Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 17 | Sitting 1 | Finance and Planning | Wizara ya Fedha | 16 | 2024-10-29 |
Name
Maida Hamad Abdallah
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza: -
Je, nini mkakati wa Serikali kumaliza tatizo la wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi nchini?
Name
Hamad Hassan Chande
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, TRA imekuwa ikijikita kwenye matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuboresha ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha ulipaji kodi unafanyika kwa uwazi na usahihi. Matumizi ya TEHAMA yameleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa kodi nchini hasa kupitia zana kama vile Electronic Fiscal Devices na mifumo mingine ya kidijiti kama vile E-filing, EFDMS, ITAX na TANCIS. Matumizi ya TEHAMA katika mifumo ya kodi yameimarisha uwajibikaji, uwazi na kuongeza ufanisi wa TRA katika ukusanyaji wa mapato. Hii imepunguza ukwepaji kodi, kuimarisha nidhamu ya walipa kodi na kurahisisha shughuli za biashara nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendesha kampeni za uelimishaji ili kuwawezesha wafanyabiashara kuelewa umuhimu wa kulipa kodi na mchango wake katika maendeleo ya Taifa letu. Elimu hii hutolewa kupitia njia mbalimbali zikiwemo semina, redio, televisheni, elimu ya mlango kwa mlango, mikutano ya wadau, pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile facebook, instagram, twitter (X) na whatsapp. Lengo ni kuhakikisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanapata uelewa wa kutosha kuhusu haki na wajibu wao wa kulipa kodi.
Mheshimiwa Spika, vilevile sheria za kodi zimeimarishwa ili kuhakikisha kuwa hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wale wanaokwepa kodi. Adhabu hizi ni pamoja na faini kubwa, kufungwa kwa biashara au kufunguliwa mashtaka ya jinai kwa wafanyabiashara watakaobainika kukwepa kodi. Ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sheria za kodi, TRA pia inafuatilia kwa karibu utendaji wa Maafisa wake ili kuondoa uwezekano wa rushwa au upendeleo unaoweza kusababisha ukwepaji wa kodi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, Serikali pia imeboresha mfumo wa kodi ili kuhakikisha viwango vya kodi vinawiana na hali halisi ya biashara, hivyo kuwaondolea wafanyabiashara mzigo wa kodi usio wa lazima na kuwatia moyo kulipa kodi kwa hiari bila kujihisi wanaonewa. Uboreshaji huu unalenga kuunda mazingira rafiki ya kufanya biashara bila kuathiri juhudi za Serikali kuongeza mapato, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved