Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Asia Abdulkarim Halamga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza:- Je, lini Wananchi waliolipia upimaji watapewa Hati za umiliki wa Ardhi - Hanang?

Supplementary Question 1

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri na niende sasa kwenye maswali yangu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kwa muda mrefu sasa ni zaidi ya miaka miwili Kata ya Masakta, Ishponga, Dirma, Balangdalalu, Mogitu, Gitting bado wananchi hawajapata hati zao huku wakiwa wamepata watu wachache tu, je, ni lini Serikali itakamilisha utoaji wa hati kwa kuwa limekuwa ni suala la muda mrefu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ambalo ni sawa na ombi: Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kwenda sasa Wilaya ya Hanang ili kwenda kutoa hati hizo kwa wananchi wa kata nilizozitaja pamoja na maeneo mengine ya Wilaya ya Hanang?

Name

Geophrey Mizengo Pinda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa haki za wananchi wa Hanang. Kwa kweli tunakiri kwamba ni mfuatiliaji mzuri sana.

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye majibu ya maswali yake mawili; moja, ni kwamba zoezi la kutambua maeneo haya linaendelea na mpaka sasa mkononi katika hatua za mwisho za kukamilisha tunazo karibu hati 300 ambazo wakati wowote zinaenda kutolewa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja yake ya pili kwamba lini naweza kwenda huko, kwanza nikiri kwamba nitakwenda na hizo hati ninaenda kutoa mimi mwenyewe ili kuzungumza na wananchi vilevile katika suala zima la kuwashukuru kwa uvumilivu wao wakati wa zoezi hili. Ni kweli ni muda mrefu na ni miaka miwili, ahsante.