Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 16 Lands, Housing and Human Settlement Development Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi 134 2021-04-23

Name

Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Primary Question

MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali wa kupima na kurasimisha maeneo yanayozunguka Mamlaka za Miji ili kuepuka kuendelea kuwa na makazi holela pamoja na kuweza kupeleka huduma za dharura kama ambulance na zimamoto?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Sura ya 355 Fungu la 7(1), mamlaka za upangaji ambazo ni Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya nchini zina wajibu wa kupanga, kupima na kurasimisha maeneo yote yaliyo chini ya mamlaka zao. Pamoja na wajibu huo wa kisheria kwa mamlaka za upangaji, bado kasi ya upangaji na upimaji ardhi nchini imekuwa sio ya kuridhisha. Hivyo, Wizara yangu imeendelea kushirikiana na mamlaka za upangaji pamoja na taasisi binafsi katika utekelezaji wa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kasi ndogo ya upangaji na upimaji, katika kipindi cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/2021 Wizara yangu imeziwezesha mamlaka za upangaji 21 nchini kupanga na kupima viwanja vipatavyo 56,792 kwa gharama ya shilingi billioni 3.5. Lengo la kutoa fedha hizo ni kuziwezesha mamlaka za upangaji kuongeza wigo wa upatikanaji wa viwanja vilivyopangwa na kupimwa katika maeneo yao na kurasimisha makazi mijini. Pamoja na kupatiwa fedha hizo, jumla ya makazi yapatayo 735,047 yamerasimishwa nchini katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Machi, 2021 katika Halmashauri 104 nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo yote yaliyopangwa, kupimwa na kurasimishwa, utengaji wa maeneo kwa ajili ya matumizi ya umma umezingatiwa ili kuruhusu utoaji wa huduma za kijamii. Natoa rai kwa mamlaka za upangaji nchini kuhakikisha zinatenga fedha katika bajeti zao kila mwaka ili kuharakisha upangaji, upimaji ardhi na urasimishaji wa makazi katika maeneo yao. Ahsante.