Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 16 Sitting 7 Education, Science,Technology and Vocational Training, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia 120 2024-09-04

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-

Je, kuna vituo vingapi vinavyotoa elimu ya watu wazima nchini na ni watu wazima wangapi wanapata elimu hiyo ikiwemo wanawake?

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuimarisha elimu ya watu wazima kupitia programu mbalimbali zilizo chini ya Sekta Ndogo ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya Mfumo Rasmi. Kulingana na Taarifa ya Tathmini ya Sekta ya Elimu (ESA 2024), katika Programu ya Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA) mwaka 2023, jumla ya wanakisomo 97,217 wamenufaika katika vituo 1,851 ambapo wanaume ni 39,789 na wanawake ni 57,428.

Mheshimwa Naibu Spika, kupitia programu ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) mwaka 2023, jumla ya wanafunzi 57,843 wamenufaika katika vituo 2,557 ambapo wavulana ni 32,141 na wasichana ni 25,702.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika programu ya Mpango wa Elimu Changamani Baada ya Elimu ya Msingi (Integrated Post Primary Education), jumla ya wanafunzi 9,368 wamenufaika katika vituo 89 ambapo wanaume ni 5,036 na wanawake ni 4,332. Aidha, katika programu ya Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Shule (Integrated Programme for Out of School Adolescents), jumla ya vijana 42,183 wamenufaika kupitia katika vituo 85, ambapo wanaume ni 20,195 na wanawake ni 21,988.

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika, katika programu ya elimu ya sekondari kwa njia mbadala, wanafunzi 11,721 ikijumuisha wavulana 5,529 na wasichana 6,192 walidahiliwa kwa mwaka wa masomo wa 2023, ikitolewa katika vituo 777; vituo vya Serikali ni 160 na vituo vya wadau binafsi 617. Ninakushukuru.