Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:- Je, Serikali imefanya Tathmini ya kujua ni Miti mingapi inayopandwa inatunzwa na kukua ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi?

Supplementary Question 1

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu hayo ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; nataka kujua mkakati wa Serikali ni upi ili kuhakikisha miti yote inayopandwa inatunzwa na kukua ili kufikia malengo yaliyokusudiwa, kwani inatumia pesa nyingi na muda mwingi wa wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; nataka kujua kuna mkakati gani wa kuwashirikisha wanafunzi hasa wa shule za msingi kuwa na tabia ya kupanda na kutunza miti katika mazingira yanayowazunguka, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi? Nakushukuru sana.

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto ya Watanzania wengi kupanda miti na hatimaye inakuwa haipati ufuatiliaji. Hata hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, tumechukua hatua mbalimbali; moja ni kwamba, tunao maafisa wetu, viungo, katika mikoa na halmashauri zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapopanda miti tunakuwa tunawapa maelekezo waifuatilie. Vilevile, tunao utaratibu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa baadhi ya barabara na baadhi ya maeneo huwa tuna utamaduni wa kumwagilia maji na kufuatilia miti hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo na madhumuni ni kwamba, kama tumepanda miti milioni moja, tuhakikishe ile miti inakua na inafikia lengo la kutunza mazingira, lakini kupitia ziara zetu za mara kwa mara katika maeneo tofauti na kupitia matukio tofauti, huwa tunapanda miti na kuiendeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu wanafunzi, wakati ule Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, alipokuwa Makamu wa Rais alianzisha kampeni mbalimbali za utunzaji wa mazingira. Alianzisha kampeni ya kutunza vyanzo vya maji, clean cooking na kampeni maalum ya kusoma na mti, ambapo Serikali ilikuwa inawataka wanafunzi wote wa shule za sekondari, msingi, vyuo na vyuo vikuu, wahakikishe kuwa wanapanda miti wakati wapo vyuoni na shuleni, lengo na madhumuni ni miti hii iweze kukua kwa muda uliokusudiwa. Nakushukuru.

Name

Maryam Omar Said

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Pandani

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:- Je, Serikali imefanya Tathmini ya kujua ni Miti mingapi inayopandwa inatunzwa na kukua ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi?

Supplementary Question 2

MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani katika kuhakikisha inaviongezea nguvu vikundi vinavyojishughulisha na upandaji miti kandokando ya bahari ili kurudisha uoto wa asili?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto kubwa ya baadhi ya watu kukata miti iliyopo pembezoni mwa kandokando ya Bahari hasa miti ya mikoko na mwisho wa siku wanaharibu mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, zipo jitihada ambazo tumezifanya; kwanza, tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi, ili kuwaeleza umuhimu wa uwepo wa mikoko. Sasa hivi kumekuwa kuna changamoto kubwa, maji ya bahari kuingia kwenye makazi, kuingia kwenye vipando vya wananchi visivyostahimili maji ya chumvi. Hii yote ni kwa sababu, mikoko imekatwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kuendelea kutoa mikoko bure ili iendelee kupandwa kwenye yale maeneo ya bahari, lakini zaidi kuendelea kutoa miradi. Pia, miongoni mwa miradi inayotolewa katika Ofisi ya Makamu wa Rais ni pamoja na upandaji wa miti pembezoni mwa bahari, hasa miche ya mikoko. Nakushukuru.