Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 49 Home Affairs Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 421 2018-06-12

Name

Susanne Peter Maselle

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:-
Wananchi wakazi wa Kijiji cha Ishokelahela, Misungwi, Mwanza, wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kihalifu, kinyama na kikatili na Vyombo vya Dola kuwaondoa katika makazi yao na kuacha kuchimba dhahabu ili eneo hilo libaki kwa Mwekezaji anayetaka kuwaondoa kwa nguvu kinyume cha sheria:-
i. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu vitendo hivyo wanavyofanyiwa wananchi hao?
ii. Je, Serikali iko tayari kuunda timu kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mgogoro huo na kuchukua hatua stahiki ambazo zitamaliza kabisa mgogoro na kuwawajibisha wote ambao wamesababisha hali iliyopo sasa?

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kijiji cha Ishokelahela ambao ni wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu wamekuwa na mvutano na Mwekezaji Isinka Federation 2014 Mining Cooperative and Society Limited anayefanya shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika eneo hilo kihalali. Mvutano huo umepelekea wananchi hao kutaka kuvamia eneo la Mwekezaji huyo bila kufuata sheria kitendo ambacho kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linao wajibu wa kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaimarishwa katika eneo hilo kwa mujibu wa sheria, hivyo haliwezi kuruhusu wananchi kuchukua sheria mkononi na kuvamia eneo hilo ambalo linamilikiwa kihalali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba vyombo vya dola vimekuwa vikiwanyanyasa na kuwafanyia unyama wa kikatili wananchi katika makazi yao bali katika eneo husika Jeshi la Polisi limekuwa likiwazuia kuingia katika eneo ambalo sio mali yao kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala hili ni suala muhimu, hata hivyo, Serikali inaendelea kulifuatialia kwa karibu na kutafuta suluhisho la kudumu ili kuondoa migongano ambayo inaweza kuhatarisha amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nitumie fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge awahamasishe na kuwashauri wananchi wa Kijiji hicho ambao ni wachimbaji wadogo wadogo kuungana katika vikundi na kuomba leseni za uchimbaji ili wafanye shughuli zao kihalali.