Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwantumu Mzamili Zodo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: - Je, lini Serikali itaweka mkakati madhubuti wa upatikanaji wa maji ya uhakika kwenye Shule za Msingi na Sekondari nchini?

Supplementary Question 1

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Serikali wameahidi watashirikiana na Wizara ya Maji kwa ajili ya kuhakikisha shule zetu zinapata maji, na kwa kuwa hali ni mbaya sana kwenye shule zetu, hasa za kutwa, naiomba Wizara ya TAMISEMI ifanye mazungumzo na Wizara ya Maji kwa kuwa, Mheshimiwa Rais pia, ametoa magari nchi nzima kila mkoa kuhakikisha shule zile zinapata maji.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, Wizara ya TAMISEMI ina mkakati gani wa kuhakikisha kwenye shule zote, hasa hii miradi mipya, zile barabara zinapitika muda wote? Kwa sababu, mbali na changamoto ya maji, pia changamoto kubwa huwa ni barabara hasa kwenye miradi mipya ambayo Mheshimiwa Rais amepeleka fedha nyingi, ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa kwa kweli, hata mimi umenichanganya kidogo. Swali lako linahusu upatikanaji wa maji, sasa hivi umesema barabara au nini, kwa ajili ya hili neno shule? Kwa hiyo, barabara zinazoenda shuleni?

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, barabara zinazoenda shuleni, kwa sababu, Naibu Waziri ambaye yupo hapo, ndiye anayeshughulikia shule.

SPIKA: Naibu Waziri kusimama hapa haimaanishi anaulizwa swali lolote. Ni kwenye swali la msingi, ndiyo maana nimekuuliza ni barabara zinazoelekea shuleni?

MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, zinazoelekea shuleni kwa sababu, changamoto kubwa huwa ni maji na barabara.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi. Kuhusiana na swali lake la kwanza, naomba nimhakikishie kwamba, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha katika shule zetu za msingi na sekondari, huduma muhimu ya maji safi na salama inapatikana.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi uliowekwa, msingi wa ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa, halmashauri zina wajibu wa msingi wa kuhakikisha kwamba katika hizi shule zetu za sekondari na msingi maji safi na salama yanapatikana.

Mheshimiwa Spika, japokuwa Serikali Kuu huwa inaleta fedha katika baadhi ya miradi kwa ajili ya kusaidia katika eneo hili la upatikanaji wa maji safi na salama katika shule za msingi na sekondari, lakini wajibu wa msingi bado upo katika halmashauri zetu. Hivyo, nichukue nafasi hii kuendelea kuwakumbusha Wakurugenzi kuhusiana na suala hili na jukumu lao la msingi la kuhakikisha kwamba, katika shule zetu za msingi na sekondari, maji safi na salama yanapatikana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameleta mitambo 26 katika kila mkoa Tanzania Bara kwa ajili ya uchimbaji wa visima. Kwa hiyo, Wakurugenzi watumie nafasi hii, wawasiliane na mamlaka za maji za mikoa kupitia Ofisi ya RAS, ili waweze kupata mitambo hii kwa gharama nafuu na kwenda kuchimba visima katika shule zao Pia kuna namna nyingine nyingi za upatikanaji wa maji safi na salama na waweze kutumia nafasi hiyo.

SPIKA: Mheshimiwa tumeelewa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, kuhusiana na upatikanaji au ujenzi wa barabara kuelekea katika maeneo ya shule zetu hizi, Serikali inafanya hivyo, inatambua kwamba, ili shule zetu ziweze kufikika kirahisi zinahitaji barabara nzuri.

Mheshimiwa Spika, kila mwaka wa fedha Serikali inatenga bajeti, kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara zetu za wilaya na kipaumbele kinawekwa kujenga maeneo yale ambayo yanaelekea katika shule, vituo vya afya na maeneo mengine yanayotoa huduma za msingi kabisa katika jamii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mwantumu Zodo, Serikali itazingatia ushauri wake.

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: - Je, lini Serikali itaweka mkakati madhubuti wa upatikanaji wa maji ya uhakika kwenye Shule za Msingi na Sekondari nchini?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali, imejenga vyoo kwenye shule nyingi sana, lakini vyoo vingi ni vya kutumia maji (flush toilets). Kwenye maeneo ambayo hawajapeleka miradi ya maji kwa ajili ya flush toilets, ni lini Serikali itapeleka huduma hiyo?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Joseph Kakunda kwamba, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha katika shule zetu za msingi na sekondari huduma ya maji safi na salama inapatikana. Kwa misingi ya ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, halmashauri zina wajibu wa msingi wa kuhakikisha kwenye hizi shule zetu maji safi na salama yanapatikana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kutoa msisitizo, kuwakumbusha Wakurugenzi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa msingi wa kupeleka huduma za maji safi na salama katika shule zetu ili wanafunzi wapate mazingira mazuri.