Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Primary Question

MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:- Miongoni mwa Mahakama za Mwanzo ambazo Serikali iliahidi na kuamua kuzijenga ni pamoja na Mahakama ya Mwanzo Mkomazi. Je, ni lini Mahakama ya Mwanzo Mkomazi itajengwa?

Supplementary Question 1

MHE. STEPHEN HILARY NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza kwa ruksa yako naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kunipa shilingi bilioni moja kwa ajili ya vituo viwili vya Afya, Kata ya Mkumbala na Kituo cha Afya Bungu, Mungu ambariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwaka 2012 Mahakama hii iliahidiwa kwamba itajengwa, mwaka 2014 iliahidiwa itajengwa, mwaka 2015 iliahidiwa itajengwa, sasa nataka tamko la Serikali mwaka 2020 ni kweli kituo hiki au Mahakama hii ya Mwanzo itajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ilijenga Mahakama ya Mwanzo ya kisasa zaidi pale Magoma katika Tarafa ya Magoma, na nikajitahidi nikakarabati Mahakama moja katika Tarafa ya Bungu, lakini Mahakama hizi mpaka zaidi ya miaka saba hazijafunguliwa.
Sasa naomba Serikali iniambie ni nini sababu zinazuia Mahakama hizi zisifunguliwe wakati wananchi wanapata shida sana kutolewa umbali wa kilometa 30 kwenda kufuata Mahakama sehemu nyingine? Ahsante sana.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kuanza kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kuhakikisha kwamba huduma hii ya Mahakama inawafikia wananchi wake kwa ukaribu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lakle la kwanza la nyongeza, nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa mwaka wa fedha wa mwaka 2019/2020 Mahakama hii ya Mwanzo itajengwa na nimuondolee hofu kwa sababu hivi sasa, kupitia Wizara tunashirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi na Baraza la Nyumba la Taifa na sasa tuna mfumo mzuri wa ujengaji wa Mahakama kutumia teknolojia ya moladi ambayo inafanya kazi kukamilika kwa muda mfupi na ukuta kuwa imara zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hiyo itafanyika na hivi sasa navyozungumza. Tunayo miradi takribani 39 nchi nzima ambayo inatekelezwa na kufikia mwaka wa fedha 2018/2019 tutakuwa tumekamisha Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mkoa takribani 70. Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ni ahadi ya Serikali na jambo hili litatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu Mahakama ya Magoma ambayo tayari ukarabati na ujenzi umefanyika lakini mpaka leo haijafunguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumuagiza Mtendaji wa Mahakama wa Mkoa wa Tanga kuhakikisha kwamba anafuatilia na kutupatia taarifa na sisi tutakwenda kufuatilia na tutampatia majibu Mheshimiwa Mbunge, lakini nataka nimuahidi tu kwamba kama hakuna vikwazo vingine vyovyote basi tutahakikisha kwamba Mahakama hii inafanya kazi na wananchi wa Tarafa ya Magoma wanapata huduma hii stahiki.