Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Bakar Hamad Bakar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Primary Question

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR aliuliza:- Je, kwa kiasi gani Zanzibar inanufaika na fedha zitolewazo na wadau wa maendeleo kupitia Serikali ya Muungano kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita?

Supplementary Question 1

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pia niipongeze Serikali kwa kuendelea kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha hizi kupitia wadau mbalimbali wa maendeleo. Nipongeze vile vile ushirikiano mkubwa wa Serikali zetu mbili ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, lakini nina maswali mawili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa utaratibu wa mgawanyo wa fedha hizi zinazotolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo utaratibu huu upo kwa muda mrefu sasa. Je, Serikali haioni ipo haja sasa kupitia upya utaratibu huu na kuweka utaratibu mpya ambao unaendana na wakati wa sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni miradi ipi ya maendeleo ambayo Zanzibar inanufaika kupitia fedha hizi? Ninakushukuru.

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bakar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana kwa kuwa amekuwa mdau mzuri wa mambo ya Muungano hasa katika kuielimisha jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu upo kwa mujibu wa sheria. Upo utaratibu maalum na utararibu huu ambao umewekwa umeshaeleza wazi kwamba Zanzibar kuna 4.5% na Bara ama kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa Tanzania Bara kuna 95.5%. Hata hivyo, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba bado vikao vinaendelea kukaliwa ili kuona namna ambavyo tunaweza tukaboresha zaidi utaratibu ili kuweza kuhakikisha kwamba tunaweka Muungano huu katika mazingira mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa miradi, miradi ipo mingi. Kuna miradi ya Covid ambayo ilisaidia kujenga shule, madarasa, hospitali pamoja na masoko. Kuna mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba tayari huo ni mradi ambao ulitokana na fedha hizi. Pia, kuna Mradi wa Ujenzi wa Barabara ambao nadhani kwa sasa umeshakamilika ambao unatoka Chake kupita Kisiwani kwa Binti Abeid kwenda Wete, kuna Mradi wa Barabara uliotoka Tunguu kuelekea Makunduchi pamoja na miradi mingi ya mazingira ambayo imetokana na fedha hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kutatua changamoto na kujenga miradi ya maendeleo ya mazingira katika maeneo ya Nungwi kwa Mheshimiwa Simai, Gando hata Lindi kutokana na changamoto kubwa ya uingiaji wa maji ya bahari katika maeneo ya wananchi. Ninakushukuru. (Makofi)