Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Daimu Iddi Mpakate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kusini

Primary Question

MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:- Je, lini Serikali itaboresha Kituo cha Afya Mtina ili kitoe huduma za upasuaji?

Supplementary Question 1

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Kituo cha Afya cha Mchesi ni kituo cha kimkakati kilichoanza kufanya kazi mwishoni mwa Desemba, 2023, lakini mpaka sasa kina mtu mmoja tu ambaye anatoa huduma. Mganga huyo huyo, Nurse huyo huyo na mhudumu ni huyo huyo. Ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha ili kile Kituo cha Afya cha Mchesi kifanye kazi kama kituo cha afya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Kituo cha Afya Nalasi ni kituo cha afya kilichojengwa na halmashauri kwa milioni zaidi ya 600 na vifaatiba kupelekwa katika kituo kile, lakini mpaka leo vile vifaa havijafungwa, ni lini Serikali itafunga vifaa vile na kupeleka watu ambao watatoa huduma sahihi? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo wamefanikiwa kufuatilia na kuanza huduma katika Kituo cha Afya cha Mchesi, Jimbo la Tunduru Kusini, lakini nimhakikishie tu kwamba, Serikali imeweka kwanza utaratibu wa kufanya msawazo wa ndani wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kumwelekeza Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, kuhakikisha anaangalia namna ambavyo anaweza akapata watumishi ndani ya mkoa kwa ajili ya kuwapeleka kwenye Kituo hiko cha Afya cha Mchesi angalau kuongeza nguvu wakati tunasubiri ajira hizi ambazo Mheshimiwa Rais amezitoa hivi karibuni na tuko hatua za mwisho za kupeleka watumishi kwenye vituo hivyo ili kupunguza upungufu wa watumishi katika kituo hicho. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kituo hicho kitapata watumishi na kitaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na vifaatiba katika kituo cha afya ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja. Ninaomba nimhakikishie kwamba Serikali imeshapeleka vifaatiba na kwa bahati njema umesema, lakini ni muhimu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tunduru na Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha wanawasiliana mara moja na wale Wazabuni walioleta vile vifaa kwa ajili ya kufunga vifaa hivyo mapema iwezekanavyo ili vianze kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawapa muda wa wiki mbili na tutafuatilia kuona kwamba wameshafunga vifaa hivyo na vimeanza kutumika katika kituo hicho cha afya. Ahsante. (Makofi)

Name

Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:- Je, lini Serikali itaboresha Kituo cha Afya Mtina ili kitoe huduma za upasuaji?

Supplementary Question 2

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati na kuweka jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya cha Round Table Mbagala Kizuiani? Kituo hicho ni cha muda mrefu, mama anapozidiwa inabidi atafutiwe gari kupelekwa Temeke au Zakiem, Serikali ina mpango gani sasa wa kuweka jengo la upasuaji?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Afya cha Round Table kule Mbagala ni kituo cha muda mrefu na ni kituo ambacho kinahudumia wananchi wengi. Serikali tulishatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuweka kipaumbele kwenye vituo vya afya ambavyo vina uhitaji mkubwa wa majengo, kama Kituo cha Round Table kule Mbagala.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nitumie nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inalichukua jambo hili kwa uzito unaostahili, lakini nimuagize Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwenda kufanya tathmini ya mahitaji ya fedha ambazo zinatakiwa kuboresha kituo hicho cha afya, kuwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, lakini pia kufanya tathmini ya uwezo wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kuanza ukarabati wa kituo hicho cha afya mapema iwezekanavyo. Ahsante.