Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stella Simon Fiyao

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: - Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na ongezeko la bei ya pembejeo za kilimo?

Supplementary Question 1

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua jitihada na bidii ambayo Serikali inaifanya katika kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya kilimo. Pia kuna changamoto kubwa sana kwenye upatikanaji wa pembejeo za kilimo hususan mbegu. Kwenye taarifa yenu inaonesha kuna utoshelevu wa 40% tu maana yake hata nusu hatujafika. Sasa nataka kujua mkakati wa Serikali ni upi ili kuhakikisha tunapata mbegu bora na za uhakika ili kuepusha changamoto ambayo wakulima wamekuwa wakikabiliana nayo kila wakati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu namba mbili, nataka kujua, Serikali mna mpango gani wa kushawishi wawekezaji ili waje kuwekeza ndani ya nchi, viwanda vikubwa vya mbolea ili tupate mbolea kwa bei rahisi na kwa uhakika zaidi? Ahsante.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nami naendelea kumwondoa hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya mikakati yetu ni kama ambavyo nimeitaja katika jibu la msingi, lakini tutaendelea kutumia mifumo ya kuagiza ili kupunguza bei kwa wakulima kwa sababu tunaamini kabisa ili tuweze kupata tija, ni lazima tuongeze matumizi ya mbegu bora pamoja na mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo haya yapo katika mkakati na tuamini kwamba tulikotoka na tulipo, tuko sehemu nzuri zaidi na mwelekeo tunakokwenda ni kuzuri zaidi. Tunaamini kwamba jambo hili, itafikia mahali tutakuwa na utoshelevu kwa 100%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu mpango wa uwekezaji wa kutengeneza viwanda vya mbolea hapa nchini, hilo lipo katika mipango ya Serikali. Sasa hivi tunafanya mazungumzo na wawekezaji kupitia Balozi zetu kama ambavyo kule Ubalozi wa Qatar wanahangaika na watu wa Qatar Energy ili waweze kutusaidia kuzalisha mbolea hapa nchini. Katika hatua za awali, waweze kutuletea mbolea ambayo sasa tutaanza kuitumia kabla ya kuwekeza katika viwanda. kwa hiyo hii ni mipango ya Serikali ambayo tupo nayo, kwa hiyo tuna mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu na yote ipo katika mchakato wa kukamilika, ahsante sana.

Name

Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: - Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na ongezeko la bei ya pembejeo za kilimo?

Supplementary Question 2

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima wa pamba anapouza pamba yake anakatwa shilingi 300 kwa kila kilo na kulipa kwa ajili ya pembejeo kwa Bodi ya Pamba bila kuangalia matumizi ya pembejeo ambayo inalingana na kile kiasi anachokatwa. Je, kwa kuwa mfumo huu unasababisha bei ya pamba kuwa chini, Serikali haioni haja ya kutafuta mfumo mwingine wa kumkata mkulima ili akatwe kulingana na kile alichokitumia (pay as you use)?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa ugharamiaji pamba, gharama ya shilingi 300 inawekwa katika mfumo wa mjengeko bei ambapo tunatazama gharama zote za uzalishaji, lakini gharama hizi za shilingi 300 tunazipunguza kutokana na profit margin ya mnunuzi kwa sababu tunaangalia future market, tunaangalia price ya export na exchange difference ya price.

Mheshimiwa Mwenyekiti, profit anayoipata kutokana na exchange rate, tunaipunguza pale ili irudi kumhudumia mkulima. Mifumo hiyo mingine yote mfano huo wa ulipe kutokana na mahitaji, toka miaka ya 1990, ni mifumo ambayo imejaribiwa na imeshindikana. Mfumo sahihi ambao tunaamini kama Serikali ni mfumo huu wa mnunuzi kukatwa shilingi 300 na baada ya hapo mnunuzi anaweka kwenye mfuko, mkulima anapewa pembejeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya pamba hivi karibuni ilianza na shilingi elfu moja na mia moja leo ipo shilingi 1,300 na minada inaendelea na mkulima bei anayoipata mnadani hakatwi hata shilingi 100. (Makofi)