Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Daraja la Mto Mpiji ili kuunganisha Kibaha na Kibwegere Wilaya ya Ubungo?

Supplementary Question 1

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili yenye kifungu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilishawahi kutengwa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili la kivuko hiki, lakini haijatekelezwa. Leo majibu ya msingi yanaonesha kwamba wanaendelea au wamekamilisha tathmini na gharama wamezipata upya, sasa wanatafuta fedha. Nini commitment ya Serikali kujenga daraja hili ili kuokoa vifo vya watoto ambapo hata jana tu mtoto mmoja amekufa kwenye kivuko hiki?

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Jimbo la Kibamba kuna Mto Mpiji wenyewe na Mto Mbezi ambapo kuna vivuko vingi sana hatarishi kwa watoto wetu na watu wanaotumia. Je, ni ipi ahadi ya Serikali kuleta fedha maalum kujenga vivuko hivi ili tuokoe maisha ya watu wetu? Nashukuru.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi, tayari Serikali imefanya tathmini na imebaini kwamba zinahitajika shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kazini na ndiyo maana kuna ongezeko kubwa la bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka muda huu Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia imeridhia kuongeza bajeti maalum ya shilingi bilioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hii. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepokea na itaweka kipaumbele kikubwa sana kuhakikisha kwamba inaanza ujenzi wa miundombinu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, vivyo hivyo nirejee maelezo yangu ya awali kwamba Serikali inaona umuhimu mkubwa sana wa miundombinu hii muhimu kwa maslahi ya wananchi, na tayari bajeti ya dharura ya TARURA imeongezeka. Vile vile kuna bajeti maalum kwa ajili ya ukarabati na marekebisho na ujenzi wa miundombinu hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalichukulia suala hili la ujenzi wa miundombinu hii kwa umakini mkubwa na itakuja kujenga miundombinu hii.

Name

Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Daraja la Mto Mpiji ili kuunganisha Kibaha na Kibwegere Wilaya ya Ubungo?

Supplementary Question 2

MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kwenye Wilaya ya Kilindi kipo Kijiji cha Mgera ambacho kina daraja limekatika takribani miaka mitatu sasa na Serikali haijarekebisha hali hiyo na upande wa pili ndipo ambapo taasisi zote za Serikali zipo huko. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutoa maelekezo kwa TARURA kwenda kurekebisha daraja hilo?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele vya TARURA ni pamoja na kuhakikisha kwamba inahakikisha miundombinu ya barabara hizi haikatiki kimawasiliano. Kwa hoja ya Mheshimiwa Mbunge naomba baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu tukutane, tukae, tuweze kufanya mawasiliano na kama ni kweli eneo hili limekata mawasiliano, kuna umuhimu na kipaumbele kikubwa sana ambacho inabidi kitolewe kwa ajili ya kuhakikisha tunarudisha mawasiliano katika eneo hili.

Name

Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Daraja la Mto Mpiji ili kuunganisha Kibaha na Kibwegere Wilaya ya Ubungo?

Supplementary Question 3

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Mpendo na Kijiji cha Amia kinatenganishwa na mto mkubwa ambao unaitwa Mto Bubu. Ni lini sasa Serikali itajenga daraja ili kuunganisha vijiji hivi viwili?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyotangulia kusema kwamba ni muhimu sana kuwe kuna mawasiliano na ndiyo kipaumbele katika mipango kazi au utekelezaji wa majukumu ya TARURA kuhakikisha kwamba mawasiliano hayakatiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadiri alivyoleta maombi yake na kwa kuzingatia vipaumbele na upatikanaji wa fedha, Serikali itamsaidia kwenda kurekebisha miundombinu hii.

Name

Dr. Alfred James Kimea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Primary Question

MHE. ISSA J. MTEMVU K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Daraja la Mto Mpiji ili kuunganisha Kibaha na Kibwegere Wilaya ya Ubungo?

Supplementary Question 4

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini kuna madaraja mawili ambayo yana changamoto kubwa. Moja lipo katikati ya mji ambalo vivuko vyake vimekatika pembeni, watoto wanapata ajali ya kuanguka; daraja lingine la Kitifu, limekatika kabisa, hakuna mawasiliano kati ya kata mbili; Kata ya Mgombezi pamoja na Mtonga: Je, Waziri haoni sababu ya kuwaelekeza TARURA kurekebisha madaraja hayo mawili muhimu kwenye Jimbo la Korogwe Mjini?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafanya mawasiliano na Meneja wa TARURA ili kufahamu changamoto iliyopo katika eneo hilo na kama ni dhahiri kwamba mawasiliano yamekatika, basi kama ulivyo utaratibu wa TARURA ni kuweka kipaumbele katika kuhakikisha inaunganisha na kuna mawasiliano katika barabara zetu hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tumelipokea na tutalifanyia kazi.