Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Charles Stephen Kimei
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Primary Question
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza:- Je, ni Shule zipi chakavu katika Jimbo la Vunjo zimewekwa kwenye Mpango wa kufanyiwa ukarabati?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, kusema kweli Jimbo la Vunjo lina shule nyingi chakavu na mazingira yake yanatishia na ni hatarishi kwa wanafunzi. Kuna Shule kama Yamu, kule Kirua Vunjo Kusini, Lekura, Mamba Kusini, Maande, Mamba Kaskazini, Lotima, Makuyuni, Lole, Mwika Kaskazini, Maua, Kilema Kaskazini, Nduoni, Kirua Vunjo, Uria, Kahe Magharibi, Mangaria, pamoja na Mawanda na Makunduchi, kule Kirua Vunjo Magharibi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza; ninaomba Serikali itupe uhakika kwamba, katika mwaka huu unaokuja basi hizi zitaingizwa kwenye bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ninaomba Waziri akubali kutembelea angalau baadhi ya hizi shule ili aone mazingira yaliyopo. Tafadhali, tafadhali! Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri atutembelee ili awape watu uhakika kwamba kweli anafahamu mazingira ya kule Vunjo kwenye Shule za Msingi. (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei kwa kuuliza maswali haya ya msingi kabisa kwa lengo la kutetea wananchi wake kwenye Sekta ya Elimu katika jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Bajeti 2023/2024 Serikali ilileta jumla ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Njiapanda, lakini katika Mwaka wa Bajeti 2024/2025, Serikali inaleta fedha kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Kahe; Miruneni, Horia, na Rua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ushauri wake wa kwamba niweze kutembelea katika jimbo lake kuona miundombinu ya shule hizi chakavu anazozitaja, nimeupokea na nitaweka kwenye ratiba ili niweze kufika nijionee mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati wa shule hizi chakavu na zikiwemo nyingine nyingi ambazo zipo kwenye jimbo lako.
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza:- Je, ni Shule zipi chakavu katika Jimbo la Vunjo zimewekwa kwenye Mpango wa kufanyiwa ukarabati?
Supplementary Question 2
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Hai, tuna shule 77 ambazo ni chakavu sana, kwa sababu shule zetu zimejengwa kuanzia mwaka 1952 na kuendelea. Nimeshawasilisha andiko maalum TAMISEMI la kuomba fedha za kufanya ukarabati, Shule kama Kyuu, Lerai, Mroma, Lukani, Weruweru, Lyamungo, Laskika, Lambo-Estate, Nkwamakuu, Mkoraya, Tumona, Gezaulole, Nkokashu, Kwa Sangire na nyingine ziko 77 ni chakavu sana. Je, ni lini Serikali itatuletea fedha ya kufanya marekebisho na matengenezo ya shule hizi? Ahsante.
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, kwa kweli amekuwa akipaza sauti yake kwa ajili ya wananchi wake wa Hai ili waweze kupata miundombinu iliyo bora katika Sekta ya Elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba, maombi yao rasmi tuliyapata, tumeyapokea, tunayachakata na nimhakikishie kwamba Serikali italeta fedha ili iweze kuzifikia shule hizo katika jimbo lako kwa ajili ya kuzifanyia ukarabati.
Name
Michael Constantino Mwakamo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Primary Question
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza:- Je, ni Shule zipi chakavu katika Jimbo la Vunjo zimewekwa kwenye Mpango wa kufanyiwa ukarabati?
Supplementary Question 3
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, uchakavu wa shule za msingi katika Jimbo la Kibaha ni mkubwa na tulishaleta maombi maalumu kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati wa Shule ya Ngwale, Dutumi, Maghindu, pamoja na Kipangege. Ni lini Serikali itatutengea pesa na kutupatia ili tuweze kuzifanyia ukarabati?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake makini sana linalolenga kuwasemea wananchi wake kuona wanapata mazingira mazuri ya wanafunzi kusomea, kwa maana ya kuboresha Sekta ya Elimu katika jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilifanya tathmini ya hali ya miundombinu ya elimu kwa maana ya elimu ya msingi na sekondari mwaka 2022/2023 na ikabaini kwamba katika miundombinu asilimia 5.3 ni mazingira au miundombinu ambayo inahitaji kubomolewa na kujengwa upya kwa maana ipo katika hali mbaya kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kuna asilimia 24.4 ambazo zinahitaji ukarabati mkubwa, kuna asilimia 44.1 ya miundombinu katika Sekta hii ya Elimu ambayo inahitaji ukarabati mdogo na 26.2% ya miundombinu katika Sekta ya Elimu ambayo ipo katika hali nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa wakati huu Serikali inajitahidi sana na inafanya uwekezaji wa kipaumbele kwenye miundombinu inayokabiliwa na hali mbaya sana, inayohitaji kubomolewa na kujengwa upya, pamoja na ile inayohitaji ukarabati mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, maombi yao tumeyapokea, tunayachakata na lengo la Serikali ni kufikia maeneo mengi yenye uhitaji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, Serikali itafika ili iweze kuleta fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu chakavu katika jimbo lako.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved