Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Latifa Khamis Juwakali

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatambua Vijana wenye ujuzi ambao hawatambuliki rasmi ili kuwaendeleza?

Supplementary Question 1

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijana wengi ambao wamepata ujuzi usio rasmi Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini Serikali bado haiwatambui. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kushirikiana na Wizara hii ya Vijana pamoja na Wizara yetu ya Elimu, ili kuwasaidia vijana hawa kuingia katika mfumo rasmi ikiwemo angalau kupata vyeti ili waweze kujisaidia katika ajira? (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninaomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Latifa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba, Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwenyewe alivyokutana na vijana pale Mwanza, ikiwa ni kundi la kwanza baada ya kuingia katika nafasi ya Urais. Alipokea changamoto nyingi sana, lakini alieleza mikakati na mipango mingi ambayo ililenga kukusudia kuwanyanyua vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya changamoto kubwa ilikuwa hii ya vijana wengi kuwa na ujuzi, lakini haujarasimishwa. Kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais na vilevile maelekezo ya utekelezaji ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwamba tuanzishe programu maalum ambayo inaitwa recognition of prior learning, tulifanya hivyo kwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na VETA. Hadi sasa zaidi ya vijana 686 kwa kupitia programu ya Building Better Tomorrow walirasimishiwa ujuzi na wanapata vyeti kwa ajili ya kutambulika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, vijana 500 wamepata vyeti kwa maana ya kutambuliwa ujuzi wao ambao wamepata mafunzo ya ziada pamoja na vijana 234 ambao nao walirasimishiwa ujuzi wao wa unenepeshaji wa mifugo kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, lakini vivyo hivyo, katika programu yote kwa ujumla kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na 2024/2025 tayari vijana zaidi ya 20,334 wameweza kurasimishiwa ujuzi kwa kupata mafunzo kwenye kada mbalimbali zikiwemo Ufundi, Useremala, Ushonaji, Uashi na pia kwenye programu nyingine za ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumewatumia vijana hawa kupitia halmashauri katika utaratibu wa force account, ambapo wametumika katika kufanya ujenzi. Hata wale waliofanya kwenye miradi mikubwa ambayo Dkt. Samia Suluhu Hassan ameikamilisha, Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na ule Mradi wa SGR walijifunza kupitia ujenzi na sasa tunawarasimishia ujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi yao wanajiandaa kuendelea na masomo katika vyuo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha ujuzi wao na tutawatumia katika kazi za maintenance. Ahsante.