Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuimarisha kilimo cha Minazi katika Ukanda wa Pwani ya Tanzania?

Supplementary Question 1

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na juhudi kubwa za Serikali, lakini bado kuna changamoto. Kwa kuwa, zao la nazi ni zao la kiuchumi katika ukanda wa Pwani na Zanzibar, minazi mingi imekuwa ikifa kwa kushambuliwa na magonjwa na hakuna juhudi mbadala. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuinusuru minazi inayokufa na inayoshambuliwa na magonjwa katika ukanda wa Pwani na Zanzibar?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa minazi mingi ni ya muda mrefu na hasa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Pwani, Mtwara, Tanga na Zanzibar na inakufa na hakuna juhudi yoyote ya kuimarisha zao la minazi: Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu katika mashule pamoja na vyombo mbalimbali vya habari ili kuimarisha zao hilo la mnazi? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Kilimo moja ya kazi kubwa tunayoifanya ni kwamba tumeandaa mipango wa muda mfupi, mpango wa kati na mpango wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango ambayo tunaendelea nayo sasa hivi ni kuendelea kufanya tafiti ili kukabiliana na magonjwa. Ndiyo maana ukiona katika jibu la msingi tumepata mbegu mpya ambayo inaweza kukabiliana na magonjwa ya nazi, kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo kwa wakulima wote wa Kanda za Pwani na tutaendelea kutuma wataalamu wetu waendelee kufanya tafiti kukabiliana na hayo magonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, tutaendelea kutoa elimu mashuleni na huo ndiyo mpango tuliokuwanao sasa hivi, isipokuwa tu tutaongeza kasi ili uweze kuanzia level ya shule kwa maana ya wanafunzi mpaka kufika kwa wanakijiji ambao ni wakulima, ahsante.

Name

Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuimarisha kilimo cha Minazi katika Ukanda wa Pwani ya Tanzania?

Supplementary Question 2

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza mara kwa mara hapa Bungeni kuhusu nini mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo katika kuimarisha kilimo cha vanilla ili wakulima wa vanilla wa Mkoa wa Kagera waweze kunufaika na zao hili? Kwa hiyo, ningependa kupata kauli thabiti ya Serikali, ni nini itakwenda kufanya ili kuhakikisha kilimo cha vanilla kinanufaisha wakulima wa Mkoa wa Kagera? Ahsante.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Wizara ya Kilimo sasa hivi tuna mpango wa kuwaita wadau wote wa sekta ya vanilla wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, wakulima pamoja na wafanyabiashara ili tuweze kukaa pamoja na kujadiliana kuona namna bora ambayo tunaweza tukasaidia kukuza kilimo cha vanilla. Miongoni mwa mipango tuliyonayo ni pamoja na kutafuta masoko na kuongeza bei ya vanilla ili wananchi wetu waweze kunufaika zaidi, ahsante. (Makofi)