Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Busanda

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBAaliuliza:- Je ni lini Serikali itapeleka gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Bukoli?

Supplementary Question 1

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa, takwimu zinaonesha kwamba katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Geita kuna changamoto kubwa sana ya vifo vya akinamama wakati wa kujifungua; na kwa sababu hiyo wengi inatokana na kwamba wakati wa kujifungua, pale wanaposhindwa kuwapeleka hospitali ya rufaa ya Mkoa inakuwa ni vigumu kwa sababu hakuna usafiri. Kwa hiyo, ni muhimu sana kituo cha afya cha Bukoli kipatiwe kwa kweli gari la wagonjwa. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuona umuhimu huo wa kupatiwa gari la wagonjwa katika kituo cha afya cha Bukoli? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile sambamba na gari la wagonjwa kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi, hasa katika vituo hivi vya afya ikiwemo cha Bukoli pamoja na kituo cha Katoro, Chikobe, vyote hivyo. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha kwamba inapunguza tatizo hili?

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri yale ya awali. Nafahamu changamoto kubwa inayolikabili Jimbo la Busanda hali kadhalika Mkoa mzima wa Geita.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ombi lake tunalichukua, pale inapopatikana fursa tutaangalia nini cha kufanya kwa ajili ya kuweza kulishughulikia eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa ajili ya kupunguza hili tatizo la vifo vya akinamama na watoto; na hasa tuna kesi kubwa sasa hivi ya akinamama wengi kupata fistula kwa sababu ya kuwapeleka maeneo mbalimbali kwa kuwa referral system inapatikana mbali; ndiyo maana tumejielekeza katika kuimarisha vituo hivi vya afya.
Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali yetu imejipanga; na mpango mkakati wa hivi sasa ni kwamba tunatarajia kukamilisha vituo vya afya 350 kwa lengo kubwa la kupunguza tatizo hili. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo; hata kule sehemu ya Songambele na sehemu ya Mkoka jambo hili lipo katika kipaumbele chetu kuhakikisha wananchi wanapata huduma vizuri.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Jafo; lakini nimesimama kwa sababu ya hoja ya Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, kwamba Geita ni moja ya mikoa yenye idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi. Kwa hiyo nakubaliana, nataka tu kuongeza majibu ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi au ukarabati wa vituo vya afya tunajikita pia katika kuboresha huduma ambazo akinamama wajawazito wanapatiwa. Kwa mfano tumeifanya tathmini, wanawake ambao wanakwenda katika vituo vya kutoa huduma za afya hawapimi, hawafanyiwi vipimo muhimu; kwa mfano wingi wa damu, labda mkojo na shinikizo la damu. Hivi leo Mheshimiwa Makamu wa Rais anazindua kampeni ya Kitaifa ya kuhimiza uwajibikaji katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi; na kipaumbele tumeweka Geita, Kigoma, Kagera na mikoa yote ya Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la kupunguza vifo halitamalizika kwa kujenga majengo tu, pia tunataka kusimamia ubora wa huduma anazopewa mama mjamzito pamoja na vitoto vichanga. Tunasema jiongeze tuwavushe salama.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)