Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanua wigo wa maeneo mapya ya utalii nchini?
Supplementary Question 1
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; moja ya changamoto kubwa inayowakabili watalii kupanda Mlima Kilimanjaro au kufikia vivutio vya Mlima Kilimanjaro ni ubovu wa Barabara. Mifano ya barabara ambazo ni mbovu sana ni Barabara ya Kata ya Mbokomu inayopeleka watalii kuona mti mrefu kuliko yote Afrika na Barabara ya Umbwe ambayo inapeleka watalii kwenda mlimani. Kwa kuwa, kuna wingi wa kazi upande wa TARURA.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutumia pesa zinazotolewa kwa jamii inayozunguka Mlima Kilimanjaro, kama CSR, kufanya ukarabati wa barabara hizi, ikiwa ni pamoja na kuziwekea lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wa Kata ya Uru Shimbwe wamekuwa na kiu kubwa sana ya kujengewa lango la kuingia Mlima Kilimanjaro kupitia katika Kata hii, ili wananchi wapate ajira ikiwa ni vijana na wananchi wanaoishi pale. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wananchi hawa wapate hili lango?
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia KINAPA imekuwa na utaratibu wa kujenga barabara hizi zinazopeleka watalii kwenye maeneo ya vivutio vya utalii. Mfano kule Kilimanjaro tumeweza kujenga barabara ya kutoka kwenye Chuo chetu cha Mweka mpaka kwenye Lango la Mweka, lile ni eneo ambalo limefungua sana utalii kwenye maeneo yetu kwa hiyo, tutaendelea kufanya shughuli hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Mbunge; kwa sababu, fedha hizi za CSR zina umuhimu mkubwa sana wa kuwafanya wananchi wajione kuwa ni sehemu ya uhifadhi katika maeneo haya. Fedha hizi tuzielekeze kwenye shughuli hizi za elimu, maji na ulinzi wa mazingira. Ndani ya Serikali tutahakikisha tunatenga fedha za kutosha kuhakikisha TARURA nayo inatimiza majukumu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la pili la kufungua Lango la Shimbwe. Kwa sasa Serikali imejipanga kujenga barabara mbili, barabara ya eneo la Tesheni upande wa Kaskazini – Magharibi mwa hifadhi. Vilevile, kwenye njia ya kupandia kule Kidia na yenyewe ipo kwenye mpango wa ujenzi kwa sasa. Namwomba Mheshimiwa Mbunge aridhie kwamba, Serikali ijielekeze kwenye kukamilisha barabara hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lake tumelipata. Baada ya kukamilisha ujenzi huu, basi kulingana na upatikanaji wa fedha tutaendelea kufanya kwenye lile eneo alilopendekeza.
Name
Felista Deogratius Njau
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanua wigo wa maeneo mapya ya utalii nchini?
Supplementary Question 2
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Katika Jimbo la Moshi Vijijini kuna vivutio vingi yakiwemo makazi waliyokaa Mangi wetu kama Marealle, Mandara na Malamia. Je, ni lini Serikali itakarabati maeneo haya, ili Serikali iweze kuingiza kipato na wananchi wa pale, mmoja mmoja, waweze kupata ajira? Ahsante.
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, kutambua vivutio vipya vya utalii ni kazi endelevu. Miongoni mwa maeneo ambayo tumeyatambua ni pamoja na haya aliyoyasema Mheshimiwa Mbunge. Tunaomba atupe muda, ili tuweke huo mpango wa kuhakikisha kwamba, vivutio vyote hivi ambavyo tumevitambua vinafikika na viweze kutumika katika kuendeleza utalii katika nchi yetu.
Name
Zaytun Seif Swai
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanua wigo wa maeneo mapya ya utalii nchini?
Supplementary Question 3
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni upi mpango wa Serikali wa kutafuta wawekezaji wa kujenga hoteli za kitalii, hususan katika Mkoa wangu wa Arusha, ambazo zimekuwa ni changamoto kubwa?
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia taasisi zake imekuwa ikishiriki katika makongamano mbalimbali ya uwekezaji, kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji kuongeza nguvu kuwekeza katika maeneo ya malazi. Nimhakikishie kwamba, kupitia TTB na taasisi zetu nyingine jukumu hilo tunalifanya kwa umakini mkubwa kwa sababu, tunaelewa kwamba, tunayo changamoto ya maeneo ya malazi katika nchi yetu.
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Primary Question
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanua wigo wa maeneo mapya ya utalii nchini?
Supplementary Question 4
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Maporomoko ya Mto Kalambo ni ya pili Afrika, lakini ukweli usiopingika ni kwamba, matangazo hayajafanyika vya kutosha. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba, inatangaza ili yaweze kujulikana?
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Kandege kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Maporomoko ya Kalambo ni maporomoko ambayo yana sifa ya kipekee na moja ya zao muhimu sana kuendelezwa. Sisi Wizara tumekwishachukua jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba utangazaji wa maeneo haya unafanyika kwa nguvu kubwa. Kama anafuatilia, kwenye Ligi Kuu yetu ya Tanzania moja ya vivutio vinavyotangazwa kwa nguvu kubwa kwenye matangazo ya viwanja vyetu vya mipira na kwenye makongamano mbalimbali ya uwekezaji ni pamoja na kivutio hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira naamini ndani ya kipindi kifupi mambo mazuri yanakuja katika eneo hili.