Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kavejuru Eliadory Felix
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Primary Question
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza migogoro ya mipaka kati ya wananchi na hifadhi za misitu nchini?
Supplementary Question 1
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa juhudi na jitihada kubwa za kutatua migogoro. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Kitongoji cha Gatoto kinachopatikana katika Kata ya Kagera Nkanda na Kitongoji cha Gachele kinachopatikana katika Kata ya Rusesa, vyote katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, ni vitongoji ambavyo sasa ni miaka miwili tangu Serikali ipange kuvihamisha na maeneo yao kuwa sehemu ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, wananchi wa vitongoji hivi wanategemea kilimo kama shughuli zao za kiuchumi; katika msimu huu wa kilimo, TFS wameharibu mazao yao, ikiwa ni pamoja na tumbaku. Kwa kuwa, Serikali bado haijatekeleza agizo la kuwahamisha, kwa nini isiwaachie mazao yao wakavuna?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Serikali ilitoa hekta 10,000 kutoka kwenye Hifadhi ya Msitu ya Makere Kusini, sehemu ambayo ilikuwa imepoteza sifa ya uhifadhi, ikatoa kwa Halmashauri ya Kasulu. Mpaka sasa hivi yapo malalamiko ya wakulima wadogo wadogo katika Vijiji vya Nyachenda, Kitagata na Mgombe ambavyo havikupata kabisa…
SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, uliza swali.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, je, Serikali iko tayari kufuata mpaka ngazi ya chini ili kuangalia mgawanyo wa hizo hekta 10,000? (Makofi)
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, vitongoji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge kimsingi ni maeneo yaliyoanzishwa kwenye hifadhi. Vitongoji hivi viliacha vijiji mama vikaenda kuanzishwa ndani ya hifadhi. Kwa hiyo, uamuzi ulikuwa vitongoji hivi virejee kwenye vijiji mama. Maeneo haya ni kitalu cha uwindaji kinachosimamiwa na halmashauri na kwamba, shughuli zote za doria zinafanywa chini ya usimamizi wa halmashauri kwa kutumia askari wanaowapata wao.
Mheshimiwa Spika, mara ya mwisho jambo hili lilipokuja tulilifuatilia na kukawa na makubaliano kwamba, hakuna mazao ya wananchi yatakayofekwa na kwamba, halmashauri itafanya kazi ya kupanga maeneo haya ambayo wananchi wanatakiwa kuhamishiwa ili wananchi wahamishwe.
Mheshimiwa Spika, taarifa tulizonazo ni kwamba, katika kipindi hicho tangu tumetoa majibu yale, hakuna mazao ya wananchi yaliyofekwa, na kwamba sasa hivi halmashauri inakamilisha upimaji wa maeneo yale ili wananchi waweze kuhamishiwa eneo linalotakiwa.
Mheshimiwa Spika, rai yetu kama Wizara ni kwamba, kwa sababu, jambo hili liko chini ya usimamizi wa halmashauri, halmashauri ikamilishe kwa haraka upimaji wa maeneo yale ili wananchi waweze kuhamishwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ni kweli kwamba, Wizara tulipokea ombi la kugawa hekta 5,000 kwa ajili ya halmashauri hii. Tuligawa eneo hili na mara baada ya kugawa eneo hili, milki inahama kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, inahamia kwa halmashauri husika. Wao sasa ndio wana jukumu la kugawa ardhi hii kulingana na mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, rai yetu, na ni kwa sababu jambo hili limepigiwa kelele muda mrefu, tunaiomba Serikali ya Mkoa na ya Wilaya ilishughulikie jambo hili, ili wananchi waweze kupata maeneo kwa ajili ya kufanya shughuli zao.
Vilevile kwa sababu, ni jambo ambalo limekuwa likijotokeza mara kwa mara, Wizara itatuma timu mara moja ili kwenda kushauriana vizuri na wenzetu wa Serikali ya Mkoa na Halmashauri, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved