Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Shally Josepha Raymond
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: - Je, ni kiasi gani cha ngozi kinazalishwa kwa mwaka mzima na kutumika nchini na kiasi gani ghafi kinauzwa nje ya nchi?
Supplementary Question 1
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, nchi yetu inauza ngozi ya bilioni 10 tu kwa mwaka, lakini nchi hii-hii ndiyo ambayo imebarikiwa kuwa na mifugo mingi zaidi.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuongeza uzalishaji huo kwenye hivyo vituo viwili ambavyo vina-process mpaka mwisho ikiwepo Himo Tanneries na Moshi Leather Industries ili waweze kukidhi uhitaji wa nchi hii baada ya kufunguliwa kiwanda cha uzalishaji wa Kilimanjaro International Leather Industries?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ina mkakati gani kutoa elimu kwa wananchi wake ili kuhakikisha kwamba, mifugo inatoa ngozi bora na salama katika kipindi chote cha mwaka, ili kutoa ajira zaidi kwa vijana, wakiwemo vijana wa Kilimanjaro? (Makofi)
Name
Abdallah Hamis Ulega
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli lengo letu kama Serikali ni kuona uzalishaji kwenye viwanda vyetu vya ndani unaongezeka, jitihada kadhaa zinafanywa, ikiwemo kuondoa changamoto na kuboresha mazingira ya biashara. Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kushughulikia changamoto hizo ikiwa ni pamoja na ile ya kuondoa tozo na kodi mbalimbali zenye kuweka mkwamo wa upatikanaji wa malighafi na ushindani kwenye biashara. Baada ya kuyafanya haya tunayo imani kuwa, viwanda vyetu sasa vitapokea malighafi nyingi kutoka kwa wazalishaji ili kuviwezesha kufanyakazi yake kwa ufasaha zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili; ni mkakati gani juu ya elimu ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetenga fedha, mwaka huu tumetenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu kwa wachunaji wa ngozi, lakini pia vilevile kununua vifaa kama computers, ili tuweze kuwa na record ya uzalishaji sahihi wa ngozi na hatimae kuwawezesha kuwaingiza katika masoko ikiwemo viwanda vyetu ambavyo vinazalisha hapa nchini, ambavyo tayari Mheshimiwa Shally Raymond ameshavitaja. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved