Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Primary Question

MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kununua Jenereta katika Hospitali ya Ilongero na Vituo vya Afya Mgori, Makuro na Msange - Jimbo la Singida Kaskazini?

Supplementary Question 1

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; nakiri kwamba tumepokea standby generators katika Hospitali ya Wilaya na Kituo cha Afya Mgori. Majenereta haya bado hayajaanza kutumika kwa kipindi kirefu sasa kutokana na kukosekana vile vibanda vya kuweka standby generators. Je, ni lini Serikali itaweza kujenga hivyo vibanda ili haya majenereta yaweze kutumika na kule kwenye Vituo vya Afya vya Mgori na Makuro ambavyo havina?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Hospitali ya Wilaya pamoja na vituo vya afya vyote vilivyopo katika Jimbo la Singida Kaskazini havina vyumba vya kuhifadhia maiti. Je, ni lini Serikali itajenga mortuary ili kuepusha usumbufu unaotokea pindi inapotokea dharura?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kutumia nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwamba, Mheshimiwa Rais ameshapeleka fedha, majenereta yamenunuliwa kwa ajili ya hospitali ya wilaya na vituo vya afya. Kazi yake ni kujenga kibanda kwa ajili ya kuweka jenereta, ili wananchi waanze kupata huduma. Kwa hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, namwelekeza kwamba ndani ya siku 45, mwezi mmoja na nusu, ahakikishe amekamilisha ujenzi wa vibanda hivyo na majenereta hayo yafungwe yaanze kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu majengo ya kuhifadhia maiti. Serikali inaendelea kutafuta fedha na kujenga miundombinu hiyo katika vituo vyetu kwa awamu. Pia, tunaendelea kusisitiza kwamba, mapato ya ndani ya halmashauri yatumike kwa ajili ya kujenga baadhi ya miradi ikiwemo majengo haya muhimu katika jamii zetu ya kuhifadhia maiti. Kwa hiyo, halmashauri ianze kufanya tathmini hiyo, lakini kama uwezo hautaruhusu, basi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa itaunga mkono juhudi ambazo watakuwa wameanza utekelezaji wake. Ahsante.