Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 59 Works, Transport and Communication Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 494 2021-06-25

Name

Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Primary Question

MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Kwa muda mrefu Jimbo la Arusha Mjini limekuwa likisumbuliwa na changamoto ya mafuriko kwenye Kata ya Sembetini, Levolosi, Osunyai, Sekei, Unga Ltd, Sakina, Baraa na Olerian yanayosababishwa na miundombinu mibovu ya barabara ya Sakina – Tengeru na Airport – Soko la Kilombero?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya Sakina – Tengeru umehusisha upanuzi wa barabara iliyokuwepo kutoka njia mbili kwenda njia nne na katika mito yote yamejengwa madaraja makubwa yanayopokea maji kutoka mlima Meru na kupeleka katika makorongo makubwa ya asili. Hivyo, mafuriko yanayotokea katika maeneo husika hayasababishwi na miundombinu mibovu ya barabara ya Sakina – Tengeru.

Mheshimiwa Spika, tatizo la mafuriko katika maeneo yaliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge yanasababishwa na sababu zifuatazo: -

(i) Mabadiliko ya kimazingira yanayohusiana na ujenzi uliofanyika katika maeneo ya juu na hivyo kuongeza maji katika maeneo ya juu kuelekea kwenye maeneo ya chini;

(ii) Ujenzi holela katika mikondo asili ya maji na kupunguza upana wa njia ya maji; na

(iii) Utupaji taka ngumu kwenye mitaro ya maji na kusababisha kuziba kwa makalvati na kupelekea maji kupita juu ya barabara na kusambaa katika maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na tatizo la mafuriko, Serikali kupitia Tanzania Strategic Cities Project unaotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha, inafanya utafiti wa kina ili kuona ni jinsi gani mafuriko haya yanaweza kuzuiwa kwa kujenga miundombinu ya kukusanya maji yote yanayotoka Mlima Meru na kuleta madhara ya mafuriko. Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya Cheil Engineering ya Korea Kusini anaendelea na utafiti huo, ahsante.