Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Kisasa cha Mabasi - Namtumbo?

Supplementary Question 1

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo yametupa mwanga. Swali la kwanza; kwa kuwa kutokuwepo kwa stendi hiyo kunasababisha watu wengi sana kupata ajali za pikipiki, bodaboda na bajaji wakati wakiunganisha kwenye vituo vidogovidogo. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka zoezi hilo kufanyika kwa haraka zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa hali iliyopo Namtumbo inafanana kabisa na hali iliyopo Moshi Manispaa, ni lini stendi ya Ngagamfumuni itakamilika? Ahsante sana.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni kweli kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ina idadi kubwa ya wananchi wapatao 271,000 na haina stendi kubwa ya mabasi kwa maana ya stendi ya wilaya. Serikali imeweka mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba halmashauri zetu zinakuwa na stendi za kisasa ili kutoa huduma bora zaidi za usafiri kwa wananchi. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tayari Serikali imetoa maelekezo kwa Halmashauri ya Namtumbo na wamekwishaandaa andiko na wameshatenga eneo kazi inayobaki sasa ni kufanya tathmni ya andiko hilo na fedha itatafutwa kwa ajili ya kujenga stendi hiyo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo nzuri ya usafiri kama ilivyo dhamira ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali hii ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusiana na stendi katika Manispaa ya Moshi, tunatambua kwamba Serikali imeshapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi lakini kuna changamoto zilijitokeza kati ya manispaa na mkandarasi; Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Manispaa ya Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro tunaendelea kutatua ule mkwamo ili ujenzi wa stendi uweze kuendelea na wananchi wa Manispaa ya Moshi wapate stendi iliyo bora zaidi. Ahsante. (Makofi)

Name

Stella Simon Fiyao

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Kisasa cha Mabasi - Namtumbo?

Supplementary Question 2

MHE. STELA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru. Ninataka kujua Serikali ina mpango gani wa kujenga stendi nzuri na ya kisasa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ileje?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba halmashauri zetu ambazo zina idadi kubwa ya wananchi zinakuwa na stendi bora kabisa kwa ajili ya huduma za usafiri. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ni moja ya halmashauri ambazo zitawekwa kwenye mpango huo na kupewa kipaumbele ili stendi hiyo iweze kujengwa. (Makofi)

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Kisasa cha Mabasi - Namtumbo?

Supplementary Question 3

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi kubwa ya Mkoa katika Eneo la TACRI pale Vwawa?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Hasunga ameuliza swali hili mara kadhaa na Waheshimiwa Wabunge wote wa Mkoa wa Songwe, lakini ninaomba niwahakikishie tu kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Serikali sikivu sana na tayari tumeshaweka mpango kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Songwe na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi ya mabasi katika eneo la Vwawa katika Mkoa wa Songwe. (Makofi)

Name

Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Kisasa cha Mabasi - Namtumbo?

Supplementary Question 4

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, haina stendi ya mabasi yaendayo Kusini, je, Serikali haioni ipo haja kwa sasa kutumia ile stendi ya mwendokasi kama stendi ya mabasi yaendayo kusini?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa stendi ya mwendokasi una madhumuni mahsusi kwa ajili ya kupunguza msongamano wa mabasi katika Jiji la Dar es Salaam na kwa hivyo ni vema sana tusimame kwenye mpango wa matumizi wa stendi ile ya Mwendokasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua sana kwamba Manispaa ya Temeke haina stendi kubwa na hasa ya Mikoa ya Kusini. Ninafahamu kulikuwa na mpango wa kujenga eneo lile linalopakana na Temeke pamoja na Mkuranga kuna eneo kubwa liliainishwa kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi yanayokwenda Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaendelea kufanya tathmini na kuandaa bajeti kwa ajili ya ujenzi wa stendi katika Manispaa ya Temeke, lakini pia stendi kwa ajili ya mabasi yanayokwenda kusini mwa Tanzania. (Makofi)