Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Primary Question

MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza:- Je, lini Barabara ya Kata ya Rutoro itajengwa kwa kuwa maombi yalishawasilishwa TARURA?

Supplementary Question 1

MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru na kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Samia kwa namna ilivyotutendea haki kwenye miundombinu ya barabara chini ya TARURA; nimebaki na deni Rutoro na Bumbile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mawili ya nyongeza ni kwamba mkandarasi aliyejenga kilomita 13 za Kata ya Ngenge kuelekea Rutoro anadai pesa zaidi ya shilingi milioni 500, na hiyo kilomita 13 karavati zimeachwa wazi, yaani watu hawawezi kupita kwa sababu kijana amefulia, ni mjasiliamali, alikuwa ameanza, sasa amefulia. Naomba Serikali mumpatie uwezo angalau wa kufukia karavati ili liweze kupitika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Eneo la Kata ya Rutoro ambalo nina imani Serikali itatekeleza ahadi yake, walipata matatizo makubwa ya El-Nino, barabara zinazopitika hizo za panya zikapata makorongo. Ombi langu, naomba Serikali mtutengenezee karavati, msipige greda, mtutengenezee karavati kwenye yale maeneo makorofi ili tukae tukisubiri kuja kupata hiyo ahadi kubwa ya bajeti ya mwaka ujao?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika amekuwa akipaza sauti yake kuhakikisha kwamba maendeleo yanapelekwa katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maswali yake yote mawili, kwanza haya ni maombi, nimeyapokea, nasi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA tutayafanyia kazi ili tuweze kufanya utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuhusiana na hili swali kwamba mkandarasi ana madai ya shilingi milioni 500, hili kwa upekee kabisa naomba Mheshimiwa Mbunge tukae kwa pamoja tufanye ufuatiliaji ili wakandarasi wetu waweze kuwezeshwa kufanya kazi hizi ambazo wanazifanya za kuboresha miundombinu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na fedha hizi za kuchonga na kutengeneza makaravati katika barabara hii ya Rutoro, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nimelibeba suala hili kwa uzito mkubwa sana na kwa sababu yeye binafsi amekuwa akilizungumzia mara nyingi, tunalifanyia kazi na litapata majawabu kwa sababu Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inataka kuboresha miundombinu ya barabara kwa kutambua umuhimu wake kiuchumi na kijamii.

Name

Francis Kumba Ndulane

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kaskazini

Primary Question

MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza:- Je, lini Barabara ya Kata ya Rutoro itajengwa kwa kuwa maombi yalishawasilishwa TARURA?

Supplementary Question 2

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia leo imetimia miezi 11 Kata za Kibata na Kata ya Tandawale hazina mawasiliano kabisa ya Barabara na Makao Makuu ya Tarafa ya Kipatimu. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa haraka ili kuhakikisha kwamba shughuli za kiuchumi na kijamii katika kata hizo mbili muhimu zinaendelea?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasemea wananchi wake. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza kwa kiwango kikubwa bajeti ya TARURA kutoka shilingi bilioni 275 mpaka sasa kila mwaka inatengwa shilingi bilioni 710.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa katika mwaka uliopita kumekuwa na madhara makubwa katika barabara zetu hizi hasa hizi barabara zinazosimamiwa na TARURA kutokana na El-Nino, basi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetambua mahitaji ya kuongezeka kwa bajeti na ndiyo maana Mheshimiwa Rais ameongeza bajeti ya dharura kutoka ya shilingi bilioni 21 kwa mwaka mpaka kufikia shilingi bilioni 254.3 katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaboresha na inarekebisha miundombinu ambayo imeharibika ili wananchi waweze kupata miundombinu iliyo bora, iweze kuwanufaisha kijamii na kiuchumi.

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza:- Je, lini Barabara ya Kata ya Rutoro itajengwa kwa kuwa maombi yalishawasilishwa TARURA?

Supplementary Question 3

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wilaya ya Makete ni moja kati ya Wilaya ambazo zimepata changamoto ya kuharibika kwa Barabara, tunaishukuru Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kujenga Barabara ya Itundu, Barabara ya Mang’oto, Barabara ya Ibaga, Barabara ya Kinyika, lakini kumekuwepo na changamoto ya wakandarasi wamesaini mikataba, site hawajaja. Mheshimiwa Waziri ipi ni kauli yako kwa wakandarasi wote ambao hawajaja kujenga Barabara ya Makate wakati Serikali imewapatia fedha? Ahsante.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya uwakilishi katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la Mheshimiwa Mbunge naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendelea kusisitiza mameneja wote wa TARURA wa ngazi ya mkoa, na wilaya kuhakikisha wanafanya usimamizi wa miradi hii ya barabara. Wakandarasi wanapokuwa wamepatikana, na fedha zikiwa zimetoka, wajibu wa msingi ni kusimamia kuhakikisha kwa uharaka kabisa miradi hii inatekelezwa na wananchi wanaweza kupata barabara zilizobora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumsisitiza Meneja wa TARURA wa mkoa huu aweze kuhakikisha kwamba anaenda kusimamia miradi yote ya ujenzi wa barabara ambazo fedha zake zimetoka na wakandarasi wamepatikana ili waweze kujenga barabara hizi kwa wakati ikiwemo Makete. Kwa hiyo, Meneja wa TARURA wa Makete pia ujumbe huu unamhusu, asimamie kwa ukamilifu kuanza utekelezaji wa miradi pamoja na kuikamilisha kwa wakati.

Name

Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza:- Je, lini Barabara ya Kata ya Rutoro itajengwa kwa kuwa maombi yalishawasilishwa TARURA?

Supplementary Question 4

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni lini Serikali itajenga barabara kutoka Rau kuelekea Materuni ambako kuna maporomoko na watalii wengi wanafika kule, lakini wanashindwa kufika kwa wakati kutokana na barabara mbovu na hivyo Serikali kukosa mapato? Ni lini sasa Serikali itajenga barabara hii ya kimkakati? Ahsante sana.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa uwakilishi wake mzuri, lakini kuhusiana na swali lake naomba niendelee kukumbusha kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaimarisha barabara zetu hizi hasa zinazosimamiwa na TARURA ambazo ni barabara zetu za wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kwamba bajeti ya TARURA imeongezeka kutoka shilingi bilioni 275 mpaka shilingi bilioni 710 kila mwaka. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kufikia barabara nyingi zaidi na kuziweka katika hali iliyo nzuri kwa ajili ya kuhakikisha kwamba haikwamishi miradi mbalimbali na shughuli mbalimbali za kiuchumi na za kijamii. Kwa hiyo, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na tutalifanyia kazi.