Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mariamu Nassoro Kisangi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, Serikali inachukua hatua gani kwa Wawekezaji wa nje ambao kila baada ya miaka kadhaa hubadili majina ya Kampuni kwa lengo la kukwepa kodi?
Supplementary Question 1
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Pamoja na majibu mazuri ninalo swali la nyongeza. Kwa kuwa, mchakato wa kubadilisha majina ya kampuni kwa Watanzania, ni mchakato mkubwa sana, unaambiwa uwe na vyeti mbalimbali mfano RITA na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kampuni za kigeni zikitoka kwenye eneo hili kwenda hili pasipo kujua Watanzania sababu gani inayowafanya watoke kwenye kampuni hii na kwenda hii, hali ambayo inawaletea Watanzania sintofahamu kubwa ya ukwepaji wa kodi. Je, Serikali inatoa tamko gani sasa la kuhakikisha hao wanaohama kwenye kampuni hii kwenda nyingine kutoa elimu ya kutosha kwa Watanzania ili wajiridhishe kwamba, wanahama kisheria na wala hawakwepi kodi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa kunakuwa na kampuni ambayo labda ina wadeni Watanzania, lakini kampuni ile imebadilisha jina ghafla. Je, Watanzania hawaathiriki na mabadiliko hayo? (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mariam kwa maswali mawili mazuri aliyoyatoa. Tuna mambo kama matatu kwenye hili jambo la kubadili majina. Moja, kubadili jina kama jina la kampuni haiathiri na wala haihusiani na masuala ya kikodi. Kinachozingatiwa sana, punde panapokuwepo na mabadiliko ambacho kinaweza kusababisha pawepo na kodi ama ukwepaji wa kodi, ni mabadiliko ya umiliki ambayo yanasababisha kama aliyekuwa anamiliki ameuza share, iwe share moja, mbili au tatu na akapata kipato cha ziada kutokana na zaidi ya uwekezaji aliokuwa amepata, hapo pana attract capital gain tax, inatakiwa alipie kodi ya faida ambayo ameipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mmiliki ni yule yule ameamua kubadilisha jina la kampuni, labda kwa ajili ya matangazo ya kibiashara na TIN Number ya mlipaji wa kodi bado ni ile ile, hili halileti badiliko lolote.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukabadili majina mara nyingi kama Musa Sima anavyobadili majina ya Timu ya Singida, hii haileti ongezeko la kodi kwenye kampuni. Kama Festo Sanga anamiliki Dodoma Hotel leo akaiita The Capital Hotel na mmiliki ni yeye mwenyewe, hii haileti jambo lolote la kodi, lakini kama Mheshimiwa Sanga alikuwa anamiliki hotel labda share kadhaa akiziuza kwa mtu mwingine, ile faida ya kuuza ndiyo ambayo tunaitaja kama capital gain tax ambayo anatakiwa alipie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna makampuni ya nje ambayo yanamiliki sehemu ya kampuni huku Tanzania na yanafanya shughuli, ukiyafatilia kule nje unakuta hayana shughuli zaidi ya kampuni inayofanya kazi hapa Tanzania. Ikitokea kule wamebadilishana umiliki unaozidi 50% hapo ndiyo na penyewe tunasema pana kodi lazima ikusanywe.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo Serikali imeshayafanyia kazi sana yalikuwepo zamani kwenye masuala ya mawasiliano, kwenye masuala ya madini, lakini sasa hivi yameshafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba yanapotokea mabadiliko ya aina hiyo, Serikali imeshaweka kwenye sheria na inafuatilia kwa ukaribu sana na mara zote yanapotokea mabadiliko ya aina hiyo Serikali imekuwa ikipata kodi inayostahili.
NAIBU SPIKA: Ahsante. Waheshimiwa tunaendelea Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, leo hewa nzito sana isije ikawa watu wameingia na ………(Kicheko)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved