Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Shally Josepha Raymond
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:- Je, kuna vituo vingapi vinavyotoa elimu ya watu wazima nchini na ni watu wazima wangapi wanapata elimu hiyo ikiwemo wanawake?
Supplementary Question 1
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Pamoja na hayo, kwa kuwa hadi sasa kuna vijana wanaomaliza darasa la saba hawajui kusoma na kuandika; na kwa kuwa hilo ni takwa maalum katika nchi yetu. Je, Serikali iko tayari sasa kurejesha ule mpango wa kutoa elimu na madarasa ya jioni kwa watu wazima ambao hawakufanikiwa kujifunza kusoma na kuandika katika shule ya msingi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, sambamba na elimu hiyo ya K.K.K, je, Serikali iko tayari kutoa mafunzo ya stadi za elimu ikiwepo kupika, kushona, kupasi kwa akina mama saa za jioni katika kata zetu na vijiji vyetu kupitia kwa Maofisa Maendeleo ya Jamii?
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya mama yangu, Mheshimiwa Shally Raymond kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Shally Raymond kwa maswali yake na vilevile kwa juhudi zake kwa kuwasemea akina mama wa Kilimanjaro pamoja na Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge anauliza kuhusiana na suala la maboresho ya elimu hii ya watu wazima katika kata zetu, ninaomba kwanza nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu. Katika matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi, eneo hili vilevile limeangaliwa, la kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa za sensa za mwaka 2022 inaonyesha kwamba, sasa hivi katika nchi yetu 17% ya Watanzania hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Asilimia hii imeshuka kutoka 22% ya mwaka 2012. Kwa hiyo, imeshuka kwa kiasi fulani, lakini bado tunasema asilimia hii ni kubwa kulingana na maisha ya sasa hivi na karne ya sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Katika maboresho ya Sera ya Elimu pamoja na mitaala tuliyofanya mwaka jana (2023), jambo hili limeingizwa. Hivi sasa katika halmashauri zetu zote tumeanzisha idara pamoja na vitengo vya elimu ya watu wazima, kwa maana ya elimu ya msingi na sekondari kwa kuteua Maafisa Elimu ya Watu Wazima ngazi ya msingi na Maafisa Elimu ya Watu Wazima ngazi ya sekondari. Sasa tunakwenda kuanzisha madarasa yale katika kata zetu na vijiji vyetu kule kote na hawa maafisa wetu ndio watakaokuwa wasimamizi wakuu katika eneo hilo. (Makofi)
Katika eneo la pili analolizungumza, kwamba sasa tuanzishe programu mbalimbali wa ajili ya akina mama, nimwondoe wasiwasi, Serikali yetu inatekeleza programu inayoitwa integrated approach. Katika programu hii ina elimu changamani ambapo stadi hii za K.K.K zinafundishwa pia zinachanganywa na stadi nyingine za ujasiriamali, stadi za maisha, upishi na masuala ya uhifadhi wa mazingira na maeneo mengine. Kwa hiyo, tayari Serikali inalifanyia kazi jambo hili na tunaendelea kulifanyia kazi kwa karibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved