Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa huduma ya maji bure vijijini kama ilivyo kwenye baadhi ya huduma za Elimu na Afya?

Supplementary Question 1

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na sheria iliyopo ambayo inataka wananchi kushirikishwa katika kupanga bei, hali halisi ni tofauti, maeneo mengi wananchi hawashirikishwi. Mfano, Wilaya ya Lushoto, Lukozi na Kata ya Lukozi, Kata ya Shume na Manolo, bei zilipelekwa kubwa ikamlazimu Mkuu wa Wilaya kwenda kushusha bei za maji kwa wananchi, nini hatua ya Serikali kudhibiti hali hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa gharama hizi zinasababishwa na wananchi kugharamia mafundi wa local fundi wanaokwenda kukarabati miradi hiyo. Je, Serikali haioni imefika muda muafaka kuwaajiri na kuwalipa mishahara local fundi na kuondoa mzigo huo kwa wananchi? Nashukuru sana. (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, bei za huduma ya maji zinapangwa kutokana na sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kwanza; uzalishaji, eneo ilipo skimu husika, aina ya utoaji wa huduma, lakini vilevile na aina ya jamii inayozunguka eneo husika, lakini kwa mujibu wa sheria na EWURA anaingia katika upangaji wa bei ya maji. Kwa kuzingatia factor hizo zote, Serikali imekuwa ikiingilia kati pale ambapo tunaona kwamba kuna changamoto na ndiyo maana Mkuu wa Wilaya ni sehemu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo Waziri wetu wa Maji Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, katika bajeti yetu tumepanga kuwepo na fedha za monitoring and evaluation kwa ajili ya wakuu wa wilaya pale ambapo kunakuwa na changamoto ya utekelezaji wa mradi au uendeshaji wa miradi, Mkuu wa Wilaya aweze kufika eneo husika na kutoa maelekezo ya Serikali, hilo tutaendelea kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linatokana na uzembe wa uendeshaji wa wataalam ambao wamekabidhiwa jukumu la kuendesha na hayo yote tumekuwa tukiyafuatilia na kuchukua hatua stahiki. Sote tutakubaliana, sheria kuwepo ni jambo moja, utekelezaji wa sheria ni jambo lingine, kwa hiyo, tumejitahidi sana kuhakikisha watu wetu wanaendelea kusimamia na kuhakikisha sheria haivunjwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu ajira kwa mafundi, ni kweli kabisa changamoto hii tumeanza kuiona baada ya kugundua kwamba kuna CBWSOs wameshindwa kujiendesha na wale local fundi wanashindwa kuwalipa, inasababisha hata ile miundombinu yetu kuendelea kuchakaa na kuharibika. Kwa sasa tayari tumeshaanza kukusanya maoni, namna bora zaidi ya kwenda kuendesha CBWSOs bila kuleta mzigo mkubwa kwa wananchi ambao wanatarajia kutumia huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, katika kufanya tathmini yetu na yeye tutamfikia kwa ajili ya kuomba maoni yake ili tuweze kuboresha zaidi na hatimaye gharama kwa wananchi iwe reasonable, lakini uendeshaji wa miradi yetu na miundombinu isiweze kuharibika kwa kukosa fedha ambazo zingesaidia sana.

Name

Bupe Nelson Mwakang'ata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa huduma ya maji bure vijijini kama ilivyo kwenye baadhi ya huduma za Elimu na Afya?

Supplementary Question 2

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaanza kuweka mita za maji ambazo unalipia kabla ya matumizi kama ilivyo kwenye LUKU ili kuepusha malalamiko ya wananchi ya kubambikiwa bili za maji? Ahsante.

Name

Bupe Nelson Mwakang'ata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Bupe, kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa sana katika sekta yetu ya maji na kwa kuendelea kuwa msemaji wa akina mama kutoka katika mkoa wake. Haya kwanza ni maelekezo ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na sisi tumeshayachukua na tayari tumeshaanza kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais. Vilevile naomba niseme kitu kimoja kwamba jambo ambalo sisi tunaenda kulifanya, tunaenda kwenye smart prepaid water meter ambayo ni tofauti kidogo na LUKU. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaponunua LUKU unamtumia mtu token anaingiza, sisi tunataka kwamba mtu akiwa Dar es Salaam maji yake yameisha Dodoma ana uwezo wa kununua maji yake ndani ya sekunde 20 tayari kule valve inakuwa imeshaachia imeshasoma na kuanza kutoa maji, hakuna haja ya kupitia njia nyingi nyingi kuhakikisha kwamba unatuma kwa mtu halafu anaingiza LUKU, hapana, sisi tunaenda kwenye smart prepaid water meter kuhakikisha kwamba itapunguza changamoto kwa wananchi kubambikiwa kama ambavyo Mheshimiwa amesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine itasaidia upotevu wa maji ambayo imekuwa ni changamoto kubwa sana, Serikali kuzalisha maji kwa gharama kubwa, lakini mengine yanapotea bila ya kuwa na sababu. Tatu, itasaidia kwa wananchi wenyewe kujua matumizi halisi ya familia zao na kuji-regulate wao wenyewe kuhakikisha kwamba hatuendi kwenye upotevu wa maji ambayo yalikuwa yanapotea bila ya kuwa na sababu za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali imeshajipanga tayari na tayari hivi tunavyoongea Mheshimiwa Waziri yupo China na ameenda kutembelea viwanda ambavyo vinazalisha smart prepaid water meter na atakaporejea tunaamini kwamba tutakuwa na jibu na muarobaini wa tatizo ambalo limekuwa likitusumbua katika Sekta ya Maji.