Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mohammed Said Issa

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Konde

Primary Question

Manufaa yatokanayo na kero za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza:- Je, kero 11 za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi zimeleta manufaa kiasi gani katika utekelezaji kwa pande zote mbili?

Supplementary Question 1

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; pamoja na kutatua kero hizi, kero hizi ni kero ambazo zimeonekana kwa utendaji wa Serikali. Je, Serikali sasa iko tayari kushirikisha Tume, Kamati za maridhiano zilizoundwa na Marais wetu wawili hawa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na ile iliyoundwa na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; baada ya kutatua kero hizi, je, Serikali itakuwa tayari kutengeneza Mkataba Mpya wa Muungano ambao utashirikisha wadau?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, najibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Said Issa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuasisiwa kwa Muungano huu, baada ya kuona kwamba tumeungana, Serikali zote mbili ziliona kuna haja ya kuunda Kamati ambayo itakuwa inashughulika na kutatua changamoto hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hizi zipo katika ngazi ya Makatibu Wakuu, Wataalam, ipo katika ngazi ya Mawaziri lakini Kamati hii ipo katika ngazi Kuu ambayo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri na Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kamati hii iko strong na inafanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi tumetoka kutoka changamoto zilizokuwepo mpaka leo zimebakia nne, maana yake Kamati imefanya kazi kubwa. Wazo alilolitoa Mheshimiwa Mbunge ni zuri, tunalichukua, tunakwenda kulifanyia kazi kwa sababu Kamati ya Maridhiano kazi yake ni kutuliza amani, kusaidia katika kuleta maelewano na ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, kuhusiana na kuiweka kwenye Mkataba Maalum. Tarehe 6 Desemba, 2022 tulikuwa na kikao cha Kamati yetu ya Maelewano baina ya Tanzania Bara na Zanzibar, hii ya Muungano. Hii hoja iliibuka ya kuiweka kwenye document maalum ya kisheria, tukawapa kazi wataalam wetu, tukawapa kazi Wanasheria wetu waende wakaone namna ya kufanya ili kikao chetu kijacho cha Kamati, watuletee majibu ya kuona namna ambavyo tunaweza tukaingiza kwenye Mkataba ama document maalum ya kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Name

Najma Murtaza Giga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

Manufaa yatokanayo na kero za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza:- Je, kero 11 za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi zimeleta manufaa kiasi gani katika utekelezaji kwa pande zote mbili?

Supplementary Question 2

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali langu la nyongeza ni, je, Serikali ina mikakati ipi ya kuweza kudhibiti madhara ambayo yanaweza kutokea kwa changamoto ambazo hazijafanyiwa kazi?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Najma Giga wa Murtaza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo tunakwenda kulifanya kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba tunazo Kamati zetu za Maelewano ambazo huwa tunakaa kwa ajili ya kutatua changamoto hizi na vikao bado vinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba Kamati hii iko makini na inafanya kazi kwa uangalifu kwa mujibu wa taratibu zote. Tutahakikisha kwamba changamoto zote zinatatuka kama ambavyo tumekusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Name

Asya Mwadini Mohammed

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

Manufaa yatokanayo na kero za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza:- Je, kero 11 za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi zimeleta manufaa kiasi gani katika utekelezaji kwa pande zote mbili?

Supplementary Question 3

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; je, Serikali haioni haja ya kuleta taarifa ya mchakato mzima wa utatuzi wa kero za Muungano katika vyombo vya kutunga sheria, Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar na Bunge kwa Jamhuri, ili tuweze kupata picha halisi ya mchakato mzima wa utatuzi wa kero za Muungano?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri wangu kwa majibu mazuri sana kuhusu masuala ya Muungano. Naomba kumpongeza dada yangu Mheshimiwa Asya kwa swali lake zuri. Katika hili, kupitia Kamati ya Utawala na Sheria ambayo ndiyo ina jukumu la kusimamia Wizara yetu ambayo tunaiongoza, mara nyingi inakuwa ikipata taarifa hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni katika vikao vya Kamati, miongoni mwa jambo kubwa ambalo limeletwa katika Kamati ni suala zima la Hoja zote za Muungano zilizofanyiwa kazi na zile ambazo zimebaki. Naomba nimtaarifu Mheshimwa Mbunge kwamba Wizara yetu inaendelea kufanya hivyo na wakati wa vikao mbalimbali tutaendelea kuleta taarifa hizi katika Bunge letu hili hususani katika kipindi cha bajeti. Mheshimiwa Mbunge asiwe na mashaka katika eneo hilo, ahsante.

Name

Christopher Olonyokie Ole-Sendeka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Simanjiro

Primary Question

Manufaa yatokanayo na kero za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza:- Je, kero 11 za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi zimeleta manufaa kiasi gani katika utekelezaji kwa pande zote mbili?

Supplementary Question 4

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali. Kwa kuwa msingi wa kutozwa mara mbili ushuru kwa bidhaa iliyokuwa inatoka Zanzibar inatokana na tofauti ya kodi au ushuru uliokuwa unatozwa kwa upande wa Zanzibar na kwa upande wa Tanzania Bara. Hivyo tofauti ndiyo iliyokuwa inatozwa kama ushuru mara mbili. Kwa kuwa Waziri amesema kwamba wamemaliza na sasa Wazanzibar hawatatozwa ushuru mara mbili, wamesema wameweka mambo vizuri. Je, Waziri anataka kutuambia kwamba sasa ushuru unaotozwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa bidhaa inayoingia na inayoingia Zanzibar sasa ni sawa au kuna utaratibu gani ambao wameweka, kuzuri huko ni kwa namna gani, tueleze?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri aliyoyatoa. Utaratibu ambao Mheshimiwa Naibu Waziri ameusema, ni ule ambao unahusisha tofauti. Unahusisha ile difference ambayo inatokana na viwango vya VAT vinavyotozwa Tanzania Bara na vile vinavyotozwa Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama bidhaa itakuwa imelipiwa kodi Tanzania Bara na ikawa imelipiwa VAT ambayo ni kubwa kuliko ile inayotozwa Zanzibar, kama bidhaa hiyo ni ya Zanzibar, maana yake mfanyabiashara huyo ana-refund. Kama mfanyabiashara amelipa kodi Zanzibar na bidhaa hiyo inatumika Tanzania Bara, maana yake itakapotumika Tanzania Bara, atalipa tofauti ile ili kuweka bidhaa ile iwe sawa, inapotumika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, bidhaa zinapotumika, kodi yake yote iko sawa. Ikitumika kule ambako ilitozwa kidogo, maana yake ikitumika Mainland inatakiwa kulipia ile tofauti ili iwe sawa na iliyoko huku. Ikitumika Zanzibar, maana yake pana¬-refund ili iwe sawa na kodi inayotozwa kwa kule Zanzibar. Kwa maana hiyo, haya tumeshayafanya kwenye vikao na elimu kwa wafanyabiashara inaendelea ili jambo hili lisilete tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitoza ama imepata msamaha Zanzibar, ikiingia bila kulipiwa tofauti huku, maana yake patakuwepo na bidhaa ambayo imeingia ndani ya nchi bila kuwa na kodi stahiki. Tumeshayawianisha yote yale na tumefanya haya kwenye vikao na tunaendelea kuwapa elimu wafanyabiashara. Kimsingi ile haikuwa kutozwa mara mbili kwa sababu ni tofauti. Kutoza mara mbili maana yake ni kutoza kule na utoze na huku. Ile ilishasuluhishwa haipo tena. Kwa maana hiyo sasa hivi tumewianisha ili mtu alipe kodi ambayo inastahili.