Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Mpira wa Ali Hassan Mwinyi - Tabora ili utumike AFCON 2027?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kumekuwa na taarifa mbalimbali kwamba kuna viwanja ambavyo vitakwenda kufanyiwa ukarabati na Serikali. Je, kiwanja cha Ali Hassan Mwinyi kilichopo Tabora ni moja kati ya viwanja vitakavyofanyiwa ukarabati huo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kutokana na Serikali kutokuwa na viwanja vingi vya michezo nchini, Serikali ina mkakati gani wa kukaa na Chama Cha Mapinduzi, kuzungumza nao na kuona namna bora ya kuchukua viwanja hivi vya michezo ambavyo wanavyo ili viweze kwenda Serikalini na viweze kufanyiwa ukarabati ili tuweze kukuza michezo nchini? Nashukuru. (Makofi)

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, kwa sasa Serikali inaweka mkazo kwenye kumalizia miundombinu ya viwanja vya michezo vitakavyotumika kwa ajili ya AFCON 2027. Aidha, kwa kujenga miundombinu mipya kama tunavyofanya kwenye uwanja wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Arusha, ama kukarabati kama ilivyofanyika kwa uwanja wa Amani na uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo ukarabati unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo Serikali inaendelea na mpango wa kukarabati kwa awamu viwanja mbalimbali vilivyopo katika majiji, mikoa, halmashauri na manispaa kote nchini na uwanja wa Ali Hassan Mwinyi utakuwepo katika awamu zitakazofuata. Kwa sasa Serikali imeanza na viwanja vitano ambavyo ni Uhuru uliopo Dar es Salaam, Mkwakwani uliopo Tanga, Jamhuri uliopo Morogoro, Maji Maji uliopo Songea na Sheikh Amir Abed uliopo Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili, mazungumzo kati ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi kuhusiana na kukabidhiwa viwanja vyake ili vifanyiwe ukarabati viweze kutumika katika matukio mbalimbali yanaendelea na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, yanaendelea vizuri na hivi karibuni Serikali itatoa tamko kuhusiana na uwezekano wa Serikali kuvichukua viwanja ambavyo vipo chini ya Chama Cha Mapinduzi na kuvifanyia ukarabati kwa ajili ya matumizi. Ahsante. (Makofi)