Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Florent Laurent Kyombo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Primary Question
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha Mradi wa Umeme Kakono – Misenyi?
Supplementary Question 1
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa majibu mazuri. Mradi huu umechukua muda mrefu na wananchi wa Wilaya ya Misenyi wamekuwa wavumilivu, lakini kupitia Serikali sikivu wameendelea kufanya kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata haki yao. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwa kuwa fidia hii imechukua muda mrefu na tathmini ilishafanyika, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tathmini hii inakidhi muda wa kisheria wa tathmini ili wananchi hao waweze kupata fidia ambayo inaendana na wakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, niwaambie nini wananchi wa Misenyi kwamba watalipwa hiyo fidia kwa kuwa wameisubiri kwa muda mrefu sana? Ahsante.
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia fidia ya wananchi wake kwa karibu sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali tunahakikisha fidia ambayo inalipwa kwa wananchi ni ile ambayo inaakisi muda na wakati. Kwa sasa tupo tayari kwa ajili ya kuanza kulipa na wenzetu wa Wizara ya Fedha wametuhakikishia mpaka ifikapo mwishoni mwa Juni, labda tutakuwa tunaanza kulipa fedha hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa jimbo lake wakae kwa utulivu, Serikali ni sikivu sana na tupo tayari kwa ajili ya kuanza kulipa fedha hizi, ahsante.
Name
Jafari Chege Wambura
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Primary Question
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha Mradi wa Umeme Kakono – Misenyi?
Supplementary Question 2
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa ni mara ya tatu sasa nasimama ndani ya Bunge kuulizia fidia ya wananchi zaidi ya 246 waliopisha mradi wa umeme toka mwaka 2011. Mheshimiwa Waziri nataka kupata kauli ya Serikali, kwa kuwa sasa ni miaka 13 imepita, ni lini wananchi hawa watalipwa fidia yao kwa mujibu wa sheria?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Chege amekuwa akifuatilia suala la fidia la wananchi hawa ambao wako 246 ambapo gharama ya fidia yao ni shilingi 220,000,000/=. Nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa jimbo lake kwamba, tayari fedha hizi tunazo na tunaanza kulipa wananchi 211 ambao taarifa zao zipo vizuri. Wale wananchi 35 ambao taarifa zao haziko vizuri, tumeielekeza halmashauri jimboni kwake waweze kuzifanyia kazi ili na wenyewe wakae katika mpango wa kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mpaka tunafika Juni 30, wananchi hawa watakuwa wameshaanza kulipwa kwa sababu fedha tayari tunazo.
Name
Mohamed Lujuo Monni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chemba
Primary Question
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha Mradi wa Umeme Kakono – Misenyi?
Supplementary Question 3
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mradi wa REA, kuna vijiji vitatu vya Wilaya ya Chemba vilisahaulika; Kijiji cha Kelema Kuu, Kijiji cha Birise na Kijiji cha Muungano na bahati nzuri hatuhitaji sisi fidia, tunahitaji umeme tu. Naomba kujua, ni lini sasa vijiji hivyo vitawekewa umeme? Ahsante.
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Monni amekuwa akifuatilia kweli vijiji hivi vitatu ambavyo vilisahaulika katika mpango, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshafanyia kazi na vijiji hivi vya Kelema Kuu, Birise na Muungano, tayari tumeshaongea na mkandarasi kwa ajili ya kumwongezea wigo ili aweze kuanza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa hakuna kijiji kitaachwa kupelekewa umeme katika mradi huu ambao unaendelea. Kwa hiyo, wakae kwa utulivu, Serikali tumesikia na tutapeleka umeme katika hivi vijiji vitatu, ahsante.
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha Mradi wa Umeme Kakono – Misenyi?
Supplementary Question 4
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Wilaya ya Makete wamepisha ujenzi wa Bwawa la Lumakali na ni takribani mwaka mzima umeisha toka watu wa ardhi wafanye tathmini. Wanauliza, ni lini Serikali itawalipa fedha ili wananchi wetu waendelee na shughuli za kiuchumi kwenye eneo lile?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti ya mwaka unaokuja wa fedha 2024/2025, tumetenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia wananchi hawa ambao wamepisha Mradi wa Lumakali. Tunaendelea kufanya tathmini ili kuweza kuelekea kwenye zoezi la fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa malipo ya fidia yapo katika bajeti kwa sababu mradi wa Lumakali ni mradi mmojawapo ambao sisi kama Serikali tunautegemea katika kuzalisha umeme, kwa hiyo, wananchi hawa watalipwa fidia. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved