Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 10 | Sitting 4 | Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives | Waziri wa Mifugo na Uvuvi | 67 | 2023-02-03 |
Name
Shally Josepha Raymond
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -
Je, ni kiasi gani cha ngozi kinazalishwa kwa mwaka mzima na kutumika nchini na kiasi gani ghafi kinauzwa nje ya nchi?
Name
Abdallah Hamis Ulega
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inazalisha wastani wa vipande milioni 13.6 vya ngozi kwa mwaka. Kati ya vipande hivyo, milioni 4.2 ni vya ng’ombe, vipande milioni 6.9 ni vya mbuzi na vipande milioni 2.5 ni vya kondoo. Kwa sasa, tunavyo viwanda vitatu vinavyofanya kazi ya usindikaji wa ngozi katika hatua ya kati (wet blue) na hatua ya mwisho (finished leather).
Mheshimiwa Naibu Spika, ngozi zinazosindikwa katika hatua ya kati ni vipande 51,866 vya ngozi ya ng’ombe na vipande 262,229 vya mbuzi na kondoo. Usindikaji hadi hatua ya mwisho ni vipande 145,000 vya ngozi ya ng’ombe na vipande 259,000 vya ngozi ya mbuzi na kondoo. Pia, kuna wasindikaji wadogo wanaosindika na kutengeneza bidhaa za ngozi maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inauza nje ya nchi ngozi ghafi na iliyosindikwa hatua ya awali, wastani wa vipande 1,630,740 vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.5 kwa mwaka. Ngozi hiyo, inauzwa katika nchi za Nigeria, Afrika ya Kusini, Ghana, Togo, Pakistan, Marekani, Italia, Dubai na China, ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved