Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Juliana Didas Masaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JULIANA D. MASABURI Aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Kiwanda cha MUTEX kilichopo Wilaya ya Musoma Mjini kinafunguliwa na kurudisha ajira kwa vijana wa Mkoa wa Mara?

Supplementary Question 1

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kuwashukuru Serikali kwa majibu yao mazuri, lakini je, Serikali imejipangaje hasa kuwachukulia hatua hawa wawekezaji ambao wanapewa hivi viwanda na wanavitelekeza na wanaenda mbali zaidi wanavichukulia mikopo na kuviacha hapo? Serikali imejipangaje kisheria kuwabana aina hii ya wawekezaji? (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza kuchukua hatua na ndiyo maana tumeona katika viwanda vile 68 ambavyo vilikuwa haviendelezwi tayari hivi 20 vimesharejeshwa Serikalini. Lakini pia tunaendelea kuvitathimini na hivyo vingine.

Kwa hiyo niwahakikishie watanzania na Mheshimiwa Juliana Masaburi na Wabunge wote kwamba Serikali ipo makini kuona sasa wawekezaji wote watakaoingia mikataba ya kuviendeleza viwanda katika sekta zote pale ambapo watakiuka masharti ya mikataba tutakayoingia nayo sheria zitachukuliwa na hatua mahsusi ikiwemo kuwanyang’anya viwanda hivyo vitachukuliwa ili kuhakikisha sasa tunapata wawekezaji makini ambao kweli wataleta tija katika uendelezaji wa sekta ya viwanda nchini. Ahsante sana.

Name

Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Primary Question

MHE. JULIANA D. MASABURI Aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Kiwanda cha MUTEX kilichopo Wilaya ya Musoma Mjini kinafunguliwa na kurudisha ajira kwa vijana wa Mkoa wa Mara?

Supplementary Question 2

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kile Kiwanda cha MUTEX, Mheshimiwa Naibu Waziri amekubali kwamba aliyekuwa anakiendesha alinyang’anywa kwa sababu alikuwa hakiendeshi kwa tija na sasa yapata ni miaka mitatu kile kiwanda kimesimama.

Je, ni kwanini basi hata huyo, huyo asingepewa akakiendeleza kuliko ambavyo sasa kile kiwanda kimesimama na watu wanakosa ajira?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa ubinafsishaji wa viwanda hivi kulikuwa na mikataba na katika mikataba hiyo kulikuwa na vigezo maalum na ndiyo maana tuliona sasa katika kuvunjwa kwa mikataba hiyo ndiyo maana imechukua muda mrefu ili kujihakikishia, ilikuwa mojawapo ni kumshawishi yule aliyepo kuona kama anaweza kuendeleza, lakini baada ya kujiridhisha kwamba ameshindwa ndiyo maana vimerejeshwa Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kupata wawekezaji mahiri ambao kweli wapo makini na watawekeza kwa tija. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Vedastus Manyinyi, kwanza tuna dhamira ya dhati ya kupata wawekezaji sasa mahiri ambao watawekeza katika viwanda hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tusingependa kuwaonea au kumpa mtu kwa upendeleo. Kwa hiyo tufuate utaratibu ambao utatangazwa na baadaye wawekezaji wengi watapatikana ambao watawekeza kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Name

Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Primary Question

MHE. JULIANA D. MASABURI Aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Kiwanda cha MUTEX kilichopo Wilaya ya Musoma Mjini kinafunguliwa na kurudisha ajira kwa vijana wa Mkoa wa Mara?

Supplementary Question 3

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala hili la viwanda tutakumbuka pia kulikuwa na viwanda vingi vya korosho vilivyopo maeneo ya kusini, Mtwara, Lindi, Masasi, Nachingwea na maeneo mengi. Serikali imesema imeamua kubinafsisha na kuna vingine vilikuwa vinatumika kama maghala ya kuhifadhia mazao badala ya kuviendeleza kuwa viwanda vya korosho ili kuweza kutoa ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tusikie commitment ya Serikali, ni lini zoezi hili wanalolifanya litakamilika ili kuweza kuvirejesha hivi viwanda, watu muda sahihi wa kukamilisha? (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil David Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi ni kweli kuna viwanda vingi ambavyo vimekuwa havifanyi kazi baada ya wawekezaji wengi kuvitelekeza au kutokuviendeleza au kuendeleza kwa kusuasua au kubadilisha matumizi ya viwanda hivyo ikiwemo wengine waling’oa hata mitambo ya viwanda hivyo na kubadilisha kuwa ma-godown.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge watuelewe kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuona sasa tunapata wawekezaji mahiri. Kwa hiyo hata viwanda vya korosho ambavyo vilikuwa vimetelekezwa kama nilivyosema tunaenda kutangaza utaratibu maalum wa kuweza kuwapata wawekezaji kwa njia ya wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya hapo naamini wengi ambao wana nia ya kuwekeza katika viwanda hivi watapatikana na hakika tunaamini viwanda hivi vitaenda kufanya kazi kwa tija kama ambavyo Serikali imekusudia. Nakushukuru sana.