyia kazi. Kwa sababu ya masuala yaliyotokea siwezi kumjibu sasa hivi, ripoti ikija naweza kumfahamisha. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba yale matatizo yote yaliyojitokeza yanatatuliwa na tuhakikishe kwamba tunakamilisha ile miradi ili wananchi waweze kutumia miradi ile ya uwagiliaji wazalishe zaidi tuweze kupata chakula.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namshuruku Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye matumaini kwa wananchi wa Mombo lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu sasa hivi una muda mrefu na tatizo la maji la Mombo ni la muda mrefu na wananchi wameanza kukata tamaa; na kwa kuwa halmashauri mbili zilishakubaliana, ya Bumbuli na Korogwe kwamba maji yale yapitie katika vile vijiji vinavyolinda chanzo cha maji, ni wakati gani wananchi wale wa Korogwe Vijijini na Bumbuli wataanza kupata maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa hivi Serikali imetutengea shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya mradi wa maji wa Korogwe Vijijini; kuna mradi wa maji wa Bungu, mradi huu hatukuwa tunatumia hela za Serikali, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yalitumia hela zao kukamilisha mradi huu ambao ulikuwa ni kwa ajili ya vijiji saba. Kati ya vijiji hivyo saba vijiji vinne tu ndivyo vimepata maji. Serikali iliombwa shilingi milioni 410 ili mradi huu ukamilike lakini mpaka sasa hivi hela hiyo haijapatikana. Vijiji ambavyo vimekosa ni Mlungui, Kwemshai na Ngulwi. Naomba sasa Serikali mtenge hela za dharura ili tukakamilishe mradi huo ambao haukutumia hela za Serikali, ni mashirika binafsi yaliamua kujenga mradi huo. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nganyani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza linaonesha Mheshimiwa Mbunge unawapenda wananchi wako na unataka hatua za haraka kuhakikisha kwamba wanapata maji. Wizara ya Maji na Umwagiliaji, wewe mwenyewe Mheshimiwa Mbunge na halmashauri yako naomba tushirikiane, tukutane ili tuone tunafanyaje kuhakikisha kwamba tunachukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na fedha ambazo umetengewa katika bajeti inayoanza Ijumaa tarehe 1 Julai, kuhakikisha wananchi watapata maji kwa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali namba mbili, kuhusu Mradi wa Maji wa Bungu ambao umefadhiliwa na marafiki zetu lakini hawakuukamilisha. Katika vijiji vilivyotarajiwa ni vijiji vinne tu ambavyo vimepata maji vingine bado, tufanyeje?
Naomba pia hili tushirikiane, Mkurugenzi wa Halmashauri atuletee taarifa. Tumeahidi katika bajeti inayokuja, miradi yote iliyokuwa inaendelea, ili mradi tu ililenga kuwapatia wananchi maji, hata kama ilikuwa inafanywa na wewe mwenyewe na umefikia ukomo tupe taarifa Serikali itatoa hela ili tuweze kukamilisha miradi hiyo wananchi wapate maji.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa na mimi nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hali iliyoko katika Mji wa Mombo inafanana kabisa na hali katika Mji wa Mafinga ambao unakua kwa kasi na kwa kuwa Mamlaka yetu ya Maji ya Mji wa Mafinga ni ile ambayo ni ya class C, kwa hiyo haijaweza kuwa na uwezo wa kuhudumia maeneo makubwa ya mji. Je, Serikali iko tayari kutusaidia watu wa Mafinga hasa katika Kata za Bumilayinga, Isalavanu na Lungemba japo kuchimbiwa visima?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Chumi, Mbunge wa Mafinga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikupongeze Mheshimiwa Chumi kwa sababu mara nyingi umekuwa unawasiliana na Ofisi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhusu kuwapatia maji wananchi wa Mji wa Mafinga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba category ya Mamlaka ya Maji ya Mafinga ni C ambayo inahitaji kupewa msaada na Wizara. Nikiri kabisa kwamba tayari kuna deni la shilingi milioni 150 kwa ajili ya kulipia TANESCO ili umeme uendelee ku-pump maji kupeleka kwa wananchi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Chumi kwamba Wizara ya Fedha kwa sasa imeweka utaratibu, itakuwa inalipa madeni hayo ya maji moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu hoja ya pili ya kuchimba visima tuko tayari, Mheshimiwa Mbunge tushirikiane. Kuna hela tuliyokutengea kama itakuwa haitoshi basi ulete taarifa ili tuweze kutenga hela nyingine tuhakikishe hivyo vijiji ambavyo havijapata visima viweze kupata visima.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri, kumekuwana kisingizio kikubwa cha sababu ya ucheleweshaji wa fedha kwa kutokukamilika kwa miradi mingi na kupelekea wakandarasi kudai kwamba wanalipwa kidogo kidogo. Kwa mfano, miradi ya maji ambayo iko katika Kijiji cha Ipalamwa, Kitoho, Ilamba na sehemu nyingine. Sasa Serikali inasemaje, nani wa kuchukuliwa hatua, ni Halmashauri husika au Mkandarasi ambaye ameshindwa kumaliza mradi kwa wakati na ubora?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zinapelekwa kulingana na certificate ambayo mkandarasi ameiwasilisha Halmashauri na imefanyiwa tathmini na imewasilishwa Wizara ya Maji ndiyo tunapeleka fedha kulingana na kiwango cha uzalishaji ambacho Mkandarasi amezalisha. Kwa hiyo hapo, Wakurugenzi wanaagizwa kuwasukuma wakandarasi waweze kuzalisha zaidi ili Serikali iweze kutoa fedha zaidi.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ucheleweshaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo limejitokeza kwenye Jimbo la Mwibara ambako Miradi ya Maji ya Bulamba, Kibara pamoja na maji ya Mji wa Bunda kutoka Nyabehu, zaidi sasa ya miaka saba, fedha bado zinacheleweshwa kwenda. Hili ambalo analisema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, lazima certificate zile ziandaliwe na zihakikiwe, sisi Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kushirikiana na Engineer ya Maji wa Wilaya, tulishasukuma sana hizi certificate na kuna mabarua mengi Wizara ya maji. Sasa je, Mheshimiwa Naibu Waziri ataliambia vipi Bunge hili kwamba hata zile certificate ambazo zilishahakikiwa bado fedha haziendi, ni uzembe wa Wizara au ni uzembe wa mtu gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane moja kwa moja, aje ofisini kwa sababu sina taarifa kwamba kuna certificate ambayo haijalipwa. Juzi Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametoa bilioni 15 na certificate zote zimelipwa, sina pending certificate ambayo imebaki kwenye ofisi ambayo haijalipwa. Kwa hiyo, kurahisisha kazi Mheshimiwa Mbunge, naomba awasiliane na mimi ili tuweze kuangalia ni nini kimetokea.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Katika Jimbo langu la Ulanga kuna mradi mkubwa wa maji wa Mahenge Mjini ambao tayari umeshakamilika. Tatizo la huo mradi umeshindwa kuanza kwa kuwa tu, Idara ya Maji haina mita za kuwafungia wateja, kwa kisingizio cha fedha zikipatikana, fedha zikipatikana. Je, ni lini Serikali itapeleka pesa ili Idara ya Maji iwafungie mita wananchi wa Mahenge Mjini ili waanze kufaidi matunda ya Mbunge wao kijana machachari?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetekeleza mradi na mradi ule umekamilika; kilichobaki ni mita. Sasa naomba anisaidie awasiliane na Halmashauri kuna tatizo gani, hatuna taarifa kwamba wana hilo tatizo la mita, watuletee taarifa. Hata hivyo, katika Mwaka huu wa Fedha tumemwekea bajeti, kwa nini wasiangalie hiyo bajeti ili wakaweza kufunga mita, halafu waendelee kupata mapato. Kwa sababu najua kwamba wananchi watakuwa wanapata maji, lakini tatizo Halmashauri haipati mapato. Kwa hiyo, kwanza Mheshimiwa Mbunge aangalie bajeti ambayo tumempatia, kama haitatosha, basi tuwasiliane ili tuweze kuliondoa hili tatizo la mita.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba niulize kwamba, kuna vijiji katika Kata ya Matola na Kata ya Uwemba katika Jimbo la Njombe Mjini; Kijiji cha Mtila na Kijiji cha Kilenzi. Vijiji hivi vinazalisha maji kwa ajili ya vijiji vya jirani kwa sababu vyenyewe viko juu ya mwinuko lakini vyenyewe kama vijiji havina maji kabisa. Je, Serikali iko tayari kutuchimbia visima virefu katika vijiji hivi viwili ili kusudi wananchi hawa wanaozalisha maji na kutunza mazingira waweze na wao kufaidi maji hayo.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJ: Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu tu kwamba, Serikali ipo tayari, ndiyo maana imemtengea bajeti, ni suala la yeye Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri yake kuweka kipaumbele ili waweze kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo maji yanatoka, basi wao wawe wa kwanza kupata maji, waweke vipaumbele, wachimbe visima, watakapokuwa wamefikia, bajeti mwakani inaanza; huu ndio mwaka wa kwanza tunaanza na tutaendelea kutenga bajeti, kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata maji.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ningependa sasa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, katika Mji wa Lindi Manispaa, kumetokea tatizo la dharura kubwa sana katika wiki hii. Wananchi wamekosa maji, wanahangaika na visima ambavyo vilikuwa vinatoa maji pale Kitunda kuleta mjini, visima viwili pampu zimekufa na kisima kimoja kimebomoka. Wananchi wanahangaika sana, ningependa kujua Serikali itatusaidiaje ili ku-solve tatizo hili la maji, wananchi waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli muda mrefu tumekuwa tunapata matatizo kwa wananchi wa Mji wa Lindi kupata shida ya maji kutokana na setup ya miundombinu jinsi ilivyo. Kwa sababu visima viko ng‟ambo ya pili vinazalisha maji, mabomba yanapita chini ya bahari, halafu yanaleta maji kwenye Mji wa Lindi, yakitokea mawimbi, yale mabomba yanakatika. Kwa hiyo, Mji wa Lindi unakosa maji na ndiyo maana Serikali ilikuja na mradi mkubwa ule wa Ng‟apa ambao ukikamilika sasa matatizo katika Mji wa Lindi yatakuwa yamekwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa sina taarifa, lakini kwa taarifa hii, leo baada ya saa saba nitafuatilia ili kujua tunafanya nini na nitampatia majibu Mheshimiwa Mbunge.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Tatizo la maji la Halmashauri ya Makambako linafanana kabisa na tatizo lililoko Halmashauri ya Nyang‟hwale. Kumekuwa na miradi mingi ya usambazaji wa maji kutoka Ziwa Victoria, leo takribani miaka minne, miradi hiyo haisongi mbele kwa sababu ya ukosekanaji wa pesa. Je, Waziri anatuambia nini wananchi wa Nyang‟hwale, kuhusu miradi hiyo kwamba itaendelea kwa kasi ili tuweze kupunguza tatizo la maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, ndiye ambaye amekuwa ananipa nyaraka nyingi kutoka kwenye Halmashauri yake na ndiye ambaye alinikabidhi hata ile barua ambayo nilikuja kugundua kwamba mwaka 2013, Wizara ilitoa waraka kuhusu utekelezaji wa bajeti katika Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili tatizo la Nyang‟hwale linafanana na maeneo mengine pia, inawezekana kuna matatizo pia katika Halmashauri ya Mheshimiwa Mbunge, lakini kwa utaratibu tuliouweka sasa kama miradi ipo na uzalishaji upo, wakileta certificate tunalipa pesa; lakini tumegundua kuna maeneo ambayo uzalishaji umekwama kwa matatizo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Wizara ya Maji, tukishirikiana na Mheshimiwa Mbunge tutapeana taarifa, ili tuweze kuona ni nini kimekwamisha na kwa bahati nzuri tuko humu humu ndani kwenye Bunge. Nakumbuka Mheshimiwa Mbunge Lusinde kwake kulikuwa na shida, lakini tumeitatua na sasa hivi mradi unaendelea vizuri. Kwa hiyo, tupeane tu taarifa kuna tatizo gani ili tuweze kuiangalia Halmashauri. Pengine ndani ya Halmashauri kuna uzembe, tutauondoa ili kuhakikisha hii miradi inatekelezeka na hasa kwa kuzingatia kwamba sasa fedha inatolewa. Kwa hiyo, hakuna sababu kabisa kwa nini mradi usitekelezwe.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, kwanza nianze sana kwa kumpongeza Rais John Pombe Magufuli, Waziri wa Maji, Naibu Waziri wa Maji, pamoja na wataalam wa Wizara hii, kwa namna walivyotutengea bajeti ya Wizara ya Maji katika Halmashauri yetu ya Makambako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu wametutengea fedha nzuri, hasa ukizingatia za mradi mkubwa ule wa Makambako ambao kwa muda mrefu wananchi wa Makambako wamekuwa wakipata tabu sana juu ya kupatikana kwa maji. Anawaambia nini wananchi wangu wa Halmashauri ya Makambako, kwamba baada ya kutenga bajeti ile mwaka wa fedha unaanza keshokutwa, ili fedha zile ziweze kwenda kujenga mradi ule mkubwa lakini ukiwepo pamoja na Kijiji cha Kiumba, Mutulingara yenyewe pamoja na Ikelu na vijiji vingine ambavyo vimekosa maji. Ni lini sasa fedha hizi tulizozitenga zitakwenda? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Makambako tuna Bodi ya Maji, kwa muda mrefu Halmashauri ilishapitisha majina ya kuja katika Wizara, mwaka mmoja na nusu sasa Bodi ya Makambako haijateuliwa katika vyombo vinavyohusika. Sijajua ni TAMISEMI au ni Wizara ya Maji. Je, ni lini sasa mtateua ili watu hawa waendelee kufanya kazi katika Bodi ya Mji wa Makambako?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge Sanga, ameshukukuru kwamba tumemtengea milioni 992.8, lakini anasema sasa nini kinafuata. Kinachofuata ni utekelezaji wa hiyo bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia mafaili, mwaka 2013 Wizara ilitoa mwongozo na ikatoa kibali kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri kwamba, baada ya kupata bajeti wanatakiwa kufanya taratibu za manunuzi na kusaini mikataba, lakini nakala ya mikataba walete Halmashauri. Hapo katikati kulitokea tatizo kidogo, tayari nimeshamwagiza Katibu Mkuu, aweze kutoa mwongozo mwingine, tutashirikiana pamoja na Hazina ili sasa utekelezaji wa hii bajeti ambayo imepitishwa, Waheshimiwa Wabunge, Wakurugenzi wa Halmsahauri wapewe mwongozo jinsi ya kufanya. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba suala hili tunalifanyia kazi, kwa ajili ya kutoa mwongozo kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la la uteuzi wa Bodi, tunatumia sheria namba 12 ya mwaka 2009. Zipo Bodi ambazo zinateuliwa na Wizara ya Maji, lakini zipo Bodi ambazo zinateuliwa na TAMISEMI. Kwa hiyo, hili nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nitalifuatilia ili tuweze kujua sasa nini kinafanyika na tuweze kuona ni wapi pamekwama Bodi yake haijateuliwa.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na kwa kuwa natoka pia katika Mkoa wa Arusha, pamoja na Mkoa huu wa Arusha kuwa na vyanzo vingi vya maji, vinavyotoka katika Mlima Meru, lakini maji haya yameonekana kuwa na madini ya fluoride na madini haya ya fluoride siyo mazuri sana. Je, Serikali inafanya jitihada gani, kuhakikisha kwamba inapunguza madini haya ya fluoride?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Mji wa Arusha katika vile visima ambavyo vinatumika kutoa maji katika Mji wa Arusha, kuna visima ambavyo vimeonekana vina kiwango kikubwa cha maji ya fluoride na visima hivyo viko Mianzini viko viwili. Tulipunguza kiwango cha utoaji maji katika hivyo visima na tukachimba visima vingine viwili ili ku-balance ile fluoride isiwe kwa kiwango kikubwa; ni kwamba fluoride inatakiwa katika mwili wa binadamu lakini kiwango kisiwe juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo suala tayari tumeshalifanyia kazi kwa ku-balance, fluoride yake siyo nyingi sana kiasi ambacho ukiichanganya na maji mengine, basi inaingia katika viwango vile vinavyokubalika. Pia naomba kumweleza Mheshimiwa Mbunge Mollel ni kwamba sasa hivi Arusha tuna mradi mkubwa, tunatarajia kuchimba visima 30 ili kuhakikisha kwamba kiwango cha maji katika Mji wa Arusha baada ya miaka miwili kukamilisha huo mradi, ambao tumepata fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na financial agreement imeshasainiwa, tatizo la maji tutakuwa tumelimaliza kabisa katika Mji wa Arusha.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo yaliyoko Longido yanafanana kabisa na ya mkoani kwangu Mkoa wa Kagera Wilaya ya Bukoba Vijijini, Kata ya Maruku na Kanyangeleko ambapo kumekuwa na mradi mkubwa wa maji uliojengwa tangu miaka ya 60 mpaka 70 na mradi huu uliweza kufanya kazi kwa miaka 10 na uliwahudumia wananchi wengi. Mradi huu tayari una vyanzo, una matenki, kinachohitajika katika mradi huu ni ukarabati. Je ni lini mtaukarabati mradi huu ili uweze kuwahudumia wananchi wa Bukoba Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze anasoma historia, mama huyu anawapenda wananchi wa Kagera na kwa sababu ni mama anahusika na kuchota maji, kwa hiyo uchungu wake anaujua. Amesoma historia miaka ya 60 na 70 kwamba mradi huu ulijengwa na kuwahudumia wananchi kwa muda wa miaka 10, lakini sasa hivi ni kwamba umechakaa unataka ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa taarifa hii na nimwagize Mkurugenzi wa Maji wa Kagera aweze kuangalia na Mheshimiwa Rweikiza ameshaniambia kuhusu mradi huu na nimeshawaagiza Wakurugenzi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, waende wakauangalie mradi huu kuona unahitaji nini ili tuweze kuufanyia ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba katika awamu ya pili ya maendeleo ya sekta ya maji, tunataka kuhakikisha kwamba miradi yote ya zamani inafanyiwa utafiti na tunaikarabati ili iendelee kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokuwa inatarajiwa.

WAZIRI OFISI YA RAIS TAMISEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwa majibu mazuri sana, yanayohusiana na masuala ya maji. Hata hivyo, nataka niongezee tu kwenye jibu hilo juu ya swali liloulizwa na Mheshimiwa Bulembo, ambaye amezungumzia juu ya miradi ya maji iliyojengwa miaka mingi na ilikuwa imefanya kazi kwa ufanisi, lakini leo hii ama imechakaa, ama miundombinu yake haitoshelezi idadi ya watu iliyoongezeka ama vijiji vilivyoongezeka na kwa hivyo inashindwa kumudu na watu wanapata shida ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, kwa ujumla wetu, sisi ndio wenye Majimbo na tunatoka kwenye maeneo haya, kama miradi hii haitabainishwa na kuorodheshwa kwenye mipango ya Halmashauri ya kila mwaka, siyo rahisi sana Serikali ikaweza kuitekeleza. Serikali inaamua mambo yake na kupanga na kuyatekeleza kupitia kwenye bajeti. Sasa kama haisomeki kwenye bajeti siyo rahisi kuiona na hata mimi ambaye kwa kushirikiana na Wizara ya Maji tunatekeleza miradi mbalimbali, kwa namna ambavyo tunaletewa na Halmashauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo la kwanza ni kuiweka kwenye mipango ya maendeleo au ya kwenye bajeti, ikisomeka hivyo inakuwa rahisi kuiona, lakini pia kuitengea fedha na kuikarabati miradi hii. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwenye bajeti inayokuja, miradi yote ile iliyochakaa muiweke kama kipaumbele cha miradi ya kukarabatiwa, siyo miradi mipya, miradi ya kukarabatiwa, ili Wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Maji tuweze kukaa na kuona kama tuje na mpango gani, au program gani ili tuweze kuitekeleza miradi hii.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa sababu tatizo la Mpwapwa linalingana kabisa na tatizo kubwa la Makambako. Mji wa Makambako una wakazi wengi zaidi ya laki moja, na tatizo la maji ni kubwa sana. Wananchi wa Mji wa Makambako alipopita Mheshimiwa Dkt. Magufuli kipenzi chao na kipenzi cha watanzania, walimueleza tatizo la maji katika Mji wa Makambako, kuna mradi ambao ulishasanifiwa wenye gharama ya zaidi ya bilioni 57, na Waziri wa Maji ambaye yupo sasa alikuwepo siku hiyo wakati anaahidi.
Je, sasa tatizo hili la mradi mkubwa wa bilioni 57 litatatuliwa lini ili wananchi wa Makambako waendelee kupata maji.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Sanga kwa ufuatiliaji wake. Maana yake pamoja na kufuatilia miradi midogo midogo ya Halmashauri ya Makambako, lakini bado kumbe amesoma na nyaraka za mradi mkubwa unaolenga kutoa maji Mto Tagamenda, kuhakikisha kwamba maji yanapatikana katika Mji wa Makambako. Lakini nikufanyie marekebisho kidogo kwamba, mradi huo unatarajia kugharimu dola milioni 32.9 na Serikali yako Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo mwenyewe uliwashawishi wananchi wako wameichagua, ilipeleka andiko Serikali ya India, na nisema tu kwamba Mheshimiwa Sanga unawaisha shughuli, tunatarajia ifikapo tarehe 15 mwezi Julai, mwezi tunaouanza kesho kutwa mambo yanaweza yakaiva kutoka Serikali ya India na tayari tukaanza na taratibu ya kutekeleza huo mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nikuhakikishie pamoja wananchi wa Mji wa Makambako, na hasa kwa kuzingatia kwamba ndugu yangu Sanga wewe ni shemeji yangu, kwa hiyo maji utapata.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii.
Matatizo ya Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mpwapwa yanafanana na matatizo ya Mamlaka ya maji ya Mji wa Mwanuhuzi. Mradi wa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mwanuhuzi ulikamilishwa mwaka 2009 na ukakabidhiwa katika Mamlaka ya Maji Mwanuhuzi. Mradi huu ulilenga kusambaza maji katika vijiji Nane lakini ni vijiji Vitatu tu vilisambaziwa maji; na kusababisha qubic mita za ujazo wa maji, ambayo yanatumika ni moja ya tatu tu, na hivyo gharama ya uendeshaji katika Mamlaka ya maji kuwa juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishiriki katika Bajeti ya mwaka huu...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, naomba uulize swali tafadhali.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri haikuwa na fedha kwa ajili ya upanuzi wa mradi huu, kwa sababu fedha iliyokuwepo ilikuwa ni kwa ajili ya Mkandarasi mshauri wa vijiji 10;
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kusambaza maji katika vijiji vilivyobaki vya Bulyanaga, Mwambegwa, Mwagwila, na Mwambiti ili wananchi waweze kunufaika na mradi huu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze yeye ni Mama anajua matatizo ya maji, kwa hiyo ufuatiliaji wake ni kwamba unamgusa moja kwa moja. Ametoa taarifa kwamba kuna mradi ulikamilika lakini umehudumia vijiji vichache. Mheshimiwa Leah Komanya, naomba sana ushirikiane na Halmashauri; kwa sababu mwaka huu tumetenga fedha kwa kila Halmashauri, kuhakikisha kwamba hayo maeneo ya vijiji yaliyokuwa yamekosa kupata maji basi muhakikishe kwamba nayo yanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kama kuna tatizo la utaalam, Mheshimiwa Komanya, naomba utakapokuwa umefika kule na mmepata shida ya wataalam basi tuwasiliane ili tuweze kushirikiana kuleta wataalam atuweze kufikisha huduma hiyo hapo. Suala la nyongeza ni kwamba hii Mwanuhuzi iko Mkowa wa Simiyu, na Mkoa wa Simiyu tuna mradi mkubwa ambao utachukua maji kutoka ziwa Victoria, usanifu sasa umekamilika; na wakati wowote tutakamilisha taratibu ili kuhakikisha kwamba Mkoa wote wa Simiyu sasa tatizo la maji tunaliondoa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Kwa kuwa, matatizo yaliyoko Mpwapwa yanafanana sana na matatizo yaliyopo katika Jimbo langu la Itigi. Watu wanaenda kilometa nyingi sana kufuata maji hasa katika vijiji vya Rungwa, Kintanula, Kalangali, Mitundu, Chabutwa na Mabondeni;
Je, Serikali itasaidiaje kutatua tatizo hili katika Jimbo la Manyoni Magharibi;
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha program ya utekelezaji wa maendeleo ya maji, iliyodumu kuanzia mwaka 2006/2007 mpaka 2015. Sasa hivi tumeingia katika program ya pili. Huu ni mwendelezo wa kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanapata huduma ya maji iliyo safi na bora, na kusogeza huduma ya maji iwe karibu ili akina mama wasitumie muda mrefu kupata maji.
Mheshimiwa Yahaya Masare nikuhakikishie kwamba tunaendelea na kama ambavyo umeona katika Bajeti ya mwaka huu tumehakikisha kwamba kila Halmashauri imetengewa fedha, tutaendelea kupeleka wataalam na tutasimamia tuhakikishe kwamba fedha hii inatumika. Sheria ndogo ndogo imepitishwa tumeweka value for money, tuhakikishe kwamba hela iliyopelekwa inafanya kazi nzuri na kuhakikisha wananchi wanapata maji.
Hivyo, nikuhakikishie kwamba tutatenga fedha kila mwaka, kuhakikisha kwamba wananchi wako wa maeneo hayo mpaka ya Rungwa wanapata maji.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona, naomba na mimi niulize swali dogo la nyongeza;
Kwa kuwa, Mji wa Manyoni ni mkongwe ni sawa na ule wa Mpwapwa na matatizo ni makubwa, mitambo ya maji iliyopo sasa hivi imezeeka sana. Sasa hivi inakisiwa kwamba asilimia 35 tu ya wananchi wa Manyoni ndiyo wanapata maji na asilimia 65 hawapati maji;
Je, Serikali inatoa kauli gani ya matumaini kwa wananchi wa ule Mji wa Manyoni Mjini, kwa sababu shida ya maji ni kubwa. Maeneo ya Sayuni, Mwanzi, Kipondoda, Mgulang‟ombe, Mwembeni, Manyoni Mjini, Majengo hali ni mbaya akina mama wanapata shida sana, Serikali ina kauli gani kuhusu shida hii ya maji katika Mji wa Manyoni. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIJAI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumeishaelekeza kwamba sasa hivi katika awamu ya pili ya program ya maendeleo ya maji, tutahakikisha kwamba miundombinu ya zamani inafanyiwa utafiti, tunatoa fedha na tunakarabati ili mfumo wa maji ule uweze kuendelea. Pamoja na kukarabati tutapanua kwa sababu katika hayo maeneo kwa mfano, kama mtambo ulijengwa muda mrefu miaka ya 1960 au 1970 wakati ule wananchi walikuwa ni wachache, sasa hivi wananchi wameongezeka, huduma za binadamu vilevile zimeongezeka kwa hiyo mahitaji ya maji yameongezeka. Hivyo, pamoja na kukarabati hiyo mifumo tutahakikisha tunaipanua ili kuhakikisha kwamba huduma ya maji inakuwa ya kutosheleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane pamoja na Halmashauri yako, ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti wa kuchimba mabwawa. Kama vile Itigi Serikali imekamilisha bwawa na ninayo taarifa bwawa hilo linavuja na nimeishaelekeza kwamba wataalam waende kuhakikisha wanaziba ili tuwe na maji ya kutosha.
Kwanza ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ni kweli mitambo imekarabatiwa, lakini bado huduma ya maji haiwafikii wananchi wa vijiji vya Ving‟awe namba 30, Mbuyuni, Ving‟awe Juu, Ilolo, Kwa Mshangu, Mahang‟u na Ising‟u; kwa hiyo nilikuwa nakupa taarifa tu kwamba maji hayafiki kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kwamba kuna vijiji ambavyo hakuna uwezekano mwingine wa kupata chanzo cha maji ni kuchimba visima. Sasa naiomba Serikali, kwa vijiji nitakavyovitaja iwachimbie visima ili waweze kupata huduma ya maji. Kwanza Ngalamilo, Mgoma, Mzogole, Kisisi, Godegode, Mkanana, Chamanda, Lupeta, Makutupa, Nana, Simai, Isalaza, Nzonvu pamoja na Iwondo. Naomba sana wananchi hawa wana shida kubwa sana ya maji Serikali iwasaidie. Je, Waziri unasemaje kuhusu hilo.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lubeleje babu yangu gereda la zamani huyu, lakini makali ni yale yale, anafanya kazi nzuri sana kwa wananchi wa Jimbo la Mpwapwa.
Mheshimiwa Naibu Spika nikupe taarifa tu kwamba, wiki mbili zilizopita Mheshimiwa Lubeleje, aliondoka na Waziri wangu kwenda Mpwapwa kwenda kuangalia ukarabati wa hizo starter na sasa hivi kwa kweli Mpwapwa maji yanapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji bado havifikiwi na hayo maji, katika jibu langu la msingi nimesema kwamba Serikali itaendelea kufanya matengenezo na nimuahidi kwenye awamu ya pili ya program ya maendeleo ya maji, tutahakikisha kwamba Mpwapwa tunahakikisha vijiji vyote vinafikiwa na maji. Swali hapa muhimu ilikuwa ni kuna vijiji kwa sababu Mpwapwa ni kubwa, kuna vijiji ambavyo bado havijapata huduma ya maji yenye mfumo na ameomba kwamba tuchimbe visima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu na Babu yangu Mheshimiwa Lubeleje katika Bajeti ya mwaka huu, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.58 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kipaumbele. Kwa hiyo, nikuombe ushirikiane na Halmashauri yako kuhakikisha hivi vijiji, basi mnafanya study na mnachimba visima ili mwaka wa fedha utakaofuata, tuendelee kutoa hela kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata huduma ya maji, kwa maana ya kuchimba visima; lakini ikiwa ni pamoja na kujenga mabwawa ili tuwe na uhakika wa maji katika maeneo ya Mpwapwa.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na umuhimu mkubwa wa bonde hili ikiwa ni pamoja na kufua umeme ili kuweza kupeleka katika Gridi ya Taifa: Je, ni lini Serikali itaona kuna umuhimu wa kuitengea hela bila kutegemea ufadhili?
La pili; katika Wilaya ya Ludewa kuna mabonde kama ya Bonde la Mkiu na Bonde la Lifua: Je, ni lini Serikali itaiwekea mpango mkakati ili mabonde haya yaweze kutumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza, Mheshimiwa ameshauri kwamba ni lini Serikali itaacha kutegemea wafadhili katika kutekeleza miradi yake. Nimfahamishe Mheshimiwa Ngalawa kwamba mwaka 2006/2007 tulianza programu ya utekelezaji wa maendeleo ya Sekta ya Maji kwa kushirikiana na marafiki na wadau mbalimbali wenye nia nzuri ya kutusaidia sisi Watanzania. Programu hiyo ya kwanza iliisha mwezi Desemba, 2015. Januari mwaka huu, tayari tena tumesaini memorandum ya utekelezaji wa maendeleo ya maji kwa kushirikana na wadau hao mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hatua hii, kwa sababu tuna memorandum tayari, hatuwezi kusema Watanzania tujitenge peke yetu. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana nao katika utekelezaji wa miradi ya maji ikiwemo ya umwagiliaji kwa kushirikiana na fedha ya Seikali ya Tanzania ambayo ni kodi ambazo Mheshimiwa Rais amesisitiza kwamba tulipe ili tufanye miradi ya maendeleo pamoja na wafadhili. Pia Mheshimiwa Mbunge ujue, bila wewe mwenyewe kutenga fedha, wafadhili hawawezi kukusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ni kwamba ni lini sasa? Yapo maeneo mengi yanayofaa kwa umwagiliaji, Serikali itahakikisha kwamba inajenga miundombinu. Ni kwamba nchi yetu tayari ilishafanya utafiti kwamba tuna hekta zinazofaa kwa umwagiliaji milioni 29.4 na kati ya hizo, hekta 461,000 zimeshaendelezwa na zinafanya kazi. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba hekta zote tumezikamilisha tumeziwekea miundombinu ya umwagiliaji ili tuweze kuondokana na tatizo la maji pamoja na tatizo la njaa. Katika hiki kipindi cha miaka mitano cha Awamu ya Tano, tumepanga kuhakikisha kwamba tunajenga miundombinu, tunapata hekta milioni moja kuendeleza Sekta ya Umwagiliaji.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa maeneo ya Ludewa yanafanana sana na maeneo ya Mvomero katika kilimo na kwa kuwa tuna miradi mingi ya umwagiliaji katika maeneo ya Kata za Kanga, Mkindo, Sungaji, Lukenge, Dakawa na Mlali; na baadhi ya miundombinu ilishajengwa, lakini Serikali haijatoa fedha za kumalizia miradi hiyo: Je, Mheshimiwa Waziri, uko tayari kufuatana nami mara baada ya Bunge hili, uende ukaone fedha ambazo zimetumika na nyingine zinazohitajika ili miradi ile ikamilike na ilete tija kwa wananchi wa Mvomero na Taifa kwa ujumla?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anasema kama tuko tayari kwenda kuangalia maeneo ambayo yanafaa kwa umwagiliaji. Hiyo tuko tayari. Nataka niongezee, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, anasema ni lini Serikali itaacha kutegemea wafadhili? Katika bajeti ya mwaka huu ambayo Waheshimiwa Wabunge mmepitisha kwenye Sekta ya Maji, asilimia 75 ni fedha ya kwetu wenyewe. Kwa hiyo, huo ndiyo mwelekeo, kwamba wafadhili wameshaanza kupunguza misaada katika miradi yetu ya maendeleo. Kwa hiyo, tunakwenda huko. Tutafika mahali tutafanya miradi yetu kwa asilimia 100.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji ya 2016/2017, miradi mingi ya umwagiliaji iliyokuwa imeanza katika hatua za awali katika Halmashauri zetu na kuombewa fedha haikupangiwa fedha; kwa mfano, katika Jimbo langu, mradi wa Nkwilo, mradi wa Uzia, mradi wa Nzogwe, mradi wa Mkanga na mradi wa Momba.
Je, Serikali ina mpango gani mbadala wa kuifanya miradi hii iweze kuondelea ili wananchi waweze kuondokana na tatizo la njaa na kukuza uchumi wao na Taifa zima kwa ujumla?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mipata kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli miradi mingi haikupangiwa fedha kwa mwaka huu na tulifanya hivyo kwa sababu ndiyo kwanza tumeanzisha hii Tume ya Umwagiliaji.
Tukasema kwanza tumalize miradi ambayo tayari ilikuwa inaendelea. Katika mwaka utakaofuata, miradi hiyo yote tutakwenda kuiangalia na kuipangia fedha ili iweze kumalizika. Kwa hiyo, lazima twende kwa hatua, lakini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti tulianza kwanza na miradi ambayo ilikuwa inaendelea, lakini nikuahidi kwamba katika mwaka utakaofuata tutakwenda kuikamilisha miradi iliyobakia.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kuna dharura kubwa iliyojitokeza katika Manispaa ya Lindi; na juzi niliizungumzia hapa ndani ya Bunge lako tukufu; lakini taarifa ambazo anapewa Mheshimiwa Naibu Waziri wetu, siyo sahihi kwa sababu dharura hii ni kubwa sana na wananchi wa Lindi wanahangaika, hawana sehemu nyingine ya kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba Kisima cha Mitwero pampu imekufa na chanzo cha Mambulu kimejaa matope kiasi kwamba hakiwezi kutoa maji, wananchi leo wanahangaika na wananunua dumu moja shilingi 1,000/=. Hili ni tatizo kubwa sana! Namwomba Mheshimiwa Waziri wetu atuambie, atatusaidiaje ili kutatua hii kero ya maji wananchi waweze kuondokana nayo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pale Mji wa Lindi kumekuwa na matatizo kwa sababu ya uchakavu wa miundombinu ya maji ya muda mrefu, ndiyo maana Serikali imebuni na inaendelea kujenga mradi wa kumaliza tatizo hilo. Tatizo la maji kwa Mji wa Lindi litakwisha ikifika mwezi wa Kumi, huu mradi ambao unaendelea utakuwa umekamilika.
Mhesimiwa Naibu Spika, kwa hii dharura ambayo imejitokeza, kwa sababu yale mabomba yanapita chini ya maji na hatuwezi ku-control kwa sasa nguvu ya maji kwenye ile bahari, kwa hiyo, mara kwa mara yale mabomba yamekuwa yanakatika. Ninapeleka wataalam wangu wakasaidiane na wataalam walioko pale Lindi ili tumalize angalau kwa dharura wananchi wa pale waendelee kupata maji. Ufumbuzi wa kudumu ni ule wa kukamilisha mradi ambao tunaendelea kuusukuma kwa nguvu zote tuweze kuumaliza wananchi wa Lindi waweze kupata maji.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Maji, hapo ndiyo umeshawaagiza hao wataalam ama utawaagiza lini ili waende huko Lindi? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba wapo tayari wanashughulikia hilo tatizo, hivi sasa wapo huko.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Igunga pamoja na upatikanaji wa maji kitakwimu wa asilimia 60, lakini kutokuwepo kwa umeme wa uhakika kunapelekea upatikanaji wa maji katika Mji wa Igunga kuwa angalau kwa wiki mara mbili. Je, Waziri ama Serikali wakati tunasubiri mradi wa maji wa Ziwa Viktoria, inaweza kutusaidia katika Mji wa Igunga kuwapatia angalau generator ili liwe pale ambapo umeme haupo, basi waweze kupata maji ya uhakika?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, tatizo la Igunga linafanana sana na tatizo la Mji wa Nzega; na upatikanaji wa maji katika Mji wa Nzega kwa sasa ni asilimia 30 tu ya maji na maji haya yanapatikana kwa wiki mara tatu: Je, Serikali ni lini itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa matenki matano na kuweka chujio la maji katika bwawa la Kilime na pampu ili wananchi wa Mji wa Nzega wasiendelee kupata shida wakati tunasubiri mradi wa maji wa Ziwa Viktoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza nashukuru amekiri kwamba asilimia 60 ya maji inapatikana katika Mji wa Igunga, lakini tatizo lililopo ni tatizo la umeme. Ameuliza kwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, lakini pamoja na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa katika Bunge hili Mheshimiwa Waziri anayehusika na umeme na nishati ameshatupa majibu kwamba sasa hivi kunajengwa umeme wa msongo wa Kilowatt 400 ambapo tatizo la umeme sasa litakwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, amependekeza kwamba, katika kipindi hiki kwa sababu ya tatizo la umeme, maji yanapatikana mara mbili kwa wiki, ni vyema tukafanya utaratibu wa kununua generator. Kupitia Bunge lako Tukufu, namwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga, aweze kuleta andiko ili tuweze kuangalia uwezekano wa kununua generator iweze kusaidia katika kipindi hiki tunaposubiri kuwa na mradi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, amezungumzia Mji wa Nzega kwamba unapata 30% na maji yanapatikana mara tatu kwa wiki. Je, Serikali ni lini itajenga matenki matano yaliyoahidiwa na Mheshimiwa Rais?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimjibu kwamba, matenki matano makubwa yanajengwa kupitia huu mradi wa kutoa maji Ziwa Viktoria na kupeleka Miji ya Tabora, Nzega na Igunga. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa kwamba matenki hayo yatajengwa kupitia mradi huu, lakini pia, mradi utahusisha ujenzi au upanuzi wa mtambo wa kusafisha na kutibu maji. Kwa hiyo, mradi huu ukikamilika, hoja zote ulizonazo Mheshimiwa Mbunge, zitakuwa zimeshapitiwa.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Miradi mingi sana ya maji imeanzishwa nchini na katika Jimbo langu kuna mradi umeanzishwa katika Kijiji cha Shimbi Mashariki, mwingine umeanzishwa katika Kijiji cha Rea, visima vile 10 na vinahitaji kujengewa miundombinu. Sasa kinachosumbua ni fedha zinasuasua kwenda ili kukamilisha umaliziaji wa miundombinu ili wananchi wapate maji. Nauliza je, ni lini fedha zitakwenda ili miradi hiyo ipate kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikuhakikishie kwamba tumeanza Program ya Pili ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Pili, fedha zimeanza kutolewa. Natoa wito kwa Wakurugenzi wote kwamba kama wana hati ziko mezani, basi waziwasilishe kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji. Fedha tunazo na tayari maeneo mengi fedha tumeshapeleka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama kazi imeshafanyika, hati zipo, hata kesho alete tutampatia fedha.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Nashukuru Mheshimiwa Spika, kwa kiasi kikubwa swali langu lilikuwa na sehemu mbili hivi, lakini limejibiwa swali moja tu.
Nilikuwa nimezungumza kwamba tatizo la maji kwa Mikoa hii ya Kusini na hasa miundombinu yake ambayo imejengwa tangu ukoloni ni miundombinu hafifu sana. Kwa mfano, mradi ule wa maji wa Makonde umejengwa mwaka 1953 na mpaka hivi sasa navyozungumza unatoa maji kwa asilimia 30 tu kwa sababu ya miundombinu yake ni hafifu. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Waziri amezungumzia suala zima la mradi wa maji wa Mto Ruvuma na akasema kwamba upembuzi yakinifu umekamilika na wananchi watapata maji na vijiji takribani 25 vinavyopitia lile bomba ambalo linatarajiwa kujengwa wataweza kunufaika na mradi huu wa maji.
Mheshimiwa Spika, swali tangu mwaka 2015 mpaka hivi sasa navyozungumza wale wananchi wameambiwa maeneo yale ambayo maji yatapita au ule mradi utapita wasiendeleze yale maeneo na hawajalipwa fidia hata senti moja mpaka hivi sasa, je, ni lini wale wananchi watapewa fidia ili waweze kutumia zile fedha kwenda kununua maeneo mengine waweze kuendeleza kilimo?
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kilio kikubwa sana Mtwara Mjini na maeneo mengine ya Kusini, kwamba watendaji wa Idara za Maji wanavyokuja kusoma mita hawasomi zile mita na wamekuwa wakikadiria malipo ya mita kila mwezi, wanaona usumbufu kwenda kuzipitia mita wakati mwingine na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi na kuwabambikia fedha nyingi za kodi ya maji kinyume na taratibu na kanuni. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba mwaka huu mwezi wa pili Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji alitembelea kule Mtwara na wananchi waliandamana kwa ajili ya tatizo hili, naomba atoe majibu ya uhakika kwamba ni lini sasa Serikali itakoma kukadiria mita za maji...
SPIKA: Mheshimiwa Nachuma yaani umehutubia.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: ...na badala yake waende kusoma mita?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nitoe majibu ya nyongeza kwa maswali mawili aliyouliza Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi huu wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma mpaka Mtwara ni kweli tumeuzungumza kwa muda lakini Serikali imedhamiria kuujega mradi huu kwa kutumia utaratibu wa PPP, imeshapata mbia ambaye atatafuta fedha kwa maana building and finance, Serikali yenyewe itachangia kwa kuweka msimamizi atakayesimia. Kazi ambazo tunafanya sasa ni kufanya due diligence ya ile kampuni kama ina uwezo wa kufanya kazi hii na tuko kwenye hatua ya mwisho na ndio maana tumesema kuanzia mwaka wa fedha huu unaoanza mwezi wa saba tunaweza kuanza kujenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa tutakapokuwa tumekamilisha hatua zote hizi ndio tutakapolipa fidia ya wale wananchi ambao mradi utapita hatutaweza kulipa fidia kabla hatujakamilisha majadiliano na ile kampuni ambayo itajenga ili kusudi tuwe na uhakika kwamba wale wanaohusika wote na watakaoathirika na mradi huu wataweza kulipwa. Lakini katika swali lake la pili la kwamba ni lini Serikali itaacha kukadiria, ninafikiri suala la kukadiria mita siyo utaratibu tunasema kila mtu atalipa maji kulingana na namna anavyoyatumia. Kwa hiyo, kuna maeneo ambayo bado yana utata kuhusu ukadiriaji hili mtuachie tutalifanyia kazi ili tuhakikishe kwamba kila mmoja alipe maji kwa kadri anavyokuwa ameyatumia, ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika jibu la msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba usanifu umekamilika katika Miji ya Isongole, Vwawa pamoja na Tunduma, lakini nisikitike kusema kwamba neno usanifu umekamilika bado haliwezi kuleta matumaini kwa akina mama wa Mkoa wa Songwe ambao wanapata shida kubwa sana ya maji. Kwa hiyo, napenda kuomba Mheshimiwa Waziri aniambie kwamba ni lini mradi huo utaanza katika maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili la nyongeza kama tunavyojua Mkoa wetu wa Songwe ni mkoa mpya na lengo la kuleta Mkoa mpya ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Huduma mojawapo ni huduma ya maji ili akinamama wale wa Mkoa wa Songwe waweze kupata huduma kama inavyostahili. Hata hivyo, nioneshe masikitiko yangu makubwa kwamba mpaka sasa, hasa…
MWENYEKITI: Naomba uulize swali tafadhali!
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza. Kwa maeneo ambayo ni ya pembezoni, mfano kule Ibaba, Ileje, ukienda Mkwajuni Wilaya ya Songwe, ukienda Iwula, ukienda Kamsamba bado miundombinu ya maji haijakaa vizuri. Naomba kupata jibu la Mheshimiwa Waziri kwamba ni lini Serikali itajenga miundombinu mizuri ya maji, hasa kwa maeneo ambayo ni ya pembezoni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyofuatilia upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wake na kwa sababu ni Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum nafikiri wananchi hawakupoteza kura zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameniuliza maswali mawili ya nyongeza, ni lini miradi hii iliyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina itaanza. Kama nilivyojibu katika swali la msingi kwamba, tayari sasa hivi Serikali inafanya majadiliano na wafadhili kwa ajili ya kupata mikopo ya masharti nafuu. Hii miradi ni mikubwa, uwezo wa Serikali tunaendelea lakini bado siyo mkubwa sana kiasi cha kuweza kutekeleza miradi mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba kuna Miji ya Mkoa wa Songwe, Mkoa ni mpya, kuna maeneo mengi bado hayajapata huduma ya maji. Serikali inaendelea, tumeanza programu ya kwanza ya maendeleo ya maji mwaka 2006/2007, programu ya kwanza ya miaka mitano imekwisha mwaka 2015 Disemba. Sasa hivi tumeanza programu ya pili, kwa hiyo ile miradi ambayo haikukamilika, miradi ambayo haikuanza katika awamu ya kwanza, basi tutaianza na kuikamilisha katika awamu ya pili.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa vile bwawa hili lilikuwa likihudumia sio Kijiji cha Mwamihanza tu ni pamoja na Kijiji cha Isulilo, Kijiji cha Kidema na Kijiji cha Kulimi; na kwa vile Halmashauri na Wizara mpango wao uko mbali sana. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa dharura wa kuwapatia maji wananchi wa vijiji hivi, wakati tunasubiri mpango wa Halmashauri na Wizara?
Swali la pili, kwa vile pia Serikali ilishachimba mabwama mengi huko nyuma na sasa hivi mengi yao yamejaa mchanga, kama vile bwawa la Shishiu, bwawa la Jihu, bwawa la Sola, yamejaa mchanga na hivyo hayaingizi maji. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuyafufua mabwawa haya yaweze kujaa maji na kuyatunza ili wananchi wafaidike na huduma iliyokuwa ikitolewa kwenye mabwawa haya pamoja na mifugo yao.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, bwawa hili tutalitengea fedha mwaka wa fedha 2017/2018, ni kweli kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge ni mbali na hasa kwa kuzingatia kwamba bwawa hili linahudumia Vijiji zaidi ya vitano, katika Kata ya Kilimi, ambavyo ni Mwabayanda, Ilamata, Kulimi na Mwandu. Kwa hiyo, wananchi hawawezIe kusubiri mpaka mwaka wa fedha 2017/2018. Namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, bwawa hili tutahakikisha tunatafuta fedha hata kama ni za dharura ili tuweze kulikarabati na kwa sababu mpango wa Serikali baada ya miezi sita, mwezi wa Desemba kunakuwa na marudio ya bajeti, kufanya budget review, basi tutahakikisha Mheshimiwa Mbunge, tunampa kipaumbele ili kuweza kuweka fedha kuhakikisha kwamba bwawa hili tunalikarabati ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ameeleza kwamba kuna mabwawa mengi ambayo yamejengwa muda mrefu, lakini mabwawa haya yamejaa mchanga na kwamba Serikali ina mpango gani kukarabati haya mabwawa. Swali la Mheshimiwa Mbunge ni zuri, lakini swali hili pia limewahi kuulizwa na Mheshimiwa Andrew Chenge, kwamba katika maeneo yake kuna mabwawa ambayo yalijengwa zamani, yana magugu maji na yamejaa mchanga. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika haya mabwawa yaliyojengwa yana matatizo makuu mawili: Moja, yanajaa michanga na pili, yanakuwa na magugu maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji sasa hivi, tayari inajipanga na itaanza kufanya ukarabati kwa kuondoa magugu maji kwa kutumia njia mbili, njia moja ni njia ya kibailojia; tayari tumeshafanya mazoezi kupitia Ziwa Victoria, tuna wadudu wanaitwa mbawa kavu, ambao wakiwekwa kule wanakula yale magugu maji. Pia tutahakikisha kwamba tunaondoa mchanga kwenye haya mabwawa kwa kufanya utaratibu ambao unajulikana kama dredging, kuhakikisha kwamba tunapanua capacity, mabwawa yaendelee kupata maji.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, tatizo linalowakabili wananchi wa Maswa Magharibi kuhusu bwawa lao, linafanana kabisa na tatizo la bwawa la Kazima Mjini Tabora ambalo maji yake yanapungua mara kwa mara hasa wakati wa kiangazi, kutokana na tope pamoja na mchanga uliojaa pale. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha lile tope pamoja na mchanga linaweza kuondolewa ili wananchi wa maeneo yale waweze kupata maji ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri bwawa la Kazima nimelitembelea ni bwawa kubwa na kweli nimelikuta lina matatizo. Moja, kipindi cha kiangazi kutokana na miti mingi iliyoko kwenye lile bwawa maji yanabadilika rangi, lakini pia bwawa lile linajaa tope kutokana na shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumeshaongea na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji wa Tabora, kuhakikisha kwamba tunashirikisha jamii. Nimwombe pia Mheshimiwa Mwakasaka, shida kubwa inayojitokeza ni kwamba wananchi wanalima sehemu ambayo maji yanatoka; baada ya kulima mvua zikinyesha zinabeba zile tope kuleta kwenye bwawa. Kwa hiyo, suala la msingi ni kwamba kwa kushirikiana na Halmashauri, tujaribu kuhakikisha kwamba tunaacha eneo la kutosha kuja kwenye bwawa, wananchi wasifanye shughuli za kilimo pamoja na ufugaji ili tuweze kulilinda bwawa letu lisijae mchanga.
MHE. SALUM K. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tatizo la bwawa la Maswa linafanana kabisa na tatizo tulilonalo katika bwawa letu la Mwenyehina Meatu na aliyekuwa Waziri wa Maji alikuja kulitembelea na akatuahidi kutusaidia chujio kwa ajili ya kusafisha maji kwa ajili ya Mji wa Mwanhuzi. Nimwombe Waziri kwa sababu ndiye aliyekuwa Naibu Waziri, atuambie bwawa hilo limefikia wapi kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naona Mheshimiwa muuliza swali alichagua mtu wa kujibu, lakini nitajibu kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji Meatu, aliahidiwa kujenga chujio, katika Bunge hili tumeelekeza kwamba tumetenga fedha kupitia kwenye Halmashauri zote. Halmashauri zote 181 tumezitengea fedha na tumeelekeza kwamba, kwanza wakamilishe miradi ambayo ilikuwa inaendelea, lakini pili wahakikishe kwamba miradi ya kipaumbele kama vile kukarabati chujio ambalo Mheshimiwa Mbunge anasema, basi ni vema ashirikiane na Halmashauri kuhakikisha kwamba wanaweka kipaumbele kutumia zile fedha tulizozitenga kwa ajili ya kufanya ukarabati wa hilo eneo husika. Kama hiyo fedha itakuwa haitoshi, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane, tushirikiane ili tuangalie ni namna gani tunaweza tukaongeza fedha baada ya kufanya budget review mwezi wa Desemba.
MHE. CAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kutambua tatizo la maji Mradi wa Maji wa Makonde na kutenga fedha za kutosha kutokana na mkopo uliopatikana kutoka Serikali ya India. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, la kwanza; kitakachoondoa tatizo la maji Mradi wa Maji Makonde ni utekelezaji wa huu mradi mkubwa wa fedha ambazo tumepata mkopo kutoka India. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini utekelezaji utaanza wa huo mradi mkubwa?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, jirani na chanzo cha maji Mitema kama alivyosema Mheshimiwa Waziri ambako kuna maji ya kutosha, kuna mji mdogo wa Kitangari na watu wengi, pana Kituo cha Afya, Chuo cha Ualimu, sekondari mbili, watu wengi sana pale, soko kubwa lakini Mji ule ambao uko kama kilometa tatu tu kutoka chanzo cha maji hawapati maji. Maji yanafika Tandahimba, yanafika Mtwara Vijijini, pale kwenye chanzo cha maji hawapati maji. Je, Serikali inajua tatizo hili na kama inajua tatizo hili inawaahidi nini wananchi wa Mji Mdogo wa Kitangari?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni lini utekelezaji wa huu Mradi wa Makonde kupitia mkopo wa masharti nafuu wa Serikali ya India utaanza.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusaini makubalianoya nchi mbili sasa hivi Serikali mbili zinaendelea na taratibu ili kuweza kufikia kusaini financial agreement, baada ya kusaini financial agreement kwa sababu tayari usanifu upo tutakuwa na muda mfupi sana ku review nyaraka za mradi wa Makonde na kutangaza tender na baadae utekeleji uweze kuanza. Kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba haitachukua muda mrefu maana yake tatizo lilikuwa ni fedha na fedha zimepatikana kwa hiyo kilichobaki ni taratibu zingine ndogo ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mji wa Kitangari ni kweli. Mji huu uko kilometa tatu na Mheshimiwa Mbunge wewe ni shahidi kwamba nilikuja pale na mpaka nikaja Mji wa Kitangari nikaongea na wananchi. Ni kweli kabisa kwamba maji yanatoka chanzo cha Mitema, bomba linapita Kitangari kwenda Tandahimba. Katika huu mradi mkubwa kwa sababu fedha ni nyingi Tutahakikisha kwamba bomba linatoka chanzo cha Mitema pale linakwenda moja kwa moja eneo la Kitangari.
Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Kitangari kwamba tatizo la maji walilokuwa nalo muda mrefu sasa kupitia mkopo huu tunalimaliza. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Moja, kwa vile umethibitisha kweli kwamba hakuna maji chini Uyui Kaskazini; je, Serikali iko tayari sasa kuanzisha mradi kabambe wa kuchimba mabwawa katika eneo hilo?
Swali la pili, katika kijiji cha Majengo kuna chanzo kizuri cha maji ambacho watu wanateka maji kila siku kwa kuchimba kwa mikono. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kwenda na mimi na Wataalam wake wa maji kuangalia eneo hili kama inaweza kuchimbwa visima virefu ili yapatikane maji ambayo ni salama badala ya haya maji ambayo hayana usalama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza mabwawa, mabwawa ndiyo sera ya Wizara ya Maji. Maeneo yote ambayo yana matatizo ya ukame na yanapata mvua tumeamua kumaliza tatizo la maji, moja kwa kuvuna maji kutoka kwenye mapaa ndiyo maana tumeagiza Halmashauri ziweke utaratibu kila wanapopitisha michoro ya nyumba wahakikishe kwamba wanaainisha uvunaji wa maji ya mvua.
Pili, ni sera yetu kwamba tuna hakikisha na tayari tumeshaagiza kila mwaka, kila Halmashauri wahakikishe wanafanya usanifu wa bwawa moja na kuleta maombi ya pesa ili tuweze kuwapa wajenge mabwawa kuhakikisha tunamaliza matatizo ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili linalohusu eneo la Majengo, Mheshimiwa amesema kwamba watu wanafukua maji na maji wanayapata. Ikolojia ya ardhi huwa ni ngumu, lakini kwa sababu umetueleza hili naomba nikuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalifanyia kazi, lakini niagize Halmashauri husika waende katika hilo eneo wakaangalie halafu watupe taarifa ili tuweze kuona tunalifanyia nini.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa swali la msingi linaongelea suala la visima; na kwa kuwa Tabora Manispaa wananchi walichangia pesa kwa ajili ya uchimbaji wa visima kwa masharti ya mradi lazima kila Kata ichangie pesa ndiyo wachimbiwe. Visima hivyo vilichimbwa maji hayakupatikana.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutuambia na kwa sababu Serikali ilifanya research Mheshimiwa Waziri anaweza kutuambia yule mtu aliyefanya research na kutupotosha wananchi pamoja na mradi, tuchimbe visima virefu wakati hakuna maji, Serikali ilimchukulia hatua gani? Ili tuweze kujua kwa sababu pesa za Watanzania zimepotea na pesa za mradi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi walichangishwa pesa, utafiti ulifanyika, lakini visima vikachimbwa na havikutoa maji! Kwa bahati nzuri Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata bahati ya kupata msaada wa Wajapani, Wajapani wana teknolojia ya hali ya juu sana ambayo wao wanaweza wakabaini kama kweli chini kuna maji. Kwa bahati mbaya pamoja na tafiti walizozifanya bado na wao kuna maeneo ambayo wamekosa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli teknolojia ya maji chini, bado dunia haijawa nayo. Kwa hiyo, bado tunakwenda kwa kubahatisha. Unaweza ukapima ukakuta maji yapo lakini unakwenda kuchimba unakuta maji hakuna. Vilevile ameuliza kwamba huyu mtu anachukuliwa hatua gani? Huu ni utafiti ulifanyika na kwa bahati mbaya kwamba maji yale hayakupatikana na kimikataba kwa sababu tunafanya kazi kwa kutumia mikataba kama hatukuweka kifungu kwenye mkataba kwamba kama utakosa maji tutakuchukulia hatua fulani basi huwezi kuchukua adhabu yoyote.

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kwamba tunafanya kwa kubahatisha ila nasema kwamba tunapofanya tunakuwa tumelenga kwamba tutapata maji. Lakini trend au historia inaonyesha kwamba mara nyingi unaweza ukafanya utafiti wa visima kumi lakini ukachimba ukapata visima saba, vitatu vikakosa maji ndiyo maana nikatumia hilo neno kubahatisha. Lakini siyo kwamba tunapofanya utafiti tunafanya kwa kubahatisha hapana tunakuwa tumedhamiria kwamba tunafanya utafiti ili tuweze kupata maji, lakini kwa bahati mbaya kutokana na mabadiliko ya miamba kule chini inatokea wakati mwingine unataka kuchimba visima 100 unachimba visima 80 vinapata maji, visima 20 vinakosa, kwa hiyo hatufanyi kwa kubahatisha.

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niongezee kipengele kidogo, ni kwamba tulivyoanza huu mradi wa vijiji kumi, aliyekuwa anafanya utafiti alikuwa ni Mhandisi Mshauri na aliyekuwa anachimba kisima alikuwa ni Mkandarasi. Sasa tumeunganisha kwamba Mkandarasi atapewa mkataba utakaofanya kazi zote za kufanya utafiti na kuchimba. Kwa hiyo, akikosa maji sasa itakuwa ni gharama kwake kutafuta eneo lingine ili kusudi isiwe hasara kwa Serikali.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la maji la Mji wa Tukuyu linafanana kabisa na Manispaa ya Mtwara Mjini, ambako kwa muda mrefu Serikali imekuwa na mpango wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma, lakini ule mradi mpaka hivi sasa umekwama kwa sababu kibali bado hakijasainiwa na Waziri husika. Je, ni lini Serikali itatoa kibali hiki ili zile pesa ziweze kutoka Exim Benki ya China na ule mradi uweze kutekelezwa mara moja Mtwara Mjini, kwa sababu kuna tatizo kubwa la maji? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko kwenye hatua za mwisho kukubaliana na Benki ya Exim kwa ajili ya kutoa fedha ya ujenzi wa mradi huo na siyo kwamba kibali hakijatolewa na Waziri, tuko katika hatua nzuri. Mwezi uliopita mimi mwenyewe nimeenda mpaka kwenye chanzo pale Ruvuma nimeenda kutembelea pale na sasa hivi hatua inaendelea vizuri kabisa, wakati wowote huo mradi utaanza utekelezaji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hakuna wasiwasi mradi upo na hiyo fedha imeshapatikana tunakamilisha taratibu ndogondogo tu ili uweze kuanza. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa vile tatizo la maji katika Mji Mkongwe wa Tukuyu linafanana sana na tatizo la upatikanaji wa maji katika Mji Mkongwe zaidi Bagamoyo, ambapo huduma ya maji iko chini, maeneo mengi hayapati maji hasa eneo la Mji Mkongwe upatikanaji wake wa maji ni mdogo hata Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo iko katika ratiba ya mgao wa maji ambapo inasababisha huduma kuwa nzito katika Hospitali hiyo na maeneo mengine kama Kisutu na Nia Njema hakuna hata mtandao wa maji. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuboresha upatikanaji maji katika Mji wa Bagamoyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba tumekamilisha ukarabati wa mradi wa Ruvu Chini ambao kwa sasa unatoa lita milioni 270 kwa siku, bomba linalosafirisha maji kutoka Ruvu Chini linapita Bagamoyo hadi Dar es Salaam. Sasa hivi tayari Serikali kupitia Wizara ya Maji imeshasaini mkataba kwa ajili ya kuweka mabomba kusambaza maji maeneo ambayo yalikuwa hayana mtandao wa mabomba na sasa hivi tumeanzia maeneo ya Kiluvya na tuna mkataba mwingine ambao Mhandisi Mshauri anatambua maeneo ya kupitisha mabomba ambayo watakwenda mpaka katika Mji wa Bagamoyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza maji tayari tunayo, kilichobaki ni kusambaza. Kwa hiyo, shughuli hiyo itafanyika wakati wowote. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuwa wananchi wa Kilwa Kaskazini walichagua Mbunge anayekimbia kamera na anayeogopa Kanuni za Bunge. Sasa swali hili naomba nilielekeze kwenye matatizo yalioko kwenye Jimbo la Geita Vijijini walikochagua Mbunge makini na asiyeogopa Kanuni na kamera.
Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Geita wana matatizo kama ya Kilwa. Swali, tumekuwa na mradi wa umwagiliaji wa Nzela Nyamboge ambao umedumu sasa kwa miaka 19 haujakamilika, ni lini mradi huu wa scheme ya umwagiliaji ya Nzela Nyamboge itatekelezwa?
Lakini naomba niulize swali la pili, wananchi wa Jimbo la Ilemela Maduka Tisa ambayo ndio center inayokuwa kwa kasi; wana malalamiko ya maji, na wameisha fuatilia hawajapata muafaka wa kupatiwa maji katika kitongoji cha Maduka Tisa, ni nini kauli ya Waziri kuhusiana na matatizo haya ya wananchi wa Ilemela na Jimbo la Geita Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza amesema mradi wa umwagiliaji wa Nzela, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu nitaufuatilia. Lakini nitoe taarifa kwamba Serikali imekamilisha kuunda Tume ya Umwagiliaji ambayo taratibu zake zimekamilika katika mwaka huu wa fedha 2015/2016. Kwa hiyo, sasa hivi Serikali inaanza kutenga fedha sasa, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ambao sasa una tume maalum ambayo ndio itashughulikia miradi ya umwagiliaji. Kwa hiyo, miradi yote ambayo ilikuwa imeanza tutahakikisha imekamilika, miradi mipya itaanza na kama mlivyoona kwenye kitabu cha Wizara ya Maji cha bajeti, tunaanza kufanya utafiti mkubwa kwa ajili ya kuweka miradi ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Maduka Tisa, Kijiji cha Ilemela, Mheshimiwa Mbunge kama unavyofahamu katika Awamu ya Kwamza ya Programu ya Maendeleo ya Maji iliyoanza mwaka 2006/2007 tulikuwa tumepanga kutekeleza miradi 1,810. Tumekamilisha miradi 1,210 sasa hivi kuna miradi 374 ambayo utekelezaji wake unaendelea na kuna miradi 226 ambayo miradi hiyo haikuanza.
Katika bajeti ambayo mmeipitisha Waheshimiwa Wabunge juzi, tunalenga kwanza kukamilisha miradi ambayo utekelezaji unaendelea na kuanza ile ambayo ilikuwa haijaanza, baadae tunaendelea sasa kuweka miradi mipya. kwa hiyo, katika hii Programu ya Pili, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hawa wananchi wa Maduka Tisa, tutahakikisha kwamba tumewapatia maji.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa matatizo ya maji vijijini, Serikali imekuwa ikifanya miradi mingi kama ilivyo katika Jimbo la Kilwa Kaskazini. Mradi wa maji wa Kata ya Itunduru - Igunga, ulitekelezwa, miundombinu ikakamilika, lakini maji hayakupatikana, miundombinu imebaki white elephant. Nauliza ni lini Serikali itatafuta chanzo cha maji ili miundombinu hii iweze kutumika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kuna miradi ambayo ilikuwa ni ya kujenga miundombinu na kutafuta chanzo cha maji. Lakini kwa bahati mbaya vyanzo vya maji vile havikupata maji, kwa sasa tunaendelea, lile eneo ambalo halikupata maji tunatafuta eneo jingine karibu, ili tuweze kupata maji, wananchi waendelee kupata maji. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwenye hii Programu ya Pili yale maeneo ambayo tulitafuta maji tukakosa, lazima sasa tutafute maji tupate tukamilishe huo mpango ambao tulikuwa tumepanga. Kwa hiyo, hilo eneo lako pia, tutahakikisha kwamba tunatafuta chanzo kingine ili uweze kupata maji.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa Wilaya ya Lushoto ni ya wakulima wa mboga mboga na matunda. Je, ni lini Serikali itawajengea mabwawa, hasa wakulima wa Mavumbai, Mavongo, Kwaiboheloi, Ubili, Mbwei, Mlola, Kichangai na ngwelo ili na wao waweze kulima kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge hili tumeelekeza na tumeagiza, kwamba Wakurugenzi wote wa Halmashauri kila mwaka wahakikishe wanasanifu bwawa moja kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na maji ya matumizi ya binadamu na mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niagize tena kila Halmashauri wahakikishe wanafanya hivyo, na wanaomba pesa Wizara ya Maji na Umwagiliaji tuweze kuwapa, ili tuhakikishe tunapata mabwawa ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ninaomba sana, pengine sasa hivi Mkurugenzi hanisikii, lakini tukimaliza Bunge leo mpigie simu ahakikishe kwamba anafanya utafiti au tunawasiliana naye kuhakikisha kwamba, katika hili eneo basi tuhakikishe kwamba tunapata bwawa ambalo litahakikisha linapata maji, kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha mboga mboga.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kukamilisha Mradi wa Maji wa Ntomoko ambao chanzo chake kipo Wilaya ya Kondoa kwa ajili ya vijiji vya Wilaya ya chemba, na Wilaya ya Kondoa. Mradi huu haujakamilika hadi sasa na tumeambiwa kwamba vijiji viwili, kijiji cha Jangalo na Madaha hawatapata maji, licha ya kwamba fedha hizi zilitolewa ili na wao wapate maji kwenye mradi huu.
Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana kwenda kukutana na Mkurugenzi wa Kondoa na Chemba ili tufanye makubaliano sasa pesa zile zilizokuwa zikamilishe mradi huu zisogezwe ili tuchimbe visima walau viwili kwa ajili ya Jangalo na Madaha
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba ni kweli tumekuwa na huu mradi wa Ntomoko ambao ulilenga kwenda mbali. Lakini baada ya kufanya utafiti zaidi, tumegundua kwamba chanzo cha maji katika hili eneo hakiwezi kutosheleza vijiji ambavyo tulikuwa tumevilenga. Kwa hiyo kwa sasa pesa tuliyotoa itakamilisha huo mradi ili kuhakikisha vijiji viwili vimepata maji. Vijiji vingine vilivyobaki itabidi tufanye utaratibu wa kuchimba visima, kuhakikisha kwamba wananchi hao wamepata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la kuongozana naye, ni sawa ngoja tumalize Bunge, lakini kikubwa ni kwamba tuhakikishe maji yanapatikana na kwamba Wizara ina taarifa na hata katika maandiko yetu tumeandika hivyo, kwamba maji yaliyopo Ntomoko yatatosheleza vijiji viwili tu, hivyo vijiji vingine vilivyobaki vinafanyiwa utaratibu mwingine.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza kama ifuatavyo. Serikali imekuwa ikitoa pesa nyingi sana kwa ajili ya miradi ya maji, lakini kumekuwa na tatizo kwamba miradi hii imekuwa inakosa ufuatiliaji; kwa maana kwamba miradi ile, hasa ya maji imekuwa katika kiwango cha chini sana. Je, Serikali iko tayari kuwa na kitengo maalum kwa ajili ya kufuatilia kuhakikisha kwamba fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maji zinakidhi mahitaji, kwa maana miradi itengenezwe katika viwango vinavyotakiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa miradi ya maji unafuata mfumo wa D by D. Wizara ya Maji inatoa fedha kupeleka katika halmashauri na halmashauri zinafanya utekelezaji.
Kuhusu suala la kufuatilia utekelezaji wa miradi hii ili kuhakikisha kwamba inakamilika katika viwango vinavyostahili; mwaka huu tulionao Wizara ya Maji imeajiri wahandisi zaidi ya 400 na imewapeleka katika halmashauri ili kwenda kuimarisha utaalam kuhakikisha kwamba sasa utekelezaji wa miradi utakwenda vizuri.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Shida ya maji ya Kilindi inafanana na shida ya maji katika Jimbo letu la Igalula. Tuna mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria unaokuja katika wilaya zote za Mkoa wa Tabora, lakini mradi huu hauleti maji katika Jimbo letu la Igalula. Je, Wizara haioni umuhimu wa kuchepusha mradi ule kuleta katika Jimbo letu la Igalula ili kuondoa matatizo ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, usanifu wa sasa wa mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kuleta Tabora hauwezi kufikisha maji hayo katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge kule Igalula. Baada ya mradi kukamilika na kwa sababu tuna mradi mwingine wa kutoa maji Mto Malagarasi, maji yakishakuwa mengi basi baadaye tutaangalia jinsi ya kusanifu na kuyatoa maji hayo kuyapeleka hadi Jimbo la Mheshimiwa Mbunge kule Igalula.
MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa tatizo la maji la Kilindi linafanana sana na tatizo la maji la Jimbo la Makete na upo mradi ambao ulikuwa unatekelezwa na Serikali kwenye Kata ya Matamba na Tandala. Nini tamko la Serikali juu ya ukamilishaji wa mradi huo, kwa sababu mpaka sasa hivi maji hayatoki maeneo yale ambayo yalitakiwa yatoke? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia kwamba mradi wa maji wa Matamba umekamilika lakini maji hayatoki. Bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeipitisha tumeelekeza kwamba kwanza tukamilishe miradi ambayo ilikuwa inaendelea kabla hatujaingia kwenye miradi mipya. Pia bajeti imeelekeza, miradi ambayo imekamilika, lakini maji hayatoki, basi tuhakikishe kwamba tunafanya utafiti kwa nini maji hayatoki na kama chanzo hakitoshi, basi tutafute chanzo kingine kuhakikisha kwamba miundombinu iliyowekwa inatoa maji na wananchi wapate maji.
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Tatizo hili linafanana sana na tatizo la maji ambalo liko kwenye Jimbo la Solwa. Tumekuwa na mradi wa World Bank ambao Serikali kama Serikali, Wizara ya Maji ilitupa approval ya kuendelea na miradi kumi, lakini mpaka leo mwaka wa pili sasa kuna fedha ambazo hatujazipata na kwenye bajeti sijaziona. Naomba Serikali au Waziri wa Maji atuhakikishe leo kwamba tatizo hili linakwisha, fedha zije na watu wanywe maji. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumekamilisha program ya kwanza ya miradi ambayo iliitwa ni ya World Bank Desemba mwaka 2005, lakini miradi hiyo si ya World Bank kama ambavyo tunaitaja, ni miradi ambayo wale wadau wanaotusaidia fedha katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye ile programu ya kwanza waliamua kwamba miradi hii isimamiwe na World Bank kwa sababu ya uzoefu wa World Bank, lakini ni miradi ambayo inachangiwa fedha na Serikali pamoja na wadau wengine wakiwemo ADB, Benki za Ufaransa pamoja na World Bank yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini programu ya kwanza tumemaliza Desemba 2015, sasa hivi tumeingia kwenye programu ya pili ambayo imeanza Januari mwaka 2016. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba miradi ile ambayo haikukamilika au miradi ambayo haikuanza utekelezaji katika kipindi kile lakini ilikuwa imepangwa, basi katika awamu ya pili tutahakikisha kwamba tunakamilisha ili wananchi waweze kupata maji.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo. Kata za Igulwa, Kanoni, Kituntu, Ihanda na Chonyonyo, zina shida kubwa sana ya maji. Kutokana na shida hii, Serikali iliahidi kuchimba mabwawa katika hizi Kata ili kuwasaidia wananchi kuondokana na adha ya maji. Je, Serikali itachimba lini haya mabwawa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bashungwa ameuliza kwamba, ni lini Serikali; kuna Kata za Igulwa pamoja na Kata zingine ambazo zina uhaba wa maji, lakini anapenda kujua ni lini basi, Serikali itachimba mabwawa au kufanya utafiti wa kupata ni chanzo kipi cha maji, ambacho kinaweza kikatosheleza Kata hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tumeagiza kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri wafanye utafiti wa mabwawa, ambayo wanafikiri yanaweza yakachimbwa katika maeneo yao ili tafiti hizo ziwasilishwe Wizara ya Maji ili Wizara ya Maji iangalie uwezekano wa kutenga fedha katika Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 kutegemea na jinsi watakavyokamilisha hizo study. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Bashungwa nikuhakikishie na naomba na wewe kama Diwani, basi ushirikiane na Madiwani wenzako katika Halmashauri yako ya Karagwe ili hatua hii, muwafahamishe watalaam waweze kuifanya.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kazi ya kuboresha miundombinu ya maji kwenye Mji wa Biharamulo imefikia kwenye upembuzi yakinifu kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini hatua ya kupata fedha bado iko mbali; na kwa kuwa hali ya upatikanaji wa maji ni dharura sasa hivi Biharamulo, wananchi wanapata maji kwa wiki moja katika wiki nne. Kwa hiyo wiki moja yanapatikana wiki tatu hayapatikani. Je, Naibu Waziri au Waziri wako tayari kuambatana na mimi twende kufanya tathmini ili kuona namna ya kutatua hali ya dharura wakati tunasubiri mradi mkubwa ufikie wakati wake?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, Mheshimiwa Mbunge Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017, Wilaya ya Biharamulo imetengewa Sh. 2,267,018, 000/= kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji. Kwa hiyo, namwomba sana, kwenye Vikao vya Madiwani, auekeze Uongozi wa Halmashauri ya Biharamulo wajaribu kuangalia matumizi ya hizi fedha ambazo tumezitenga kwa kufanya utafiti kama ni kuchimba visima, kama kujenga mabwawa au kama kuna maeneo ambayo yanaweza yakawa na maji ya mtiririko ili kuweza kutekeleza miradi kuhakikisha wananchi wanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama fedha hazitatosha, basi tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili kuona ni jinsi gani sasa tutashirikiana pamoja kuhakikisha kwamba, wananchi hawa wa Biharamulo, ambao wanapata shida ya upatikanaji wa maji kwa muda mrefu hasa kwa kuzingatia kwamba, mradi huu utakaoleta ufumbuzi wa kudumu bado usanifu haujakamilika. Kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Simanjiro, naomba niishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kusikia kilio chetu, lakini sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa swali la msingi lilikuwa linahusu ahadi za viongozi; na kwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano alipopita kwenye maeneo mbalimbali alitoa ahadi kuhusu maji ikiwepo Wilaya ya Kilolo maeneo ya Ilula na aliahidi kwamba suala la maji litakuwa ni historia kwa Wilaya ile. Je, Serikali inasemaje na mwaka huu imetenga fedha kwa ajili ya wananchi wa Ilula?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tatizo la maji linatatuliwa kwa ujenzi wa mabwawa na kwa kuwa kuna mabwawa yaliyojengwa sehemu za Nyanzwa, Ilindi, Ruaha Mbuyuni na Mahenge na wakati yanajengwa wananchi walikuwa wachache, sasa wameongezeka kwa hiyo maji yale hayatoshi. Serikali itakuwa tayari kuongeza fedha ili wananchi wale waweze kupata maji ya uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza suala la ahadi, ahadi zote zimeishaainishwa. Wizara ya Maji tuna ahadi zaidi ya 60 ambazo Mheshimiwa Rais wetu Magufuli wakati anapiga kampeni aliwaahidi wananchi. Kwa hiyo, tutahakikisha kwamba tunatekeleza ahadi za viongozi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Ilula nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari mazungumzo yanaendelea na Serikali ya Australia na mradi huu wa Ilula utagharimu dola milioni tisa, kwa hiyo, tunaufanyia kazi. Pia katika mwaka huu wa fedha kwenye bajeti tumemtengea shilingi milioni 800.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mabwawa, hii ni ahadi yetu, kama tumejenga mabwawa, sasa hivi wananchi wameongezeka, tutakachofanya moja ama ni kulipanua bwawa lile kama lina uwezekano wa kupanuliwa lakini pili ni kuongeza bwawa jipya. Kwa sasa tumeshaagiza Wakurugenzi wote wajaribu kufanya utafiti, waainishe maeneo yote ya kujenga mabwawa na walete ili tuweze kutenga bajeti kwa ajili ya shughuli hiyo.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa eneo hili la Simanjiro na hasa eneo la Orkesumet ambako ametoa majibu Mheshimiwa Waziri kuhusiana na suala la maji katika eneo la Orkesumet limekuwa likiimbwa kuanzia mwaka 2005. Orkesumet ni eneo dogo tu tofauti na maeneo mengine ambayo yana shida kubwa ya maji. Lile ni eneo la wafugaji ambako akina mama wanatoka kwa saa zisizopungua nane kwenda kutafuta maji. Naomba kauli ya Serikali ni lini haidhuru wananchi wa Simanjiro katika Kata za Narakauo, Kimotorko, Emishie, Naberera, Kitwai, Lobosoiret watapata maji? Pia ni lini hasa mradi huo utaanza rasmi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari awamu ya kwanza ya kusaini mkataba mazungumzo yamekamilika. Kwa hiyo, wakati wowote ule pengine kwenye mwezi wa saba, tutakuwa tumesaini mkataba wa awamu ya kwanza na kuanza hiyo kazi. Pia vijiji alivyovitaja, vyote vitapewa maji ikiwa ni pamoja na maji ya mifugo.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda na mimi kuuliza swali dogo la nyongeza. Pamoja na Jimbo la Mbeya Vijijini kuwa na vyanzo vya uhakika wa maji kutoka Mlima Mbeya, lakini maji yamekuwa yakipelekwa Jijini Mbeya badala ya kupelekwa kwenye sehemu zenye uhaba mkubwa wa maji kwenye vijiji vya kata ya Mjele na Utengule Usongwe. Je, ni lini Wizara itapeleka maji safi kwenye vijiji vya kata za Mjele na Utengule Usongwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru ameuliza swali zuri sana, ni swali la kisera. Nimhakikishie kwamba tayari tumeshatoa maelekezo eneo lolote ambalo chanzo cha maji kinaanzia pale, vijiji vilivyo karibu na chanzo ndiyo viwe vya kwanza kupata maji.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tunalielekeza kwa Wakurugenzi wa mamlaka ambao wanahusika na huo mradi, wahakikishe katika eneo hilo kwanza wanawapa maji wananchi waliopo pale baadaye sasa ndiyo wanapeleka maeneo mengine ya mjini. Kwa hili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitalifuatilia mimi mwenyewe.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba sasa niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali tayari imekiri kusambaza mabomba na kupeleka pampu, napenda kujua ni lini sasa utekelezaji wake unaanza kufanyika?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la maji ni kubwa katika Jimbo la Singida Mjini hususani kata za pembeni, Serikali inawaambia nini wananchi wa Jimbo la Singida Mjini kwa ajili ya kuhakikisha tatizo hili linaisha?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni lini mradi wa kusambaza maji katika Mji wa Singida utafanyika, tunahitaji shilingi milioni 730 na tayari tuna vyanzo viwili vya kupata hiyo fedha. Kwanza tumeshaomba fedha kutoka BADEA, lakini pili tumetoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Mamlaka wa Singida kuna fedha kidogo ambazo zipo, kwa hiyo wakati wowote mradi huu utaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua ni lini tutakuwa na mkakati wa kuhakikisha kwamba Mji wa Singida unakuwa na maji ya kudumu. Kama nilivyojibu wakati wa bajeti kwamba tunaanza kujipanga ili tuweze kufanya usanifu wa kutoa maji Igunga kuyaleta Mji wa Singida ili kuhakikisha kwamba sasa tatizo la maji katika Mji wa Singida tunalimaliza. Tutamuagiza Mhandisi Mshauri, aanze kufanya kazi hiyo ili kuona ile pressure iliyoko Igunga inaweza ikafika Singida? Kama itakuwa inapungua basi wataalam watatushauri tufanyeje lakini Mji wa Singida ni mkame tutahakikisha kwamba tunawapa chanzo cha maji chenye uhakika.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa kuleta maji katika Mji wa Singida. Mahali ambapo mitambo, mashine na matanki yale yalipo katika Kata ya Mwankoko ambako ndiko maji yanatoka kwenda kwenye Mji wa Singida wao wenyewe hawana maji. Je, Serikali sasa iko tayari kutumia yale maji kuwasambazia wananchi wa Kata ya Mwankoko ili na wenyewe waweze kufaidi maji ambayo yako kwenye chanzo cha eneo lao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nijibu kwamba Serikali iko tayari na ndiyo malengo yetu kuhakikisha kwamba sehemu ya chanzo cha maji wananchi waliopo pale lazima tuwaheshimu kwa sababu kwanza wamelinda kile chanzo hawajakiaribu, kwa hiyo lazima wafaidi juhudi waliyoifanya na pili wataendelea kulinda miundombinu yetu.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kuuliza maswali mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira ya Jimbo la Mlimba yanafanana kabisa na mazingira ya Jimbo Mbinga Vijijini, je, Serikali itapeleka maji lini katika Miji ya Maguu, Matiri na wa Rwanda ambao una taasisi nyingi sana zikiwemo sekondari za form five na six?
Mheshimiwa Naibu Spia, swali la pili, katika Jimbo la Mbinga kuna miradi miwili ya maji iliyokuwa ikiendelea katika Kata ya Mkako lakini pia mradi mwingine katika Kata ya Ukata kupitia Kijiji cha Litoho. Ni lini Serikali itakamilisha miradi hii ya Mkako pamoja na Ukata ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji salama na safi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itahakikisha inapeleka maji katika maeneo ya Mbinga Vijijini, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tayari tumeanza Programu ya Pili ya Utekelezaji wa Maendeleo ya Sekta ya Maji Nchini. Kama nilivyokwishatoa majibu kwamba wafadhili wametuahidi dola za Kimarekani bilioni 3.3 ambazo zitatumika kutekeleza miradi ya maji hapa nchini, hii ikiwa ni pamoja na miradi ya Mbinga Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu wa fedha Mbinga Vijijini tumewatengea fedha. Niagize na naomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane tutengeneze mpango mzuri wa matumizi ya fedha hizi tulizozitoa katika hii bajeti ya mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai ili kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo ya Mbinga Vijijini wote wanapata maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili umesema kwamba kuna miradi miwili ambayo bado haijakamilika. Tumeshaelekeza kwamba miradi ile ambayo haikukamilika katika Programu ya Kwanza ya Utekelezaji wa Sekta ya Maji ndiyo tunaanza kuikamilisha kabla hatujaanza miradi mipya. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane na Halmashauri yake kuhakikisha kwamba kwanza tunakamilisha miradi hii kabla hatujaanza kuingia kwenye miradi mipya.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Jimbo la Mlimba inafanana kabisa na hali ya Mkoani Pwani kuwa na vyanzo vingi na vikubwa vya maji ikiwemo Mto Ruvu na Mto Rufiji lakini bado wananchi wake wa Wilaya za Kibiti, Rufiji, Mkuranga na Kisarawe wanakabiliwa na adha kubwa ya maji safi na salama.
Je, ni lini sasa Serikali itaanzisha mradi wa kuyavuta maji ya Mto Rufiji ili kuwanufaisha wanawake wa Mkoa wa Pwani?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze, Mheshimiwa huyu mara nyingi sana amekuwa ananifuata na kuniuliza maswali mengi kuhusu miradi ya maji na ameniuliza pia hata kuhusu DAWASCO au DAWASA wanapelekaje maji Pwani, lakini nikuhakikishie kuhusu swali lako moja hili tayari tumeanza mazungumzo ya kufanya utafiti wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji kuyaleta Dar es Salaam ikipitia na maeneo uliyoyataja ya Ikwiriri, kuja Kibiti, kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo tufahamu kwamba tunataka pia kufanya mradi mkubwa wa kujenga bwawa la Kidunda wa kuleta maji. Sasa kama tutakamilisha huu mradi wa Kidunda basi tutaangalia uwezekano kwamba tufanyaje je, tupeleke maji kutoka Kidunda kupeleka huko kwako au tufanye mradi wa Rufiji kwa sababu wakati mwingine unaweza ukafanya miradi miwili mikubwa yale yakawa mengi sana mpaka watu wakashindwa kuyatumia au taasisi za Serikali zikashindwa kuyatumia. Lakini ni kwamba swali lako la msingi ni kwamba ni kweli Serikali sasa hivi inaanza kujiweka tayari kufanya utaratibu wa kufanya utafiti wa kutoa mto Rufiji na kuyaleta Mikoa ya Pwani pamoja na Dar es Salaam.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza naomba nipongeze juhudi za Serikali katika kutatua tatizo la maji nchini, lakini namba mbili naomba niendelee kuipongeza Wizara ya maji kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata ya Mnanila, wananchi wa Kata ya Mwayaya na Kata Mkatanga katika majibu ya Waziri anasema utekelezaji wa maradi huu utaanza katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Maji, watu wale hawaelewi programu ya pili, ya tatu hawaelewi. Swali lao, je, mradi huu unaanza kutekelezwa lini?
Swali la pili Jimbo letu la Buhigwe bado lina vijiji na Kata ambazo kwa kweli bado tuna matatizo makubwa ya maji. Je, Waziri anaweza akatuma wataalamu wake kwenda kwenye Kata ya Rusaba Kibande, Kilelema, Mgera, Kibigwa na Nyaruboza ili kufanya tathimini ya gharama za kupeleka maji katika vijiji vile ili navyo tuweze kuviingiza kwenye programu hapa baadaye?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza hii Programu ya Pili ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inaanza lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Programu ya Kwanza ya Maendeleo ya Sekta ya Maji tuliianza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2006/2007 ambayo imekamilika mwaka 2015 Disemba na katika programu hiyo tulikuwa na wadau wanaotuchangia fedha pamoja na Serikali yenyewe nayo imekuwa inatoa fedha kwa ajili ya utekelezajiwa miradi ya maji. Katika programu hiyo Mheshimiwa Mbunge mwenyewe ni shahidi kwamba miradi ya Munzenze, Kirungu na Nyamgali, ilianza kutekelezwa na sasa hivi ina maendeleo mazuri tu katika hiyo programu ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa programu ya pili tumeianza mwezi Januari, 2016, inaendelea, nayo itadumu kwa muda wa miaka mitano na katika programu hiyo wadau wa maendeleo tayari wameshatoa ahadi ya kutuchangia dola bilioni tatu na nukta tatu. Lakini hiyo ni pamoja na Serikali nayo itaendelea kukusanya fedha na kuchangia kwenye utekelezaji wa miradi kwenye vijiji ambavyo bado havijapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna vijiji ambavyo bado havijafikiwa na hii programu na Mheshimiwa Mbunge ameomba kwamba je, tutatuma wataalam lini? Mheshimiwa Mbunge natambua kwamba unayo Halmashauri ya Buhigwe, lakini Halmashauri ya Buhigwe bado ni changa, tutakachofanya na ambacho tumeshaanza kufanya sasa hivi ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji, inaendelea kuajiri wataalam na kuwapeka katika Halmashauri yako na Halmashauri nyingine zote ambazo zina upungufu wa wataalam. Ili tuwe na wataalam maeneo husika kuliko kuwachukua wataalam kutoka Wizarani. Lakini pale inapohitajika kama utaalamu unahitajika zaidi basi tutakuwa tuko tayari Mheshimiwa Mbunge kuja kutoa utaalamu zaidi kwenye eneo lako.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujua tu katika Wizara ya Maji kuna miradi sugu katika Jimbo langu la Bunda, kuna mradi wa maji Mgeta Nyang’alanga, Nyamswa Salama na kuna mradi wa maji Kiloreli na fedha zinazodaiwa Mgeta ni milioni 119 na Nyamswa ni milioni 229 na Kiloreli milioni 400. Naomba kujua tu hizi fedha zitaenda lini ili miradi hii ikamilike? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Halmashauri ya Bunda Vijijini kiasi kumekuwa na matatizo na kuna miradi ambayo haijakamilika lakini pili, katika utekelezaji Halmashauri haijatuletea hati ili tuweze kulipa hiyo fedha. Kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi na yeye tutasaidiana kufuatilia kuangalia kuna tatizo gani kwenye hii Halmashauri. Kwa nini hii miradi imechelewa sana utekelezaji, kuna tatizo gani? Je, ni ni tatizo la kiutaalam au ni uzembe? Mimi pamoja na yeye tutalifuatilia hili kuweza kuhakikisha miradi hii inakamilika.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, nina swali la nyongeza. Kwa kuwa Mradi wa Maji wa Nyamugali unafanana na Mradi wa Maji wa Mvomero hususani katika eneo la Dihinda, Kanga, Mzia na Lubungo; na kwa kuwa katika maeneo hayo kuna visima virefu vilichimbwa na Wizara mwaka jana. Visima vile vimeachwa kama maandaki na Serikali imetumia mamilioni ya fedha.
Je, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wako tayari kufuatana na mimi kwenda kuangalia visima vile na kutoa kauli ni lini miradi ile itapata fedha ili ikamilike na wananchi wapate maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeshachimba visima, kilichobaki sasa hivi ni kuweka mtandao wa mabomba ili maji sasa yaweze kuchukuliwa kutoka kwenye visima kuwafikia wananchi. Mheshimiwa Mbunge wewe mwenyewe ni shahidi kwamba mwaka huu tayari tumeweka fedha kwenye Halmashauri zote ili kuhakikisha kwamba sasa fedha hizo zitumike kuweka mtandao huo wa maji ili wananchi waweze kupata maji kwa sababu uwekezaji wa visima tayari umeshafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kufuatana naye, tusubiiri tumalize Bunge, Mheshimiwa Mbunge hiyo ni kazi yetu tutapita kila eneo ili kwenda kuangalia matatizo yaliyopo na kushauriana jinsi ya kuyatekeleza.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la kutopeleka fedha kwenye miradi ya maji ambalo kwa mujibu wa swali la msingi liko pia katika miradi mbalimbali inayotekelezwa Mkoa wa Pwani. Mfano mradi wa Ujenzi wa Bwawa Kata ya Chole, Wilaya ya Kisarawe, lilitengewa kiasi cha shilingi 1,500,000,000 lakini zilipelekwa 500,000,000 na bwawa lilipojengwa pamoja na mvua bwawa lile limeharibika.
Je, Naibu Waziri yupo tayari kufanya ziara Wilaya ya Kisarawe kwa kuwa ipo karibu na Dar es salaam ili kuona namna gani watakavyofanya na Wizara ili bwawa lile likamilike kwa wakati na wakazi wa Chole wapate maji kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimwambie kwamba niko tayari kuongozana naye baada ya Bunge kwenda kuangalia hilo bwawa. Lakini pili nimuhakikishie kwamba tayari tunayo tume ambayo kazi yake itashughulikia masuala ya kujenga mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji. Tume hiyo sasa hivi iko tayari na tutahakikisha kwamba tunapeleka fedha na tatizo hili kwamba ilipelekwa fedha lakini nyingine haijaenda nafikiri tatizo kubwa ni huu utaratibu tuliouweka kwamba kama ujaleta hati sasa na sisi tutashindwa kuomba fedha kutoka Hazina. Tunachataka kwanza utuletee hati ili ile hata tuipeleke Hazina na Hazina wapate ushahidi kwamba kazi imefanyika waweze kutupa fedha ili tuweze kuzileta.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona, kwa kuwa tatizo la maji lililopo Urambo linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo la maji lililopo katika mji wangu mdogo wa Mlowo, na kwa vile katika Mji huo kuna mto uitwao Mto Mlowo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuchimba mabwawa katika mto huo ili kuhakikisha kwamba wananchi wa mji mdogo wa Mlowo, hususani wanawake ambao Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba ndio wachotamaji wakubwa wanaondokana na adha hiyo ya mji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ametuomba kwamba tuna Mto Mlowo na akinamama wanakwenda kuchota maji Mto Mlowo, sasa haoni kwamba kuna umuhimu wa kuchimba mabwawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaagiza tayari kwamba Halmashauri zote zifanye utafiti na zilete mapendekezo ili Serikali iweze kutenga fedha kuhakikisha kwamba kila Halmashauri na tumeomba kwamba kila Halmashauri kila mwaka ihakikishe inachimba bwawa moja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Shonza naomba na wewe ni Diwani, tusaidiane kwenye vikao vyetu tuelekeze kwamba Wakurugenzi na wahandisi wa maji wa Halmashauri zetu wafanye utafiti ili tuweze kupata maeneo ya kuchimba mabwawa tuweze kuondoa hii kero ya maji.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mwaka 2013 Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kuchimba visima vinane katika vijiji vinane, lakini hadi sasa shilingi milioni 184 tu zilizopelekwa.
Naiuliza Serikali ni lini sasa kwa sababu azma ya Serikali ilikuwa ni kuchimba visima vinane; ni lini sasa Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya visima hivyo?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ujasikia vizuri swali? Mheshimiwa Ndassa sehemu ya mwisho ya swali ni lini?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Katika Jimbo la Sumve na Jimbo la Kwimba Serikali ilipanga kuchimba visima vinane katika vijiji vinane vya Isunga, Kadashi, Gumangubo, Shilima, Mande na Izimba A. Fedha zilizotengwa ni shilingi bilioni 3.6 lakini hadi juzi ni shilingi milioni 185 tu ndizo zilizopelekwa, kwa hiyo, miradi hii imekwama, ni lini sasa Serikali imepeleka fedha hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumeishaelekeza tayari, kwamba ukishapata bajeti, Halmashauri ikipata bajeti, kitu cha kwanza ni kufanya taratibu za manunuzi. Kuhakikisha kwamba mkandarasi anaanza kazi, na akishatekeleza kazi utuletee hati, ya madai ya mkandarasi tuweze kuipeleka kwa Waziri wa Fedha aweze kutupatia fedha.
Nina wasiwasi lakini tutashirikiana na Mheshimiwa Ndassa kuangalia ni kazi ipi imeishafanyika tangu kupeleka hiyo hela, inawezekana kwa sababu hata wakati wa ziara yangu niliona hiyo. Unakuta mtu ametengewa bajeti lakini hajafanya kazi yoyote, anasubiri kwamba kwanza aletewe hela, utaratibu huo kwa sasa hatunao. Ukishapata bajeti basi fanya taratibu za manunuzi na mkandarasi afanye kazi akifanya kazi ndio tutampatia hela.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona, aliyoyazungumza Mheshimiwa Ndassa yanafanana na Jimboni kwangu Mbagala. Kuna mradi ule wa maji, Mpera na Kimbiji, ambao sasa hivi unafika miaka nane, haujatekelezwa na wala maji hakuna. Lakini vilevile kulikuwa na mpango wa kuchimba visima virefu katika Jimbo langu, mpaka leo mpango ule haujatekelezwa kwa kukosa fedha.
Je, Waziri anatupa jibu gani wakazi wa Mbagala, na wananchi wa Mbagala kwa ujumla, lini visima vile vitaanza kuhudumia Jimbo la Mbagala na Dar es Salaam kwa ujumla na je, ule mpango wa visima virefu upo au umekufa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maji inaendelea na mradi wa kuchimba visima vya Mpera na Kimbiji; na mpaka sasa tunavyoendelea tayari tumeishafikia asilimia 60, na mradi huo unakamilika mwezi Disemba mwaka huu. Baada ya hapo tutaanza na mradi mwingine sasa wa kuweka mabomba, ambayo sasa yatatoa maji kwenye visima na kuyasambaza mpaka kwenye maeneo yake, ya Mheshimiwa Mbunge ya Mbagala. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba hakuna wasiwasi ule mradi unaendelea, na mwaka huu unakamilika. Lakini pia ameomba kwamba je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima virefu? Ni kwamba tunaendelea kulingana na bajeti tunavyotenga, tutaendelea na kama maji yanapatikana tutaendelea kuchimba visima virefu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kufahamu, kule Jimboni Mbulu kuna Bwawa la Dongobesh lililokamilika takriban miezi sita. Mkandarasi ameshaleta certificate yapata miezi miwili. Waheshimiwa Mawaziri wanajibu majibu hapa, lakini kule Wizarani hakuna mchakato wa kuwalipa hao Wakandarasi. Naomba, kama itawezekana, Waziri ana kauli gani kumlipa Mkandarasi wa Bwawa la Dongobesh?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Dongobesh ni kweli ujenzi wake umeshakamilika, kilichobaki ni miundombinu ili lile bwawa sasa liweze kufanya kazi kwenda kumwagia kwenye mashamba. Tumeweka utaratibu kwamba certificate zifike. Wiki iliyopita niliongea na Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka wiki iliyopita certificate zilikuwa hazijawasilishwa katika Wizara, lakini tunaendelea kufuatilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshamwagiza Mkurugenzi wa Maji Vijijini ili aweze kuwasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbulu Vijijini ili waweze kuangalia hizi certificate ziko wapi, kwa sababu kule wanasema zimetumwa, lakini Wizarani hazijafika. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hili suala tunalifanyia kazi na pindi certificate zikifika hela tunazo, tunalipa, ili hili bwawa liweze kukamilishwa.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kama Serikali ipo tayari kupeleke pesa hizo, lakini nataka kujua ni shilingi ngapi zitapelekwa kwa ajili ya kumalizia huo mradi wa Skimu ya Lwafi? Nataka kujua kiasi cha pesa.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, fedha itakayopelekwa kule ni shilingi milioni 550 na fedha hii inatolewa na Serikali ya Japan na tayari taratibu za kuipeleka hiyo fedha zimeshafanyika ila kumekuwa na matatizo kidogo kupanua ile item ya kulipia kwa upande wa Halmashauri, ndiyo Serikali inaendelea kupanua. Fedha hiyo ipo tayari na wakati wowote itaingia.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa hali iliyopo Lwafi inafanana sana na hali iliyopo na mpango wa Wilaya ya Bukombe ambapo skimu ya umwagiliaji ilijengwa, iliyokuwa inagharimu shilingi milioni 606, lakini fedha ambazo zimeshatoka ni asilimia 58 peke yake. Skimu hiyo ilikuwa inakusudiwa kuhudumia Vijiji vya Kasozi, Nampangwe pamoja na Kijiji cha Msonga na hekta 100 zingeweza kuhudumiwa na skimu hii. Mpaka tunavyozungumza hapa, mradi huo umesimama: Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Nampangwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba skimu hiyo haijakamilika na kwamba fedha iliyolipwa ni asilimia 58 tu. Namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tumeamua kwanza kukamilisha miradi iliyokuwa inaendelea; na kwa sasa tupo vizuri. Tume ya Umwagiliaji imeshaundwa na ipo sasa hivi inajipanga, kwa hiyo, sasa hivi tutakuwa na mfumo mzuri wa kuhakikisha miradi hii inakamilika.
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Miradi ya maji iliyopangwa kutelekezwa katika mwaka wa fedha 2015/2016 katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida Vijijini ya ukarabati wa miundombinu ya visima ya Sagara, Mdilu, Ihanuda na Mwasawiya pamoja na ile inayotumia pampu za mkono ya Vijiji vya Muhamo, Mkimbii, Mwanyonye, Mitula, Mwakiti, Ndugwire, Gauri na Kinyeto haijatekelezwa mpaka sasa na hii ni kutokana na ukosefu wa fedha:-
Swali; ni lini na wakati gani fedha zitaletwa kukamilisha miradi hii? Je, ni lini Serikali itawatua ndoo wanawake wa Mkoa wa Singida?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Aysharose swali la nyongeza, unauliza moja tu. Kwa hiyo, chagua kati ya hayo maswali, unalotaka ujibiwe.
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Je, ni lini na wakati gani fedha zitaletwa kukamilisha miradi hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi ya visima Singida, nimeeleza katika Bunge hili kwamba kuanzia sasa hivi Serikali haitapeleka fedha kwenye miradi ya maji kabla miradi haijatekelezwa. Kinachotakiwa ni kwamba lazima kwanza ulete certificate ili tuwasilishe Hazina kuomba fedha tuweze kuzileta.
Swali lake, ni lini fedha zitaletwa? Fedha tutapeleka kulingana na upatikanaji wa fedha katika Serikali na nina hakika kwamba mwaka wa fedha unaokuja, akituletea certificate kuhusu hivi visima, kwa vyovyote vile fedha tutapeleka.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la Busega linafanana na tatizo la Mkoa wa Tabora, hususan Tabora Manispaa; na kwa kuwa tuna bwawa la Kazima ambalo kina chake ni kifupi: Je, Serikali ipo tayari sasa kukarabati bwawa hilo ili tuweze kupunguza tatizo la maji Mkoa wa Tabora hususan Tabora Manispaa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa la Kazima lilijengwa mwaka 1946 na bwawa hili lilijengwa na watu wa reli kwa ajili ya kupata maji ya kupoza engine zile ambazo zilikuwa zinatumia mkaa. Mwaka 1990 matumizi yalibadilika baada ya kupata engine ambazo zinatumia diesel, kwa hiyo, ikaamuliwa bwawa hili liwe linatumika kwa ajili ya maji ya kunywa. Sasa hivi linamilikiwa na Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Tabora (TUWASA) na linazalisha lita milioni 1,400 ya maji safi na salama kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka imeomba shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuimarisha lile tuta kwa sababu mwaka huu maji yalijaa sana, lakini pia lipo shirika linalohudumia maeneo ya Lake Tanganyika. Mamlaka wameomba ili waweze kulikarabati lile bwawa liendelee kuhimili kuweka maji mengi na kuendelea kuwahudumia wananchi wa Tabora. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwanne nikuhakikishie kwamba suala hili linafanyiwa kazi kuhakikisha kwamba bwawa hili linakarabitiwa.
MHE. NDAKI M. MASHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa mradi wa maji kutoka Busega, Bariadi, Itilima hata Maswa Mjini unaishia Maswa Mjini kwa maana ya Jimbo la Maswa Mashariki na kwa kuwa Wizara Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri nimewashauri kwa Jimbo la Maswa Magharibi tuunganishwe na mradi wa maji unaotoka Ngudu, Malya, kuja Malampaka. Je, Serikali ipo tayari sasa kuchukua ushauri wangu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme tunaupokea ushauri, tutaufanyia kazi, lakini maji yatatoka wapi? Itategemea na utafiti wa wataalam kuangalia sehemu ambayo itakuwa ni rahisi kuyafikisha maji. Kwa hiyo, niseme tu kwamba ushauri wake tunaupokea na lengo siyo kupeleka maji mijini tu, hapana. Kama nilivyosema katika jibu nililojibu muda mfupi uliopita ni kwamba tutakuwa tunaendelea kutenga fedha, kama maji yanatosheleza, yaendelee hata nje ya miji.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na kwa Serikali yetu kwa mpango mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu kwa kweli ni mradi ambao una tija kubwa sana kwa wananchi wa maeneo husika katika Wilaya ya Busega, Wilaya ya Itilima, Bariadi, Maswa na Meatu. Kwa kuwa mradi huu utakapopita vijiji ambavyo vipo umbali wa kilomita 12, kushoto na kulia mwa bomba kuu, vitapata huduma ya maji: Je, Serikali ina mpango gani kwa vijiji ambavyo vipo nje ya mradi huu kupatiwa maji ili waweze kunufaika na mradi wa namna hii? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Ziwa Victoria lina maji mengi sana na mikoa mingi ina matatizo ya maji, kwa nini Serikali isiwe na mpango mwingine kabambe; baada ya Mkoa wa Simiyu kupata maji, basi Mkoa wa Singida na wenyewe upate maji na mpaka Dodoma nao waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa kunipa pongezi; lakini pili, vijiji vinavyotarajiwa kunufaika na mradi huu ambavyo vipo umbali wa kilomita 12 kutoka katikati ya bomba ni vijiji 223.
Swali lake namba moja ameuliza, vijiji ambavyo vipo nje ya zile kilomita 12; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya mradi kukamilika huwa tuna utaratibu wa kuendelea kutoa fedha kwenye mamlaka zilizo karibu na hilo bomba ili ziweze kuendeleza kupeleka maji kwenye maeneo ambayo hayakupitiwa na huo mradi. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo kama ambavyo tumeshaendelea kufanya kwenye mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Shinyanga.
Swali la pili, Ziwa Victoria lina maji mengi; ni kweli lina maji mengi. Kuna utaratibu gani wa kupeleka maji kwenye maeneo ambayo hayajapata maji ikiwemo pamoja na Mkoa wa Singida?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tayari tuna mradi tumepata Dola milioni 265 na mwaka wa fedha unaokuja tunasaini mkataba kwa ajili ya kupeleka maji ya Ziwa Viktoria, Nzega, Mkoa wa Tabora hadi Igunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumesema kwamba sasa hivi tutaanza kufanya utafiti, upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kupeleka maji pia katika Mkoa wa Singida ambao ni mkoa kame na hauna maji ya kutosheleza kule chini. Kwa hiyo, tunaendelea kufanya tafiti ili kuhakikisha kwamba maji yanawafikia wananchi wote.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili mafupi ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali ina mpango wa kusambaza mabomba maeneo ambayo hayana mabomba ya maji, nataka kujua muda gani ambao Serikali itasambaza mabomba hayo?
Swali la pili, kuna baadhi ya maeneo Morogoro Mjini hawapati maji karibu miezi miwili, lakini cha kushangaza wanapelekewa bili za kulipa maji, je, ni lini Serikali itaondoa kero hiyo ambayo imekuwa kama dhuluma kwa wananchi wa Jimbo la Morogoro Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni muda gani tutakamilisha kuweka mtandao wa mabomba ya kusambaza maji ili yaweze kufika maeneo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge Abood aangalie katika kitabu cha bajeti, tumetenga zaidi ya shilingi bilioni nne kwa mwaka wa fedha unaokuja wa 2016/2017 kwa ajili ya kuendelea na kazi ya kuweka mabomba ya mtandao katika Jimbo lake la Morogoro Mjini. Kwa hiyo ni muda gani, kwa sababu utekelezaji una mchakato wake, mchakato wa bajeti tayari umekamilika fedha Serikali imetenga. Kwa hiyo, tutaendelea na usanifu, tutaendelea na kutangaza tenda na baada ya kutangaza tenda kumpata mkandarasi ndiyo program kamili lini tutatekeleza mradi kwa miezi mingapi itapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tatizo la bili za maji. Nashukuru kwamba nimepata hii taarifa, Mheshimiwa Mbunge hili suala tutalifuatilia kuona inakuwaje kwamba mtu analetewa bili za maji wakati maji hatumii?
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili nililikuta pia katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara nilipokwenda kule. Suala hili wakati mwingine linakuwa na udanganyifu. Kuna connection ambazo hazijatambuliwa na mamlaka, mtu anaiba maji, sasa wakimtambua wanakwenda kumpiga bili analalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi ambayo yanajitokeza katika hili suala la bili, lakini pia kuna uzembe vile vile hata ndani ya watendaji wetu kwa upande wa mamlaka. Kwa hiyo, nimwombe tu Mheshimiwa Abood tushirikiane. Nitatoa taarifa kwa Mamlaka ya Mji wa Morogoro ili waweze kuliangalia hili na tutampatia majibu.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Jimbo la Morogoro Mjini linafanana kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini juu ya tatizo hili la ukosefu wa maji. Kwa kuwa Waziri alishaniahidi kwamba tukipeleka certificate atawasaidia wakandarasi kuwalipa fedha waendelee na mradi. Je, ni lini sasa watapatiwa fedha, miradi ya Mbulu iliyopo Haidom na Dongobeshi ili wakandarasi waweze kumalizia na wananchi wapate maji? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru. Tumekuwa na matatizo huko nyuma kwamba, tunapeleka fedha katika Halmashauri wanachelewa kutekeleza miradi. Sasa hivi tumeweka utaratibu kwamba tukishatenga bajeti, basi Halmashauri zitangaze tenda zianze kutekeleza miradi. Certificate ikipatikana watuletee tutaipeleka Hazina, halafu wakitupatia pesa ndiyo tuweze kupeleka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama tulivyoongea kama ulivyosema Mheshimiwa Massay naendelea kusisitiza kwamba walete certificate halafu pesa tutalipa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona ili niulize swali dogo tu la nyongeza, kwa kuwa swali la msingi wananchi wa Morogoro linafanana sana na wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi hususan Mji mdogo wa Itigi. Je, ni lini Serikali itasaidiana na Halmashauri yangu kuhakikisha Vijiji vya Rungwa, Kintanula, Kalangali, Mitundu, Kingwi, Dodiandole, Mbugani, Mabondeni, Njirii, Gurungu, Majengo, Songambele, Kitalaka, Kihanju na Tambuka Reli vitapatiwa maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kushirikiana na Halmashauri zote nchini kwa kuzipangia bajeti ili ziweze kutekeleza miradi ya maji. Hilo limeshafanyika, katika Mwaka wa Fedha unaokuja Serikali imehakikisha Halmashauri zote inazipatia fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zilizotolewa kwanza ni kuhakikisha kwamba miradi iliyokuwa inaendelea inakamilika, baada ya hapo ndipo wanakwenda sasa kwenye miradi mipya. Kwa hiyo, kwa mujibu wa swali lake Serikali tayari inashirikiana na Halmashauri, sasa ni wajibu wake Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu na yeye ni Diwani, kukaa katika kikao cha Madiwani na uongozi wa Halmashauri ili waweze kupanga bajeti kwa hela iliyotengwa ili hivyo vijiji viweze kufikiwa. Kama fedha haitatosha basi mwaka ujao wa fedha wataleta maombi, tutatenga fedha nyingine.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya maji katika Jimbo la Lushoto yanafanana sana na matatizo ya Jimbo la Handeni Vijijini. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuweza kufanya ziara katika Jimbo la Handeni Vijijini na kujionea matatizo ya Maji katika Jimbo hili? Je, yuko tayari ama anatoa commitment gani kwa fedha ambazo amesema zitatoka kwa miradi ya maji katika Jimbo la Lushoto? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na swali la mwisho. Mheshimiwa Naibu Waziri anatoa commitment gani; tayari Bunge lako limeshapitisha bajeti ya Mwaka wa Fedha wa 2016/2017 na katika bajeti hiyo kuna shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya Lushoto, kwa hiyo, hakuna commitment zaidi ya hiyo. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge sasa ashirikiane na Halmashauri ili kuendelea sasa kufanya matumizi ya hizi fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya Handeni. Tayari tuna mradi wa HTM ambao utekelezaji wake unaanza mwaka wa fedha unaokuja. Ni mradi mkubwa ambao utapitia maeneo mengi katika Mji wa Handeni na hatimaye kuhakikisha kwamba, tunakamilisha mradi huu. Maeneo ambayo hayatafikiwa na mradi huo Halmashauri zihakikishe kwamba, zinatumia fedha iliyopangwa kwa ajili ya ama kuchimba visima au kutengeneza mabwawa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, wananchi wote wa eneo hilo wanapata huduma ya maji. Kama fedha hazitatosha zilizopangwa basi ni wajibu wa Halmashauri kuhakikisha wanaleta maombi ili tuweze kutenga fedha katika Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Tatizo la Lushoto linalingana kabisa na Korogwe Vijijini hasa kwenye Mji Mdogo wa Mombo. Serikali kwa kupitia Benki ya Dunia ilitenga milioni 900 kwa mradi wa maji ambao unakwenda kutoka Vuga mpaka Mombo kwa kupitia Mombo kwenda Mlembule. Mradi huu umekamilika kwa asilimia 80, tatizo ni kwamba, wananchi wanaolinda chanzo cha maji katika Wilaya ya Bumbuli au katika Mji wa Bumbuli ambao wanatoka Vuga walikuwa wanaomba wapatiwe maji na sasa hivi Serikali iliahidi kwamba, wale wananchi wanaolinda chanzo cha maji watapatiwa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini mradi huu wa Mombo ambao Serikali imetumia gharama zaidi ya milioni 900, lakini mpaka sasa hivi haujakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji katika Sera yake na katika mipango yake imeweka mpango kwamba, Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 kwanza inakamilisha miradi iliyokuwa inaendelea kabla haijaingia katika miradi mipya. Kwa hiyo, mradi wako Mheshimiwa Mbunge ambao umeuita ni mradi wa Benki ya Dunia na imebakia kidogo mradi huo utakamilika, lakini pia ni sambamba na kuwapelekea maji wananchi wa eneo ambalo ni chanzo cha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu imepanga kwamba, maeneo yote ambayo maji yanatoka katika lile eneo, basi maji lazima na huko yapatikane. Kama utaratibu huo haukuwepo, naomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na
Halmashauri washauriane ili mwaka wa fedha 2017/2018 tuweze kutenga fedha kuhakikisha wale wananchi wa kwenye chanzo cha maji wanapata maji.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, vilevile katika Jimbo langu la Mpwapwa kuna matatizo makubwa sana ya maji katika Vijiji vya Mima, Chitemo, Berega, Nzase, Lupeta, Bumila na Makutupa na kulikuwa na mradi mkubwa sana wa maji na mpaka sasa umechakaa. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuusaidia ule mradi uanze kuhudumia wananchi wa vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari na ndiyo maana inatenga bajeti na imetenga bajeti kwenye Wilaya zote ikiwemo pamoja na Wilaya ya Mheshimiwa Lubeleje. Katika malengo yetu tunakamilisha miradi inayoendelea, lakini pia, tunaomba Halmashauri mtuletee maombi ya fedha kwa ajili ya ukarabati wa miradi ya zamani ili iendelee kufanya kazi kama ambavyo nilijibu katika swali la msingi la Mheshimiwa Abood kule Morogoro kwamba, tunataka tuhakikishe kwamba, miradi yote inayoendelea inakarabatiwa, ili kuondoa matatizo ya uvujaji wa yale mabomba unaosababisha maji kupotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa tu kwamba, tuko pamoja na yeye na Serikali iko pamoja na Halmashauri yake. Kinachotakiwa watumie fedha tuliyowapa, lakini mwaka wa fedha utakaokuja basi walete maombi tena ili tuweze kutoa hiyo fedha.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, Bunge lililopita kuna fedha zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ile miradi 10 ya World Bank katika Vijiji Mji vya Mji wa Korogwe ikiwemo Lwengela Relini, Lwengela Darajani na Msambiazi. Je, Serikali ina mpango gani kwa sababu kwenye bajeti hii sijaona hiyo fedha? Safari iliyopita hawakupewa zile fedha, safari hii wana mkakati gani kuhakikisha kwamba vijiji hivi vinachimbiwa vile vile visima virefu kama ambavyo ilikuwa imepangwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya Miradi ya World Bank ambayo haikukamilika, kama ambavyo nimeshajibu awali kwamba, katika bajeti tuliyoitenga mwaka huu, basi tuhakikishe kwamba tunakamilisha kwanza ile miradi ambayo haikukamilika kabla hatujaingia kwenye miradi mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, natambua pia, kwamba, eneo la Korogwe lina matatizo makubwa ya maji, baadhi ya vijiji bado havijapata. Kupitia mradi wa HTM ambao chanzo chake nacho kinatoka katika ule Mto Ruvu tutahakikisha kwamba, sehemu ya maji hayo yanapita kwenye Vijiji vya Korogwe ili kuhakikisha kwamba, wananchi wote wa eneo la Korogwe wanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo hayatafikiwa na mradi tuhakikishe kwamba tunashirikiana na Halmashauri kwa ajili ya kuchimba visima au kujenga mabwawa. Kama fedha haipo katika Mwaka wa Fedha 2016/2017 basi wahakikishe wanaharakisha kuleta maombi, ili katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tunatoa fedha. Katika hiki kipindi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutatembelea hilo eneo, tutatembea kuja kujionea hali halisi.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, kwa vile Serikali imebuni mradi huo ambao utatusaidia sana sisi Wana-Uyui hasa Tabora Kaskazini, je, Serikali sasa iko tayari kuviorodhesha vijiji ambavyo vitakuwa katika mradi huo ili vijiji ambavyo havitakuwa ndani ya mradi tuvishughulikie kuvipatia maji?
Swali la pili kuhusu mradi wa Malambo ya maji, je, Serikali sasa iko tayari kutoa ahadi kwamba iko tayari kuanza utafiti wa wapi malambo hayo yatachimbwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na swali la pili kuhusu mpango wa Serikali kujenga mabwawa, kwanza naomba nitoe taarifa kwamba kulingana na survey ambayo tumeifanya, tuna mabwawa 3,000 ambayo yameshajengwa hapa nchini kwetu. Katika hayo, asilimia 50 yanafanya kazi na asilimia 50 hayafanyi kazi.
Kwa hiyo, mpango tulionao ni kuhakikisha kwamba haya asilimia 50 ambayo hayafanyi kazi tunayafanyia ukarabati. Pamoja na hiyo, Bunge la Bajeti lililopita tulielekeza kila Halmashauri wahakikishe kila mwaka wanasanifu bwawa moja na wanaleta ili tuweze kutenga fedha kuhakikisha kwamba kila Halmashauri kila mwaka inajenga bwawa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu ni vijiji gani ambavyo vimeainishwa kwenye huu Mradi wa Kutoa Maji Ziwa Victoria kupeleka Tabora? Maeneo yatakayopitiwa na mradi huu ni pamoja na Kata ya Upuge; ambayo ni Kijiji cha Upugwe, Muhogwe, Lungunya na Kasenga vitapata maji.
Kata ya Magiri ambayo ni kijiji cha Magiri, Imalampaka, Kalemela vitapata maji. Kata ya Isikizya; ambapo kijiji cha Ilalwasimba, Isikizya, Igoko, Ibushi vitapata maji. Kata ya Ibelamailundi; kijiji cha Ibelamailundi, Mtakuja, Itobela, Isenegeja vitapata maji na pia Kata ya Ilolangulu; ambapo Kijiji cha Kasisi „A,‟ Ngokolo na Isenga vinatarajiwa kupata maji kupitia katika mradi huu. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wanawake wa Mkoa wa Simiyu ni wajasiriamali wazuri sana. Je, ni lini Serikali itaanzisha Benki ya Maendeleo ya Wanawake ili wanawake wa Mkoa wa Simiyu waweze kujikomboa na kujinufaisha na benki hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais ni kupeleka kila kijiji na kila mtaa shilingi milioni 50 ili kuwawezesha wanawake na vijana. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kusimamia pesa hizo na kuhakikisha kwamba zimewafikia walengwa, zisije zikaishia mikononi mwa watu wachache, wajanja kama mapesa ya JK? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumbukumbu ya Wabunge yote wakati Waziri wa Afya ambaye anahusika na mambo ya maendeleo ya jamii ambapo Benki hii ya Wanawake iko katika dhamana yake, nakumbuka katika bajeti ya mwaka huu alizungumza wazi kwamba suala la ufunguaji wa matawi ya benki hii utafanyika kwa kadri rasilimali fedha inavyopatikana. Imani yangu ni kwamba kauli ile ya Mheshimiwa Waziri itaendelea kusimamiwa na katika Ukanda ule wa Ziwa benki hii itafunguliwa lengo kubwa likiwa ni kufikisha huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la shilingi milioni 50, ni kweli, sisi tunafahamu kwamba katika mchakato wa bajeti ya mwaka huu zile fedha zilitengwa na naamini Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inahusika na kusimamia jambo hili inapanga utaratibu mzuri na ndiyo maana wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anapita maeneo mbalimbali alikuwa akitoa maelekezo kwamba watu waache kuunda vikundi vya kitapeli ambapo mwisho wa siku fedha zile zitakuja kupotea. Imani yetu ni kwamba katika kipindi tutashirikiana vizuri wananchi wote na Serikali ili tusifanye makosa yale yaliyojitokeza katika kipindi cha nyuma katika fedha zile za mamilioni ya JK, sasa tunasema hatutarudia tena utaratibu ule wa mwanzo.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu, hata hivyo naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkoa mzima wa Dodoma hakuna sehemu ambayo tuna mto unaotiririsha maji mwaka mzima, na kwa kuwa mradi ule haukuzingatia uchimbaji wa bwawa kwa maana ya kuyahifadhi maji ili baadaye wananchi waweze kuyatumia kwa kumwagilia.
Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini juu ya uchimbwaji wa bwawa ili tuweze kuvuna maji na baadae tuweze kuyatumia na ili ule mradi uweze kuleta ufanisi?
Swali la pili, kwa kuwa kwenye majibu ya Serikali kuna baadhi ya vitu vingi vimeachwa, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kujionea kwa macho hali ilivyo kwenye mradi huo? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni kweli Mkoa wa Dodoma hauna mito ambayo inatiririsha maji mwaka mzima na ndiyo maana Mheshimiwa Lusinde wewe ni shahidi, kupitia Bunge la Bajeti ambalo limeisha juzi juzi hapa la mwaka huu wa fedha tuliagiza kwamba kila Halmashauri ifanye usanifu wa bwawa moja kila mwaka kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua na pia kukinga maji ya mifereji au mito ili tuwe na maji toshelezi kwa ajili ya matumizi ya binadamu mifugo na kilimo cha umwagiliaji.
Pamoja na hilo Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maji tumeeamua kwamba miradi yote mikubwa ya maji kuanzia sasa tutakuwa tunaweka mabomba mawili, bomba la maji safi ya kunywa pamoja na bomba kwa ajili ya umwagiliaji na kwa kuanza, mradi ambao unakuja ambao utahusisha ujenzi wa Bwawa la Farkwa kwa ajili ya maji ya Dodoma tumesanifu na tumeweka mabomba mawili, moja kwa ajili ya maji masafi ya binadamu na maji ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, swali la pili umeuliza kama niko tayari kuongozana na wewe kwenda kwenye eneo lako kwa sababu sasa hivi ni kipindi cha Bunge, Mheshimiwa Spika kwa ruksa yako niko tayari, lakini baada ya Bunge basi itabidi nipewe ruhusa na Waziri wangu wa Maji na Umwagiliaji.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuchelewa kukamilisha kwa miradi ya maji ya vijiji vya Nandembo, Nalasi, Lukumbule na Amani; je, Serikali haioni kwamba kuchelewa kukamilisha miradi hiyo kutaongeza gharama ya miradi?
Swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji amesema vijiji vya Majimaji, Muhesi, Nakapanya na Mchoteka utekelezaji wake haukufanikiwa kutokana na kukosa vyanzo. Je, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha vyanzo vinapatikana na utekelezaji huu unaanza mara moja kwa sababu jambo hili ni la muda mrefu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza amezungumzia Serikali haioni kwamba kuchelewa utekelezaji wa miradi kuna ongeza gharama; ni kweli ukichelewa utekelezaji wa mradi gharama inaongezeka kwa sababu kuna mabadiliko ya bei ambayo yanatokana na vifaa vya ujenzi, lakini pili wale wakandarasi wanaojenga wameajiri watu wao ile gharama ya mishahara muda unakuwa mrefu, kwa hiyo ni kweli kabisa kwamba kuchelewa kunaongeza gharama ya miradi. Kuchelewa kwa miradi kunatokana na matatizo ambayo yanajitokeza katika mkataba siyo kwamba ni suala ambalo linapangwa na binadamu basi tu ni kwamba, kwa mfano tunachelewa kwa sababu katika utekelezaji wa hii miradi tunasaidiana na wadau ambao ni marafiki zetu ambao wanatusaidia katika utekelezaji wa miradi sasa hela ikichelewa kupatikana basi kwa vyovyote vile lazima mradi uchelewe.
Mheshimiwa Spika, wakati mwingine tuna-design mradi kumetokea mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na binadamu vyanzo vinakosa maji kwa vyovyote mradi ule lazima utachelewa.
Swali lake la pili amezungumzia suala la vyanzo, ni kwamba Serikali kwa sasa tayari kwa miradi ambayo haikupata vyanzo study zinaendelea kuhakikisha kwamba miradi hiyo inapata vyanzo na lazima vyanzo vipatikane ili tuweze kukamilisha utekelezaji wa hiyo miradi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya kuhudumia miradi ya maendeleo ya maji katika Kijiji cha Igagala na Kijiji cha Majalila ambacho ni Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Tanganyika. Serikali ilipotoa hizo fedha usimamizi wa mradi huu haukwenda sahihi. Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia miradi ambayo tayari fedha ilikuwa imetengwa na wafanyakazi ambao ni wasimamizi wamesababisha hasara ya kutokukamilika kwa mradi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya ziara Mkoa wa Katavi na mimi niliungana naye na hii miradi tuliitembelea na yale matatizo tukayakuta, kwamba miradi imeanza, miundombinu imejengwa lakini bado kuna matatizo madogo ya kuweka pump ili wananchi waendelee kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuta pia kweli kulikuwa na tatizo la kimikataba lakini tatizo hilo tayari nimeshaliwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ili waweze kuwasiliana na Katibu Mkuu wa TAMISEMI kwa sababu Halmashauri ya Mji wa Mpanda ndiyo iliyosaini ule mkataba. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hili tayari tumeshalichukua tunalifanyia kazi.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo la maji katika Jimbo la Nyangh‟wale ni kubwa sana. Kuna mradi ambao unaendelea pale wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka Wilayani Nyangh‟wale. Mradi huo umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu na nimejaribu kuongea na wakandarasi wanadai kwamba wamesimama kuendeleza mradi ule kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Kuna mabomba mengi ambayo yameshasambazwa na yapo nje yanapigwa jua kwa zaidi ya miaka mitatu. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwapatia fedha hawa wakandarasi ili waweze kukamilisha mradi huo wa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwamba Bunge lilipitisha Mfuko wa Maji na Mfuko huu tunashukuru kwamba kila mwezi fedha inatoka na ninyi wenyewe ni mashahidi huko mlikotoka kutokana na Mfuko huu tayari yale madeni yanalipwa na tunaendelea kulipa. Kama madeni hayajalipwa basi ujue kuna matatizo madogo madogo ya kiutendaji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Hussein mimi nalibeba niangalie kwa nini huko hakujalipwa ili tuhakikishe kwamba mradi huo wakandarasi wanalipwa ili waweze kuukamilisha.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja tu la nyongeza. Katika Mji Mdogo wa Makongorosi na Mji Mkubwa wa Chunya, matatizo ya maji ni makubwa sana. Ni makubwa kiasi cha kuweza kuvunja ndoa za watu wanapofuata maji kwenye visima mbugani.
Sasa toka alipokuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda aliona Makongorosi na Chunya, Mheshimiwa Kikwete akiwa Rais ameona matatizo ya maji Chunya na Makongorosi na Mheshimiwa Magufuli katika safari yake ya kampeni ameona matatizo ya maji katika Mji Mdogo wa Makongorosi na Mji wa Chunya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka commitment kutoka kwa Serikali. Ni lini Waziri pamoja na kwamba ziko milioni 500 sijui anasema zimepangwa kwa mwaka huu, lakini ikija mwisho wa mwaka watasema Treasury haijaleta hela. Je, ni lini Waziri au Naibu Waziri atakuja Chunya nimwoneshe hali mbaya ya maji katika Mji wa Makongorosi na Mji wa Chunya ili tukija hapa Bungeni aweze kunijibu vizuri.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Mji wa Makongorosi na Chunya una matatizo makubwa ya maji lakini pia, kuna kikundi ambacho kilikuwa kinachimba madini eneo linaitwa Ujerumani, imeonekena pana maji mengi sana. Sasa hivi Wizara inafanya utafiti kama yale maji yanafaa ili yaweze kuwekewa miundombinu yasambazwe katika maeneo ya Makongorosi na Chunya.
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya Mheshimiwa Mbunge kwamba ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja, hakuna wasiwasi tutatembelea hilo eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutajipanga baada ya Bunge hili.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwenye majibu yake ya msingi amesema zimetumwa shilingi milioni 358; je, zimetumwa lini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili uendelezaji unaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, shilingi milioni 358 zilitumwa miezi miwili iliyopita na tulipata fedha kutoka Serikali ya Japan bilioni 29.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba uendelezwaji unaanza lini. Katika hizo fedha sasa hivi kinachofanyika ni kuandaa mikataba, ni maeneo mengi ambayo yalikuwa bado mikataba haijaandaliwa. Ni kuandaa mikataba kwa sababu usanifu ulishafanyika ili kuweza kuingia sasa mikataba na wakandarasi na kazi hiyo iendelee kutekelezwa.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mkoa wa Tabora hususani Tabora Mjini tuna mabwawa makubwa mawili, Bwawa la Igombe na Bwawa la Kazima, pia tuna mradi wa bwawa ambalo lipo Kata ya Ndevelwa ambalo limeigharimu Serikali zaidi ya shilingi bilioni moja ambalo mpaka sasa hivi halifanyi kazi kwa sababu linavuja.
Mheshimiwa Spika, sijui Serikali ina mkakati gani wa kufanya mradi huu ambao kwanza umekwama, lakini pamoja na haya mabwawa mengine yaweze kutumika katika kilimo cha umwagiliaji ili wananchi kwa ujumla waweze kupata ajira pamoja na kuweza kupata mazao kwa ajili ya kujikimu kutokana na hali mbaya ya chakula ambayo inaikabili nchi yetu kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, mabwawa mawili ya Igombe na Kazima yanatumika kwa ajili ya maji ya matumizi ya binadamu na Bwawa la Igombe limeshaboreshwa tayari lina maji ya kutosha, sasa kuangalia uwezekano kwamba yanaweza yakatumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji basi tunalichukua tuweze kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu bwawa hili ambalo limebomoka, hili kwa sasa tayari tumejikita kuhakiksha kwamba mabwawa yote ya zamani yanaboreshwa ili yaweze kufanya kazi zilizotarajiwa.
MHE. ZAINAB M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Pwani hususani Wilaya ya Rufiji naomba nirudi kwenye swali la msingi.
Sote tunafahamu Rufiji ina mto na ina bonde zuri sana la kilimo; tuna Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Rufiji kwa maana ya RUBADA. Je, Serikali itaweza kutuambia nini kazi za hiyo mamlaka? Kwa sababu bonde liko pale, maji yapo pale hakuna kinachoendelea katika uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali.
Je, kuna sababu ya hii mamlaka kuendelea kuwepo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kwamba ipo haja ya mamlaka hiyo kuwepo. Kilimo cha umwagiliaji katika nchi hii kimeanza mwaka 1940 na kilianzia Rufiji, wakati huo ilikuwa hekta 160 ndio zilianza kutumika kule Rufiji. Baada ya hapo muda uliofuata tuliahamia Mbarali, hiyo ilikuwa ni mwaka 1960. Kutokana na mamlaka hiyo kuwepo uboreshaji kuhusu kilimo cha umwagiliaji umeendelea kutokana na hiyo mamlaka, hatimaye mpaka tumekuja kuwa na Tume ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeipitisha mwaka 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutokana na data ambazo zilikuwa zinaandaliwa na hiyo mamlaka ndiyo imetufikisha hapa tulipo sasa hivi. Tayari Serikali imeshaainisha maeneo mengi kama nilivyojibu katika swali la msingi kuhakikisha kwamba sasa bonde hili la Mto Rufiji ambalo linatokana na Mto Ruaha na mito mingine ya Kilombero na kutokana na mamlaka hii imeainisha hayo maeneo na sasa hivi maeneo mengi yamesanifiwa sasa hivi tunachosubiri ni fedha kuanza utekelezaji. Kwa hiyo, mamlaka hii uwepo wake ni wa muhimu, data zote kuhusu kilimo cha umwagiliaji zina hii mamlaka.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa TANESCO wameondoa service charge na hawa ndiyo wanatusaidia kusukuma maji katika vyanzo vyetu lakini wenzetu wa Wizara ya Maji kwenye bili zetu za maji bado kuna service charge. Je, ni lini hii service charge itaondolewa kwa wananchi wetu kwa sababu kwa kweli ni gharama kubwa pamoja na bili hizi ambazo zimepanda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Gekul kuhusu ni lini tutaondoa service charge kwenye bili za maji. Mpango huo tumeuanza na kwa sasa Mkoa wa Iringa meter reading haisomwi tena na watendaji, meter reading hakuna kwa sababu tumeweka mita za LUKU. Ukitaka maji unakwenda kulipia kwa kutumia mfumo uliopo, unapata maji kama jinsi ambavyo unanunua umeme. Kwa kufanya hivyo, sasa hivi Mkoa wa Iringa bado muda kidogo hakutakuwa na service charge. Kwa hiyo, tukifanya hivyo nchi nzima service charges zitaondolewa.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali langu.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Bwawa la Gidahababieg siyo la umwagiliaji tu, maeneo yote yale hayana maji ya uhakika kwa hivyo litakuwa ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo pamoja na umwagiliaji ikiwezekana. Baada ya bwawa lile kuvunjika kutokana na athari za mvua mwaka 2006, nilifikisha suala hilo kwenye Serikali mwaka 2007 na mpaka leo hakuna lililofanyika. Nataka kujua kama ni kweli mchakato utaanza na bwawa hili lirudi kwa sababu ndiyo linakusanya maji ya mlima Hanang yanayomwagika na kupotea bure?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Vijiji vya Hirbadaw, Dajameda, Mwanga, Gidika, Lalaji na Wandela vyote vilikuwa kwenye Mradi wa Benki ya Dunia na maji hayakuweza kupatikana. Naomba nijue ni lini vijiji hivyo vitaanza kutafutiwa vyanzo vingine ili watu wale waweze kupata maji kwani Bonde la Ufa halina maji? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niseme kwa bahati nzuri nimetembelea Wilaya ya Hanang na wakati nikiwa kule tulishirikiana na Mheshimiwa Mbunge tukazunguka maeneo yote ambayo yanahitaji huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza ameonesha kwamba Bwawa la Gidahababiegh sio kwa ajili ya umwagiliaji tu na kweli nilikwenda kwenye lile bwawa likishakamilika litatumika kwa umwagiliaji, mifugo na maji yale yakichakatwa yatatumika pia kwa matumizi ya majumbani. Sasa anauliza ni kweli bwawa hili litatengenezwa? Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumetenga fedha katika robo ya pili ya mwaka wa fedha huu tulionao. Fedha tunazo tayari na wakati wowote wataalam watatumwa kwenda kule kwa ajili ya kufanya survey. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kwenye hivi vijiji ambavyo havikupata vyanzo vya maji, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulitembea naye na kweli wakati tupo kwenye ziara tuliwaahidi wananchi kwamba haya maeneo ambayo hayakupata vyanzo vya maji kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 ambayo sasa hivi inaandaliwa tutahakikisha tunaweka fedha ili twende kukakamilisha miradi hiyo.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Swali la kwanza, kwa kuwa vyanzo vya maji ya Mto Ruaha Mkuu vinatoka nje ya Bonde la Usangu katika Milima ya Chunya, Mbeya, Mufindi, Mpanga na Kitulo, je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kushirikisha wananchi katika kutunza vyanzo vya maji visiendelee kuharibika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Bwawa la Lugola ili kunusuru uhai wa Hifadhi ya Ruaha na Bwawa la Mtera na Kidatu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Risala amesema Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inashirikisha wananchi kwenye utunzaji wa vyanzo vya maji. Katika muundo wa Wizara ya Maji tunayo Idara maalum ambayo inashughulikia utunzaji wa rasilimali za maji.
Mheshimiwa Spika, katika hali hiyo tunashirikisha maeneo ya vijiji, tunaunda kamati ndogo ndogo kwenye maeneo husika ili ziweze kulinda vyanzo vile ambavyo vina manufaa na wao wenyewe. Kwa hiyo, tunafanya ushiriki kupitia kwenye Wilaya, Halmashauri, Mikoa pamoja na vijiji ili kushirikisha hao wananchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu sasa ni lini tutajenga hili Bwawa la Lugoda, sasa hivi tumeshakamilisha usanifu. Sasa hivi Serikali inafanya juhudi ya kuwasiliana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kupata fedha ili tuweze kujenga hili Bwawa la Ndembera ambalo litatunza maji na kipindi cha kiangazi maji yatafunguliwa kuhakikisha kwamba Ruaha Mkuu inatiririsha maji wakati wote.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa mradi wa maji wa Ikorongo umeshindwa kutosheleza mahitaji ya wananchi wa Wilaya ya Mpanda; Kuna vijiji 20 vilivyoko Wilaya ya Nsimbo havina maji; kuna vijiji 13 na vitongoji viwili vilivyoko pale Mpanda Mjini havina maji; kuna vijiji tisa vilivyoko Wilaya ya Tanganyika, havina maji. Je, Serikali ni lini itachimba visima kwenye vijiji hivi na Kata hizi ili imtue ndoo mwanamke wa Mkoa wa Katavi?
Swali la pili; Mradi wa kuvuta maji kutoka Ziwa Tanganyika ni programu ya muda mrefu ambayo haiwezi ikatekelezwa leo au kesho na wananchi na akinamama wa Mkoa wa Katavi wanaendelea kuteseka: Je, Waziri anaweza akatueleza hiyo programu ya kuvuta maji kutoka Ziwa Tanganyika itaanza lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kwamba mradi wa Ikorongo haujitoshelezi, ni kweli. Mradi wa Ikorongo unatoa lita milioni 3.5 kwa siku wakati mahitaji ya Mji wa Mpanda pekee ni lita milioni 11 kwa siku. Kwa hiyo, kuna upungufu mkubwa. Wakati tunasubiri huu mpango wa muda mrefu, tumeendelea na uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali ya vijiji ambavyo amevitaja. Kwa mfano, tayari tumeshachimba visima katika Halmashauri ya Nsimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaendelea kuchimba visima katika Halmashauri ya Mpimbwe na tayari tumechimba visima katika Halmashauri ya Mlele na Halmashauri ya Tanganyika, sasa hivi tunaendelea kufanya mazungumzo nao ili tuweze kupeleka fedha kwa ajili ya kuchimba visima ikiwa ni hatua ya muda mfupi.
Swali la pili; Mpango huu wa muda mrefu unaanza lini? Mpango huu unaanza katika mwaka wa fedha 2017/2018. Tumeshapokea maandiko tayari, kwa hiyo, katika bajeti inayokuja, tuombe tu Mheshimiwa Mbunge na wewe upitishe hiyo bajeti ili tuweze kuweka Mhandisi mshauri aweze kusanifu ili kuandaa Makabrasha ya Zabuni ya kutoa maji kutoka Karema katika Ziwa Tanganyika kuleta Mji wa Mpanda na kutoa maji upande wa Sumbawanga kuleta Mji wa Sumbawanga kutoka kule Kasanga.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Moja, kwa vile Waziri amekiri kwamba maji yanapatikana kwa mgao: Je, Waziri atakuwa tayari kuiagiza DAWASCO ili iiondoe hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo katika utaratibu wa mgao ili kuweza kuboresha huduma ya afya katika hospitali hii ya Wilaya?
Swali la pili; je, mradi huo wa usambazaji mabomba utajumuisha kata zote tisa za Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bagamoyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Shukuru Kawambwa nikuhakikishie, baada ya mradi huu kukamilika mwezi Juni, 2017 Hospitali ya Bagamoyo haitakuwa na matatizo ya maji tena. Katika Mkataba unaoendelea, suala hili limeainishwa kuhakikisha kwamba Hospitali ya Bagamoyo isiwe na matatizo ya maji tena.
Swali la pili; mpango huu ukikamilika Mheshimiwa Kawambwa ni kwamba Kata zote tisa za Jimbo lako Bagamoyo zitapata huduma ya maji kutokana na mradi huu.
MHE. CHARLES M. KITWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niulize swali la nyongeza.
Natambua kwamba chanzo cha maji Ihelele ndicho kinachopeleka maji katika Mji wa Shinyanga na Kahama; lakini tangu tumepewa ahadi ya kuwekewa maji katika vijiji hivyo mwaka 2008 maji hayatoki mpaka leo. Sasa Serikali ina mpango gani, maana wananchi wanasema kama hakuna mpango mkakati, tutaungana na mimi nitaungana nao kwenda kuzima mtambo wa maji wa kwenda Shinyanga. Nitawasindikiza wananchi kwenda kuzima.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais mwaka 2008 alitoa ahadi ambayo itahakikisha eneo lote la Ihelele linapata maji ya kutoka KASHWASA. Baada ya ahadi hiyo; na kwa kwa mujibu wa taratibu za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, tulianza kufanya utafiti na utafiti huo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba umekamilika. Ili kuweza kusambaza maji katika eneo lako la Ihelele tunahitaji shilingi bilioni nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika hii bajeti sasa ambayo tunaiandaa sasa hivi ya mwaka 2017/2018, basi tutaanza kutenga fedha ili kutekeleza sasa mradi wa kuwapatia wananchi maji Ihelele kutoka kwenye huo mradi wa KASHWASA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kwa ahadi hii yeye na wananchi wake hamna haja ya kufunga yale maji kwa sababu tunawaletea maji.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na
majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naipongeza Serikali kwa jinsi
ambavyo wameushughulikia mradi huu wa masoko na miradi mingine iliyo ndani
ya Wilaya ya Rungwe. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza; kwa kuwa,
mradi huu wa maji umechukua muda mrefu na Mkandarasi aliyekuwa amepewa kazi hiyo Osaka, baada ya kutangazwa tenda ya mara ya pili anaondolewa.
Tungependa kufahamu ni sababu gani zimesababisha Mkandarasi huyu wa
mara ya kwanza ashindwane na Halmashauri?
Swali la pili; kwa kuwa, miradi hii ya maji ni ya thamani kubwa, zaidi ya
bilioni tano tungependa tumwombe Mheshimiwa Naibu Waziri aweze
kuitembelea hii miradi pamoja na ya Mwakaleli One pamoja na Kapondelo
ikiwemo na hii ya Masoko. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,
ameuliza sababu zilizofanya Mkandarasi asimamishwe kuendelea na kazi,
sababu ziko kimkataba. Kwa hiyo, sababu za kimkataba hatuwezi kuzijadili sisi
Waheshimiwa Wabunge, lakini la kuelewa tu ni kwamba, alishindwa ku-perform
vile ilivyokuwa imetakiwa kimkataba ndiyo maana Halmashauri kwa kutumia
vifungu vya mkataba ikamsimamisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Rungwe. Kwa mara ya kwanza ameleta bajeti ya miaka mitano na nimefurahi
sana. Ameweka mpango wa miaka mitano na bajeti inayotakiwa akaweka na
kifungu cha matengenezo ya miradi atakayokuwa ameitekeleza ili kuhakikisha
kwamba miradi tunayojenga basi inakuwa ni ya kudumu na mabomba
yanaendelea kutoa maji mwaka mzima.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa
kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu
Waziri, nauliza swali ambalo kama ilivyo Rungwe ule mradi wa Masoko, Tabora
Mjini ule mradi wa Ziwa Victoria, kuna vijiji ambavyo niliviorodhesha kwenye swali
Na. 57 lililojibiwa hapa Bungeni ambavyo ni Vijiji vya Itetemla, Uyui, Ntalikwa,
Kabila, Mtendeni, Itonjanda na baadhi ya maeneo ambayo ni ya Kata za Tumbi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji hivi na hizi Kata havijaorodheshwa kwenye
huu mradi wa Ziwa Victoria na vina shida sana ya maji. Sijui vitapitiwa lini na
mradi huu wa Ziwa Victoria? Naomba swali langu lipatiwe majibu. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,
kwanza kabisa Tabora Mjini kuna mradi mkubwa wa maji ambao umekamilika
kutoka bwawa la Igombe na kwamba maji yanayozalishwa ni lita milioni 30 kwa
siku wakati mahitaji ni lita milioni 24. Kwa hiyo, kwa maana ya Tabora Mjini tayari
imeshakamilisha huduma maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tupo na mradi ambao sasa hivi upo kwenye
zabuni ambao utatoa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Nzega, Tabora na Igunga. Kwa hiyo, nina hakika kabisa kwamba sasa Tabora itakuwa na maji
mengi na ndiyo maana tunataka hayo maji yakishafika tuyaelekeze yaende
mpaka eneo la Sikonge. Kwa hiyo, Vijiji vyote Mheshimiwa Mbunge ambavyo
havina maji nje ya Manispaa ya Tabora kupitia mradi huo tutakuwa na maji ya
uhakika kuhakikisha sasa kata na vijiji vyote vinapata maji ikiwemo na sehemu ya
eneo la Uyui.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Katika
Mkoa wa Katavi kumekuwa na changamoto kubwa ya miradi ya maji kuendelea
kusuasua kwisha. Je, ni lini sasa Serikali itasema mikakati ya kujenga hii miradi ili
iishe kwa wakati, kwa sababu pesa nyingi zimekuwa zikitumika mfano, kwenye
Kata ya Ugala ambako kuna mradi mpaka sasa ni miezi sita, mradi umesimama.
Sasa, ni lini Serikali itamaliza kujenga hii miundombinu ya umwagiliaji.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,
kwanza kabisa Mkoa wa Katavi, eneo la Mpanda linahitaji lita milioni 11 kwa siku,
lakini sasa hivi maji yanayozalishwa ni lita milioni 3.5. Tayari tumeshakamilisha
mradi wa Ikolongo na wananchi wanaendelea kupata huduma; lakini tuna
miradi miwili ambayo tunasaini mwezi huu kwa ajili ya kuleta maji Mji wa
Mpanda. Kwa upande wa eneo la Ugala kwanza lina bwawa moja kubwa
ambalo linaweza kuhudumia ule Mji wa Ugala. Sasa hivi kupitia kwenye
Halmashauri tunayo miradi ambayo inaendelea kuhakikisha kwamba wananchi
wa Ugala wanapata huduma ya maji.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na
majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji nina maswali
mawili ya nyongeza. Naibu Waziri amekiri miradi hii imechukua muda mrefu
kutoka 2012 mpaka leo hii haijakamilika; Je, Wizara haioni sasa ni muda muafaka
wanapokuwa wamepelekewa certificate waweze kulipa malipo haya kwa
muda muafaka kwa sababu wanawachelewesha wakandarasi. (Makofi)
Swali la pili; miradi hii imechukua muda mrefu sana mpaka muda huu
imefikia asilimia 70 ya utekelezaji. Mheshimiwa Naibu Waziri haoni ni muda
muafaka sasa wa kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali
la kwanza amesema Serikali ione haja ya kulipa haraka certificate, tunafanya
hivyo Mheshimiwa Mbunge kwamba certificate ikishawasilishwa kwenye Wizara
yetu na Halmashauri yoyote, kitu cha kwanza lazima tuihakiki, hatuwezi kulipa
moja kwa moja bila kuhakiki kwa sababu imetokea huko nyuma tulipotoka, mtu
analeta certificate unatoa hela, halafu hela inakwenda kukaa kwenye
Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati mwingine ucheleweshaji wa
kulipwa unatokana na ule uhakiki ili kujiridhisha kwamba kweli kazi imefanyika na
kwamba hela ile ikifika ni moja kwa moja inakwenda kwa mkandarasi mhusika ili
kazi iweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwamba Serikali sasa haioni kwamba
ni wakati muafaka wa kutafuta fedha. Kwa bahati nzuri Waheshimiwa Wabunge
katika bajeti iliyopita ambayo sasa hivi tunaitekeleza mlipitisha ninyi wenyewe
fedha za Mfuko wa Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri katika Bunge hili amesema
mpaka sasa tayari tumeshapokea zaidi ya bilioni 71 ambazo zimetokana na
Mfuko wa Maji na fedha hizi mpaka hapa ninapoongea Waheshimiwa Wabunge
kwamba tayari tuna fedha kwenye Wizara, kwa hiyo, wakati wowote certificate
ikifika tunailipa. Kwa hiyo, Serikali tayari inakusanya fedha kuhakikisha kwamba
miradi mingi ambayo ilikuwa imekwama inaendelea na utekelezaji wake ili iweze
kukamilika.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa
kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Miundombinu ya mradi
wa umwagiliaji wa Bwawa la Dachi lililopo katika Kata ya Malolo liligharimu
takribani sh. 600,000,000 ambazo zilifadhiliwa na Shirika la JICA la Japan lakini
miundombinu hiyo imeharibika vibaya na imejengwa chini ya kiwango.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwashughulikia wale wote waliofanya
ubadhilifu huu na inachukua hatua gani ya kuokoa mradi huu ambao sasa Mto
Mwega umejaa mchanga na kuharibika na wananchi wakiwa wanategemea
sana bwawa hili kwa ajili ya umwagiliaji pale Malolo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,
kwanza nashukuru kwa kunipa taarifa kwamba kuna mradi wa umwagiliaji
umejengwa eneo la Malolo na kwamba mradi huo pengine umepata shida
kutokana na mafuriko au pengine kutokana na usanifu haukuwa sawasawa au
ujenzi haukufanyika vile inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kitu tutakachofanya tutakwenda
kuchunguza kuona ni nini kilichopo na tukishachunguza kitu cha kwanza ni
kuhakikisha tunaboresha mradi huo ili uendelee kufanya kazi iliyotarajiwa. Baada
ya kufanya uchunguzi kama kuna tatizo lolote ambalo tutaliona kwamba lipo,
basi litashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa, Halmashauri tayari ilishatoa certificate Wizarani: Ni lini sasa fedha hizo zitaenda ili kusudi wananchi wa Nkoma na Mwalushu, takriban 14,000 waweze kupata huduma iliyo sawa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Itilima inayo mabwawa 17; mabwawa haya yana upungufu wa miundombinu: Serikali iko tayari sasa kukutana na Wataalam wa Halmashauri yangu ya Itilima ili watakapoleta maombi waweze kuyashughulikia hayo mabwawa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tumeshaweka utaratibu kwamba tutatoa fedha kwa kuwasilisha certificate. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara tu certificate itakapofika, fedha tunazo na kutokana na Mfuko wa Maji, Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekuwa anatupatia fedha kila wakati. Kwa hiyo, fedha ipo, ila wakati mwingine tunachelewa kwa sababu ya uhakiki; lazima tuhakikishe kwamba certificate hiyo ni ya kweli na kwamba ikienda iende ikalipe malipo ambayo ni ya halali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la mabwawa 17; sasa hivi tayari bwawa moja tumemaliza ukarabati Bwawa la Habia, ambalo ni fedha zilizotolewa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Wizara imeshaagiza kwamba ikiwezekana kila mwaka kila Halmashauri itenge fedha na kujenga bwawa moja. Pia tuko tayari kukaa pamoja na Halmashauri ya Itilima ili kuangalia ni jinsi gani tunaweza tukashirikiana katika utekelezaji wa hayo mabwawa 17.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali langu dogo la nyongeza.
Kwa kuwa, katika Wilaya ya Kilolo kilimo cha mvua ni kilimo ambacho hakitegemewi; sasa hivi kilimo cha uhakika ni umwagiliaji; na kwa kuwa, katika Wilaya ya Kilolo kuna maeneo ambayo tayari mabwawa yalishachimbwa kwa muda mrefu, lakini yanashindwa kusaidia wananchi kwa sababu ya ongezeko la watu; sehemu za Nyanzwa, Ruaha Mbuyuni na Mahenge. Je, Mheshimiwa Waziri kwa kuwa, ni ahadi ya muda mrefu ya kuboresha mabwawa hayo, atakuwa tayari kufika na kuona ili katika bajeti hii aweze kutenga fedha ili kuboresha mabwawa hayo ili yaweze kulisha wananchi wengi wa Tanzania tuondokane na njaa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme niko tayari kwenda kuangalia hayo mabwawa. Katika orodha tuliyonayo kwa sasa ya mabwawa, tumeainisha pamoja na bwawa hili kulifanyia usanifu upya ili kuyakarabati yaweze kutoa huduma iliyokuwa inatarajiwa.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo kubwa la miradi hii ya umwagiliaji ni ule upembuzi yakinifu sijui na usanifu. Kwa sababu, katika Jimbo langu la Liwale kuna Mradi wa Umwagiliaji wa Ngongowele umetumia zaidi ya shilingi bilioni nne na mradi ule sasa hivi uko grounded, hautegemei tena kufufuka. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya pesa zile zilizopotea pale na hatima ya mradi ule?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa Mradi wa Ngongowele ni kweli Mheshimiwa Mbunge tumeshaongea naye. Mradi huu umeshakamilika na tulikuwa tunatarajia kwamba sasa wananchi wagawane na kuanza kuutumia.
Mheshimiwa Spika, kama alivyoongea Mheshimiwa Waziri muda mfupi uliopita, miradi mingi hii ya umwagiliaji ilisanifiwa. Nimejaribu kuzungukia miradi ya umwagiliaji, unakuta mradi umekamilika, lakini umekumbwa na tatizo la chanzo cha maji; kimekauka. Sasa hivi tulikuwa tunafikiria kurudia usanifu kuhakikisha miradi yote ambayo imekamilika, basi tunajengea mabwawa ili muda wote iwe inafanya kazi.
Mheshimiwa Spika, miradi mingine imekamilika, lakini unakuta inafanya kazi kipindi cha mvua tu. Baada ya mvua kunakuwa hakuna maji, miradi haifanyi kazi, jambo ambalo siyo lengo. Ni miradi michache tu kama miwili katika mzunguko niliozunguka ndiyo nimekuta kwamba ina vyanzo vya maji vya kudumu ambavyo vinafanya kazi muda wote, watu wanalima mara mbili mpaka mara tatu. Kwa hiyo, alichokizungumza Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwamba, huu mradi ulikamilika na umetumia fedha nyingi, lakini una shida kwamba haufanyi shughuli iliyokuwa inatarajiwa.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ambayo yamejielekeza kwenye sehemu ndogo tu ya swali langu la msingi; kwa sababu ameelezea juu ya mpango wa maji kwenye miji sita ya Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kwamba Wilaya yangu ya Ngara, takriban asilimia 50 ya maeneo ya vijijini kuna tatizo kubwa hili la maji; na bahati nzuri tarehe 30 mwezi Desemba mwaka jana, 2016, Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo alifika akaona mito hiyo na mlima huo ninaousema; na kwa kutumia vyanzo hivi maana yake ni kwamba tutaondoa kabisa kero ya maji katika vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara na hizi nyingine ambazo nimezitaja; na huu ndiyo utakuwa ni mwarobaini:-
Sasa swali langu namba moja: Je, Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI wako tayari kutuma wataalam ili waweze kufika maeneo yale na kuweza kuweka mkakati wa kuandaa mradi mkubwa ambao unaweza ukaondoa kero hii ya maji kwenye Vijiji vya Wilaya ya Ngara, Karagwe, Kyerwa, Biharamulo na Chato kama ilivyoelezwa kwenye swali la msingi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; mwaka 2016 mwezi wa Pili Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ngara ilipeleka barua kwenye Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa ajili ya kuomba mitambo miwili ya kusukuma maji kwenye eneo la K9 ambapo kuna taasisi za Serikali na wananchi kwa maana Kambi ya Jeshi, Shule mbili za Sekondari na wananchi wa Kijiji cha Kasharazi; na pampu ya pili kwenye eneo la Mamlaka ya Mji wa Ngara Mjini, ambayo pamoja mamlaka kushugulikia usambazaji wa maji mjini, bado kulingana na umuhimu wa taasisi zilizopo pembezoni kama Shule ya Sekondari Ishunga walikuwa wakipeleka maji kule, lakini baada ya mtambo kuharibika uliokuwa unasukuma maji, imekuwa ni tatizo.
Je, Wizara kwa sababu tayari ilishaji-commit tangu tarehe 25 mwezi wa Pili kwamba itapeleka pampu hizi mbili mwaka jana…
SPIKA: Mheshimiwa Gashaza, sasa si uulize swali!
Mheshimiwa Spika, swali langu je, ni lini sasa Wizara itapeleka fedha hizi ambazo ni takriban shilingi milioni 50 kwa ajili ya kununua pampu hizi za kusukuma maji katika maeneo haya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Gashaza amezungumzia matatizo ya maji ya Ngara na Wilaya zote Mkoa wa Kagera akihusisha pia na vijiji vya wilaya hizo; na ameomba kwamba tupeleke wataalam.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa yupo mtaalam mshauri ambaye anaangalia uwezekano wa kutumia mito hiyo miwili ambayo ni mikubwa ili kuweza kupeleka maji kwa wananchi. Miradi hii ambayo itatekelezwa chini ya Wizara ya Maji, itahakikisha inapeleka maji kwenye miji mikuu ya hizo Wilaya na vijiji vinavyopitiwa na bomba kuu kuelekea kwenye hizo Wilaya.
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Vijijini, katika bajeti ya mwaka huu tumehakikisha kwamba kila Wilaya imepewa bajeti ili waweze kushughulikia kupeleka maji kwenye Kata na Vijiji vinavyozunguka hizo Halmashauri. Mheshimiwa Waziri ametoka kuzungumza sasa hivi kwamba tayari baada ya kuona kwamba utekelezaji unasuasua tuliamua kuandika mwongozo kupeleka kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maji kupitia bajeti ambayo imetengwa na Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Spika, pia nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba tupo tayari na tumekuwa tunafanya hivyo. Kama Halmashauri zinahitaji wataalam, basi tunaweza tukashirikiana kutoa wataalam ili kwenda kuangalia hilo tatizo kwa pamoja tuone jinsi ya kulishughulikia.
Mheshimiwa Spika, nikiri katika swali lake la pili, ni kweli na mimi mwenyewe waliniambia na aliniletea nakala ya barua kuhusiana na maombi ya pampu kwa ajili ya kufufua zile pampu ambazo zimeharibika.
Mheshimiwa Spika, nizungumze suala moja. Waheshimiwa Wabunge, ikishakuwa Mamlaka, maana yake, inajitegemea kwenye running. Serikali inasaidia katika uwekezaji. Sasa inawezekana barua hizo baada ya kwenda kule kwenye Wizara zilikutana na tatizo hilo. Mara nyingi kwenye uwekezaji ndiyo tunasaidia mamlaka, lakini kwenye yale matumizi ya kila siku huwa tuaachia wao wenyewe wafanye kazi hiyo kwa kutumia mapato yao. Inategemea sasa, Mamlaka kama ipo chini ya Wilaya, kama kuna matatizo inabidi waripoti kwenye Wilaya. Mamlaka zilizopo chini ya Mikoa, kama kuna tatizo, wanaripoti kwenye Mikoa.
Mheshimiwa Spika, namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hili suala kwa sababu nalifahamu, nitajaribu kuwasiliana na Wizara kuona limefikia wapi.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa wokovu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati maeneo mengi tatizo ni miundombinu na vyanzo vya maji, Mbeya hatuna tatizo la kati ya hayo kwa maana ya vyanzo vya maji, hatuna au hatutakiwi kuwa na tatizo la vyanzo vya maji; lakini pia miundombinu Mbeya ilishakamilika mwaka 2013 ikazinduliwa na Rais Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete mradi ambao ulifadhiliwa kwa mabilioni na EU. Leo hii pamoja na yote hayo, tuna wiki ya nne, takriban mwezi mzima Mbeya maji hayatoki kuanzia Uyole kwenda Mwakibete, Mama John na Sai, maji hayatoki kote.
Mheshimiwa Spika, naomba Waziri wa Maji asimame hapa awaambie wana Mbeya anatusaidiaje kutuokoa kwa sababu tupo kwenye hatari ya kukutana hata na magonjwa ya milipuko ukizingatia hiki ni kifuku, mvua zinanyesha, halafu maji ya kufanya usafi hamna. Kwa kweli Mbeya ni disaster na inahitaji neno la haraka sana kutoka kwa Waziri Mheshimiwa Engineer Lwenge.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la Mheshimiwa Sugu kuhusiana na matatizo ya maji katika Mji wa Mbeya; wiki iliyopita ilinyesha mvua kubwa sana Mbeya ya muda mfupi lakini ilikuwa mvua kubwa. Maji yalitiririka yakaenda mpaka kwenye chanzo cha Nzogwe sehemu ambayo ina pampu zinazosukuma maji katika Mji wa Mbeya.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hilo, kwa sababu zile pampu zinatumia umeme na kwa teknolojia, kukiwa na maji huwezi kuwasha umeme, kwa hiyo Mji wa Mbeya umekosa maji kwa muda wa siku nne. Taarifa hii kabla Mheshimiwa Sugu hajasema, nilikuwa nimetaarifiwa tayari na Mheshimiwa Mwanjelwa kwamba Mji wa Mbeya una matatizo.
Mheshimiwa Spika, jana tatizo hilo lilikamilika, baadhi ya mashine zikawashwa; na leo asubuhi mashine zilizobaki tayari zimeshawashwa. Kwa hiyo, nakuomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tukitoka Bungeni saa 7.00 naomba upige simu tena utakuta hali ya maji tayari imeshakaa vizuri.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la maji Ngara linafanana kabisa na tatizo la maji katika Mkoa wa Morogoro, licha ya Mkoa Morogoro kuwa na mito mingi, lakini wananchi wa Morogoro hawapati maji safi na salama. Je, Serikali haioni kama kuna haja sasa ya kujenga bwawa lingine liweze kusaidiana na Bwawa la Mindu ili kutosheleza maji kwa wakazi wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la Mheshimiwa Devotha Minja kuhusiana na kuongeza kiwango cha maji katika Bwawa la Mindu; kwa bahati nzuri pia nimeuzunguka Mkoa wote wa Morogoro, nimeenda Bwawa la Mindu.
Mheshimiwa Spika, nimpe taarifa Mheshimiwa Minja kwamba tayari Benki ya Ufaransa imetupa Euro milioni 70 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 170 kwa ajili ya kuongeza kiwango cha Bwawa la Mindu ili Bwawa la Mindu liweze kuwa na maji mengi. Wakati nafanya ziara kule, nilikuta uzalishaji wa maji ni lita milioni 25 badala ya lita milioni 45 zinazohitajika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa hivi makabrasha ya zabuni yamekamilika, tumeshasaini mkataba wa mhandisi mshauri ambaye atapitia nyaraka zilizopo kwa muda wa miezi sita na baada ya hapo tunatangaza tenda ya kuanza ujenzi ili tuweze kuongeza kiwango cha maji katika Mji wa Morogoro. Kwa hiyo, suala hilo la Mheshimiwa Minja tunalifanyia kazi, lakini naomba Mheshimiwa Mbunge anisaidie. Wakati nafanya ziara pale tumekuta lile bwawa linachafuliwa sana.
Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa tunaimba kila siku kuhusu uchafuzi wa mazingira, naomba tusaidiane. Watu tayari wanafanya kilimo cha umwagiliaji juu ya mito ambayo inaingiza maji katika Bwawa la Mindu. Tusaidiane, tuwatengenezee utaratibu mwingine ili tuwe na uhakika wa maji katika Bwawa la Mindu.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya hatua husika za mradi huu, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri ametueleza kuhusu awamu ya kwanza inayotarajiwa kukamilika Disemba, 2019. Je, huo ndiyo wakati ambapo mabomba ya Same yatafungua maji hayo na kuona maji yakitiririka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Same haiko vizuri kifedha kuwasaidia watu wa Same ambao mpaka sasa hawana maji safi na salama zikiwepo Kata za Njoro, Same Mjini, Makanya na Hedaru. Je, Serikali iko tayari sasa kuwapatia fedha za kuchimba visima virefu ili watu hao wapate maji safi na salama wakati wakisubiri kukamilika kwa mradi huo mwaka 2019?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu la msingi limezungumzia mradi wa Same-Mwanga-Korogwe kwamba ifikapo mwaka 2019 utakuwa umekamilika kwa maana kwamba maji tayari yatakuwa yamefika Mwanga na yatakuwa yamefika Same, yatafunguliwa wananchi wanaanza kupata maji na miradi hiyo inaendelea vizuri na fedha zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili kuhusu Same, katika bajeti hii tuliyonayo kwa sasa na ninyi Waheshimiwa Wabunge mliipitisha, tulihakikisha kila Halmashauri tumeipatia fedha ili Waheshimiwa Wabunge na Madiwani katika Halmashauri zao wapange miradi kutokana na hiyo fedha ambayo tumeituma kwenye Halmashauri. Kwa bahati nzuri Halmashauri ya Same ilipewa Sh. 663,847,000 kwa ajili ya miradi ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni matarajio yangu kwamba Halmashauri hizi sasa zinao uwezo, zitekeleze miradi kutokana na fedha hii kwa kuchimba visima au maji ya mtiririko kutokana na hali ya mazingira ya Halmashauri husika ili kuhakikisha wananchi wanapata maji. Mwaka huu wa fedha unaokuja tutaendelea kutenga fedha kwenye Halmashauri ili wao wenyewe waweze kutekeleza miradi ya kuwapelekea maji wananchi wao.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Kaliua na Jimbo la Kaliua wana adha kubwa ya maji na ardhi ya Tabora nzima ikiwepo na Kaliua visima vikichimbwa vinatoa maji kidogo sana. Namna pekee ya kusaidia wananchi wa Kaliua na Wilaya nyingine ni kuweza kupata maji kutoka mto mkubwa wa Malagarasi. Je, ni lini mradi mkubwa wa kutoa maji Malagarasi kwenda Kaliua mpaka Urambo utaanza na utakamilika lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imekamilisha mradi wa upembuzi yakinifu wa kutoa maji kutoka Mto Malagarasi kupeleka Kaliua na Urambo. Sasa hivi mkandarasi anaendelea na usanifu wa kina wa mradi huo. Baada ya kukamilisha usanifu wa kina Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya mradi huo kukamilika sasa tutakuwa na chanzo cha uhakika kutoka Malagarasi kuleta maji Kaliua, Urambo na hatimaye kupeleka Tabora. Ni kweli kabisa ulichosema chini ya ardhi katika Mkoa wa Tabora maji ni kidogo sana.
MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Waziri wa Maji, tulifanya ziara ya kukagua vyanzo vya maji katika eneo la Manispaa ya Lindi na kuna mradi mkubwa wa maji wa Ng‟apa, Lindi. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuniambia mradi ule utakamilika lini na wananchi wa Lindi wakaweza kupata maji ya kunywa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na nyaraka za kimkataba na utekelezaji unaoendelea, tunategemea mwezi Aprili mwaka huu wa 2017, mradi huo utaanza kutoa maji kwa ajili ya wananchi wa Lindi.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Pamoja na kuwepo kwa changamoto kubwa ya uhaba wa maji katika Mji wa Singida, lakini pia kuna changamoto kubwa ya miundombinu mibovu kwa maana miundombinu yake ni ya muda mrefu sana. Ni lini sasa Serikali itatatua changamoto hii kwa sababu ni ya muda mrefu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunatakiwa kutenga fedha za maintenance. Mnapoleta bajeti Waheshimiwa Wabunge kupitia kwenye Halmashauri zenu kama ambavyo wamefanya watu wa Rungwe, tunatakiwa pia kutenga bajeti kwa ajili ya matengenezo ili hii miundombinu ifike mahali kwamba isichakae kabla hatujafanya ukarabati. Pia sasa hivi kama miundombinu imeshachakaa, basi tunaomba muainishe kwenye Halmashauri mtuletee ili tutenge fedha kwa ajili ya ukarabati.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wengi wa Wilaya ya Singida Vijijini wanataabika sana kutokana na shida kubwa ya maji na matumaini yao waliweka katika ukarabati wa miundombinu ya maji ya visima inayogharamiwa na chanzo cha fedha cha LCDG ambapo fedha hizo hazijaletwa hata senti moja kwa muda wa miaka mitatu mfululizo sasa, miradi hiyo inahusisha Vijiji vya Mughamo, Sagara, Kinyeto, Mkimbii, Kihunadi, Mwanyonye…

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Kijota na Semfunga: Swali; je, Serikali itapeleka lini fedha hizo ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 300 ili kuvikarabati visima hivyo na kuondolea kero wananchi wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Mji wa Itigi ni miongoni mwa miji midogo inayokua kwa kasi sana na ni Makao Makuu ya Jimbo la Manyoni Magharibi, lakini mji huu hauna kabisa mtandao wa maji: Je, sasa Serikali ipo tayari kutenga fedha za kutosha kwa mwaka ujao wa fedha, 2017/2018 ili kuwawezesha wananchi wengi kupata maji safi na salama? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto kubwa ya maji katika Wilaya ya Manyoni, ni ombi…

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Matembe, hoja yake anayoizungumza katika Bunge siyo hapa tu; ananifuata ofisini, tukikutana huko mtaani, anazungumzia kuhusu maji Singida. Tumeshaongea kuhusu mikakati yote itakayohakikisha kwamba Mkoa wa Singida sasa matatizo ya maji tunayakamilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza awali, ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji tuliamua kuhakikisha kila Wilaya tunaipatia fedha ili pamoja na miradi mikubwa ambayo inatekelezwa moja kwa moja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Halmashauri pia ziweze kutekeleza miradi kwa kujipangia wao wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu Itigi; napo tumefanya utaratibu huo huo, lakini pamoja na hilo, Itigi tumekamilisha ujenzi wa Bwawa la Itagata ambalo litahudumia kilimo, lakini pia Halmashauri inaweza ikaona uwezekano kama maji yanatosha, basi yaweze kusambazwa kupelekwa na kwa matumizi ya majumbani.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu WazirI ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kutangaza na kutafuta mkandarasi sasa hivi imeanza muda mrefu toka mwezi wa pili na imechukua karibu miezi sita sasa, ukisema mpaka Juni itachukua miezi sita. Swali langu, je, kutafuta
mkandarasi kisheria inatakiwa miezi mingapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Jimbo langu la Mufindi Kusini tuna tatizo kubwa sana la maji, ukizingatia Serikali ilijenga matenki ya maji katika kijiji cha Igowole, Nyororo, Idunda, Itandula, Kiyowela matenki haya yote yameharibika sasa hivi yana miaka karibu sita, je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha watu wa Igowole na Nyororo na
vijiji nilivyotaja vinaweza kupata maji na kukarabati mitandao ambayo imeharibika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja anasema muda au mchakato wa kumpata Mkandarasi unakuwa mrefu sana unatumia muda gani; upo kwa mujibu wa sheria. Muda wa manunuzi upo kwa mujibu wa sheria ambayo ilipitishwa katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kuna matenki 11 yaliyojengwa na sasa hayana maji, ni kweli tatizo hili nilikuta pia Nanyamba, kuna matenki zaidi ya saba ambayo yalijengwa na AMREF na yalikuwa hayana maji. Matenki yale
yalikuwa yamejengwa pamoja na visima. Sasa jumuiya za watumiaji maji ambazo tuliziunda tumekuta changamoto ziko nyingi unakuta kulikuwa na pump, pump imekufa, kuna jenereta, jeneretaimekufa. Wakati mwingine kisima kinakuwa kimekosa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sasa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunachokifanya sasa hivi tumefanya uchunguzi tukakuta kwamba hzi jumuiya zinaelekea kushindwa kufanya hii kazi; lakini sio kwamba ni
kwa sababu yao tu, hapana; ila ni kwa sababu ya
miundombinu iliyowekwa hawana uwezo wa kuiendesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumechukua
utaratibu wa kuweka solar na visima vilivyopo tutavisafisha maeneo yaliyokuwa na mtiririko tutayaweka vizuri kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma na yele matanki yanafanya kazi iliyotarajiwa.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mosi, kuhusu Mradi wa Kitere pamoja kwamba majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanasema mradi umekamilika, lakini mradi huo umekamilika lakini haufanyi kazi kama unavyotakiwa na mwenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri shahidi amepita pale na hakuona hizi ekari 3,000 zimelimwa.
Kwa hiyo, naomba kauli ya Serikali kwamba, kuna mkakati gani wa kukamilisha mapungufu yaliyopo ili mradi huo sasa uweze kufanya kazi pasavyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kupitia Ofisi za Umwagiliaji Kanda, kuna miradi mingi hapa nchini ambayo haifanyi kazi. Juzi Kamati yetu ya LAAC ilikuwa Tabora, kuna mradi haufanyi kazi, kuna mradi Liwale, kuna mradi Mkuranga na miradi mingine. Sasa Serikali ina kauli gani kuhusu ushauri unaotolewa na ofisi hizi za umwagiliaji kanda ambazo miradi mingi ambayo inabuniwa na ofisi hizi huwa haifanyi kazi ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge Chikota, ambayo yote ni kama swali moja kwamba, miradi hii haifanyi kazi vizuri. Lakini pia ameonesha kuwa na utata kidogo katika ushauri wa taasisi yetu inayohusika na umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza
katika swali la msingi, Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba sasa hivi miradi yote hii ya umwagiliaji tunaifanyia mapitio. Na tulichokibaini ni kwamba tulijenga skimu za umwagiliaji, lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi zile skimu za umwagiliaji
zimekuwa ama zinafanya kazi mara moja kwa mwaka na wala sio mara mbili kutokana na ukosefu wa huduma ya maji kwa kuwa miradi hiyo hatukuijengea mabwawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutapitia katika mpango
huu kabambe wa mwaka 2002 tuhakikishe kwamba, miradi hii sasa inafanyiwa usanifu na kutekelezwa kuhakikisha kwamba, inafanya kazi ile iliyotarajiwa. Lakini mapungufu pia yaliyojitokeza katika miradi hiyo tutayapitia, ikiwa ni pamoja na kuimarisha tume yetu ambayo Waheshimiwa Wabunge ninyi wenyewe mmeunda Tume ya Umwagiliaji kwa ajili ya kusimamia moja kwa moja shughuli ya umwagiliaji.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Kwa kuwa tatizo la maji limekuwa ni kero ya nchi nzima, ni kwa nini sasa Serikali, hususan kupitia kwenye bajeti ya Bunge hili, isikubali kutengeneza Wakala wa Maji Vijijini ambaye atasaidia kupeleka maji vijijini kote kama ambavyo tumefanya katika REA ambapo kwenye suala la umeme wameweza kufanikiwa vizuri. Kwa nini wasifanye hivyo ili maji yafike hata kule Momba, Chitete, pamoja na vijiji vingine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako Tukufu katika bajeti iliyopita liliagiza Wizara ya Maji ianze taratibu za kuunda Wakala wa Maji nchini, tayari tumeshaanza kazi hiyo na wakati wowote itawasilishwa hapa kwa ajili ya kupewa mjadala na kupitishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo suala hilo tayari
linafanyiwa kazi.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na jitihada za Serikali za kukamilisha huu mradi wa World Bank, Mji wa Mikumi ni Mji wa kitalii na umekuwa ukipata wageni mbalimbali na idadi ya watu imeongezeka wamekaribia wakazi 30,000, lakini Mikumi kuna vyanzo vingi kama Iyovi, Madibila na pia Mto Muhanzi.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweza kutumia
vyanzo vingine ili viweze kusaidiana na mradi huu ili iweze kusaidia wananchi wa Jimbo la Mikumi na kadhia hii?
Swali la pili, katika ziara ya Naibu Waiziri ulipokuja uliagiza watalaam waje kuangalia chanzo cha maji cha Sigareti pale Kata ya Ruaha ambapo kingeweza kusaidia Kata ya Ruaha na Rwembe, wameshafanya hivyo na kukuletea taarifa na imeonekana takribani shilingi bilioni mbili zinahitajika ili kuwezesha wananchi wa Ruaha waweze kupata mradi huo.
Je, Mheshimiwa Waziri unaweza kuwaahidi vipi wananchi wa Ruaha ambao sasa wanakutazama kwamba je, huu mradi utaingizwa katika Bajeti ya 2017/2018 ili uweze kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Mikumi kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyotaja kwamba ni kweli nilishawahi kutembelea Jimbo la Mikumi kwenda kuangalia miundombinu ya maji. Ni kweli tulienda na yeye mpaka Kijiji cha Ruaha na tukaona chanzo cha Segereti na tukaagiza. Kwa sababu kwa sasa hivi tuna utaratibu Wizara kwamba tunaweka fedha kila Halmashauri, basi kwa kutumia nafasi hili niagize ule mradi ambao tuliagiza kamba waufanyie mchakato wa kufanyiwa usanifu ukikamilika basi watumie fedha tutakazozitenga katika Bajeti ya mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia chanzo cha Madibira tayari tumeshamuagiza Mkurugenzi wa Maji wa Mamlaka ya Morogoro (MORUWASA) ambaye Aprili anatanganza tender, ifikapo Juni na Julai tayari atakuwa amempata mkandarasi kwa ajili ya kuboresha kile chanzo cha Madibira ambacho kina umbali wa kilometa 17 kutoka chanzo kuja mjini Mikumi na kazi zitakazofanyika ni pamoja na kwanza kuboresha chanzo chenyewe cha maji cha Madibira ili kiweze kupanuliwa kuongeza kiwango cha maji na kuweka mabomba mapya ambayo yataleta maji katika Mji wa Mikumi.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuniona. Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Handeni Vijijini, Kata ya Mkata tulibahatika kupata mabwawa mawili, moja likiwa Mkata lakini la pili likiwa eneo la Manga.
Mheshimiwa Naibu Spika, mabwawa haya yako chini ya kiwango na mpaka sasa hayajaweza kuanza kutumika. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri katika ziara yake katika Jimbo la Handeni Vijijini alipita na kujionea hali halisi ya yale mabwawa. Pia aliweza kutuahidi wananchi wa Jimbo la Handeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja hapo. Mheshimiwa Naibu Waziri alituahidi baada ya kuona yale mabwawa kwamba wangefanyia kazi na kuweza kutupa ripoti ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wale ambao wamefanya ubadhilifu ili kuweza kupata utatuzi wa maji.
Wananchi wa Handeni Vijijini wangependa kujua, je, utatuzi umefanyika na ripoti imeshafanyiwa kazi ili tuweze kujua na hatua stahiki ziweze kufanyika kwa wale ambao wamefanya ubadhilifu huu? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitembelea kweli eneo hilo la Mkata nikakuta kazi iliyofanyika na kazi hiyo nilizungumza kwenye vyombo vya habari kwamba hata mimi sikuridhika nayo. Baada ya hatua hiyo Katibu Mkuu aliunda Tume ya Wahandisi kwenda kukagua hilo eneo, sasa hivi wanakamilisha kuandaa taarifa ili iweze kuwasilishwa Wizarani ili kuweza kuchukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji. Tuliweka utaratibu mwingine tumeshatangaza tenda tayari kwa ajili ya kupanua mradi wa HTM pale Korogwe ili uhakikishe kwamba unapeleka maji hadi Handeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tulishasema tunaweza tukatumia chanzo cha Wami ili tuweze kuchukua yale maji kuhakikisha kwamba eneo la Handeni Vijijini linapata maji ya kutosha.
MHE. ORAN M. NJENZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, suala la Mji Mdogo wa Mbalizi kuna changamoto kubwa za maji kama iliyokuwa kwa Mji wa Mikumi. Je, ni lini mtatatua changamoto kubwa ya maji kwenye Mji Mdogo wa Mbalizi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tuliwasiliana nae nikiwa kwenye ziara Mbeya na tukawa tumekubaliana kwamba tufanye mapendekezo, Wizara imeshaagiza tayari kwamba Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Mbeya ijipanue ili iweze kuhudumia mpaka eneo la Mbalizi. Tayari wanaendelea na utaratibu huo wameshafanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbalizi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbalizi ameonekana kuridhia ili Mamlaka ya Maji ya Mbeya iweze kupeleka miundombinu mpaka Halmashauri ya Mbalizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niahidi kwamba taratibu hizi zitakamilishwa na wananchi wa Mbalizi watapata huduma ya maji kutokana na Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mbeya.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Spika, takribani mwezi sasa wakazi wa Jiji la Tanga wanapata maji kupitia mamlaka ya maji ambayo siyo safi na salama.
Je, Serikali ina taarifa kwamba wakazi wa Tanga wanaweza kupata maradhi ya milipuko kutokana na kutokunywa maji ambayo siyo safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mamlaka ambazo zinaongoza kutoa huduma ya maji iliyo bora ni pamoja na Mamlaka ya Maji ya Tanga na Mamlaka ya Maji ya Moshi. Sasa kama hilo limejitokeza basi Mheshimiwa Mbunge nikuahidi kwamba tutalifuatilia kuona ni nini kimejitokeza katika hilo. Kwa taarifa tulizonazo ni kwamba mamlaka zinazoongoza ni pamoja na Mamlaka ya Maji ya Moshi na Tanga. Kwa hiyo, nikuahidi kwamba tutalifuatilia kuona ni eneo gani ambalo lilipata hiyo shida ya maji kutokuwa salama.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara katika Jimbo la Babati Mjini na akabaini kero za maji. Kwa hiyo, haya nitakayoyauliza anayafahamu vema na atanipa majibu.
Swali la kwanza, kwa kuwa mradi wa maji wa kijiji cha Malangi umechukua muda mrefu sana na kwa kuwa mradi huu ulitelekezwa na mkandarasi wa awali, na kwa kuwa mradi huu sasa thamani yake siyo shilingi milioni 400 ni shilingi milioni 600.
Je, Serikali iko tayari kutupatia fedha hizo shilingi milioni 600 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji Malangi ili wananchi hao wapate maji kwa muda mrefu ambao walikuwa wameyakosa?
Swali la pili, kwa kuwa mradi wa maji wa kijiji cha Nakwa wenye thamani ya shilingi milioni 801 umekuwa na changamoto nyingi, mabomba yapo juu hayajawekwa chini, yamekuwa yakipasuka wakati huu ambapo mradi unafanyiwa majaribio, na kwa kuwa vijana ambao pia walichimba mitaro kwa ajili ya kulaza yale mabomba hawajalipwa na mkandarasi ambaye anafanya kazi hiyo. Ilikuwa vijana hao walipwe shilingi 4,000 kwa kila mita wamelipwa shilingi 700.
Je, Naibu Waziri Wizara yako iko tayari kuunda timu ya wataalam kwenda kukagua mradi wa kijiji cha Nakwa ambao umekuwa ukisumbua wananchi hawa kwa mradi huo kuchakachuliwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli nilitembelea Babati na hizi changamoto tukiwa pamoja na Mheshimiwa Mbunge tuliziona na tulizijadili na kutoa maekelezo. Nikuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa utaratibu tuliouweka kwamba kila Halmashauri inapata bajeti. Kwa hiyo, hii fedha kwenye mradi wa Malangi tutahakikisha sasa unasimamiwa vizuri na pale nilitoa maelekezo kwamba Waheshimiwa Wabunge mnapoona inasua sua kwenye Halmashauri kama Mamlaka ya Maji ya Mkoa ambayo ipo chini ya Wizara ya Maji basi ni lazima tushirikiane katika utaalam ili kuhakikisha kwamba miradi inatekelezwa katika viwango vinavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumetenga fedha katika mwaka wa fedha unaokuja. Ile bakaa ya upungufu iliyobaki itaongezwa kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kijiji cha Nakwa, Mheshimiwa Mbunge mwenyewe ni shahidi unakumbuka kwanza tulitengeneza utaratibu kwamba kama mradi wa maji uliotekelezwa na Halmashauri uko karibu na Mamlaka ya Maji ya Mkoa, wakati wanapotekeleza ule mradi inabidi washirikiane ili kuhakikisha kwamba vile viwango vinavyotakiwa katika mradi viweze kufikiwa na hasa kwa kuwa mara nyingi miradi kama hiyo kwa sababu mamlaka za maji zina maji mengi, kumekuwa na tabia ya Wakurugenzi wanaomba mradi huo uunganishwe kwenye Mamlaka ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala hili pale tuliagiza kwamba Mkurugenzi wa Maji wa Babati sasa ashirikiane na Halmashauri ili kuweza kuhakikisha kwamba huu mradi ambao haukutengenezwa vile inavyotakiwa basi uhakikishe kwamba kwanza wanautekeleza katika viwango vinavyotakiwa. Pia nakubaliana na wewe kwamba Serikali italiangalia hili ili kuhakikisha wale walioharibu hatua stahiki zinachukuliwa.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Geita na Kasamwa kuna shida kubwa sana ya maji na Mheshimiwa Waziri tangu mwaka jana alisema wamepata pesa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika Mji wa Geita. Je, ni lini sasa mradi huo wa maji utatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Geita una miradi miwili, mradi mmoja ni ule ambao tunashirikiana na GGM na umeshatekelezwa mpaka tukafikia asilimia 30 tayari Mji wa Geita unapata maji. Pia unapata kutokana na ufadhili unaotokana na uboreshaji wa mazingira wa Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Kanyasu, tayari katika mkopo tuliopata wa milioni 500 kutoka Serikali ya India, sehemu ya fedha hiyo inatarajiwa kuboresha maji katika Mji wa Geita. Sasa hivi tunaendelea vizuri kwa ajili ya kumpata consultant atakayefanya mapitio na kuandaa tender document baada ya hapo kutangaza tenda ili tuweze kupata sasa maji ya uhakika kwa Mji wa Geita.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tabora Mjini lina kata 29, katika kata hizo kata 11 hazipati maji kabisa. Ni tatizo linalotokana na Serikali kudaiwa kiasi cha shilingi bilioni mbili na mkandarasi. Je, ni lini Serikali italipa pesa hizo ili hizi kata 11 ziweze kupatiwa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza bahati nzuri kwenye sherehe ya Pasaka nilienda Jimboni kwangu nimepita Tabora, nimekuta Mamlaka yetu ya Tabora imenunua mabomba mengi kuhakikisha kwamba katika hizi kata zilizosalia ni kata tisa ambazo zimebaki hazipati huduma ya maji mjini. Kwa hiyo, kata moja tayari inawekewa miundombinu ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi ambao tarehe 22 Mheshimiwa Waziri anakwenda kushuhudia kusaini mikataba ya mradi wa kutoa maji Solya kupeleka Nzega, Igunga na Tabora, kata zote zilizobaki sasa zitapata huduma ya maji kutoka kwenye huu mradi mpya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge baada ya mwaka mmoja au miwili Mji wa Tabora tutakuwa tumemaliza kabisa matatizo ya maji.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, lakini swali langu la msingi lililenga mahsusi vyanzo vya maji vilivyopo katika
Mkoa wa Morogoro hususan katika Milima ya Uluguru katika Vijiji vya Tegetero, Kinole, Mgeta na

Hewe lakini majibu yamekuwa ya jumla mno. Sasa nataka
kujua katika pesa hizi zilizotengwa shilingi 2.1 bilioni kwa ajili ya utunzaji wa maji ni kiasi
gani kimetengwa kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji katika Mkoa wa Morogoro ambao ndiyo chanzo cha
Mto Ruvu ambao unategemewa kwa ajili ya maji ya Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na kadhalika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Mkoa wa Morogoro tuna Chuo cha cha Kilimo cha Sokoine
ambacho kina wataalam waliobobea katika masuala haya ya utunzaji wa mazingira hususan katika kilimo na wako tayari kutumika kama muda wote wanavyojitolea lakini tatizo ni uwezeshaji. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuwawezesha wataalam hawa ili washiriki katika utunzaji huu wa mazingira kwa weledi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anasema alitaka kusikia kuhusu Milima ya Uluguru na ni kweli Mto Ruvu unatokea milima hiyo na katika ziara yangu nimekwenda kuona kule unakotokea. Kwanza kabisa, ni kiasi gani cha fedha kimetengwa, Mheshimiwa Mgumba kwa vile maji
yanatumika Mkoa wa Dar es Salaam zaidi, DAWASA peke yake wanatoa shilingi bilioni 1 kwenye Bonde la Wami Ruvu kwa ajili ya kushughulikia Mto Ruvu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kiasi hiki cha shilingi bilioni 2.1 kilichotengwa siwezi kusema ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili hiyo lakini ni fedha nyingi sana ambayo inapelekwa kwenye Bonde letu la Wami Ruvu kwa sababu hii Taasisi ya Bonde la Wami Ruvu iko moja kwa moja chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Hata hivyo, upo ushirikiano mzuri na Mkoa wa Morogoro kuhakikisha kwamba rasilimali hii inatunzwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu wataalam wa Chuo cha Sokoine, kama nilivyosema ushirikiano upo, kwa hiyo wote tunashirikiana, tunapata utaalamu wa wasomi wetu wa Chuo cha Sokoine na wanajadili na ndio maana utaona kwamba Bwawa la Mindu limewekewa mipaka na tayari kuna miti inapandwa kwa ajili ya kulinda bwawa lile. Utaalamu wote huo tunaupata kutoka Chuo cha Sokoine. Kwa hiyo, tunawashirikisha hawa watu ili kuweza kuwa na makubaliano ya pamoja kuhakikisha kwamba tunatunza rasilimali hizi.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa kuchimba visima vya maji katika kijiji cha Bumila, Iyoma na Mima. Hata hivyo, sasa ni miezi nane tangu visima vimechimbwa, hakuna pampu zilizowekwa, hakuna mabomba ya kusambaza maji wala matenki. Je, Serikali inasemaje kwa wananchi wa vijiji hivi ambao wana shida kubwa sana ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 na bajeti hiyo bado inaendelea. Kwa kutumia nafasi hii nimuagize Mkurugenzi wa Mheshimiwa Lubeleje, suala la pampu ni rahisi sana, maeneo yote ambayo visima vimeshachimbwa tunahitaji quotation ambayo tunaiweka kama ni certificate, ukiileta tunatoa hela ili uweze kununua pampu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kama inahitajika miundombinu ya ujenzi wa tenki na mabomba ya kusambaza maji na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, Mheshimiwa Lubeleje Mkurugenzi wako afanye usanifu wa haraka, atangaze tender. Kama ana upungufu wa wataalam Wizara ya Maji tuko tayari, atuandikie barua ili tuweze kumpa support ya kumpelekea wataalam ili kazi hiyo ifanyike haraka wananchi wa Jimbo lako Mheshimiwa Lubeleje waweze kupata maji kwa haraka.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nachukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya mradi huu mkubwa kwa takriban shilingi bilioni 90 ambao umekamilika. Pamoja na pongezi hizi, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Bado kuna tatizo la msukumo wa maji kutoka Ruvu Juu ili yaweze kuwa na pressure ya kutosha kuwafikia watejea, tatizo linalotokana na uhafifu wa umeme. Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha tatizo hili, ili mradi huu uweze kuwa na mafanikio makubwa zaidi hususan kwa wananchi wa Kibaha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; pamoja na kazi
nzuri hii, lakini bado maeneo ya Kidenge, Muheza, Kidagulo, Kikalabaka, Mikongeni na Mbwawa hawajakamilishiwa mradi wa usambazaji wa maji ili waweze kufaidi mradi huu. Je, kupitia bajeti hii tunayokwenda nayo Mheshimiwa Waziri yupo tayari kushughulikia na kuhakikisha miradi hii inakamilika ili wananchi waweze kupata huduma hii nzuri kwa mradi huu ulio bora ambao umeshakamilika. (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Koka kwa jinsi ambayo anawapenda wananchi wake wa Kibaha Mjini. Kwa sababu mara zote anafuatilia kwa kupiga simu kwa kuja Ofisini moja kwa moja, kumwona Mheshimiwa Waziri pamoja na mimi kuhusiana na tatizo la maji la Mji wa Kibaha, kwa sababu Mji wa Kibaha kwa sasa unapanuka sana. Swali la kwanza, pressure ni kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji tuligundua kwamba hakukuwa na umeme wa kutosha ili kuweza kuendesha mtambo ule kwa sababu ni mkubwa. Kwa sababu hiyo, tulitenga fedha na tayari sasa kazi inafanyika na imeanza kukamilika ili kuwa na umeme wa kutosha ambao utaweza kuendesha mtambo uliojengwa ambao ni mtambo mkubwa. Kwa hiyo, hili suala Mheshimiwa Koka ni kwamba tunalimaliza muda wote wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama nilivyozungumza katika swali letu la msingi kwamba kupitia awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, tunatenga fedha kuhakikisha kwamba maeneo yote ya Kibaha na maeneo yote yanayopitiwa na bomba kuu la kutoka Ruvu kwenda Dar es Salaam tutahakikisha kwamba tunaweka miundombinu ya kutosha ili wananchi waweze kupata maji, umbali wa kilomita 12 kutoka eneo la bomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba programu hiyo tunayo ambayo imeanza kutekelezwa kwenye mwaka wa fedha.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika ziara yake Naibu Waziri pale Wilayani Kilosa alitembelea bwawa la Kidete na alijionea jinsi ambavyo limekuwa likileta madhara makubwa ya mafuriko na kuharibu mpaka reli kwenye Wilaya yetu ya Kilosa. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Bwawa hili la Kidete ambalo ni muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa nilitembelea hilo eneo na nikaenda kuona shida iliyoko katika lile bwawa. Palikuwa na mkataba lakini tayari Serikali imechukua hatua ya kuhakikisha kwamba sasa unafanyika usanifu upya na fedha ilishatengwa katika bajeti ya mwaka huu tunaokwenda nao. Kwa hiyo, wakati wowote tutatangaza tenda baada ya kukamilisha usanifu mpya ili tuweze kulijenga lile bwawa katika standard ile inayotakiwa isilete madhara tena kwa wananchi wa Kilosa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali moja tu dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, Mkoa wetu wa Iringa una mito kama Ruaha, Mto Lukosi na kadhalika, lakini wananchi wamekuwa wakipata shida sana kwa suala la maji hasa vijijini ikiwepo Kilolo na Mufindi. Ni kwa nini Serikali sasa isitumie mito hii kuondoa huu upungufu ambao upo katika Mkoa wetu wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mkoa wa Iringa una utajiri mkubwa sana wa mito ikiwepo Ruaha Mkuu, lakini bado kuna Ruaha Mdogo, kuna Mto Lukosi ambao unatokea maeneo ya Kilolo. Kutokana na utajiri huo wa kuwa na mito mingi, kwanza kabisa Mto Ruaha Iringa Mjini tumeutumia, maji yanapatikana kwa asilimia 100 katika Mji wa Iringa. Sasa hivi tunaanza kusambaza maji kuyapeleka nje ya Mji wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia Mto Lukosi, nimeenda kule Kilolo, sasa hivi tunafanya utaratibu wa kuhakikisha tunasanifu mradi ili tuweze kutoa maji Mto Lukosi kuyapeleka maeneo yanayopitiwa na huo mto kuhakikisha kwamba maeneo mengi ya Iringa yanakuwa na maji ya kutosha ambayo ni safi na salama.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mji wa Maswa umekosa maji kwa mara nyingine tena kwa muda zaidi ya wiki moja baada ya operesheni kata umeme. Kata umeme imeathiri hadi mamlaka ambazo ziko daraja la tatu ambapo kama Mamlaka ya Maji ya Mji wa Maswa iko daraja la tatu kwa hiyo bili zake zinalipwa na Wizara, hawajilipii bili wao wenyewe. Kwa hiyo Wizara haijalipa TANESCO …
TANESCO wanakata. Swali langu, napenda kupata commitment ya Serikali ni lini Maswa watarudishiwa umeme katika Mamlaka ya Maji ili wananchi wa Maswa waweze kupata maji katika Mji wa Maswa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hilo nakiri kweli lipo lakini Serikali tumekaa kikao Wizara ya Maji na Hazina pamoja na TAMISEMI tumekubaliana. Vilevile tarehe 8 Mei Makatibu Wakuu wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Maji watakaa kukamilisha suala hili ili kuhakikisha tatizo la malipo lililokuwepo tukishakaa na Hazina tutalimaliza ili maeneo yote umeme uweze kurejeshwa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, kwenye bajeti ya mwaka huu hakutupatia pesa kwa ajili ya mradi mkubwa ambao uko kwenye usanifu. Naomba awaeleze wananchi wa Jimbo la Kyerwa, mradi huu utakapokuwa umekamilika kwa ajili ya usanifu.
Je, yuko tayari kuhakikisha anawapatia wananchi wa Jimbo la Kyerwa maji safi na salama kwa sababu maji ni tatizo Wilaya ya Kyerwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri ya Mheshimiwa Bilakwate ilipata shilingi milioni 200 na fedha hizo tayari zimeshatumika kuboresha chanzo cha maji kwenye kijiji kimoja eneo la mjini na tayari maji yanapatikana. Pia, kupitia vyanzo vingine vya Wizara yetu ya Maji na Umwagiliaji, tayari tumesaini mkataba wa usanifu ambao ukikamilika, umelenga kuvipatia vijiji zaidi 57 maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kesho tunawasilisha bajeti kwenye Bunge hili na katika bajeti hiyo tayari utaona wewe mwenyewe ni nini tumetenga ambacho kitahakikisha kwamba baada ya kukamilisha mradi wa usanifu, basi ujenzi utaanza bila wasiwasi wa aina yoyote.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii adimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililoko Madaba linafanana sana na tatizo lililoko Jimbo la Buyungu. Wilaya ya Kakonko ina miradi ya maji ya Mradi wa World Bank katika vijiji vya Muhange, Katanga na Nyagwijima kata ya Mgunzu. Miradi ile inaendelea kusuasua na wananchi hawanufaiki na miradi ile wakati fedha zilitolewa na fedha hizo ni za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Kauli ya Serikali ni lini miradi hiyo itakamilishwa ili wananchi wa Muhange, Katanga na Nyagwijima waweze kupata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bilago mwenyewe ni shahidi, Serikali imetoa fedha. Utekelezaji wa miradi unafanywa na Halmashauri. Katika hiyo Halmashauri, Mheshimiwa Mbunge wewe ni Diwani kule, hebu naomba tusaidiane kusimamia hao Wakandarasi waweze kukamilisha hii miradi. Tatizo la hela halipo, hela tunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Halmashauri ya Kakonko na sisi Madiwani na Mheshimiwa Mbunge, tuwasimamie Wakandarasi ipasavyo ili miradi iweze kukamilika.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Mhagama, matatizo yaliyoko Madaba yanafanana moja kwa moja na matatizo yaliyoko Jimbo la Ndanda. Kwenye bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Waziri utakumbuka zilitengwa fedha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kupeleka MANAWASA ili kununua viunganishi pamoja na mabomba ambayo yangeweza kupeleka maji katika kata za Chikukwe, kijiji cha Maparagwe pamoja na kijiji cha Chikunja. Wananchi walikubali watajitolea nguvu zao, lakini mpaka sasa hivi mabomba yale hayajakwenda.
Je, unaweza kutueleza ni lini Serikali itapeleka pesa hiyo, wakati tumebakisha siku chache tu kumaliza mwaka wa bajeti? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa kwamba Serikali ilitenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza Mradi wa Mbwinji pale Masasi, kupitia Mamlaka ya MANAWASA. Juzi juzi hapa Mheshimiwa Mbunge tuliwasiliana, walileta andiko na andiko hilo tayari limesapitishwa ili MANAWASA waweze kusaini mkataba kwa ajili ya procurement ya hivyo vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari kwa maana ya Wizara imeshaidhinisha kwa hiyo, ni kazi ya Mkurugenzi wako sasa kusaini mkataba na mkandarasi yule ambaye mmempa kazi. Ile kazi ni ya kununua vifaa; vifaa vile ni kitu cha wiki mbili vitakuwa vimeshanunuliwa na mkishamaliza, kwa utaratibu wetu, mnaleta certificate tunatoa hela, mkandarasi analipwa. Kwa hiyo, kama MANAWASA watafanya haraka, hela hiyo lazima mtaipata katika huu mwaka wa fedha.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa vile Halmashauri ya Wilaya ya Madaba sasa ipo kisheria na tayari kumekuwa na mgawanyo wa mali na miradi mbalimbali kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Songea; na kwa vile Halmashauri ya Wilaya ya Songea ipo mbali sana kijiografia na Halmashauri ya Wilaya ya Madaba; kwa nini sasa miradi isikabidhiwe kwa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ili iweze kusimamiwa kwa ukaribu na kwa ufanisi zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa vile yapo mabomba ambayo yalinunuliwa kwa kupitia mradi huu na mkandarasi na kwa miaka zaidi ya miwili yapo nje, yapo juani, yanazidi kuwakiwa jua na yanapoteza ubora; kwa nini sasa Wizara isimshauri mkandarasi kwa kushirikiana na Halmashauri ili yale mabomba sasa yaweze kufukiwa katika njia ambazo zimekusudiwa na mradi huu ili miradi midogo midogo ya maji ambayo wananchi wameianzisha na wanaiendeleza iweze pia kuingia kwenye mtandao huu na kuanza kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, miradi hii iliibuliwa ikiwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea na sasa hivi Madaba sasa ni Halmashauri. Anasema, kama vitu vingi vimeshagawiwa tayari, kwa nini ile miradi ibakie kuwa Songea? Hatuna tatizo na hilo na halitakuwa la kwanza. Kuna Halmashauri nyingi mpya. Kwa hiyo, kama wameshakamilika, basi utuletee barua kuomba hilo na Wizara itakubaliana na hiyo hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba kuna mabomba ambayo yameshanunuliwa na mkandarasi na yanaungua na jua; kwa nini yasifukiwe ili wananchi wapate maji?
Mheshimiwa Mhagama, kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha 2016/2017 ulitengewa zaidi ya shilingi milioni 800 ambayo matumizi yake inapanga Halmashauri yenyewe. Naomba tu kushauri kwamba Halmashauri yako basi watumie hizo fedha kwa sababu mnazo ili waweze; ama kwa kutumia nguvu ya wananchi ama huyo mkandarasi basi, kwa nini asiyafukie kwa sasa na hela inatolewa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba tu Mheshimiwa tuwasiliane ili tuweze kulijadili hili kwa pamoja, mabomba haya yafukiwe haraka wananchi wapate huduma ya maji.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mamlaka ya Maji ya Mji wa Karatu (KARUWASA) ina kisima kimoja na kisima hicho kimeharibika na ni miezi miwili wananchi hawana huduma ya maji; na Mamlaka hiyo iko katika kundi la Mamlaka Daraja la C ambalo zinapata ruzuku kutoka Serikalini:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kuokoa kisima hicho ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea Karatu na nilikuta kweli kisima hicho kilikuwa kimepata shida ya pampu. Akiba ya fedha niliyoikuta kwenye Mamlaka ya Karatu ilikuwa shilingi milioni tano na tulitoa maelekezo kwamba ashirikiane na Mamlaka ya Arusha ili waweze kum-support kupata pampu nyingine. Sasa Mheshimiwa Mbunge kwa sababu imekuwa ni muda kidogo, naomba tuwasiliane baadaye, nitafanya mawasiliano na Mamlaka ya Arusha kuona wamefikia wapi ili kurudisha ile huduma pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tulikubaliana, viko visima vitatu ambavyo tayari vimeshachimbwa na Serikali, tuhakikishe kwamba, kwenye bajeti tunayoitoa tuwekee miundombinu na kuweka pampu ili kuhakikisha wananchi wa Karatu wanapata maji safi na salama.
MHE. HASSANI S. KAUNJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naibu Waziri yuko tayari kuwaambia wananchi wa Lindi kumwambia Mbunge wao na Mheshimiwa Rais kwamba ahadi ya Mheshimiwa Waziri wake ya kwamba mradi huu utakamilika tarehe 3 Julai, 2017 kwamba, itatekelezwa kama walivyoahidi? Swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri awe tayari kuweza kunifikishia salamu zangu za pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu na yeye mwenyewe kwa kuweza kukamilisha mradi mwingine pacha na huo wa kijiji cha Chikondi. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kunifikishia salamu zangu hizo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge, ahadi ya Mheshimiwa Waziri itatekelezwa na nikwambie tu kwamba ni siku kumi tu zimepita nimeenda Lindi, nimeenda kukagua ule mradi, nimekuta vifaa vyote vilivyokuwa vinatakiwa kwenye mradi vimewasili na tayari kuna kundi kubwa ambalo liko pale linafunga na mabomba yaliyobaki yanakamilishwa na eneo ambalo kutokana na mvua kubwa mabomba yalifumuliwa, linarekebishwa. Kwa hiyo, uwe na uhakika kabisa kwamba maji yatatoka na inawezekana hiyo tarehe 3 au kabla ya tarehe 3 Julai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, Mheshimiwa Mbunge, Waheshimiwa Wabunge wamecheka, hawakujua wewe una maana gani? Ni kwamba baada ya ziara ya Mheshimiwa Rais, tuliamua kuchimba kisima kingine ili kuongeza uwezo wa upatikanaji wa maji Lindi na kisima kile tayari kimekamilika, na mimi mwenyewe nimeenda kukagua juzi. Tumekuwa na matatizo kidogo yaliyokuwa yamejitokeza kuhusiana na ukataji wa huduma ya umeme kwenye mitambo, ambapo jana tumekaa nao kikao; tunatarajia kulikamilisha mapema. Kwa hiyo, Mheshimiwa nikuhakikishie kwamba huduma ya maji Lindi inafika na Mheshimiwa Waziri yupo humu ndani, ameshasikia salamu zako. Nakushukuru sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Mji mkongwe wa Mbulu ni mji wa zamani. Umekumbwa na tatizo kubwa la maji hivi karibuni, lakini tatizo hili la miradi ya maji kusuasua katika utekelezaji limeikumba Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Serikali mwaka huu ilitenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa maji Mbulu Mjini. Mradi huu hadi sasa utaratibu umeshafanyika wa tenda kwa kupitia Mamlaka ya Maji Mji wa Babati, lakini hakuna hatua iliyofikiwa umebaki mwezi mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika Mheshimiwa Naibu Waziri mwenye dhamana, alifika Mbulu akafanya ziara. Mradi wa Maji ulioko katika kijiji cha Moringa Daudi una takribani miaka minne, hadi sasa mradi huo umeshindikana kukamilika na mkandarasi alimdanganya Mheshimiwa Naibu Waziri alipotembelea site.
Je, ni hatua gani ichukuliwe kwa mkandarasi wa namna hii ambaye alimdanganya Mheshimiwa Waziri hadi leo ni miezi minne hajakamilisha mradi huo, ambapo aliahidi mbele ya Mheshimiwa Naibu Waziri wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba nijibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kwa mujibu wa Kanuni. Maana ameuliza maswali mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za mkataba zinashughulikiwa kwa masharti yaliyoko ndani ya mkataba. Kwa hiyo, naomba tuwasiliane mimi na wewe ili tuone huyu mkandarasi ni wapi ambapo ameteleza tuweze kushauri. Kwa sababu mkataba huo umesainiwa na Halmashauri yake, Wizara ya Maji na Umwagiliaji iko tayari kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha kwamba tunashauriana ili kumfanya huyu Mkandarasi aweze kutekeleza miradi. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la kutokamilika kwa miradi ya maji kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara linaonekana kuwa sugu na moja ya chanzo chake ni wakandarasi kutokaa site; na mfano mzuri Naibu Waziri anajua ni miradi ya maji ya Jimbo langu, maeneo ya Ingawali, Linoha, Nyangamala, Namangale na maeneo mengine; tatizo kubwa ni kwamba hawa Wakandarasi hawakai site; wanakwenda mnapokwenda kufanya ziara. Msipoenda na wao wanarudi Dar es Salaam, ndiyo maana miradi hii haikamiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni hatua gani mnachukua ambazo zitasaidia hawa wakandarasi wakae site ili miradi ikamilike kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea kwenye Jimbo lake na huo mradi mkubwa niliutembelea na siku nilipokuwepo pale ni kweli mkandarasi alikuwepo. Kama kuna hilo tatizo la mkandarasi kutokukaa kwenye eneo la kazi yake na mkataba tunao na vifungu vya mkataba viko ndani ya mkataba, wasiwasi wangu ni kwamba wale wanaosimamia mkataba hawachukui hatua za kimkataba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge nitawasiliana nawe ili tumpigie Mkurugenzi simu tumwulize kama hilo linatokea. Nami vifungu navijua kwa sababu nimesimamia mkataba, tumwelekeze kitu cha kufanya.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri katika jibu lake la msingi amesema kwamba vijiji vya Mkarango na Nandete katika kata ya Kipatimu na vijiji vya Kata ya Kinjumbi na Kibata vitapata mawasiliano katika mradi utakaokamilika ifikapo Novemba, 2017; sasa tunazungumza ni mwezi Mei. Nataka nijue tu, je, programu ya utekelezaji wa miradi hiyo umeshaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kumekuwa na utaratibu kwa kampuni moja kujenga minara ya simu, baadae makampuni mengine kuja kufunga mitambo yao ya mawasiliano. Nataka nijue katika kata ya Chumo pana kampuni imejenga mnara wa simu na kuna kampuni moja tu ya Vodacom ndiyo imefunga mitambo yake ya mawasiliano.
Je, ni lini makampuni ya Airtel na Tigo yatakuja kufunga mitambo yao ya mawasiliano, ili kutanua wigo wa mawasiliano kwa wananchi wa kata ya Chumo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kutokana na jibu la msingi kwamba ifikapo Novemba mwaka 2017, mwaka huu tulionao kwamba, miradi ambayo inaendelea itakuwa imekamilika. Kwa msingi wa jibu hilo ni kwamba, programu hii inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la pili, amesema kwamba, kuna Kampuni ya Viettel imetajwa, lakini kuna Kampuni ya Vodacom, kuna Kampuni za Tigo, umeona kampuni moja ipo pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala moja dogo
Mheshimiwa Mbunge, ni suala la fizikia nyepesi tu kwamba hii minara inafanya kazi kwa kutegemea mawimbi na mawimbi ya Vodacom, mawimbi ya Airtel, minara ya Airtel, mawimbi ya Viettel ni mawimbi yanayotegemeana, kwa hiyo, kukishakuwa na Mnara mmoja wa Vodacom
unarahisisha pia Mnara wa Viettel kuja kujengwa pale. Kwa hiyo, ukishatangulia mnara mmoja, basi tarajia kabisa kwamba, na minara mingine na makampuni mengine yatakuja kuwekeza kwa sababu kumeshakuwa na urahisi wa kuwepo mawimbi katika lile eneo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Matatizo ya Mawasiliano ambayo yanalikabili Jimbo la Kilwa Kaskazini yanafanana na yale ya Jimbo la Nanyamba kwa sababu kuna kata za Njengwa, Nyundo, Nitekela na Kiyanga ambayo hayana mawasilinao. Na nilishawahi kuuliza swali hili hapa Bungeni nikaambiwa kwamba Mfuko wa Mawasiliano utapeleka mawasiliano huku na mradi huo bado mpaka sasa hivi haujatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nipate majibu ya Serikali kuhusu miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO):
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Mawasiliano upo na huu unatekelezwa moja kwa moja na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini pia kuna programu nyingine ambayo ni ya watu binafsi ambao wamependa kuja kuwekeza katika nchi yetu. Kwa hiyo, kama hukupata kwenye mradi wa mawasiliano, basi tarajia pia unaweza ukapata kwenye hawa wawekezaji ambao wamekuja kufanya biashara kwenye eneo letu la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika hoja yako tayari umesema tayari ulishaahidiwa kupitia kwenye huu Mfuko wa Mawasiliano, Mheshimiwa Mbunge, niseme tu kwamba hebu tuvute subira kidogo, kama umeshaahidiwa hili lazima litatekelezwa.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mradi wa dharura ambao anaouongelea Mheshimiwa Waziri hatua za awali zilianza tangu 2015, mradi ambao unatoka Pongwe kuleta maji Muheza. Hata hivyo, nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini mradi huu utakamilika ili uweze kupunguza adha ya maji kwa wananchi wa Muheza Mjini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameongelea Mto Mnyodo. Kuna madhara makubwa yametokana na mvua zinazoendelea kunyesha, vyanzo vingi vya maji vimeharibika, lakini Waziri amejibu hapa kwamba wanategemea upatikanaji wa fedha ndipo watarekebisha vyanzo hivi vya maji. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie, kwa sababu hili ni suala la dharura la uharibu wa vyanzo vya maji, ni lini hiyo fedha itapatikana ili kutengeneza vyanzo hivi ili wananchi waendelee kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Komba tukubaliane tu, si kwa nia mbaya lakini ni kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Muheza amekuja ofisini mara tatu na nilimuagiza aje pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji ya Tanga, tukafanya utaratibu, sasa hivi tuko kwenye utaratibu wa manunuzi. Ni kweli kwamba mradi unaanza utekelezaji mwezi Juni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini utakamilika, baada ya kukamilika kwa taratibu za manunuzi na kumpata mkandarasi, ndani yake sasa baada ya kusaini mikataba ndipo tutajua ni lini sasa mradi utakamilika; lakini shughuli imeshafanyika na mradi unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 2.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la uharibifu, mvua imenyesha sana Tanga na taarifa ninayo, Kamati ya Ulinzi na Usalama na nimeshaipata ile nyaraka ya uharibifu uliotokea kwenye maeneo mengi. Kwa hiyo, sasa hivi taarifa hiyo, kwanza itapelekwa kwa Mheshimiwa Jenista kwenye ile Kamati ya Maafa, lakini wakati huo hu na sisi tutachukua hiyo nakala, baada ya kupata taarifa ya Mheshimiwa Jenista na sisi tutafanyia kazi ili tuhakikishe tumekarabati miradi hiyo kwa haraka ili wananchi wapate huduma ya maji. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi hilo tunalifanyika kazi. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Napenda niulize swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri shemeji yangu. Hivi tunavyoongea mradi mkubwa wa maji katika Mji wa Bunda unakaribia miaka 10 bila wananchi wa Bunda kupata maji safi na salama, yaani kama mihula ya Mheshimiwa Rais ni mihula miwili. Tatizo kubwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ni mkandarasi, mkandarasi yule ni mwizi, ana madeni, kila pesa mnayoiweka Serikalini kwa ajili ya kukamilika mradi ule ili wananchi wa Bunda wapate maji safi na salama…
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 tumetenga bilioni 1.6 kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa kutengeneza chanzo cha maji. Tumeendelea na shughuli ya kufanya ununuzi wa makandarasi, tukapata makandarasi wabaya, kwa hiyo tumetangaza tena. Hata hivyo, kuhusu hao wakandarasi hao wanaoendelea Mheshimiwa Bulaya nimuahidi kwamba nitaenda huko niende nikawaone. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali. Mheshimiwa Waziri wa Maji nimewahi kuonana naye mara nyingi sana kuhusu mradi wa maji kutoka Nyamtukuza kwenda mpaka Bukwimba. Mradi ule umepangiwa 15,000,000,000 mpaka sasa hivi Serikali imeshatoa bilioni 3.5 lakini cha ajabu hata kijiji kimoja hakijawahi kupata maji. Je Serikali ina mpango gani ili kuweza kukamilisha mradi huo wa maji ili wananchi wa Nyangh’wale waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Hussein tumeweka utaratibu kuhakikisha kwamba miradi yote ambayo ilianza tunaikamilisha kwanza kabla ya kuingia kwenye miradi mipya. Sasa hivi tunaendelea kuzunguka kubaini mahali popote pale ambapo pamehujumiwa Mheshimiwa Mbunge taratibu za kisheria zitafuatwa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa inaonekana utaratibu wa usambazaji maji unakuwa mgumu sana na ziko mamlaka za maji kwa mfano mamlaka ya MWAUWASA pale jiji la Mwanza; Serikali ina mpango gani kuziwezesha mamlaka hizi ili ziweze kuwa zinatatua changamoto za maji zinakabiliana nazo kwenye maeneo zilizopo? Hii itakuwa msaada mkubwa sana kwa Halmashauri hizi lakini pia kwa wananchi wenyewe. Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawekeza, inaweka miundombinu ambayo ndio imekuwa chanzo cha maji. Kwa mfano tuna bomba la KASHWASA likishapita kwenye maeneo mamlaka Halmashauri na kwa sababu tunaendelea kutenga bajeti kila mwaka kile ndio chanzo chao cha maji. Kwa hiyo wanaweza wakatumia ile fedha; na tayari matoleo yanawekwa kila sehemu wanaweza wakaunganisha pale wakaendelea kusambaza maji ili wananchi wapate maji safi na salama.
MHE. SEVERINA S. MWIJAGE. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa mradi wa Shinyanga – Kahama uko karibu sana na Bukoba, ni lini Serikali itafanya upembuzi yakinifu kuunganisha maji kuanzia Wilaya ya Muleba, Bukoba Mjini na Wilaya zingine zilizopakana kwa sababu tunapata matatizo ya maji na sisi tuko karibu na mradi huo, ni lini Serikali itaunganisha maji kuwapa watu wa Bukoba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza maji Bukoba tayari, mradi tumeshakamilisha na wananchi wanapata maji. Kazi iliyopo sasa hivi ni kuendelea kutanua mabomba ili yale maji yaweze kufika kwenye maeneo mengi. Kwa hiyo, kwa Mji wa Bukoba maji tayari tunayo.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kuna mradi mwingine unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika Mji Mdogo wa Malinyi unaosuasua toka mwaka 2013. Kwa sasa mabomba ya usambaji maji ya mradi huo yamekwama katika Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu ya tozo ya storage. Halmashauri tumeomba kuondolewa kwa tozo hiyo lakini mpaka sasa hatujafanikiwa. Je, Serikali inatusaidiaje katika ombi hilo ili kukamilisha mradi huu ili wananchi wapate maji safi na salama?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa matatizo ya maji yanayowakabili wananchi wa Malinyi yanafanana na matatizo yanayotukabili wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki; na kwa kuwa vijiji vya Mtego wa Simba na Newland vilikuwa ni vitongoji wakati wa mradi wa maji Fulwe - Mikese unafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2006; na kwa kuwa mradi huo sasa unatekelezwa tangu mwaka 2016 na vitongoji hivi viwili vya Newland na Mtego wa Simba sasa ni vijiji kamili.
Je, Serikali inavisaidiaje vijiji hivi vya Mtego wa Simbana Newland kupata maji safi na salama ukizingatia vilikuwa ni sehemu ya mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mradi wa Malinyi, kwa bahati nzuri nimeshatembelea kule na niliyakuta mabomba yapo na mkandarasi alikuwa anaendelea kufanya kazi. Kama kuna mabomba ambayo yamesalia, yako bandarini na yanaendelea kuongeza storage, kwangu hii ni taarifa mpya lakini hili ni suala la kiutawala, tupate taarifa ni kwa nini mabomba hayo yamekwama, tutasaidiana ili yaweze kutoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu kupeleka maji Mtego wa Simba na Newland. Tunaendelea na Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kama alivyosema mwenyewe kwamba kuna mradi unaendelea tutahakikisha kwamba mradi huu unakamilika ili na hayo maeneo mawili yaweze kupata maji ama ya mabomba au kwa kutumia visima ili mradi wananchi hao wapate maji safi na salama.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mradi wa maji wa kijiji cha Getamok katika Wilaya ya Karatu uliojengwa kwa zaidi ya gharama ya shilingi milioni 600 chini ya Programu ya Kwanza ya WSDP hivi sasa haufanyi kazi kwa sababu ya kujengwa chini ya kiwango. Mabomba yaliyofungwa kwenye mradi huo yanapasuka kila kukicha na hata matenki yanavuja. Halmashauri ya Wilaya imejaribu kurejesha huduma kwa kutumia vyanzo vyake lakini imeshindikana kwa sababu fedha nyingi zinahitajika.
Je, Serikali itawasaidiaje wananchi wa kijiji hicho kupata huduma hiyo ya maji safi na salama na pia wale waliofanya ujenzi huo chini ya kiwango Serikali itawachukulia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ipo miradi mingi katika nchi yetu ambayo imepata shida hiyo kwamba kiwango cha utendaji kilikuwa chini aidha mabomba yaliyonunuliwa hayakuwa yamenunuliwa katika viwango vinavyotakiwa. Kwa sasa tunatakiwa ku-review ili tuweze kununua mabomba ambayo ni bora sambamba na kuchukulia hatua wale ambao wamehusika kutufikisha hapo tulipo. Sheria na taratibu tunazo, tutumie Halmashauri na kama utaona kwamba mambo hayaendi, naomba tuwasiliane. Kupitia kwenye Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Wizara ya Maji na Umwagiliaji tutaingilia.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, miradi hii ya World Bank katika Jimbo langu la Mbagala ilikuwepo Kijichi, Kiwika, Kizinga na Bugdadi ambapo visima vimechimbwa, maji yamepatikana lakini mpaka sasa hivi miundombinu ile haijasambazwa, wananchi bado wana kero kubwa. Je, ni lini Serikali sasa itasambaza miundombinu ile ili wananchi waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni hatua nzuri na ndiyo tunavyokwenda, tunachimba tunapata maji, tunafanya test, tunaona kwamba maji haya yanafaa kwa matumizi ya binadamu. Baada ya hapo tunaweka bajeti kwa ajili ya kuweka sasa miundombinu ya kusambaza na kuhifadhi maji ikiwemo na kujenga matanki. Kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 na juzi Mheshimiwa Mbunge umepitisha bajeti basi naomba kwa kutumia Halmashauri yako na fedha mnapanga wenyewe mhakikishe kwamba mnaweka sasa miundombinu ili wananchi waendelee kupata maji.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Waziri maswali ya kwamba tunatambua Bwawa la New Sola yaani Bwawa la Zanzui linapokea maji kutoka mito mitatu, Mto Mwashegeshi, Mto Sola na Mto Mwabayanda na bwawa hili lilikuwepo wakati Bwawa la Old Sola likiwepo na lilikuwa linatunza maji ya ziada. Je, hamuoni kwamba kuna umuhimu wa kulijenga hili Bwawa la Old Sola ili kuhifadhi maji na kukabiliana na ukame wa maji katika Wilaya yetu ya Maswa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nimejibiwa kama Mbunge wa nchi nzima, mimi ni Mbunge wa Maswa, mabwawa 35 yalishafanyiwa upembuzi yakinifu, leo mnasema mnaangalia inventory ya nchi nzima halafu mtafanya ukarabati. Mimi naomba kwa ajili ya Wana-Maswa, ni lini mtawajali Wana-Maswa ili muweze kuwajengea mabwawa haya na vijiji vya Maswa viweze kupata maji ya kutosha? Kwa sababu katika Mradi wa Ziwa Victoria tuko phase ya pili, tutachelewa kupata maji. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anawapenda wananchi wake kuhakikisha kwambwanapata maji safi na salama. Pia nishukuru kwamba nilivyofanya ziara Maswa tulikuwa wote, tulitembea mpaka tukaenda mabwawa yote mawili. Mheshimiwa Mbunge tunafuata wataalam wanatushauri nini na bado tunaendelea kuongea nao kwamba kwa nini tusikarabati Old Sola ili liweze kutunza maji wakati haya ya hili bwawa lililopo yakiisha tunaweza tukatumia lile. Wameniambia kwamba hiyo inawezekana lakini kama lile likaweka maji bila kutumika chochote kinaweza kikatokea, kama ilivyotokea kwamba lilibomoka, linaweza likaja kuathiri na hili bwawa ambalo tayari limeshawekewa miundombinu. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge siyo kwamba tumeishia hapo, bado wataalam wanajaribu kufanya uchunguzi kuona ni namna gani watafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukija kwa upande wa swali la pili, ujenzi wa mabwawa hayo, ni kwamba ndani ya Bunge hili tulishatoa maelekezo kwenye Halmashauri nchi nzima kwamba kila Halmashauri iainishe mabwawa. Pia tumeelekeza kwamba Halmashauri zenyewe zinatakiwa kutenga fedha na kuhakikisha kila mwaka walau wanajenga bwawa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia hivi kwa ujumla kwa sababu sisi Wizara tunafanya kazi ya maji kwa nchi nzima, hatufanyi kwa Halmashauri moja. Kwa hiyo, pamoja na Halmashauri yake na Halmashauri nyingine zilizopo hapa nchini zinatakiwa kutekeleza hilo.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maji na umwagiliaji nchini imetekelezwa chini ya kiwango ukiwemo mradi wa maji unaotekelezwa katika Kata ya Mkako, Wilayani Mbinga. Mradi huu wa Mkako ulikuwa ukabidhiwe katika Mbio za Mwenge zilizofanyika wiki iliyopita, wananchi waliukataa kwa sababu hautoi maji kabisa. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam Wilayani Mbinga kukagua Mradi wa Mkako pamoja na miradi mingine ya Kigonsera, Litoho na ya kijiji cha Kiongo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, amesema kwamba miradi mingi ya maji imejengwa chini ya kiwango. Sawa inawezekana ni hilo, lakini sisi taarifa tuliyonayo ni kwamba miradi mingi ilibuniwa lakini baada ya kujengwa vile vyanzo vya maji vimekosa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inawezekana ni kwa ajili ya kukosa maji au ilikuwa vimejengwa vibaya, hilo linahitaji utafiti ili tuweze kulidhihirisha na tuweze kulitolea majibu katika Bunge hili.
Hata hivyo, kama kweli mradi umejengwa chini ya kiwango, basi Halmashauri husika inatakiwa ilione hili, iweke wataalam walifanyie uchunguzi kuona tatizo lilikuwa liko wapi. Wakiona kuna tatizo sheria stahiki zitachukuliwa ili tuweze kuhakikisha kwamba mradi huo tunauboresha wananchi wapate maji safi na salama.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa, mikoa niliyoitaja inakumbwa na tatizo la upungufu wa chakula mara kwa mara; na kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema wanao huo mpango kabambe wa kuanzisha au wa kujenga mabwawa kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini. Je, Serikali inaonaje juu ya kuyapa kipaumbele maeneo ya Mikoa hii ya Shinyanga, Mwanza, Singida, Dodoma, Tabora ili kuweza kujenga mabwawa hayo ili wazalishe chakula wakati mvua zinapokuwa hafifu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa, pia katika Wilaya ya Maswa tuna mabwawa madogo madogo mengi, likiwemo bwawa la Seng’wa, Mwamihanza, Masela, Sola na mengine. Je, Serikali ina mpango gani wa kuyafufua mabwawa haya kwa kuwa, sasa yamejaa mchanga, ili yatumike kuwapatia wananchi wetu maji, lakini pia yatumike kwa kilimo cha mboga mboga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ametaja Mikoa ya Shinyanga, Tabora na mikoa mingine ambayo ina uhaba wa mvua na kwamba, je, Serikali ina mpango gani wa kuipa hii mikoa kipaumbele katika ujenzi wa mabwawa. Sasa ipo timu ya wataalam ambao wanapitia maeneo yote yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yao itatuelekeza sasa ni sehemu gani ambayo inaonekana kuwa na kipaumbele kwa ajili ya kuwekewa hayo mabwawa. Wakishakamilisha hiyo taarifa, mwaka huu wa fedha tulionao basi tafiti zitaelekea kwenye hayo mapendekezo ya maeneo ambayo yanahitaji kujengwa mabwawa na maeneo ambayo yana ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili limezungumzia kuhusu Maswa, wilaya yake na kwamba kuna mabwawa yaliyopo tayari, lakini yameshajaa mchanga. Sasa Serikali ina mpango gani. Tulishasema katika Bunge hili, tumeelekeza halmashauri kuhakikisha ama zinasanifu kujenga mabwawa kila wilaya, kila halmashauri au kufanya ukarabati wa mabwawa hayo yaliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale ambapo wanashindwa tumewaelekeza kwamba, wawasiliane na sisi, ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba, tunafanya ukarabati au tunajenga mabwawa na hasa pale inapokuwa kwamba, mabwawa hayo yanahitajika kwa ajili ya maji safi na salama ya matumizi ya majumbani. Kwa hiyo, niendelee tena kusisitiza halmashauri zihakikishe kila mwaka zinatenga fedha kwa ajili ya miundombinu ya mabwawa madogo ya maji.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Matatizo yaliyopo katika Mikoa ya Simiyu, Dodoma na Shinyanga yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Halmashauri ya Temeke, pia hatuna maji. Mheshimiwa Naibu Waziri anakumbuka kwamba, Halmashauri ya Temeke si wanufaika wa maji yanayotoka Mto Ruvu hivyo, hatuna mfumo wa mabomba na tunatumia maji ya kisima na taarifa za wataalam zinasema kwa sababu Halmashauri…

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, mfumo wa maji taka umechanganyika na mfumo wa maji safi ya kisima tunayotumia Temeke. Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kuhakikisha kwamba, mnatuletea maji ya bomba Temeke, ili tuachane na kunywa haya maji machafu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Temeke kwanza tunao mtambo wa maji wa Mtoni, ila kweli kwamba, maji yanayotoka pale ni machache. Hata hivyo, tayari tunakamilisha uchimbaji wa visima 20 Kimbiji na Mpera na sasa hivi tunatafuta fedha na tunayo ahadi kutoka Benki ya Dunia, ili tuweze kuweka miundombinu ya usambazaji kuhakikisha kwamba, maeneo yote yale Mheshimiwa Mbunge Temeke na Mbagala yaweze kupata maji safi na salama. Kwa hiyo, ni suala la wakati tu, tayari maji tunayo, tunachoshughulikia ni kupata fedha za kusambaza miundombinu ili wananchi wake waweze kupata maji safi na salama.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala iliamua kupambana na tatizo hili la maji wakaamua kuchimba bwawa katika Kijiji cha Chilangala, Wilaya ya Newala, lakini kutokana na ufinyu wa fedha lile bwawa hawakulimaliza. Je, Serikali iko tayari kwenda kumalizia lile bwawa ili tuweze kutatua tatizo hili la maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ndiyo kwa mara ya kwanza ananipa taarifa kwamba, kumekuwa na mradi wa bwawa ambao unafanywa na Halmashauri katika maeneo ya Jimbo lake kule Newala. Niseme kwamba, niko tayari tufanye mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo tayari kupitia mkopo wa India ambao tunasubiri Financial Agreement isainiwe, hela nyingi imepelekwa kwenye maeneo hayo ili kwenda kuhakikisha kwamba sasa tunachukua maji kutoka Mkunya kule Ruvuma, tunachukua Mitema na kuhakikisha kwamba, maeneo yote ya Newala yanapata maji safi na salama na hasa kwa kuzingatia kwamba, Newala iko juu sana, huwezi ukachimba kisima ukapata maji. Kwa hiyo, mradi mkubwa unakwenda kwa Mheshimiwa Mbunge, lakini pamoja na hilo bwawa naomba tuwasiliane ili tuweze kuona cha kufanya.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, matatizo ya maji yaliyoko huko Maswa Mashariki yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Halmashauri ya Itigi na shida kubwa iko kwa wafugaji katika suala zima la kunywesha mifugo yao. Sasa Serikali kwa maana ya Wizara ya Maji iko tayari kukubaliana na mapendekezo ya Halmashauri ya Itigi kwa ajili ya kuchimba malambo tu madogomadogo katika vijiji vyake?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi kabisa ni kwamba, Mheshimiwa Mbunge tuko tayari kushirikiana na halmashauri yake kuhakikisha tunachimba mabwawa madogo madogo kwa ajili ya mifugo. Kwa hiyo, tuendelee kuwasiliana.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pia niishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi yake ya kuwalipa wananchi hawa pale niliposhika Shilingi hapa ndani na wananchi wangu wakawa wamelipwa fedha hizi, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.Kwanza; ningependa kujua kutoka kwa Serikali hususan Waziri; ni lini wananchi hawa watalipwa riba ya fedha walizolipwa za fidia zaidi ya milioni 200 ambazo wanadai hadi sasa na hawajalipwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa bahati nzuri wananchi wa Bukoba Town wana Mbunge mahiri ambaye anaweza akasimamia na wakalipwa madai yao. Serikali inasemaje kwa watu wa maeneo mengine katika maeneo mbalimbali ya nchi hii ambao hawajalipwa fidia zao?Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme fidia inalipwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2001 kupitia Tangazo la Serikali namba 79. Si suala la umahiri wa Mbunge, ni Sheria imewekwa katika utaratibu wa kulipa fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijibu swali lake la kwanza la juu riba. Mheshimiwa Mbunge tarehe 10 Februari, 2017, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Salama BUWASA alileta barua ya kuomba fedha Sh.202, 164,107.75 kwa ajili ya malipo ya nyongeza baada ya malipo ya fidia kuchelewa zaidi ya miezi sita. Malipo hayo yalichelewa kwa muda wa miezi kumi na sita na sasa hivi Serikali tayari inafanya utaratibu wa kupeleka fedha hiyo ili wananchi waweze kulipwa haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maeneo mengine; utekelezaji wa miradi; na nizungumze kwamba Waheshimiwa Wabunge fidia siyo ajenda yetu, ajenda yetu ni miradi ya maji safi na salama; suala la fidia linaingia katika utaratibu wa kawaida wa kisheria, kwamba unapotekeleza mradi ukikutana na mali ya mwananchi Serikali imeweka Sheria kwamba lazima umlipe fidia kabla utatekeleza huo mradi. Kwa hiyo, Sheria hii inatekeleza kwa nchi mzima na tutaendelea kufanya hivyo.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Singida Jimbo la Iramba Magharibi kuna Mradi wa World Bank ambao ulijengwa mwaka 1978 wa matenki ya maji ambayo mpaka leo yamekaa kama sanamu. Naomba Mheshimiwa Waziri aseme ni lini au Serikali ina mkakati gani wa kumalizia mradi huu kwa sababu ni muda mrefu sana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoa maelekezo, tumeandaa bajeti ya mwaka uliopita kwamba katika bajeti hiyo tuhakikishe kwamba tunatekeleza miradi ile ambayo bado haijakamilika; na tunaendelea hivyo na mwaka huu pia tumeandaa bajeti. Kwa hiyo katika halmashauri yake kama kuna miradi ambayo ilikuwa haijakamilika basi fedha katika mpango kazi wao wahakikishe kwamba wanaielekeza kwenda kukamilisha miradi ambayo haijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano anaouzungumzia Mheshimiwa Mbunge nimeukuta Nanyamba ambapo Mheshimiwa Mbunge alinifuata na tukaenda kukaa na halmashauri. Kulikuwa na matenki yamejengwa lakini hayana maji. Sasa hivi Nanyamba tayari wananchi ile fedha ya mwaka jana wameshaitumia vizuri, wameelekeza kwenye miradi ambayo ilikuwa haijakamilika, wananchi wanapata maji. Naomba na Mheshimiwa Mbunge afanye hivyo.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Geita kuna mradi wa maji ambao unafahamika kama LV WATSAN ambao unafadhiliwa na African Development Bank. Ulitakiwa kuwa umekamilika tangu Novemba mwaka wa jana lakini mpaka leo haujakamilika. Nataka kujua mradi huu utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba mradi huo hupo na ni mradi mkubwa unakwenda kwa phases. Una financing tatu; iko financing ya Serikali, watu wa madini wa GGM, lakini na financing pia kutoka lile fungu la Lake Victoria Water and Sanitation Project. Mheshimiwa Mbunge, tunakwenda kwa phases, kwa hiyo, kiasi tumeshakamilika na wananchi wanapata maji kama asilimia 30, lakini tunaendelea, hatimaye tuhakikishe tumekamilisha mradi huo ili wananchi wengi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayofanya. Nina swali kuhusu mradi wa Rwakajunju namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri awaambie akinamama wa Karagwe ni lini mradi wa Rwakajunju utatekelezwa ili kuwatua ndoo kichwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwatulize wananchi wa jimbo la Mheshimiwa Mbunge kwamba Mradi wa Maji wa Rwakajunju unatekelezwa. Mradi wa maji wa Rwakajunju una finacing ya uhakikika kutoka Serikali ya India na tunasubiri sasa hivi Mheshimiwa Waziri wa Fedha asaini mkataba wa fedha. Tayari Wizara tumeshaanza kutafuta Wahandisi Washauri ambao wanahakikisha wanaweka document vizuri. Yule Mhandisi anayefanya usanifu wa mradi huu anakaribia kukamilisha. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuwasiliana, nina imani katika mwaka huu fedha tuliouanza juzi 2017/2018 tutaanza utekelezaji wa Mradi wa Rwakajunju ili tuweze kuwatua wananchi ndoo kichwani.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Manispaa ya Morogoro kumekuwa na tatizo kubwa la maji hasa kwenye mitaa kama mitaa ya Mlima Kola, Lukobe, Foko land, Manyuki na mitaa mingine na kwa kuwa Serikali inafanya vizuri; naishukuru Serikali ya Ufaransa na ya Tanzania kwa kupata fedha hizo Euro milioni 70; lakini napenda kujua mradi huo ni lini utakamilika ili wananchi ambao wamepata matatizo ya maji kwa muda mrefu wapate subira ya kupata maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pli, miradi ya maji katika Mji Mdogo wa Mikumi imechukua muda mrefu kiasi wananchi wa Mji wa Mikumi wana matatizo makubwa ya maji. Je, ni lini miradi hii itakamilika kusudi na wananchi waweze kupata maji safi na salama ya kutosha? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa amesema Morogoro ina matatizo makubwa ya maji. Serikali imetambua hilo na imeweka miradi ya dharura, tunachimba visima vitano na visima viwili tayari vimeshachimbwa eneo la Kola. Visima viwili vinaendelea kuchimbwa eneo la SUA ili kuweza kupunguza tatizo la maji lililopo wakati tunasubiri utekelezaji wa mradi huu mkubwa. Hata Mbunge wa Jimbo Mheshimiwa Aboud, jana alikuwa ofisini nikawa nimepata taarifa hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunaendelea vizuri na mhandisi tuliyemweka na tunatarajia ifikapo mwezi wa 12 atakuwa amemaliza, tutangaze tender. Baada sasa ya kumweka mkandarasi na kusaini mikataba, Mheshimiwa Mbunge tutajua sasa mradi utakamilika lini. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Morogoro kwamba tayari Serikali imeshaanza huo mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mikumi sasa hivi tumekamilisha mradi mkubwa wa maji pale na nimeenda kutembelea na mradi umeanza kutoa maji tayari. Kwa hiyo, wananchi wa Mikumi tayari wanapata maji. Kama kutakuwa na upungufu, basi tutaendelea kuongeza kwa sababu watu wanazidi kuongezeka katika Mji wa Mikumi, lakini tayari mradi ule mkubwa umeshakamilika.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ambayo nimepewa na Mheshimiwa Naibu Waziri kusema kweli sijui Bunda kuna nini hata nashindwa kuelewa. Kwa sababu unapotaja Kijiji cha Karukekere, Mumagunga, Kung’ombe, Ligamba na kama unavyotaja majibu kwenye paper ambayo nimepewa kwa maana ya kujibiwa kama Mbunge, yakaonyesha sehemu kubwa ya miradi inayotajwa sio ya Jimbo lako, hivi Mbunge unajisikiaje!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nafikiri kwamba ni vizuri wakati fulani haya majibu, na nazani hili ni tatizo la Bunda tuna miradi mikubwa iko Bunda na Mabilioni ya hela, viongozi hawafiki pale kuona hela zinaliwa pale hawafiki, sasa naomba kuuliza niache kwa sababu leo ni siku nzuri tunaenda nyumbani tusilete shida huko mbele niseme sasa nimuulize Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuache haya ambayo ameyasema kwa sababu mimi sioni kama yako kwenye maeneo yangu, kuna kilometa nne za mradi wa maji mkubwa kutoka Ziwa Victoria huko Halmashauri jirani ya Butiama, sasa kama ni kilometa nne kuja kwenye maeneo ambayo yana uhaba wa maji ni lini Serikali itachukua mpango wa kuleta yale maji kutoka bomba la Ziwa Victoria kuja Nyamuswa, Bigegu, Tiring’ati na Malambeka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa kuna mradi mkubwa ulikuja wafadhili kutoka SNV wa shilingi milioni 987 kuja Kijiji cha Nyamuswa na mradi ule unaonekana umefanyiwa ubadhirifu mkubwa sana ni lini Serikali itaenda kushughulikia wabadhirifu wa hela hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, miradi tunaitekeleza kihalmashauri, hatutekelezi kijimbo, sasa hii ndiyo maana inawezekana katika programu ya huo mradi ilichukua vijiji vingi vya Jimbo lingine na vijiji vichache vikawa vya Jimbo la Mheshimiwa Getere, lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Getere kwamba utekelezaji unaendelea na mwaka huu tumeweka bajeti, kwa hiyo, tutaendelea ili kuhakikisha kwamba na vijiji vingi vilivyo sehemu ya kwako vinapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, umezungumzia kwamba kuna vijiji kama Nyamuswa ambavyo viko kilometa nne tu kutoka ziwani, ninaomba tushirikiane na Wilaya yako tuangalie kwamba ni kitu gani kitafanyika japo katika swali lako la pili umezungumzia fedha zilizotolewa kutoka kwenye hii programu ya Lake Victoria Water and Sanitation Project na mradi huo mkubwa unaendelea kuzunguka Ziwa letu la Victoria. Kwa hiyo, tutaangalia ni namna gani sasa tutaweza tukaweka mradi mwingine kuupeleka maeneo haya ambayo umeyapendekeza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi tuko pamoja na tutahakikisha wananchi wako wanapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ila napenda nikuambie Mheshimiwa Waziri ni asilimia chini ya 30 tu ya wakazi wa Mji wa Tarime wanaopata maji kutoka kwenye Bwawa la Nyanduruma na ambayo siyo safi na salama. Nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria kuanzia Shirati kupitia Utegi, Ngiri Juu na kufikisha maji Sirali na Tarime, design ilimalizika mwaka 2011, lakini hapa kwenye jibu lako la msingi umesema design review itamalizika mwaka 2017. Lakini tunafahamu kwamba Benki ya Maendeleo ya Ufaransa, (France Development Bank) walikuwa tayari kufadhili mradi huu, ni nini sasa kinasababisha Serikali itafute mfadhili mwingine ili hali Benki ya Maendeleo ya Ufaransa iko tayari kufadhili mradi huu?
Swali la pili, kwa kuwa Mji wa Tarime ndiyo makao makuu ya Wilaya ya Tarime na ina taasisi mbalimbali kama hospitali, magereza, shule na kadhalika na ukosefu wa maji husababisha mlipuko wa magonjwa, ni lini sasa Serikali itachimba visima hasa kwenye taasisi hizi kama suluhisho la muda mfupi kwa kata zote za Mji wa Tarime?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa review ya mradi bado haijakamilika, hili ni suala la kitaalam unaweza ukalipata juu juu, lakini sisi tunasema review inakamilika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili amedai kwamba anataarifa sijui umezipata wapi, mimi ninafikiri taarifa unazipata za uhakika kutoka kwa sisi wenye Wizara, usipate taarifa za kutoka mtaani. Taarifa za kwetu za ndani ni kwamba bado hatujapata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa huo mradi na kwa sababu hatujui ni kiasi gani kinahitajika, kwa ajili ya huo mradi. Kwa hiyo, tukishajua kiasi gani kitahitajika ndio sasa tutachukua hatua za kutafuta fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kweli kwamba Tarime ni Makao Makuu ya Wilaya, lakini kwa kwa hatua za dharura Mheshimiwa Catherine ni kwamba tumechimba kisima kimoja tayari, tumekarabati visima viwili, tumeongeza mtandao wa kilometa 30 wa mabomba na ndiyo maana sasa tunaingia mkataba kwa ajili ya kuboresha chanzo cha Nyandurumo kama nilivyokuwa nimezungumza katika swali langu la msingi, lakini pia tutaendelea na kwa sababu tumetenga fedha niombe kwamba mwambie Mkurugenzi wako, aendelee kuweka mapendekezo kwa ajili ya kuongeza visima vingine ili maeneo ya mji, hospitali, taasisi za shule, ziweze kupata maji bila matatizo yoyote.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Naishukuru Serikali kwa namna ambavyo imeonesha nia nzuri ya kutatua tatizo kubwa la maji lililoko katika Mji wa Makambako. Swali la kwanza, kwa sababu Serikali imetenga fedha hizo dola ambazo amezitaja hapo, dola milioni 38, nataka kujua ni lini sasa mradi huu utaanza ili wananchi wa Makambako waepukane na tatizo kubwa wanalopata Makambako na hata wawekezaji wa viwanda inashindikana kwa sababu maji hatuna?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu mradi huu mdogo ambao kama alivyosema tenda imetangazwa ambao ni kwa ajili ya bwawa dogo la Makambako, nilipofuatilia Mkoani wanasema tayari iko Wizarani lakini Wizara bado haijarudisha kule ili mkandarasi aanze kazi. Je, ni lini sasa mkandarasi huyu ataanza kazi kwa mradi huu kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza anauliza ni lini huu mradi mkubwa wa dola milioni 38 unatarajiwa kuanza. Kwa faida ya Wabunge wengine ambao watafaidika na mradi huu wa dola milioni 500 za mkopo nafuu kutoka Serikali ya India, niseme kwa sasa hatua inayoendelea tayari Hazina imekamilisha taratibu za kusaini makubaliano ya fedha kwa maana ya financial agreement. Pia Wizara inaendelea sasa kufanya manunuzi ya ma-consultant watakaokamilisha usanifu na makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi huu. Mheshimiwa Deo Sanga baada ya kukamilisha taratibu hizi basi tutaendelea na kutangaza tenda na kuhakikisha kwamba mradi huu unaanza kwenye mwaka wa fedha wa 2017/2018. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu tenda inayoendelea ambayo inafanywa na Halmashauri ya Mheshimiwa Deo Sanga, niseme kwamba kwa vile ametoa taarifa kwamba tayari wameshaleta hizo nyaraka Wizara ya Maji, naomba nifuatilie kama kweli zimeshaletwa na tusimamie ili waweze kurudisha haraka ili shughuli iendelee. Mheshimiwa Sanga naomba tuwasiliane kwa hili.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza na namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la upembuzi yakinifu limekuwa likijibiwa hata Bunge la Kumi kwenye swali hili la msingi na kwa kuwa hata majibu ya msingi ya swali hili yameonesha hakuna hata kiwango cha fedha kilichotajwa waziwazi kutengwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018, hali inayopelekea wasiwasi wa utekelezaji wa kazi hii. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana na Mbunge Mheshimiwa Azza kutembelea eneo hili la Masengwa ili asikie kilio cha wananchi hawa na ikizingatiwa Mkoa huu wa Shinyanga umekuwa ukiendelea kunyemelewa na janga la ukame?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa matatizo ya maji ya Halmashauri ya Shinyanga yanafanana kabisa na matatizo ya maji ya Halmashauri ya Chalinze yanayotokana na kusuasua kwa mradi wa Chalinze Wami Awamu ya Tatu na kwa kuwa mradi huu pia ulitembelewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu miezi miwili iliyopita na kutoa maelekezo kwa mkandarasi kukamilisha kazi hii kwa siku 100. Je, mpaka sasa Wizara imefikia hatua gani katika ufuatiliaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu ili tatizo la maji linaloikumba Halmashauri ya Chalinze hususani Mji wa Chalinze, Ubena na maeneo mengine lipate majibu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Subira kwamba utaratibu wa utekelezaji wa miradi huwa unaanza na hatua ya awali ambao kwa lugha ya kigeni tunaita basic concept baada ya hapo tunakwenda kwenye feasibility study. Kumekuwa na lugha ya kiujumla ambayo inafahamika kwa wengi (usanifu wa awali). Kwa hiyo, hiyo iliyokuwa inatajwa mwanzoni ilikuwa ni kwa ajili ya basic concept sasa ni kweli tunaenda kwenye feasibility study ambao ni usanifu wa awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia amesema hajaona fedha iliyotengwa Mheshimiwa Mbunge leo ndiyo tunaanza kusoma bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka 2017/2018. Asingeweza kuiona kabla ya hapo lakini kwa leo baada ya kuanza kusoma bajeti nina uhakika ataona tunaelekea wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa ameomba pia tuambatane na Mheshimiwa Azza, ni kazi ya mimi Naibu Waziri kuhakikisha kwamba natembelea Majimbo na Halmashauri zote kujionea utekelezaji wa miradi ya maji safi na salama pamoja na miradi ya umwagiliaji. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi hata huko Shinyanga nitafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa amezungumzia utekelezaji wa mradi wa Chalinze, kwanza nimwambie kwamba sasa hivi mkandarasi ana kasi kubwa ya utekelezaji wa mradi wa Chalinze. Mheshimiwa Waziri pamoja na mimi tunapata taarifa kila siku na taarifa ya jana ni kwamba mkandarasi amefikisha asilimia 44.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembelea pale na wakati ule tulitamka siku 100 za kumpima mkandarasi, tunakupa siku 100 ili tuone kama utaongeza speed basi tutaendelea na wewe. Sasa anaendelea kuthibitisha kabla ya hizo siku 100 kwamba ameongeza kasi. Kama ataendelea hivyo, tutaendelea naye kuhakikisha kwamba mradi ule unakamilika.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa wanannchi wa Jimbo la Manyoni Mashariki wanategemea maji ya mabwawa na visima na kwa muda murefu sana wamekuwa wakitaabika na kero kubwa ya ukosefu ya maji safi na salama. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Jimbo la Manyoni Mashariki linapata maji safi na salama kwa uhakika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumekamilisha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa program ya maji hapa nchini na tumeanza awamu ya pili Julai mwaka huu 2017. Tumeweka utaratibu wa kutenga fedha kwa kila Halmashauri ili zenyewe zihakikishe kwamba zinabuni na kutekeleza miradi ya maji. Zaidi ya hapo, kuna bwawa kubwa tumejenga katika Halmashauri ya Manyoni Mashariki ambalo lile litafanya kazi mbili, moja ni umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga, lakini pili litasaidia katika maji ya matumizi ya majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wala asiwe na wasiwasi, tunaendelea na utelekezaji kuhakikisha kwamba wananchi wa Manyoni Mashariki wanapata maji. Nimshukuru kwa sababu yeye ni mama wananchi wake wa Singida anawapenda ndiyo maana anawatetea. (Makofi)
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Waziri Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi takribani wiki mbili inakwenda ya tatu sasa Shinyanga, Kahama maji hayatoki. Wale watu wanatumia maji ya kununua hakuna maji kabisa. Tatizo inasemekana kwamba hamjalipa bili ya umeme kama Mheshimiwa Rais alivyoagiza. Mheshimiwa Waziri wale watu wanapata shida, hivi ni lini mtarudisha yale maji ili watu waendelee ku-enjoy tunu za Taifa hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wiki mbili zilizopita Mamlaka nyingi za maji zimekumbwa na tatizo la kukatiwa umeme hivyo kufanya mitambo ya kuzalisha maji isifanye kazi, hii ni kwa Shinyanga pamoja na maeneo mengine pia. Kutokana na tatizo hilo, tarehe 8 Wizara ya Maji, Hazina na Mkurugenzi wa TANESCO walikaa kikao na kuna makubaliano ambayo yamefikiwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya muda mfupi suala hili litatuliwa ili liwe na ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini napenda Mheshimiwa Mbunge ajue kwamba ni kweli kabisa kwamba Mamlaka zimekuwa hazilipi bili za umeme na kama Mamlaka hazilipi bili za umeme TANESCO itakufa. Kwa hiyo, tumeweka utaratibu kwamba tuhakikishe tunalipa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamekuwa na nia nzuri kabisa ya kuwatetea wananchi wao, wengine wanasema kwamba bili ni kubwa na kadhalika lakini bila kuweka bili ya kiwango ambacho kitawezesha hizi Mamlaka ziweze kujiendesha wenyewe tatizo hili tutaendelea kuwa nalo. Kwa hiyo, naomba sana EWURA wanapopita kufanya hesabu za maji tuwe waangalifu tunapojaribu kuziingilia zile kwa sababu zinatusababisha tufike kwenye hii hali ambayo tumefika.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa suala la lililopo kule Masengwa linafafanana kabisa na bwawa ambalo Serikali imetuahidi katika Kata ya Mnazi na Kivingo kule Lushoto. Je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha kuanza mradi huo wa uchimbaji mabwawa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza eneo la Lushoto ni zuri sana, ni green, lina mvua za kutosha na linafaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Sasa hivi Wizara yetu imepata fedha kutoka Serikali ya Japan na inashirikiana na wataalam wa Serikali ya Japan kupitia mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba unaainisha maeneo yote yaliyotambuliwa kwa kilimo cha umwagiliaji ili uweze kuweka mkakati na kuweka mbinu kama nilivyozungumza kwenye swali moja la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika huo mpango ambao tunatarajia ukamilike mwaka 2018 maeneo yote yataainishwa na matatizo mengi ambayo yamejitokeza yataangaliwa ili tuhakikishe tunajenga miundombinu ambayo itawezesha kilimo cha umwagiliaji. Nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kwamba katika kazi hii inayoendelea tutahakikisha kwamba tunafika mpaka Lushoto.
MHE. GIBSON B. OLE-MEISEYEKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matokeo ya utekelezaji kazi wa Wakala hawa wa Serikali imekuwa tofauti kabisa na makusudio ya uundwaji wa sheria hizi, nikiwa na maana kwamba vyombo hivi vinaisababishia Halmashauri na Taasisi za Serikali usumbufu mkubwa wa ucheleweshaji wa utengenezaji wa mitambo lakini pia gharama kubwa za utengenezaji wa mitambo hiyo ukilinganisha na bei zilizoko kwenye masoko ya kawaida. Kwa mfano, TEMESA haina kabisa karakana na wataalam wa kutengeneza mitambo yetu hii, kwa maana hiyo Wakala hawa wamekuwa kama kupe wa kufyonza fedha za Serikali badala ya kuisaidia Serikali kuweza kutengeneza miradi kwa gharama nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliuliza kwenye swali langu la msingi kwa nini isifanyiwe marekebisho ya utekelezaji wao wa kazi ili sasa iweze kuleta tija na maendeleo ya haraka katika maeneo yetu badala ya kuweka vyombo ambavyo vinasababisha gharama kubwa katika utekelezaji wake wa kazi. Kwa hiyo, swali langu linabaki pale pale, kwa nini Serikali isibadilishe utaratibu wa utekelezaji kazi wa mamlaka hizi ili kuweza kuleta tija na ku-save fedha badala ya kusababisha gharama kubwa mara mbili, tatu ya gharama sahihi zilizoko mitaani? Kwa nini utaratibu wa utekelezaji wake wa kazi usibadilishwe? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge nikuambie mimi nimeitumia TEMESA, nilikuwa Meneja wa TANROADS na nilikuwa Wizara ya Ujenzi, kwa hiyo TEMESA naielewa vizuri kwa undani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, amesema kwamba TEMESA imekuwa na usumbufu, gharama kubwa na ucheleweshaji, hayo anayoyazungumza ni kweli. Ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema kwamba TEMESA sasa hivi uongozi umebadilishwa na karakana zilizopo zinaboreshwa kwa kuwekewa vifaa vilivyo bora. TEMESA ilikuwa na shida ya namna ya kutumia sheria mliyoiunda ninyi Wabunge ya PPRA, sasa hivi wamewekwa wataalam ambao wataitumia ile sheria vizuri. Sheria ni nzuri sana lakini kulikuwa na wafanyakazi ambao sio waadilifu na Serikali hii ya Awamu ya Tano imechukua hatua ya kuhakikisha kwamba inawaondoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wazo lake la kusema chombo hiki kwa sasa kibadilishwe, ukianza kuunda kingine leo utaanza tena kuwafundisha mpaka wafike huko watakakofika. Sasa hivi hawa tayari wameshaiva, tunahakikisha wanaboreshwa ili TEMESA iwe na ufanisi mzuri kuliko garage nyingine yoyote ya kawaida. Naomba atupe muda na tushirikiane tuendelee kutekeleza suala hili.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Waziri yanaonesha kwamba watajenga mtaro mkubwa Mbezi Samaki lakini kuna eneo lingine ambalo ni hatarishi na sasa hivi kutokana na mvua zilivyonyesha liko kwenye hali mbaya sana na barabara inaweza ikakatika, ni eneo la Afrikana - Salasala - Kinzudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili tumeshafanya ziara mara kadhaa na Mkurugenzi wa TANROADS Mkoa tukashauriana kwamba wauweke mtaro mkubwa, lakini vilevile waweke utaratibu wa kujenga hata mita mia za lami kwenda mbele kwa sababu ile barabara inahudumiwa na Halmashauri ili kuweka mapokeo makubwa ya maji vilevile kuokoa ile barabara. Sasa napenda Mheshimiwa Naibu Waziri anijibu mahsusi kwa eneo la Afrikana - Salasala - Kinzudi ambapo sasa hivi barabara imechimbika sana?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni mwaka wa
tatu mfululizo Manispaa ya Kinondoni haijapata fedha za Mfuko wa Barabara kutokana na makosa yaliyofanywa na ma-engineer wetu ambao walijenga barabara chini ya kiwango. Matokeo yake ni kwamba wananchi wa Kinondoni ikiwemo Jimbo la Kawe wanaathirika kwa sababu barabara ziko katika hali mbaya sana. Hawa ma-engineer wameshapewa adhabu zao, wengine wamesimamishwa kazi, wengine wamehamishwa vituo. Nataka Waziri atuambie ni lini fedha husika za miaka mitatu zitakuwa released ili maboresho ya barabara za Kinondoni yaweze kufanyika na kupunguza kero ya wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO): Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo la tafsiri ya mradi, nini maana ya mradi? Mradi unaanza na basic concept, feasibility study, detail design, ujenzi lakini mradi pia una operation na wakati wa operation ni operation and research. Nikiri kwamba Mheshimiwa Mbunge aliyoyasema ni kweli, ile barabara na mimi naitumia. Kwanza yeye ni Mbunge wangu maana nakaa Kinondoni. Tangi Bovu, Afrikana, Kilongowima na maeneo mengine maji yanapita pale lakini kipindi cha operation and research tayari mpaka sasa hivi Wizara imeshatambua maeneo hayo na inaanza kuingia mikataba. Kwa mfano, eneo la Tangi Bovu mkandarasi amepatikana kwa maana sasa ya kuboresha na kupanua ile sehemu ya kupitisha maji katika eneo la barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo lingine kwamba TANROADS inashughulikia eneo la hifadhi yake na kwa eneo lile hifadhi ni mita 80, 40 kila upande kutoka katikati ya barabara, nje ya hapo ni eneo la Halmashauri. Kipindi cha mvua kutokana na mabadiliko haya, mimi huwa nasema ni mabadiliko ya binadamu, storm water yanapotembea yanakuja na takataka nyingi sana zinaingia kwenye yale makalavati zinaziba, matokeo yake sasa maji hayapiti katika dizaini iliyotakiwa yanapita juu ya barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hoja yake pia amezungumzia kuhusu street light, nazo katika hiki kipindi cha operation and research need imeshaonekana. Kwa hiyo, Serikali italifanyia kazi ili wananchi wanaotembea usiku waweze kupata huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo hili suala ambalo mwenyewe amekiri kwamba kulikuwa na ubadhirifu na uzembe ama wa wahandisi ama wa watu gani kuhusiana na ujenzi wa barabara, wakajenga barabara ambazo haziko katika standard inayotakiwa. Ni kweli, kwani yeye Mheshimiwa Mbunge anapenda? Mtu ambaye anafanya kitu ambacho hakiko kwenye standard inayotakiwa lazima achukuliwe hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala kwamba fedha za Mfuko wa Barabara hazijaja mfululizo kwa miaka mitatu kwangu ni geni. Naomba nilichukue, nitaliwasilisha kwa wahusika ili waweze kuliangalia.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yanayotia moyo. Kwa kuwa mradi wa maji wa Ziwa Victoria utachukua muda mrefu ili kuwezesha Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu kupata maji, je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuwapatia maji ya uhakika wananchi wa Mkoa wa Simiyu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mji wa Maswa sasa hivi una matatizo makubwa ya maji, wanakunywa maji machafu na kuna mradi wa chujio ambao ni wa muda mrefu. Je, ni lini Serikali itakamilisha ili wananchi wa Maswa wapate maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza amesema kwa sababu mradi huu utachukua muda mrefu, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha sasa wananchi wanapata huduma ya maji? Kupitia mpango wa uendelezaji wa hii sekta ya maji, tayari tumeshatekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Simiyu na kuna maeneo ambayo kwa mfano, Nyangili, Mwamanyili, Bukapile, Bulima, Lamadi, Lukugu, Manara, kuna ambayo imekamilika na mingine inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia juzi tumepitisha bajeti na katika Mkoa wa Simiyu tumeweka shilingi bilioni tisa ili Halmashauri ziendelee kutekeleza miradi ya maji kuhakikisha kwamba wakati tunasubiri ule mradi mkubwa, lakini wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji. Vilevile Bariadi kuna huu mradi wa visima vya Misri tumechimba visima pale na nimeenda mwenyewe Simiyu maji yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Maswa, ni kweli ukiangalia ule mradi hata utakapoanza eneo la mwisho utakwenda Maswa. Kutokana na hilo, hata jana tulikuwa na kikao, tayari tumeagiza KASHWASA washirikiane na Halmashauri ya Maswa ili tuweze kuona uwezekano wa kutoa maji kutoka bomba lile pale Shinyanga kupeleka maji kwa muda pale Maswa wakati tunasubiri mradi mkubwa. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa upendeleo wa kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Songwe lina uhaba mkubwa sana wa maji lakini niongelee Kata moja inaitwa Totowe ambapo mimi mwenyewe kwa juhudi za Mbunge niliomba mradi wa Mheshimiwa Sabodo nikachimba kisima kikubwa sana na kisima hicho mpaka ninavyosema hivi bomba hilo linatoa maji kutoka mwaka 2012 mpaka leo yanatiririka na yamesambaa pale kijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuomba pale Halmashauri angalau watupe fedha hata shilingi milioni 50 tuweze kujenga tanki la kutunzia maji yale angalau yaweze kusambaa vizuri kwa kujenga mabomba kwa wananchi wa Totowe na maeneo ya Namambu. Je, Serikali inanisaidiaje mimi kama Mbunge nimefanya juhudi kutafuta maji halafu maji yanatiririka bila kujengewa tanki ili angalau wanipe fedha nikajenge tanki maji yaweze kuenea pale Totowe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mweyekiti, alichokisema ni kweli. Baada ya kumaliza Bunge mwezi wa Julai, nitamwomba Mheshimiwa Waziri nianze na Mkoa wa Songwe kwa sababu Halmashauri za Mkoa wa Songwe katika suala la utekelezaji wa miradi ya maji hawakufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Katibu Mkuu anaongea nao kule Morogoro ili kuona hizi Halmashauri ambazo haziku-perform vizuri zina matatizo gani wakati tulitoa maelekezo baada ya bajeti wanatakiwa kufanya manunuzi, lakini hawakufanya manunuzi kabisa. Nitakapokuwa nimekwenda tutaliangalia hili na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuweka utaratibu wa kwenda haraka wananchi wapate maji.(Makofi)
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba kumuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa fidia kamili kwa wale waliohusishwa na kuchukuliwa maeneo yao haijalipwa kama alivyozungumza Mheshimiwa Waziri kwamba kuna bakaa ya shilingi bilioni mbili ambayo wametenga kwa ajili ya kulipwa; na kwa kuwa, ninayo taarifa kwamba DAWASCO wameshapeleka mabango ili yawekwe kwenye maeneo yote ya sehemu hizo kuzuia wananchi wasifanye shughuli zozote za maendeleo, kwa maana kwamba tayari wameshakabidhiwa maeneo hayo.
Je, sasa Serikali iko tayari kusitisha uwekaji wa mabango hayo hadi wananchi watakapolipwa fidia yao kamili? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa maeneo ya Bwakila Chini, Kiganila na Magogoni katika kata hii ya Serembala imekumbwa na mafuriko makubwa sana na wananchi wako kwenye maji kwa wiki tatu sasa.
Je, Serikali itapeleka msaada wa chakula na madawa ya dharura? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ni kweli tayari tumeshalipa zaidi ya shilingi bilioni saba katika hilo eneo na kilichojitokeza ni kwamba baada ya DAWASCO kulipa ile fedha yale maeneo kwa taarifa ambazo tulizipata wananchi walianza kuwauzia watu maeneo yale ambao hawajui kwamba maeneo yale yameshalipwa fidia. Baada ya taarifa hiyo kupatikana, Mkurugenzi wa Halmashauri yako Mheshimiwa Mbunge ndiye aliyeamua kuweka vibao ili kuweza kuwapa tahadhari wananchi kwamba lile eneo wasiuziwe kwa sababu lilishalipwa fidia vinginevyo tutapata matatizo zaidi katika Serikali. Kwa hiyo mabao yale niseme kwamba hayajawekwa na DAWASCO yamewekwa na Mkurugenzi wa Halmashauri yako.
Swala la mafuriko, kwanza nikupe pole kweli nami ninayo taarifa kwamba kuna baadhi ya vijiji ambavyo vimeingiliwa na maji, kwa vile taarifa hii uliyoitoa ya mafuriko na kuomba msaada Serikali imesikia na iko Idara husika inayohusika na jinsi ya kusaidia maeneo ya maafa basi nafikiri naomba ulifikishe huko ili liweze kushughulikiwa.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nishukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini nataka kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali pia ilitenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kufanya usanifu na ushauri kwa mradi huu wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwa miji hiyo mitatu. Mwaka huu pia wameweka kama shilingi bilioni mbili kama alivyosema. Je, Serikali inatuhakikishiaje sisi wananchi wa Maswa Magharibi, kwamba kazi hii sasa itafanyika mwaka huu na mradi uweze kuanza mwakani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa miradi mingi ya visima vifupi alivyovitaja Mheshimiwa Waziri inakauka wakati wakiangazi kikali, mwezi wa nane, wa tisa na wa kumi. Je, Serikali haioni sasa kutupatia maji kutoka vyanzo vya kudumu kama mabwawa makubwa pamoja na miradi kama hii ya kutoa maji Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Ndaki kwa sababu kwanza ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji, lakini pia amekuwa ni Mheshimiwa ambaye tunaongea naye sana, anakuja ofisini kufuatilia suala la maji katika jimbo lake na nilishawahi kutembelea katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la kwanza ni kwamba katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tumetenga shilingi bilioni moja na mwaka huu haujaisha, hela hiyo ndio iliyotufanya tuanze kufanya usanifu wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda kupeleka Malampaka, na kuna kazi kubwa ambayo imeshafanyika, na ni matarajio yetu kwamba baada ya kukamilisha uzanifu tunaanza sasa kutangaza, na fedha hiyo tutaangalia utaratibu ili iweze kuanza kutumika katika mradi huu tukishapata wakandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya utaratibu, kama nilivyokwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeona tuwatumie KASHWASA. Wale KASHWASA wana utaalamu mkubwa wameshatekeleza mradi mkubwa, kwa hiyo kutakuwa na wepesi kidogo kwa kushirikiana na halmashauri yako tuhakikishe kwamba mradi huu unatekelezwa kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la visima vifupi, ni kweli kabisa maeneo mengi tumechimba visima vifupi lakini hivi vinapata maji kipindi cha mvua na muda kidogo wa miezi michache baada ya mvua. Kutokana na hilo basi sasa hivi tunafanya utaratibu, kama ulivyopendekeza mwenyewe, kuangalia sehemu inayofaa kuchimba mabwawa tunahakikisha kwa kushirikiana na halmashauri tunasanifu na tunachimba mabwawa yaweze kutunza maji kama ambavyo bwawa lile la Maswa linatunza maji na kulisha vijiji 11 pamoja na mji wa Maswa, lakini pia na kutumia vyanzo vya kudumu kama bomba la KASHWASA kama tunavyotaka kufanya sasa hivi ili kuachana na visima vifupi.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka kufikia hatua hii kuna juhudi kubwa ambazo zimefanywa na ninapenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watu wa Tume ya Umwagiliaji kuweza kuhakikisha kwamba tunafikia hatua hii. Lakini kumekuwa na tabia ya miradi ambayo tayari inakubaliwa na wafadhili lakini hatua za kuchukua mpaka kupata hiyo miradi inakuwa ni ya muda mrefu sana mfano wa mradi huu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali. Kwa hiyo, kwa mfano mradi huu toka mwaka 2015 tumepewa haya masharti na sasa hivi ndiyo kwanza tunakwenda kwenye hatua za manunuzi ya mtalaamu mwelekezi.
Sasa Waziri anaweza kutufahamisha hatua hizi za kukamilisha detailed design na hii feasibility study zitakamilika lini ili kuweza kuona mradi wenyewe utaanza kutekelezwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kwa upande wa Serikali ni hatua gani zitachukuliwa katika kuhakikisha kwamba miradi ambayo tunakuwa tumeahidiwa na imeshakubalika tunapunguza muda ambao tunauchukua kuikamilisha ili hii miradi isiende nchi nyingine? Kwa sababu sasa hivi miradi mingi inaenda Kenya na Mozambique kwa sababu ya kuchelewa kwetu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameonesha concern yake kwamba wafadhili wanatoa fedha lakini pengine taratibu zinachukua muda mrefu. Nikuhakikishie Mheshimiwa Kabwe kwamba ni utaratibu wa kawaida, kunapokuwa na mradi ni lazima ufanye feasibility study ili uweze kuonesha economic viability ya mradi ule na huwezi ku-rush, lazima uende uweze kupata taarifa za uhakika zinazotakiwa. Baada ya hapo unaingia kwenye hatua nyingine sasa ya detailed design. Information hii tunayoifanya Mheshimiwa Mbunge kama haikukaa vizuri haiwezi kupitishwa kule tunakopeleka. Kwa hiyo, tunachokifanya ni utaratibu wa kawaida kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, Serikali inaitaka hiyo fedha, haiwezi kuiacha na ndiyo maana Hazina wanaendelea kufanya mawasiliano na hii Falme ya Kuwait ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kututunzia hiyo fedha na taarifa tayari zipo. Sasa hivi tunafanya manunuzi ya kumpata mtaalamu mshauri na huyo ndiye atakaye-define, kwa sababu tunapoweka ile proposal ya kwa wale ma-consultant ndipo tunawapa muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kutokana na complexity ya ile site tunaweza tukasema mfanye kwa miezi sita wakasema haitawezekana tukafanye miezi nane kulingana na hali yenyewe ya eneo wanalofanyia kazi. Hatuwezi kutoa muda kwa sasa, ngoja kwanza tusaini mikataba ya consultant ambayo itaonyesha period watakayotumia na wao ndio watakaotushauri muda tutakaouanza suala la ujenzi; baada ya hapo Mheshimiwa Mbunge tutakupa taarifa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Huu mradi wa umwagiliaji wa Mto Luiche umefanana sana na mradi wa umwagiliaji wa Bonde la Titye na Bonde la Rungwe Mpya. Sasa ningependa kujua, miradi yote hii miwili kwa kweli inasuasua sana, imeshaanza lakini uendelezaji wake wa kujenga mifereji umekwama sana. Nilitaka kujua ni lini sasa Wizara hii itaangalia scheme hizo mbili ambazo zimeshaanza kufanya kazi lakini shida imekuwa ni mifereji ya kupeleka maji kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Nsanzugwanko kuhusiana na miradi miwili kwenye jimbo lake ambayo anadai kwamba ilishaanza kufanyiwa kazi lakini kuna mambo ambayo hayajakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba katika ziara nilizozifanya kwenye maeneo mengi ya umwagiliaji ni kweli kabisa hoja ya Mheshimiwa Nsanzugwanko, kwamba unakuta miradi kwenye vyanzo yale mabanio yameshajengwa, mifereji mikubwa imejengwa lakini midogo ya kusambaza maji kupeleka kwenye mashamba bado. Hata hivyo kuna miradi mingine ambayo imesanifiwa vizuri na imejengwa vyanzo vya maji kutokana na uharibifu wa mazingira vimekauka na ile miradi haifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndio maana sasa Serikali ya Japan imetusaidia fedha na mshauri ameanza kufanya kazi, ili kupitia miradi yote hii tuweze kubaini changamoto na aweze kuainisha zile hekta 1,000,000 tulizoahidi kuzijenga katika hiki kipindi cha miaka mitano. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba timu iliyopo itafika mpaka kwako ili kubaini changamoto gani imefanya hiyo miradi isikamilike, kuna shida gani baada ya hapo tunaweka fedha kuhakikisha tunakamilisha ili wananchi waweze kulima na tuwe na uhakika wa chakula.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serilkali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imetenga shilingi milioni 368.5 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya maji katika vijiji vya Mkuyuni na Madam. Na kwa kuwa mwaka wa fedha 2016/2017 umebaki mwezi mmoja tu kumalizika, lakini mpaka sasa pesa hizi hazijafika; na kwa kuwa bajeti ya maji kwa ajili ya Morogoro imepunguzwa kutoka shilingi bilioni 4.2 ya mwaka jana mwaka huu imekuwa ni shilingi bilioni 1.5.
Je, Serikali inanipa commitment gani ya kuleta hela hizi shilingi milioni 368.5 kabla ya mwaka wa fedha uliobaki mwezi mmoja kuisha?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika mpango wa muda wa kati, Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kupeleka maji katika Vijiji vya Lolole, Madam, Mwalazi, Kibuko na kitongoji cha Misala katika Kijiji cha Mkuyuni. Na kwa kuwa huu mradi wenyewe kwamba…
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna mradi wa maji katika kijiji cha Kibwaya ambao unakamilika muda si mrefu, je, Serikali badala ya kutafuta chanzo kingine cha maji, kwa nini isiongeze pesa katika mradi huu ili kupeleka maji katika vijiji hivi ambavyo nimevitaja vya Lolole, Misala, Madam na Kibuko?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli, mwaka huu wa fedha tulionao tulitenga zaidi ya shilingi bilioni 4 na kwamba mwaka unaokuja fedha hiyo imepungau kidogo. Lakini ni kwamba hivi sasa tunavyoongea tayari tumempatia shilingi milioni 976 na kwamba fedha hivyo wiki ijayo itatumwa kwa ajili ya kwenda kuendelea na utekelezaji wa miradi. Kutenga fedha kidogo ni kwa sababu wakati tunatenga shilingi bilioni nne kulikuwa na miradi inayoendelea na baadhi imekamilika. Ndio maana mwaka huu tumepunguza kidogo kwa sababu ya miradi iliyopo sasa ambayo imeelekea kukamilika haitakuwa na thamani kubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, lakini pili kuhusu usanifu, tumetenga fedha kwa ajili ya usanifu wa miradi katika kijiji ambacho kinahitaji kupata maji, ameshauri kwamba tutumie chanzo kilichopo, tunaweka consultant, consultant ndiye atakayebainisha kama tutumie chanzo hicho au kingine kitakachokuwa kimepatikana.
Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafanyia kazi kuhakikisha maeneo yake yote yanapata maji safi na salama. Na bahati nzuri nilishatembelea kwake na tulienda kuzindua miradi ambayo tayari mingine imeshakamilika. Utekelezaji utaendelea na katika Jimbo lake Fulwe itapata maji ya kutoka Chalinze mara baada ya mradi wa Chalinze kukamilika.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni ukweli usiopingika kwamba swala la changamoto ya maji ni tatizo kubwa nchini.
Je Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuchukua ushauri kwamba ili kutatua tatizo hili tuweke utaratibu wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi kwa mpango wa PPP ili kuondoa suala la changamoto ya maji nchi?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuchukua ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu sasa umefika ili kupata thamani ya fedha katika miradi yetu ya maendeleo ya maji kuhakikisha kwamba mnaanzisha kitengo cha ufuatiliaji pale Wizarani ili msitoe tu fedha lakini fedha zile ziwe zinamaana katika miradi yetu mbalimbali katika Halmashauri zetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NAUMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ushauri wake kwanza ni mzuri kwamba kuna haja Serikali kuangalia utekelezaji wa miradi na uhusishe sekta binafsi kupitia mpango wa PPP. Kweli hilo suala ni zuri lakini Waheshimiwa Wabunge na naona wengi wanazungumza sana hili suala la PPP. Suala hili tumeshalifuatilia na tumelijadili sana, lina changamoto zake tumefanikiwa kwenye Daraja hili la Kigamboni kwa sababu tumetumia taasisi ya ndani lakini unapokuja kutumia taasisi ya nje repayment program ndio inaleta shida sana kwenye hii miradi ya PPP. Usiopoangalia unaweza ukajikuta kwamba nchi unaipeleka pabaya kwa sababu pia na sisi kama Serikali tunatakiwa kuweka viwango ambavyo mwananchi atavimudu. Unaweza ukaweka viwango vya kulipa wakati wa matumizi ya hiyo huduma ikawa ni kubwa mno wananchi wasiweze ikatuletea shida lakini tunalipokea hili na nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kitengo cha ufuatiliaji wa miradi Mheshimiwa Mbunge nakushukuru sana na kweli kitengo hiki tumeanza kukiunda na iko mifano, nilitembelea Handeni nikaunda tume imefanya kazi nzuri imebaini mapungufu mengi sana katika utekelezaji wa ile miradi. Pungufu moja wapo ikiwa ni kwamba tumekosa kitengo ambacho kinasimamia moja kwa moja utekelezaji wa miradi, matokeo yake sasa hii hela hatupati ile value for money. Kwa hiyo, nikushukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tayali Wizara inalifanyia kazi ili usimamizi wa miradi uweze kuwa mzuri zaidi.
MHE. LAZARO S. NYALANDU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na kwa kweli Serikali nzima, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa wanavyoshughulikia suala zima la maji katika maeneo ya vijiji tunavyotoka. Nawashukuru sana kwa niaba ya wananchi wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nitoe ombi la pekee, wananchi wa Tarafa ya Mtinko na Mji Mdogo wa Mtinko ambao ni mji unaokuwa kwa kasi sana na una watu wengi. Mfumo wao wa maji ulitegemea kuwepo na pampu iliyoharibika na hapa tunavyozungumza kuna dharura kubwa sana ya maji katika Mji huu Mdogo wa Mtinko. Naomba kwa kadri inavyowezekana Serikali iangalie uwezekano wa haraka wa kuweza kusaidia tatizo hili la Mtinko. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, ameipongeza Serikali kwa kutekeleza miradi ya maji hapa nchini, Mheshimiwa Nyalandu nakushukuru sana lakini pia na mimi nakupongeza wewe kwa sababu juhudi kubwa umeifanya katika Jimbo lako. Pamoja na Serikali kuwa na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji lakini wewe mwenyewe binafsi umekuwa unawasiliana na wafadhili ndiyo maana jimbo lako limefikia katika hatua hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu ombi lako la pumpu tunalichukua na nakuomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane leo leo, tushirikiane pamoja na Mkurugenzi hili ni tatizo dogo ili tuhakikishe pumpu hii inapatikana kwa haraka ili wananchi wa Mtinko wapate maji.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali. Kwa kutambua na kukiri umuhimu wa mradi huu, naomba nipatiwe majibu; lini mradi huu utakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba commitment ya Serikali kwamba hiyo 2018/2019 hakika pesa itatengwa kwenye bajeti.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na swali la Mheshimiwa Mbunge kwamba lini utakamilika, mradi huu kujua ni lini utakamilika ni baada ya kukamilisha usanifu na kuingia mikataba ndipo tarehe itapangwa, kulingana na scope ya kazi itakayojitokeza ndiyo tutajua ni lini mradi utakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni commitment. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu iko commited kuhakikisha kwamba inanyanyua kilimo cha umwagiliaji ili tuweze kuondokana na njaa. Na Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa mitano ambayo inazalisha chakula kwa wingi, kwa hiyo kwa mikoa hii Serikali iko commited kuhakikisha kwamba tunaendeleza kilimo cha umwagiliaji; tutahakikisha kwamba bajeti hii tunaitenga.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Skimu ya Umwagiliaji ya Ulumi inafanana sana na Skimu ya Umwagiliaji ya Mwakijembe. Mwaka 2010 Serikali ilitumia shilingi bilioni 1.2 kujenga Skimu ya Umwagiliaji ya Mwakijembe, lakini bahati mbaya sana skimu ile mifereji haikujengewa wala hakuna bwawa lililojengwa kuvuna maji. Matokeo yake, leo hii tunapozungumza its hardly 10 percent ya mradi ndiyo imetumika. Nini kauli ya Serikali kuhakikisha skimu ile inafanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, ndiyo maana Serikali kwa kupitia msaada wa Serikali ya Japani sasa hivi mhandisi mshauri anapita nchi nzima ili kubaini matatizo ya miradi ya umwagiliaji ambayo imefanya efficiency ya miradi ya umwagiliaji isiwe nzuri. Ni kweli kabisa kwamba miradi mingi imejengwa lakini imekuwa na matatizo kwamba inalimwa mara moja tu, kipindi cha masika, baada ya hapo kilimo hakuna, kunakuwa hakuna maana. Ndiyo maana mpango huu unaoendelea wa mwaka 2002 kupitia miradi yote ya umwagiliaji kubaini shida ni nini ndipo tutagundua kwamba kumbe skimu zilijengwa lakini hazina maji kwa hiyo tuna mpango wa kujenga mabwawa. Lakini tusubiri ripoti ya wahandisi washauri, watakapokuwa wameikamilisha ndipo tutaendelea sasa kurekebisha mapungufu yote ili miradi hii iweze kufanya kwa uwezo mkubwa ule unaotarajiwa.
MHE. MAULID SAID A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokanana taarifa zilizotolewa na TMA wameeleza kwamba baadhi ya mikoa yetu katika Tanzania itapata chini ya wastani wa kiwango cha mvua, kwa maana ya Pwani, Tanga, Zanzibar na Morogoro Kaskazini. Je, Serikali ina mpango gani kukabiliana na tatizo litakalotokana na upungufu huo wa mvua?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali yetu kwa kushirikiana na wataalam mbalimbali duniani tunaanza kuandaa miradi ambayo itakuwa na efficiency kubwa kwa maana ya kutumia maji kidogo kwenye uzalishaji wa mimea. Teknolojia hiyo tunazidi kuichukua na kuiendeleza ili maji kidogo yanayopatikana yaweze kutumika vizuri na uzalishaji uwe mkubwa. Kwa hiyo, tumejiandaa, taarifa ya TMA tunayo na sisi tunaendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba production ya mazao hasa ya chakula itaendelea kuwa kama ambavyo matarajio yapo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la maji kwenye Wilaya ya Kilolo ni kubwa na kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ina utajiri mkubwa wa mito na vyanzo vya maji; na kwa kuwa tayari kuna utekelezaji mkubwa wa mradi wa maji ambao uliahidiwa na Mheshimiwa Rais ambao Wizara hii inafanya; je, kwa maeneo yale mengine ambayo tumekuwa tukipigia kelele kwa mfano Ruaha Mbunyuni, Wambingeto na sehemu nyingine, Waziri anasemaje? Ni pamoja na kuja kutembelea miradi hiyo ambacho ndicho kilio cha muda mrefu cha wananchi; Serikali inasemaje?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Jimbo lake ni miongoni mwa Majimbo ambayo yaliahidiwa kupata msaada kutoka Austria. Mpango huo unaendelea lakini kwa kuona kwamba unachelewa, sasa tumeanza utekelezaji kwa kutumia fedha za ndani. Mfano, Ilula sasa hivi tumepata chanzo cha maji kizuri kutoka Mkombozi na mradi umeanza ambao unatekelezwa na Mamlaka yetu ya Maji ya Iringa (IRUWASA) na pale ni kilometa 14, kilometa mbili zinatekelezwa na tutakuongezea shilingi bilioni tano kuhakikisha kwamba sasa maji yanafika mpaka Mji wa Ilula; na mipango mingine yote uliyoomba Mheshimiwa Mbunge tunaifanyia kazi ikiwemo Ruaha Mbuyuni, lakini pamoja na kuchukua maji Mto Mtitu kupeleka kwenye Makao Makuu ya Wilaya pale Kilolo, tunaendelea kuifanyia kazi.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali inakiri kwamba ujenzi wa bwawa hili ulikamilika mwaka 1958, kwa maana hiyo ujenzi huu uliwakuta wananchi wengi ambao walikuwepo pale kwa miaka mingi kabla ya hapo na kwa kuwa wananchi wanaendelea kunyanyasika maeneo yale na hasa kwa kukosa sehemu ya kilimo; na kwa kuwa kuna wananchi ambao wao ni waaminifu na hawaharibu mazingira.
Je, Serikali iko tayari angalau kuwapa wananchi maeneo mbadala ya kuweza kufanya shughuli zao za kilimo maeneo yale?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa maeneo yale kumekuwa na matatizo ambayo yanahusiana pia na mifugo ya wananchi hao hao wamekuwa wakikamatiwa mifugo yao na maafisa wa wanyamapori na wengine wala siyo maafisa wa wanyamapori wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi, wakikamata ng’ombe zao na wengine kuwapiga fine ambazo hazina hata receipt.
Nini tamko la Serikali kuhusu hawa maafisa wa wanaymapori hewa ambao wanakuwa wanafanya uhalifu ndani ya maeneo yale?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, mwaka 1958 eneo la Hifadhi ya Igombe halikuwa na wati wowote waliokuwa wanaishi pale katika kipindi hicho, kwa hiyo wote wameingia baada ya huo mwaka kwahiyo hakuna uhalali wowote kusema kwamba wananchi wameingiliwa na Mkoa wa Tabora bado ni mkubwa kwa hiyo watu wanaweza wakatafuta maeneo mengine kwenda kuendeleza maisha yao.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la unyanyasaji, ni kwamba mifugo na wewe Mheshimiwa Mbunge unafahamu kwamba sasa hivi Serikali inajitahidi. Tumekuwa kwamba watu hawakuwa na maeneo kwa ajili ya mifugo yao, lakini tumeendeleza kuongeza mifugo bila kutafakari ni jinsi gani ambavyo tunaweza tukamiliki maeneo yetu kwa ajili ya mifugo, kwa hiyo, ni kwamba mifugo imeingia katika lile eneo. Hata hivyo ni lazima tu-balance, ni kwamba lile bwawa likipotea, Tabora haina chanzo kingine cha maji.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi angalau tunatoa maji kutoka Ziwa Victoria lakini kabla ya hapo hatukuwa na chanzo kingine. Hebu tujionee huruma sisi kam binadamu. Mifugo imeingia pale, tuache lile bwawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu watu wa mifugo watafute eneo lingine. Mimi niseme hakuna unyanyasaji wa aina yoyote lakini mnyanyasaji ni yule mfugaji ambae anaingia katika lile eno halafu anasingizia watu wa Serikali.
MHE. RADHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa katika majibu ya Serikali inaonyesha kwamba mifereji imejengewa na mimi ninatoka kule ninafahamu kama mifereji hii haikujengewa.
Je, Waziri yuko tayari kuungana na mimi kwenda kukagua ili aweze kujionea kabla ya hiyo bajeti ya mwaka 2018/2019?
(b) Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ni sehemu ya ushirika huu, haoni kwamba ni vizuri wakaguzi hawa wakatoka Serikali kuu ili kuondoa mgongano wa kimaslahi lakini pia kuweza kuleta uwazi na uwajibikaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILAJI: Mheshimiwa Spika, sasa hivi tayari kuna timu ya Mhandisi Mshauri ambaye anapitia skimu zote za umwagiliaji nchini na ndiyo maana tumeonesha kwamba kuanzia bajeti ya mwaka 2018/2019 tutangiza kwenye bajeti.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kumaliza hiyo taarifa tutaangali hicho kitu kinachozungumzwa, kwamba mifereji ipo lakini haipo, basi tutaainisha; lakini pia na mimi niko tayarai kuongoza na Mheshimiwa Mbunge ili tuende tukaangalie; lakini la msingi tusubiri hiyo taarifa ya Mhandisi Mshauri.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ukaguzi; Mheshimiwa Mbunge kwa sasa hatuwezi kusema tutamtuma nani kwa sababu tayari tutakuwa tumewaonyesha wale wabadhirifu kwamba ni yupi wanaweza wakamuwahi. Hata hivyo nikuhakikishie kwamba tutaunda timu makini sana ambayo itakuja kufanya ukaguzi na itatuletea taarifa ambayo ni ya uhakika kabisa na wewe mwenyewe utaifurahia.
Mheshimiwa Spika, pia katika hiyo shughuli nitaendelea kushirikiana na wewe ili kuhakikisha kwamba hatua stahiki, ukaguzi unaostahili umefanyika ili Serikali iweze kushauriwa ipasavyo.
MHE. DKT. HAJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Nabu Spika, usimamizi na ushauri wa kitaalam wa jinsi ya uendeshaji wa Skimu hii ya Itete unafanywa na wataalam ambao wanakaa Makao Makuu Malinyi, kilometa 80 kutoka ilipo skimu hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umbali huo na uhaba mkubwa unaoikabili Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi watumishi hao, wataalam hao wanashindwa kutekeleza majukumu yao ya kikazi. Je, Serikali hasa Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji mnaisaidiaje Halmashauri ya Malinyi, ili kuwezesha skimu hii ifanye kazi kwa kiwango chake hata kuwapatia gari lililotumika tu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, eneo hili la Malinyi lina neema kubwa ya mito ambayo inatiririka maji masika na kiangazi ambayo kama ikitumika vyema tutaweza kumaliza kabisa tatizo la uhaba wa chakula katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu fupi sana; Serikali ina mpango gani sasa kuweza kuongeza skimu nyingine katika Wilaya ya Malinyi kwenye mito kama ya Sofi, Laswesa, Mwatisi, Fuluwa pamoja na Mto wa Mafinji ambayo kama itawekewa skimu tatizo la uhaba wa chakula hasa mpunga, litakuwa limeondoka kabisa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza anazungumzia habari ya usimamizi wa scheme ambayo tayari imeendelezwa na Tume yetu ya Taifa ya Umwagiliaji. Katika mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya mapitio ya kuangalia hizi scheme zote ambazo zimejengwa kwa miaka mingi na kuweza kupanga namna bora ya kuziendeleza ikiwa ni pamoja na kuzisimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunajipanga katika mwaka wa fedha huu unaokuja tuweze kuangalia scheme zile kubwa ambazo kwanza kulingana na sera tulikuwa tunakabidhi kwa Halmashauri au jumuiya ya watumiaji kuziendesha, lakini maeneo mengi tumeona kwamba hayaendi na jinsi tunavyopanga. Kwa hiyo, tunafanya mapitio na kuona namna bora ya kuweza kuweza kuziangalia namna ya kuzisimamia scheme hizi kwa ajili ya faida ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili; ni kweli Wilaya yake ina mito mingi na ndio maana tumesema Tume ya Taifa inafanya kazi ya mapitio ya mpango kabambe wa sera yetu ya Umwagiliaji na kuona namna gani bora tunaweza kuyaendeleza maeneo haya kwa kuweza hata kuwakaribisha wawekezaji wakubwa ili wajenge miradi mikubwa ya umwagiliaji katika maeneo ambayo maji yanaweza kupatikana kwa urahisi.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Tatizo la maji salama na maji safi katika nchi hii ni kubwa sana na Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI na Naibu Waziri wa Maji hivi majuzi walikuwa kwenye semina maalum ya programu ya maji inayoitwa “Uko Tayari?” Takwimu zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa katika hospitali wanaugua magonjwa yanayotokana na maji machafu. Je, Serikali kupitia Wizara zote (TAMISEMI na Maji) zina mkakati gani kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na salama hasa katika Awamu hii ya Tano?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yake amedai kwamba kuna magonjwa mengi mahospitalini ambayo yanatokana na kutokuwepo kwa maji safi na salama. Kuanzia bajeti ya mwaka 2006/2007 tulianzisha Programu ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji ambayo ilikwenda kwa muda wa miaka mitano, imekwisha Juni, 2016 sasa hivi tumeingia programu ya pili. Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba tunaweka fedha ya kutosha na miradi mingi sasa inatekelezwa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na salama na kwa karibu zaidi.
Kwa hiyo, tumeshaanzisha na tumelenga kwamba itakapofika mwaka 2020 vijijini tuwe tumeshakwenda zaidi ya asilimia 85 na mijini twende asilimia 95. Kwa hiyo, tupo na tumeshaanza siyo kwamba tumekaa, tunaendelea na tutahakikisha kwamba wananchi hawapati shida ya magonjwa yanayotokana na maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi ya hapo, sasa hivi tume-centralize kuhusiana na ununuzi wa dawa za kutibu maji. Utaratibu uliokuwepo ni kila Mamlaka inanunua dawa hizo kivyake sasa tutanunua kutoka center moja kwamba Serikali sasa itakuwa inafanya bulk purchase ya dawa za kutibu maji ili tuhakikishe kwamba maeneo yote tunakuwa na maji safi na salama. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, naomba wafanye kama walivyosema. Lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, mapema mwaka huu Waziri wa Maji alitembelea Mkoa wa Rukwa na akatembea Wilaya ya Nkasi, pia alipata nafasi ya kutembelea Mradi wa Kawa. Mradi wa Kawa una umri wa miaka sita na umetumia zaidi/karibu shilingi bilioni tatu, lakini wananchi wa vijiji vya Shengelesha, Kundi na Kalundi hawajaanza kupata maji, licha ya miundombinu yote kuwa imeshajengwa ya kupeleka maji.
Je, Serikali inawaambia nini wananchi hawa juu ya kupata maji mapema iwezekanavyo?
Swali la pili, hivi karibuni Serikali iliifunga shule ya sekondari ya Milundikwa na kuihamishia Kasu. Kijiji cha Kasu hakina maji ya uhakika ya kuweza kusaidia wananchi pamoja na shule.
Je, Serikali ipo tayari kufanya utafiti ili kipatikane chanzo kizuri kitakachowezesha kusaidia shule na kijiji cha Kasu, Katani, Milundikwa na Kantawa kwa ajili ya huduma ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mipata.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niipongeze Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Mipata kwamba utekelezaji wa mradi wa bwawa la Kawa umekamilika.
Mheshimiwa Spika, baada ya Mheshimiwa Waziri kutembelea pale Mheshimiwa Mipata ulimshauri Mheshimiwa Waziri kwamba mradi ule sivyema uendeshwe kwa kutumia jenereta inayotumia mafuta ya diesel, ukamshauri kwamba ni vyema tutumie umeme wa jua. Kutokana na huo ushauri wako nikufahamishe kwamba sasa tumekamilisha usanifu na wakati wowote tutanunua umeme wa solar na kufunga pale ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, ninaahidi ya kuwa ni muda mfupi tu unaokuja wananchi watapata huduma ya maji, kwa sababau maji yapo na miundombinu yote imeshakamilika.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili ni kweli baada ya Serikali kuhamisha shule ya Milundikwa na kuipeleka Kasu kumejitokeza tatizo la maji pale, ikiwemo vijiji vya Kantamwa, Milundikwa na Katani.
Mheshimiwa Spika, ninamuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri husika ashirikiane na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, kwa sasa mtaalam tunaye kule tayari ili tuweze kufanya usanifu tupate chanzo kitakachohudumia hii shule ya Kasu pamoja na vijiji vinavyozunguka ili wananchi wa maeneo hayo wasipate tatizo la huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi ni mwalimu wa hesabu na chemistry, nimesahihisha majibu ya Serikali na Mheshimiwa Naibu Waziri amepata 5% kati ya 100% ya majibu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo yake Mheshimiwa Naibu Waziri, ambaye ni rafiki yangu sana, ameandika kimoja tu cha ukweli kwamba mradi huu wa Kipunguni B umekamilika, mengine yote ni ya uongo.
Mheshimiwa Waziri, inaonekana ninaposema Jimbo la Ukonga lina shida ya maji hujui, upo tayari kutafuta taarifa sahihi ya miradi ya maji Jimbo la Ukonga uniletee kabla Bunge hili halijaisha? Hilo ni swali la kwanza.
Swali la pili, kipengele (b) hukujibu kabisa. Mimi nimeuliza kuchimba bwawa katika Mnada wa Pugu ambao ni Mnada wa Kimataifa, Dar es Salaam, hakuna mnada mwingine tofauti na huu, haukugusa kabisa. Umezungumza habari ya Kipera ambao ni mradi wa tangu mwaka 2016, uliandikwa kwenye Bajeti ya Maji na mwaka huu umeandikwa, haujaanza kutekelezwa. Nimeuliza bwawa la maji, hujajibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali la pili, upo tayari sasa nikuitie akina mama wote wa Ukonga pale ambao wanapata shida na hasa pale ambapo wanakwenda kujifungua hakuna maji zahanati kule Yongwe, Chanika, Msongola, Buyuni na Kivule ili uende Ukonga uzungumze nao wakueleze shida ambazo wanazipata wakienda kujifungua, wanaambiwa njoo na maji ambapo ndoo inauzwa shilingi 500? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa amesema kwamba taarifa niliyotoa siyo sahihi na amezungumzia suala la bwawa la Pugu.
Mheshimiwa Mbunge ni kwamba Serikali imefanya juhudi kubwa sana kupeleka maji katika Jiji la Dar es Salaam na miradi miwili mikubwa imekamilika ambayo inatoa kiwango kikubwa sana cha maji. Mradi wa tatu ambao utahusika na visima vile vya Mpera nao unakamilika mwezi Juni na utakuwa na lita zaidi ya milioni 260. Kazi iliyobaki ni kuyasambaza na tayari maeneo mengi ikiwemo na Kipunguni tayari mabomba yameshaanza kufika kule ikiwa ni pamoja na kuchimba visima. Siyo maeneo yote lakini tunaendelea. Matarajio yetu baada ya kupata fedha za kusambaza maji, maeneo yote yatapata huduma ya majisafi na salama, hilo nakuhakikishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza kama niko tayari kuongea na wananchi? Nimhakikishie kwamba niko tayari, wakati wowote nitakwenda kutoa majibu kwa wananchi bila wasiwasi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia amezungumzia suala la bwawa, ni kweli Mheshimiwa Mbunge swali hilo nimeliona, lakini wewe kwanza nikwambie umelelewa na CCM. Umechanganya maswali. Swali moja limekwenda Wizara ya Maji na Umwagiliaji lakini swali lingine lilikuwa ni swali la Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Eneo la Pugu, soko lile linahudumiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali hilo lilitakiwa lielekezwe huko, bahati mbaya lilikua ni namba moja. Kama namba zingekuwa mbili ningelipeleka kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu kama ameuliza kama swali la nyongeza, nitajibu kama Serikali. Ni kwamba tayari Wizara husika imechimba kisima kirefu, kisima kile kinatoa lita 1,500 kwa saa na tenki kubwa limejengwa ambalo lina ujazo wa lita 10,000. Kisima hicho hakijaanza kutumika kwa sababu kwa sasa mvua inayonyesha ni nyingi, kwa hiyo, mifugo inapata maji ya mvua. Lakini pia baada ya huu mradi mkubwa wa kutoka Mpera na Kimbiji kukamilika, tenki lililojengwa pale Pugu na Wizara husika litapata maji hayo ili kuhakikisha kwamba mifugo inapata maji na hakutakuwa na wasiwasi wa aina yoyote Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii. Pamoja na majibu mazuri na yenye kutia matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisiwa cha Jibondo kimejengeka kutokana na mawe na miamba mikubwa, huwezi ukachimba kisima pale ukapata maji. Wananchi wa Jibondo wamekuwa kwenye kadhia ya ukosefu wa maji toka dunia hii iumbwe, wanapata maji ya bahari na mara chache maji ya mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba usanifu pamoja na ujenzi utaanza mwaka ujao wa fedha.
Nilikuwa naomba aliahakikishie Bunge lako, ujenzi huu utaanza lini? Kwa sababu usanifu na ujenzi vyote vimewekwa pamoja, utaanza lini na utachukua muda gani ili nikitoka hapa niende nikawaambie wananchi wa Jibondo kwamba tarehe fulani maji yataanza kutoka Jibondo? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuingia katika vitabu vya historia na kuwa Waziri wa pili kufanya ziara katika Kisiwa cha Jibondo toka Mzee Malecela alipofanya hivyo miaka ya 1970 akiambatana na mimi Mbunge wa Jimbo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameuliza ujenzi utaanza lini? Kama nilivyosema kwamba usanifu umekamilika na wanakamilisha nyaraka za zabuni, tutatangaza tender. Kwenye ule mchakato wa tender ndiyo tutapata tarehe kamili kwamba mkandarasi ataanza lini na atakamilisha lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi ni kwamba kazi hiyo itafanyika katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, Mheshimiwa Mbunge tutahakikisha tunafanya kazi hiyo na tunakamilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema kwamba Kisiwa cha Jibondo kimejaa mawe, ni kweli na ndiyo maana tumechimba kisima eneo lingine la Kiegeani na bomba lile litapita chini ya bahari mpaka liende kwenye Kisiwa cha Jibondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeniomba nitembelee pamoja na wewe, Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari. Baada ya kumaliza bajeti hii, basi tutazungumza na tutatengeneza ratiba ili twende mpaka Kisiwa cha Jibondo nikawahakikishie wananchi kwamba wanapata maji. (Makofi)
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nataka kujua kwa nini hasa Jimbo la Ulyankulu lilitengwa kwa miradi hii mikubwa kwa sababu kutoka Tabora Mjini kwenda Ulyankulu centre ni kilometa 90, kutoka Kaliua kwenda Ulyankulu ni kilometa 90, kutoka Kahama kwenda Ulyankulu ni kilometa 90…
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini Serikali isi-plan kuhakikisha mradi mmojawapo unapeleka maji Ulyankulu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Naibu Waziri yuko tayari sasa kuambatana na mimi baada ya Bunge hili akaone mwenyewe vyanzo vya maji badala ya kusubiri taarifa za maandishi za wataalam wake ambao mimi naamini kabisa taarifa wanazoleta siyo sahihi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge niseme Jimbo la Ulyankulu halijatengwa, ni jimbo jipya, limetangazwa juzi juzi. Nafahamu Ulyankulu ina miradi ya maji ambayo kidogo haina hali nzuri, inatakiwa tuifanyie ukarabati kwa sababu kuna mabwawa ambayo muda mrefu yanatumika na mabomba yapo. Kwa hiyo, tutayafanyia kazi ili kuhakikisha yanaimarika na wananchi wanapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tutafanya utafiti na kufanya ulinganisho ama kutoa maji Kahama au kutoa maji upande wa bomba hili litakalotoka Malagarasi sehemu ya Kaliua. Pale patakapokuwa pako cost effective, tutahakikisha kwamba maji yanatoka ama Ziwa Victoria au kutoka Malagarasi na kuhakikisha wananchi wanapata maji yenye uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameomba kufuatana na mimi. Mheshimiwa Mbunge niko tayari tukimaliza Bunge tufuatane ili na mimi niende nikajionee huko na tushauriane pamoja na Halmashauri ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na salama kwa haraka.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ya tambarare ya Kilimanjaro yana shida ya maji safi na salama. Ni lini sasa Serikali itatumia Lake Chala ili kuyapatia maeneo ya tambarare maji vikiwemo vijiji vya Mahida, Malawa, Ngoyoni, Ngareni, Holili na kwingineko?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari na inatekeleza miradi mingi ya maji na mipango kemkem ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutoa maji kutoka Lake Chala, naomba tushirikiane na Halmashauri yako ambayo hilo bwawa liko katika hiyo Halmashauri ili tuone jinsi gani tunaweza tukafanya utafiti na kuweka fedha kuhakikisha vijiji vinavyozunguka sehemu hiyo vinapata maji.
MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Rungwe ni moja kati ya Wilaya ambazo zimebarikiwa sana kuwa na vyanzo vingi vya maji. Hata hivyo, kuna baadhi ya maeneo maji yamefungwa yasiendelee kutiririka kwa sababu ya uhaba wa maji, hakuna matenki, miundombinu ni ya kizamani mno na watu wameongezeka.
Je, Serikali ina mpango gani na Wilaya ya Rungwe ili kuisambazia maji ambayo hayana taabu ni maji ya kutega? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa kwamba Wilaya ya Rungwe kuna maji ya mtiririko/mserereko. Ndiyo maana tumehakikisha kwamba kila Halmashauri inapatiwa fedha na Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili sasa hilo suala la miundombinu, matenki na watu wameongezeka, kwa sababu maji yapo tuhakikishe kwamba tunaiboresha na wananchi wanaweza kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshauri Mheshimiwa Mbunge kama anaona wataalam wake kidogo wana upungufu, Wizara ya Maji na Umwagiliaji tuko tayari kusaidiana kutoa wataalam ili kwenda kukamilisha hiyo miradi kwa sababu fedha ipo.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Jimboni kwangu Kata ya Mbangala nina Kampuni inaitwa Shanta Gold Mining. Kampuni hiyo imefunga Mto Lwika na kusababisha wananchi wa Mbangala kutopata maji. Miezi miwili iliyopita kulitokea vurugu kubwa sana kati ya Polisi na vijana wa pale Mbangala lakini Serikali ipo na wanaona kabisa bwawa limefungwa na mto hautiririki kwenda hata vijiji vya Maleza. Je, Serikali inaniambia nini juu ya Ashanti wafungue ili na sisi kijiji cha Mbangala tuweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kampuni ya Shanti kufunga bwawa Mbangala, Mheshimiwa Mbunge ndiyo anatoa taarifa sasa hivi. Naomba tuwasiliane ili tuhakikishe tunatatua hili tatizo kwa haraka sana. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na naipongeza Serikali kwa kuja na huu mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa Bonde la Mto Songwe linaendelea kuwa endelevu kwa ajili ya matumizi ya wananchi wanaozunguka mto huo. Lakini nataka niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji iliyowasilishwa hapa Bungeni kwa ajili ya mwaka 2016/2017 tulielezwa kuwa kuna mambo ambayo tayari yameshafanyika kuhusiana na juhudi za kuendeleza rasilimali za bonde hili, lakini vilevile katika masuala mazima ya kutengeneza mpango wa biashara kwa ajili ya kuendeleza bonde hili. Nataka kujua na ilisemekana kuwa vingekuwa vimekamilika kwa mwaka 2015. Je, jambo hili lilifanyika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyozungumzia mkakati mzima wa uendelezwaji wa Bonde la Mto Songwe, wananchi wa kawaida katika maeneo ambayo yanahusika na yanaguswa na bonde hili hawana taarifa zozote wala elimu ya aina yoyote wala hawajui ni nini kinachoendelea.
Je, hii ofisi ndogo ya muda iliyoundwa imeanza kufanya kazi gani ili wananchi wetu waanze kupata uelewa ili hata mkakati huu utakapoanza kufanya kazi wawe tayari kuupokea? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nishukuru Bunge lako Tukufu, katika Bunge lililopita tulipitisha hii Kamisheni ya Songwe ambayo imeanza kazi na kwamba ofisi ipo Kyela pale na wananchi wanaitambua. Lakini tayari tumeshaomba fedha kwa ajili ya kujenga mabwawa matatu kupitia hilo Bonde la Mto Songwe ili kuweza ku-control mafuriko. Mabwawa hayo yatatumika pia kuzalisha umeme, lakini pia na kilimo cha umwagiliaji zaidi ya hekta 6,200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa mchakato mzima wa uandaaji wa huo mradi, wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya walishirikishwa kupitia Halmashauri zilizopo ndani ya Mkoa wa Mbeya; kwa hiyo, wananchi wapo aware.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tuendelee kushirikiana kama kuna hitaji la kuendelea kuwafahamisha basi tuendelee kuwafahamisha, lakini mradi unakuja na kwamba tayari kupitia taasisi yetu ya SADC mradi huu umeshaingizwa kwa ajili ya kuombewa fedha na utekelezaji uweze kuanza. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Waziri wa Maji na Waziri wa TAMISEMI kwa kuteua Bodi ya Maji na pili kuwatuma wataalam kule Mbulu kwa ajili ya suala hili la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Mbulu na hasa Mji wa Mbulu, hali ya maji imekuwa mbaya kwa takribani sasa miezi sita. Katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 tulitenga fedha shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya utafiti na usanifu wa maji katika Mji wa Mbulu. Je, ni lini mpango huu sasa Wizara itatusaidia ili tuweze kupata maji ya uhakika kuepukana na adha hii ya ukosefu wa maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kubaini upungufu katika Halmashauri yake nilimwelekeza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji BAWASA, ameenda kule kuangalia, akagundua matatizo mengine ni madogo sana, ni pampu tu zimekufa zinahitaji matengenezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari ameshaandaa quotation na wiki hii nakutana naye ili tuweze kumpatia hela akafanye kwanza ufufuaji mdogo ili wananchi wapate maji, lakini baada ya hapo tutatekeleza mradi mkubwa kuhakikisha kwamba Halmashauri yake na kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi tunapata asilimia 95 ya huduma ya maji.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pia naishukuru Serikali kuchimba visima vya Dumbeta, Waranga, Hirbadaw, Gidika na Dawar lakini ndiyo imebakia hivyohivyo wamechimba visima lakini havitumiki kwa sababu hawakuweka pampu na hatukusambaza maji. Naomba niiulize Wizara ya Maji watasaidiaje Wilaya yangu ya Hanang kuona kwamba hivi visima vilivyochimbwa vinawapatia maji wananchi kwa sababu wanayasubiri na lile ni eneo kame sana? Naomba jibu la swali hili.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumechimba visima na maji yamepatikana kinachofuatia sasa hivi ni suala la kitaalam, wanafanya pamp test kuhakikisha kwamba maji yaliyopo yana utoshelevu wa kutosha na ili waweze ku-design miundombinu itakayowezesha hasa kujenga matenki na mtandao wa mabomba ili wananchi waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maagizo yangu baada ya maji kupatikana Halmashauri sasa waanze kufanya kazi hiyo ili tuweze kutekeleza hiyo miradi na ndiyo utaratibu wetu, huwezi kutekeleza miradi bila kuanza kupata chanzo cha maji. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa kwamba chanzo cha maji sasa amepata kinachofuatia ni kuweka miundombinu.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Mradi wa Ntomoko ambao ulipangwa kuhudumia Wilaya za Kondoa na Chemba unaonekana dhahiri ni kama umechezewa. Je, Serikali iko tayari sasa kupokea ushauri wangu kwanza kusimamisha malipo ya mkandarasi aliyekuwepo na ifanye ukaguzi wa kutosha kwa sababu mradi huu ni kama hauna manufaa yoyote kwa wananchi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwamba tayari nimesimamisha malipo, hakuna malipo mengine yatakayolipwa katika mradi wa Ntomoko na mkandarasi alikuwa anadai shilingi milioni 700, nimesimamisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili tumefanya kikao cha pamoja kati ya TAMISEMI, Wizara ya Maji na Mamlaka ya Maji ya Dodoma wanapitia usanifu kwa muda wa mwezi mmoja na nimekabidhi huo mradi baada ya hapo utatekelezwa na Mamlaka ya Maji ya Dodoma yaani DUWASA. Kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ule mradi umechezewa, hatua nyingine zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria kwa wale wote ambao wamechezea huo mradi.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Rais alipokuja kufanya kampeni yake katika Mji Mdogo wa Nyamongo ambao una wakazi karibia 45,000 aliahidi kuwapatia maji. Kwenye kitabu cha bajeti ya mwaka jana ilioneshwa kwamba upo mradi kwa ajili ya kutoa maji Mto Mara na kupeleka kwenye Mji wa Nyamongo ambao vyanzo vyake vyote vya maji vimechafuliwa na mgodi na sumu ambazo zimeingia mgodini samaki wanakufa na watu hawana maji ya kutumia. Serikali imefikia wapi kuwapelekea watu wa Nyamongo maji kwa sababu ni ahadi ya Rais na ilikuwa kwenye mpango wa Serikali wa mwaka uliopita? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakamilisha usanifu wa mradi mkubwa utakaotoa maji Ziwa Victoria kupeleka mpaka Tarime kupitia kwenye eneo la Nyamongo. Kwa hiyo, tuko kwenye hatua nzuri, Mheshimiwa asubiri tu tunakamilisha na kutafuta fedha na tutatekeleza mradi huo.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nina maswali mawili ya ngongeza. Hali ya upatikanaji wa maji hasa katika eneo la Bonde la Ufa katika Jimbo la Manyoni Mashariki ni ngumu sana, hivi ninavyozungumza mifugo inahangaika, watu wanahangaika, akinamama wanalala kwenye visima ambavyo havina uhakika wa kupatikana kwa maji, hali ni ngumu sana kwa kweli. Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba litawekwa katika kipaumbele cha bajeti inayokuja, ninaomba tu ni ombi, kwa emergency, kwa hali ambayo nimeielezea hii, hali ni ngumu, naomba liingizwe kwenye bajeti ya mwaka unaofuata.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Kata ya Sorya Wilayani Manyoni, kwenye Jimbo langu katika harakati za kuhangaika kuwatafutia ajira vijana na akina mama tumetenga eneo, zaidi ya eka 400 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na tumechimba visima vitatu kwa fedha yetu wenyewe. Tuna shida ya umeme kwa ajili ya kufunga pampu za kutoa maji ili tuweze kumwagilia.
Je, Serikali inaweza kutusaidia sasa kupeleka umeme kwenye visima vile ili kunusuru wananchi hawa wanaohangaika, hasa vijana, tuweze kumwagilia maeneo haya na tuweze kujinusuru kwa suala la njaa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie kama tulivyoji-commit kwenye jibu la msingi, kwamba tutaweka kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa hiyo naomba nimhakikishie kwamba tutafanya hivyo kwa sababu tumeshatoa jibu la namna hiyo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu ekari 400 ambazo mmepanga kuendeleza kilimo cha umwagiliaji; nilipokee ombi lake lakini tutaangalia uwezo wa bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu wa fedha, kama itawezekana tutasaidia, lakini vinginevyo tutaangalia katika bajeti ya mwaka utakaofuata.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya kuridhisha, lakini naomba tunapouliza maswali haya tuwe tuna kumbukumbu ya majibu. Swali hili nimeshaliuliza zaidi ya mara ya tatu, katika bajeti ya mwaka 2017/2018 nimeuliza swali hili hapa Bungeni, Naibu Waziri wa Maji na sasa Waziri alijibu kwamba kwa mwaka wa bajeti 2016/2017 malambo haya yangefanyiwa ukarabati na bajeti ya Halmashauri ikaletwa hapa Bungeni sasa tena kipindi hiki wanasema bajeti itakuwa 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimshukuru Naibu Waziri wa Maji ambaye sasa ni Waziri alikuja kwenye Jimbo langu akaangalia miradi akamuuliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya kwa hali iliyoko hapa Bunda unajua bajeti kiasi gani ya maji unayo. Mkurugenzi akasema haelewi, akatuambia ana bilioni 1.7 ya Halmashauri ya Bunda kwa ajili ya maji. Ni kwa nini hizi hela zisitumike kutengeneza haya malambo wakati yanahitaji shilingi milioni 350? Naomba Waziri atoe tamko la kutengeneza malambo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tuna mradi mkubwa sana Mkoa wa Mara unatoka Mgango unakwenda Butiama lakini Vijiji vya Kata za Nyamswa, Kitare, Nyamamta na Salama viko jirani kilomita tatu kutoka kwenye mradi huu. Naomba Serikali ione namna gani inaweza kufanya vijiji hivyo viingie kwenye mradi mkubwa kutoka Ziwa Victoria. Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Getere kwa jinsi ambavyo anahudumia jimbo lake na alishawahi kunichukua tukaenda mpaka jimboni kuangalia matatizo ya miradi hii ya maji. Alichokisema ni kweli bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri yake hawakutumia hata senti tano, fedha yote ikarudi wakati wana matatizo ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Jafo, Waziri wa TAMISEMI aniruhusu niagize Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bunda na Mwenyekiti, siku ya Jumatano wiki ijayo waje tukutane pamoja na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kutatua matatizo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, tumetangaza tender kwa ajili ya kuweka bomba kubwa jipya la mradi wa Mgango-Kyabakari. Kwa hiyo, wakati wanaweka bomba hilo Mheshimiwa Mbunge nitaomba tuwasiliane ili tuweze kuainisha na hivyo vijiji vitatu alivyovisema navyo vipate maji kutoka Mgango. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kutokamilika kwa miradi ya maji katika Halmashauri zetu kumekuwa ni tatizo sugu, niliwahi kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wakati huo ambaye sasa ndiyo Waziri alisema pesa Wizarani zipo ila watu wapeleke certificate. Ninasikitika kumwambia kwamba hapa ninayo makabrashi ambayo ni copy ya hizo certificate ambazo zimeshafika kwenye Wizara yake sasa ni zaidi ya mwaka mzima hizo pesa hazijawahi kutolewa, na kuna miradi kadhaa katika vijiji vya Kipule, Ngongowele pamoja na Mikunya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kauli ya Serikali ni lini miradi hii itakamilika ili wananchi wa vijiji hivi waweze kupata maji. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa sababu certificate, ni masula ya kiutendaji Mheshimiwa Mbunge, ninaomba baada ya Bunge hili leo tukutane, twende kwa watendaji tukaangalie certificate kama zipo, kama nilivyosema kwamba tayari nina fedha ili wiki ijayo tuweze kulipa.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza Wilaya ya Lushoto ina vyanzo vingi sana vya maji lakini wananchi wa Lushoto hawana maji safi na salama.
Je, Serikali ina mpango gani wa kumtua mama ndoo kichwani hasa akina mama wa Makanya, Kilole, Kwekanga, Kwemakame, Ngulwi, Ubiri, Handeni na Miegeo? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea Lushoto nikakuta hilo tatizo na nikamuelekeza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Tanga aweze kutekeleza miradi ya maji katika Halmashauri yake, hadi jana nimepiga simu tayari wamekamilisha taratibu za manunuzi, Baada ya siku 14 mikataba itasainiwa, utekelezaji uanze.
Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba maeneo yote ya Halmashauri yako yatapata maji.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya upatikanaji wa maji katika Mikoa ya Lindi na Mtwara bado ni mbaya sana na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji ambaye sasa ni Waziri wa Maji alipotembelea Mikoa ya Lindi na Mtwara alikagua baadhi ya miradi ambayo inaendelea katika Jimbo la Mtama, Mradi wa Maji wa Nyangamara na pengine hakufika lakini Mradi wa Maji wa Namangale na alituhaidi kwamba certificates za miradi hiyo zikifika Wizarani mara moja pesa zitalipwa, mpaka sasa huu ni mwezi wa pili au wa tatu certificates hizo zimefika Wizarani na hazijalipwa.
Je, ni lini Serikali italipa pesa hizi za hawa wakandarasi ili miradi hii ipate kukamilika wananchi wangu wapate maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha na Mipango jana ametupatia shilingi bilioni 12. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba hizo certificates kama zimeshaletwa wiki ijao tutahakikisha tumezilipa ili mkandarasi aendelee kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya maji nchini kwa ujumla siyo nzuri na lengo Namba 6 la ajenda ya 2020/2030 ni maji, upatikanaji wa maji safi, salama kwa wote duniani na Tanzania ni mwanachama. Katika Jimbo la Vunjo sehemu za kata….
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa. Katika Kata ya Mwamba Kusini na Mwika Kusini hali ya maji ni mbaya sana na wananchi wananunua maji ndoo moja kwa shilingi 500.
Je, Serikali inachukuliaje jambo hili kwa dharura ili upatikanaji wa maji uweze kupatikana kwa haraka?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya upatikanaji wa maji nchi ni nzuri kupitia programu ya maendeleo ya sekta ya maji awamu ya kwanza. Tulilenga kutekeleza miradi 1,810, tayari tumeshatekeleza miradi 1,433, tumejenga vituo vya kuchotea maji 117,000 na vituo vyote vingetoa maji vijijini sasa hivi tungekuwa na asilimia 79 ya upatikanaji wa maji safi na salama. Kutokana na mabadiliko kidogo ya tabianchi vyanzo vingi vya maji kukauka sasa hivi hiyo asilimia kidogo imeshuka, lakini tayari tumejipanga kuhakikisha maeneo yote ambayo hayatoi maji tumetenga fedha kwenye bajeti ya mwaka huu tulionao ili hayo maeneo yaweze kupatiwa vyanzo vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Vunjo Mheshimiwa Mbunge naomba tukutane, tujadili ili tuone ni namna gani tutatoa kitu cha dharura kuhakikisha wale wananchi wanapata maji.
MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa swali la msingi linafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Wilaya ya Urambo na Kaliua na Serikali imekuwa ikituambia kwamba imekamilisha mchakato wote wa kutoa maji Mto Malagarasi kupeleka Kaliua na Urambo, fedha tu ndiyo bado hazijapatikana toka mwaka jana walituambia fedha hizo zitapatikana.
Je, status ya kupata pesa kupeleka maji katika Wilaya ya Urambo na Kaliua ikoje mpaka sasa kwa sababu hali ni mbaya sana kwa wananchi hao? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunao mradi wa usanifu unakamilika wa kutoa maji Malagarasi kupitia Kaliua kuja Urambo hadi Tabora, pia Mheshimiwa Rais ametuagiza kwamba huu mradi unaotoa maji Solwa kutoka Ziwa Victoria kupeleka Tabora wakati unaendelea tayari tumeshaagiza Mamlaka yetu ya Maji ya Tabora iangalie uwezekano wa kuweka mabomba mengine kutoka matanki ya Tabora kupeleka Urambo na ikiwezekana yafike mpaka Kaliua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie Mheshimiwa Munde kwamba Serikali inafanya kazi kuhakikisha Kaliua na Urambo wanapata maji safi na salama. (Makofi).
MHE. MAULUD S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii na mimi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubaliana kwamba maji ni uhai na kila mwananchi anahitaji maji; lakini tunakubaliana pia kwamba zamani tulikuwa na mabomba yetu ya Serikali ambayo wananchi walikuwa wanapata maji bure, lakini sasa hayapo.
Je, Serikali ian mpango gani kuyarejesha yale mabomba yetu ili wananchi wetu wapate maji bure kwa wale ambao hawana uwezo ukizingatia kwamba kuhitaji maji hakutegemei uwezo wa fedha za mtu? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba zamani kulikuwa na mabomba ambayo yalikuwa yanatoa maji bure na hivyo kusaidia wale watu wasiojiweza, lakini kwa sasa mamlaka zote zimepewa maelekezo na zina sheria kwamba kila mamlaka kwenye mkoa inashirikiana na uongozi wa mkoa kubaini wananchi wote ambao hawana uwezo kama wazee na wagonjwa, kwa hiyo wakiorodheshwa wanaendelea kupata kupata huduma ya maji bure.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mkoa wa Katavi ni mkoa ambao bado hauna chanzo kizuri cha maji; Mkoa wa Katavi umepakana na Ziwa Tanganyika. Je, Serikali ina mpango gani kuweza kuyatoa maji Ziwa Tanganyika na kuyaleta Makao Makuu ya Mkoa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kutumia maji ya Ziwa ya Tanganyika kupeleka Mkoa wa Katavi, tayari andiko limeshaandikwa na limeletwa. Wizara tunafanyia kazi na mwaka ujao wa fedha tutaweka mshauri ili aanze kufanya kazi na baadaye tuongeze fedha kwa ajili ya kuchukua maji kutoka Kalema kuyaleta Mji wa Mpanda kupitia Jimbo lake. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mwaka jana tumepitisha kwenye bajeti miradi 17 mikubwa nchini Tanzania, ikiwemo 16 Tanzania Bara na mmoja Zanzibar, ikiwemo na Makambako, kutokea fedha za kutoka India. Je, Waziri anawaambia nini wananchi wa Makambako juu ya ule mradi mkubwa ambao utajengwa katika Mji wa Makambako, lini utaanza ili wananchi hawa waweze kuondokana na adha na tabu ya maji wanayoipata katika Mji wa Makambako?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tumepata mkopo wa dola milioni 500 kutoka Serikali ya India na sasa hivi Wizara ya Fedha inakamilisha taratibu, wakishamaliza tunasaini financial agreement na mimi niko tayari, nimeshaandaa. Baada ya hilo tukio tu nitapeleka Wahandisi wakasanifu haraka. Wakishamaliza usanifu, tukiingia mikataba, tutajua mkataba utaanza lini na utakamilika lini, kwa hiyo niwahakikishie wananchi wake wa Makambako kwamba huo mradi unakuja.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Tatizo la maji lililoko Mkoa wa Pwani linafanana kabisa na tatizo la maji lililopo Jimbo la Ngara ambapo tunapata maji kwa wiki mara moja au mara mbili. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hili la maji katika Wilaya ya Ngara?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Wizara yangu inatafuta mkandarasi mshauri ambaye ataanza kufanya design ya kutumia maji ya Mto Rubuvu kupeleka Ngara kwa sababu yale maji ni mengi kwa hiyo yatasambaa maeneo mengi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikwambie tu kwamba Serikali, Wizara yangu haijalala tayari inaangalia maeneo yote na kutumia vyanzo vilivyopo kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata maji safi na salama.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mradi wa maji wa Kijiji cha Getamog Wilayani Karatu, uliojengwa katika ule mpango wa Benki ya Dunia ambao uligharimu takribani shilingi milioni 600 haufanyi kazi kwa sababu umejengwa chini ya kiwango. Nimshukuru Waziri wa Maji kwa kutuma wataalam wake ili kubaini tatizo hilo, ili mradi huo uweze kurekebishwa.
Je, ni lini Serikali sasa itapeleka fedha ili wananchi wa Kijiji cha Getamog waendelee kupata huduma hiyo muhimu? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilipata hiyo taarifa na nikamuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Arusha, ambaye ameenda kule kuangalia uchunguzi namna gani mradi ulijengwa chini ya kiwango. Taarifa hiyo ikishapatikana, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba Serikali itafanya maandalizi ya kuweka mkandarasi wa kuboresha ule mradi na fedha itatolewa baada ya kuleta hati za malipo.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe lina vyanzo vingi sana vya maji, lakini vijiji vyake vingi havina maji. Je, ni lini Serikali itapeleka maji katika Kata za Ikuna, Ninga, Kichiwa, Kidegembye, Lupembe, Matembwe, Mtwango na Igongolwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza. Waheshimiwa Wabunge katika Halmashauri ambazo zimetumia fedha vizuri kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 ni pamoja na Halmashauri ya Lupembe, ilitumia fedha zote ambazo zilikuwa zimetengwa na tukawaongezea nyingine. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi hiyo tutahakikisha tunatenga fedha zaidi, ili vijiji vingine vyote vilivyobaki vipate maji.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Arusha una majimbo ambayo kijiografia yana mazingira magumu sana, hasa Jimbo la Ngorongoro na mara nyingi Mawaziri mmekuwa mkifika pale mmeona mazingira yale na kumekuwa na tatizo kubwa sana la upatikanaji wa maji kwenye vijiji vilivyoko katika Jimbo la Ngorongoro.
Je, Serikali sasa ina mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha Jimbo la Ngorongoro linatizamwa kwa upekee na wananchi wake wanaweza kupata maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali ambalo limeelekezwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya maji katika Halmashauri ya Ngorongoro kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Januari, tumesaini mkataba wa milioni 270 kwa ajili ya mradi wa maji katika Halmashauri ya Mji wa Ngorongoro, sasa hivi tunafanya design ambapo tunatarajia mwezi Aprili, tutasaini mkataba mkubwa ambapo tutapeleka maji zaidi ya vijiji tisa likiwemo eneo la Mageli. Kwa hiyo, suala la maji upande wa Ngorongoro linashughulikiwa na tutahakikisha kwamba asilimia 85 itakapofika 2020 inafikiwa pia katika Halmashauri ya Ngorongoro. (Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mto Kagera, pamoja na Mto Ruvugu ni mito ambayo ikitumiwa vizuri inaweza kuondoa kero ya maji kwa Mkoa wa Kagera na Mkoa wa Geita; na kwa kuwa tayari mwaka 2017 Mheshimiwa Rais alipokuja Jimbo la Ngara wananchi wa Jimbo la Ngara kupitia Mbunge wao tulimwomba kuanzisha mradi huu mkubwa wa maji kwa ajili ya kutatua kero ya maji Wilaya za Ngara, Biharamulo, Karagwe, Bukombe, Mbogwe na Chato kwa kutumia fursa ya kijiografia Wilaya ya Ngara.
Ni lini mradi huu sasa utaanza kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu ili kuondoa kero kwa wananchi wa Mkoa wa Geita na Kagera? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lililoulizwa na Mheshimiwa Dkt. Kamala linahusu pia Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ambapo huyu mkandarasi ambaye anamalizia usanifu wa kina, anahusisha miji sita kama alivyoitaja Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunarajia kwamba kwa vile tayari upembuzi yakinifu tunao, tunamalizia usanifu wa kina, tunarajia kupanga bajeti kwenye mwaka ujao wa fedha na kuanzia mwezi wa tisa tutaanza kutangaza tenda ambayo itahusha pia na Mji wa Ngara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie pamoja na wananchi wako wa Ngara kwamba tunatekeleza hiyo miradi ili uweze kupata huduma ya maji. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri wa Maji kwamba Bunge lililopita niliwaomba kwamba Kata ya Msongola ina matawi tisa na ina maji kwenye visima vitatu katika mitaa mitatu tu. Kata ya Zingiziwa, Chanika, Buyuni na Pugu, hazina maji. Mvua ikinyesha ndiyo wananchi wanachota maji yale wanatumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, ni kwa nini Mawaziri hawa wamekataa kuja Ukonga kuongea, hata kuwapelekea akina mama wenye shida ya maji pale na wanakaa Dar es Salaam?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyolieleza Bunge, kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam na Miji ya Kibaha tayari tumeshakamilisha miradi miwili na tuna maji ya kutosha zaidi ya lita milioni 510 ambayo ni maji toshelevu. Kinachoendelea sasa hivi, tulikuwa tunahitaji dola milioni 100 ili tuweze kukamilisha usambazaji katika eneo lote la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani na awali tulipata dola milioni 32 mradi ambao sasa utakamilika tarehe 15 Februari, 2018 lakini tumepata tena dola milioni 45 kutoka Benki ya Dunia. Tunarajia kutangaza tenda mwezi huu wa pili; tunaendelea, itakuwa imebaki fedha kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka maeneo yote ya Zingiziwa unayoyazungumza tutahakikisha kwamba maji yanafika.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tatizo lililopo Mlimba linafanana kabisa na tatizo la ukosefu maji safi na salama lililopo katika Mkoa wa Katavi. Serikali iko tayari kutumia maji ya Mto Mpanda, Mto Manga, Mto Katuma ili wakazi wa Kata ya Mwamkulu, Kakese pamoja na Kasokola wapate maji safi na salama hususani katika suala la kilimo katika Mkoa wa Katavi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshatekeleza miradi mingi ya visima katika Mkoa wa Katavi na tayari tumetumia mito iliyopo kupeleka maji katika Mji wa Mpanda na sasa hivi tunaelekea kuwa na asilimia zaidi 70 ya maji safi na salama katika Mji wa Mpanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshapokea andiko na tunalifanyia kazi ili tuweze kumaliza tatizo la maji kabisa katika Mkoa wa Katavi kwa kuchukua maji kutoka katika Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya kazi kunakikisha mikoa yote inapata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Bwawa la Nyumba ya Mungu kwenda Wilaya ya Same na Mwanga ni mradi ambao ulipaswa uwe katika hatua za mwisho za utekelezaji, lakini mpaka ninapoongea leo mradi huu umeonekana kutokufikia hata asilimia 40 ya utekelezaji wake.
Je, Serikali imejipangaje katika kuwakwamua wakazi wa Wilaya ya Same na Mwanga na especially wanawake wote na wapiga kura wangu wa Wilaya ya Same na Mwanga? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Same/Mwanga kutokutoa maji kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu, mkandarasi wa kwanza yuko asilimia 75, mkandarasi wa pili tayari anafika asilimia 30 na kazi inaendelea. Sasa hivi tank kubwa la Mlima wa Kiverenge linajengwa ambapo tank hilo likishakamilika, sasa maji yatakwenda Mji wa Mwanga na Same; na kazi inaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya miezi sita wananchi wa Same na Mwanga wataanza kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ingawa baadhi ya maeneo aliyosema yamekamilika, miradi yake haijakamilika. Nina maswali mawili ya nyongeza:
Swali la kwanza; maeneo niliyoyataja haya ya Kata ya Ruhunga, Kibirizi, Izimbya, Mugajwale, Rukoma, Kikomelo na mengine kama Kaitoke, Kyamuraire yana shida kubwa sana ya maji na swali hili nimeliuliza leo ni mara ya nne. Je, niulize mara ngapi ili hawa wananchi nao wafikiriwe kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa vile tumeshapata ufumbuzi wa tatizo la maji nchi nzima maana yake siyo kwangu tu ni nchi nzima kuna tatizo la maji nao ufumbuzi huo ni kuunda wakala au Mfuko wa Maji nchi nzima kama ilivyo REA kwenye umeme. Tumelijadili humu mara nyingi na tumekubaliana. Je, kwa nini Mfuko huu hauanzi ili tatizo hili liweze kupata ufumbuzi. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza huo mradi wa maji kwenye eneo lake tulishaujadili na tukaangalia uwezekano wa namna gani tunaweza tukapeleka maji pale kwa kutumia chanzo cha maji cha Ziwa Victoria kutoka kwenye mradi uliokamilika pale Bukoba na tayari tulishaagiza wataalam wanafanyia kazi ili tuweze kufikisha maji katika hayo maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu uanzishaji wa Mamlaka ya Maji Nchini tunalifanyia kazi na tuko katika hatua nzuri kabisa wakati wowote tutaleta tangazo kwamba tayari Wakala wa Maji Nchini utaanzishwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji pale tutakapopata ridhaa ya Bunge. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Swali langu narudia pale pale kwamba kama alivyouliza Mheshimiwa Rweikiza ni kwamba ni lini Serikali itafikiria kuanzisha Mfuko huu wa Maji ili kuweza kuondoa kero kubwa kwa wananchi kuhusu matatizo ya maji kama ambavyo tumeweza kuondoa kero ya umeme sasa katika sehemu nyingi vijijini. Je, ni lini tutaanzisha huu Mfuko wa Maji? Nadhani ndiyo hoja ya msingi zaidi hapa.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna mambo mawili; Mfuko ulishaanzishwa. Mfuko tayari tunao na Mwaka huu wa Fedha tulionao Mfuko una jumla ya shilingi bilioni 158. Suala la pili sasa tunataka kuanzisha Wakala kwa ajili ya kutumia huo Mfuko ili tuwe na wakala utakaohakikisha kwamba tunapata huduma ya maji vijijini kwa haraka. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utangulizi tu nipende kusema kwamba jibu ni jibu hata kama halikutosha kwa muuliza swali huwa ni jibu. Hii bla bla yote iliyotolewa kwenye aya ya pili mimi sioni kama ni jibu linalijitosheleza kwa sababu mradi huu umehujumiwa kwa kiwango kikubwa sana. Kwenye ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kwenye Jimbo langu, mimi na Mkuu wetu wa Wilaya na Mkurugenzi wetu wa Halmashauri tulipanga ziara Mheshimiwa Waziri Mkuu akakague aone nini kimefanyika kwenye mradi ule. Hata hivyo, hao watu wa Kanda wa Umwagiliaji wakishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi waliifuta hiyo ziara katika mazingira yasiyofahamika na ni kwa sababu tu huu mradi umehujumiwa kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, Serikali iko tayari sasa kama hii awamu wanayotaka kuisema awamu ya tatu, kutukabidhi Halmashauri mradi huu tuutekeleze badala ya kuwaachia hawa watu wa Kanda ambao wamekuwa wakiuhujumu mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kutembelea mradi huu ili aangalie pesa hizi shilingi milioni 746 za Serikali ambavyo zimepotea bila sababu zozote zile za msingi? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na la mwisho, tuko tayari kuongozana na wewe kwenda kuangalia ule mradi. Kwanza nishukuru kwamba umekubali kwamba ule mradi tumetekeleza lakini mafuriko yalitokea, sasa kama tulivyojibu katika swali la msingi tutaunda timu ya wataalam tuipeleke kule iende ikachunguze na huo ndiyo utaratibu wa kisheria wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimuombe Mheshimiwa Mbunge tu kwamba Halmashauri ni taasisi ya Serikali, umwagiliaji ni taasisi ya Serikali, hawa wote wanafanya kwa niaba ya Serikali. Kwa sababu wote ni wa Serikali hakuna kitu chochote kwamba pengine Mkuu wa Mkoa alifuta ratiba ya Waziri Mkuu ili asije kuangalia mradi ule, tusilete mgongano kati ya Halmashauri na Idara ya Umwagiliaji iliyo chini ya Wizara ya Maji, zote ni Serikali.
Suala la msingi ni kwamba changamoto ipo, tushirikiane na Mheshimiwa Mbunge tutume timu ikaangalie na kama tulivyojibu kama kuna hujuma yoyote imetokea basi waliofanya hivyo watawajibishwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo Mradi wa Maji wa Haydom, Mradi wa Maji wa Chujio Wilaya ya Maswa na wenyewe umekuwa wa muda mrefu sana. Mkandarasi amepewa extension ya kwanza hakumaliza, akapewa ya pili, hakumaliza akapewa ya tatu hakumaliza.
Je, Serikali inaonaje kumwondoa huyu mkandarasi na kuweka Mkandarasi mwenye uwezo zaidi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mkandarasi yule amechukua muda mrefu katika utekelezaji wa mradi, lakini mradi ule uliharibiwa tangu wakati wa usanifu wake. Walisanifu kujenga chujio sehemu ambayo siyo yenyewe, baadaye walivyoingia katika eneo la mradi ikabidi tena wakae kubadilisha, lakini hali m ulipofikia kwa sasa amebakisha sehemu ndogo sana, ameagiza vifaa kutoka nje ya nchi, hatuoni kwamba kwa sasa itakuwa ni busara kumsimamisha kwa sababu vile vifaa vikishafika ni kazi ya kufunga tu na mradi unaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na nishukuru hata bwawa ambalo litahudumia lile chujio sasa hivi mvua zimenyesha maji yamejaa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ninakuomba uwe na subira baada ya muda kidogo tu huo mradi utaanza kufanya kazi. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa nia ya Serikali ni kumtua mama ndoo, kumsogezea huduma jirani ili kuweza kupata maji hasa vijijini na mijini; na kwa kuwa kuna miradi 17 mikubwa ya maji hasa fedha za kutoka India ambazo zilipitishwa kwenye bajeti hapa; na kwa kuwa Mji wa Makambako umekuwa ni miongoni mwa miji ya kupata mradi huu mkubwa wa maji katika miji ile 17.
Je, Serikali inawaambia nini wananchi wangu wa Mji wa Makambako ili waweze kupata maji, ni lini miradi hii itaanza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Deo Sanga kwa kufuatilia mradi huu wa mkopo wa dola milioni 500 kutoka Serikali ya India. Hata jana tulizungumza naye na alinituma niende kwa Waziri wa Fedha na majibu niliyopewa na Waziri wa Fedha ni haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu sasa zinakamilishwa ili tuweze kusaini mkataba wa fedha (financial agreement) na baada kukamilisha kusaini basi moja kwa moja Wizara ya Maji na Umwagiliaji itaanza kutangaza tender kumalizia usanifu ili pamoja na hiyo miji 17 bwawa lako la Tagamenda litajengwa ili Mji wa Makambako upate huduma ya maji.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nipate kuuliza swali moja dogo tu la nyongeza.
Nheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaipongeza Serikali kwa kutoa shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi wa maji wa Ntomoko kule Kondoa na Chemba.
Swali langu ni kwamba pamoja na Serikali kutoa fedha hizi mradi ule umehujumiwa Serikali inajua na wananchi wa Kondoa na Chemba wanajua na waliohujumu mradi huu wamehamishwa kutoka Halmashauri ya Kondoa kwenda Halmashauri nyingine. Nilitaka kujua ni nini kauli ya Serikali kuhusu hali hii? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli zipo dalili za ule mradi kuhujumiwa kutokana na utekelezaji kuchukua muda mrefu, lakini tumeamua kuchukua hatua mbili kwa sababu wananchi wa Kondoa/wananchi wa lile eneo wanahitaji maji tumechukua hatua mbili. Sasa hivi utekelezaji wa ule mradi tumeukabidhi kwa Mamlaka ya Maji Dodoma (DUWASA) wakati wowote tunatangaza tender.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuhakikisha kwamba sasa hawa wananchi wanapata huduma ya maji, ndiyo tunarudi nyuma kuangalia ni watu gani waliotufikisha hapa, kwa hiyo, stahiki zao zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria na Mheshimiwa Nkamia hata kama wamehamishwa hawajapelekwa nje ya nchi wako Tanzania hapa, kama mtu atabainika kwamba alihujumu atafuatwa, atakwenda kuchomolewa aliko ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. (Makofi)
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Muheza kuna mradi wa maji kutoka kwenye Kata ya Pongwe kuja Muheza Mjini, mradi ambao umeanza tangu mwaka 2016, lakini wananchi wa Muheza wamekuwa na wasiwasi juu ya ukamilishwaji wa mradi ule.
Mheshimiwa Waziri anaweza kutuambia ni lini wananchi wa Muheza tutapata maji kutokana na mradi ule ili kupunguza adha ya maji katika Wilaya ya Muheza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa
Naibu Spika, mradi wa Muheza ni kweli tumesaini mkataba mwaka jana na kazi inaendelea vizuri na juzi tumelipa fedha, tunatoa bomba la maji kutoka tenki la Pongwe kupeleka katika Mji wa Muheza. Sasa hivi mkataba bado unaendelea siyo kwamba mkataba umekamilika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba ule mradi ukisha kamilika maji yatapatikana Muheza.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE:Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Waziri nafikiri leo unatambua kwamba leo ndio tarehe ya mwisho ya ule mradi maji Chalinze, ninachotaka hapa ni kusikia kauli ya Serikali juu ya nini sasa kinafuata baada ya leo kuwa deadline ya ule mkataba wetu wa ujenzi wa Mradi wa Maji Chalinze?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kauli hiyo unayoizungumza iko katika taratibu za kimikataba, nikishauri tu Mheshimiwa Mbunge sisi wanasiasa watunga sera si vyema tuingilie mikataba, tusubiri kwanza utekelezaji wa mikataba ufanyike hatua zitakazochukuliwa basi tutazitolea taarifa.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali na pia natambua kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikifanya kazi nzuri kwenye suala maji. Nina maswali mawili ya nyongeza.(Makofi)
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni kweli kabisa kwamba tangu mradi huu uanze, wananchi wa Matamba, Nakinyika, Itundu na Mlondwe hawajawahi pata maji hayo. Nini kauli ya Serikali ya kuhakikisha kwamba inakamilisha mradi huo?
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Tarafa hii ya Matamba pia linafanana sana kwenye Kata za Tandala, Mang’oto pamoja na Ukwama; nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba pia Kata hizi tatu zinapata maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Norman Sigalla, nimefanya ziara kule na hilo tatizo nililikuta, kwamba mradi umetekelezwa lakini wananchi hawapati maji, lakini pia wananchi wameongezeka na tukakubaliana. Tumetengeneza mpango ambao utakuwa na gharama ya zaidi ya bilioni nne, na tutatekeleza miradi katika eneo lake katika hiki kipindi cha miaka miwili iliyobaki kwenda mwaka 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Norman Sigalla, amesimamia Halmashauri, andiko wameleta, tunakamilisha kulifanyia kazi ili utekelezaji uendelee. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Norman Sigalla pamoja na wananchi wa Matamba na Kinyika kwamba Serikali ya CCM itahakikisha ikifika 2020 wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza mradi mkubwa sana wa maji wa kutoka Ziwa Victoria kwenda Tabora na mradi huo kuna kipindi vifaa vya ujenzi vilikuwa vina mikwamo kwamo. Swali langu ni dogo tu, je, mradi huo umefikia kwenye hatua gani ya utekelezaji na wananchi wa Tabora wategemee kupata maji hayo lini? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji unaendelea vizuri sana, tulikuwa na matatizo machache ya kuhusu masuala ya msamaha wa kodi lakini tumeshayamaliza, na Mheshimiwa Mbunge wewe mwenyewe ni shahidi; wakandarasi wote watatu wameshaanza kazi, mabomba wanaendelea kuleta na sasa hivi kama unaenda barabara ya kwenda Dar es Salaam utakutana na malori yanabeba mabomba kupeleka Tabora; kwa hiyo mradi unaendelea vizuri. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukrani za wananchi wa Bagamoyo kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa namna ambavyo amesimamia ujenzi wa tenki kubwa la maji Bagamoyo, swali langu ni kuwa, je, lini mradi wa usambazaji wa mabomba ya maji katika Mji wa Bagamoyo pamoja na kata zote za Bagamoyo utaanza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Programu ya Maendeleo ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji katika Mkoa wa Dar es Salaam tunakaribia kuikamilisha. Baada ya kupata vyanzo vya maji tunayo maji ya kutosha, tuliweka makadirio ya dola milioni 100 kwa ajili ya usambazaji. Awamu ya kwanza tulipata dola milioni 32 na miradi hii inaendelea, ndiyo ambayo imejenga hilo tenki analolisema Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa hivi tumepata tena dola milioni 45 na mwezi huu tunatangaza tender ili tuweze kupata mkandarasi ili ahakikishe kwamba sasa tunaweka mabomba ya kusambaza maji katika maeneo yote likiwemo eneo la EPZ kule Bagamoyo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake kwamba huduma ya maji katika eneo lake tunakamilisha. (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Waziri wa maji kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri mradi wa maji wa Mombo - Mlembule ulikuwa wa Serikali imetenga shilingi milioni 900 lakini cha kushangaza sasa hivi mradi huo umekuwa wa shilingi bilioni nne. Nini tamko la Serikali kuhusiana na mradi wa shilingi milioni 900 mpaka ukafika shilingi bilioni nne? Hizo shilingi bilioni nne ni kwa ajili ya mradi gani mwingine?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tulikuwa na mradi wa shilingi milioni 900, lakini usanifu wake haukuhusisha vijiji vya Mji wa Mombo pamoja na maeneo yanakotoka maji Vuga. Kwa hiyo tukafanya review, hiyo review sasa imekamilika lakini sina taarifa kwamba hiyo review imefikia shilingi bilioni nne.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba baada ya Bunge hili leo mimi na wewe twende pamoja, nitakusanya wataalam wangu ili tuweze kuangalia mradi huo uweze kutekelezwa haraka.(Makofi)
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniruhusu niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwanza naipongeza Serikali kwa kuhakikisha kwamba miradi ya Kayenze, Kakora, Ikangala, Nyamtukuza na Kharumwa inakamilika, hongera sana kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sasa napenda kuuliza, je, Serikali inaweza ikawaambia watu wa Nyang’hwale ni lini sasa huu mradi mkubwa wa vijiji tisa utakamilika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Wilaya ya Mbogwe ipo jirani kabisa na Wilaya ya Kahama ambako kuna mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria, je, Serikali haioni kwamba ni wakati sasa umefika kuiweka Wilaya yetu ya Mbogwe katika programu ya kuweza kupata maji haya kutoka Kahama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tuwahakikishie wananchi kwamba mradi huu utakamilika. Mradi huu wa Nyang’hwale umepata shida kidogo ya kiutendaji na shida yenyewe ni kwamba Halmashauri ilitafuta mkandarasi mwingine wa kuleta mabomba na mkandarasi mwingine wa kujenga. Sasa yule mkandarasi wa kujenga hawezi kufanya kazi kama wa kuleta mabomba hajaleta na yule wa kuleta mabomba inaonekana kwamba ni kama kidogo yupo dhaifu kwa sababu hadi leo hajaleta mabomba na mkataba ni wa tangu mwaka 2014 mwezi wa pili. Hivi tunavyoongea sasa hivi ni kwamba tayari yapo mazungumzo kati ya Wizara yangu na Halmashauri ya Nyang’hwale kuhusiana na huyu mkandarasi ambaye ameshindwa kutekeleza majukumu yake na mkataba wake ulikuwa ni wa shilingi bilioni tano. Yule mkandarasi wa kujenga tayari ameshakamilisha matenki, anachosubiri ni mabomba aweze kuyalaza ili wananchi wapate maji.
Kwa hiyo, hili Mheshimiwa Mbunge tunalishughulikia na mara tutakapomaliza nitakupatia majibu ili wananchi sasa waweze kuwa na uhakika ni lini hayo maji yatapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Mbogwe, kwa sasa tunaendelea, tayari kuna visima ambavyo tumechimba na kwa sasa Halmashauri imesaini mkataba wa visima sita ili tunaposubiri mradi mkubwa na kwa kuwa Geita ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata msaada wa hizi fedha kutoka Serikali ya India, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia fedha hiyo basi tutaendelea kuhakikisha pia na Mbogwe inapata maji kutoka Ziwa Victoria.
Pia unayo fursa nyingine kupitia bomba la Lake Victoria linalokwenda Solwa, napo tayari tunaanza kuangalia kama tunaweza tukachukua maji kutoka Kahama pale kwenda kwenye ile milima kilometa 40 na baadaye tukayashusha kwenda Mbogwe. Wataalam wanafanyia kazi kama hilo litakuwa limekaa vizuri basi pia unaweza ukapata maji kutoka bomba la KASHWASA. (Makofi)
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, tatizo hili la maji katika Wilaya ya Nyang’hwale linafanana kabisa na tatizo la maji Mtwara Mjini na kwa kiasi kikubwa Mtwara Mjini kuna mradi ambao ulipangwa kutekelezwa kwa kupata pesa kutoka Benki ya Uchina ambapo mpaka sasa bado hizp pesa hazijapatikana.
Juzi nilikuwa namuuliza Mheshimiwa Waziri akaniambia kuna pesa zingine zimesainiwa maji yatoke Bonde la Ziwa Kitele mpaka Mtwara Mjini.
Je, Serikali iko tayari hivi sasa kutekeleza mpango wa muda mfupi wa kuchimba visima kwa kutumia gari za Idara ya Maji ambazo zipo pale Mtwara katika maeneo ambayo maji hakuna kama Kata ya Ufukoni na Likombe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba Mji wa Mtwara unapata maji safi na salama. Mwezi uliopita tumesaini mkataba wa shilingi bilioni tano ambao utatoa maji Mbuo kwenye Bonde la Kitele kupeleka mjini. Kwa bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge wewe ni Mbunge wa Mji wa Mtwara, kwa hiyo, maeneo yote ambayo yalikuwa hayajapata maji safi tunahakikisha kwamba yanapata hata kabla ya huo mradi mkubwa wa kutoa maji Mto Ruvuma kuleta Mtwara Mikindani.
Mheshimiwa Spika, pia kuhusiana na huu mradi mkubwa wa kutoa maji Ruvuma, tayari Serikali iko kwenye hatua za mwisho kukamilisha mazungumzo na Exim Bank ya China ili sasa utekelezaji uanze. Kwa hiyo, nikuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba uvute subira Serikali yako kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inaendelea kuzungumza na hawa wafadhili kwa maana ya Waziri wa Fedha (Hazina) wanaendelea kuzungumza na mfadhili ili mambo yakikamilika tuanze utekelezaji.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mji wa Itigi wenye Kata tatu za Majengo, Itigi Mjini na Tambukareli na vijiji saba vya Kihanju, Songambele, Tambukareli, Majengo, Ziginali, Itigi Mjini na Mlowa havina kabisa huduma ya maji toka nchi hii ipate uhuru na hata kabla ya wakati huo ikitawaliwa na mkoloni na kwa kuwa Halmashauri yetu inafanya juhudi na tumeandika barua kwa Wizara ya Maji kuomba Mhandisi wa Wizara hii aje atushauri namna gani ya kuweka miundombinu ya maji na kwa kuwa hadi leo hatujapata majibu.
Mheshimiwa Spika, nini kauli ya Serikali kwamba dhamira ya Serikali ikoje kuwasaidia wananchi wa Itigi na wenyewe wapate huduma hii ya maji kwa kuleta Mhandisi aweze kutushauri namna ya kuweka miundombinu ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikuhakikishie kwamba kutokana na utaratibu uliowekwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji Awamu ya Tano ya kuhakikisha kila Halmashauri inatengewa bajeti, tumeendelea kutenga bajeti kwa kila Halmashauri ili waweze kutekeleza miradi ya maji katika Halmashauri zao kwa sababu wapo karibu na wanaelewa matatizo yanayowazunguka.
Mheshimiwa Spika, nakiri ni kweli Mheshimiwa Mbunge uliniambia kwamba barua kuomba wataalam kutoka Wizara ya Maji inawezekana imeshakuja tayari lakini nitaifuatilia. Tatizo kubwa ambalo liko kwenye Halmashauri yako ni kukosa wataalam wenye weledi na tuliongea na kushauriana kwamba sasa ulete barua ili tuweze kukusaidia wataalam ama tukuchukulie wataalam kutoka Mamlaka ya Maji ya Singida au Makao Makuu ili wakasaidiane na wataalam wa Halmashauri yako kuhakikisha kwamba tunafanya usanifu wa haraka na ulio bora na utekelezaji uendelee. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba tutakupatia wataalam Mheshimiwa Mbunge.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kero ya maji iliyopo Nyang’hwale inawasumbua sana wanawake wa Wilaya ya Kongwa na Mheshimiwa Naibu Waziri nimekuuliza mara nyingi ukipita hapa jirani yangu kuhusu Wilaya ya Kongwa na ukaniambia umetoa fedha kwa ajili ya maji Wilayani Kongwa. Visima vinavyotoa maji Wilayani Kongwa havizidi vitatu, visima vingine vilivyobaki vilivyochimbwa na World Bank havitoi maji. Ni jana tu nimeongea na Mkurugenzi wa Kongwa akaniambia shida ya maji ya Kongwa ipo palepale, maji yanayotoka ni kwa maeneo machache sana.
Naomba leo Naibu Waziri aniambie maji yatatoka lini Kongwa ya kuwatosha wanawake wa Kongwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nina umakini mkubwa sana na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa nimeifanyia kazi sana tangu nakuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Ni juzi tu nilipeleka mtambo wa kuchimba visima Kongwa na kwamba tayari kuna visima vya kutosha ambavyo vimechimbwa lakini siyo kwamba tumekamilisha Jimbo zima au Halmashauri nzima ya Kongwa, kwa hiyo, tunaendelea. Kama bado kuna maeneo yanahitaji kupata visima tupo tayari kuendelea kuchimba na hasa kwa kuzingatia kwamba katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 tumeweka fedha tena kwa ajili ya kuendelea kuwapatia akina mama maji.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie mama yangu Mheshimiwa Bura kwamba sisi tumedhamiria kuhakikisha kwamba kweli tunamtua mama ndoo kichwani. Yule ambaye hatatuliwa ndoo kichwani ni kwamba atakwenda kuchota maji umbali usiozidi mita 400 kutokana na sera yetu. Kwa bahati nzuri na mimi mwenyewe naishi Dodoma Mama Bura, kwa hiyo, tutakuwa pamoja na kwa vyovyote vile tuambatane tukaangalie maeneo mengine ambayo hayana ili tuweze kuyapatia maji. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ili kulinda Kiti cha Spika kwa sababu wewe huwezi kuuliza swali la nyongeza, naomba nikiri kwamba Mji wa Kongwa tumepata kisima ambacho kinatoa maji mengi. Sasa hivi kinachotakiwa ni kupeleka fedha ili tuweze kujenga miundombinu. Naomba nikuahidi kwamba tutapeleka fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ili wananchi wa Kongwa waweze kupata maji ya kutosha. (Makofi)
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa takwimu hizi, kutokana na bajeti ya Mheshimiwa Waziri, bado Serikali hii haijajipanga kutatua tatizo la maji nchini. Mkoa wa Katavi una vituo zaidi ya 148 vinahitaji ukarabati na hivi tunavyoongea, wakazi wa Mpanda pamoja na Katavi hawajapata maji karibu wiki mbili zimepita. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha hivi vituo 148 vinafanyiwa ukarabati na wananchi wanapata maji kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani na kuunda Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mkoa wa Katavi tayari tumeshachimba visima zaidi ya 40 na wananchi wanapata maji. Kwa hiyo, huduma ya maji katika Mkoa wa Katavi imeongezeka. Kwa sasa tumeshasaini mkataba mmoja ili kuleta bomba lingine kutoka Ikorongo kwa ajili ya Mji wa Mpanda na tayari mkandarasi yuko kazini na tunatarajia kusaini mkataba mwingine wa pili ili kuongeza kiwango cha maji kutoka kilichopo sasa hivi cha lita 3,150,000 ili twende zaidi ya lita milioni sita. Kwa hiyo, kwanza ni kwamba maji Katavi tayari yanaendelea kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, lakini pili tulipeleka mashine ili kufanya ukarabati wa visima vyote ambavyo vilikuwa havitoi maji kwa maana ya kuvifanyia flushing na zoezi hilo limefanyika na linaendelea kufanyika ili kuhakikisha vile visima ambavyo uwezo wake wa kutoa maji ulikuwa umepungua basi vinaendelea kutoa maji wananchi waendelee kupata huduma. Kwa hiyo, si kweli kwamba Serikali imeshindwa kutoa maji, tayari kiwango kilichokuwepo tumeongeza na tunaendelea na tutafikisha asilimia 85 itakapofika mwaka 2020.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa ninasikitika tu kwamba hili swali halijajibiwa; kwa sababu hapa nilizopewa ni story tu, nimeona hapa zimepatikana story tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tatizo letu Liwale ni kwamba Mji wa Liwale unategemea maji kutoka Mto Liwale na Mto Liwale sasa umekauka, kwa hiyo, shida yetu ni kutafuta chanzo cha pili mbadala cha maji. Sasa hapa Mheshimiwa Waziri anasema kwamba hatua ya awali yaani kwa muda mfupi wanakarabati matenki, wanakarabati chanzo cha maji na wananunua dira. Sasa unakarabati chanzo cha maji, unakarabati vipi? Mto umekauka unaukarabati vipi? Matenki unayokarabati unataka uweke nini na mita unazokwenda kufunga unataka zitoe nini? Hapo naona swali bado halijajibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, katika muda mrefu wanasema wametenga shilingi bilioni 3.5 lakini hizi shilingi bilioni 3.5 kuna Halmashauri 14 zimewekwa hapa. Kwa nini sasa Mheshimiwa Waziri hajatenganisha kujua kwamba Halmashauri fulani ina kiasi gani maana kuzifumba hapa ni nini?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ninalouliza mo wamba, scheme ya Umwagiliaji ya Ngongowele itakamilika nini? Nimepewa story tu. Sasa nataka nijue hatua gani imefikiwa ili tuweze kupata chanzo cha maji mbadala kwa Mji wa Liwale, hilo ndio swali ambalo naomba niulize. Vilvile naomba nirudie, tunaomba mradi wa Ngongowele ukamilike. Je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kwenda na mimi kuangalia huo mradi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, utangulizi umesema majibu yote ni story, sio story ndiyo ukweli ulivyo. Mto Liwale ambao ndiyo chanzo cha maji cha Mji wa Liwale unakauka kiangazi na ndio maana tunaweka sasa upembuzi yakinifu. Lakini nikwambie maana ya ukarabati, ukarabati ni kuongeza uwezo ndani ya huo ukarabati basi tutabaini ni eneo gani sasa baada ya mto kukauka tunaweza tukapata maji ambayo yatahakikisha yanahudumia Mji wa Liwale bila matatizo yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye swali namba moja; hatua tunayoichukua ni kufanya upembuzi yakinifu, upembuzi yakinifu utabaini chanzo cha maji cha kudumu pamoja na huo Mto Liwale. Ikiwa siwezi kuanza kuzungumza utafiti utakaofanyika lakini baada ya kufanyika itabainisha ni wapi tutakuwa na maji ambayo yatakuwepo kwa miezi 12 ama kwa visima ama kwa kujenga bwawa ili yale maji yanapokuwa ni mengi kipindi cha kiangazi tuyapeleke kwenye bwawa tuyahifadhi ili tuweze kuhakikisha kwamba sasa Mji wa Liwale unakuwa na maji mwaka mzima. Ndio hatua tunayoichukua sasa hivi tunachukua hatua ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeuliza swali kuhusu mradi wa umwagiliaji utakamilika lini. Mradi ule ulikamilika, umepata madhara ya mafuriko. Sasa hivi tumepata fedha kutoka Serikali ya Japan, tunapitia miradi yote ambayo ilikuwa imekamilika lakini imepata matatizo mbalimbali yakiwemo ya kukosa maji, unakuta kwamba kilimo kinafanyika mara moja badala ya mara mbili. Kwa hiyo, tunafanya mapitio ya hiyo miradi ikiwemo mradi wako wa Ngongowele ili tuweze sasa kuhakikisha kwamba tunauimarisha ili wananchi waweze kunufaika na kile walichokitarajia. (Makofi)
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha kutokukamilika mradi wa maji wa Kibara, mradi wa maji wa Bulamba na mradi wa maji wa Nyabehu na hata Mheshimiwa Waziri Mkuu Pinda alifika maeneo yale na Mheshimiwa Maghembe. Sasa nataka kujua miradi hiyo mitatu kwasababu ni zaidi ya miaka nane itakamilika lini kwa sababu Mbunge wao amepiga kelele sasa mpaka hata mate yamenikauka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, umesema kwamba mradi umechukua miaka nane ni ukweli. Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji tumeianza kwenye bajeti ya mwaka 2006/2007; kwa hiyo, umakta ijumlisha mpaka leo unakuta inakwenda kwenye hiyo miaka saba mpaka miaka nane. Ndani ya hiyo programu tulikuwa na miradi 1810, hadi leo tumeshakamilisha miradi 1333, bado 477. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndani ya hiyo ambayo imebaki ni pamoja na miradi yako Mheshimiwa Mbunge na tumeendelea kutenga fedha na mwaka wa fedha huu tulionao 2016/2017 tuliamua sasa kila Halmashauri kuiwekea bajeti, tukaweka maelekezo kwamba wakamilishe kwanza miradi inayoendelea kabla ya kuingia kwenye miradi mipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Mbunge, kama kuna changamoto yoyote ile ambayo kama Wizara tunaweza kuingilia kitaalam basi naomba tuwasiliane ili tuweze kushughulikia hilo kuhakikisha kwamba miradi hiyo imekamilika.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wanawake wa Mkoa wa Singida wametaabika sana na kero kubwa ya ukosefu wa maji safi na salama kwa muda mrefu sasa. Je, Serikali haioni imefika wakati muafaka wa kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria kupitia Igunga hadi Mkoa wa Singida ili kuwaondolea wananchi wa Mkoa wa Singida kero hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikupongeze wewe ni mama na unawapenda akina mama na unajua jinsi wanavyopata shida ya maji. Mkoa wa Singida ni miongoni mwa Mikoa ambayo haina vyanzo vya uhakika vya maji na mabwawa yaliyopo kama Kindai, Lake Singidani yote yana maji ya chumvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa mawazo mazuri na sisi tunawaza hilo. Kupitia mradi wa maji wa Ziwa Victoria sasa tunafikisha maji Igunga tunafikiria kwamba tufanyeje kuyatoa pale Igunga tupandishe Mlima Sekenke ili yaje mpaka Singida. Hayo ni mawazo namba moja ambayo na sisi tunayapokea, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba tutayafanyia kazi. (Makofi)
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona.
Kwa kuwa katika Mkoa wa Njombe na hasa katika Halmashauri ya Mji wa Njombe kumekuwa na tatizo kubwa sana la maji kwa muda mrefu, kuna mradi wa Hagafilo ambao wananchi wale waliahidiwa kwamba wataletewa mradi huo na kwamba fedha zingetoka huko India lakini hadi sasa hakuna chochote kinachoendelea. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ni kweli Mji wa Njombe unapata huduma ya maji kutoka kwenye Mto unaopita pale Njombe na hiyo huduma haitoshelezi, lakini ni kweli kwamba Mji wa Njombe ni kati ya Miji 16 ambayo itafaidika na mkopo kutoka Serikali ya India.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ni kwamba kinachoendelea ni kwamba Kamati ya Madeni Hazina imeshakaa na kuridhia mkopo huo wa dola milioni 500. Kwa sasa Serikali kupitia Hazina wanakamilisha taratibu za kusaini ile financial agreement, pia Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji sasa hivi inaandaa makandarasi watakaofanya usanifu wa haraka ili tuweze kuwaza tenda kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya huo mradi kukamilika nikuhakikishie Mheshimiwa Mlowe kwamba Mji wa Njombe sasa utakuwa na maji ya uhakika ambayo wananchi watapata maji safi na salama kwa wakati wote.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru tu Serikali kwa huu mradi wa World Bank wa Euro milioni 54 kwa niaba ya Jimbo la Nyamagana pamoja na Ilemela. Lakini niseme tu kwa hali ya kawaida kama wananchi wa Jimbo la Nyamagana wangekuwa wanapata maji kwa asilimia 90 sidhani kama Mbunge wao ningekuwa na sababu ya kusimama hapa na kuomba maji. Niseme tu ukweli ni kwamba inawezekana mtandao wa maji umesambazwa kwa kiasi kikubwa lakini upatikanaji wa maji sio sawa na takwimu zinavyosomwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; zipo Kata za Buhongwa, Lwanima, Kishiri, Igoma na Nyegezi ni lini Serikali itakuwa tayari pamoja na huu mradi wa Euro milioni 54 kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha zingine nyingi zaidi ili wananchi kwenye maeneo haya ya Buhongwa na maeneo ya Lwanima na Kata zingine nilizotaja waweze kupata maji kwa uhakika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pale kwenye
Jimbo la Ilemela umekuwepo mradi wa Vijiji kumi toka mwaka 2010 mpaka hivi tunavyozungumza leo ni Kijiji kimoja peke yake cha Kayenze ndio kimepata maji.
Ni lini Serikali itahakikisha Vijiji vya Nyamadoke, Kahama, Kabangaja, Igogwe, Igombe, Kabusungu na Nyafula vinapata maji haya kwa wakati kama ambavyo ilikuwa imekusudiwa? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kumpokea Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kila wakati anakuja ofisini kuhusu Mradi wa Maji wa Nyamagana, ndiyo maana Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na juhudi za wafanyakazi wote na Serikali tumehakikisha kwamba tumepata hizi Euro milioni 54 tukiwa pamoja na Mheshimiwa Mbunge. Maana yake kila wakati alikuwa anakuja kuzungumza kuhusu wananchi wake na amekuwa anasema inakuwa ni aibu kwa sababu Ziwa Victoria liko pale na watu hawana maji, ndiyo maana amesaidia katika kulisukuma hili ili tuweze kupata mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia baadhi ya Kata. Mradi huu utakapokuwa umekamilika zipo kata ambazo zitapata huduma ya maji, Kata hizi ni pamoja na Kishiri, Buhongwa, Bugarika, Nyegezi, Lwanima pamoja na Igoma. Aidha, vitongoji ambavyo vinazunguka katika hizo kata tutahakikisha kwamba zimepata maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema kwamba tunakarabati miundombinu iliyopo, ikiwa ni pamoja na mabomba yaliyochakaa, yakichakaa maana yake kupeleka huduma ya maji kwa wananchi inakuwa kidogo kuna shida tutahakikisha sasa na vijiji vingine vyote vilivyobaki vinapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia amehoji kuhusu tamko la asilimia 90. Hesabu ya asilimia 90 tunaihesabu kwa kuchukua population ya watu waliopo katika lile eneo na kuangalia ni watu wangapi wanaopata maji, hatu-cross over kwenda kwenye vijiji vyote, hapana! Tunaangalia una watu wangapi katika Kata ya Nyamagana, je, ni wangapi ambao wanapata maji ndiyo tunapiga mahesabu kuhakikisha kwamba sasa hiyo asilimia tunaipata. Kwa hiyo, kunaweza kukawa na Kata lakini kwa sababu zina watu wachache ukakuta kwamba asilimia hii ni kubwa kumbe kuna Kata ambazo bado hazijapata maji. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo tumeendelea kushirikiana kufuatilia suala la wananchi wa Nyamagana kupata maji, tuendelee kuwasiliana ili kuona ili mradi utakapokamilika kusiwe na eneo litakalobaki bila kupata maji. (Makofi)
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kwanza naishukuru Serikali kwa kutupa mradi wa maji pale Magu Mjini, mkandarasi yuko site; lakini pia nipongeze Kampuni ya Alliance Ginnery, mwekezaji amechimba kisima kirefu pale salama na kinatoa lita 9,000 kwa saa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala hili la Nyamagana linafanana kabisa na Jimbo la Magu, kijiografia na kwa fursa zilizopo. Katika Tarafa ya Sanyo kwa maana ya Kisesa yote na vijiji vyake pamoja na Tarafa ya Ndagalu kuna hali mbaya sana ya maji katika Vijiji vya Ng’aya, Salama, Ndagalu, Nyabole, Kabila na Mahala...

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwa sababu Halmashauri tumeomba dharura, ni lini Serikali sasa itatupatia fedha kwa ajili ya kuchimba visima virefu ili tuweze kusaidia wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa kwamba tumesaini mradi mkubwa ili kupata maji Wilaya ya Magu Mjini, lakini nikiri kwamba kuna kata ambazo ziko pembezoni na huo Mji ambazo bado hazijapewa huduma ya maji, lakini nichukue ombi lako, tuhakikishe kwamba tunapeleka visima, nikuombe Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane. Sio wewe tu katika tarafa zako, zipo tarafa nyingi, wengine ni majirani zako, pale Kasoli hakuna maji. Kwa hiyo, niombe tuwasiliane ili tuweze kuangalia tufanyeje kupitia kwenye bajeti zako au maeneo mengine yoyote utakayoona yanawezekana tuhakikishe kwamba hayo maeneo yaliyobaki ya vijiji nayo pia yanapata walau dharura kwa kuchimbiwa visima kama maji yatakuwepo chini ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lengo la Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhakikisha kwamba wananchi wote wa Tanzania popote pale walipo, tunawapatia maji safi na salama. (Makofi)
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam bado ni mkubwa sana, hasa kwenye maeneo ambayo hayana miundombinu ya maji. Miradi ile mikubwa ya maji imeainishwa kwamba itatekelezwa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa Serikali itatekeleza miradi hiyo ya maji ipasavyo ili wananchi hao wa Mkoa wa Dar es Salaam waweze kupata maji kwa uhakika na umakini, hasa kwenye maeneo ya Makabe, Goba, Msigani na maeneo yote ya Gongo la Mboto? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kama tulivyotoa taarifa katika Bunge hili, tumekamilisha miradi miwili mikubwa, Ruvu Juu na Ruvu Chini. Ruvu Chini inatoa lita milioni 270 kwa siku, Ruvu Juu inatoa lita milioni 196 kwa siku, pia mwezi huu tunakamilisha vile visima 20 Mpera na Kimbiji ambavyo vitatoa lita milioni 260 kwa siku. Kwa hiyo huduma ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam na sehemu ya Pwani itakuwa ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko changamoto ya kupeleka miundombinu, kwa sasa hivi tumesaini mkataba mmoja wa bilioni 32 ya kuweka mtandao wa maji pamoja na kuongeza matenki ya kuhifadhi maji kupeleka kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tumeshafanya mipango tayari, tunahitaji dola milioni 100 ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakamilisha usambazaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam. Tunaendelea baada ya muda ambao siyo mrefu sana tutaona kwamba vijiji vyote, maeneo yote, mitaa yote ya Dar es Salaam inapata maji safi na salama, kwa sababu maji yapo kilichobaki ni kusambaza.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Pamoja na Jimbo la Mbeya Vijijini kuzungukwa na milima inayotiririsha maji mwaka mzima, lakini wananchi katika vijiji vingi hawana maji salama.
Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu kwa kuwapatia maji salama wananchi wa vijiji vya Mbeya Vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tunaendelea na usanifu na baadhi tumeshasaini mikataba kwenye Jimbo lake kuhakikisha kwamba wananchi wote wa Mbeya Vijijini, Jimbo la Mheshimiwa Mbunge wanapata maji safi na salama. Tulikuwa tumebuni miradi kwenye vijiji kadhaa lakini baadae tukagundua kwamba yale maji yatakwenda kwenye kijiji cha mwisho na kuacha vijiji vya katikati, tumechelewa kwa sababu ya kuhakikisha kwamba tunaainisha na vijiji vya katikati. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwaka ujao wa fedha mapema kabisa tutasaini mikataba, na mimi Mheshimiwa Waziri ameshanipangia ratiba, katika ratiba Mikoa nitakayoizungukia ni pamoja na Mkoa wa Mbeya. Kwa hiyo ntahakikisha tunaambatana na wewe kwenda kwako ili tuweze kuona hivyo vijiji vyenye uhaba mkubwa wa maji.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza niishukuru Serikali kwa kupeleka fedha kwa ajili ya miradi hii ambayo imeorodheshwa, lakini kwa uhalisia ni kwamba miradi hii haijakamilika kwa asilimia mia, miradi miwili mradi wa Mfyome na Mradi wa Magunga – Isupilo kuelekea Lumuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii kwa sababu imekaa kwa muda wa miaka miwili haijakamilika na Halmashauri imeshapelekwa Mahakamani kwa ajili ya kufanyiwa arbitration, napenda sasa kupata commitment ya Serikali ikiwa kama arbitration itaenda kinyume na matakwa ya Serikali, yaani Serikali ilipe fedha hizi kwa mkandarasi, itatumia mida gani kukamilisha malipo haya kwa wakandarasi ili wananchi wangu waweze kupata maji katika miradi yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika utaratibu wa kutafuta wakandarasi, Serikali inawaagiza wakandarasi kununua vifaa na hivyo katika ununuzi wa vifaa wakandarasi hawa wanatozwa kodi ya VAT, lakini wakati wa malipo baada ya kupeleka zile certificates Wizarani, Serikali hailipi zile fedha ambazo wakandarasi wameingia kwa maana ya VAT na hivyo basi miradi inaendelea kusimama…

MHE. GODFREY W. MGIMWA: ...miradi inaendelea kusimama kwa sababu ya kutofanyika kwa malipo haya. Napenda kujua, je, Serikali ina mtazamo gani sasa kuhakikisha kwamba VAT inalipwa kama fidia kwa hawa Wakandarasi ambao wako katika miradi hii? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linahusu shauri lililopo katika taasisi inayoitwa Arbitration, kwamba je, ruling ikishatokea Serikali italipa Mkandarasi kwa muda gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, swali hili nilijibu tu kwamba shauri linaendelea na linazungumzwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za mikataba, kwa hiyo ruling itakapofikia pia tutalipa kutokana na taratibu zinazoendelea za kimkataba bila wasiwasi wowote. Labda niseme, nikuhakikishie kwamba Hazina, Serikali yako ya Awamu ya Tano kwa sasa hatuna mgogoro mkubwa; wakandarasi wakishaleta certificate wakati wowote tunalipa, hatuchukui muda mrefu. Kwa sasa nina shilingi bilioni saba, angeleta hata leo basi tusingechukua wiki moja tungekuwa tumeshamlipa tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili linahusu kodi, VAT; Mheshimiwa Mbunge, sisi tushughulikie utekelezaji wa miradi. Serikali imejigawa katika taasisi mbalimbali, suala hili lina wahusika na wahusika hao wameainishwa katika mikataba na Mkandarasi anajua inapofikia suala la VAT aende wapi. Kwa hiyo, tuliache suala hili litekelezwe na wahusika ambao ni watu wa TRA.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Mchinga, katika vijiji vya Lihimilo na Kitowavi katika mwaka wa fedha 2016/2017 vilichimbwa visima ambavyo vinahitaji umaliziaji wa takribani kama shilingi milioni 142 kwa kisima kimoja na kingine shilingi milioni 132. Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba tayari wanazo pesa shilingi bilioni saba na anajua nimeshamsumbua sana juu ya suala hili, nihakikishie sasa ni lini hizi fedha, shilingi milioni 142 kwa Lihimilo na shilingi milioni 132 kwa Kitowavi mtazipeleka ili mkakamilishe vile visima?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri yeye mwenyewe ni Mjumbe, kwenye hii Kamati ya Maji na Umwagiliaji. Tumeweka utaratibu Mheshimiwa Mbunge, visima tumechimba, maji yamepatikana kilichobaki ni miundombinu. Utaratibu wetu tuliouweka, mwambie Mkurugenzi wako, wewe ni Diwani kwenye Halmashauri Mkurugenzi aingie mikataba na wakandarasi kwa ajili ya miradi ya kusambaza hayo maji kupeleka kwa wananchi, wakishasaini, wakitekeleza, certificate ikapatikana, Mheshimiwa Mbunge nakuomba uiwasilishe hata kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba hatupeleki hela bila kuwa na hati ya madai, tulifanya hivyo huko nyuma tukapata shida sasa hivi tumeboresha na niwaambie tu kwamba tumekwenda vizuri sana, hadi mwezi wa nne tarehe 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana na Hazina wanaendelea kuleta fedha, Wizara ya Maji kupitia Mfuko wa Maji tumeshapokea shilingi bilioni 118. Kwa hiyo, fedha tunayo, wakamilishe huo mradi walete tutalipa hiyo hela.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Bunda kuna miradi ya maji ya Nyamswa, Salama Kati, Mgeta, Nyang’alanga, Kiloleli, Nyabuzume, Kambugu na mradi wa umwagiliaji wa Maliwanda. Miradi yote hii ni ya muda mrefu sana. Nataka kujua tu Waziri kwamba hii miradi ambayo tayari mingi wameshaitolewa fedha na haijakamilika kwa muda mrefu, ni lini sasa hii miradi itakamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni mara kama ya nne kuuliza maswali haya kwenye Bunge hili.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikiri, sio kwamba amekuja mara nyingi tu lakini ameandika barua zaidi ya mara tatu kulalamikia utekelezaji wa miradi katika Halmashauri yake ya Bunda, na kwamba fedha nyingi zimepelekwa, sio na Wizara ya Maji tu, zimepelekwa fedha na Wizara ya Maji, zimepelekwa fedha na JICA shilingi milioni 207 nakumbuka, lakini kuna own source pia ya Halmashauri imetoka miradi ile haijakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona nitume watalaam wangu wa Wizara ya Maji waje kwako kuangalia hili baadae mimi pamoja na wewe tutakwenda kuangalia kuna tatizo gani, kama alivyosema Mwenyekiti pengine kuna shida ya makandarasi au kuna shida ya utekelezaji kwenye Halmashauri kama tulivyobaini katika maeneo mengine.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa watu wanaokwenda kwenye Magereza ni wahalifu na huwa wamehukumiwa, naomba Wizara ya Mambo ya Ndani iniambie na itoe kauli hapa, ni lini Gereza la Muleba litaenda kuzungushiwa fensi, maana yake leo Gereza la Muleba lina uzio kwa maana wafungwa wakiamua kuondoka leo, kesho wanaondoka, mtawakamata wale viongozi bure, sasa nataka commitment ya Serikali ni lini itafanya emergence ya kwenda Muleba kuweka uzio wa Magereza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli Gereza la Muleba linahitaji kuwekewa uzio, tunatambua na tumejipanga kwamba wakati wowote ambapo tutakamilisha kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio huo tutafanya hiyo kazi. Jambo hilo tunalitambua na lipo katika vipaumbele vyetu.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza linahusu tafsiri ya kijiji kwenye huu usambazaji wa maji. Ninataka kujua anaposema maji yatafika Kijiji ya Ilagaja, Kijiji cha Ilagaja kina Vitongoji kumi. Je, maji yatafika makao makuu tu ya kijiji au katika vitongoji vyote kumi vinavyounda Kijiji cha Ilagaja?
Swali la pili, sasa maji haya yatakapofika Nzega na kwa sababu maeneo yetu ya Bukene yana shida ya water table kupata maji kutoka chini. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuanza mipango ya muda wa kati ili maji haya sasa yatakapofika Nzega yatoke Nzega yafikishwe Bukene ambako ni umbali wa kilometa 40?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameomba tafsiri kwamba maji yatafika Kijiji cha Ilagaja, je, vitongoji itakuwaje?
Naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kuwa lengo letu ni kuhakikisha kwamba maji safi na salama yanawafikia wananchi wote. Yatatoka Nzega ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya, yataenda Ilagaja yakifika pale basi tutaendelea kuyaendeleza kwenda mpaka kwenye vitongoji mpaka kwenye point ya mwisho ili wananchi wote eneo la Ilagaja na vitongoji vyake wapate maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na labda tu nizungumze kwamba ndio maana katika bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji tunatenga fedha kwa kila Halmashauri. Bomba la KASHWASA maji ya kutoka Ziwa Victoria yakishafika kwenye kitongoji kwa upande wa Halmashauri kile ndio chanzo cha maji, zile fedha tunazotenga basi muendeleze mpeleke kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, jibu lake ni hivyo hivyo kuwa yakishafika pale basi Halmashauri kile ndio chanzo, watenge fedha waunganishe kutoka pale kwenda kwenye maeneo ambayo hayana maji. (Makofi)
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza Wizara swali lifuatalo; kwa kuwa mradi wa vijiji kumi vya maji umefika mpaka Nduguti ambako ndio Makao Makuu ya Wilaya ya Mkalama na chanzo cha maji kimepatikana. Sasa ni lini Wizara itajenga miundombinu ili watu waweze kunywa maji na hiyo ni Wilaya kamili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kwanza ya sekta ya maji ni kutafuta chanzo. Chanzo kikishapatikana kinachofuata sasa ni kuyasambaza maji kuyapeleka kwa wananchi na ndio maana kama nilivyosema kwamba tunatenga fedha. Kwa hiyo, baada ya chanzo kupatikana tayari tumetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri na kwa sababu fedha iko kwenye Halmashauri na wewe ni Diwani katika hiyo Halmashauri basi tushirikiane kuyatoa maji pale yalipopatikana tuwapelekee wananchi. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, pamoja na Mkoa wa Rukwa kupata mvua nyingi kuwa na Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika wananchi wake bado wanapata adha kubwa ya maji. Serikali haioni umuhimu wa kutumia Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika kuwafikishia maji wananchi hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa, Mji wa Sumbawanga mwaka huu wa fedha tumekamilisha mradi mkubwa ambao unatoa lita milioni 13 kwa siku, kwahiyo wananchi wa Sumbawanga wanapata huduma ya maji safi na salama. Lakini pili, katika mwaka ujao wa fedha tayari Mkoa wa Rukwa wameleta andiko ambalo sasa tutaweka consultant aweze kufanya feasibility study na usanifu wa kina kwa malengo ya kuyatoa maji kutoka Ziwa Tanganyika kupitia vijiji vinavyokuja Sumbawanga mpaka Sumbawanga ili tuwe na chanzo cha uhakika cha maji.
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ya kuuliza swali la nyongeza; kwa kuwa sera hii ya kupeleka maji ndani ya vijiji vyote ambavyo vinapitiwa na bomba hili la Ziwa Victoria ziwe ndani ya kilometa 12 imepelekea baadhi ya vijiji katika maeneo yanayopita hasa kwenye Jimbo la Solwa ambalo bomba hili kuu kutoka Solwa linakwenda kwenye maeneo mengi katika Mikoa ya Shinyanga na Tabora. Je, kwa nini sasa Wizara isione namna bora ya kuweza kupeleka maji haya zaidi ya kilometa 12 kwa sababu vijiji vingi vimeachwa kwa kuongeza tenki dogo kuongeza gravity ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na maji haya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtandao wa bomba la KASHWASA umeacha matoleo katika maeneo mbalimbali na ndiyo maana matoleo yaliyopo Shinyanga sasa tunapeleka maji Tinde. Kwahiyo, kwenye mradi hizi kilometa 12 ni yale maeneo ambayo yatachukua maji moja kwa moja kutoka kwenye hili bomba kuu, mradi unaoendelea kupeleka kwenye vijiji vya kilometa 12. Lakini kupitia kwenye matoleo yaliyopo tunaweza tukaenda hata kilometa 50 na tumeanza kufanya hivyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge hiki ni chanzo cha maji tutaendelea kupeleka maji mpaka zaidi ya kilometa hata 100 kutoka kwenye hili bomba.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Wilaya ya Pangani miundombinu ya maji imechakaa mno na hii ni kutokana na maji ya chumvi ambayo yamekuwa yakitoka. Swali langu ni kwamba, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ambayo imekuwa ikiahidi kila mara ya kutumia maji ya Mto Pangani ili kuweza kuwapatia wakazi wa Pangani maji ambayo hayana chumvi? Lakini pia kukarabati ile miundombinu ambayo imeharibika kwa kiasi kikubwa kutokana na maji haya ya chumvi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu miaka ya sabini Serikali tayari ilishaanza kutumia maji ya Mto Pangani na pale Korogwe tayari tunayatumia maji ya Mto Pangani. Tunao mradi mkubwa ambao umefadhiliwa na BADEA, sasa hivi Kampuni ya Karathi inatoa maji kupeleka maeneo ya Mwanga, yatafika mpaka Korogwe pia. Lakini pia tumepata ufadhili wa aina mbili; tuna fedha kutoka Serikali ya India lakini pia tuna fedha kutoka Serikali ya Netherlands, usanifu unaendelea ili tuhakikishe kwamba tunapeleka maji maeneo mbalimbali, tutafika mpaka Pangani Mheshimiwa Mbunge, wala usiwe na wasiwasi.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani ina mito mingine mikubwa kama Mto Mbwemkuru, Mto Matandu na Mto Lukuledi lakini cha kushangaza maeneo yanayozungukwa na hiyo mito bado yanakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia mito hiyo katika kujaribu kutatua tatizo hili la uhaba wa maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa hii mito mikubwa kama Mto Rufiji na Mto Ruvuma na mingineyo iliyopo katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ni mikubwa ambayo ingeweza hata kusaidia katika upatikanaji wa umeme.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwezesha mito hii kuwekwa kwenye mpango wa hydro-electric kwa ajili ya kuleta umeme katika vijiji ambavyo REA imeshindwa kuvifikia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza amehoji, ni kweli tunayo Mito ya Mbwemkuru, Matandu, Lukuledi katika eneo hilo, lakini sasa mito hiyo Mheshimiwa Mbunge na mimi nimekaa kidogo kule, uzoefu unaonesha kwamba inakuwa na maji mengi sana kipindi cha masika lakini baadhi ya mito kipindi cha kiangazi inakauka. Kwenye taratibu tunazoendelea nazo kufanya utafiti ili tuweze kujenga mabwawa makubwa ya kuvuna maji basi tutahakikisha kwamba mabwawa hayo tutayawekea na skimu za umwagiliaji ili wananchi wanaoishi pembezoni na hiyo mito waweze kufaidika na kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, umeuliza kuhusu umeme. Mheshimiwa Mbunge, zipo taratibu zinaendelea kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaweka kituo cha kuzalisha umeme katika Mto Rufiji kwenye hilo neno linaitwa Stiegler’s Gorge ambapo kutakuwa na kilimo kikubwa pamoja na kuzalisha umeme mkubwa ili tuweze kuongeza nguvu ya umeme katika Tanzania.
Kwa hiyo, Serikali yako Mheshimiwa Mbunge ya Chama cha Mapinduzi tayari imeshaliona hilo na inaendelea kufanya mawasiliano na wafadhili mbalimbali pamoja na kutumia vyanzo vya ndani ili tuweze kutekeleza huo mradi. (Makofi)
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwa kuwa Naibu Waziri naye amekiri kwamba mito mingi ni ya misimu na kwamba wakati wa mvua tunapata mafuriko na wakati wa kiangazi ni ukame. Sasa Wizara inaonaje ikajikita katika shughuli za kukinga maji ya mvua kuyahifadhi ili yaweze kutumika kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo na shughuli nyingine za kimaendeleo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea na jitihada za kuhakikisha tunakinga maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya binadamu majumbani lakini pia na umwagiliaji kwa kujenga mabwawa na tumeshaelekeza kila halmashauri kila mwaka ihakikishe inatenga fedha na kufanya utafiti bwawa moja ili ikiwezekana kila halmashauri ijenge bwawa moja kila mwaka. Na pia tumeelekeza halmashauri wanapopitisha ramani za nyumba basi wahakikishe kwamba wanaweka na utaratibu wa kuvuna maji kutoka katika mapaa ya nyumba kama inavyofanyika maeneo mengine.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa swali la msingi limetaja Mto Rufiji ambao upo kwenye Mkoa wa Pwani ninaotoka, na kwa kuwa watu wa Mkoa wa Pwani wamezungukwa na mito mingi, na kaulimbiu ya Serikali ni kumtua ndoo mwanamke. Je, Serikali ina mpango gani kwa kuanzia na Mto Rufiji kuweza kusambaza mabomba ya maji kwa wananchi na kuwaondoa na adha ya kuliwa na mamba mara kwa mara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ni kwamba tayari tunatenga fedha kila Halmashauri na zimeshaanza kutekeleza miradi ya maji, upo ushahidi wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wananchi wengi wanaliwa na mamba kwa Mto Rufiji, wale wanaokaa pembezoni na Mto Rufiji, lakini kama nilivyojibu katika swali langu la msingi kwamba tunatafuta fedha ili tuweze kufanya utafiti tutengeneze mradi mkubwa wa maji tuyatoe maji kutoka Mto Rufiji tuwapelekee wananchi pembezoni mwa huo Mto Rufiji ili wasiwe na haja tena ya kushuka kwenda kule mtoni kuchukua maji.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Makambako ni mji unaokua kwa kasi na Serikali ilishatenga fedha kutoka Serikali ya India ili kutatua tatizo la maji Makambako ambalo kuanzia mwezi huu wa nane, wa tisa, wa kumi na kuendelea mpaka Desemba hali huwa inakuwa ni ngumu sana.
Je, Serikali ina mpango gani sasa kuwathibitishia wananchi wa Makambako juu ya fedha za India kwamba sasa watapata maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepata dola milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika miji 16 Bara na mmoja Zanzibar ikiwemo pia na Mji wa Makambako. Sasa kinachoendelea kwa sasa hivi, Mheshimiwa Mbunge, tunasubiri financial agreement isainiwe kati ya Hazina na Serikali ya India, lakini Wizara ya Maji na Umwagiliaji tunajiandaa na kuwapata wahandisi washauri kwa ajili ya kukamilisha usanifu haraka na kutangaza tender. Kwa hiyo, nikuhakikishie wananchi wa Makambako baada ya muda watapata maji ya uhakika kutoka kwenye huo mradi mkubwa utakaotekelezwa na fedha za Serikali ya India.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la maji Pangani ni kubwa na kwa kuwa katika Wilaya yetu ya Pangani tumejaliwa kupitiwa na Mto Pangani katikati ya Mji wa Pangani. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuutumia Mto Pangani ili kuondoa tatizo la maji katika Mji wa Pangani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikupongeze Mheshimiwa unawahudumia sana wananchi wako kwa sababu juzi umekuja ofisini, tumezungumza na tukaelekeza hatua za haraka uwasiliane na watu wa DDCA na Mhandisi aliniahidi kwamba katika muda wa wiki mbili atanipa majibu ili tufanye kwanza hatua za dharura. Lakini pia tunaendelea kutumia Mto Pangani ili tuhakikishe kwamba tunawapatia maji watu wa Pangani bila wasiwasi wowote Mheshimiwa Mbunge.
MHE. BAKARI M. MUSSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri ya Jiji la Tanga ni moja ya Halmashauri zilizobahatika kupata mradi wa vijiji 10 kila Halmashauri. Upande wa Kusini mradi wa maji umekamilika lakini upande wa Kaskazini hadi leo mradi haujakamilika kwa kuwa mzabuni anadai.
Je, ni lini Serikali itamlipa mzabuni ili akamilishe mradi wa maji na Wananchi waweze kupata maji safi na salama kwa vijiji vya Kiruku, Kibafuta, Bwagamoyo na Chongoleani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweka utaratibu Serikali inatoa fedha baada ya kuleta certificate na wewe kama Mbunge naomba usaidiane kusimamia huo mradi ili mkandarasi azalishe. Akileta certificate Mheshimiwa Mbunge dakika yoyote fedha tunayo na fedha kutoka Mfuko wa Maji na kwa bahati nzuri flow yake ni nzuri, akileta certificate tunalipa ili akamilishe huo mradi.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Bwana Waziri naomba nikuulize swali. Serikali ina mpango gani mahususi kwa ajili ya kutumia mabonde yetu kama Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria pamja na Mito mikubwa, Serikali ina mpango gani mahususi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuna mabonde tisa katika Nchi yetu na mpango mahususi tayari tunaanzisha commission kwa kila bonde kwasababu mabonde mengine ni kwamba matumizi ya maji yako shared na nchi zingine kwahiyo kupitia kwenye hizo commission ndiyo tunaratibu maji tuyatumiaje, tutatumia kwa maji safi na salama kama tunavyoyatoa Lake Victoria kupeleka Igunga lakini pia tutatumia kwa ajili ya vilimo vya umwagiliaji. Kwa hiyo, tunao mpango mahususi kuhakikisha kwamba mabonde yote tuliyonayo ambayo yako nchini kwetu tunayatumia vizuri kwa ajili ya umwagiliaji na pia kwa ajili ya maji safi na salama na maana ya mabonde ni nini? Ni pamoja na maziwa na mito.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sikubaliani na majibu ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, hayaridhishi kabisa. Ukiangalia kwa mtiririko ulioko kwenye majibu haya imesema wazi mwaka 2006/2007 walifanya upembuzi na kugundua kwamba shilingi bilioni kumi na tatu ilihitajika kwa ajili ya mradi huu lakini wakafanya upembuzi tena mwaka 2014/2015 ikaonekana shilingi bilioni 1.54 zilitakiwa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hili lakini bado wakafanya mwaka 2015/2016 wakatenga milioni 800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walitenga fedha hizi shilingi milioni 800 hazikutoka, halafu mwaka 2016/2017 hawakutenga fedha…

… 2017/2018 hawakutenga fedha, sasa ni kwa nini wanazungumza uongo? Kwa nini hawakutenga fedha katika miaka miwili hii ambayo imo mpaka bajeti ya safari hii wanazungumza…

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni sasa kwamba kutokutekeleza mradi hii hawawatendei haki wananchi wa Wilaya ya Korogwe hususan Manga Mkocheni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya shemeji yangu Mheshimiwa Mary Chatanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeonyesha taratibu mbalimbali zilizofanywa na Serikali na kwamba utendaji lazima tufuate tathmini ya wataalam. Sisi kazi yetu ni kutunga sera na kupitisha bajeti, lakini utekelezaji unazingatia taarifa za wataalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi nimesema kwamba utafiti wa awali ulionesha kwamba bwawa lingejengwa kwa shilingi bilioni 13; lakini tathmini ya kimazingira ikaonyesha kwamba bwawa hilo lingejengwa lingezamisha baadhi ya maeneo na vijiji vya wananchi wa Manga, tusingeweza kufanya hivyo. Kwa hiyo, Tume ya Umwagiliaji kupitia Mkoa wa Kilimanjaro wakafanya tathmini nyingine upya ambayo kama ingetekelezwa basi hayo maeneo ambayo yangeathirika na bwawa yasingekuwemo, ndiyo maana bajeti sasa ikaja shilingi bilioni 1.5, hilo ndilo jibu la msingi. Lakini bado tumetenga shilingi milioni 800 mwaka uliofuata 2014/2015 lakini kwa bahati mbaya bajeti haikutoka ndio maana utekelezaji haukufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba malengo yetu ni kuhakikisha tunajenga hili bwawa na ndio maana Serikali ya Chama cha Mapinduzi...

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: ...imeunda Tume ya Umwagiliaji ambayo sasa kazi yake itakuwa ni kusimamia moja kwa moja suala la utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi hakuna haja ya hasira kazi hii tutaifanya na wananchi wa Manga watapata huduma wanayoihitaji. (Makofi)
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Songea kwanza naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla pamoja na Serikali kwa kuanza ukarabati katika vituo 89, hivyo, katika vituo 187 tunabakiwa na vituo 98 vya maji ya mtiririko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengi ambayo yana matatizo ya maji, maeneo hayo ni pamoja na Mlete, Lilambo, Chandarua, Mahilo, Ndilima Litembo, Lizaboni, Tanga na Mletele, Subira na Mwenge Mshindo na Making’inda. Nataka nipate uhakika wa Serikali. Je, Serikali inaweza kuwahakikishia wananchi wa Songea ni lini tatizo la maji litakuwa limekwisha kabisa katika Mji wa Songea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili naomba nimuulize Waziri liko tatizo kubwa sana la mamlaka za maji hasa SOWASA, kuwabambikizia wananchi bili za maji za uwongo. Mtu anaweza asitumie maji mwezi mzima lakini akakuta anabambikiziwa bili isiyo na sababu. Je, ni lini Serikali itahakikisha inasimamia kidete kuhakikisha bili zinazokwenda kwa wananchi ni zile zinazotokana na matumizi ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Gama kwa jinsi ambavyo anawahangaikia wananchi wake. Wakati tuko Dar es Salaam amekuja zaidi ya mara saba ofisini na ndiye aliyefanya tukafanikisha ukarabati wa hivi visima vifupi 89, nampongeza sana. Hata hivyo, hata wakati anaondoka kwenda kutibiwa aliniachia maagizo kwa ajili ya kushughulikia Mji wake wa Songea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumemaliza awamu ya kwanza ya maendeleo ya sekta ya maji sasa tumeingia awamu ya pili. Tutahakikisha kwamba maeneo yote aliyoyataja vijiji vinavyozunguka Mji wa Songea katika awamu ya pili na katika hii miaka miwili inayofuata ya bajeti tutahakikisha kwamba maeneo yote tumeyapatia maji. Hilo ndiyo lengo la Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba tutakapofika mwaka 2020 basi tuwe tumefikia asilimia kubwa ya wananchi wa vijiji kuwapatia maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la bili, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na nilizungumze kwa niaba ya Wabunge wote sasa. Ni kweli Mamlaka zetu za Maji Mijini kuna hiyo hali ya kwamba unaletewa bili hata kama maji yalikuwa hayatoki hata Mheshimiwa Rais juzi ameizungumzia hii, lakini hili tumeshaliona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo mawili ambayo tumeyagundua; moja kuna kitu wanaita service charge inakuwa kwamba wewe umekodi ile mita, kwa hiyo kwa maana ya kuikodi walikuwa wameweka utaratibu kwamba hata kama maji hayajatoka kwa sababu umekodi wanakuchaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji juzi baada ya bajeti Wakurugenzi wote walikuwa hapa amewaagiza wakaiangalie hii kwa maana ya kuitoa. Kwa sababu siwezi nikakodi kifaa sipati huduma lakini naendelea kukilipia kwa kuwa nyumbani kwangu. Kwa hiyo, suala hili Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tayari tumeanza kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko tatizo la pili ambalo nimelifanyia study kupitia Mamlaka ya Maji DAWASCO. Hawa wahudumu wetu system yetu ya kusoma mita unasoma halafu unakwenda kupachi kwenye computer. Unaweza ukakuta unit 15 ukapanchi ukaona 15 baadaye ukarudia tena ile inaji-double ndio maana bili zinakuwa kubwa. Kwa hiyo, hilo nalo tunaliangalia kitaalam ili hiyo double isitokeze, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge niwahakikishieni kwamba hili suala tumeshaliona, tunalishughulikia na tutalimaliza.
MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, mradi wa maji wa visima Gairo umekamilika lakini kwa bahati mbaya maji haya ni ya chumvi kiasi wananchi wanapata shida kuyatumia. Je, mradi wa maji ambayo hayana chumvi kutoka milima ya Nongwe utakamilika lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tulichimba visima saba pale Gairo vina maji mengi lakini yale maji hayafai kwa matumizi ya binadamu. Ndani ya ule mkataba tulikuwa tumepanga kununua mashine kwa ajili ya kitu wanaita desalination tumeiondoa hiyo badala yake tumeenda kutafuta sasa visima kwenye milima iliyoko na Gairo na ripoti yake inakamilika leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuwasiliane na Mheshimiwa Mbunge wiki ijayo tutapata majibu tunataka sasa tuchukue maji kutoka kule milimani ambayo hayana chemicals tuyalete pale Gairo ili wananchi wapate maji yaliyo safi na salama, tutatumia miundombinu ile ambayo imeshajengwa iko pale Gairo.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza linalohusiana na masuala ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji lililopo Songea linafanana kabisa na tatizo lililopo Wilayani Masasi hasa katika Vijiji vya Lukuledi, Chikunja, Maparagwe, Liputu, Mlingura pamoja na Namajani. Maeneo haya yote yanahudumiwa na mradi wa maji wa MANAWASA kutokea mradi wa Mbwinji ambao unapeleka maji mpaka Nachingwea. Tunataka kufahamu sasa kwa sababu tatizo kubwa ni miundombinu ya kusambaza maji haya kwa watumiaji. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kupeleka pesa kwa ajili ya kununua vitendanifu kwa ajili ya kuunganisha maji katika maeneo niliyoyataja? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki mbili zilizopita nilienda Masasi mpaka mradi wa Mbwinji, Mamlaka ya Maji MANAWASA Mkurugenzi wake ameomba milioni 500 na tunampatia ili akamilishe kuunganisha vijiji vilivyobaki ambavyo viko pembezoni mwa bomba linalotoa maji Mbwinji kupeleka Masasi Mjini, lakini pia kwenda Nachingwea pamoja na vijiji kadhaa vya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, kwa hiyo kote tunapeleka maji.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo la maji la Songea linashabihiana na kwa kiasi kikubwa na tatizo la maji katika Wilaya ya Mkinga. Hivi karibuni tumewasilisha taarifa ya Maafa kwa kuharibika mabwawa takribani saba katika Wilaya ya Mkinga na kwamba watu wanashida kubwa ya maji. Je, ni nini kauli ya Serikali kwa tatizo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uharibifu mkubwa ulioharibu miundombinu ya maji Mkoa wa Tanga kutokana na mvua, Mheshimiwa Mbunge nimuahidi kwamba, ni kweli taarifa niliipokea ambayo imeandikwa kwenda upande wa maafa na mimi ninayo, lakini kabla hatujachukua hatua, basi baada ya Bunge tu naomba mimi na yeye mguu kwa mguu, twende nikajionee kule na nitakuwa na wataalam ili tuweze kuona sasa tutafanya nini. (Makofi)
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mji wa Mkuranga ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi sana; na kwa kuwa visima vya maji vilivyoko katika Mlima Kurungu vilishachimbwa na maji yanamwagika kuelekea mashambani; na kwa kuwa tumeshaomba shilingi milioni 800 Serikalini ya kuhakikisha tunayatoa maji yale ya Mto Kurungu kuyaleta Mkuranga Mjini na Vijiji vya jirani vya Kiguza, Dundani, Kiparang’anda, Magoza, Tengelea na kwingineko. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kunihakikisha kwamba milioni 800 zile tutazipata kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mkuranga na vijiji hivyo vingine nilivyovitaja?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ulega, ni kweli ameniletea andiko kuhusiana na maji ya Mlima Kurungu. Maji ni mengi, yanamwagika, yanapotea na sasa hivi Wizara yangu tayari nimeshawakabidhi wataalam lile andiko wanalifanyia kazi. Nimhakikishie kwamba milioni 800 itatolewa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na wataalam washirikiane na Halmashauri ili yale maji yasipotee wananchi wayatumie. (Makofi)
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa mazingira ya Mitaa ya Matogolo, Ndilimalitembo, Lizaboni na Bombambili kwa upande wa Songea Mjini, yanafanana kabisa na matatizo ya Mitaa ya Luwiko, Lusaka, Bethlehemu, Misheni, Mbinga A, Mbinga B, na Lusonga kwa upande wa Mbinga Mjini ni lini Serikali italeta neema ile ile inayotaka kuipeleka Songea Mjini kwa upande wa Mbinga Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, neema inakuja tunamsubiri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, akamilishe finance agreement ya milioni 500 kutoka India ambayo sehemu ya fedha hiyo pia na Jimbo la Mheshimiwa Mbunge litafaidika na huo msaada. Tayari sasa hivi tupo katika hatua ya kuwapata Consultants ambao watafanya study kwa muda mfupi sana tutangaze tenda. Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba Jimbo lake na Mji wake wa Mbinga utapata maji safi na salama baada ya muda mfupi. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa swali la nyongeza. Halmashauri ya Mji wa Liwale ulikuwa na miradi ya maji wa vijiji 10, lakini mpaka sasa hivi vijiji vyote 10 vimeshatobolewa lakini vijiji vilivyofungwa miundombinu ya maji ni vijiji vitatu tu. Vijiji ambavyo sasa hivi vina maji ni Kijiji cha Mpigamiti, Barikiwa, pamoja na Namiu. Je, vile vijiji saba vilivyobaki lini watatoa pesa kwa ajili ya kujenga miundombinu kumalizia vile visima ambavyo tayari vimeshatobolewa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwamba chanzo cha maji cha Mji wa Liwale kinatokana na Mto Liwale na ni kweli kwamba chanzo kile kidogo kimeleta shida. Katika bajeti ya fedha ya mwaka unaokuja tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya study ili tuweze kuimarisha chanzo au kutafuta chanzo kingine kuhakikisha vijiji vilivyobaki sasa vinapata maji bila wasiwasi wowote na hii itatekelezwa kwenye mwaka wa fedha unaokuja ambapo bajeti yake Mheshimiwa na yeye mwenyewe nafikiri aliikubali siyo kwamba aliikataa.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Jimbo la Babati Mjini pamoja na kwamba ni Halmashauri ya Mji kuna baadhi ya maeneo bado hayana maji. Tulipeleka maombi katika ofisi ya Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya kuchimbiwa visima katika Mtaa wa Wa’wambwa, Kijiji cha Singu na cha Hala, maombi hayo yameishafika kwa Wakala wa Uchimbaji Visima. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya maombi yetu haya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa wakala wetu wa kuchimba visima unapeleka maombi kwao moja kwa moja hatuwaingilii, wanakujibu, mkiingia mikataba sisi kazi yetu ni kuchukua sehemu ya hela yako uliyotengewa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, wakishachimba tunawalipa ili shughuli ziendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri wa taasisi yetu hii, ina- survey yenyewe, inachimba yenyewe, haikupata maji haidai ndiyo uzuri wake. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwamba tujaribu kutumia taasisi yetu na sisi tunaendelea kuiimarisha kwa kuiongezea mitambo ili iweze kutusaidia katika hili suala la matatizo ya maji vijijini. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Suala la msingi liliuliza ni lini, maeneo yaliyotajwa yatapata maji, ni lini? Tanzania kijiografia Mwenyezi Mungu ametujalia tunayo maji ya kutosha kwa matumizi ya binadamu na viumbe vingine vyote vilivyo hai kwa kuwa maji ni uhai, tatizo ni namna ya kuvuna maji, kuyatawala maji na kuyatumia maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwenye swali hili la Mheshimiwa Mnyika, ambapo wakazi wenyewe wanatumia maeneo yote aliyoyataja ni zaidi ya milioni mbili uhai wa binadamu hawa kukuza utu wao ni lini watapatia huduma ya hii ya msingi ya kukuza utu wao?
Swali la pili; maeneo ya Jimbo la Vunjo, Kata za Mwika Kusini, Makuyuni, Njia Panda, Kirua Kusini, Mamba Kusini yana tatizo kubwa la maji na wananchi wananunua maji ndoo moja kwa shilingi 500 mpaka shilingi 1,000. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza programu kwa Wabunge wote ikiwemo na Vunjo ndani ya miaka hii mitatu ya kipindi chetu cha Ubunge tuweze tukajua kila programu inatekelezwa kwa muda gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kwenye swali la msingi wamesema ni lini. Mheshimiwa Mbunge Mbatia ni kwamba kuhusu maji ya kuyatoa Mtambo wa Ruvu Juu, ambapo juzi Mheshimiwa Rais ameuzindua, maji yako tayari, mradi uliobaki ni wa usambazaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mkataba huo Mkandarasi anatakiwa kukamilisha mradi huo mwezi Julai mwishoni. Kwa hiyo sijaelewa sasa jinsi anavyoendelea lakini tutauangalia kama utakamilika kama ulivyo, mwishoni mwa mwezi Julai, ni kwamba mwezi Agosti wananchi wataanza kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni kweli tulikuwa na programu ya kwanza ambayo ilianza kwenye bajeti ya mwaka 2006/2007 imekamilika mwaka 2016 mwezi Juni, ni Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Ndani ya programu hiyo tukaibua miradi 1,810 na mpaka tunapozungumza miradi 1,333 imekamilika bado 477.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeingia kwenye programu ya pili. Mahitaji ya programu ya pili ni dola za marekani bilioni 1.6 na mpaka ninavyozungumza wafadhili wameshatupatia ahadi ya zaidi ya dola bilioni moja. Kwa hiyo, nina hakika kabisa kwamba, kupitia mpango huu mwingine wa miaka tano, nimhakikishie Mheshimiwa Mbatia kwamba, tutapita maeneo yote, tutatengeneza studies tutatekeleza miradi ili wananchi wa Jimbo lake la Vunjo na vijiji vilivyobaki wafaidi utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongezaKwa kuwa, matatizo yanayokabili Jimbo la Kibamba yanafanana kabisa na matatizo yanayokabili Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, hususani katika Kata ya Mkambarani katika Vijiji vya Pangawe na Kizinga. Mheshimiwa Mwenyekiti, Pangawe na Kizinga tuna mradi mkubwa wa maji pale, lakini mradi ule maji hayatoki hasa wakati wa kiangazi ambao kunasababishwa na kile kidaka maji ambao sisi ndio watu wa Pangawe tulianza, lakini watu wenzetu wa MORUWASA wakaja kuweka juu yetu, matokeo yake wanatuathiri sisi hatupati maji pale, lakini tumechanga wenyewe pesa tumeweza kujenga lakini tumekatazwa na Mamaka ya Maji ya Bonde la Ruvu. Je, Serikali inatusaidiaje watu wa Pangawe na Kizinga kuzungumza na Mamlaka ya Maji ya Bonde la Ruvu, ili waturuhusu hicho kibali na sisi tuhamishe hicho kidaka maji kwenda kwa wenzetu kule juu cha MORUWASA na Jeshi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri chanzo cha Pangawe nilifanya ziara Mkoa wa Morogoro, nimeenda mpaka pale kwenye chanzo nikakiona. Kipindi cha kiangazi ndio chanzo pekee ukiachana na bwawa la Mindu ambacho kinaleta maji ya mtiririko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kile chanzo Jeshi la Wananchi wa Tanzania wanachukua pale, Mamlaka ya Maji Safi Morogoro nao wanachukua pale, vijiji vingine vilivyo karibu navyo vilikuwa vinahitaji kuchukua pale, sasa hivi tumeelekeza yafanyike mazungumzo ili menejimenti ya chanzo ibaki kwenye eneo moja la Mamlaka ya Maji ya Morogoro, baada ya kuwa kwenye hilo eneo moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutakubaliana, tutawapa assignment hawa watu wa MORUWASA ili wahakikishe wanapeleka maji kwenye maeneo yote, kwa sababu kama chanzo kimoja kimoja kitafanyiwa menejimenti na taasisi nyingi kwa vyovyote vile tutarajie kwamba performance yake haitakuwa nzuri. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona, Mji wa Mafinga ni kati ya Miji inayokua kwa kasi na hasa kutokana na shughuli za uzalishaji wa mazao ya misitu na bidii ya kufanya kazi ya wananchi wa Mafinga na hivyo uhitaji wa maji umeongezeka. Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza miradi iliyotengwa kwenye bajeti hii ambayo tunaenda kuimaliza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, tumetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya Mafinga, lakini pia tayari kuna mikataba ambayo tumeshaanza kuisaini, tayari tumesaini mkataba wa ujenzi wa tenki la lita 500,000 kwenye Kijiji cha Kinyanambo na tunaendelea kusaini mikataba mingine kama Bumilainga na Muduma pia. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunaendelea na hiyo kazi vizuri kabisa tutahakikisha wananchi wake wanapata maji.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wakazi wa Kata ya Rotia hususani vijiji vya Rotia, Rotia, Kainam, Kilimatembo, Chemchem na Kilimamoja wanapatwa na shida kubwa ya upungufu wa maji kutokana na chanzo chao pekee cha Mto Marera kukauka hasa wakati wa kiangazi kutokana na ama miundombinu chakavu, au maji kupungua sana. Je, ni lini Serikali itachimba visima katika vijiji hivyo ili waondokane na tatizo hilo la maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Qambalo, eneo hilo nalifahamu ni eneo kame sana kipindi cha kiangazi na pale mahali pana Airport, kwa hiyo tuwasiliane na Halmashauri ili tuone tufanyaje, ili kufanya study inayotakiwa, tuchimbe visima wananchi wa sehemu hiyo waweze kupata huduma ya maji kupitia kwenye bajeti yake ambayo tumemtengea, kwenye mwaka wa fedha 2017/2018. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza. Tatizo la maji lililoko Kibamba linafanana kabisa na tatizo la maji lililoko Wilaya ya Ngara hasa Kata ya Mbuba, ambayo ina shule za sekondari mbili wanafunzi wanatembea kilomita mbili kwenda kufuata maji mabondeni na husababisha wanafunzi kukatisha masomo yao kwa kupata mimba na ukizingatia tamko la jana la Mheshimiwa Rais. Je, Serikali ina mpanga gani wa kumaliza tatizo hili, hasa katika Kata hii ili kunusuru ndoto za wadogo zetu, au watoto wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba katika hizo shule mbili kiko kisima pale Ngara Mjini ambacho pampu yake ilikuwa imeharibika, tayari Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hilo amefanya juhudi, mashine imepatikana. Wizara ya Maji na umwagiliaji tunampelekea fedha ili akaongeze mashine nyingine na kumpa fedha kwa ajili ya kutandika mabomba kutoka kwenye hicho chanzo ili shule zote mbili hizo ziweze kupata maji, tuondoe usumbufu wa watu kutembea mwendo mrefu na kupata hayo madhara ambayo unayazungumza.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante kwa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni tuna mradi mkubwa sana wa maji wa visima 20 ambao ulianza mwaka 2013 na mradi huo ulitarajiwa kukamilika mwaka jana Desemba, lakini haukukamilika. Kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa Maji alitutembelea Oktoba mwaka jana na akatoa maelekezo kwa Kampuni ya Serengeti kwamba ikamilishe mradi huo kabla ya Desemba mwaka jana na ikiwa haitakamilisha basi watatakiwa kulipa gharama za ucheleweshaji.
Niombe sasa Serikali itusaidie kufahamu ni nini kinachoendelea katika mradi ule mpaka sasa haujakamilika wakati ingekuwa suluhu ya tatizo la maji katika sehemu kubwa sana ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani Wilaya kama Mkuranga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo ni eneo la Kimbiji na Mpera tunachimba visima 20, visima 17 viliishakamilika, vitatu bado vinakamilika mwezi Julai. Ni kweli teknolojia ya kuchimba visima katika eneo hilo imetusumbua kidogo, ni visima virefu sana vinakwenda zaidi ya mita 300 mpaka 600 na kuna maji mengi sana. Kutokana na hilo ilibidi tuwape addendum kutokana na hiyo teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo uchimbaji wa visima utakamilika mwezi ujao mwishoni visima vitakuwa vimekamilika, kazi itakayofuatia sasa tunatafuta fedha kwa ajili ya kuweka miundombinu ya usambazaji. Kwa hiyo maeneo ya Kigamboni na Temeke yote yatapata maji. Visima hivyo vitatoa lita millioni 260 kwa siku, ndio maana tunasema Dar es Salaam haitakuwa na shida ya maji.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Serikali inafanya juhudi kubwa sana ya kuupa Mji wa Namanyere maji, lakini mpaka sasa Mji wa Namanyere unapata chini ya asilimia 20 maji. Zipo juhudi zimefanyika na Serikali lakini tatizo kubwa ni ununuzi wa mashine ya kusukuma maji, mpaka sasa mashine hiyo haijanunuliwa. Naiomba Serikali itueleze ni lini wananchi wa Namanyere watapata mashine ili waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mipata akishirikiana na Mheshimiwa Ally Kessy walinifuata ofisini, wakaniomba wataalam ili waende wakajaribu kuangalia ni jinsi gani watanunua hiyo mashine. Wataalam niliowatuma, taarifa wamekamilisha, nimhakikishie Mheshimiwa Mipata kwamba, sasa hivi tunatuma hela ili mashine inunuliwe na wananchi wa Nkasi wapate huduma hiyo ya maji. (Makofi)
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kuuliza swali dogo. Tatizo la maji katika Halmashauri ya Mji wa Nzega ni kutokana na uchakavu wa miundombinu iliyokuwepo toka miaka ya 70 na mwaka jana Desemba tulipata ahadi ya Mheshimiwa Rais ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya kutatua tatizo hili. Tukapokea millioni 200. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambia nini wananchi wa Mji wa Nzega juu ya utekelezaji wa milioni 200 ambayo tumekuwa tukiisubiri toka mwezi wa Nne mwaka huu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kupeleka shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Nzega. Milioni 200 tumeshaitoa na tumekabidhi kwenye Mamlaka ya Maji ya Tabora na mradi huo wameshaukamilisha tayari. Kwa sasa tunajiandaa kuwapatia milioni 200 nyingine ili waendelee kuboresha miundombinu ya Mji wa Nzega. Pia kupitia mradi mkubwa huo uliosainiwa juzi wa kutoa maji kutoka Solwa kupeleka Nzega na Tabora miundombinu itakarabatiwa pia. (Makofi)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nishukuru kwa mradi wa maji wa vijiji kumi katika Jimbo langu, nimefanikiwa vijiji vitano na vitano nimeambiwa Mkandarasi yule apeleke certificate. Hata hivyo, kuna vile vijiji ambavyo havikupitiwa na mradi ule. Kwa mfano, Kijiji cha Pande Muheza, Mondura na Bagamoyo. Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima virefu katika vile vijiji ambavyo havikupitiwa na mradi ule wa vijiji 10 katika kila Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea na Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya pili ili tuhakikishe vijiji vyote ambavyo havikupitiwa tuvikamilishe. Pia tunatenga bajeti kila mwaka kupitia kwenye Halmashauri ya Mheshimiwa Mbunge na tayari tumeshatoa taarifa kwamba Halmashauri iwasiliane na Mamlaka yetu ya uchimbaji wa visima na atupe taarifa anapokwama ili tuweze kusimamia waende haraka vijiji vipate maji.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Mheshimiwa Waziri alifika Hydom akaona matatizo ya maji yaliyoko pale na Dongobesh na certificate ziko Ofisini kwake, je atatusaidiaje sasa Certificates zilipwe kwa haraka ili miradi hii ikamalizika kwa wakati na kama alivyoahidi siku ile ulivyofika Hydom? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana ndugu yangu Mheshimiwa Flatei anafuatilia. Certificate kila zikifika hazichukui muda tunalipa, kuna moja iliyokuja tumeshalipa tayari, kwa hiyo, kama kuna nyingine imekuja asiwe na wasiwasi Wizara ya Fedha kupitia kwenye Mfuko wa Maji ambao Waheshimiwa Wabunge mnatusaidia sana kuutetea uongezeke fedha zake zinakuja bila wasiwasi. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Flatei tutalipa. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Jimbo la Urambo lina uhaba mkubwa sana wa maji, pamoja na kuishukuru Serikali kwa hatua yake ya uamuzi wa kupata maji kutoka Mto Malagalasi. Kwa sasa hivi kutokana na shida kubwa tuliyonayo; je, Serikali inachukua hatua gani za dharura ili wananchi wa Urambo wapate maji wakati wakisubiri mradi ambao utachukua muda mrefu wa maji kutoka Mto Malagalasi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishafika Urambo, tuna huo mradi mkubwa lakini ni kweli mradi mkubwa utachelewa. Hatua za dharura tunaendelea kutenga fedha kila mwaka kupeleka Halmashauri ya Urambo, lakini pia tumeshazungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba naomba atukutanishe mimi Naibu Waziri pamoja na Halmashauri yake kwa maana ya Mkurugenzi na Engineer wa Maji ili tuzungumze, tushauriane kuchukua hatua za haraka ili kuweza kupata maji hasa kwa kuzingatia kwamba Tabora haina maji chini ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshazungumza na Mheshimiwa Mbunge, baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani naomba tukutane na hao watu wake ili tutatue hili suala.
MHE. FRANK. G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mji wa Tunduma una shida kubwa sana ya maji na mwaka jana katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ilikuwa imetengwa fedha Euro milioni 100 ambayo ilitaka kutekelezwa na Kampuni ya Aspac International kutoka Ubelgiji, lakini katika bajeti hii fedha hiyo haijatengwa na mradi huo hauonekani kabisa. Nataka nijue mradi wa kupunguza tatizo la maji katika Mji wa Tunduma utatekelezwa siku gani na kwa nini umeondolewa hauonekani katika bajeti ya mwaka 2017/2018?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba Serikali imepanga kukopa fedha kutoka Ubelgiji. Mazungumzo yanaendelea kati ya Hazina na Serikali ya Ubelgiji kupitia Benki hiyo ambayo imeonesha nia ya kutuazima hiyo fedha. Kwa hiyo mazungumzo yakishakamilika, basi huo mradi utaendelea, anashangaa kwa nini haujaonekana katika mwaka ujao wa fedha ni kwa sababu mazungumzo hayajakamilika Mheshimiwa Mbunge. Hata hivyo, nimhakikishie sasa hivi nazunguka kwenye Miji yetu ya mipakani nchi nzima. Namwahidi kwamba ninapokwenda nyumbani nitapita Tunduma lazima tufanye hatua za dharura kama nilivyofanya Namanga na maeneo mengine ili wananchi wapate maji safi na salama pale Tunduma.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza. Tatizo la maji katika Wilaya ya Kilolo hasa sehemu za Ilula Mheshimiwa Waziri analifahamu na ameahidi mara nyingi kufika pale, sasa hivi mradi umeanza kwa sababu ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Je, atuambie leo ni lini atakwenda pale kuona ule mradi ambao ni ahadi ya Mheshimiwa Rais unaendelea vizuri na unakwisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba nimepanga ziara ya mikoa 15 baada ya Bunge hili la Bajeti ikiwemo Iringa. Nitafika pamoja na kwenda kuangalia Mto Lukosi una maji mengi sana mwaka mzima ili tuone ni jinsi gani tutashusha maji pale Ilula, lakini pia huo mradi nitakwenda kuukagua Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Katika Wilaya ya Mpwapwa, Vijiji vya Bumila, Mima na Iyoma vilichimbwa visima vya maji na maji yalipatikana, sasa ni miezi nane hakuna cha bomba, hakuna cha pampu. Sasa nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri vile visima vilichimbwa kwa ajili ya mapambo kuonyesha wananchi tu au ni lini wataweka pampu na mabomba wananchi wanapata tabu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulishazungumza naye na nimeshazungumza ndani ya Bunge lako hili Tukufu, ukishachimba kisima maji yakapatikana Mkurugenzi unatakiwa utengeneze quotation ya kununua pampu. Ukishatuletea quotation sisi hiyo tunaiweka kama ni certificate tunakupa hela ili uende ukanunue pampu na pampu hizi zifungwe wananchi wapate maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kama tulivyoongea nje kwamba amwambie Mkurugenzi wake wa Halmashauri atengeneze quotation na kama hana huo utaalam basi tuwasiliane ili Wizara ya Maji na Umwagiliaji, tutume mtaalam wetu akamsaidie Mkurugenzi wake wananchi wapate maji.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri sasa naomba niulize swali moja. Kwa kuwa, miradi ya maji imekuwa ikisumbua sehemu nyingi hata Wilaya ya Kilolo imekuwa haiishi vizuri na kwa kuwa kuna watu wanaitwa Wakandarasi Washauri wamekuwa wakilipwa pesa kwa ajiili ya kushauri miradi yetu ili iende vizuri pale inapokuwa imeharibika wanachukuliwa hatua gani hawa Wakandarasi Washauri?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba huyu Mkandarasi Mshauri au Consultant kwenye usajili wake akipata kazi yoyote ya Serikali kuna kitu kinaitwa Design Liability Insurance. Insurance hiyo inalinda performance ya kazi yake na kama hakufanya vizuri kupitia kwenye ile insurance au kupitia kwenye ile bond basi anatakiwa arudishe hela kama mradi haukufanyika vizuri. Kwa hiyo, kama haujafanyika vizuri kwenye eneo lake naomba sana Mheshimiwa Mbunge awasiliane na TAMISEMI au na Wizara ya Maji ili tuweze kumwajibisha huyo Mhandisi Mshauri. (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nipate kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali ina nia njema ya kupeleka nishati mbadala katika maeneo mbalimbali ya Tanzania; na kwa kuwa, Jimbo la Kavuu lina idadi kubwa ya wafugaji na kinyesi cha wanyama kinapatikana kwa wingi hasa ng’ombe, nguruwe na mbuzi. Pia, kwa kuwa, bado hatuna mtandao mzuri wa majitaka katika miji mingi ya vijijini ikiwemo Jimbo langu la Kavuu. Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka kupitia taasisi za TADETO na UN Habitat katika kuanzisha miradi ya biolatrine ambayo inatumia kinyesi cha binadamu katika maeneo ya mashule, ili tuweze kupata gesi ya uhakika kutokana na kwamba sasa uharibifu wa mazingira katika Jimbo la Kavuu umekuwa mkubwa especially katika kukata miti hovyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, naomba niulize si kwa Serikali na Watanzania kwa ujumla, je, matumizi ya mkaa na gesi yapi ni bora zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme kwamba, Serikali inaupokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa tufanye utafiti wa kutosha ili tuweze kutumia human waste kutoka kwenye pitlatrin na ku-convert kuwa energy ambayo inaweza ikasaidia matumizi ya binadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba, Serikali iko tayari kutumia hii taasisi ya TADETO ambayo tayari imeshafanikisha miradi miwili Dar es Salaam kwa kujenga bioelectric ambayo sasa hivi inatumika kwenye sekondari mbili pale Dar es Salaam ikiwemo Sekondari ya Manzese. Teknolojia hii inatumiwa zaidi na Uganda kwenye shule za sekondari na shule za misingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake pili kuhusu yapi matumizi bora, tutumie gesi au tutumie mkaa. Ni bora kutumia gesi kwa sababu kwanza gesi bei yake ni nafuu ukilinganisha na bei ya mkaa. Kwa mfano, Dar es Salaam gunia moja la mkaa la kipimo cha kawaida ni Sh.75,000/= lakini ukienda kwenye teknolojia ya nguvu gani inapatikana katika mkaa, wataalam wameshafanya vipimo wakaona kwamba, tunapata unit 2.645 kwenye gunia la mkaa ni energy ambayo inayojulikana kwa kwa jina la Gigajoule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, unit moja ya gunia la mkaa inauzwa kwa Sh. 28,000/=, lakini ukienda kwenye gesi unit moja inauzwa kwa shilingi 18,000. Pia, ukitumia gesi tayari unakuwa umeshaokoa mazingira yetu, watu wa mazingira ukikata miti unaleta uharibifu wa mazingira ambao unaweza ukatuathiri kwenye mambo mengine kama kutopatikana kwa mvua inayostahili kwa masuala ya kilimo.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika awamu ya pili ya REA ambayo imekwisha kuna vijiji ambavyo havijapitiwa na katika upelekaji wa umeme ule ulienda kwenye makao makuu ya kata. Kwa mfano, pale Malangali Vijiji vya Isinikini, Kingege, Ibangi na Ikaning’ombe pale bado havijapata umeme. Je, Serikali itarudi kwenye kutekeleza ile ambayo ilikuwa ni awamu ya pili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ilisema kwamba itapeleka umeme kwenye vituo vya afya, zahanati, pamoja na shule za sekondari na shule za msingi, lakini mpaka sasa hivi shule za msingi bado hatujaona programu kwamba, Serikali inapeleka. Je, katika awamu hii ya tatu mnatuhakikishia kwamba, katika maeneo haya niliyoyataja watapewa umeme?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme utekelezaji wa miradi ya umeme unafanana sana na miradi ya maji. Katika utekelezaji wa miradi ya umeme Wilaya zote kwa sasa wanafungua Ofisi za TANESCO. Awamu ya pili amesema kwamba, kuna vijiji ambavyo vimeachwa, kama tayari Ofisi ya TANESCO iko pale, basi wale ambao hawajapata wapeleke maombi kwenye zile ofisi ambazo zitaendelea kufanya extension ikiwa ni pamoja na kuingiza umeme kwenye majumba ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, Taasisi za Serikali naomba sana Mheshimiwa Mbunge kwamba, kukishakuwa na ofisi ni vema hizo taasisi za Serikali kama zina mahitaji ya umeme na ni lazima zina mahitaji ya umeme, basi ni kuwasiliana na ofisi zilizopo jirani kupeleka maombi, ili waweze kufikiriwa kupelekewa umeme kwenye hizo taasisi. Kama bajeti itakuwa haitoshelezi kwenye ofisi za Wilaya au Mkoa wao basi wata-forward moja kwa moja hayo mahitaji Makao Makuu ya TANESCO ili waweze kupatiwa pesa au waweze kuingiza hizo shule na taasisi za Serikali ziweze kuingizwa katika mradi mkubwa. (Makofi)
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Ningeomba niulize maswali mawili ya nyongeza mafupi. Kwa kuwa, Serikali inatambua kuwa eneo hilo ambalo limetajwa kama vyanzo vya maji kwamba halipashwi kupewa huduma zozote na inawataka wananchi kuhama. Serikali inasemaje kuhusu huduma nyingine ikiwamo ya kuwepo viongozi ambao wamechanguliwa kwa kura na kura zinaendelea kufanyika pale eneo hilo na viongozi waliochaguliwa wengine ni wa CCM ambao wanaongoza eneo hili, Serikali inasemaje hiyo huduma ya kiuongozi nayo hawaitambui. Kwa hiyo, waondokeje wakati kuna uongozi uliochaguliwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Sheria namna ilivyo kwa hali halisi inajichanganya sana kutokana na tafsiri ya chanzo cha maji cha mita 60, lakini Serikali imewahi kujibu hapa kutokana na hali halisi kwamba kuna maeneo ambayo kijiografia leo hii ukiwaondoa watu kwa mita hizo 60 wakiwemo wananchi wa maeneo mbalimbali ya Bukoba Town ni kwamba Mji wa Bukoba Town hautakuwepo kwa sababu kila mita 60 kuna mto kuna chanzo cha maji. Serikali inasemaje katika kuleta kanuni ambazo ilisema itazileta ambazo zinaweka tafsiri pana na inayofafanua hizi mita 60 zina maana gani? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, huduma za kiuongozi katika eneo tengefu, niseme watoke. Watoke na wala huduma ya kiuongozi huko haitakuwepo, wala huduma ya aina yoyote watoke, wakisubiri wataondolewa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu mita 60, namshukuru sana Mheshimiwa Lwakatare, definition ya mita 60 inalenga maeneo fulani fulani. Sasa hivi tumeanza kuzungumzia suala hili ukiangalia katika mito kuna mito kuna vijito na kuna vi-stream vingine ni vidogo sana ambavyo pengine mvua ikinyesha kinaweza kikatiririsha maji kwa wiki moja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, inabidi tuwe na definition pana, mita 60 inalenga wapi, ni kwa kila kamto hata mto kama Rufiji kwenye mito ambayo ni mikubwa ina mabonde makubwa definition ya mita 60 haipo na ndiyo maana kwenye bwawa la Nyihongo mipaka yake imekuwa ni mikubwa zaidi kuliko hiyo mita 60. Tunalenga pia lile eneo ambalo ni oevu ambalo ndiyo linafanya sasa lile bwawa liweze kuishi. Kwa hiyo, hii tutaiweka vizuri ili kuondoa mkanganyiko kama uliotaka kujitokeza hapa wa vinyungu.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mepesi mepesi ya ndugu yangu Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, inaonyesha jinsi ambavyo mtiririko wa project management engineering pattern usivyokuwepo katika majibu yake ya swali ya msingi. Haiwezekani leo Serikali inapanga kuchukua kufanya usanifu wa kina na kuandaa vitabu vya zabuni halafu wakati huo huo mtaalam mshauri anaendelea na usanifu ambao unatakiwa kwisha mwezi Julai, 2017, wakati mtu wa Environmental Impact Assessment hajafanya kazi yake. Hiyo inanipa mashaka kama kweli huu mradi upo au haupo. Sasa naomba Serikali itoe tamko kama kweli huu mradi upo na utaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, amezungumzia kiasi cha shilingi milioni 300 zilizotolewa kwa ajili ya Mji wa Kibondo kupanua miundombinu. Hata hivyo, ninayo uhakika na yeye Mheshimiwa Naibu Waziri niliwasiliana naye mwezi wa Aprili mwanzoni, kwamba kuna milioni 300 zilizotolewa kwa ajili ya Mji wa Kibondo toka mwaka jana bajeti iliyopita hii tunayoimalizia, lakini ziliendelea kuchezewa chezewa pale Mkoani mpaka sasa hivi tunavyoongea pesa haijaenda Kibondo. Lakini tunaambiwa tuna milioni 300 zina…

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nijue hiyo milioni 300 anayoizungumza kwamba itatolewa mwaka huu ni ile tuliyodhulumiwa Kibondo mwaka jana au inakuwa carried forward au ni ya mwaka huu? Naomba kujibiwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa amesema majibu ni mapesi, mtiririko wa mipango hauonekani vizuri ni kweli. Moja, tunataka kwanza tuwe na chanzo na chanzo ni Malagalarasi. Usanifu unaofanyika ni wa kutoa maji mto Malagalarasi kuleta Kaliua, Urambo na Tabora. Chanzo hicho hicho kikishakamilika ndiyo kitachukua maji kupeleka katika Jimbo lake ndiyo maana kidogo inamchanganya Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba mradi upo tukishakuwa na chanzo cha maji tayari kitakachobaki ni kuweka fedha kufanya utafiti mdogo wa kuyatoa maji kwenye chanzo ambacho kipo na kuendelea kukipeleka katika Jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na shilingi milioni 300, ni kweli, tulishaliongea hili nje na Mheshimiwa Mbunge, nikajaribu kufuatilia nikakosa majibu na juzi nilikuwa Kigoma. Hata hivyo, nimhakikishie kwamba sasa tutaunda Tume ndogo ili kuweza kuangalia kuhusu hizi shilingi milioni 300, moja je, ni kweli zilitolewa, na kama zilitolewa ziko wapi? Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge hapa hakiliwi kitu, kama kuna mtu atakuwa amefanya fujo, taratibu na Sheria za Kiserikali zipo atashughulikiwa. (Makofi)
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Ningeomba Naibu Waziri nami anithibitishie je, ni lini Serikali italeta maji au mtandao wa DAWASA utafika katika Kata za Kiburugwa, Kilungule na Chamazi kwa sababu tangu nchi hii kupata uhuru eneo hilo halijawahi kupata maji na wala hakuna mpango wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, visiwa vya Kimbiji vinakamilika lini? Maana yake...
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilishatamka katika Mbunge hili kwamba vyanzo tumekamilisha, visima vya Mpera pia vimekamilika, Ruvu Chini imekamilika, Ruvu Juu imekamilika. Kilichobaki sasa hivi tayari tunaendelea sasa na mikataba ya kutengeneza usambazaji wa hayo maji kuyapeleka kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo napenda, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sasa hivi tuna mkataba mmoja, tumeshapata fedha kutoka Benki ya Dunia dola milioni 50, tunajipanga kuhakikisha maeneo yote ya Dar- es - Salaam yanapata huduma ya maji kwenye vijiji, vitongoji na mitaa yote. Kwa hiyo asiwe na wasiwasi maji yatapatikana. (Makofi)
MHE. FAIDA MOHAMED. BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu hapa kwamba maji yanatosheleza kulingana na ujazo uliopo, lakini cha kushangaza ni kwamba maji hayo hasa vijijini hayapatikani kwa ukamilifu.
Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuyasambaza hayo maji anayosema yapo, maana kuwepo tu ardhini na juu ya ardhi si sababu ya kuyasambaza maji hayo ili yawafikie wananchi na kuwapunguzia matatizo hususani wanawake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maji ya baharini tunayaona, hasa mvua ikinyesha maji ya mvua yanaelekea baharini, mwisho wake ni baharini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga mabwawa yaliyo mengi katika nchi yetu kila eneo ili kuyahifadhi maji hayo kwa matumizi ya wananchi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni kwamba kweli kuna kiwango kikubwa cha maji hapa nchini, lakini yapo maeneo hapa nchini ambayo hayana maji. Hilo ni kweli kabisa kwamba yapo maeneo na ndiyo maana Serikali kuanzia bajeti ya mwaka 2006/2007 ilianzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Malengo yake ni kuhakikisha kwamba tumeyachukua haya maji na kuyafikisha maeneo ambayo yana ukame. Programu hiyo imeenda mpaka Juni mwaka 2015, na sasa hivi tumeingia kwenye awamu ya pili.
Mheshimiwa Spika, lakini matokeo ya programu hiyo ni nini? Tayari tumesaini mikataba ya kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka Shinyanga na sasa hivi tumesaini mkataba mwingine tunatoa Shinyanga kupeleka Nzega, Tabora hadi Igunga. Hiyo ndiyo tunaendelea utekelezaji wa kuichukua sasa hiyo hazina ya maji iliyopo ili tuweze kuyasambaza kwa wananchi, na tunapoyapeleka tunapita kwenye vijiji mbalimbali vingi kuhakikisha wananchi wanapata maji.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kweli mvua zinanyesha ni nyingi katika nchi yetu na maji haya yanapotea yanakwenda baharini, tunafanyeje? Tayari tumeshatengeneza utaratibu, tumeagiza kila Halmashauri kila mwaka kwenye bajeti zao watenge fedha ili kuhakikisha wanavuna maji. Si hilo tu, ni kwamba kwenye maeneo ambayo Halmashauri wanahitaji hayo maji kwa ajili ya wananchi kupata maji safi na salama, Wizara ya Maji na Umwagiliaji pia tunatoa fedha kwa ajili ya kujenga hayo mabwawa madogo na ya kati. Pia tunaendelea sasa kujenga mabwawa makubwa ya kimkakati ambayo yatazalisha umeme wakati huo huo tutapata maji kwa ajili ya umwagiliaji na tutapata maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu. (Makofi)
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mkoa wa Katavi bado una changamoto ya kupata maji safi na salama, lakini kibaya zaidi katika Jimbo la Katavi ambalo ni Jimbo la Mheshimiwa Waziri, katika maeneo ya Songambele, Kamsisi na Ilunde hakuna maji kabisa. Sasa Mheshimiwa Waziri ni lini utapeleka maji kwa sababu wananchi hawa umewatelekeza kwa muda mrefu? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, nijibu tu swali kwa ufupi kwa Mheshimiwa Rhoda Kunchela kwa sababu amechokoza jimbo langu.
Mheshimiwa Spika, Kamsisi wana visima vitatu tayari na wanapata maji. Songambele wana visima vinne na tayari wanapata maji, Ilunde tayari wana visima vitano na tayari wanapata maji, ndiyo tunaongeza vingine, kwa hiyo tayari jimbo langu linatendewa haki. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Wanaulanga kwanza naomba niishukuru Serikali kwa ukamilishaji wa Daraja la Mto Kilombero, haya ndiyo matunda ya Serikali ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo yanazunguka Mto Kilombero yana shida kubwa sana ya maji…
Mheshimiwa Spika, Daraja la Mto Kilombero la kwenda Ulanga, limelamilika.
Mheshimiwa Spika, lile limekamilika, lile kubwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, kabisa na tunapita pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu ni hili, maeneo ambayo yanazunguka huu Mto Kilombero yana shida kubwa sana ya maji kwa upande Wilaya ya Kilombero, kwa maana ya Ifakara Mjini, pamoja na Tarafa ya Lupilo. Je, sasa Wizara ina mpango gani wa kubadilisha matumizi ya Mto Kilombero ili uwe unatumika kwa matumizi ya binadamu, kwa maana ya maji ya kunywa na kupikia?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri nimetembelea Morogoro kwenye Majimbo yote na Halmashauri zote, nimefika mpaka Mto Kilombero. Kwanza baada ya kuvuka Kilombero, Lupilo pale tayari tulishaweka mfumo wa maji na wananchi wanapata maji safi na salama. Maeneo mengi tunaendelea kuhudumia kwa kutumia Bonde la Mto Kilombero, lakini mawazo yako pia pale itakapofika sasa inahitajika tutajenga bwawa kulingana na uwekezaji uliopo na idadi ya watu waliopo. Tutajenga bwawa kubwa Mto Kilombero ili tuweze kuwahudumia wananchi. Lakini kwa sasa bado tunaendelea kutumia Bonde la Mto Kilombero, wananchi wote wanapata maji safi na salama.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi zake za kuhakikisha viwanda vinakuwa vingi nchini.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika majibu yake ya swali la msingi amegusia upatikanaji wa faida kwa kuhusisha kwa kuwa na miundombinu rahisi kwa kufikisha malighafi kwenye viwanda.
Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba hadi sasa baadhi ya maeneo miundombinu ya barabara si rafiki kwa magari yanayobeba bidhaa, hali kadhalika miundombinu hiyo haileti tija kwa wafanyabiashara wa viwanda na wanaokwenda viwandani kununua na kupelekea walaji kwa maana ya wananchi kuwauzia?
Je nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha miundombinu hiyo itaboreshwa na kuimarishwa ili kuwapa nafuu wale wanaozalisha na wanunuzi wa hizo bidhaa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kujua, viwanda vinapoanza kunakuwa na utaratibu wa kuangalia hali ya mazingira rafiki kwa wananchi. Viwanda vile vinapoongezwa kwa maana ya wanavyopanua au kuongeza idadi ya miundombinu ya uzalishaji mali.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuangalia usalama wa raia wanaozunguka kiwanda, hali kadhalika na wale wanaofanya kazi katika viwanda vile? Tumeshuhudia wengi wakiathirika, naomba majibu ya maswali hayo.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI):
Mheshimiwa Spika, ninaamini kwamba Mheshimiwa Mbunge yupo Tanzania. Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika suala la miundombinu yeye mwenyewe ni shahidi, kila kona zinajengwa barabara za lami ili kuunganisha Mikoa na Wilaya kwa barabara imara zinazopitika mwaka mzima.
Mheshimiwa Spika, kuhusu upande wa umeme, maana mali ikishazalishwa inahitaji kusafirishwa kwenda kwa wananchi inatumia barabara, lakini pia kuna miundombinu imara na Wizara ya Nishati na Madini inaendelea kuweka umeme wa msongo mkubwa ili viwanda visipate shida kwa ajili ya kupata power, pia pamoja na matumizi ya gesi. Kwa hiyo, suala la miundombinu, Mheshimiwa Mbunge linakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, lakini pia ni mwaka huu tu kupitia TAMISEMI tayari na ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, tumeunda Rural Road Agency ili kuhakikisha sasa utekelezaji wa barabara zile ndogo (feeder roads) zinafika kila kona ili mali zinazozalishwa viwandani ziweze kwenda kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la usalama viwandani; kuna usalama kupitia kwenye mazingira, lakini kuna usalama wa watumishi wanaofanya kazi ndani ya viwanda. Suala hili linashughulikiwa vizuri sana na idara husika ya mazingira kuhakikisha kwamba matatizo yanayojitokeza ndani ya viwanda hayaathiri wananchi wanaoishi katika mazingira ya pembezoni mwa kiwanda kama tulivyojibu katika swali la msingi, lakini pia yapo masuala ya usalama yanayokuwa-addressed ndani ya watumishi kwenye viwanda.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi uliyonipa, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na Mheshimiwa Vulu kwa maswali yake mazuri sana ya mazingira hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, ameuliza swali linalohusu miundombinu. Actually, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyoeleza, kwamba tunafanya tathmini ya mazingira kabla kiwanda hakijaanza ili kuona kwamba kiwanda hicho mahali kinapowekwa kama hakitakuwa na madhara yoyote katika mazingira au kwa wananchi wanaoishi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, sasa pale inapojitokeza kiwanda kinataka kupanua miundombinu yake katika eneo husika, tunafanya tena tathmini ya athari kwa mazingira ili kujiridhisha, je, upanuzi na miundombinu inayoongezwa haitakuwa na athari yoyote ile kwa mazingira? Kwa hiyo, Mheshimiwa Vulu wala asiwe na wasiwasi, kila kiwanda kinapopanua miundombinu huwa tunashiriki na kujiridhisha kwamba hakuna athari yoyote ile kwa mazingira.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umeme wa gridi mpaka kufika Mkoa wa Katavi utachukua muda mrefu; na kwa kuwa umeme hautoshi Mkoani Katavi, lakini pia napenda kuishukuru Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uholanzi kwa ujenzi wa jenereta mbili na jenereta hizo zimeanza kufanya kazi kutoka tarehe 27 Mei, 2017 , lakini jenereta hizo hazitoshi.
Mheshimiwa Spika, umeme unaotakiwa Mkoa wa Katavi ni megawati tano, jenereta zinazalisha megawati 2.2. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza jenereta nyingine mbili kwa Mkoa wa Katavi? Kwa sababu mahali pa kuzifunga jenereta hizo tayaripameshajengwa, maana eneo la hizo jenereta limejengwa sehemu za kufunga jenereta nne, lakini Serikali pamoja na Serikali ya Uholanzi imefunga jenereta mbili, eneo hilo lipo. (Makofi)
Meshimiwa Spika, je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza jenereta mbili?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa jenereta hizi zinatumia mafuta ya dizeli na ni gharama zaidi, je, Serikali haioni kwamba matumizi ya jenereta kwa Mkoa wa Katavi ni gharama zaidi kuliko kufunga umeme wa gridi? Naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, maswali yake ni mazuri na kwa faida ya Mkoa wa Katavi ambao na mimi mwenyewe natoka kule siwezi kuahidi lakini niseme kwamba nitalifikisha hili ili waweze kuongeza jenereta nyingine mpya kuongeza umeme. Lakini pia haya masuala ni ya kiuchumi. Ipo historia kwamba matumizi ya umeme katika mkoa wetu, hasa katika masuala ya viwanda bado hatujawa na viwanda vingi, kwa hiyo umeme sehemu kubwa unatumika majumbani tu na taarifa iliyopo ni kwamba TANESCO imekuwa inatoa gharama kubwa zaidi kuliko makusanyo yanayofanywa kutokana na matumizi ya umeme, lakini suala hili tutalifikisha.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili linalozungumzia dizeli. Ni kweli kabisa kwamba kutumia dizeli ni gharama kubwa kabisa na ndiyo maana sasa hivi Serikali nzima inataka kwenda kwa kutumia umeme ama wa gesi au wa maji, na ndiyo maana sasa Serikali imeshalitambua hili, inaleta umeme wa msongo mkubwa ambao sehemu kubwa utatumia uzalishaji kwa kutumia maji badala ya kutumia dizeli. Kwa hiyo, mawazo yako Mheshimiwa Mbunge ni mazuri na tayari Serikali imeshaanza kuyatekeleza.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, tatizo la umeme wa Gridi ya Taifa kutokufika kwa wananchi haliko tu Mkoa wa Katavi, bali pia liko katika Jimbo la Kibamba, Jijini Dar es Salaam ambapo kwenye Kata ya Mbezi maeneo kama ya Msumi kwa Londa hayana kabisa miundombinu ya umeme. Kata ya Goba kuna mitaa ambayo haina umeme, Kata ya Msigani kuna mitaa ambayo haina umeme, Kata ya Kwembe kuna mitaa haina umeme, Kata ya Saranga kuna mitaa haina umeme na Kata ya Kibamba kuna mitaa haina umeme.
Sasa kwa kuwa TANESCO iko jirani kabisa na Jimbo la Kibamba, je, Serikali iko tayari baada ya Mkutano huu wa Bunge kufanya ziara maalum kwenye kata hizi zote sita kwenda kuwaeleza wananchi ni lini hasa maeneo haya yatapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI): Mheshimiwa Spika, niseme kwanza Serikali iko tayari ndiyo maana imeanzisha REA III, na tayari maeneo mengi miradi imezinduliwa kuhakikisha kwamba vijiji vyote tulivyonavyo katika Tanzania vinapata umeme. Kwa hiyo, tayari imeshaanza, lakini niseme Mheshimiwa Mbunge mimi na wewe ni Madiwani tuna uwakilishi ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, ni kazi yetu sasa kwamba wewe kwasababu ni Mbunge uko ndani ya Bunge na matamshi haya ya Serikali umeyasikia, urudi kwenye Jimbo lako ukawaambie kuwa “jamani sasa Awamu ya Tatu ya REA inafika na kwetu tunapatiwa vijiji moja, mbili, tatu” na vijiji vyako vimeainishwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, kwa hiyo uende ukatoe taarifa.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante; nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya ufafanuzi. Kwa kuwa tumeshuhudia kwenye luninga wakiteketeza vifaa hivi na wanaoingiza kupata hasara, Je, ni hatua gani zaidi zinazochukuliwa kwa wale wanaoingiza ili kukomesha hali hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vifaa bandia havitoki tu nje ya nchi, vingine vinatengenezwa humu humu nchini. Mimi naomba kujua ni hatua gani zinazochukuliwa na Serikali ili kukomesha kabisa vifaa hivyo, vikiwemo viatilishi, pembejeo za kilimo, vipodozi vya kina mama, na hata vingine ambavyo si rahisi kutamka hapa hadharani? Naomba kujua. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI):
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza nakiri na amekubali jibu kwamba kweli vile vifaa vinateketezwa na yeye mwenyewe ameona; lakini ni hatua gani zinachukuliwa sasa kwa wale ambao wameshikwa na hizo bidhaa bandia.
Mheshimiwa Spika, ni kwamba, tunazo sheria nchini, yule anayeshi kwa na vifaa bandia ni kwamba anapata stahili kulingana na sheria. Wakati mwingine wanatozwa faini na pengine inaweza hata zaidi ya hiyo akapewa adhabu stahiki.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili amesema kwamba hivi vifaa bandia sio kwamba vinatoka nje ya nchi tu, kuna vingine vinatengenezwa humu ndani. Kwa mfano, kama vipodozi wapo watu wanachanganya vipodozi na wamewaathiri sana wale ambao wanatumia.
Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kufunga viwanda vile ambavyo havijasajiliwa na mara nyingi hivi vitu ambavyo vinafanywa ambavyo havipo katika viwango vinafanywa na viwanda bubu. Kwa hiyo, Serikali inafanya ukaguzi, kama tulivyojibu katika swali la msingi ili kuhakikisha kwamba hawa wote wanaofanya hivyo wanakamatwa na wanapewa adhabu stahiki kwa mujibu wa sheria na viwanda vinavyojihusisha na hivyo tayari vinafungwa ili kuhakikisha kwamba suala hilo haliendelei. Vilevile pia nimeongea na Mheshimiwa Waziri akasema kwamba wanatarajia kuleta sheria itakayotoa adhabu kali zaidi hasa kwa hawa watu ambao wanatengeneza vitu bandia.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa vifaa vya bandia kwenye maduka sasa hivi siyo siri tena, hata ukienda wanakwambia kuna hiki hapa ambacho ni dhaifu, kuna hiki hapa na bei pia ni tofauti. Kwa hiyo si kwa njia ya vichochoroni hata madukani vipo na vinauzwa halali kabisa.
Je, Serikali haioni, kuruhusu kuwepo kwa bei aina mbili/tatu kwenye kifaa kimoja dukani ni kuruhusu kuwepo kwa vifaa bandia kihalali kitu ambacho tunapiga marufuku katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI):
Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri ni kweli, unakwenda dukani unakutana na hiyo hoja. Na hoja yenyewe inakuwa kwenye kukata mapato kwenye TRA, na ndio maana juzi juzi hapa, kama umeongea na wafanyabiashara TRA imeendelea kuweka sheria ngumu ikiwepo pamoja na kila duka hata kama ni dogo lazima liwe na ile mashine ya EFD kwa ajili ya kupata zile recept ili waweze kulipa kodi.
Mheshimiwa Spika, lakini Wizara ya Fedha inaendelea kuweka sheria kali na ukaguzi mkubwa sana katika bidhaa. Suala moja ambalo ni zuri kwa sisi Waheshimiwa Wabunge ndugu zangu tuendelee kuwaelimisha wananchi wetu. Sasa kama wewe unapewa hiyo kauli, kwamba ukitaka bidhaa hii itakuwa na shilingi kadhaa lakini hii itakuwa na bei chini zaidi, wewe mwenyewe lazima ujiulize kwamba kwa nini hii ni chini?
Mheshimiwa Spika, kama ningelikuwa ni mimi ningeweza nikasema basi naomba uniuzie hiyo hiyo ya bei ambayo ni kubwa lakini unipe receipt. Kwa sababu hiyo moja kwa moja ameshakwambia hii haina ubora, sasa wewe kwa nini uende ukanunue.
Mheshimiwa Spika, lakini nakiri pia kwamba, si wananchi wote wa Tanzania hasa vijijini wenye elimu ambayo naweza nikawa nayo mimi au unaweza ukawa nayo Mheshimiwa Sakaya. Sasa ni suala letu sisi Waheshimiwa Wabunge na Madiwani na Serikali kwa pamoja tuendelee kuwaelimisha wananchi ili waweze kukwepa haya na ndiyo maana Serikali sasa inaweka viwanda vya ndani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hiyo kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba hata viwanda vya ndani nao wanaweza wakafanya vitu vya namna hiyo. Ndugu zangu tunayo kazi kwa hiyo tuendelee kuelimisha jamii na kutunga sheria zilizo kali na tuzisimamie ili haya yaweze kuondoka.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, na mimi niungane na wenzangu kukupa pole na kushukuru na kufurahi kukuona leo Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge aliyetangulia, Mohamed Kigua, kwamba kwa kweli miradi ya maji ina matatizo mengi na ni vizuri kwa kweli tathmini ikafanywa. Wilaya yangu ya Hanang ina visima vilivyochimbwa vina mwaka mmoja hakuna kuendeleza maji yakapatikana na watu wanatoa machozi pale, na mimi naomba na tathmini hiyo au Tume nayo iende kule Hanang kuona tatizo ni nini ili tuweze kusahisha wananchi wapate maji.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, na mimi nichukue nafasi hii kukukaribisha. Karibu sana kwenye Bunge, tangu ulivyotuacha, tunaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Mary Nagu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kuhusu changamoto za miradi, Wizara yangu tayari imeunda timu ya wahandisi ambayo imeshaanza kazi, ambayo itakuwa inapitia maeneo yote ya changamoto. Ni wataalam wazuri, wataainisha changamoto zote ili tuweze kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, pili, kuhusu miradi ambayo tumeshapata vyanzo vya maji kama kwa Mheshimiwa Mary Nagu kule Katesh, katika Programu ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji kwanza tunatafuta chanzo, tukishapata chanzo ndiyo tunatafuta sasa fedha kwa ajili ya kuweka mtandao wa mabomba.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mary Nagu kwamba bajeti inayokuja tutaweka fedha za kutosha ili tuweze sasa kuyachukua maji na kuyapeleka kwa wananchi. (Makofi)
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa kumuuliza swali moja la nyongeza.
Kwanza, tunataka tupate ripoti na siyo cheti kwa sababu cheti kinakuwa ni uthibitisho tu, lakini ripoti ndiyo kitu ambacho tunaweza kuona athari iliyopo au hakuna athari.
Pili, nilitaka kuelewa kwamba bwawa lile liko maeneo ya upande wa Morogoro, lakini wananchi wa pale wanategemea sana kuzalisha pamoja na mazao ya miwa na mpunga lakini na mazao mengine mbalimbali ambayo yako katika eneo lile.
Je, wasiwasi wangu uliokuweko maporomoko ya maji na mwelekeo wa maji ambayo yanashuka katika lile bwawa hayatoweza kuathiri mmomonyoko na uharibu wa lile bwawa pengine labda ikasaidia kuingia na kufanya contamination ya maji ambayo yatakuwa yanaingia katika maeneo yale.
Je, Serikali iko tayari kuweka utaratibu mzuri wa kilimo ambacho kitakuwa hakitumii kemikali ili kuepukana na athari za kikemikali katika maji yale ambayo wanatumia binadamu na kilimo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameomba kwamba kile cheti cha NEMC kiwasilishwe Bungeni, lakini kwa mujibu wa swali lake aliuliza, je, Serikali inaweza kuleta Bungeni ripoti ya tathmini pamoja na Environmental Impact Assessment juu ya mradi huo. Tumesema ndiyo tunaweza, sasa kama swali la pili unataka tulete basi utuagize tulete tutaleta, lakini kwa mujibu wa swali lako tumeshajibu kwamba tunaweza tukaleta.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kama ilivyojibiwa kwenye swali la msingi na Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba ripoti ya NEMC ipo na imeweka tayari na Environmental Management Plan. Kwa hiyo, hakutakuwa na athari ya aina yoyote pale ambapo kutakuwa na athari basi ripoti ile itafuatwa wataweka utaratibu kuhakikisha kwamba madhara ya aina yoyote kuhusu kemikali hayatajitokeza, madhara kuhusu mmomonyoko pia hayatajitokeza. Kwa sababu utokaji wa maji kwenye bwawa utakuwa controlled kulingana na matumizi ya kupeleka maji kwenye mashamba pamoja na kupeleka maji Mto Ruvu.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza kuhusu Bwawa la Kidunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu mradi huu mpaka sasa accessibility ya kufika sehemu ambayo inajengwa bwawa haifikiki kirahisi ni pamoja na utekelezaji huu, lakini kulikuwa na mpango wa kuiboresha na kuitengeneza barabara hii ili ujenzi huu uweze kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua katika upande wa Serikali, ni lini barabara hii itaanza kujengwa ili kurahisisha ujenzi wa bwawa huu kuanza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mgumba kwa kuuliza swali ambalo ni la msingi, lakini jibu ni moja dogo kwamba katika mwaka wa fedha unaokuja tumetenga fedha, kwa hiyo utaiona hiyo fedha kwenye wasilisho la bajeti ya Waziri wa Maji ambapo tutaanza na ujenzi wa barabara ili kumwezesha Mkandarasi sasa awe na uwezo kwenda kujenga bwawa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina swali dogo kwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ya Morogoro inafanana sana na shida iliyoko Kigoma ambapo Mkoa wa Kigoma tuna mradi wa maji wa Ubelgiji ambao fedha zake zimeshasainiwa. Katika Mji wa Kasulu vijiji vya Nyansha, Nyantale na Kibondo vina shilingi bilioni mbuili katika mradi huo. Hata hivyo tangu fedha zimesainiwa kati ya Waziri wa Fedha na Balozi wa Ubelgiji mpaka sasa hakuna kazi yoyote iliyofanyika.
Mheshimiwa Mwneyekiti, ni kwa nini Wizara haifuatilii mradi huu ambao tayari una fedha zake; lakini bado haujaanza kwa sababu ya urasimu tu? Nilikuwa naomba majibu katika swali hilo.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Nsanzugwanko kuhusiana na shilingi bilioni 18 kutoka Ubelgiji ambazo zimeelekezwa moja kwa moja Kigoma kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kwenye eneo lake la Kasulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi una hatua zake. Hatua ya kwanza, kusaini mkataba wa kifedha, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameshasaini. Hatua ya pili sasa hivi Katibu Tawala wa Mkoa anaendelea na kufanya manunuzi kwa ajili ya kupata wakandarasi. Baada ya kukamilisha hayo manunuzi basi utaratibu wa utekelezaji wa miradi utaanza.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Liwale ni mji unaokua kwa kasi sana hasa baada ya korosho kufanya vizuri na kuna mradi wa kutafuta chanzo cha maji mbadala kwa Mji wa Liwale. Mradi ule sasa hivi una zaidi ya miaka minne umesimama. Nini kauli ya Serikali juu ya kuwapatia maji wananchi wa Mji wa Liwale? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeelekeza kwamba maeneo yote ya vijijini yatapata maji kufikia asilimia 85 na mijini asilimia 95. Mheshimiwa Mbunge naomba uvute subira kidogo, tarehe 7 mpaka 9 Mei, 2018 tutawasilisha bajeti yetu kwa hiyo miradi yako yote ambayo ilikuwa imekwama utapata kidogo maelekezo kule ndani na tutahakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Katika vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, ni pamoja na vijiji vya Wilaya ya Namtumbo. Nampongeza sana kwa safari yake na mambo makubwa tuliyoyafanya katika Wilaya ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka tu nifahamu, kwa kasi ile aliyoitumia kutatua miradi mitano ambayo ni ya World Bank, atatumia kasi ile ile kutatua miradi mitano mingine ili tutimize ile miradi kumi ya World Bank?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kasi hiyo hiyo ambayo tumeitumia kukamilisha miradi inayoendelea, tutaendelea nayo kwa sababu bado tuna miradi 376 ambayo haijakamilika kutoka kwenye miradi 1,810. Kwa hiyo, kasi ni hiyo hiyo. Tunachosisitiza ni kwamba Halmashauri ziendelee kusimamia vizuri wakandarasi watekeleze miradi na sisi wakati wowote kutoka kwenye Mfuko wa Maji ukileta certificate tunalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji aliyomjibu Mheshimiwa Chikambo, Mheshimiwa Chikambo katika swali lake aliomba aletewe orodha ya miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge wote, nilitaka tu nizungumze kwamba Wizara ya Maji inatenga fedha na inapeleka katika Halmashauri. Watekelezaji ni Halmashuri. Wao ndio wanaoweka mpango kazi kuona ni vijii gani watatekeleza. Kazi yetu sisi kuweka ni miongozo na wakishatekeleza, wanaleta hati, sisi tunalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pia hilo ni jukumu la Waheshimiwa Wabunge wao wenyewe kwa sababu ni Madiwani kwenye maeneo yao kujua ni miradi ipi inatekelezwa ni miradi mingapi.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Bwawa la Kidete pale Kilosa ni bwawa ambalo kila mwaka linaleta maafa makubwa sana, reli inang’oka, wananchi wa Mabwelembwele, Masanze, Tindiga pamoja na Magomeni wamekuwa wakiathirika sana mafuriko makubwa. Mwaka 2017 nilipouliza Mheshimiwa Waziri alinijibu kwamba Serikali imeshatenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hili muhimu la Kidete.
Je, ni lini Serikali itapeleka pesa hizo ili ziweze kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Kilosa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Kidete nimelitembelea, nikakuta topography jinsi ambavyo imekaa, kidogo ni tete, kwa sababu juu ya bwawa kuna reli, chini kuna kijiji. Ukijenga bwawa ukaweka tuta kubwa ni kwamba maji yatazamisha reli.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na changamoto hiyo, tumeunda timu ya wataalam ambao walianza kazi mwezi uliopita na Mheshimiwa Mbunge nitakuomba tu wiki hii, nina imani watakuwa wameshamaliza kazi hiyo ili niweze kukujibu ni nini sasa kinafuata baada ya kukamilisha huo usanifu? (Makofi)
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuwa Wilaya ya Ugunga na Jimbo la Igunga kwa ujumla lina uhitaji mkubwa sana wa mabwawa kama ilivyo Lupa; na kwa kuwa mabwawa ya Mwanzugi na Igogo sasa yamefikia uhai wake, yalijengwa miaka ya 1970, hayana nafasi tena ya kuendelea.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutujengea mabwawa mengine mawili kwa ajili ya umwagiliaji kama yalivyokuwa haya mabwawa mawili? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwamba mabwawa mengi uhai wake umeisha kwa sababu ya mabwawa hayo kujaa udongo badala ya kujaa maji. Kwa bahati nzuri Jumamosi iliyopita, nilikwenda kutembelea Chamwino, nimeenda kutembelea Bwawa la Chalinze nalo nikakuta lina shida hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimeunda kikundi cha wataalam ili tujaribu kutafuta teknolojia ambayo inaweza ikayaondoa matope kwenye bwawa bila kutumia gharama kubwa. Tukishafaulu hilo Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie, tutatumia teknolojia hiyo ili kuhakikisha mabwawa yote nchini tunaondoa udongo badala ya kuanza kuchimba mengine. Sawa, mengine tutachimba, lakini haya yaliyopo ni lazima tuyahifadhi.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nipongeze kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii, inaonekana wanakwenda kwa kasi nzuri, lakini miradi mingi ya mabwawa na miradi ya umwagiliaji mingi inaanzishwa lakini haikamiki, aidha, kutokana na upungufu wa fedha au kuwa imekuwa designed vibaya. Mfano mzuri ni miradi ya vijiji vya Utimbe, Runyu na Longa katika Jimbo la Mtama.
Sasa Serikali haioni kwamba ni vizuri wakaacha kubuni miradi mipya wa-concentrate na kumalizia miradi hiii ambayo kwa miaka mingi hawajaimaliza na pesa zimezama kwenye miradi hii?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba changamoto hiyo tumeiona katika Wizara yangu kwamba miradi mingi ilibuniwa lakini haikukamilika na haikukamilika kwa sababu miradi mingi imekuwa inatekelezwa na hela za wafadhili ambao wao wenyewe walikuwa wanachagua miradi, lakini pia wanaweka ceiling ya fedha na wanalazimisha kwamba mradi huo lazima utekelezwe kulingana na design kwamba ile hela iliyotolewa haiwezi kufanya mradi sasa ukawa umekamilika na kuweza kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri na Kamati yangu imeliona hilo, tumelijadili na kuanzia sasa tunataka kuweka utaratibu maalum kwamba kama kuna fedha haitoshi, hakuna haja ya kutekeleza huo mradi. Lazima tuweke fedha ambazo tukishauanzisha mradi, tuchimbe bwawa, tuweke na scheme ili wananchi waendelee kufaidi matunda ya Serikali yao. Hilo Mheshimiwa Mbunge tumeshaliona na tunalifanyia kazi.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na swali moja la nyongeza. Mji wa Kibondo unakaabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa maji, na mji huo uko kilimani. Pampu zinazosukuma maji kusambaza ndani ya mji wa Kibondo zimechakaa, ni lini Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya mradi wa maji Wilayani Kibondo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Genzabuke kuhusiana na matatizo ya maji ya Kibondo, kwanza Mheshimiwa Genzabuke pamoja na wananchi wa Jimbo la Kibondo nikufahamishe tu kwamba tayari tunasaini mkataba wa mkopo wa fedha nafuu kutoka Serikali ya India na katika ya fedha hizo sehemu ya fedha itashughulikia utoaji wa maji, huduma ya maji katika mji wa Kibondo, kwa hiyo sasa hivi vuta subira mambo baada ya muda mfupi yatakuwa mazuri. (Makofi)
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo lililopo Maswa Magharibi linafanana na la Mvomero, na kwa kuwa Mvomero kuna maji mengi, kuna mabonde mazuri sana na kwa kuwa wananchi wa Mvomero wamejipanga katika kilimo cha umwagiliaji, na kwa kuwa kuna ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Maji injinia Isack kwa kusaidia mabonde mawili, Bonde la Kigugu na Bonde la Mbogo, je, ni lini fedha zile zitatoka ili kuleta tija kwa wananchi wa Mvomero na Taifa kwa ujumla? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika bajeti ya mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kuendelea na usanifu wa miradi ya Kigugu na usanifu umekamilika, wakati wowote Mheshimiwa Murad nikuhakikishie hatutaingia kwenye kutangaza tender kuhakikisha kwamba hiyo miradi imetekelezwa.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Dar es Salaam pale kwenye kulaza bomba la kutoka Bagamoyo kuja Chuo Kikuu kuna watu walivunjiwa na watu wengine wakakataa wakapelekwa mahakamani, walipopelekwa mahakani wameshindwa mpaka leo wanasema wanalindwa na wakubwa hawataki kuvunja nataka Wizara iniambie wanavunjiwa lini ili Dar es Salaam tupatae maji Chuo Kikuu? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanayo taarifa kwa sababu wameshapewa notice kwamba wanavunjiwa, kwa hiyo ni wakati wowote hatua za kuvunja zile nyumba zitafanyika.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pia ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya swali la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri hao wote wawili wa Wizara hii; Waziri na Naibu wake wamefika eneo hilo. Mara ya mwisho mwezi wa pili Mheshimiwa Naibu Waziri amefika na wana Malinyi tumempa jina la Dogo Janja. Ameona hali halisi pale katika Skimu ya Itete, kwa kuwa imetokana na usanifu wa kina ambao haukuwa mzuri na hata ujenzi ule uliofanyika haukuwa mzuri imesababisha skimu ile inashindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu ile haina barabara za kuingia kwenye mashamba, skimu ile wakati wa kiangazi haina maji ya kutosha kumwagilia mashamba yale na Serikali wameadhidi kwamba watafanya marekebisho swali langu la kwanza, ni lini mtafanya marekebisho ambayo mmehaidi kwenye Skimu ya Itete?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, menejimenti ya skimu ile inasimamiwa na injinia ambaye anakaa Malinyi kilometa 50 kutoka pale kwenye skimu mpaka anapoishi yule injinia; tuliomba ombi maalum apatiwe usafiri injinia yule, ni lini sasa ombi hili litatekelezwa? Nakushukuru sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nimefika pale Itete na Mheshimiwa Naibu Waziri amefika. Tatizo moja kubwa la Itete ni kwamba skimu ipo haijakamilishwa ujenzi lakini inafanya kazi. Tatizo lililo kubwa ni kwamba sasa hivi baada ya kumaliza huu mpango kabambe tunataka kujenga bwawa kubwa ambalo litatunza maji ili wananchi waendelee kulima wakati wote. Tatizo lingine lililokuwepo ni kwamba ile Kamati iliyokuwa imeundwa ambayo inasimamia kilimo kile cha mpunga ilikuwa na makosa kidogo, tukaivunja na sasa hivi tumeweka nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ombi lake la kwamba injinia sasa awe sehemu ya karibu kwa ajili ya kusimamia ile skimu tutalitekeleza tuwasiliane Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kumpatia huyo injinia. (Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyogeza. Kwanza sina budi kuwashukuru vyombo vyote vya ulinzi na usalama, Kibiti hali shwari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, wananchi wa maeneo ya Delta, Mbwela, Msala, Salale, Mapaloni, Kiongoloni wana shida kubwa ya maji ambayo sasa inapelekea hata ndoa kulegalega kwenye nyumba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia maji safi na sala katika maeneo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Delta tayari tumelifanyia utafiti na tumechimba visima kiasi. Ukienda zaidi ya mita tano unapata maji ya chumvi, kwa hiyo, sasa tunajaribu kuangalia mfumo mzuri ambao utahakikisha kwamba wananchi wa Delta wanapata maji bila shida, lakini ukienda mita nne tayari tumechimba visima wanapata maji safi na salama.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yaliyopo huko kwenye jimbo Mheshimiwa Mgimwa yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika jimbo langu ambapo Serikali imeonesha nia njema ya kujenga skimu ya umwagiliaji katika Bwawa la Itagata. Sasa kwa kuwa bwawa hili lilikuwa lilishaanza kuvuja na ile pesa ya kujenga skimu Serikali; maana ya Wizara ilituambia tutoe ili tuwape wale wakandarasi wa umwagiliaji kutoka Wizarani wa kuziba mabwawa; sisi pesa tumeshalipa.
Je, Serikali sasa iko tayari kurudisha ile pesa haraka ili na sisi certificate iliyioko kwenye halmashauri tuweze kumlipa mkandarasi katika Skimu ya Umwagiliaji ya Itagata? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kwanza nimpongeze kwa jinsi anavyofuatilia shughuli za ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji na kweli Bwawa la Itagata limekamilika. Naomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki leo tukutane ili tuweze kuangalia jinsi ya kukupa hiyo fedha muende mkakamilishe miradi mingine inayoendelea.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Mheshimiwa Waziri amekuwa akija Mkoani Lindi mara kwa mara, zaidi ya mara mbili au tatu nimekutana naye kwa ajili ya mradi ule wa maji pale Napa. Lakini tuna Skimu ya Umwagiliaji iliyopo kwenye Jimbo la Mchinga, ya Kinyope na skimu nyingine iko Jimbo la Mtama kwa Mheshimiwa Nape, ya Kiwalala. Skimu hizi zilijengwa chini ya kiwango na hivi sasa hazifanyi kazi vizuri ingawa zilitumie pesa nyingi ya Serikali. Je, Waziri uko tayari kutuma wawakilishi wako au wewe mwenyewe kwenda kujionea kinachoendelea katika skimu hizo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli skimu hizo zilitekelezwa, zilikumbwa na matatizo ya mafuriko lakini kwa sasa tayari tunazifanyia kazi ili ziweze kujengwa na kutimiza matakwa ambayo yalikuwa yanatakiwa kwa ajili ya kuwapatia wananchi huduma nzuri ya maji ili waweze kufanya kilimo cha umwagiliaji. Niko tayari kwenda kutembelea eneo hilo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lilikuwa linauliza habari ya ahadi za viongozi. Mheshimiwa Rais aliahidi pale Ilula, Kilolo kwamba suala la maji litakuwa ni historia. Nataka nijue Mheshimiwa Waziri ni lini mkataba ule utasainiwa ili wananchi wa Kilolo, Ilula tatizo la maji liwe historia kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu ujenzi wa mfumo wa maji Kilolo. Tulikuwa tunatarajia kwamba fedha ambazo zingetumika ilikuwa ni fedha kutoka Austria, lakini baada ya kuona kwamba fedha za Austria zinachelewa Serikali kwa kutumia makusanyo ya ndani imefanya mchakato imekamilisha na tarehe 30 Aprili, Jumatatu ijayo tunakwenda kutia saini mkataba ili sasa utekelezaji uanze wananchi wa Kilolo wapate maji. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa vitunguu katika Tarafa ya Eyasi wanayo miundombinu ya umwagiliaji ambayo imejengwa na World Vision na fedha za DADPs na Shirika na Maendeleo la Jimbo Katoliki la Mbulu na Waziri Mkuu alikuja kuzindua. Tatizo kubwa si miundombinu kama ambavyo imeelezwa na Mbunge mmoja hapa, suala ni uhifadhi wa chanzo ambao wakulima wale wanatumia kumwagilia vitunguu vyao. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhifadhi chanzo kile ili wananchi waweze kulima zao hilo? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bonde la Eyasi linatumia chanzo cha maji ya mbubujiko kutoka chini ya ardhi eneo la Mang’ola. Nilikwenda kule na tayari tumeshaweka mipaka ili kuzuia wananchi wasifanye shughuli za kibinadamu karibu na vile vyanzo. Mipaka hiyo inaendelea kuwekwa na Mheshimwa Mbunge tuendelee kushirikiana, na kama utaona kwamba kuna kitu ambacho hakiendi vizuri, tuwasiliane. Lengo ni kuboresha ili yale maji yaendelee kutoka kila wakati.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Naibu Waziri ametusaidia. Hili tatizo liko kutoka mwaka 2006. Sheria zipo, kanuni zipo na Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema hivyo, lakini iaonekana ni hadithi na ni mazungumzo tu humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutuambia ni vyanzo vingapi ambavyo tayari wamevifanyia demarcation na rehabilitation kama sampling areas ya kuhifadhi vyanzo vya maji, kama kweli wana nia ya kuhifadhi vyanzo vya maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge kwamba ni vyanzo vingapi. Hadi mwaka 2017 tayari tulishabaini vyanzo 18, tumeshaviwekea mipaka tayari. Mwaka huu wa Fedha tulionao tulibaini vyanzo sita, tunaendelea kuviwekea mipaka na tutaendelea kufanya hivyo. Mheshimiwa Mbunge usubiri hotuba yangu inaanza Jumatatu tarehe 7 Mei, kwa hiyo, taarifa kamili utaipata vizuri zaidi kupitia kwenye hotuba yangu. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye ameonesha dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwatua ndoo kichwani akinamama, nina maswali madogo mawili.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; wananchi wa Itigi kwa sasa wananunua maji ndoo moja Sh.1,000 hususani akinamama. Je, sasa Serikali, Mheshimiwa Waziri anaweza akawaambia nini wananchi wa Itigi ambao wanamsikiliza na kumwona katika TV muda huu, kwamba mradi huu utatangazwa lini, kwa kuwa kila kitu kimeshakamilika na wananchi wa Itigi tunataka kumsikia leo anasema nini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, yuko tayari sasa kwenda kuongea na wananchi wa Itigi kwamba mradi huu tunauanzisha lini katika kipindi cha mwezi huu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kama majibu ya msingi ambavyo yameelezwa na Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba utekelezaji wa miradi unakwenda katika awamu tatu na awamu zote sasa zimekamilika, tunakwenda kwenye utekelezaji. Pia tuna utaratibu ambao tunachimba visima na kufunga pampu za mkono wakati tunasubiri mradi mkubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama shida iko namna hiyo watu wananunua ndoo moja Sh.1,000 namwomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane, kwa sababu bajeti yake ipo, tutachimba visima vya haraka na kufunga pampu ili wananchi waachane na hilo la kununua maji ndoo Sh.1,000.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili; nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kuongozana naye kwenda Itigi tukaongee na wananchi huko baada ya bajeti yangu. (Makofi)

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, wananchi wa Longido wamekuwa wakisubiri kwa hamu kukamilishwa kwa mradi mkubwa wa maji safi na salama kutoka Mlimani Kilimanjaro, Mto Simba kuja Longido. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba mradi huu kwa kasi inayoendelea sasa hivi unatarajiwa kukamilika lini?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru kwa jinsi anavyofuatilia utekelezaji wa miradi ya maji katika Jimbo lake na Serikali hii ya Awamu ya Tano tayari ina mkataba wa zaidi ya bilioni 16 kwa ajili ya Halmashauri yake ya Longido.
Mheshimiwa Spika, uko mradi mkubwa unaotoa maji Mlima Kilimanjaro kilomita 64. Kulikuwa na matatizo ya kupata bomba la chuma lakini Serikali, Wizara imeingilia kati Mkandarasi ameingia mkataba na kiwanda cha kuzalisha mabomba na mabomba yameanza kuingia tayari kule site.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake kwamba kuanzia sasa tunaenda haraka ili tuhakikishe wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. JOSEPHINA T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kujitosheleza. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mahitaji ya maji katika Mji wa Geita na vitongoji vyake ni makubwa mno ukilinganisha na maji tunayopata; mahitaji halisi ni lita milioni 15 kwa siku, lakini maji tunayopata ni lita milioni nne kwa siku. Kwa hiyo, tuna upungufu wa lita milioni 11 ambayo ni sawa na asilimia 29 kwa siku. Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuongezea nguvu na uwezo Mradi wa Ziwa Victoria ili tuweze kupata maji ya kutosha kulingana na mahitaji yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna mradi wa maji katika Wilaya ya Nang’hwale. Mradi huu ni wa siku nyingi sana, hivi sasa ni miaka sita tangu uanzishwe, bado wananchi wanateseka wanahangaika kwa kupata maji. Naishukuru Serikali kwa kuweza kutenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya maji katika Wilaya ya Nang’hwale, je, Naibu Waziri yuko tayari sasa kwenda Nang’hwale ili akajionee hali halisi ya mradi ule ambao sasa hivi ni miaka sita haujakamilika na wananchi wanaendelea kuteseka mpaka sasa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Chagula, yeye ni mama na anadhihirisha kwamba mama wajibu wake ni kuhakikisha familia inapata maji. Nimkumbushe kwamba Serikali tayari imeshatekeleza awamu mbili za Programu ya Kulinda Ziwa Victoria, awamu ya kwanza ilikamilika na awamu ya pili imekamilika Desemba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumeanza awamu ya tatu na katika awamu hii Mheshimiwa Chagula, tayari tumepanga kutekeleza miradi kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka Ilemela, Buchosa, pale Geita, Katoro Buseresere. Pia tunatarajia haya maji tutapeleka hadi Mbogwe. Hili eneo la Mbogwe linaweza likapata maji kutoka eneo la Katoro, Buseresere au kutoka Msalala.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mradi huu utahusisha pia kupeleka maji Buhongwa, Sumve na Usagara. Majadiliano na wafadhili wakiwemo European Investment Bank, Benki ya Maendeleo ya Afrika, yanaendelea vizuri na pia tutahakikisha kwamba hili eneo la Geita Mjini ambao ni mkoa mpya nalo limeingizwa ili tuweze kuongeza kiwango cha maji katika hilo eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu Nyang’hwale, kwa bahati nzuri nimetembelea Nyang’hwale nikakuta ule mradi umekaa muda mrefu sana. Nilitoa maelekezo na kila siku tatu naongea na Mbunge wa Nyang’hwale ili awe ananipa progress nini kinaendelea. Ameniridhisha kwamba mkandarasi sasa yuko site. Na mimi sasa kwa sababu ameomba kwenda na Mheshimiwa Naibu Waziri, nampa kibali hapa hapa Mheshimiwa Mbunge aende naye. (Makofi/Kicheko)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ninayo maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Lucy Magereli. Swali la kwanza, wakati wa Bajeti ya Wizara ya Maji, Kamati ya Kisekta na Waheshimiwa Wabunge walipendekeza kwamba tuongeze Sh.50 katika mafuta ili kupata fedha ya kupeleka maji vijijini na mijini ili kumaliza tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni je, kwa maelezo ya majibu ya Wizara hii, na mradi umeanza tangu mwaka 2013 ulipaswa kuisha mwaka 2016, huu ni mwaka 2018; si kwamba kuna upungufu wa fedha ndiyo maana mradi huu unasuasua? Kwa hiyo ningeomba nipate kauli ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa mjadala wa Wizara ya Maji, ukurasa wa 56, mradi huu wa visima virefu wa Kimbiji na Mpera vinahusu pia Jimbo la Ukonga Kata ya Msongola, Chanika, Buyuni, Pugu, Kitunda na Ukonga. Sasa ningeomba nipate kauli ya Serikali hapa wamesema watu wa Kigamboni kuna mradi mbadala wa kupeleka maji katika eneo hilo. Nini kauli ya Serikali kuwasaidia watu wa Ukonga Kata ambazo nimezitaja, mradi wa dharura ili waweze kupata maji safi na salama? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri kabisa. Nami pia niseme kwamba nimeshukuru Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo moja kwa moja kwamba, sasa Wizara ya Maji ni eyes on, hands on kwenye halmashauri. Baada ya kauli hiyo kabla ya tarehe 30, nitafanya kikao kikubwa na Wahandisi wa Maji wote katika halmashauri ili tupeane mwelekeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichukue nafasi hii kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge. Kwanza kabisa kuhusu Visima vya Kipimbi na Mpera, tumefanya kazi kubwa sana, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, tumekuwa naye na tulikutana na Benki ya Maendeleo ya Ufaransa ambao wamekubali kwamba watatusaidia fedha kwa ajili ya kuweka miundombinu ya maji Wilaya ya Temeke pamoja na Kigamboni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Serikali inaendelea na mazungumzo. Kwa hiyo, suala la fedha halina shida tena ni utaratibu tu, baada ya kusaini financial agreement mambo yote yatakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna shida yoyote kwamba mradi umechelewa kwa sababu hii Sh.50, hapana, kwa sababu hii Sh.50 kwanza inaelekezwa moja kwa moja vijijini. Hii ni miradi mikubwa ambayo inatekelezwa kwa fedha kutoka Central Government.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, tushakamilisha mazungumzo na Serikali ya Ufaransa na tukapata hiyo fedha, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hii ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi, itahakikisha kwamba maeneo yote ya Dar es Salaam yanapata maji safi na salama pamoja na kata alizozisema, pamoja na hata kwa Mheshimiwa Zungu kule Ilala, tunahakikisha kwamba tunakamilisha ili wananchi waweze kupata maji safi na salama sambamba na kuondoa majitaka.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza naomba niseme kwamba mradi huu una zaidi ya miaka 35 na idadi ya watu ambao wapo katika eneo hili sasa hivi imeongezeka zaidi ya mara tatu na miundombinu yake imechakaa. Halmashauri imeomba fedha jumla ya shilingi milioni 276 lakini fedha zilizopelekwa ni shilingi milioni 59 tu, napenda kufahamu, hizi shilingi milioni 59 ambazo zinagawanywa katika majimbo mawili katika wilaya moja zitawezaje kukamilisha mradi wenye idadi ya watu wengi kama huu ambao unategemewa na wananchi zaidi ya 36,000? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba, je, Naibu Waziri au Waziri wanaweza wakawa wako tayari kuungana na mimi ili twende Kalenga tukaone mradi huu ambao kwa kweli ukikamilika utakuwa unaleta tija kwa wananchi wangu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa faida ya Wabunge wote, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mgimwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa tumeshaweka utaratibu kwamba, hatukuletei fedha mpaka uzalishe. Kwa hiyo, hiyo shilingi milioni 59 imekuja kulingana na certificate uliyoleta. Ungeleta certificate ya shilingi milioni 200 basi tungekupa shilingi milioni 200. Hatuleti fedha ukae nayo, kwanza lazima uzalishe ndio tuweze kuleta fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, nilishafika huko, lakini pia nitamruhusu Naibu Waziri wangu tukishamaliza Bunge ataambatana naye. Hata hivyo, niwape utulivu wananchi wa Kalenga kwamba ule mradi sasa ni mkubwa tunahitaji fedha nyingi siyo shilingi milioni 200 tena. Ndiyo maana katika jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri amesema tunataka tuufanyie usanifu kwa sababu utagharimu hela nyingi ili tuweze kutafuta fedha kwa wafadhili tuhakikishe kwamba maji yanawatosheleza wananchi wote wa eneo hilo.
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niiulize Serikali badala ya kutumia fedha nyingi kujenga mabwawa makubwa au yale ya kati kwa nini isiweze kununua mitambo yenye thamani hiyo hiyo ya bwawa ikaipa halmashauri husika ili baada ya kumaliza kuchimba hilo bwawa moja waweze kuendelea kuchimba mabwawa mengine mengi na thamani ya ile kazi itakuwa ni kubwa? Hii itakuwa ni njia moja ya kutumia force account vizuri sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali zuri sana la Mheshimiwa Mbunge Soni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo hayo ni mazuri lakini mara nyingi mabwawa Mheshimiwa Mbunge hatuchimbi, tunakinga ili tuweze ku-retain maji yaweze kufanya kazi. Mawazo yako naomba tukutane baada ya kikao hiki ili uweze kunieleza vizuri tuweze kuyafanyia kazi. Sisi kazi yetu kama Wizara tunasikiliza mawazo ya Waheshimiwa Wabunge, tunayapeleka kwa wataalam ili wakiyafanyia kazi vizuri basi tuweze kuyaingiza katika mfumo wa Serikali.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri. Pamoja na kazi kubwa mnayofanya, je, mko tayari sasa kwenda katika Halmashauri ya Mji wa Nzega na kulifanyia tathmini bwawa ambalo limekuwa likitumika kwa ajili ya umwagiliaji katika Kijiji cha Idudumo ili kuweza kulirudisha katika hadhi yake na miundombinu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa yote ambayo utendaji wake unasuasua baada ya kukamilisha mpango kabambe, nia yetu ni kuhakikisha wananchi wanalima mara mbili, mara tatu kwa mwaka. Tutakwenda na tutalifanyia kazi vizuri.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kumueleza Mheshimiwa Waziri kuna bwawa katika Kata ya Urugu, Wilaya ya Iramba ambalo limekuwa na manufaa makubwa sana kwa muda mrefu kwa wananchi wanaoishi kwenye kata ile lakini sasa hivi linaelekea kupotea kwa sababu tope linajaa. Je, ni lini Serikali sasa itakwenda kusaidia wananchi wale ili tope lile liondolewe na shughuli zile ziendelee?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mama yangu Mheshimiwa Martha Mlata kwa jinsi ambavyo anashughulikia Mkoa wa Singida kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilielekeza Idara yangu ya Umwagiliaji watengeneze teknolojia ya kuhakikisha kwamba inaondoa matope kwenye mabwawa kwa sababu mabwawa mengi yamejaa tope na leo wanakuja kunipa taarifa. Nipongeze sana Mkoa wa Singida, katika mikoa ambayo imeyatunza mabwawa na mifugo inapata maji kwa zaidi ya asilimia 60 ni Mkoa wa Singida. Kwa hiyo, Mheshimiwa Martha Mlata nalifanyia kazi, teknolojia ikishapatikana tunataka tuyaokoe mabwawa yote.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji kwa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Mradi huu wa maji ni ahadi ya toka mwaka 2006 ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais Mstaafu hivyo imekuwa ni ahadi ya muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Wizara ya Maji ipo tayari sasa kuondoa vikwazo vyote vilivyopo Wizara ya Maji na kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuhakikisha mradi huu unaanza mara moja?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na hofu kubwa kwa wananchi wangu wa Mji Mdogo wa Tinde kutokana na kwamba mradi wa maji wa Ziwa Victoria bomba kubwa linapita mbali sana na Mji Mdogo wa Tinde, hivyo kuwa na hofu kubwa kwamba mradi huu hautawezekana kufika kwa wananchi wa Tinde. Je, Wizara ya Maji imefikia wapi kuwaondoa hofu wananchi wa Tinde kuhakikisha kwamba wanapata maji safi na salama katika mradi huu wa mkubwa wa maji ya Ziwa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge Azza kwa jinsi ambavyo anawapenda wananchi wa Shinyanga na jinsi anavyowatetea katika Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kabisa kwamba miradi hii ilianza bajeti ya mwaka 2006/2007 na Mheshimiwa Mbunge naomba tu akumbuke ndipo tulioanza ile program ya maendeleo ya sekta ya maji, tukaweka kwamba tutajenga miradi 1,810. Tumeshakamilisha miradi 1,468, bado miradi 366 na mradi wake ukiwa ni mmojawapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, umechelewa kwa sababu usanifu ulichelewa, lakini kwa sasa tunamhakikishia kwamba hakuna vikwazo vya aina yoyote, tunatekeleza kwa mujibu wa sheria. Mradi wowote baada ya usanifu, baada ya manunuzi ili kuepuka upotevu wa fedha lazima tuupeleke kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaufanyie vetting, tusaini, ndiyo tuanze utekelezaji. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba mradi utatekelezwa bila ya wasiwasi wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli bomba la KASHIWASA limepita mbali kidogo mbali na ule Mji wa Tinde, nimemwagiza Mhandisi Mshauri anayesimamia huu mradi wa Tabora na tayari ameshabaini vijiji vitakavyopelekewa maji ukiwemo Mji wote Tinde na vitongoji vyake na amekamilisha utaratibu wa awali sasa hivi tunaingia kwenye usanifu wa kina.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati tunaendelea na utekelezaji wa mradi wa Tabora basi wakati unakamilika na Tinde yote itakuwa imeshapata maji. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Mji wa Makambako ni Mji mkubwa na ni Mji ambao una tatizo kubwa sana la maji. Baadhi ya wananchi wanashindwa kujenga viwanda kwa sababu ya uhaba wa maji. Kuna miradi 17 ya fedha kutoka Serikali ya India. Serikali iniambie hapa je, ni lini sasa miradi hii ambayo mmojawapo ni ya Mji wa Makambako utaanza ili wananchi wa Makambako waweze kunufaika na wajipange kwa ajili ya kujenga viwanda?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mbunge wa Makambako pamoja na Ludewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Mheshimiwa Mbunge wa Makambako, kwanza kabisa tunaishukuru Serikali kwamba mkataba wa kifedha kati ya Serikali ya India na Tanzania umeshasainiwa tayari. Pili, kulingana na masharti ya mkataba huo, Serikali ya India imeshaleta Wahandisi Washauri tayari, wengi ambao sasa hivi tutafanya manunuzi kupitia kwenye hilo group.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba shughuli hii inakwenda kwa kasi sana na matarajio yake ni kwamba kabla ya mwaka huu tulionao 2018 haujafika Desemba, tunataka tuhakikishe kwamba Wakandarasi wako site na wanaanza utekelezaji wa miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ludewa. Mheshimiwa Mbunge yeye mwenyewe ni shahidi kwamba nilishaelekeza mamlaka yangu ya maji ya Iringa na wanaendelea kutekeleza miradi katika Jimbo lake na mwaka huu tumetenga fedha. Kwa hiyo, tutaendelea kutekeleza pamoja na pale Mjini ambapo mimi mwenyewe nilipatembelea, tutahakikisha kwamba tunawapatia maji safi na salama wananchi wake. (Makofi)
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Tatizo la maji katika Wilaya ya Ludewa limekuwa ni la kudumu na ikizingatiwa kwamba Wilaya ya Ludewa ina vyanzo vya maji vingi sana. Je, Serikali inajipangaje katika kuhakikisha kwamba Ludewa inapata maji ya uhakika hususan Ludewa Mjini na Mavanga?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mbunge wa Makambako pamoja na Ludewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Mheshimiwa Mbunge wa Makambako, kwanza kabisa tunaishukuru Serikali kwamba mkataba wa kifedha kati ya Serikali ya India na Tanzania umeshasainiwa tayari. Pili, kulingana na masharti ya mkataba huo, Serikali ya India imeshaleta Wahandisi Washauri tayari, wengi ambao sasa hivi tutafanya manunuzi kupitia kwenye hilo group.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba shughuli hii inakwenda kwa kasi sana na matarajio yake ni kwamba kabla ya mwaka huu tulionao 2018 haujafika Desemba, tunataka tuhakikishe kwamba Wakandarasi wako site na wanaanza utekelezaji wa miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ludewa. Mheshimiwa Mbunge yeye mwenyewe ni shahidi kwamba nilishaelekeza mamlaka yangu ya maji ya Iringa na wanaendelea kutekeleza miradi katika Jimbo lake na mwaka huu tumetenga fedha. Kwa hiyo, tutaendelea kutekeleza pamoja na pale Mjini ambapo mimi mwenyewe nilipatembelea, tutahakikisha kwamba tunawapatia maji safi na salama wananchi wake. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, Serikali imejenga Mradi wa Maji wa Kibena Howard lakini mpaka hivi sasa mradi ule bado haujaanza kutoa maji. Je, ni lini Serikali itahakikisha mradi huu unaanza kutoa maji ili wananchi wa Kibena na Hospitali ya Mkoa wa Kibena ili iweze kupata huduma hii ya maji?
Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, ni lini Serikali itaanza kutekeleza Mradi wa Maji Tarafa ya Matamba, Wilaya ya Makete?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mradi wa Kibena umekamilika tatizo ambalo lipo ni umeme na tulishaagiza walete quotation kutoka TANESCO tuwalipe ili waunge umeme na wananchi wa Kibena waendelee kupata maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na suala la Matamba, nilitembelea Matamba na nikatoa maelekezo. Nishukuru kwamba Mheshimiwa Mbunge ameleta makadirio yale na katika mwaka ujao wa fedha tutatekeleza mradi mkubwa ili wananchi wa eneo la Matamba waweze kupata huduma ya maji safi na salama kwa kukarabati mradi uliokuwepo ambao ulikuwa na bomba dogo sasa tutaweka bomba kubwa ili maji yaweze kupatikana kwa wingi.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na uzuri umeona idadi ya Wabunge waliosimama hii ni kuashiria kwamba maji ni tatizo.
Mheshimiwa Spika, mimi tu niulize swali dogo ambalo litaambatana na ushauri. Moja ya sababu inayopelekea kuwepo kwa tatizo kubwa la maji ni kwa sababu Serikali haijakita maji kama moja ya kipaumbele chake. Ni kwa nini sasa Serikali isikubali maji kuwa moja ya vile vipaumbele vitatu vikubwa vya Taifa, kwamba tutenge bajeti walau asilimia 20 kwa kuhakikisha tunatatua tatizo la maji nchi nzima? Kwa nini msikubaliane na jambo hilo ili tuondoe tatizo hili nchi nzima? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Silinde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishaweka kipaumbele kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya maji safi na salama. Ilianza mwaka 2006/2007 ambapo tulianza programu ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini na ndiyo tulipoweka mikakati ya kujenga miradi 1,810 na hadi leo tumeshatekeleza miradi 1,468.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mkakati huo tume-ring fence, tumeweka fedha Sh.50 zinatolewa katika kila lita ya mafuta. Huo ni mkakati maalumu kuonyesha kwamba sasa Serikali imeshaona suala la maji ni la kipaumbele na ndiyo maana kutoka kwenye huo mfuko kila mwaka tunatengewa shilingi bilioni 158.5. Ninyi Waheshimiwa Wabunge mmeendelea kusema kwamba fedha hiyo iongezwe ili iweze kutumika kwenye miradi. Kwa hiyo, Serikali tayari ilishaweka kipaumbele cha maji na tutahakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, tatizo sugu linaloonekana kwenye swali la msingi la Wanging’ombe linafanana kabisa na tatizo sugu la kukosekana maji Mbulu Vijijini. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amefika katika Jimbo langu, kwanza namshukuru, lakini sasa tumesaini Mkataba na DDCA wa kuchimba visima sita (6), tangu Januari mpaka leo hawaonekani na hawakuchimba visima vile. Waziri atatusaidiaje sasa DDCA waje kuchimba visima ambavyo tumeingia nao mkataba na Halmashauri yangu Jimbo la Mbulu Vijijini? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Massay kwa jinsi anavyoshughulikia Jimbo lake. Nilishawahi kufika kule na ni kweli kwamba DDCA wamesaini mkataba wa visima sita. Kwa sababu hili suala ni la kiutendaji, mimi na yeye baada ya Bunge leo tuwasiliane ili tuweze kuwauliza DDCA kwa nini hawajapeleka mitambo kwenda kuchimba.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Tatizo la miundombinu hii ya maji halipo tu Wanging’ombe lipo pia pale Temeke ambako miundombinu ya maji taka pale Kurasini imekufa kabisa na sasa hivi mazingira yale kwa kweli yanatia kinyaa kwa sababu vinyesi vinatapakaa nje. Wizara ilisema kwamba wanataka wajenge mitambo ya kisasa ya kuchakata taka na nimeona wameanza kulipa fidia japo kidogo kidogo sana. Sasa kwa sababu jambo hili ni la hatari linaweza kusababisha magonjwa mlipuko pale, Wizara ina mpango gani wa kuanza kujenga mitambo hiyo mipya haraka?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekit, kwanza nimshukuru amekiri kwamba na fidia tumeanza kulipa na tumeshapata fedha kutoka Serikali ya Korea Dola milioni 90. Kwa hiyo, wakati wowote tunatangaza tenda tuanze utekelezaji wa mradi huo. Hata hivyo, katika kipindi kuna miradi midogo midogo tunayotekeleza ili kuhakikisha kwamba suala la kipindupindu haliwakuti wananchi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nishukuru sana kunipa nafasi hii, nishukuru majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo yanatia matumaini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa vijiji 16 ambavyo vipo katika eneo la Mishamo ni vya muda mrefu na miundombinu yake ilishakuwa chakavu. Serikali haioni sasa ni wakati muhimu wa kupeleka miradi mikubwa ambayo itawasaidia hawa wananchi kupata maji yenye uhakika?
Swali la pili, ipo Miradi ya Maji ya Mwese, Kabungu, Kamjera yenye thamani ya shilingi bilioni 2.4 na tayari wakandarasi walishafanya kazi kwa kuanza na fedha zao; je, ni lini Serikali itapeleka fedha hizi ili waweze kukamilisha hiyo miradi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali kwanza ni kujenga miundombinu mikubwa kwa ajili ya maji ili yaweze kuwafikia wananchi mbalimbali na katika hivyo vijiji 16 vya Mishamo ambavyo amevisema Mheshimiwa Mbunge, tutahakikisha kwamba tunajenga miundombinu mikubwa ambayo itaweza kuwafikia wananchi wote kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Mheshimiwa Kakoso tunazo takribani kandarasi tano. Tuna makandarasi watano ambao wanafanya kazi na kazi hiyo ina gharama takribani ya shilingi bilioni 2.78. Mpaka sasa hivi makandarasi wawili bado hawaja-rise certificate yoyote, mkandarasi mmoja tumeshamlipa advance payment na makandarasi wawili ambao ni Dar Huduma na DDSA tayari wameleta certificate na hivi sasa tunaendelea na kuzichambua ili tuweze kuwalipa makandarasi hao.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza, nina maswali mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Waziri amekiri kwamba kuna tatizo la upotevu wa maji kutokana na miundombinu mibovu. Hivi navyoongea bado kuna tatizo kubwa sana la uvujaji wa maji, mfano, Kisasa kuna mabomba hivi sasa yanaendelea kutiririsha maji lakini sioni juhudi inayoendelea hadi sasa hivi. Je, wana mkakati gani kuhakikisha tatizo hili linatatuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Jimbo la Njombe Kusini, Kata ya Ihungilo kuna mradi wa Utengule – Ngalanga ambao vifaa vilivyonunuliwa vilinunuliwa chini ya kiwango na hadi sasa hivi vifaa hivi, mabomba na viungio vyake vinaendelea kutitirisha maji na wananchi wanakosa huduma ya maji. Je, Waziri yuko tayari kwenda kutatua tatizo hili katika Kata hii ya Ihungilo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mlowe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, upotevu wa maji ni changamoto kubwa kwa sababu lina sehemu mbili, kwanza ni miundombinu yenyewe na pili ni wafanyakazi tunasema non commercial revenue water losses ambalo linatokana na baadhi ya wafanyakazi kushirikiana na wananchi katika kuiba maji. Tunapamba na mambo yote haya mawili na kuhakikisha kwamba tatizo la upotevu wa maji linamalizika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema sasa hivi kuna changamoto hizo lazima mtu akiona changamoto hiyo tuwasiliane na Mamlaka za Maji, tuwape taarifa ili waweze kwenda kumaliza tatizo hilo. Kila kwenye Mamlaka ya Maji tumeweka toll free number ambayo ni namba ya simu ambapo unaweza kupiga simu bure kueleza wapi kuna tatizo la upotevu wa maji na mara moja utakapofanya hivyo sisi tutachukua hatua za kuweza kupambana na upotevu huo wa maji. Hili la Kisasa kama alivyosema Mheshimiwa naamini wataalam wangu wamesikia na watakwenda kulishughulikia mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusu vifaa vilivyo chini ya kiwango. Ni kweli kabisa katika miradi mingi sana iliyojengwa vijijini, vifaa vingi vilivyopelekwa na wakandarasi viko chini ya kiwango na tumechukua hatua mbalimbali za kisheria na tutaendelea kuchukua. Naomba tu nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda pamoja tuhakikishe kwamba tatizo hili tunaliondoa ili wananchi wale waweze kupata maji safi na salama.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Miradi ya maji katika Vijiji vya Getamok, Endonyawed, Kansai, Matala na Fusmai katika Wilaya ya Karatu ambayo ni zaidi ya asilimia 50 ya ile miradi kumi katika kila Wilaya haifanyi kazi kwa sababu ya kujengwa chini ya kiwango. Tatizo kubwa ni kama ilivyoelezwa katika swali la msingi mabomba yanavuja. Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuja Karatu ili ajionee mwenyewe jinsi wananchi na Serikali walivyohujumiwa lakini pia akae na Halmashauri ili kuona ni namna gani miradi hiyo inafufuliwa? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama nilivyosema maeneo mengi hasa ya vijijini miradi mingi iliyotekelezwa ilitekelezwa chini ya viwango. Wameweka mabomba ambayo yako chini ya viwango, wameweka valve ambazo ziko chini ya viwango. Sisi tunahakikisha kwamba sasa tatizo hili linamalizika na pale ambapo mkandarasi ameweka vifaa ambavyo viko chini ya viwango anatakiwa aviondoe na afanye kazi hiyo na aweke vifaa ambavyo vina viwango vinavyokubalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekubaliana na Mheshimiwa Mbunge tutakwenda tutaona tatizo hilo na tutalitatua kwani nia ya Serikali naendelea kusema tena ni kuhakikisha kwamba tunawapelekea wananchi maji safi na salama.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wananchi wa Jimbo la Ludewa huwa wana kawaida ya kujiongeza. Miradi mingi ambayo inafanyika kwenye Jimbo la Ludewa wananchi wanakuwa wameianza kabla ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni shahidi alipofika maeneo ya Mlangali alishakuta watu wameshajichangisha shilingi milioni 90 na wakawa wanaiomba Serikali shilingi milioni 50 kwa ajili ya kumalizia. Niishukuru Serikali ilitupa ile hela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna miradi mbalimbali inaendelea kwenye Kata ya Mavanga na Ludewa Mjini. Je, Serikali ipo tayari kutusaidia na kuhakikisha mfano miradi ile ya Ludewa Mjini, Iwela na Lifua inakamilika katika kipindi kifupi iwezekanavyo? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kawaida nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama na kwa muda mfupi. Kwa hivyo, nitahakikisha kwamba miradi ya Ludewa Mjini na maeneo mengine aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tutatekeleza kwa muda mfupi ili Watanzania wa maeneo yale na maeneo mengine yote Tanzania waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni miaka zaidi ya 50 ya Uhuru lakini maeneo mengi ya wafugaji bado wanakunywa maji kwenye mabwawa pamoja na wanyama, binadamu wanachota maji, wanyama pia wanakunywa hapo. Nimeona hili Mkuranga Kijiji cha Beta, nimeona hili juzi Monduli katika Kata ya Nararami. Kwa nini hii shilingi milioni 50 iliyotolewa kwa kila kijiji isitumike kwenda kuchimba visima virefu katika yale maeneo ambayo hakuna maji na binadamu wanakunywa maji kwenye mabwawa na wanyama? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ruth, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelewa kwamba maeneo mengi ya nchi yetu yana changamoto kubwa ya maji, mijini na vijijini. Serikali tumejipanga vizuri, kwa mfano tu, juzi tumepata mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Dunia ambapo tumepata takribani shilingi za Kitanzania bilioni 800 na pesa nyingi kati ya hizo zitapelekwa vijijini kutatua changamoto ya maji kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Siyo hivyo tu, kwenye bajeti yetu hii ya mwaka huu tuna takribani shilingi bilioni 630 kwa ajili ya kupeleka maji vijijini. Nataka niwahakikishie Watanzania kwamba Serikali tumejipanga na kila kijiji tutawapelekea maji safi na salama.
MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri lakini tumekuwa na tatizo kubwa la wakandarasi hawa, kwa mfano, Mradi wa Nguruka Mheshimiwa Rais alifanya ziara tarehe 23 Julai, 2017 akatoa tamko hadi Desemba. 2017 Mradi wa Nguruka uwe umekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa zinaletwa na Serikali wakandarasi hawa hawakamilishi miradi hii na mradi wa Nguruka wananchi wanaona pesa zinaingia lakini hawapati maji. Mradi wa Uvinza pesa zinaletwa lakini wakandarasi hawakamilishi ili wananchi wapate maji. Mradi wa Kandaga Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi tarehe 17 Julai, 2018 tulifanya ziara pale ukampa mkandarasi wiki mbili lakini hadi leo hii hakuna maji yanayotoka pale. Swali langu la kwanza, je, Serikali ina kauli gani kwa hawa wakandarasi ambao wanalipwa pesa lakini hawakamilishi miradi kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, tarehe 29 Julai, 2018, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwenye Kijiji cha Mwakizega na wananchi wakamlilia kwamba tunahitaji maji na tamko tukaambiwa tuandae taarifa ya mradi wa maji ili tuweze kuwasilisha Wizarani. Hivi navyoongea Injinia wa Maji Halmashauri ya Uvinza yuko hapa Dodoma ameshawasilisha andiko hilo la mradi ambalo linagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.9. Je, ni lini sasa Wizara itatuletea pesa ili tuanze kutekeleza huu mradi mpya wa Mwakizega? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kwamba Serikali inachukua hatua gani kwa wakandarasi ambao wanashindwa kukamilisha kazi kwa wakati. Kuna taratibu mbalimbali Serikali inachukua kama mkandarasi anashindwa kukamilisha kazi kwa wakati. Hatua ya kwanza, kama mkandarasi anachelewesha kazi tunampiga faini kutokana na ucheleweshaji na kila siku mkandarasi huyo analipa faini inategemeana na mradi wenyewe na kiasi cha gharama za mradi. Hatua ya pili ambayo kama mkandarasi atashindwa kutelekeza kazi kwa wakati tunaweza kumfutia usajili na mwisho wake hatoweza kufanya kazi yoyote ya ukandarasi kwenye sekta zote za ujenzi pamoja maji na sekta zote hapa nchini. Tutawasimamia wakandarasi wote tuhakikishe kwamba wanafanya kazi kwa wakati na wanazimaliza kwa wakati ili Watanzania ambao wamesubiri maji kwa muda mrefu waweze kupata maji na salama kwa muda unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge amezungumzia kuhusu andiko, andiko tumelipokea na kama kawaida andiko lolote lazima lipitie michakato mbalimbali. Mara litakapokamilika tutaweza kutoa fedha ili mradi huo uweze kutekelezwa. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko mradi ambao unataka kutekelezwa kwenye Mji wa Tunduma na SADC na Mheshimiwa Waziri katika Bunge lililopita alisema kwamba ameshampeleka consultant pale. Wananchi wa Tunduma wanataka kujua mpaka sasa mradi umefikia kiwango gani katika maandalizi ya utekelezaji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Tunduma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli consultant ameenda kwa ajili ya mradi huo lakini taratibu za utekelezaji zinakwenda hatua kwa hatua. Kwanza consultant anakwenda kufanya study analeta hiyo study tutaipitia baadaye kama pesa ipo utafuata mchakato wa kutafuta mkandarasi ili aweze kufanya kazi hiyo.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya usanifu wa Mradi wa Kupeleka Maji Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga kutoka Mto Zigi kuelekea Horohoro lakini mpaka sasa hakuna dalili yoyote ya jambo hili kufanyika. Ni lini usanifu huu utaanza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba usanifu huo utaanza mara moja, tunajipanga kuhakikisha kwamba tunatafuta wataalam ili wakafanye kazi hiyo.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwanza tunaishukuru Serikali kwamba tumechimbiwa visima vinne kupitia Halmashauri ya Mji wa Kondoa. Pamoja na visima hivyo ambavyo vimechimbwa bila ukarabati wa miundombinu ya maji, uchimbaji wa visima hivi havitawasaidia sana wananchi wa Kondoa Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo katika bajeti iliyopita tuliomba fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu hiyo. Naomba kujua Serikali imetenga fedha kiasi gani kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya zamani ukizingatia kwamba maeneo kama Kwapakacha, Kilimani na Bicha katika uchimbaji wa visima hivyo kuna maeneo watatumia miundombinu ya zamani? Je, Serikali iko tayari kujenga baadhi ya miundombinu ili wananchi wa Kondoa Mjini wapate maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ahadi ya ukarabati wa miundombinu ya maji katika Mji wa Kondoa ni ya ahadi ya viongozi wa Kitaifa na hasa waliotembelea Kondoa Mjini mwaka jana akiwemo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Je, ahadi hizo zitatekelezwa lini? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ninavyosema mara nyingi, nia ya Serikali ni kuhakikisha kila eneo tunapeleka maji safi na salama. Kwa upande wa Kondoa Mjini sasa hivi tuna mradi ambao utahakikisha kwamba tunapeleka maji kila eneo la Kondoa Mjini ambapo kama nilivyosema kwenye swali la msingi kwamba sasa hivi tunajenga miundombinu ya kilomita 9.12, tunajenga miundombinu ya kusambaza maji kilomita 30.172 kwa sababu kuchimba visima ni jambo lingine na kuweka miundombinu ni jambo linguine. Kwa kulijua hilo, Serikali tunaendelea sasa hivi kujenga miundombinu hiyo tuhakikishe mwananchi kila eneo anapata maji safi na salama. Tunategemea mradi huu utamalizika hivi karibuni na wananchi watapata maji hayo.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mji wa Kasulu ni kati ya miji ambayo inasubiri kwa hamu sana fedha za mkopo wa India katika ile miji 17. Hii ni kwa sababu Mji wa Kasulu unakabiliwa na tatizo la maji na hata machache yaliyopo ni machafu, kwa hiyo, kutibu tatizo hilo ni fedha za Mfuko wa India. Sasa niapenda kujua miradi hiyo 17 inaanza lini ikiwa ni pamoja na Mji wa Kasulu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kasulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tuna mradi mkubwa wa India ambapo siyo miji 17 sasa itakuwa miji 25 na mradi huo utagharimu shilingi za Kitanzania trilioni 1.2. Tenda ya kwanza ilitangazwa tarehe 17 Agosti, kwa ajili ya pre- qualification na consultancy na itafunguliwa tarehe 17 Septemba. Kwa Mheshimiwa Mbunge yeyote anayehitaji kujua information za mradi huu anaweza kupata kwenye website ya Benki ya Exim ya India. (Makofi)
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Moshi Vijijini hali iko kama Kondoa, miundombinu mingi imejengwa siku nyingi na imechakaa. Kwa kutambua hilo, Mamlaka ya Maji (MUWSA) imefanya kazi kubwa ya kukarabati miundombinu hiyo katika Kata mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana kulikuwepo na mradi mmoja katika Kata ya Mabogini ambao ilikuwa inahusu vijiji vinne na Wizara ilipokuja kuzindua kwa kuona kazi kubwa iliyofanywa na MUWSA katika Kata zingine iliahidi kutoa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kuendelea kusambaza maji kwenye vijiji vingine vitano vya Mvulei, Muungano na Msarikia. Nataka kujua ni lini fedha hizo zitapelekwa MUWSA ili waweze kutekeleza ahadi hiyo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Komu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakubaliana na yeye kwamba MUWSA inafanya kazi nzuri na tunawapongeza sana na tumewapa miradi mingi kwa ajili ya Moshi Vijijini na wanafanya kazi kubwa. Serikali tuko tayari wakati wowote wakituletea, kwa sababu tumeshawapa kibali cha kupeleka mkandarasi kuanza kufanya kazi hiyo na wakati wowote watakapoleta certificate kwa ajili ya malipo ya mkandarasi sisi tumejipanga vizuri na tutaweza kuwalipa ili kazi hiyo iendelee. Mheshimiwa Mbunge naomba uwasiliane na MUWSA kujua wamefikia wapi lakini sisi tuko tayari fedha tunayo wakati wowote tutaweza kuwalipa waendelee na kufanya kazi hiyo.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mtwara Mjini kuna Mradi wa Maji ambao unatekelezwa na Serikali kutoa maji Kijiji cha Lwelu kuelekea Kata za Ufukoni, Magomeni na maeneo mengine ya Mtwara Mjini lakini mkandarasi yule anasuasua sana na tayari kasha-rise certificate Wizara bado haijamlipa na mradi umesimama. Je, Serikali inatoa kauli gani ili kuhakikisha mkandarasi yule analipwa na mradi ule unaendelea haraka ili wananchi wa Mtwara Mjini wapate maji? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna miradi mingi hapa nchini inaendelea na huu mradi wa Mtwara tunaufahamu vizuri na kila mwezi sisi tunaendelea kulipa, hata leo tunafanya malipo kwa wakandarasi. Tutahakikisha kwamba na mkandarasi huyo tunamlipa ili aweze kuendelea kumaliza kazi hiyo ili wananchi wa Mtwara Mjini waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nipende sasa kuuliza maswali mawili madogo.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa usanifu ulikwishafanyika, je ni lini sasa huu mpango kabambe utaanza kutekelezwa katika Kijiji cha Chomachankola? (Makofi)
• Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa maeneo ya Ziba, Ndebezi, Nkinga, Mwisi, Simbo, Igoeko na Uswaya wanategemea sana kilimo cha mpunga ambapo sasa wanalima msimu mmoja na hawana scheme wala mabwawa.
Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalam wako mtaweza kuzuru maeneo hayo mjionee ukubwa wa tatizo ili kuja na majawabu ambayo yataweza kutatua changamoto katika maeneo tajwa? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuliandaa na kulijibu swali vizuri sana. Sasa nijibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni lini tutaanza utekelezaji wa skimu ya Chomachankola. Nimhakikishie tu kwamba mpango kabambe umekamilika na kuanzia mwaka ujao wa fedha tunaanza ku-mobilize fedha na hasa kwa nje na kuanza kutekeleza hiyo progamu kwa sababu hiyo programu itashirikisha taasisi nyingi sana za wadau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mpango kabambe umeanisha maeneo yote, kwa hiyo tutakachofanya ni kuhakikisha kwanza tunajenga chanzo cha maji na baadaye ku-develop hizo skimu ili tuhakikishe kwamba maeneo yote yanayofaa kwa kilimo cha mazao ya aina yote yanalimwa kwa umwagiliaji. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza itambulike kuwa huu mradi umeanza kubuniwa muda mrefu sana na ninashukuru kuwa hii awamu ya tatu sasa ndiyo inaafikiwa. Lakini ninapenda kujua, huko nyuma ilionekana kabisa kama tayari kuna uwezekano mkubwa wa kupata mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. Je, hatua hizo zimefikia wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inaweza ikatupa timeline au ratiba maalum itakayoonesha kabisa hatua zinazoendelea kwenye mradi huu ili tuanze kupata manufaa yake? Huu ni mradi ambao kwetu sisi Mkoa wa Songwe ni wa kimkakati kwa sababu utatuzalishia umeme, utatuwezesha kulima kwa kumwagilia na vilevile utaboresha miundombinu mbalimbali. Kwa hiyo, naomba sasa kujua kama kuna timeline ambayo imeshatengenezwa na Serikali ya kujua ni lini sasa hasa tutaanza kuona matokeo ya utekelezaji? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kabisa, ni kweli amekuwa anakuja ofisini kufuatilia utekelezaji wa mradi huu na malengo yake alipenda uanzie kutekelezwa Songwe Juu, eneo ambalo ni la jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kuhusu mkopo, kwa sasa hivi Serikali hizi mbili mkopo huu utakopwa na Serikali mbili, Serikali ya Malawi na Serikali ya Tanzania.
Kwa hiyo, naomba tu Mheshimiwa Mbene uziachie Serikali, tunaifanyia kazi kwa haraka sana ili kuhakikisha tunapata huu mkopo, tuweze kutekeleza huu mradi. Na kama mwenyewe ulivyosema kwamba una manufaa makubwa, kuna kilimo cha umwagiliaji, kuna kuzalisha umeme lakini pamoja na kupata huduma ya maji ya kunywa safi na salama na pia tutazuia mafuriko ya Mto Songwe ambao umekuwa unabadilisha mpaka kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu muda (time frame), ni lini; Mheshimiwa Mbene nikwambie tu kwamba tukishapata fedha programu imeshaandaliwa, lakini sasa ile programu itakuwa effective kwamba inaaza tarehe ngapi, baada ya kupata fedha ndiyo tutaweza kukupa majibu ambayo yana uhakika.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bonde la Eyasi Wilayani Karatu ni maarufu sana kwa kilimo cha umwagiliaji, hasa wa zao la vitunguu maji wakitumia miundombinu ya kiasili ambayo inasababisha maji mengi kupotea njiani kabla hayajawafikia wakulima walioko chini. Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kutosha ili kuboresha miundombinu hiyo ya umwagiliaji? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imekamilisha mpango kabambe kupitia skimu zote za umwagiliaji na tutaleta teknolojia ambayo itatumia maji kidogo na kwenye bonde lile nimeshafika, na juzi mvua zilinyesha mchanga ukafukia yale macho lakini wananchi wakajitolea, ninayo taarifa na wakati wowote nitakwenda huko ili tuhakikishe kwamba tunaboresha ile skimu ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa eneo la Eyasi. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali. Kwa kuwa matatizo yaliyopo huko Ileje yanafanana kabisa na yaliyopo katika Jimbo la Manyoni Magharibi, Halmashauri ya Itigi. Mvua zinazonyesha maji yake yanapotea na ni dhamira ya Serikali ya kuwatua akinamama ndoo kichwani. Je, sasa Serikali iko tayari basi kujenga angalau bwawa moja tu katika mwaka ujao wa fedha katika Halmashauri ya Itigi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko tayari na katika huu mpango kabambe uliokamilika tumeainisha kwamba maeneo mengi tutajenga mabwawa tuweze kuvuna maji ili wananchi wasipate shida ya maji ya kunywa, pia umwagiliaji hata mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze kwamba Bwawa la Itagata kwenye jimbo lake tumekamilisha kujenga. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu ya Serikali na ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Moshi Vijijini ina skimu ya umwagiliaji inayoitwa Lower Moshi Irrigation ambayo ilifadhiliwa na Japan, lakini skimu hiyo sasa iko taabani kwa sababu ya upungufu wa maji na miundombinu mibovu na imesababisha kupungua sana kwa zao la mpunga. Ni lini Serikali itakuwa tayari sasa kutuchimbia visima au mabwawa ili kuongeza maji ili skimu hiyo iweze kuwa endelevu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ni wengi sana wanategemea mpunga kutoka eneo hilo la Lower Moshi, ni lini sasa Serikali itafanya jambo la dharura kutupelekea wataalam hao ili hali irudi kama ilivyokuwa siku za awali? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala ya maji. Lakini pia hata masuala ya umwagiliaji na hasa kwa eneo la Lower Moshi. Lakini katika hoja zake mbili naomba kumjibu kwamba ni kweli tunayo taarifa kwamba Lower Moshi Irrigation ilijengwa miaka ya nyuma na Serikali ya Japan na ilifanya kazi kubwa sana kule Moshi ya kuzalisha mazao ya mpunga. Lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni kweli maji yamepungua na ndiyo maana huu mpango kabambe ambao tunaukamilisha tutahakikisha ama tunachimba visima na bahati nzuri Kilimanjaro kule chini ya ardhi maji ni mengi au tunajenga mabwawa ili kuvuna maji ili wananchi wale. Lakini pia miundombinu ya Lower Moshi pia kidogo imechakaa, tutahakikisha pia tunaiboresha ili wakulima wale waendelee kufaidi matunda ya kilimo.
Kuhusu suala la wataalam kama ambavyo nimejibu katika suala la Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza suala la wataalamu Mheshimiwa Shally Raymond tunalifanyia kazi na tumeelekeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji itaajiri wataalam wa umwagiliaji kwa ajili ya kutengeneza scheme za umwagiliaji. Lakini baada ya kutengeneza kwa sababu utekelezaji wake utafanywa na Halmashauri tumeelekeza pia Halmashauri nao iajiri wataalamu wa umwagiliaji ili wakati wanapojenga wawe wanatoa taarifa jinsi miundombinu inavyobadilika ili tuweze kwenda vizuri.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa Ruafi Katongoro umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.8 ili kusaidia wakulima zaidi ya 4,000 katika vijiji vya Kata ya Itete, Kirando na Kipili. Lakini mpaka sasa huo mradi haunufaishi wakulima na umejengwa chini ya kiwango.
Je, Waziri yuko tayari kutuma wataalam kwenda kukagua kama huo mradi kweli hizo pesa zimetumika za JICA Japan bilioni 1. 8 ni halali na scheme yenyewe haifanyi kazi yoyote?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Keissy kwamba niko tayari wakati wowote baada ya Bunge Mheshimiwa Mbunge tuambatane na wewe twende tukaangalie hiyo scheme. (Makofi)
MHE. LEAH. J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona kupitia mradi wa uwekezaji katika sekta ya kilimo (DASP) Serikali ilitumia shilingi bilioni 1.1 fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika kutekeleza mradi wa umwagiliaji katika kijiji cha Mwagwila Wilayani Meatu, lakini mradi huo ulitelekezwa.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari tutaongozana naye.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi na nimpongeze tu Waziri anavyojua hii miradi ya maji na scheme za maji na jinsi anavyoifuatilia, hongera sana Mheshimiwa Waziri.
Kuna Ziwa la Chala pale kwetu Rombo na Wabunge wote wa Rombo waliopita Mzee Mramba, Ngalei na wengine tumekuwa tukiomba maji yale yametumike kwa ajili ya wananchi wa vijiji 28 vya Ukanda wa chini na nashukuru sasa ruhusa imetoka kwa sababu yale yalikuwa maji ya kimataifa. Sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri Halmashauri tumeleta andishi, tunaomba shilingi milioni 130 kwa ajili ya kufanya usanifu ili vijiji vyote vya Ukanda wa chini katika Jimbo la Rombo viweze kupata maji.
Je, Wizara iko tayai kulishughulikia andishi hili ili litatue kabisa moja kwa moja shida ya maji katika Wilaya ya Rombo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa natambua kwamba Ziwa Chala lipo na tumeanza kulifanyia kazi. Lakini kufuatia matamshi na maelekezo ya Mheshimiwa Rais mwezi uliopita kwamba sasa wahandisi kutoka Halmashauri watatekeleza miradi yao wakiwa wana ripoti kwa Katibu Mkuu. Kweli andiko tumeshalipokea naomba unipe siku mbili, siku mbili hizi tutatoa taarifa kwenye Serikali kwamba sasa…
...utekelezaji wa miradi utakuwaje, lakini ninayo taarifa kwamba lazima tutumie Ziwa Chala kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji pale Kilimanjaro kupitia ziwa hilo.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kule Moshi Vijijini kuna mifereji ambayo ilikuwa ni ya asili na ya kwa kikubwa sana ndiyo ilikuwa ina support zao la kahawa na ilikuwa inatunzwa na KCU. Baada ya KCU kuyumba na zao la kahawa limeyumba.
Sasa nilitaka kumuomba Waziri anipe commitment kama anaweza akapeleka wataalam wakaenda wakakagua ile mifereji ya asili na vyanzo vyake kwa sababu kutokana na mabadiliko ya tabianchi vyanzo vingi vimeharibika na kwa sababu hiyo ile mifereji haifanyi kazi kwa ufanisi ambao unatakiwa.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari nimeshatuma wataalam wangu, nilimtuma Naibu Katibu Mkuu kwenda kule ili aniletee taarifa ya awali halafu baadae tuweke kikundi cha wataalam kiende kule. Lakini si kweli kwamba ile miundombinu haitoi maji kwa sababu imeharibika ni kwamba kilimo maeneo ya juu kimepanuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wale wanayatumia maji yote yanashindwa kufika huku chini. Lakini hilo suala tutalirekebisha ili kuhakikisha kwamba yale maji yatumike kwa watu wote. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tutalifanyia kazi hilo suala.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Katika Jimbo la Njombe Mjini kuna kilimo cha umwagiliaji wa zao la viazi, kilimo hiki ni maarufu kwa jina la kipalila, wananchi hawa wamekuwa wakilima kwa kujitegemea hawana mbinu bora za umwagiliaji na wala hawana scheme yoyote. Je, Serikali sasa iko tayari kuja Jimbo la Njombe na kusaidia wananchi hawa kujengewa miundombinu bora kabisa ya umwagiliaji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa asili yake kilimo cha vinyungu kinakwenda kulimwa kwenye maeneo oevu na kwa mujibu wa taratibu za kimazingira tunasema kwamba maeneo haya hayafai kulimwa kwa sababu yanaharibu eco system ya mtiririko wa maji. Tuko tayari na tumeshaanza kulifanyia kazi, wananchi hawa hawawezi kuacha kulima vilimo vya vinyungu. Lakini tutaweka utaratibu ambao watalima vinyungu, lakini siyo kwenye maeneo oevu ya mabonde yale ambayo yanatunza maji.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Serikali imekuwa jitihada kubwa kuboresha huduma za maji katika Jimbo la Mafinga Mjini, hata hivyo hamu ya wananchi ni kuona kuwa jitihada hizo zinasambaa na kufika maeneo mengi.
Je, Serikali iko tayari kutusaidia hasa katika maeneo ya Kisada, Matanana, Itimbo, Ndolezi na Maduma na Ugute walau kupata visima virefu ili wananchi wale nao wapate na kunufaika na huduma za Serikali ya Awamu ya Tano?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mhehimiwa Chumi kwamba katika Halmashauri ambazo zimetekeleza miradi ya maji vizuri ni pamoja na Halmashauri yake. Lakini kufuatiwa huu utaratibu unaokuja, sasa nikuhakikishe Mheshimiwa Chumi kwamba sasa utekelezaji unafanywa moja kwa moja na mimi hebu naomba niombee nipe mwaka mmoja uone shughuli nitakayoifanya. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna unaoitwa Endagaw ambao namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kufika kule na kuona changamoto ambazo zipo kwenye ule mradi wa umwagiliaji. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri katika changamoto alizoziona ni zipi ambazo sasa zimeondolewa ili wananchi wa Hanang waweze kunufaika na umagiliaji katika Mbuga ya Endagaw?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kwa jinsi ambavyo anafuatilia miradi katika Jimbo lake na alinibeba mpaka hilo eneo la Endagaw na nikafika pale nikakuta katika mifereji miwili iliyojengwa mmoja unatiririsha maji mmoja uko juu. Katika bajeti hii ambayo Waheshimiwa mmeipitisha tayari tumetenga fedha kwa ajili ya kwenda kurekebisha ule mfereji ili uwe unapeleka maji vizuri. (Makofi)
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa Jimbo la Mlimba kuna vijiji 18 ambavyo vyote vinaingia kwenye ardhi oevu na ile eneo ni eneo la wakulima.
Je, Waziri yuko tayari sasa kutembelea wakulima hawa walioko pembeni pembeni ili waone kwenye hiyo mito mikubwa iliyopo ndani ya Jimbo la Mlimba kuweka mabwawa ili wananchi wapate kilimo cha umwagiliaji kwa sababu watakuwa hawana tena mahali pa kulima?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kutembelea hilo eneo, lakini hatuwezi kuwaondoa wakulima kwenye maeneo ya oevu wanayolima mpaka tuwe tumshawawekea scheme maalum za umwagiliaji, tunamuondoa anaendelea na shughuli yake.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekuwa kwa kweli na jitihada kubwa sana ya kushughulikia suala la maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini; na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri anajua kabisa kwamba rambo la Rutubiga ambalo lilichimbwa kupitia DASP ikatumia milioni zaidi ya 300 na halikufanya kazi mpaka leo hii.
Je, Mheshimiwa Waziri pamoja na rambo la Rutubiga, rambo la Rwangwe Shigara, Kijereshi na Nyaruhande?
Je, una mkakati gani wa kuhakikisha kwamba malambo haya yanafanya kazi na kuwapatia wananchi maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikwambie nimefanya utafiti wa kutosha na nimejiridhisha, Bwawa la Rutubiga lilipasuka wakati wanajenga lile tuta kwa sababu ya ukosefu wa maji kiangazi walifanya kitu kinaitwa dry compaction kwa jina la kitaalam walishindilia udongo bila kuuwekea maji. Ndiyo maana maji yalivyofika ikawa ni rahisi kupasuka, lakini wao wakasingizia kwamba kuna ndege alitoboa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sasa Mheshimiwa Mbunge tumejianda vizuri kabisa, tunatafuta teknolojia kwanza ya kuhakikisha kwamba mabwawa yote yaliyojaa mchanga, mchanga ule unatoka bila kutumia gharama kubwa. Lakini pia tutahakikisha tunajenga mabwawa mengi kwa kadri jinsi ambavyo itawezekana na kulingana na uwezo wa fedha.
Kwa hiyo, hata hayo uliyoyataja Mheshimiwa Mbunge na kwenye eneo lako kuna mabwawa mengi sana yaliyojengwa tutahakikisha tunayajenga.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na pamoja na kazi nzuri ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ya kufikisha maji pale Ilula kwa ahadi za Mheshimiwa Rais naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nia na lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kumtua ndoo mama kichwani, na kwa kuwa Wilaya ya Kilolo eneo kubwa ni eneo ambalo lina miundombinu mibaya kwa maana barabara hazipitiki. Sasa, je, Serikali itakuwa radhi kuweza kutoa fedha ambazo tumeshaleta maandiko katika Vijiji ambavyo vinapata shida vya Idete, Ndengisivili, Kihesa Mgagao na Winome? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa chanzo kikubwa cha maji kiko pale Ilula ambapo Serikali imetoa zaidi ya bilioni tano na sasa hivi mradi unaendelea; je, Serikali itakuwa tayari sasa kuhakikisha yale maji yanafika Mlafu, Ikokoto, Image na Wambingeto? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mwamoto kwa jinsi ambavyo analitetea Jimbo lake na jinsi ambavyo anafuatilia miradi ya maji katika Jimbo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza Idete; Mheshimiwa Mwamoto yeye mwenyewe ni shahidi, Mheshimiwa Rais wetu tarehe 10 Mei, alielekeza sasa muundo mpya wa utekelezaji wa miradi ya maji. Nimwombe tu, kwamba asiwahishe shughuli leo saa sita mchana tutatoa press release na Mheshimiwa Jafo kuhusiana na utekelezaji wa miradi kuanzia sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo katika utekelezaji huo tutahakikisha vijiji vyote alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge, ikiwemo Idete na vinginevyo tunahakikisha vinapata maji kwa sababu kazi yetu ni kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo tuliwaahidi wananchi na wananchi wakaamini Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Ilula Mheshimiwa Mbunge yeye mwenyewe ni mashahidi tayari Serikali imetoa bilioni tano, mkataba umeshasainiwa, utekelezaji unaendelea vizuri na maeneo mengine yaliyo jirani na Ilula ikiwemo Image na Image nilienda mwenyewe nikaelekeza lazima bomba lifike Image na maeneo mengine yote ya jirani ili yaweze kunufaika na huu mradi wa Ilula. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwanza kabisa niishukuru Serikali kwa Mradi wa Ziwa Victoria ambao unaendelea katika Wilaya ya Nzega, Igunga na Tabora Manispaa. Naomba niulize swali, kwa kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Kaliua, Uliyakhulu na Urambo ni mbaya kwa sasa na Serikali iliahidi kutuletea maji kutoka Mto Malagarasi au Ziwa Victoria; je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha maji yanakwenda katika hayo Majimbo matatu ili wananchi wa huko waweze kuondokana na tabu kubwa waliyonayo upatikanaji wa maji? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana, ndiyo uzuri wa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa sababu Mkoa wote ni wa kwako. Nimjibu tu kwamba baada ya kuanza utekelezaji wa Mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka Tabora, tayari kupitia ile shilingi milioni mia tano kutoka Serikali ya India ambayo mkataba wake wa kifedha umesainiwa tunapeleka maji Sikonge, Urambo na Kaliua na utekelezaji utaanza mwaka ujao wa fedha. Kuhusiana na eneo la Uliyankhulu la Mheshimiwa Kadutu nalo tunalifanyia kazi kutafuta fedha nyingine ili tuweze kupeleka maji katika hilo eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria, ule Mradi tumeona kwamba bado unafanyiwa kazi. Mhandisi Mshauri hajakamilisha usanifu, lakini kwa sababu Tabora sasa tutakuwa na maji mengi, tutakuwa hatuna haja ya kuwekeza tena hela nyingi kwenda kutoa Malagarasi. Kwa baadaye tunaweza tukatumia chanzo cha Mto Malagarasi, lakini kwa sasa maji ya Ziwa Victoria yatakuwa yanatosheleza kupeleka maeneo mengine.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la Kilolo halina tofauti na tatizo lililoko katika Mkoa wa Mara. Mkoa wa Mara tuna chanzo cha maji Ziwa Victoria lakini ni Mkoa ambao unaongoza kwa shida ya maji. Wananchi wale wanaenda kuchota maji kwenye Ziwa. Ni lini Serikali itatatua tatizo hili ili wananchi wa Mkoa wa Mara wapate maji safi na salama? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpe taarifa; tayari Mji wa Musoma tumekamilisha Mradi Mkubwa wa Maji ambao unatoa lita milioni thelathini na sita kwa siku na sasa hivi tunafanya kazi ya usambazaji. Vile vile tunaanza utekelezaji wa Mradi wa Mgango Kyabakari, fedha tumepata, tunaanza utekelezaji mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu; tunaanza utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa Maji Rorya ambao utachukua maji kutoka Ziwa Victoria na Mradi huu utapeleka maji mpaka Tarime na Sirari. Kwa hiyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi vyote ilishaviona kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais na eneo la Rorya alilitembelea Mheshimiwa Waziri Mkuu na mimi nikafuatilia. Kwa hiyo mama yangu usiwe na wasiwasi, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inapenda watu wake, miradi yote ya maji itatekelezwa.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la maji Jimbo la Kilolo ni sawasawa na tatizo la maji lililokuwepo katika Jimbo la Lupembe, Mkoani Njombe. Ni zaidi ya nusu ya vijiji ndani ya Jimbo la Lupembe havina maji, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kupeleka maji katika vijiji hivyo vya Jimbo la Lupembe kikiwemo Kijiji cha Kanikelele?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Lupembe. Miongoni mwa Halmashauri ambazo zimekuwa zinatumia hela za maji vizuri ni pamoja na Halmashauri ya Lupembe, ndiyo maana kila bajeti tumekuwa tunaiongezea fedha. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna wasiwasi, Halmashauri ya Lupembe imekaa vizuri itatekeleza miradi mingi na kazi ya Serikali na Wizara inayoongozwa na mimi ni kuhakikisha kwamba nawapa bajeti ya kutosha Halmashauri ya Wilaya ya Lupembe ili waweze kutekelezaji miradi kweye vijiji vyote ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika Kata ya Mabanda, Diwani wa Kata hiyo alijitolea kukarabati bwawa kwa fedha zake mwenyewe milioni tano; lakini Bwawa hilo linatumiwa na wananchi hao pamoja na wanyama. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwachimbia haraka visima ili kunusuru afya zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Kata ya Madanga Wilaya ya Pangani katika Vitongoji vya Jaira, Nunda, Barabarani, Zimbiri, Kidutani wananchi wanatumia maji kutoka katika taasisi za dini. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwachimbia visima ili waepukane na adha ya kusumbuliwasumbuliwa wakati wanapokwenda kuchota maji kwenye hizo taasisi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza huyo Mheshimiwa Diwani ambaye alikarabati bwawa kwa ajili ya matumizi ya wananchi wake, lakini pamoja na matumizi ya wanyama. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradina fedha hizo tulizielekeza katika Halmashauri husika. Hata hivyo baada ya kuona pengine mambo hayo yalikuwa hayatekelezwi vizuri, ndiyo maana Mheshimiwa Rais sasa ameelekeza kwamba utekelezaji wa miradi yote itafanywa moja kwa moja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyomjibu Mheshimiwa Mwamoto kwamba mchana leo saa sita tunatoa tamko la Serikali ni jinsi gani sasa miradi kwa sasa hivi itatekelezwa. Kwa hiyo, tutahakikisha kwamba wananchi katika hilo eneo pamoja na Mheshimiwa Diwani kukarabati bwawa, lakini na visima vitachimbwa ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; maeneo ya Nunda na maeneo mengine ambayo amesema taasisi za dini zinasaidia, huwezi kutenganisha Serikali na taasisi za dini. Tunazishukuru sana taasisi za dini, zimetusaidia sana katika kuhudumia wananchi. Hata hivyo, nimeshaelekeza katika Halmashauri ya Handeni tutachimba visima zaidi ya 20 na huo ni uchaguzi wa Mheshimiwa Mbunge Mboni pamoja na Mbunge mwenzake kuhakikisha ni maeneo gani ya vijiji ambayo tutachimba visima.
Mheshimiwa Naibu Spika, jioloji ya Handeni ina tatizo la maeneo mengi maji yana chumvi, kwa hiyo katika kuchagua miradi hiyo itabidi tuwe waangalifu na pia nimeshaelekeza Mradi unaotekelezwa wa Wami, ule Mradi wa Wami bomba litachukuliwa kutoka Tenki la Manga ili maji yaweze kupelekwa mpaka Mkata. Kwa hiyo suala la maji Handeni baada ya muda mfupi litakuwa ni historia. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kwenye miji 17 ikiwemo Wilaya ya Karagwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwa vile Serikali imeshapata fedha ni lini Mradi wa Rwakajunju utaanza? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kuwa kufuatilia kwake kuhusiana na fedha kutoka Serikali ya India mkopo nafuu. Katika huo mkopo pia na yeye ana kiasi cha fedha kwa ajili ya Mradi wa Rwakajunju.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu kwa ufupi kabisa, utekelezaji wa kutandaza mabomba katika eneo lake la Rwakajunju na kujenga matenki unaanza katika mwaka ujao wa fedha.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Naomba nifahamu huu Mradi wa Maji ambao ameutenga muda mrefu katika Wizara ya Maji wa Mji wa Mtwara na Mji wa Babati na uko kwenye ukurasa wa 71 kwenye Kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha Hotuba; huu mradi wa bilioni sita; umekuwa hautekelezwi kwa muda mrefu sasa, kila mwaka anaweka kwenye bajeti lakini hizi fedha hatuzipati za Euro milioni 18.9. Naomba nifahamu ni lini fedha hizi zitapatikana ili Mji wa Babati na Mji wa Mtwara wapatiwe maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza fedha ipo, lakini kulikuwa na matatizo ndani ya Wizara yangu na wenyewe ni mashahidi naendelea kuyatatua yale matatizo. Fedha ipo tuliajiri Mhandisi Mshauri akafanya mchezo tumemwondoa, sasa hivi tumeweka Mhandisi Mshauri mwingine. Fedha hizo ni sawa na fedha za mradi wa Mgango Kyabakari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge huo Mradi wa Babati pamoja na Mradi wa Mtwara ambao unatumia fedha hiyo hiyo nahakikisha mwaka ujao wa fedha kazi ya kujenga miundombinu ya maji inaanza.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Changamoto ya maji ya Mji wa Handeni inafanana na Miji ya Nanyamba, Tandahimba na Newala, ambao wanategemea sana Mradi wa Makonde na hivi karibuni tuliwaambia miradi 17 financial agreement imeshasainiwa kwa mkopo kutoka Serikali ya India. Ningependa kupata kauli ya Serikali, je, ni nini kinaendelea baada ya kusainiwa ile financial agreement?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kabisa jinsi ambavyo amefuatilia sana kuhusu mkopo huu wa Serikali ya India pamoja na Mheshimiwa Mkuchika, kwa sababu wanajua kwamba wana-share kubwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba, kuanzia jana shughuli imeanza, wataalam tumewaweka mahali maalum na katika muda wa siku 14 watakuwa wameshakamisha nyaraka ili hatua zingine ziendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kwa jibu fupi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wa maeneo ya Makonde na Nanyamba, mwaka ujao wa fedha tunaanza utekelezaji wa huo mradi mkubwa tatizo la maji sasa litakuwa ni historia kwa maeneo hayo. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Tatizo la Handeni linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Jimbo la Tunduru Kusini, kwamba wananchi wanapata shida kubwa ya maji, visima vilivyopo havitoshi. Je, ni lini Serikali itachimba visima katika Jimbo la Tunduru Kusini hasa katika Kata ya Mchoteka, Malumba, Tuwemacho, Lukumbule na Mchesi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kabisa kwamba eneo lake sijafika na baada ya bajeti hii mwezi wa Saba ndio eneo litakalokuwa la kwanza. Pia ninayo taarifa kwamba, utekelezaj wa baadhi ya miradi haukutekelezwa vizuri, haukusimamiwa vizuri na halmashauri ambapo waliuchelewesha mradi na kufanya wananchi wasipate hiyo huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaambatana na Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili, ili twende tukatatue changamoto zote zilizoko kule. Kwa sababu, kuanzia sasa utekelezaji wa miradi utasimamiwa moja kwa moja na Wizara yangu mpaka ngazi ya halmashauri. Nimhakikishie kwamba, tutachimba visima vya kutosha, tutatafuta vyanzo vya kutosha ili wananchi wetu waweze kupata huduma ya maji kama walivyoahidiwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawaili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika Manispaa ya Mtwara Mikindani tatizo kubwa ni miundombinu ya usambazaji wa maji, maji yapo, lakini miundombinu ndilo tatizo. Namuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini miundombinu ile itaboreshwa, ili kusudi zile kata za pembezoni zipate maji ya uhakika? Maana tumekuwa tukiliongea suala hili siku nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kumekuwa na kero, watumiaji wa maji katika Manispaa ya Mtwara Mikindani wanalalamika kwamba, wanabambikiwa bill na hiyo inatokana na mamlaka kushindwa kusoma bill katika nyumba zote kutokana na ufinyu wa wafanyakazi. Je, Mheshimiwa Waziri, anatambua kama kuna ufinyu wa wafanyakazi katika mamlaka na kuna jitihada gani za kuhakikisha wanapatikana wafanyakazi wa kutosha? Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimtaarifa Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tumesaini mkataba wa shilingi bilioni tano kwenye Mamlaka ya Maji ya Mtwara ambayo katika huo mradi utaongeza vyanzo lakini pamoja na miundombinu ya kusambaza maji katika Mji wa Mtwara na hiyo ni hatua ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na usomaji wa bills kwenye nyumba za watu tayari sasa hivi malalamiko yaliyokuwepo baada ya muda mfupi, yatakwisha kwa sababu, sasa tunatumia teknolojia mahususi ambayo kwanza hakutakuwa na mtu kuzidishiwa bill. Ni kwamba, zile mita zitasoma unit baada ya maji kupita sio baada ya hewa kupita, kwa hiyo, suala hilo Mheshimiwa Mbunge tutalimaliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo Mheshimiwa Mbunge Ilani ya Chama cha Mapinduzi tayari itatekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma ambao utaleta maji Mjini Mtwara na baada ya hapo Mji wa Mtwara hautakuwa na tatizo tena la maji, maji yatakuwa mengi, yatahudumia maji ya majumbani pamoja na maji ya viwanda. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira tu, Serikali yake ya Chama cha Mapinduzi inafanyia kazi hili na tayari baada ya muda mfupi utekelezaji wa mradi huo mkubwa utaanza.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kuna mpango wa kujenga mradi mkubwa wa maji ambao unatakiwa kutekelezwa na SADC katika Mji wa Tunduma pamoja na Mji wa Nakonde upande wa Zambia. Ni nini mkakati na Serikali imefikia wapi katika kujenga mradi huu mpaka sasa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza mradi wa muda mfupi, imechimba visima viwili pale Mjini Tunduma, imeweka pump na juzi nilienda kule kwenda kuangalia. Changamoto ni kwa kisima kimoja ambacho waliweka bomba lenye diameter ndogo, kwa hiyo, maji yakawa hayatoki kwa wingi, lakini na matenki tumeshajenga, tumetoa maelekezo tunaboresha hiyo huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mradi mkubwa wa Tunduma/Nakonde, tayari consultant ameanza kazi ya kufanya feasibility study. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi tutatekeleza huo mradi kwa ajili ya Tunduma kwa upande wa Tanzania na Nakonde kwa upande wa Zambia na hasa kwa sababu chanzo cha maji kinatoka upande wa Zambia.
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza. Wakazi wa Jimbo la Kinondoni wanasumbuliwa na ukosefu wa maji hasa kutokana na mtandao wa maji, kwa maana ya mabomba mengi kuharibika au kutokuwa na huo mtandao. Je, Waziri ana mpango gani wa kutuletea mtandao wa maji katika Kata zetu za Tandale, Makumbusho, Kijitonyama, Kigogo, Hananasifu, Magomeni, Mzimuni ili kuhakikisha watu wote wanapata mtandao wa maji? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe taarifa, wakati tunatekeleza miradi ya kupanua vyanzo vya maji vya Ruvu Juu na Ruvu Chini idadi ya wananchi Dar-es-Salaam ilikuwa milioni tano, leo hii idadi ya wananchi Jiji la Dar-es-Salaam ni milioni sita na laki nne, kwa hiyo, mahitaji ya maji yameongezeka, sio lita milioni 500 tena ni lita milioni zaidi ya 800. Kwa bahati nzuri tumeshachimba visima vya Kimbiji, Mpera, kwa hiyo, hatuna wasiwasi na maji yapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wiki moja iliyopita, Mheshimiwa Mbunge mwenyewe ni shahidi, tumetangaza tenda kwa ajili ya usambazaji wa maji katika Jiji la Dar-es- Salaam baada ya kupata mkopo wa fedha Dola za Kimarekani milioni hamsini na saba. Kwa hiyo, maeneo yote aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tunahakikisha kwamba, tunapeleka maji ili wananchi waweze kufaidi Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, wananchi wote watapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Mradi wa Maji wa Ziwa Viktoria ni mradi mkubwa na ni mradi wa muda mrefu. Mkoa wa Tabora ni moja kati ya mikoa ambayo wananchi wake wana matatizo makubwa ya maji. Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Tabora wanapata maji safi na salama? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimuulize kweli, yupo? Kwa sababu, katika Mkoa wa Tabora tumekamilisha mradi mkubwa kutoka lile bwawa kubwa la pale Tabora, Bwawa la Igombe, ambao sasa hivi unatoa lita milioni 30 kwa siku na mahitaji ya maji kwa Tabora ilikuwa lita milioni 24 na kwa hiyo tulikuwa na excess ya lita milioni sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo tunatekeleza mradi mkubwa wa maji ambao tumepata fedha kutoka Serikali ya India. Ndiyo maana tumeamua sasa, kwa sababu maji yatakuwa mengi tutapeleka mpaka Sikonge, tutapeleka mpaka Urambo na tunaweza tukayafikisha mpaka Kaliua. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge sasa hivi tayari kuna mradi mwingine unaendelea pale Tabora kwa sasa, tunasambaza maji kupeleka kwa wananchi, maji yapo, Ilani ya Chama cha Mapinduzi inafanya kazi yake.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji Mdogo wa Kilwa Kivinje kuna vitongoji tisa ambavyo vyote havina maji; na kuna mradi mkubwa wa maji ulikuwa wa kutoka Mavuji kuja Kilwa Kivinje, mpaka sasa hivi hatujajua hatima yake. Je, Waziri anazungumzia vipi upatikanaji wa maji katika Mji Mdogo wa Kilwa Kivinje?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Kivinje naufahamu uko baharini, lakini juzi nilimpa Mheshimiwa Mbunge shilingi milioni 500, tumetoa fidia kwa ajili ya kutunza eneo la chanzo cha maji. Kwa hiyo, chanzo hicho sasa tutatekeleza mradi mmoja mkubwa wa kuchukua maji yaliyo baridi pale na kuyapeleka katika eneo la Kivinje. Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi Ilani ya Chama cha Mapinduzi iko makini, itatekeleza huo mradi kuhakikisha wananchi wa Kivinje wanapata huduma ya maji.
MHE. INNOCENT L. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa kuleta maji kwenye Mji wa Lubwera pale Makao Makuu ya Wilaya, lakini maji yale yaliyoletwa hayawatoshelezi wananchi. Naiuliza Serikali,ni lini itapanua ule mradi ili uweze kuwatosheleza wananchi kwa sababu ule mji unapanuka sana? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi anavyofuatilia matatizo ya maji katika jimbo lake, jimbo ambalo lina vyanzo vingi vya maji, lakini lilikuwa halina maji ambayo yalikuwa yamewafikia wananchi; na jana alikuja ofisini kwangu kuendelea kufuatilia huo mradi wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo Lubwela tulichimba visima viwili, lakini mtandao umekuwa mkubwa, maji hayatoshi. Namwongezea kisima kimoja, tutaanza kuchimba mwezi huu pamoja na kujenga tenki, lakini hiyo ni sambamba na kupitia sasa huo mradi mkubwa ambao tayari usanifu wake unakamilika ambao utapeleka maji kwenye vijiji 57 katika jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie tu wananchi wa Mheshimiwa Mbunge kwamba, yeye yuko makini, atahakikisha kwamba, wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa maboresho makubwa ya miradi ya maji katika Jiji la Dar es Salam. Kwa kweli katika maeneo ya Masaki, Oysterbey, Tabata, Segerea, masuala la maji yalikuwa magumu mno, sasa hivi Oysterbey, Masaki wanapata maji hawanunui kwenye maboza, ni jambo kubwa naipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nakiri kwamba bado kuna maeneo yana changamoto ya maji ikiwemo hilo Jimbo la Ukonga pamoja na maeneo ya Mbande, Chamanzi, Majimatitu, Mianzini, Kiburugwa, Mbagala Kuu, Kibondemaji na Kilungule, huko bado kuna matatizo ya maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kuyasaidia maeneo hayo wakati tukisubiri visima vya Mpera?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe taarifa na kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tumepata fedha shilingi bilioni hamsini na saba kutoka Benki ya Dunia na tumeshatangaza tender tayari kwa ajili ya kuendelea kusambaza maji katika Jiji la Dar es Salaam. Kwa hiyo niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote kwamba Jiji la Dar es Salaam tutahakikisha tunakamilisha maji yanapatikana katika maeneo yote.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru. Kwa kuwa tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa kubwa, katika Majimbo karibu yote ya Jiji la Dar es Salaam; na kwa kuwa Serikali imekuwa inasema Bungeni karibu miaka mitano sasa kwamba imepata fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha mfumo wa maji katika Jiji la Dar es Salaam.
Je, ni lini hasa mradi huu wa Benki ya Dunia utaanza rasmi katika Jiji la Dar es Salaam?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaanza mwaka ujao wa fedha kwa sababu tayari tumeshatangaza tender.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa swali dogo la nyongeza. Nimpongeze kwanza Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kuja katika Mkoa wetu wa Iringa na kujionea jinsi ambavyo Mji wetu wa Iringa ulivyokua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kuuliza swali dogo; kwa kuwa Mji wa Iringa unakua kwa kasi kubwa sana, kuna baadhi ya maeneo ambayo hayapati maji kama kule Tagamenda, Isakalilo na Kigonzile. Je, Serikali ina mpango gani wa kutuletea pesa ili kuongeza ule mtambo wa kusambaza maji pamoja na kuwa sasa hivi tunapata asilimia 96, lakini maji yetu tunaweza tukapata asilimia 100?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama cha Mapinduzi wakati inajenga mtambo wa kutibu maji Iringa iliweka matoleo ili population itakapoongezeka basi tuweze kupanua ili maji yaweze kuongezeka. Katika mwaka ujao wa fedha tumetenga bajeti kwa ajili ya kuanza kupanua mtambo wa kutibu maji ili maji yaweze kuenea katika kata zote.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Njombe tunaishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imetupa pesa kwa miradi mikubwa ya maji ya Njombe Mjini, Wanging’ombe na Mji wa Makambako. Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza miradi mikubwa ya maji Wanging’ombe pamoja na Mji wa Makambako? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, ni lini Serikali itaenda kutatua kero ya maji Wilaya ya Ludewa katika Kata za Milo, Mavanga na Mkomang’ombe? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Njombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeza kwamba swali lake ni zuri na swali hili linahusu pia maeneo mengine ambayo mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India Dola milioni 500 utakwenda kutekeleza miradi ya maji katika miji 17. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 6 Juni, Katibu Mkuu ameunda kikundi cha Mainjinia nane ambao wanatengeneza terms of reference, watafanya kazi kwa muda wa siku 16, tarehe 20 tutakuwa tumeanza kuaandaa nyaraka kwa ajili ya kuanza kutangaza zabuni. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Neema Mgaya kwamba tayari tunalifanyia kazi pamoja na wote watakaofaidi mkopo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na Ludewa Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza miradi katika maeneo hayo. Kwa sasa tunaingia katika Programu ya Awamu ya Pili, tutahakikisha kwamba vijiji vyote alivyovitaja vinapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuzungukwa na Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa lakini bado wanakabiliana na changamoto kubwa ya maji. Njia zote ambazo Serikali wamekuwa wanatumia wameshindwa kabisa kumaliza changamoto za wananchi wa Mkoa wa Rukwa. Je, Serikali haioni kwamba ni muda muafaka sasa kutumia Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa kuweza kumaliza tatizo hilo la maji kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye mwenyewe anakaa Mkoa wa Rukwa ni shahidi kwa macho sio kuambiwa kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekamilisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji pale mjini Sumbawanga na Mheshimiwa Rais anakwenda kuzindua mwezi huu, huduma ya maji inapatikana kwa asilimia 100 katika Mji wa Sumbawanga. Pia tunaendelea kutekeleza miradi mingine katika Mkoa wa Rukwa na kwenye Awamu Pili ya Programu ya Sekta ya Maendeleo ya Maji tutahakikisha mkoa mzima unapata huduma ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Mbunge, Ziwa Rukwa maji yake hayafai kwa matumizi ya binadamu. Kwa hiyo, ziwa linalofaa ni Ziwa Tanganyika na tayari tuna andiko la kuchukua maji kutoka Ziwa Tanganyika kupeleka Mkoa wa Rukwa.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Tabora Kaskazini lina vyanzo vichache sana vya maji, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kusafiri na mimi kwenda kutembelea chanzo kikubwa cha maji pale Kijiji cha Majengo Ikuza ili kuona kama kinafaa kugawa maji kwenye vijiji vya karibu vya Kanyenye, Ikongolo, Kiwembe na Majengo yenyewe?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari na tayari nimeshazungumza naye, majukumu hayo nimemkabidhi Mkurugenzi wa Mamlaka wa Maji ya Tabora ili aende akatembelee eneo lake na kutumia chanzo hicho cha maji ili Jimbo lake lipate maji safi na salama.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante. Pamoja na majibu mazuri na jitihada za Waziri mwenye dhamana kutatua kero ya maji hapa nchini, naomba majibu ni lini Serikali itatusaidia wananchi wa Halmashauri ya Arusha DC katika Kata za Oldonyosambu na Oldonyowasi ambako wananchi na hasa watoto wameathirika na maji yenye kiwango kikubwa cha madini ya fluoride?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anawatetea wananchi wa Arusha ambao kuna maeneo ambayo maji chini ya ardhi yana madini ya fluoride. Siyo Arusha tu, madini ya fluoride yapo Shinyanga na juzi nimegundua juzi yapo hata katika Mkoa wa Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuona umuhimu na athari hii inayosababishwa na madini ya fluoride ilitengeneza kiwanda na kuna utafiti wa kutengeneza madini kwa kutumia mifupa ya ng’ombe kwa ajili ya kuondoa fluoride na tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa. Mwaka jana tulitengeneza mitungi zaidi ya 200 na kusambaza kwa wananchi na mwaka ujao wa fedha tunatengeneza zaidi ya mitungi 1,000 kwa ajili ya kusambaza kwa wananchi ili kuondoa hayo madini ya fluoride.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza kupata mafanikio makubwa. Wazazi walipata madini hayo lakini watoto wanaozaliwa sasa hivi wako vizuri hawana athari ya madini ya fluoride.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia Mto Rufiji kupeleka maji Ikwiriri, Bungu na Nyamisati?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa mjukuu wangu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imepata grant kutoka Serikali ya Korea na tumeanza feasibility study ambayo inakamilika Julai, 2018 kwa ajili ya kuchukua maji kutoka Mto Rufiji kuyaleta Dar es Salaam kupitia kwenye maeneo yote ikiwepo pamoja na eneo Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara Naibu Waziri alitoa ahadi ya kusaidia kupatikana kwa mtandao wa maji katika Jimbo la Mbagala. Hata hivyo, katika tenda waliyotangaza mwezi uliopita maeneo yote ya Mbagala hayajatajwa, wameendelea na maeneo yale yale ambayo kila siku wamependelea kupeleka maji. Je, wananchi wa Mbagala tutegemee nini juu ya upatikanaji wa maji safi na salama kutoka katika chanzo cha Ruvu Juu na Ruvu Chini?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwaambie wananchi wake wa Mbagala wakae mkao wa kula. Jumatatu pale Dar es Salaam nakutana na Benki ya Maendeleo ya Ufaransa, walishatuahidi kutoa dola milioni 130 kwa ajili ya mradi wa maji safi na maji taka eneo la Temeke ikiwemo na Mbagala. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba tu asubiri kidogo atapata majibu, wananchi wa Mbagala hawajaachwa. Tunahakikisha Dar es Salaam yote inapata maji safi na salama ikiwemo pamoja na visima vya Kimbiji na Mpera. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dodoma linakua kila kukicha na uwezo wa DUWASA kuwahudumia wananchi wa Dodoma unapungua kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali. Wananchi wanaoishi Ntyuka, Ng’ong’ona, UDOM, Mtumba hawana maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watu wanaohamia Dodoma na walioko Dodoma wanapata maji safi na salama kwa wakati? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bura, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki hii nimeshuhudia utiaji wa saini wa mradi wa kupeleka maji katika mji wa Serikali pamoja na eneo la Mtumba, kwa hiyo, maji yatapatikana. Hata hivyo, chanzo cha Makutopora Mzakwe kina uwezo wa kutoa lita milioni 61.5, kwa hiyo, maji yapo na sasa hivi tunazalisha lita milioni 46. Kwa hiyo, maji bado tunayo Mheshimiwa Mbunge. Sasa hivi tunaweka mradi wa kusambaza maji ili tuweze kufika maeneo yote aliyotaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Bunge lako lilipitisha hapa kwamba kilimo cha umwagiliaji ndiyo tu kinachoweza kutoa umaskini katika nchi hii. Kwa kuwa Jimbo la Same Mashariki tumepeleka maombi yetu yana miaka 16 sasa ya kujengewa miundombinu kupitia Bwawa la Yongoma kwa ajili ya umwagiliaji. Je, Waziri anaweza kuniambia lini Bwawa hili la Yongoma litajengwa ili tukuze kilimo cha umwagiliaji? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inakamilisha stadi ya mpango kabambe kwa ajili ya suala la kilimo cha umwagiliaji. Mpango ambao ukishakamilika utaainisha maeneo yote tutakayotekeleza miradi ikiwemo pamoja na kutumia Bwawa la Yongoma. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo. (Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mradi wa barabara hii ya Kaliua-Urambo wa kilomita 28 ambao unatekelezwa na fedha ya Tanzania shilingi bilioni 37 ulitakiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2019 ambapo ni sasa hivi lakini mpaka leo wakati mradi unatakiwa ukabidhiwe una asilimia 37 tu kwa hiyo huu ni udhaifu wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, wakati wakandarasi hawa watatu wanaomba zabuni mpaka wanapewa walikuwa watatu na ndiyo maana walikidhi vigezo lakini wengine walikuwa ni kama mwavuli sasa hivi ni mkandarasi mmoja tu ambaye ni Jossam ndiyo anatekeleza mradi huo na hana uwezo wa kutosha ndiyo maana anakwenda speed ndogo sana na barabara hii ni muhimu kwa uchumi na haiwezi kukamilika kwa wakati. Kwa kuwa wakati wanapewa kazi walikuwa makampuni matatu na sasa hivi amebaki mmoja ambaye ni Jossam na udhaifu unaonekana, kwa nini Serikali isielekeze wale wote watatu ambao waliomba tenda waungane pamoja na kwa kuwa wameomba kuongezewa muda waweze kukamilisha barabara hii kwa wakati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kigezo kwamba mvua ilikuwa nyingi ndiyo maana barabara haiendi kwa wakati nakikataa kwa sababu majira ya kanda mbalimbali Tanzania za mvua na jua yanajulikana lakini hata wakati wa jua barabara hii bado haitengenezwi. Unaona wakati wa jua kabisa wamelala usingizi na mvua ikija wanasema ni mvua. Toka mwezi wa Julai na Agosti tuko kwenye jua karibu miezi tisa hapa imekwenda lakini bado speed ni ndogo. Kwa hiyo, tunaomba kisingizio kwamba majira hayajulikani kiondoke lakini pamoja na muda walioongezewa Serikali inatuambie barabara hii itakamilika lini kwa viwango vinavyotakiwa? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mbunge wa Jimbo la Kaliua, Mheshimiwa Magdalena Sakaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, barabara ya kutoka Tabora – Urambo - Kaliua - Uvinza - Kigoma yote sasa hivi itakamilika kwa sababu vipande vitatu vilivyobaki, kimojawapo hicho anachokizungumzia Mheshimiwa Magdalena Sakaya cha kutoka Urambo - Kaliua ambacho kina mkandarasi lakini pia Kazilambwa - Chagu tumetangaza tenda na wakati wowote tutatangaza tenda ya Malagarasi – Uvinza. Kwa hiyo, barabara nzima itakamilika na fedha tunayo kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, nimetembelea kule na nimewakuta wale wakandarasi wote watatu na msingi wa wakandarasi watatu ulianzishwa na Mheshimiwa Rais akiwa Waziri. Unakumbuka kule Mbutu aliwaunganisha wakandarasi 10 wakafundishwa na hao sasa hivi ndiyo wanakuwa wakandarasi wazuri. Kwa Urambo - Kaliua nimemtembelea yule mkandarasi nikaona changamoto zilizokuwepo, tumekaa, tumezungumza na tumekubaliana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Magdalena Sakaya mwenyewe ni shahidi, wamenunua mtambo mkubwa sana kwa ajili ya kusaga kokoto, kwa hiyo, barabara itakamilika kwa muda uliowekwa. Hakuna haja ya kuwasimamisha, tayari nimeshakwenda kule nikaongea na Mhandisi Mshauri na wale wakandarasi watatu wote wamerudi sasa wanaendelea na kazi, kwa hiyo, mradi huo utakamilika kwa muda walioongezewa. Nimhakikishie Mheshimiwa Sakaya na wananchi wa Urambo kwamba hapana shaka mradi huo unakamilika pamoja na barabara yote kuelekea Kigoma.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru niko kwenye runway, ningependa kujua kwa Mheshimiwa Waziri ni lini ujenzi wa jengo la abiria pamoja na taa kwenye njia za kurukia yaani runway zitakamilika kwenye uwanja wa ndege wa Songwe Mbeya ili uwanja ule uweze kufikia full capacity?

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasa hivi hata kukiwa na ukungu tu kidogo kwa sababu hakuna taa na unajua ndege nyingi pilot hawezi kutua kama haoni umbali wa futi 700 kutoka juu kwenda uwanja wa ndege kama haoni hawezi kutua. Sasa kukiwa na ukungu kidogo ndege haitui, mwenyewe nimesharudi Dar es Salaam mara mbili na ndege kwa kushindwa kutua mchana kabisa kwa sababu ya ukungu na tatizo kubwa likiwa ni taa za kwenye runway.

Sasa ningependa kujua lini vitu hivi vitakamilika jengo la abiria pamoja na taa ili Songwe International Airport iwe full capacity?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na kukamilisha mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Songwe ni kwamba tunatangaza tender mwezi huu, mwezi wa tatu tutakuwa tumeshampata mkandarasi na kukamilisha runway kutachukua miezi miwili. Baada ya hapo sasa tutaenda kwa ajili ya tender ya kukamilisha jengo. Kwa hiyo, usiwe na wasiwasi kiwanja cha Songwe ni katika viwanja vikubwa kikiwepo cha Julius Nyerere kiwanja cha Mwanza na KIA. Kwa hiyo, malengo ya Serikali ni kuhakikisha viwanja vyote hivyo vinaboreshwa na kufanya dreamliner iweze kuruka viwanja vyote.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, runway ya uwanja wa ndege au uwanja wa ndege wa Kigoma ni uwanja wa kimkakati kiuchumi ukizingatia mali iliyopo katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na majirani zetu. Sasa mgogoro uliokuwepo wafidia kwa wananchi umekwisha, sasa ni lini Serikali na European Investment Bank ambao ndiyo finance wa mradi ule sasa watakaa pamoja ili uwanja wa ndege ule uweze kupanuliwa na kutujengea jumba la wageni na maegesho ya ndege?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Nsanzugwanko na jibu lake ni fupi, mazungumzo kati ya Serikali na European Investment Bank yamekamilika tunachosubiri watuletee no objection ili tusaini mkataba mkandarasi aendelee na kazi.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Na mimi napenda kujua pamoja na ujenzi wa hii reli ya Mtwara –Mbambabay, Serikali ina mkakati gani wa kujenga reli kati ya Inyala (Mbeya) na Kyela kwenye Ziwa Nyasa ambayo itakuwa ni kiungo kizuri kuunganisha reli ya TAZARA pamoja na Bandari yetu ya Mtwara?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya TAZARA ilijengwa kwenye miaka ya 1975. Sasa hivi Serikali ya Tanzania na Zambia tunafanya ukarabati mkubwa pamoja na kuongeza vichwa na mabehewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Ziwa Nyasa tumejenga matishari matatu ambayo tayari yanabeba mzigo. Hata hivyo, baada ya kukamilisha ukarabati huu na kuimarisha ili reli ile iweze kubeba mzigo uliotarajiwa wa tani milioni 5 kwa mwaka, basi tutaanza na stadi kwa ajili ya kuunganisha hicho kipande cha kutoka Mbeya kuelekea kule Kyela.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naipongeza sana Serikali kwa juhudi kubwa ambayo inafanya kwenye ujenzi wa reli mbalimbali ikiwepo ya standard gauge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kipande cha reli kutoka Manyoni kwenda Singida ambacho ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Singida. Je, Serikali ina mkakati gani wa kufufua kipande hiki ambacho hakijafanya kazi kwa muda mrefu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilijenga kipande cha reli hii ya kati kuelekea Singida lakini baada ya ukarabati mkubwa wa barabara ya kutoka Dodoma kwenda Singida hapo katikati mizigo mingi imekuwa inatumia barabara. Suala hili tumeshaanza kulifanyia kazi ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza tukakarabati hiyo reli na kushawishi sasa wabeba mizigo ikiwepo ni pamoja na kuweka taratibu na sheria ndogo ndogo ili wengi watumie reli badala ya barabara. Kwa sasa suala hili Serikali inalifanyia kazi.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pia kumekuwa na mpango wa kujenga reli itakayopita Kaskazini mwa nchi itakayounganisha Miji ya Tanga, Moshi, Arusha hadi Musoma. Je, mpango huo umefikia hatua gani? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Mbunge Qambalo lakini kikubwa nimwombe leo tunawasilisha bajeti, asiwahishe shughuli, taarifa zote atazipata kwenye kitabu cha bajeti.
MHE. DANIEL N. NSANZUKWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya matawi ya reli ya SGR ni kujenga reli kutoka Uvinza – Kasulu - Msongati nchini Burundi. Je, mchakato wa kuanza upembuzi yakinifu umefikia hatua gani?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, niomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Mbunge Nsanzugwanko ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati yangu ya Miundombinu na yeye pia najua anafahamu, kwa hiyo, tutoe muda kidogo, ni dakika chache zimebaki ili nitoe hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano halafu mambo mengine yatafuata, tusiwahishe shughuli, dakika bado ni chache.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika kutokana na jibu la msingi la Wizara nataka kujua kwanza, je, Serikali haioni kwamba inapoteza muda katika utekelezaji wa miradi mbalimbali hususan miradi ya barabara kwa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, barabara hii ni barabara muhimu sana katika uchumi wa Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Songwe. Je, hawaoni kuna umuhimu wa kuongeza muda wa kufanya kazi kwa haraka ili hii barabara iweze kukamilika na wananchi wa mikoa hii miwili waweze kufaidika katika ujenzi wa kiuchumi katika Taifa hili la Tanzania?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu, usanifu wa kina utaratibu wa manunuzi na ujenzi ni utaratibu wa kimataifa na maana yake ni kuhakikisha kwamba hiyo kitu inaitwa value for money inapatikana vizuri kwa sababu msipofanya taratibu mkaainisha mahitaji yote, matokeo yake ndio kufanya upembuzi ambao ni pungufu na mkiingia tenda mnaweza msipate value for money.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, hoja yake ya kwenda haraka Serikali inaenda haraka ili kuhakikisha na sehemu kubwa ni msongamano wa pale Mbeya Mjini, ndio maana tunataka kuchepusha ili tutajenga mchepuo kwa ajili ya malori, lakini pale katikati kwa ajili ya kupanua ili msongamano usiwe mkubwa pale mjini Mbeya.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu na mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alikuwepo Mbeya kwenye ziara na Mheshimiwa Rais Mkoani Mbeya na aliona mwenyewe msongamano ulivyo kwa barabara hiyo ya TANZAM, ambayo kwa kweli inahudumia sio Mikoa ya Mbeya na Songwe tu, ni nchi nzima pamoja na nchi ya DRC, Zambia, Malawi pamoja na nchi zingine.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa fedha yake yenyewe ikisubiri fedha za Benki ya Dunia?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mwambalaswa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuanza kabla ya kukamilisha usanifu, lakini suala la msongamano wa magari lina solution nyingi pia ukisimamia taratibu za kiusalama na ndio maana tuna Jeshi la Polisi bado wanameneji vizuri ili msongamano ule usiwe mkubwa na ndio maana msongamano upo kwa muda fulani fulani tu, lakini muda mwingine panakuwa pamekaa vizuri.

Mheshimiwa Mwambalaswa, hili tunalifanyia kazi, Serikali inatambua hiyo changamoto, kwa hiyo asiwe na wasiwasi, baada ya muda mambo yote yatakwenda vizuri.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa daraja Sibiti sasa limekamika kwa maana magari yanapita pale juu na Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya ile lami, sasa tungependa kujua kwamba ujenzi wa hizo kilomita 25 za lami umefikia wapi?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kiula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Daraja la Sibiti limekamilika na tayari tumesaini mkataba na mkandarasi yule yule ili aweze kujenga zile kilomita 25 za lami. Kwa hiyo, fedha ipo na mkandarasi yupo na mkataba umesainiwa, anaendelea kujenga kwa kiwango cha lami hizo kilomita 25.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama ilivyo katika Jimbo la Simanjiro vivyo hivyo Jimbo la Rungwe kuna shida ya mawasiliano hasa katika Kata za Ilima, Swaya, Bujera pamoja na Ikuti. Je, ni lini Serikali itasaidia wananchi wa maeneo haya waweze kupata mawasiliano mazuri hususan katika mitandao yote wana shida ya mawasiliano? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna maeneo katika Jimbo la Rungwe ambayo yana changamoto ya mawasiliano. Ni kweli pia kwamba hata Mbunge wa Jimbo la Rungwe, Mheshimiwa S. H. Amon amekwishafika ofisini lakini pia bahati nzuri ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu ambako ndiyo tunashughulikia masuala hayo, tumekwishaongea, amekwishaleta barua kwa maandishi na tayari zabuni ya Awamu ya Tano maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Sophia ambayo hata Mbunge anayafahamu yatajumuishwa kwa ajili ya kupelekewa mawasilinao. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, naomba kwa ruhusa yako unipe nafasi nitoe pole kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi, hasa wananchi wa Kilwa pamoja na Mchinga ambao wamepata maafa ya mafuriko. Sisi kama Wabunge wa Mkoa pamoja na Taifa tunaungana nao na tuko pamoja nao. Pia nikumbushe hoja ambayo ilitolewa na Mbunge mwenzangu jana juu ya kuona umuhimu wa Bunge kuchangia Mkoa wa Lindi, hasa wale wahanga ambao wamepata maafa. Kwa hiyo, kupitia Kiti chako tutaomba mwongozo wako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Rais wetu alifanya ziara tarehe 16 Oktoba, 2019 na katika ziara hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri aliambatana na Mheshimiwa Rais. Moja ya ahadi kubwa ambayo aliitoa na ambayo wananchi wa Masasi, Nachingwea na Ruangwa wanasubiria ni kuona utekelezaji wa kile ambacho alikitolea maagizo juu ya kuanza kwa ujenzi wa lami kwa barabara hii ambayo kwa muda mrefu wananchi kwao imekuwa kero. Sasa naomba kufahamu kauli ya Serikali kwa nini mpaka sasa bado maagizo yale hayajaanza kufanyiwa kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Wilaya ya Nachingwea inaungana na Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma. Kwa muda mrefu wananchi wa maeneo ya Tarafa ya Kilimarondo ambao wanaunganishwa na Mto Lumesule wamekuwa wanapata changamoto kubwa sana ya kupata mawasiliano. Naomba kauli ya Serikali kupitia Wizara, wana mpango gani juu ya kufungua barabara hiyo ya Kilimarondo kwenda Namatunu kutokea Lumesule kwenda kuunganisha Tunduru ili tuweze kufungua barabara hii tuweze kunufaika kiuchumi?

Mheshimi Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Wizara yangu inatekeleza ahadi zote za Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini pamoja na viongozi wetu wakuu wa Serikali. Ni kweli Mheshimiwa Rais aliahidi na sisi Wizara tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo hatua, baada ya ahadi lazima tujipange na kuandaa bajeti ndiyo tuendelee kutekeleza. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na sasa hivi ndiyo tunaandaa bajeti, kwa hiyo tutaendelea kutekeleza hilo lakini pia kumbuka kwamba tunapenda kwanza kukamilisha ujenzi wa barabara zote za mikoa halafu baadaye ndiyo twende kwenye regional roads. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia feeder roads kwa vile kuna TARURA kuna ambazo zitaingia kwenye TARURA lakini kuna ambazo zitatekelezwa na Wizara ya Ujenzi. Kwa hiyo, barabara hiyo aliyoisema kwenda Kilimarondo tutaipitia na kuona kwamba itekelezwe na taasisi gani. (Makofi)
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya yetu ya Bukoba Vijijini tuna barabara ya kutoka Kanazi – Ibwela – Nakibimbiri – Katoro mpaka Kyaka. Barabara hiyo ni mbovu sana hasa kipindi hiki cha mvua haipitiki. Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na uharibifu wa barabara Mkoa wa Kagera, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha barabara nyingi sana zimeharibika na niliagiza TANROADS wafanye makadirio, mpaka tarehe 31 Januari tunahitaji shilingi bilioni 25 kwa ajili ya kurejesha miundombinu ya barabara katika hali waliyokuwa nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na barabara ambayo ameiulizia, kwa sababu ndiyo ametupa taarifa sasa hivi tutaiangalia na kumuagiza Meneja wa TANROADS ili kwanza tuone, je, ni barabara ya TARURA au ni barabara ambayo inahudumiwa na TANROADS tuweze kuifanyia kazi na Mheshimiwa Mbunge tutamjibu kadiri inatakavyowezekana.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni mara ya 15 nauliza kuhusiana na barabara muhimu sana ya Chuo cha Ardhi – Makongo – Goba. Mara ya mwisho nilijibiwa tukiwa tunaelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali ya Mtaa ambapo Mkuu wa Mkoa alienda na mkandarasi wakaweka vifaa pale wakawaambia wananchi barabara itajengwa watalipwa fidia. Leo baada ya uchakachuzi mkandarasi ameondoka, ile lami kilometa moja ambayo tulijenga Halmashauri imekwanguliwa, wananchi hawajui mustakabali wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama mwakilishi wao, naomba Waziri anipe jibu na jibu liwe la ukweli na uhakika, ni lini barabara ya Makongo inayoanzia Chuo cha Ardhi – Makongo Juu – Goba itajengwa kwa kiwango cha lami na wananchi kulipwa fidia yao wanayostahili? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Makongo tayari tumeanza kuijenga, kama unavyosema ni kweli mitambo ilienda lakini huwezi ukajenga barabara katika kipindi cha mvua nzito, huo ndiyo utaratibu, hiyo ndiyo sayansi yake, kwa sababu udongo unakuwa umeloana, kuna kiwango maalum kinachohitajika kwenye maji ya ujenzi wa barabara, huwezi ukafanya ushindiliaji kama moisture content iko high.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na suala la fidia, kwa vile tumeshasaini mikataba tayari fidia ni lazima ilipwe. Huwezi ukajenga barabara bila kulipa fidia lakini pia fidia italipwa kwa mujibu wa sheria. Kama kuna mtu alijenga ndani ya hifadhi ya barabara hatuwezi kumlipa lakini yule ambaye tumemfuata, alikuwa yuko nje ya hifadhi ya barabara, huyo lazima tutamlipa, kwa hiyo fidia italipwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara ya kuanzia Mombo – Soni - Lushoto ni nyembamba mno hata kuhatarisha maisha ya watu pamoja na mali zao. Je, ni lini upanuzi wa barabara ya Soni – Mombo - Lushoto utaanza ili kuondoa kadhia wanayoendelea kuipata wananchi wa Lushoto?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na barabara ya Mombo – Lushoto, kwamba ni nyembamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara ile ni nyembamba lakini imepita katika milima mirefu na udongo ule uko sensitive sana kwenye erosion. Kwa hiyo, tulijenga katika hali ile lakini baadaye tuta-redesign na kuipanua huku tukiwa waangalifu kwa sababu ni lazima ukate milima. Sasa utakapokata milima maana yake unaifanya tena ielekee kwenye mwelekeo ikinyesha mvua nyingi iweze kubomoka. Mwaka jana Mheshimiwa Mbunge ni shahidi, udongo uli-slide ukaifunika barabara moja kwa moja.

Kwa hiyo, ile barabara lazima ijengwe kwa uangalifu sana kwa sababu udongo wake mvua ikinyesha mara nyingi unaporomoka.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nilikuwa na swali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Tabora mjini pamoja na kwamba liko mjini lina Vijiji vipatavyo 41 ambavyo mawasiliano yake si mazuri na Mheshimiwa Naibu Waziri Nditiye hivi karibuni tulitembea wote baadhi ya sehemu.

Swali kwa kuwa tayari andiko lilishaandikwa la kuomba minara ya simu kwa TTCL sijui zoezi hilo limefikia wapi kuhakikisha Vijiji hivyo vinapata mawasiliano ikiwepo eneo tulilokwenda pamoja Mheshimiwa Waziri linaloitwa Iteteme?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Mwakasaka kama ifuatavyo. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake kuhusiana na masuala ya tenda, lakini kwa nyongeza ni kwamba nchi yetu kwa sasa ina usikivu wa asilimia 94, imebakiza asilimia 6, na kama alivyozungumza kwamba tumetangaza tender nyingine ambayo Vijiji 1222 sasa vitapata minara.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwakasaka na ndugu zangu majirani zangu wana Tabora baada ya hii tenda tunakamilisha minara kwenye maeno yote usikivu utakuwepo maeneo yote pamoja na eneo la delta.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi, nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri au Waziri, mwaka jana tulikwenda Jimboni Serengeti na Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Kamati ya Miundombinu, moja eneo tulilowapeleka sisi Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ni kutembelea uwanja wa Mugumu ambao ilikuwa ujengwe na mwekezaji mmoja anaitwa Grumet, lakini Grumet akawa ameacha; sisi kama halmashauri tunakibari cha NEMC, tunakibari cha Mamlaka ya Viwanja vya ndege tuna Hati Miliki ya kiwanja, TANAPA kwa kushirikiana na halmashauri wameamua kujenga uwanja ule.

Je, Wizara iko tayari kuchangia chochote kwenye mwaka ujao wa bajeti kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Serengeti ambao utakuwa unapokea ndege karibia 200 kwa siku? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu ya Kiserikali tunaomba wasilisho hilo mwambie Mkurugenzi wa halmashauri aliandike na kulipeleka kwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI halafu Katibu Mkuu wa TAMISEMI atawasiliana na Katibu Mkuu wa Uchukuzi huo ndiyo utaratibu wa Serikali kwa sababu hiyo ni taarifa unaisema hapa Wizara yangu haijui ukifanya namna hiyo Mheshimiwa Mbunge tutashirikiana.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa ajili ya kununua ndege nyinghi ili kiinua na kuboresha uchumi wan chi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa kazi kubwa anayofanya ameshafika Manyara mara kadhaa kutatua kero za sekta yake. Nina maswali mawili, kwa kuwa Serikali imeainisha kwenye Mwongozo wa mpango 2020/2021 kwamba itaboresha viwanja kadhaa vya ndege hapa nchini, lakini katika orodha hiyo kwa bahati mbaya sijaona uwanja wa ndege wa Arusha kulingana na umuhimu wake.

Je, Serikali ina mkakati gani sasa kwa umuhimu ambao tumeutaja wa uwanja huo kuboresha uwanja huo ili kukuza uchumi wa nchi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa manufaa ya kuwa na ndege nyingi ni ndege hizo kutumika. Sasa kwa kuwa pia uwanja huu uko katikati ya mikoa mingi ikiwepo Mkoa wa Manyara, Mkoa wa Singida, Mkoa wa Simiyu, Mkoa wa Mara na hata Mkoa wa Dodoma.

Je, Serikali ina mkakati gani ili kuboresha uwanja huo na wananchi walio wengi wa mikoa tajwa waweze
kuhamasika kutumia usafiri wa ndege ili kutumia ndege zetu ambazo zinatosheleza hapa nchini kwa sasa hivi?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Arusha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipongeze majibu ya Naibu Waziri, ni kweli tumeweka bajeti kwa ajili ya kuendelea kuimarisha uwanja wa ndege wa Arusha na kama alivyozungumza tumeshaweka tender na bajeti hii ambayo sasa hivi mpango Waheshimiwa Wabunge mnaongea tutaweka bajeti kwa ajili ya kuurefusha. Na maana yake ni nini, katika kiwanja ambacho kinaongoza kuwa na ndege nyingi kiwanja cha Arusha ni cha tatu, kinarusha kwa siku zaidi ya ndege 125.

Kwa hiyo, ni biashara kubwa ndiyo maana tunataka Bombardier iende ikatue pale. Kwa hiyo, mpango wa kuboresha upo ili hiyo Mikoa ambayo umeitaja nayo iweze kufaidi kutumia usafiri wa ndege na tutaendelea kufanya hivyo Mheshimiwa Mbunge.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Barabara ya kutoka Iringa Mjini kwenda Ruaha National Park Iringa ni ahadi ambayo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Nne na Awamu ya Tano na mpaka sasa ni upembuzi yakinifu tu unaendelea kwa miaka yote hiyo kumi na tano. Ni lini sasa barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami ili kusaidia wale watalii wanaokwenda kule waweze kwenda kwa ufasaha? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara anayoizungumza inaitwa jina Iringa - Msembe (km 104). Barabara hiyo ilikuwa imewekwa kwenye mafungu mawili; moja ni la ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli ambao tumeshatangaza tenda na mkandarasi amepatikana wakati wowote tutasaini mkataba. Hizi km 104 tayari tumeshamaliza mpaka usanifu wa kina na tumeomba fedha kutoka Benki ya Dunia. Kwa hiyo, wananchi wa Iringa, tena ndiyo nimeoa kule, shemeji zangu wale, wala asiwe na wasiwasi barabara ile inajengwa.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nangurukuru - Liwale ni ya vumbi na kokoto lakini naishukuru Serikali mwaka huu tumetengewa fedha shilingi milioni 300 kuanza usanifu wa kina. Hata hivyo, mvua zilizonyesha mwezi uliopita zimelaza watu siku tatu barabarani. Ni nini mkakati wa Serikali kuifanya barabara hii ipitike majira yote? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Kuchauka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema mwenyewe tumetenga fedha kwa ajili ya kuifanyia usanifu wa awali na usanifu wa kina, malengo ni kuijenga kwa kiwango cha lami ili haya matatizo ya mvua yanapojitokeza yasije yakaleta athari kwa wananchi. Hata hivyo kwa vile umetuambia tutaifanyia kazi, hela ya emergency ipo ili tuweze kurudisha hiyo miundombinu wananchi waendelee kutumia barabara hiyo.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ahadi hizi za Rais ziko maeneo mengi na Vunjo maeneo ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Himo iliahidiwa kujengewa barabara kwa lami km 7 na sasa kuna mafuriko eneo la lower area Kahe kuanzia Fungagate, Kahe, Kiomu mpaka maeneo ya Chekereni na Kilema Hospital. Barabara zote hizi ziliahidiwa na Mheshimiwa Rais kujengwa kwa kiwango cha lami na Serikali inajua. Ni lini watatekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme ni kweli ziko ahadi nyingi za Mheshimiwa Rais lakini katika barabara zimewekewa utaratibu wake. Tunaanza kwanza kukamilisha barabara kuu na zile zinazounga mipaka ya majirani zetu baadaye tutakwenda kwenye barabara za mikoa na tunarudi tena chini kwenye barabara hizo za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wewe tulia tu ni kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ahadi za viongozi lazima zitekelezwe.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niulize swali langu la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa ziarani Wilayani Ruangwa alitoa maelekezo kwamba barabara kutoka Ruangwa - Nachingwea - Masasi na Ruangwa -Nachingwea - Nanganga zijengwe kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Rais akitoa kauli inakuwa ni maagizo. Je, lini upembuzi yakinifu utaanza kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Salma Kikwete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Salma Kikwete ni kwamba upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tumeshakamilisha. Ujenzi tumeshaanza na tayari tumeshajenga km 5. Kwa hiyo, maagizo ya Mheshimiwa Rais kama alivyosema ni sheria lazima tutayatekeleza.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Barabara ya kutoka Mangamba - Kilambo - Msimbati itajengwa lini kwa kiwango cha lami kwa sababu ni Sera ya Serikali barabara zinazounganisha nchi kuzijenga kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba usanifu wa barabara hiyo ya kutoka Mtwara Mjini - Kilambo tumeshakamilisha. Ni nia ya Serikali kuhakikisha tumeijenga kwa kiwango cha lami pamoja na daraja ili tuweze kuungana kwa daraja la pili kwa ajili ya kwenda Mozambique.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeahidi kujenga barabara ya Kaliua - Chagu (km 48) na walituambia kwamba tayari walishapata mfadhili wa kuijenga barabara hiyo. Ni lini sasa ujenzi wa barabara wa hiyo km 48 tu utaanza? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza barabara hiyo siyo kilometa 48 ni kilometa 36, tenda tumeshatangaza wakati wowote tunasaini mikataba. Baada ya kusaini mikataba kuanzia tarehe ile tuliyosaini tutakwambia sasa tunaanza lini na tunakamilisha lini.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujenga daraja la muda la Nderema ambalo linaunganisha Wilaya ya Kilindi na Handeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuipongeza Serikali, naomba niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mvua hizi hazikutegemewa na zimeharibu sana barabara kuanzia Handeni – Kibirashi - Songe – Gairo. Je, Serikali iko tayari kutuma wataalamu kwenda kuangalia hali ya uharibifu ili kuweza kurejesha mawasiliano katika eneo hili? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Kigua, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitoe taarifa kwamba kwa mujibu wa usanifu wa barabara mvua zina return period tatu; kuna ya miaka kumi, hamsini na miaka mia moja. Mvua iliyonyesha juzi Tanga inaonekana ina return period ya miaka mia moja na ambayo design huwa haijumuishi returned period hizo lakini kwa mujibu wa swali lako Mheshimiwa Mbunge tuko tayari.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa barabara ambayo inatoa Makao ya Wilaya kwenda Utegi inasumbua kwa muda mrefu na kwa muda mrefu imekuwa ni ahadi ambayo bado haijafanyiwa kazi. Je, Serikali sasa itakuwa tayari kuiangalia wakati inasubiri hiyo ahadi ya Rais ya muda mrefu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ahadi za Rais ziko nchi nzima na Wilaya ya Kilolo pia tulikuwa na ahadi kama hiyo ambapo Rais alikuwa amesema barabara ya kutoka Kilolo - Iringa ingeanza kujengwa mara moja. Sasa tayari tunaelekea kwenye uchaguzi na ilikuwa ahadi ya kabla ya uchaguzi. Je, Serikali inasemaje ili wananchi wa Kilolo wajue umuhimu wa Serikali ya Awamu ya Tano? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme Serikali inatekeleza maagizo na ahadi zote za Ilani ya Chama cha Mapinduzi na pia itaendelea kutekeleza maagizo yote ya Viongozi wetu Wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Utegi itajengwa kutokana na upatikanaji wa fedha ndiyo maana usanifu umeendelea. Kwa hiyo, tukishamaliza usanifu, tukapata fedha itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini barabara yako Mheshimiwa kama ambavyo tumeshaongea hata nje ya hapa kwamba barabara ile tayari imeingizwa kwenye Mpango wa Benki ya Dunia. Ni taratibu zinaendelea baadaye itajengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kumekuwa na kawaida ya hawa service providers pamoja na ruzuku wanayopata kutoka Serikalini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote wamekuwa wanajikusanya kwenye maeneo ambayo tayari kuna mawasiliano badala ya yale madhumuni ya kupeleka mawasiliano kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano. Mfano katika jibu lake la swali langu, katika Kata ya hiyo ya Tura, Kijiji cha Karangasi, tayari kuna mawasiliano lakini bado tena kumepelekwa mtandao mwingine, lakini yapo maeneo ambayo hayana mawasiliano. Je, kwa nini sasa hawa Service Providers wasipeleke mawasiliano kwenye maeneo yale ambayo hayana mawasiliano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kata ya Mmale yote haina mawasiliano; je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika Kata hiyo ya Mmale? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Tura kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, hoja yako uliyoizungumza ni kweli, kwamba service providers, watoa huduma za mawasiliano walikuwa wanajirundika kwenye maeneo machache, maeneo ambayo yana biashara kubwa au yana population kubwa ya watu. Baada ya kuliona hili, Bunge hili hili liliamua kuunda Mfuko wa Masiliano kwa Wote. Maana yake nini, ni kwamba ule Mfuko sasa unaenda kwenye maeneo yale ambayo, hawa wanaofanya biashara tu bila kujali utu wa mwanadamu Mtanzania, kwamba sasa tuwalazimishe waende kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko huu tayari, sasa hivi tunaenda maeneo yote bila kujali kwamba kuna faida kubwa na ndiyo maana hata kwenye maeneo anayoyahitaji Mheshimiwa Mbunge sasa, baada ya kutangaza hii tenda tutahakikisha kata zote, maeneo yote ili mradi yana Watanzania yanapata huduma ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, Moja kati ya barabara ambazo ni muhimu sana hasa katika foleni za Dar es Salaam ni barabara ya Chuo cha Ardhi - Makongo – Goba. Ninatambua kwamba baada ya kero ya muda mrefu sana hatimaye barabara itaanza kujengwa. Sasa swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, changamoto kubwa iliyopo ni fidia ya wananchi ya shilingi bilioni 3 na tumekuwa tukizungumza kwa kipindi kirefu sana.

Mheshimiwa Spika, nilitaka nipate commitment ya Serikali ni lini wananchi hawa ambao wako tayari kuachia maeneo yao watalipwa fidia yao stahiki ili barabara ijengwe kwa viwango ambavyo ilikuwa imetarajiwa kujengwa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Halima kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumeanza kujenga ile barabara ya Makongo lakini kuhusiana na swali lako fidia italipwa kwa mujibu wa sheria, sheria ipo ilitungwa na Bunge. Kwa hiyo, siyo commitment ya mtu hapana, kwa mujibu wa sheria.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona nina swali la nyongeza, shida iliyoko Kalenga inafanana sana na shida iliyoko katika Mkoa wa Kigoma. Barabara ya Uvinza – Malagarasi ni ahadi ya muda mrefu na tumeambiwa huu ni mwaka wanne kwamba kuna fedha za Abu Dhabi Fund.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kujua hizo fedha Abu Dhabi Fund zipo kweli au hazipo ili tujue kwamba barabara hiyo haitajengwa.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, fedha zipo.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili. Kwanza nianze na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri sana ambazo wamekuwa wakizifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze sana Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi kwa ujenzi wa mtandao wa barabara katika Mkoa wetu wa Iringa, wamefanya kazi nzuri sana. Pia kuwalipa wananchi hao fidia kwa hiyo barabara ambayo imetajwa hapo.

Katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba wananchi hao wanatakiwa walipwe fidia na riba, sasa nimuombe Waziri anijulishe. Je, ni lini? Na wanalipwa bila usumbufu kwa sababu kwa kweli kwanza walitumia karibu miaka mitano kutolipwa baada ya tathmini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa changamoto ya kupitisha magari makubwa katikati ya Mji wa Iringa kumesababisha wafanyabiashara hasa wenye maduka, hoteli, migahawa kupata shida sana na wale wananchi wanaofuata huduma kwa sababu magari yao yanafungwa, kwa hiyo wanasababisha kutofanya biashara vizuri. Vilevile kumesababisha Serikali kutopata kodi ya uhakika na vilevile kuna ajali kubwa sana itakuja kutokea kwa sababu magari makubwa ya mafuta yanapita barabarani.

Je, Mheshimiwa Waziri sasa leo hii uniambie na uwaambie wananchi wa Iringa ile barabara ya mchepuo kwa sababu tumeshapata ahadi nyingi sana. Kila siku, nimeuliza kama maswali matano, lini sasa mtaijenga ili kuondoa hiyo changamoto ambayo imekuwa ni tatizo kubwa mno katika Mkoa wa Iringa? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mbunge Viti Maalum, Mheshimiwa Ritta Kabati kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza suala la riba ni commitment ya Serikali kwamba riba hiyo kwa wananchi italipwa baada ya fedha kutolewa kwa sababu tuko mwezi wa tisa na kwa mujibu wa sheria za kifedha, mwezi wa tisa ndiyo fedha zinaanza kutolewa. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Ritta Kabati kwamba fedha hiyo ya riba italipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usumbufu mwingine uliousema Serikali ilishaona, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwamba kuna umuhimu wa kuweka barabara ya mchepuo ili kuweza kuondoa hivyo vikwazo ambavyo mwenyewe umevitaja kwa wananchi. Kwa hiyo, nikuhakikishie, usanifu umekamilika na kama hatua tayari fidia tumeshalipa bado riba. Kwa hiyo sasa hivi taratibu za Kiserikali zinaendelea ili kuhakikisha barabara hiyo inajengwa haraka. (Makofi)
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini nina maswali ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri.

Swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Mapili na Namyomyo, Chikolopola, Lupaso pamoja na maeneo ya Lipumburu wamekuwa wakipata shida ya mawasiliano kwa muda mrefu sana. Ahadi ya Serikali ni kwamba kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha minara inajengwa hasa maeneo ya kandokando mwa vijiji vilivyomo mipakani mwa nchi yetu na nchi jirani. Kwa kuwa kuna tatizo kubwa sana la ucheleweshaji wa kupatikana vibali vya ujenzi iliyopelekea hata kwenye jibu la msingi, kwamba mradi mmoja unasainiwa mwezi Desemba, 2018 lakini unakuja kumalizika kutekelezwa Desemba, 2019.

Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha inaondoa tatizo la urasimu wa upatikanaji wa vibali ili minara ijengwe kwa haraka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kuahidi kwamba katika Bunge lililopita kwamba atatembelea vijiji hivi vilivyopo mpakani mwa Tanzania, Msumbiji ili kuzungumza na wananchi. Je, yupo tayari sasa baada ya Bunge hili kutembelea vijiji hivyo pamoja na Kijiji cha Lupaso ambacho Kiongozi Mkuu wa nchi mstaafu ndiyo nyumbani kwake? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nishukuru Bunge lako tukufu ambalo lilitunga Sheria ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Mfuko huu utahakikisha kwamba sasa nchi nzima inakuwa na mawasiliano. Ijumaa nilikuwa na mkutano na watoa huduma wote wa mawasiliano tukizungumzia miradi ya kata 521. Tumekubaliana baada ya wiki mbili tunakutana, kwa hiyo, hayo majibu ya msingi yaliyotolewa Mheshimiwa Bwanausi, vijiji vyote hivyo vyote vitapata mawasiliano na hiyo ndiyo ahadi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili la vibali, suala la vibali sasa hivi halina mgogoro tena, NEMC wamejiandaa vizuri tukiomba vibali tunavipata haraka. Ufumbuzi wa kutoka vibali haraka ulitokana na mradi wa makaa ya mawe pale Mtwara, Mheshimiwa Rais alielekeza kwamba sasa vibali vinatakiwa vitoke haraka na sasa vibali vinatoka haraka hakuna kikwazo tena cha kutoka vibali. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nitoe masikitiko kwamba leo ni mara ya nne ninauliza swali kuhusu kulipwa fidia kwa wananchi wa Kipunguni. Leo najibiwa kwa mara ya nne, mara ya tatu majibu yalibadilika nikaambiwa wangelipwa kwa mwaka wa fedha ulioisha, lakini kwa jibu la leo naona tumerudi nyuma. Serikali inasema watalipwa pale itakapopata fedha, sio sahihi kabisa hawa wananchi wamezuiwa kuendeleza maeneo yao kwa muda mrefu. Wananchi wengi wanakufa, wengine wanashindwa kujiletea maendeleo ni changamoto kubwa sana. Sasa swali langu halijajibiwa ni lini hawa wananchi watalipwa fidia kwa kuwa tuliambiwa wangelipwa mwaka jana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili zaidi ya wananchi 322 walienda mahakamani baada ya kutoridhishwa na mchakato ambao ulikuwa ni pamoja na kutolipwa viwango stahili na kutokubalina na tathimini.

Sasa Serikali ipo tayari kurudi na kuongea na wananchi hawa waondoe kesi mahakamani wafanyiwe tadhimini upya ili walipwe stahili zao sambamba na tathimini ya sasa ili wapate faida ya maeneo yao? Naomba majibu.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mbunge Anatropia kuhusiana na fidia ya Ukonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitajibu swali la mwisho, suala la mahakamani kwa sababu wao wameenda mahakamani hatuwezi kulizungumza humu Bungeni. Niombe Mheshimiwa Mbunge tuache hatua za kimahakama ziendelee, ruling inatakapokuwa imekuja basi sisi ndio tutaendelea nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu fidia ndio utaratibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalipa fidia pale ambapo inatekeleza mradi. Awamu ya kwanza tulikuwa tunajenga Terminal III tulilipa fidia kupata lile eneo na ukuta tumejenga. Tutakapohitaji kufanya maendelezo ya ule mradi tena kama ambavyo jibu la msingi limesema basi tutaendelea, tutachukua hilo eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni kweli kwamba tumezuia wananchi wasifanye maendelezo katika eneo ambalo tumeli-earmark kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Na hilo sio kwenye uwanja tu hata kwenye barabara. Kwa hiyo, tunafanya hivyo ili serikali pia isiingie gharama kubwa wakati wa ujenzi wa barabara wakati wa fidia.

Kwa hiyo, nikujibu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ipo makini itahakikisha kwamba pale ambapo inatekeleza mradi watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli aliahidi kwamba kabla ya kufika mwaka 2020, barabara hiyo ya kutoka Mlowo kwenda Kamsamba hadi Kibaoni itakuwa imekamilika. Ukiangalia kuanzia sasa hadi mwaka 2020 bado miezi michache tu. Je, ni lini sasa ahadi hii ya Serikali itatekezwa kwa vitendo badala ya maneno?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika majibu ya Serikali kwamba kukamilisha usanifu wa kina hawajataja kwamba ni lini usanifu wa kina utakamilishwa. Je, Serikali kutotaja muda wa kukamilisha usanifu wa kina haioni huku ni kutowatendea haki wananchi wa Mikoa ya Songwe, Katavi, pamoja na Rukwa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Haonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, umetaja ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni, lakini ujenzi wa barabara ni mchakato, lazima ufanye upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, baadaye uingie mikataba uanze kujenga. Hauwezi ukafanya kabla ya kukamilisha hizo hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vipande vya barabara ambavyo unavizungumzia tayari kuna kimoja mwezi huu wa tisa cha kutoka Mlowo kwenda mpaka pale tulipokamilisha daraja, mwezi wa tisa usanifu wa kina utakamilika baada ya hapo mambo mengine yanaanza. Upembuzi yakinifu umeanzia kule Muze unakuja kuunga Kamsamba, na tuna matarajio ya kuendelea huko na pia tumeshaanzia Inyonga kuja mpaka Maji ya Moto. Kwa hiyo, utaratibu unaendelea ahadi ya Mheshimiwa Rais inatekelezwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi na wananchi jirani zangu wa kule wawe na uhakika kwamba barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba kuuliza swali langu la nyongeza:-

Barabara ya kutoka Senga Ibisabageni mpaka Sima ni barabara inayotuunganisha Mkoa wa Geita na Mkoa wa Mwanza na Serikali ilitupa fedha upande wa Geita na upande wa Mwanza. Upande wa Geita tulishalima eneo letu tukamaliza lakini upande wa Mwanza umebakiza kama kilomita tatu na leo ni mara ya tatu namuuliza Mheshimiwa Waziri.

Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kufuatana na mimi kwenda kuona zile kilomita tatu tu ambazo upande wa Mwanza wameshindwa kumaliza ili watu waanze kupitisha magari yao pale? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kufuatana naye. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba niulize swali la nyongeza, kwa kuwa barabara ya Kenyatta itokaya Mwanza Mjini kwenda Usagala kuelekea Shinyanga ni barabara ambayo inahudumia watu wengi na kwa sasa inaendelea kuwa finyu sana. Ni lini Serikali kupitia mipango yake ya uboreshaji miundombinu itaitolea fedha barabara hii walau iwe ya njia tatu mpaka nne ili kuweza kukidhi mahitaji makubwa ya watu wa Mwanza?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanua barabara, kuongeza reli, hatuendi hivi hivi lakini mpaka traffic iweze kufikia kwamba sasa yanapita magari 20,000 au 40,000 kwa siku ndiyo tunaipanua ili kuiongezea uwezo. Kwa hiyo, itakapofikia itafanyika.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kama ilivyo katika Wilaya ya Momba, kule Moshi Vijijini katika Kata ya Uru Shimbwe Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli wakati anagombea alikuja pale akahutubia na akaahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mamboleo mpaka Shimbwe. Kwa kweli ile barabara sasa hivi iko katika hali mbaya sana, sasa naomba kujua toka kwa Serikali ni lini ahadi hii ya Mheshimiwa Rais itatimizwa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Komu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni kuunganisha mikoa kwa barabara za lami, lakini na mipaka ya majirani zetu kuunganisha kwa lami halafu baadaye ndiyo tunaendelea na barabara nyingine.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Barabara ya kutoka Iringa Mjini kuelekea Ruaha National Park ambayo ni Jimbo la Kalenga imekuwa ni changamoto na ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa Awamu ya Tano. Ni lini sasa barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile itajengwa pamoja na Uwanja wa Ndege wa Nduli na itajengwa kupitia fedha za Benki ya Dunia, taratibu za kupata hizo fedha zinaendelea itakapokamilika mradi utaanza.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Kwa kuwa barabara hii inapita eneo muhimu sana eneo ambalo wanachimba makaa ya mawe, Kijiji cha Magamba, na kwa kuzingatia pia kwamba barabara hii inaunganisha wilaya mbili kwa maana ya Wilaya Mbozi pamoja na Wilaya ya Songwe, je Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuanza kufikiria kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa sehemu (b) ya swali hili haikujibiwa, inayohusu vivuko pamoja na madaraja Kata za Itumpi, Halungu, Itaka pamoja na Bara, je, Serikali inawaambia nini wananchi wa maeneo haya ambao wanakosa mawasiliano ya vivuko na wanakosa maeneo ya kuvukia; je, Serikali inawaambia nini na kwa kutokujibu vizuri swali hili, je, Serikali haioni kwamba wananchi hawa wataendelea kuteseka kwa kuwa maeneo mengi hawa wananchi hata kuvuka kutoka kijiji kimoja kwenda kingine inakuwa ni shida kubwa sana? Je, Serikali haioni kuwa ni kuwatesa wananchi wa maeneo haya?.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Haonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, Mheshimiwa Mbunge Sera ya Chama cha Mapinduzi, Sera ya Wizara ni kuunganisha mikoa kwa lami; lakini tunaendelea kuziunganisha wilaya kwa barabara za changarawe. Itakapofikia tumemaliza kwanza sera yetu ya kuunganisha mikoa kwa lami; na nishukuru kwamba Mkoa wako tayari umeshaunganishwa kwa lami tutaendelea sasa na barabara za wilaya, kwa hiyo uvute subira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la madaraja na vivuko, sijui tofauti yake ni nini, lakini nafikiri umezungumzia madaraja; suala la madaraja tunaendelea kujenga kwenye barabara zote za TANROADS pamoja na barabara za TARURA pia. Kwa hiyo tutaendelea kujenga kadiri ya ukusanyaji wa fedha kutoka kwenye Mfuko wa Barabara. Nina imani na wewe mwenyewe unafahamu, TARURA sasa hivi inakwenda vizuri, matatizo yake tu ni kwamba fungu halijawa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kwa sababu linatokana na Mfuko wa Barabara na kuna Kamati inaendelea sasa ili iweze kuweka uwiano ambao ni mzuri kulingana na barabara za TARURA baada ya muda tutakuwa na hela ya kutosha madaraja hayo ambayo unayaita vivuko pia yatajengwa.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, majibu hayajaniridhisha kwa sababu mimi mwenyewe natokea hukohuko Musoma Vijijini. Barabara hii ni kiunganishi kikubwa sana kwa wakazi wa maeneo hayo na barabara hii haipitiki kama anavyoelezea. Watambue kwamba kuna wakulima na wafanyakazi na wafanyabiashara pamoja na wafugaji. Barabara hii ni mateso sana kwa wakulima kutoa mazao yao kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Serikali haioni sasa ni wakati wa kuijenga barabara hii ili kuinua uchumi wa maeneo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ahadi ya muda mrefu sana ya Serikali, naomba commitment ya Serikali; Je, ni lini ujenzi wa barabara hii utaanza, kwani wananchi wa maeneo hayo wanateseka sana? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kutekelezwa na barabara hii imeendelea kujengwa kulingana na upatikanaji wa fedha na ni ahadi kwamba hawa wananchi tutahakikisha kwamba wanapita katika hiyo barabara. Barabara hiyo kwa sababu imegawanyika; upande wanasimamia TANROADS, upande wanasimamia TARURA na ndiyo maana sasa hivi iko Kamati Maalum ambayo inapitia barabara zote ili kuweza pia kuweka mgawanyo mzuri wa Mfuko wa Barabara. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Ilani ya Chama cha Mapinduzi, akawaambie hao wananchi kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi itatekelezwa, hiyo barabara itatengenezwa na wasiwe na wasiwasi wowote kwa sababu tunaendelea kufanya hivyo. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa Serikali kujibu swali langu Na. 22 vizuri. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; mnara wa Airtel uliojengwa kwenye Kata ya Kipili, Kitongoji cha Madoletisa ambao haujawashwa kwa miaka miwili sasa na mnara wa Vodacom kwenye Kata ya Kilumbi ambao nao haujawashwa kwa miaka miwili hadi sasa: Je, ni lini itawashwa ili wananchi waanze kufaidika na huduma za mawasiliano?

Mheshimiwa Spika, je, Miradi ya Mawasiliano Vijijini iliyomo kwenye Mpango wa Maendeleo wa 2019/2020 ambayo orodha yake ipo kwenye randama pia kwenye kijitabu cha taarifa ya Wizara ya Julai 2019, itatekelezwa lini?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, mnara uliojengwa katika Kitongoji cha Madoletisa ni kweli ni wa Kampuni ya Simu ya Airtel. Mnara huu ulijengwa kama mnara wa kupeleka mawimbi ya simu kwenda katika minara mingine ya mbali (Transmission Site). Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliliona tatizo la mnara huo ambapo unatumika kama transmission site bila kutoa huduma kwa wananchi waliopo Madoletisa na kuiagiza Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel wauwekee vifaa vya radio ili mnara huo pia utumike kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi. Tumewasiliana na Airtel ili wakamilishe kazi ya kuwapelekea wananchi mawasiliano mara moja ndani ya mwezi huu wa Aprili, 2020.

Mheshimiwa Spika, Miradi ya Mawasiliano Vijijini kwenye Vijiji vya Igigwa, Migumbu, Nyahua na Tumbili kutoka Kata ya Igigwa, Vijiji vya Ipole, Makazi, Udongo na Ugunda kutoka Kata ya Ipole, Vijiji vya Kanyamsenga, Kiloleli na Mtakuja katika Kata ya Kaloleli, Vijiji vya Imalampaka na Mibono katika Kata ya Kipanga pamoja na Kijiji cha Kiyombo kutoka Kata ya kipili, havikupata watoa huduma katika zabuni ya mwezi Julai, 2019. Miradi hiyo itatangazwa tena mwezi Juni, 2020.