Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Juma Kombo Hamad

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wingwi

Primary Question

MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:- Kumekuwa na mgongano mkubwa wa Katiba kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko la Kero za Muungano na mgongano wa kimamlaka baina ya Serikali mbili:- Je, ni lini Serikali ya Muungano italeta mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto zilizomo ndani ya Katiba hizo?

Supplementary Question 1

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kwa ruhusa yako sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika siku za karibuni kupitia Vyombo vya Habari tulimuona Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akitoa maagizo kwa Waziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kikatiba, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana Mamlaka Kikatiba kutoa maagizo kwa Waziri kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika level ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tunashuhudia Mawaziri wakizungumzia masuala mbalimbali ambayo hayahusu Muungano, yakiwemo masuala ya kilimo, masuala ya biashara na shughuli nyingine. Je, Mheshimiwa Waziri anataka kudhihirisha sasa au anataka kutuambia kwamba, Tanzania Bara itaendelea kula kwa niaba ya Zanzibar hadi lini? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)

Name

Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema amesoma katika magazeti na magazeti siyo njia au sababu ya kueleza mambo hayo, ndio. Yeyote anayetumia magazeti hajui mamlaka na nafasi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maagizo ya Serikali yanatolewa kwa nyaraka, kwa barua. Sijawahi kupokea maagizo kwa gazeti au sms, napokea maagizo kwa barua au waraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo mamlaka yote ya mambo yote yanayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama nchi huru. Kwa hiyo, katika mambo yote yanayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mkuu wa nchi ni mmoja tu, ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Yeye peke yake ndiye Amiri Jeshi, hakuna mtu mwingine yeyote wa kuyaamuru Majeshi ya Tanzania isipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa sababu yeye peke yake ndiye Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu na Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwenye heshima na hadhi ya Urais kwa mambo yote yasiyokuwa ya Muungano yanayoihusu Zanzibar, lakini pia ni Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi yake hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia usawa wa wabia wa Muungano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atatoka Tanzania Bara, Makamu atatoka Tanzania Zanzibar na ikiwa Rais atatoka Tanzania Zanzibar Makamu atatoka Tanzania Bara. Huo ndio usawa uliowekwa ndani ya Katiba na Ibara iko wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo basi, anayeiwakilisha nchi hii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mambo yote ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wetu ni wa aina yake ya kipekee na mara nyingi umewafanya watu wasielewe, ndiyo maana katika mambo yote duniani inayoonekana ni Jamhuri ya Muungano, lakini ndani ya Tanzania yenyewe kuna pande mbili, Tanzania Bara ambayo mambo yake yanasimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tanzania Zanzibar ambayo mambo yake yanasimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ndio maana nchi hii ina Katiba mbili, Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. (Makofi)

Name

Rukia Ahmed Kassim

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:- Kumekuwa na mgongano mkubwa wa Katiba kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko la Kero za Muungano na mgongano wa kimamlaka baina ya Serikali mbili:- Je, ni lini Serikali ya Muungano italeta mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto zilizomo ndani ya Katiba hizo?

Supplementary Question 2

MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, aliyekuwa Waziri katika Wizara ambayo ilikuwa ikishughulikia mambo ya Muungano, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye sasa hivi ni Makamu wa Rais, aliwahi kutuambia kwamba kuna kikao ambacho kilikaa kati ya pande hizi mbili, Wajumbe kutoka Zanzibar na Wajumbe kutoka Tanzania Bara waliokuwa wakizungumzia kuhusu kero ambazo zinahusu mambo ya Muungano. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutuambia ni Wajumbe gani hao ambao walikuwa wakikutana kuzungumzia kero hizi?

Name

January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma kumekuwa na taratibu mbalimbali za kushughulikia changamoto za Muungano hatuziiti kero ni changamoto za Muungano. Mwaka 2006 ukaanzishwa utaratibu mpya wa kikao cha Kamati ya Pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Kikao kile cha Kamati ya pamoja kilikuwa kinaongozwa na Makamu wa Rais pamoja na Watendaji Wakuu wa Serikali za pande mbili. Maana ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar au Waziri Kiongozi kabla ya mabadiliko ya Katiba ya 2010.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao kile kinajumuisha Mawaziri wote ni Mabaraza ya Mawaziri ya pande zote mbili za Muungano wetu. Kwa taarifa tu kikao cha mwisho kilikutana tarehe 13 Januari, 2017 kule Zanzibar ambapo kilijumuisha Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao hicho kinatanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makatibu Wakuu wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kabla ya hapo kinatanguliwa na kikao cha wataalam wa masuala husika yatakayozungumzwa katika kikao hicho kwa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kikao hiki na utaratibu huu ni mkubwa, ni mzuri na umetusaidia sana kupunguza changamoto za Muungano. (Makofi)

Name

Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Primary Question

MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:- Kumekuwa na mgongano mkubwa wa Katiba kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko la Kero za Muungano na mgongano wa kimamlaka baina ya Serikali mbili:- Je, ni lini Serikali ya Muungano italeta mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto zilizomo ndani ya Katiba hizo?

Supplementary Question 3

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sheria Namba 4 ya mwaka 1992 ya Jamhuri ya Muungano inampa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kimikoa, Kiwilaya na kadhalika kwa kadri anavyoona. Pia Sheria Namba 2 (E) ya mwaka 1997 ya Katiba ya Zanzibar, pia inampa mamlaka Rais wa Zanzibar, kuvigawa visiwa vya Zanzibar Kimikoa, Kiwilaya kwa kadri anavyoona. Je, ni nani aliye na mamlaka zaidi juu ya Zanzibar. Je huu siyo mgongano wa Kikatiba? (Makofi)

Name

Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yeyote yenye Katiba zaidi ya moja, kama ilivyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tofauti na India ambayo ni Muungano una Katiba moja. Tanzania ni sawa sawa na Ethiopia yenye Katiba 13.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ujue ni jinsi gani unatafsiri na kuisoma Katiba ziko njia kuu tatu; unaangalia Originalism, Textualism na Purposive. Kwa maana hiyo haya ni mambo ambayo pia yamerejewa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. Kwa anayeangalia utaratibu wa kuziangalia Katiba mbili zinavyotekelezwa na zinapoonekana zina mgongano kazi ya kwanza ya Mahakama ni kufanya harmonization of interpretation. Hiyo nikusaidie nenda ukasome kesi ya Attorney General versus Butambala iliyoamuliwa na Mheshimiwa Jaji Samatta wa Mahakama ya Rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, ukitumia purposive approach hakuna mgongano kati ya Ibara hizo mbili. Maana yake Mamlaka ya Juu Residuary Power inabaki na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:- Kumekuwa na mgongano mkubwa wa Katiba kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko la Kero za Muungano na mgongano wa kimamlaka baina ya Serikali mbili:- Je, ni lini Serikali ya Muungano italeta mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto zilizomo ndani ya Katiba hizo?

Supplementary Question 4

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na mjomba wangu Profesa Kabudi na timu yake kwenye Wizara ya Katiba na Sheria, itakumbukwa mwaka mmoja na zaidi uliopita niliuliza hapa na kuiomba Wizara itusaidie tufungue jengo la Mahakama ambalo tumeshalijenga, tumelikamilisha ni zuri na la kisasa, nikaahidiwa hapa kwamba Serikali itasaidia kukamilisha utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana, sasa ni mwaka na utaratibu haujakamilika. Sasa kama jambo hili limeshindikana Serikali ituambie ili tubadilishe matumizi tufanye shughuli nyingine kwenye lile jengo la Mahakama ambalo nia yetu ilikuwa ni kusogeza huduma za kimahakama kwa watu wetu.

Name

Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Nape swali hilo nilichukue nilifanyie kazi, kwa sababu amesema ni mwaka mmoja na nusu na mimi leo ni mwezi wangu wa Kumi wa Uwaziri. Naomba anisaidie tuonane nilifuatilie ili tuone jengo hilo linatumika kwa Mahakama.