Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdul Yussuf Maalim

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Amani

Primary Question

MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM aliuliza: - Je, tathmini ipoje juu ya maendeleo ya kaya maskini zilizodhaminiwa na TASAF kwa upande wa Zanzibar?

Supplementary Question 1

MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa fedha hizi za Mfuko wa TASAF huwa zinachelewa, je, Serikali ina mkakati gani wa kuharakisha fedha hizi ili ziweze kunufaisha wananchi kwa wakati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza wanufaika wa Mfuko huu wa Maendeleo wa TASAF ili kuweza kuwanufaisha wananchi wakiwemo wa Jimbo la Amani? (Makofi)

Name

Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nimpe pole Mheshimiwa Abdul kwa matatizo aliyoyapata, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu, amerudi akiwa salama na anaendelea kupambana kuwatetea wananchi wake wa Jimbo la Amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali yake mawili ya nyongeza, kwanza ameuliza habari ya fedha za Miradi ya TASAF kuchelewa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, siyo kwamba fedha hizi zinachelewa, isipokuwa utekelezaji wa miradi hiyo unahusisha wadau mbalimbali. Kwa mfano, tunapopeleka fedha zile zinakwenda kuhudumia sekta ya elimu, maji na afya. Sasa pale kuna wadau kama Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya na Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na michakato mingi, lakini sisi pamoja na hawa wadau tumekaa, tumeweza ku-stream line na baada ya hapo tumeboresha zaidi kupunguza urasimu ili fedha hizo zifanye kazi kwa wakati na kuwanufaisha wananchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuondoe shaka, tutahakikisha jambo hilo linafanyika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuongeza wanufaika ni kweli baada ya programu hii kukamilika mwitikio umekuwa mkubwa na kila mahali watu wanataka kunufaika na mpango huu wa TASAF. Nakuhakikishia kwamba, baada ya awamu hii ya pili kukamilika, mwezi Septemba mwaka huu tunakuja na awamu ya tatu, na awamu hii Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha wanufaika wanakuwa wengi zaidi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)

Name

Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM aliuliza: - Je, tathmini ipoje juu ya maendeleo ya kaya maskini zilizodhaminiwa na TASAF kwa upande wa Zanzibar?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, tulipokuwa tunahamasisha sensa, tulikuwa tunawahakikishia wananchi kwamba kati ya matumizi ya takwimu zile, ni kutathmini upya zile orodha za watu wanaonufaika na TASAF, na kulikuwa na maswali mahsusi kuhusiana na hali ya umaskini kwenye kaya.

Mheshimiwa Spika, nataka nimwulize Mheshimiwa Waziri, je, ni lini sasa watatumia zile takwimu ili kuhakikisha kwamba kaya kadhaa za wananchi wa Vunjo ambazo wanaendelea kulalamika wanapata haki yao? (Makofi)

Name

Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kimei, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika utekelezaji wa awamu ya pili ya TASAF kulikuwa na changamoto na malalamiko mengi. Baada ya kutambua hilo, ili kuboresha zaidi, Ofisi ya Rais, Utumishi tukishirikiana na taasisi nyingine kama Wizara ya Fedha kupitia Ofisi ya Takwimu, tumekaa pamoja na tayari tumefanya tathmini.

Mheshimiwa Spika, katika mpango mwingine, kwa maana ya awamu ya tatu ya TASAF itakayoanza baada ya Septemba, 2025, tutahakikisha tunatumia hizi taarifa ambazo tunashirikiana na Ofisi ya Takwimu kuhakikisha kwamba yale manung’uniko na lawama zote tunazimaliza kwa kuhakikisha wale walengwa sahihi wananufaika na mfuko huu, ahsante. (Makofi)