Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 46 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 396 2016-06-20

Name

Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Primary Question

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Wakulima 1,128 wa msitu wa derema kata ya Amani Muheza wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu kupunjwa fidia ya mimea yao kutoka shilingi 3,315 kw a shina moja:-
(a) Je, ni lini wakulima hapo watalipwa stahiki zao,
(b) Je, kwa nini kwenye malip hayo Serikali sijijumiushe fidia ya ardhi yao?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa jumla ya wananchi 1,128 waliokuwa wakifanya shughuli za kilimo ndani ya hifadhi ya msitu wa Derema, walihamishwa na kulipwa stahiki zao ili kupisha uhifadhi kati ya mwaka 2001 na mwaka 2009, lakini siyo kweli kuwa wananchi hao walipunjwa fidia ya mazao yao. Ukweli zaidi ni kuwa katika mchakato wa kuhakikisha eneo lote la msitu linahifadhiwa kama ilivyokusudiwa, mazoezi mawili tofauti yalifanyika kwa vipindi tofauti na kwa ufadhili wa taasisi tofauti ambazo ni Shirika la Maendeleo la Nchi ya Ufini, FINNIDA lililofadhili fidia kwa mazao kwenye mpaka na Benki ya Dunia waliofadhili fidia kwa mazao ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika zoezi la kwanza lililofanyika mwaka 2001 mpaka 2002 chini ya ufadhili wa FINNIDA kupitia mradi uliojulikana kama East Usambara Conservation and Management Programe, idadi ya wakulima 172 waliokuwa wakifanya shughuli za kilimo upande wa nje wa eneo la msitu walilipwa fidia ya mazao yao. Kwa kuzingatia muda mfupi uliokuwa umebaki hadi mradi kufikia tamati yake, shirika hilo liliwalipa wakulima kiwango cha shilingi 28,000/= kwa kila shina moja la mmea wa Iliki, bila ya masharti au kigezo kingine chochote mahsusi kutumika, lengo likiwa ni kuharakisha uhamishaji wananchi na uwekaji wa mipaka rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2002 hadi 2008 wananchi 1,128 waliokuwa na mazao ndani ya msitu walilipwa stahiki zao zenye jumla ya shilingi 1,633,893,595.85. Malipo hayo yalitokana na ufadhili wa Benki ya Dunia ambayo ilitoa jumla ya shilingi 1,238,653,060.85 na vyanzo vingine mbalimbali ambavyo vililipa jumla ya shilingi 395,240,535/=. Tofauti na zoezi la kwanza ulipaji katika zoezi hili ulizingatia masharti ya Benki ya Dunia, Sheria ya Ardhi 1998 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999 pamoja na miongozo mingine ya fidia za mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, thamani ya fidia iliwekwa katika viwango tofauti kulingana na sifa za ukomavu wa mazao, umri wa miche, utunzaji wa shamba na idadi ya mazao. Kulingana na vigezo hivyo, viwango vilivyokubalika vilikuwa shilingi 102/=, shilingi 204/=, shilingi 2,040/=, shilingi 3,315/= na shilingi 5,100/= kwa shina. Tathmini kwa mazao ya wananchi yaliyomo ndani ya msitu ilifanyika kwa ushiriki wa karibu wa timu huru za Wakaguzi kutoa Wizara, Taasisi za Umma na Taasisi Binafsi, Mashirika ya Kimataifa na wananchi wenyewe. Aidha, kiwango cha chini kilichofidiwa ni shilingi 3,315/= na kiwango cha juu ni shilingi 22,832,172.32 kwa mkulima mmoja. Nakala ya nyaraka za tathmini na malipo yaliyofanyika zinapatikana katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Muheza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia ya ardhi, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Mkoa wa Tanga iliahidi kuwapatia wananchi ardhi mbadala ambapo hadi sasa jumla ya maeneo 408 yenye ukubwa wa hekta tatu kila moja yamekwishapimwa na kwamba zoezi hilo la upimaji linaendela hatua kwa hatua kilingana na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya gharama za upimaji. Namshauri Mheshimiwa Mbunge awasiliane na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ili kufahamu zaidi hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa zoezi la ugawaji wa ardhi na namna linavyoendelea.