Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Conchesta Leonce Rwamlaza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: - Je, lini Serikali itatunga sheria itakayolinda utoaji wa huduma za matibabu bure kwa wazee na watoto?
Supplementary Question 1
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, Sera ya Afya ya nchi yetu inatamka wazi kwamba, wazee na watoto wanapaswa kupata huduma ya afya bila malipo. Nakubaliana na Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kuna Sheria ya Bima ya Afya ambayo haijatekelezwa mpaka sasa hivi. Nia yangu kuuliza swali hili ni kutaka kujua, wazee kama hawakupata huduma stahili kutoka kwa mtoa huduma, ni ipi kinga yao? Yaani wanaweza kwenda kulalamika wapi ili waweze kusaidiwa kuhakikisha huduma yao inatolewa?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Magonjwa ya wazee ni mengi. Ukitaka kuyakwepa, ufe haraka. Mengi yanahitaji wataalamu kama ilivyo kwa watoto. Nashukuru katika nchi yetu watoto wanapata huduma zao na wana madaktari wao, sasa ni lini Serikali itahakikisha kwamba wazee wanapata madaktari wao ambao ni wataalamu bobezi kuhusu magonjwa ya wazee? (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa Mkoa wake wa Kagera, lakini kwenye eneo hili la kuwatetea wazee, amekuwa akifanya kazi nzuri, ndiyo maana natamani kumwambia Tundu Lissu ahakikishe huyu mama anarudi humu Bungeni tena kwa mara ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ameuliza maswali mawili ya msingi sana. Swali lake la kwanza ni kuhusu wazee na huu mfuko. Kwanza hili suala la Bima ya Afya kwa Wote siyo kwamba halijatekelezwa, ni bado Bunge mnaendelea kutushauri kuhakikisha tunafanya vizuri hili jambo likae vizuri.
Mheshimiwa Spika, la pili kuhusu wazee, ni kwamba wanahudumiwa, ndiyo maana nilisimama hapa Bungeni nikasema Serikali inatumia shilingi bilioni 661 kwenye eneo hili la exemption. Maana yake wazee wakiwa ni moja ya sehemu, lakini kwenye mfuko wetu wa Bima ya Afya inatumika shilingi bilioni 187 kutibu wazee, na hao wazee hawachangii kwenye Mfuko wa Bima ya Afya.
Mheshimiwa Spika, hivyo, nakubaliana na Mbunge kwamba hatuwatibu wazee kwa 100%. Ni kweli hatujafikia 100% ndiyo maana tumekuja na Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ili kutenga lile kundi la watu wasiojiweza 26%, ili tukishaingia kwenye Bima ya Afya tuwezeku-cover tufike 100% kama ambavyo anasisitiza Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunachukua wazo la Mheshimiwa Mbunge na tutaendelea kuchakata na wakati wowote tutaongeza nguvu kwenye eneo hilo kama ambavyo ametamani liwe.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba wazee wanahitaji madaktari maalumu, ni wazo zuri mno kwa sababu kwanza tunakwenda kwenye Samia Scholarship ambapo sasa hivi Mheshimiwa Rais wetu ametoa scholarship kwa ajili ya madaktari. Kuna madaktari ambao wanakwenda, na wanaenda pia ku-specialize kwenye eneo hilo la kuwahudumia wazee.
Mheshimiwa Spika, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba magonjwa ni yale yale, hata ma-specialists (madaktari bingwa tulionao) magonjwa ya madaktari bingwa ni hayo hayo, lakini wazee wanahitaji uangalizi maalumu kisaikolojia na kisosholojia na ndicho anachokisema. Tutakwenda kuwekeza kwenye eneo hilo na tutaweka rekodi kwamba ni mojawapo ya mambo ambayo dada yangu au mama yangu amehakikisha yanatokea kwenye eneo letu la afya.
Name
Janeth Elias Mahawanga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: - Je, lini Serikali itatunga sheria itakayolinda utoaji wa huduma za matibabu bure kwa wazee na watoto?
Supplementary Question 2
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kwa namna gani Serikali inashughulikia malalamiko ya wazee na watoto wanaokosa huduma za bure katika baadhi ya vituo vya afya na hospitali za umma?
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kuna utaratibu wa kuhakikisha yule ambaye hawezi kulipa kuna utaratibu uliowekwa ndani ya hospitali ambao unafuatwa na kuhakikisha wanapata huduma. Kama ambavyo Mheshimiwa anasema kwamba ni watoto, ni kweli sheria yetu inawataka watoto wote walipiwe na wale ambao watashindwa kulipiwa kuna utaratibu ambao uko ndani ya hospitali ambao unafuatiliwa.
Mhehimiwa Spika, nitumie tu fursa hii kuwaambia madaktari wetu na hospitali zetu za umma asiwepo Mtanzania anayekosa huduma eti kwa sababu hana fedha au jambo lolote.
Name
Agnes Elias Hokororo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: - Je, lini Serikali itatunga sheria itakayolinda utoaji wa huduma za matibabu bure kwa wazee na watoto?
Supplementary Question 3
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, pamoja na wazee, Sera ya Afya inataka watoto wachanga na akina mama wakati wa kujifungua wapewe huduma bure, je, hilo linahitaji sheria mpya ili litekelezwe?
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, hilo halihitaji sheria mpya ili litekelezwe. Ndiyo maana toka mwanzo kama mnakumbuka nilisema hapa kwamba tunatenga dawa shilingi bilioni 200, lakini kuhudumia tu eneo hilo la akina mama na watoto linahitaji shilingi bilioni 227. Ndiyo maana hapa nimezungumzia kwenye kusamehe (exemption) maana ya kutibu hilo kundi unalolisema tunatumia shilingi bilioni 661 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, ninachoweza kusema, ni kweli hawahudumiwi kwa 100%, ndiyo maana tumekuja na Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ili tuweze kwenda kufikia malengo ambalo ninyi Wabunge hapa mnatamani lifikiwe.
Name
Riziki Saidi Lulida
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Primary Question
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: - Je, lini Serikali itatunga sheria itakayolinda utoaji wa huduma za matibabu bure kwa wazee na watoto?
Supplementary Question 4
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru. Hata ukisikiliza majibu ya Mheshimiwa Waziri, hakutaja watu wenye ulemavu hasa watoto chini ya miaka mitano hawamo katika jumuishi ya matibabu hayo.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha hili kundi maalumu la watu wenye ulemavu wakiwemo watoto wa chini ya miaka mitano wanakuwemo katika jumuishi na kupata haki ya matibabu bure? Ahsante.
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwa kweli katika fedha zote ninazozitaja hapa za exemption, hata unapozungumzia mama na mtoto unamaanisha na mtoto chini ya miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, hili eneo nataka kuwaambia, linafanyiwa kazi vizuri na ndiyo maana unaona Mheshimiwa Rais wetu ameleta mashine maalumu ambazo zimesaidia watu ambao wamekuwa miaka sita mpaka kumi ya nyuma na watoto ambao wamezaliwa bila kusikia, sasa wanasikia na uliona walitibiwa bure pale Muhimbili. Makamu wa Rais alikwenda na akabonyeza kitufe na wakaanza kusikia wote kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, eneo hili wakati wote linazingatiwa na kwenye hospitali zetu zote tunaendelea kuhakikisha sasa hivi zile process na vitu vyote vinavyoweza kuwasaidia walemavu zinafanyika na tunaweka utaratibu mzuri wa kuwasaidia hao walemavu na wao waweze kuishi maisha kama watu wengine.
Name
Edward Olelekaita Kisau
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Primary Question
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: - Je, lini Serikali itatunga sheria itakayolinda utoaji wa huduma za matibabu bure kwa wazee na watoto?
Supplementary Question 5
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wazee hawa (wastaafu) wamekuwa na taabu nyingi za kuja kuhakiki taarifa zao za NHIF, kwa nini msiweke mpango mwafikie hawa wastaafu maeneo walipo, wajikusanye na mkawapa taarifa maalumu? Nakushukuru (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Olelekaita ameandika barua Wizara ya Afya akilielezea hili eneo kwamba wazee wanatakiwa wasije hapa Dodoma au kwenda kwenye ofisi za mikoa kuhudumiwa kule.
Mheshimiwa Spika, tumeiona barua yake, nami ni kuwaambia sasa wale wazee wa Kiteto wakusanywe, na wataalamu wataenda Kiteto. Itakuwa hivyo kwa Waheshimiwa Wabunge wote sasa, watu watashuka kuwafuata wazee kule waliko. (Makofi)