Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 14 Sitting 1 Good Governance Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) 6 2024-01-30

Name

Amina Daud Hassan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMINA DAUD HASSAN aliuliza:-

Je, Serikali inatambua uwepo wa rushwa kwa wanafunzi katika vyuo vyetu hapa Nchini?

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Daud Hassan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa rushwa katika sekta ya elimu kwa kuzingatia matokeo ya utafiti wa Hali ya Utawala na Rushwa wa Mwaka 2020. Rushwa ya Ngono ni kosa la jinai kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329. Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuzuia rushwa katika vyuo vyote nchini kupitia tafiti na mikakati ya kuzuia rushwa ikiwemo programu mbalimbali za kuelimishaji umma na vilabu vya wapinga rushwa shuleni na vyuoni.

Mheshimiwa Spika, mathalani mwaka 2019, Serikali ilishirikiana na wadau kuendesha kampeni ya Vunja Ukimya kwa ajili ya kupiga vita rushwa hususani rushwa ya ngono kwa kuhamasisha jamii isikae kimya dhidi ya vitendo hivyo. Katika kipindi cha mwaka 2020 - 2023, taarifa 11 za malalamiko ya vitendo vya rushwa ya ngono katika vyuo vyetu zilipokelewa na majalada tisa ya uchunguzi yalianzishwa; ambapo majalada mawili yamefungwa baada ya kukosekana ushahidi. Jalada moja limepata kibali cha kumfikisha mtuhumiwa mahakamani na majalada mawili yamependekeza watuhumiwa wake wachukuliwe hatua za kinidhamu na jalada moja, kesi imeshindwa mahakamani. Majalada manne yanaendelea na uchunguzi.