Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Afya Vwawa?
Supplementary Question 1
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naishukuru Serikali kwa majibu hayo mazuri ambayo imeyatoa, lakini ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 fedha hizi zilikuwa zimetengwa, hasa ningependa kujua nini kimetokea chuo hicho kimeshindwa kuanza kujengwa kwa mwaka huu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, ni aina gani ya mafunzo na katika ngazi gani chuo hiki tarajiwa kinategemea kuyatoa? (Makofi)
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Hasunga kwa kuwa mfuatiliaji mzuri wa ujenzi wa Chuo cha Afya Vwawa, lakini kubwa maswali yake mawili pia la kwanza, kipi kimetokea fedha zilizotengwa 2023/2024 hazijafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kuchelewa kwa kulipwa kwa fidia na hivyo tumeshindwa kuanza ujenzi kwa sababu fidia ilichelewa kulipwa, lakini jambo la pili Mheshimiwa Hasunga ni kwa sababu bado chuo hakijapata hatimiliki na hili nikuombe sana Mheshimiwa Hasunga ukatusaidie pamoja na mamlaka nyingine za Serikali mkoani Songwe na hususani Vwawa kuweza kupata hati ili tuweze sasa kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni muhimu sana kwa sababu tunatumia fedha pia za World Bank...
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tupunguze sauti tafadhali.
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sharti ambalo Benki ya Dunia imetupa ni kutokuanza ujenzi hadi tuwe na hati ya eneo husika kwa ajili ya kujenga chuo. Kwa hiyo naomba sana utusaidie katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lako la pili kozi gani au level gani ya mafunzo ya afya itatolewa, itakuwa ni ngazi ya cheti (certificate) pamoja na diploma. kwa hiyo tutaendelea kufanya kozi ya uuguzi lakini pia tutaongeza na kozi nyingine ambazo ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya ikiwemo wataalamu wa maabara. (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Afya Vwawa?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Hospitali ya Rufaa ya Bugando inazidi kukua siku hadi siku na pale kuna Chuo Kikuu cha Afya na kuna Chuo cha Afya. Je, Serikali ipo tayari sasa kuhamisha Chuo cha Afya katika Manispaa ya Ilemela ambayo imetenga eneo la ekari 20 karibu na hospitali mpya ya wilaya ambayo Serikali imejenga? (Makofi)
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula nimpongeze sana kwa jinsi anavyowapambania wananchi wa Ilemela na ni kweli nataka kukiri kwamba chuo chetu cha afya ambacho kipo katika Hospitali ya Rufaa Bugando kipo ndani ya hospitali, lakini hospitali nayo wana Chuo cha Afya Kikuu, kwa hiyo Wizara tayari ilishaliona hili la kukihamisha Chuo cha Afya cha Mafunzo ya Kati kilichopo Bungando. Kwa hiyo, kwa sababu umekuwa ni Mbunge wa kwanza wa Mkoa wa Mwanza kutupa ofa ya eneo naomba nikuahidi kwamba tutakuja Ilemela ili kujenga Chuo cha Afya Ilemela, tuwaachie Bugando waweze kufanya upanuzi wa majengo. (Makofi)
Name
Tecla Mohamedi Ungele
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Afya Vwawa?
Supplementary Question 3
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ujenzi wa jengo la Chuo cha Uuguzi Nachingwea ulioanza mwaka 2022 ulitarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2022 lakini hadi leo bado haijakamilika, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa chuo kile ili kuongeza idadi ya wauguzi na kupunguza shortage ama upungufu wa wauguzi nchini Tanzania? Ahsante.
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia taarifa zangu kama Nachingwea ipo, kwa kweli Mheshimiwa Tecla amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana wa ujenzi wa Chuo cha Afya Nachingwea, lakini kwa sababu na yeye ni mwanataaluma wa kada ya wauguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukiri ni kweli ujenzi umechelewa, lakini tumepata fedha hizi za Benki ya Dunia na tumeweka katika orodha yetu Nachingwea moja ya majengo ya kumaliza. Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie na mimi tukimaliza Bunge nitafanya ziara Nachingwea kufuatilia ujenzi wa jengo hili ambalo lilikwama kwa muda mrefu. (Makofi)
Name
Cosato David Chumi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Afya Vwawa?
Supplementary Question 4
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Vyuo vingi vya zamani kikiwemo Chuo cha COTC Mafinga miundombinu yake imechakaa sana. Je, Serikali ipo tayari kuwa na mpango maalumu wa kufanya ukarabati mkubwa katika vyuo vya zamani kikiwemo Chuo cha COTC Mafinga?
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Cosato Chumi kwa swali lake la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli majengo au miundombinu ya majengo katika vyuo vyetu vya afya vya mafunzo ya kati yamechakaa na ndiyo maana sasa tumekuja na huu mpango mahususi wa kufanya ukarabati wa majengo katika vyuo vyetu vya afya, lakini naomba niseme tunakwenda awamu kwa awamu. Kwa hiyo, Mafinga nayo tutaifikia na tumeamua kabisa siyo tu tujenge majengo ya hosteli, lakini kubwa tuwe na academic complex, lakini jambo la pili ni kuweka skills lab kwa ajili ya kuongeza ujuzi ili kuweza kuzalisha wanataaluma wa kada za kati za afya wenye uwezo, ujuzi na stadi zinazohitajika katika utoaji wa huduma za afya kwa sasa hivi. (Makofi)
Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Afya Vwawa?
Supplementary Question 5
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inatambua vipi mchango wa wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakijenga majengo katika Wizara ya Afya kwa mfano katika Mkoa wetu wa Iringa tunaye mdau ambaye ni Salim Asas - MNEC amejenga jengo la mama na mtoto, amejenga jengo la ICU VIP, amejenga jengo la damu salama na kajenga karakana ya viungo bandia na majengo mengine katika wilaya na vituo vyetu vya afya. (Makofi)
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati kwa kufuatilia masuala ya afya katika mkoa wa Iringa, lakini ni kweli pamoja na jitihada za Serikali, tumekuwa pia tukiungwa mkono na wadau mbalimbali kwa ajili ya kujenga majengo ya kutolea huduma za afya. Nikifanya tathimini ya haraka haraka nchi nzima mdau ambaye namwona binafsi amejitolea kujenga majengo mengi ya huduma za afya kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati ni Mheshimiwa Salim Asas - MNEC wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nikuahidi sisi kama Wizara na Serikali kwa ujumla tutamuandalia tuzo maalumu Bwana Salim Asas - MNEC ili kuweza kumshukuru na kumpongeza kwa jitihada zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ili kumuunga mkono kwa sababu ametujengea karakana ya viungo bandia na sisi Wizara sasa hivi na mimi nikiwa Waziri mwanamke na ni mama, tumeona ipo haja ya kuongeza mkazo katika huduma za utengamao hususani kwa watoto wenye ulemavu. Kwa hiyo, karakana hii tutaifanya ni moja ya karakana kubwa za nchini kwetu ili kutengeneza viungo bandia kwa watoto wenye ulemavu na watu wengine wenye uhitaji. (Makofi)
Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Afya Vwawa?
Supplementary Question 6
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na niishukuru Serikali tunacho chuo cha afya katika Mkoa wa Tabora ambacho kipo katika hospitali ya Kitete, changamoto iliyopo ni ukosefu wa vifaa vya kufundishia pamoja na wakufunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka vifaa vya kufundishia na wakufunzi ili tuweze kupata wahudumu wa afya waliyo na elimu bora? (Makofi)
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, kwa swali lake zuri kuhusu Chuo cha Afya Tabora na nataka kukubaliana naye umuhimu wa kuwekeza kwenye vifaa tiba pamoja na wataalamu ili kuweza kuzalisha wataalamu wa afya wenye ujuzi.
Kwa hiyo, kwa upande wa vifaa tiba Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, aah samahani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia tutaomba tupate orodha rasmi kutoka kwa Mkuu wa Chuo Tabora ili tuone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwa upande wa wakufunzi jana nilitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu kupeleka wakufunzi katika vyuo vya afya, lakini nimempa angalizo badala ya kuchukua wakufunzi ambao ndiyo wamemaliza tu masomo yao ya vyuo vikuu, wachukue wakufunzi ambao tayari wana uzoefu wa kufundisha na kutoa huduma za afya ndiyo wawe wakufunzi katika vyuo vya kutoa huduma za afya lakini pia waangalie kama vyuo vikuu vinavyofanya wanachukua wakufunzi ambao wamepata GPA kubwa.
Kwa hiyo, hili jambo nimelisistiza sana siyo tu kupeleka mtu aliyemaliza chuo kikuu mnampeleka akawe mkufunzi wa Chuo cha Afya, Hapana, lakini lazima tuwekeze kwenye wakufunzi wenye sifa na uwezo. (Makofi)
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Afya Vwawa?
Supplementary Question 7
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye sekta hii ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kufahamu wananchi wa Kata ya Narumu wameandaa eneo kubwa na la kutosha kwa ajili ya kujenga kituo cha afya, lakini na Chuo cha Afya Narumu. Je, hauoni ni wakati sahihi sasa Serikali kuweka kwenye mpango kwa ajili ya kuandaa maandalizi ya kujenga Chuo cha Afya cha Narumu? (Makofi)
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Saashisha kwa swali lake la nyongeza, lakini kwa kazi nzuri anayofanya kwa wananchi wa Hai na tunaamini wananchi wa Hai wataendelea kumuunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la ujenzi wa kituo cha afya na chuo cha afya na Kituo cha Afya Narumu niombe kwanza kitangulie kujengwa kituo cha afya kabla hatujaja kuweka chuo cha afya. (Makofi)