Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Primary Question

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: - Je, lini Serikali itachimba visima virefu vya maji kwenye taasisi za umma hususan mashuleni?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza niipongeze Serikali kwa kuleta miradi ya maji katika Jimbo la Muhambwe. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kumtua mwanamke ndoo kichwani Jimbo la Muhambwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, je, Serikali haioni kwamba iko haja sasa ya kuwa na programu maalumu ya kupeleka maji katika taasisi hizi za elimu na afya katika vijiji vyetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni mwaka mmoja sasa mitambo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopo katika Jimbo la Muhambwe imechimba kisima katika Kijiji cha Lusohoko ambacho kinatoa maji zaidi ya lita milioni moja kwa saa na nikushukuru Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika katika kijiji kile.

Je, Serikali haioni iko haja sasa ya kuleta mradi katika kijiji kile ili wananchi waweze kupata maji tofauti na sasa ambavyo maji yanapotea tu? (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Florence Samizi kwa kazi kubwa anayoifanya kwa wananchi wa Muhambwe. Nilifika katika eneo hilo na eneo hilo linatoa maji ya kutosha na visima ambavyo vimeshachimbwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, eneo la Lusohoko tayari Serikali imeshatangaza tender ya kumpata mkandarasi ambaye atakwenda kujenga mtandao wa maji ili uwafikie wananchi. Hiyo ni kwa ajili ya awamu ya kwanza, lakini kwa awamu ya pili tuna wataalamu pale ambao wameanza kufanya usanifu mradi mkubwa wa kutoka katika visima vilevile ili kwenda kusaidia vijiji 11 vikiwepo vijiji vya Bitale na Mji wa Kibondo wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba baada ya kukamilisha kwa huu mradi, basi utaweza kusaidia kuhakikisha kwamba wananchi wa eneo hilo wanapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kwamba Serikali inaendelea? Kama nilivyojibu swali la msingi, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba tunazingatia katika usanifu wetu. Taasisi za umma, vituo vya afya, shule, sekondari na hata taasisi za kidini, tunaendelea kushirikiana nao na sisi tutaendelea kufanya vikao vyetu na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Kilimo, Mifugo ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na programu ya pamoja tunapokwenda kutekeleza ili tusije kuwa na mwingiliano na kuwa na (duplicate of effort).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaamini kwamba tukifanya hivyo tutakuwa tumetatua changamoto hiyo. Napokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo amesema, ahsante sana.

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: - Je, lini Serikali itachimba visima virefu vya maji kwenye taasisi za umma hususan mashuleni?

Supplementary Question 2

MHE DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, Serikali ilichimba kisima katika eneo la Mtandika, Wilaya ya Kilolo, je, lini itatoa pesa za usambazaji katika eneo la Kichangani, Kituo cha Afya Ruaha Mbuyuni pamoja na eneo ambalo Mzee Julius anaishi na kujenga tenki la Ikula?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati amekuwa akifuatilia sana kuhusu eneo hili. Pia tunatambua kwamba kulikuwa na uhitaji wa fedha, napenda kutumia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali tumeshapeleka fedha na kazi inaendelea. Kitua cha Afya cha Ruaha Mbuyuni pamoja na Kichangani watapata maji safi na salama, ahsante.

Name

Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Primary Question

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: - Je, lini Serikali itachimba visima virefu vya maji kwenye taasisi za umma hususan mashuleni?

Supplementary Question 3

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Serikali imefanya kazi nzuri sana ya kuchimba visima kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini kupitia mitambo aliyoitoa Mheshimiwa Rais, tuna zaidi ya visima kumi.

Mheshimiwa Naibu Waziri, je, Serikali ipo tayari kutoa fedha kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya visima hivi ili viwasaidie wananchi kupata huduma ya maji kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hili tumeliona nchi nzima, programu ya visima 900 na mpaka kufikia Desemba, takribani visima 920 vilikuwa vimechimbwa kati ya visima 864 ambavyo tulikuwa tumepanga kuvichimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kabisa kwamba wananchi wanahitaji kupata maji. Sasa tulichoamua ni kwamba kabla hatujatengeneza miundombinu au ile point source ya wananchi kupata maji, basi tuna uwezo wa kuunganisha maji kwenye mtandao na wananchi wakaanza kupata maji wakati tukiwa tunaendelea kuzijenga zile point source.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunalipokea na kwa msisitizo mkubwa tutalifanyia kazi ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama kwa wakati, ahsante sana.

Name

Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Primary Question

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: - Je, lini Serikali itachimba visima virefu vya maji kwenye taasisi za umma hususan mashuleni?

Supplementary Question 4

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.

Kwa kuwa katika miji 28 iliyopata miradi mikubwa ya maji na Makambako tupo, je, Serikali mpaka sasa imefikia asilimia ngapi kwenye mradi mkubwa wa Makambako?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba Mji wa Makambako ni katika Mradi wa Miji 28 ambao unasimamia kutoka Njombe, Makambako na kuelekea jimbo moja ambalo liko upande wa Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili tulikuwa na mkandarasi ambaye kidogo kulikuwa na changamoto na baadaye akatafuta sub-contractor ambaye kidogo uwezo wake haukuwa unajitosheleza, tukatoa maelekezo ya kuhakikisha kwamba anambadilisha yule sub-contractor ili kazi iende kwa wakati. Mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo unakwenda vizuri. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali tumeweka jicho pale ili kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati kulingana na mkataba ambao tulisaini na mkandarasi, ahsante sana.