Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nicodemas Henry Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: - Je, lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuchimba malambo kwa ajili ya mifugo ili kurahisisha shughuli za ufugaji Mbogwe?

Supplementary Question 1

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza nashukuru kwa majibu ya Serikali japokuwa sijaridhika, naomba kuuliza maswali mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021 aliyekuwa Waziri wa Mifugo alikuja Lulembela Namasumbo akawaahidi wananchi wa Mbogwe kwamba atatekeleza bajeti ya 2023. Je, lini Serikali itachimba hayo malambo yaliyoahidiwa na Serikali mwaka 2021?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ukurasa wa 54 tuliwaahidi wananchi wafugaji wa Mbogwe kwamba tutatenga maeneo kwenye hifadhi zetu ya Kigosi maeneo ya kufugia, lini sasa hiyo ahadi itatekelezwa ili wananchi waweze kupewa hayo maeneo ya kuchungia ng’ombe? Ahsante sana.

Name

Alexander Pastory Mnyeti

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Misungwi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Waziri Mstaafu wa Mifugo Mheshimiwa Mashimba Ndaki alipotembelea mwaka 2021/2022 kule kwenye Jimbo la Mheshimiwa Maganga alitoa ahadi ya kuchimba mabwawa kwenye maeneo ya wafugaji na baada ya hapo Wizara ilichokifanya ilichukua ahadi hizo na kuziingiza kwenye mpango wa Serikali. Ndiyo maana nimesema katika jibu la msingi kwamba mpango wa Serikali upo na tunatambua ukame mkubwa uliopo katika Jimbo la Mbogwe, Nyangw’ale pamoja na Bukombe. Huo ukanda wote una hali ngumu sana ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo yetu na baada ya hapo tuliingiza kwenye mpango, na mpango huo baada ya upatikanaji wa fedha tutakwenda kutekeleza uchimbaji wa mabwawa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inao mpango wa kwenda kuchimba mabwawa katika maeneo hayo, hivyo awe na subira, tutakwenda kuchimba kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake hili la pili la kutenga maeneo ya wafugaji. Jambo hili liko chini ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa sababu hawa ndio wenye maeneo ambapo wanao uwezo wa kupanga kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi, kwamba Serikali za Vijiji sasa zinaweza zikaamua kwamba eneo hili wafuge, eneo hili walime na eneo hili wafanye kwa ajili ya malisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbogwe akae na wataalam wake watenge maeneo ya wafugaji ili wafugaji hao waweze kupata maeneo ya malisho kadri ambavyo maeneo hayo yanavyowaruhusu, ahsante.