Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Innocent Edward Kalogeris
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini
Primary Question
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga vituo vya afya Kata ya Singisa na Bwakila Juu katika Jimbo la Morogoro Kusini?
Supplementary Question 1
MHE. INNOCENT E. KALEGORIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini ninataka nijue, swali la kwanza; ni idadi ya watu wangapi ambacho ndicho kigezo cha kuwa na kituo cha afya, wakati sera tuliyokuwa nayo nyuma ilikuwa inazungumzia suala la kila kata kuwa na kituo cha afya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Kata ya Singisa katika mazingira iliyopo inaonekana kwamba inaweza kukidhi vigezo. Je, katika vile vituo vya afya ambavyo tuliahidiwa kila Mbunge hapa Bungeni, je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa kupeleka kituo cha afya hicho katika Kata ya Singisa? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ujenzi wa vituo vya afya unazingatia vigezo kadhaa, moja ya kigezo ni idadi ya wananchi katika eneo husika na kiwango cha chini cha wananchi ambao wanaweza wakafikiriwa kujengewa kituo cha afya ni wananchi wasiopungua 15,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na idadi ya wananchi kuna vigezo vingine kama umbali kutoka kituo cha jirani zaidi cha huduma, lakini na hali ya kijiografia ya eneo husika. Kwa hiyo, kwa Kata ya Singisa kwa idadi hii ya wananchi tunaamini hii ni sensa ya 2022 walikuwa 14,000 na zaidi wanaweza wakawa wameshafika 15,000. Kwa hiyo, tutafanya tathmini ya kuona uwezekano wa kujenga kituo cha afya katika Kata hii ya Singisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la vituo vya afya kwa kila jimbo. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikwishatoa maelekezo kwa ajili ya kujenga vituo vya afya kila jimbo katika majimbo yote Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge ikiwa kipaumbele cha jimbo lake ni kituo cha afya katika Kata ya Singisa, sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI tulishaomba wawasilishe mapendekezo ya kata hizo na ikiwa uliwasilisha pendekezo la kata hii tutahakikisha fedha ikipatikana inakwenda kujenga kituo cha afya katika kata ambayo umeipendekeza. Ahsante. (Makofi)
Name
Nicholaus George Ngassa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igunga
Primary Question
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga vituo vya afya Kata ya Singisa na Bwakila Juu katika Jimbo la Morogoro Kusini?
Supplementary Question 2
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana. Kwenye Jimbo la Igunga, Kata ya Kining’inila Serikali ilikuwa imetuahidi kutujengea kituo cha afya kupitia hiyo Programu ya Fedha za World Bank kwa ajili ya kuwahudumia Wananchi wa Kata ya Kining’inila, Mwamashimba, Mwamakona, Mbutu na Isakamaliwa. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huu wa kituo hicho cha afya? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa vituo vya afya kupitia Benki ya Dunia kwa maana ya Mradi wa TMCHIP na ni kweli kwamba Jimbo la Igunga lina kata ambayo imeingizwa kwenye huu mpango pamoja na majimbo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali imeshaanza utekelezaji wa awamu ya kwanza katika vituo vyote ambavyo vimewekwa kwenye mpango huo. Hivi karibuni tutakwenda kwenye mpango awamu ya pili ambapo vituo vingine vyote na zahanati ambazo zimeainishwa zitapelekewa fedha kwa ajili ya utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kata yako hiyo ipo na ni kipaumbele na ipo kwenye mradi huu. Tutahakikisha fedha inakwenda kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved