Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE K.n.y. MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa mafunzo kwa Watumishi wa Umma ili kuendana na kasi ya maendeleo na kuongeza ufanisi?

Supplementary Question 1

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; katika miaka minne ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeajiri takribani watumishi 140,000. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inatoa mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya ambao wanaajiriwa katika utumishi wa umma?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba taasisi zinapanga bajeti ya mafunzo kwa watumishi kazini?

Name

Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Simon kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia mambo ya watumishi hasa wa Jimbo lake la Busega. Nikianza na suala la mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya, ni kweli Serikali kwa kipindi hiki cha miaka minne imeweza kuajiri watumishi takribani 140,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mwaka 2011 Serikali ilitoa waraka kwa taasisi zote za umma kuhakikisha watumishi wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza wanapewa mafunzo elekezi ndani ya miezi sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutumia Bunge hili Tukufu kukumbusha waajiri wote, wanapowapokea waajiriwa kwa mara ya kwanza wahakikishe wanawapa mafunzo hayo elekezi ili waweze kujua taratibu, misingi ya utumishi wa umma, kanuni na sheria na pia utendaji bora katika utumishi wa umma. Hii imeelezwa wazi kwamba wale wanaoajiriwa Serikali Kuu na mashirika ya umma watapewa mafunzo na Chuo chetu cha Utumishi wa Umma; wale wanaoajiriwa kwa maana ya Serikali za Mitaa jukumu hilo kimepewa Chuo cha Serikali za Mitaa pale Hombolo; na wale wanaoajiriwa kwa kada za sheria watatakiwa kupata mafunzo elekezi na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa maana ya Lushoto. Ninashukuru sana.

NAIBU SPIKA: Ahsante.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, anataka kujua juu ya bajeti, tayari Serikali tulishatoa waraka kwa maana Ofisi ya Rais, Utumishi, kuhakikisha waajiri wote kwa mwaka huu wa fedha wanatenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya mafunzo na mwishoni mwa mwaka huu wa fedha tutafanya tathmini tuone utekelezaji wa jambo hilo kwa kuwa ni muhimu katika ufanisi wa watumishi wetu wa umma, ninakushukuru.