Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Primary Question
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:- Je, lini Serikali itatekeleza mkakati wa kujenga Zahanati kwenye Vijiji vyote nchini?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nimepokea hii taarifa ya zahanati 980 katika kipindi hicho ambacho katika Halmashauri ya Sikonge tulipata Zahanati tatu za Kidete, Mwamayunga na Mkola. Sasa tumebakiza maboma 13 ambayo wananchi wameyafikisha kwenye lenta na tunahitaji milioni 650. Swali la kwanza; je, lini tutapewa hizo fedha ili kukamilisha maboma 13 yaliyobaki?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; sera ya kila kijiji zahanati na kila kata kituo cha afya ni ya mwaka 2007, ni ya Serikali. Sasa leo tunaambiwa umbali, badala ya kila Kijiji; hii sera imebadilishwa lini na Serikali? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Kwanza niwapongeze wananchi wa Jimbo la Sikonge kwa namna ambavyo wameendelea kuchangia nguvu zao katika ujenzi wa zahanati na kuwa na maboma 13 ambayo yamekwishapauliwa na kwa mujibu wa Mheshimiwa Mbunge yanahitaji takribani milioni 630 kwa ajili ya ukamilishaji.
Mheshimiwa Spika, ninaomba tu nimhakikishie kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele cha hali ya juu katika kuchangia nguvu za wananchi kukamilisha maboma haya na ndio maana maboma 980 yamekamilishwa na Sikonge imepata maboma matatu. Tutaendelea kutenga fedha hizo kwa awamu ili kukamilisha majengo hayo.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kumwelekeza Mkurugenzi wa Sikonge kutenga fedha kwenye mapato ya ndani, kuweka vipaumbele kwenye zahanati ambazo zinahitajika kwa haraka zaidi na wananchi kwa ajili ya ukamilishaji.
Mheshimiwa Spika, pili, Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi ni mpango uliobuniwa na ulibuniwa mwaka 2006, ulipangwa kukamilika mwaka 2017. Mpango huu ulikuwa unaelekeza; kujenga hospitali ya halmashauri kwa kila halmashauri, ujenzi wa kituo cha afya kwa kila kata, ujenzi wa zahanati kwa kila kijiji na ujenzi wa zahanati kwa kila mtaa.
Mheshimiwa Spika, kiuhalisia, tuna vijiji zaidi ya 12,000, mitaa zaidi ya 4,000, kata zaidi ya 3,500 na halmashauri zaidi ya 184. Kiuhalisia hatuwezi kujenga zahanati kwenye kila mtaa, iko mitaa mingine ni midogona iko jirani sana, itakuwa ni misuse of resources kujenga zahanati kila mtaa, lakini pia itakuwa ni burden kubwa sana kwa Serikali kwa maana ya wage bill kuwa na zahanati kila kijiji, mtaa na kata kuwa na kituo cha afya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tume-review ule Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi wa 2006 – 2017, sasa tunakwenda kimkakati, tunaangalia factors kwa maana ya idadi ya wananchi na umbali kutoka kituo cha jirani cha huduma na ndiyo maana tunajenga kimkakati. Hii itakuwa na faida zaidi kwa vituo hivyo kuliko kujenga kila sehemu kituo ambacho hakitokuwa na tija. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Twaha Ally Mpembenwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibiti
Primary Question
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:- Je, lini Serikali itatekeleza mkakati wa kujenga Zahanati kwenye Vijiji vyote nchini?
Supplementary Question 2
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kumekuwa na changamoto kubwa sana kwenye Zahanati ya Nyamisati, kwenye Kata ya Salale ukizingatia kwamba zahanati ile inahudumia Wilaya mbili za Mafia pamoja na Kibiti. Je, nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha wanajenga Kituo cha Afya kwenye Kata ya Salale?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kata zote ambazo zinakidhi vigezo kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya tulishafanya kazi ya kuziainisha katika halmashauri zetu zote 184, ikiwemo Halmashauri ya Kibiti.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ikiwa hii kata ambayo Zahanati ya Nyamisati ipo, kwenye kata ambazo zimeainishwa, tutaipa kipaumbele, lakini kama haipo na unahitaji kujenga kituo cha afya, basi nimwombe Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Mkurugenzi na DMO waweze kuwasilisha ili iingizwe kwenye mpango wa kujenga vituo vya afya. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved