Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Njombe – Kibena – Madeke - Lupembe kuelekea Mkoa wa Morogoro?
Supplementary Question 1
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini kwa sisi Wananjombe hususan watu wa Lupembe hii ilikuwa ni moja kati ya ndoto zao kuona Barabara inayotoka Morogoro inapita Mlimba inakuja hadi Lupembe, Njombe inajengwa na Serikali niiweke wazi kwamba wamefika kwenye hilo eneo na tayari mkandarasi anaendelea na taratibu nyingine. Kwa hiyo, kwa niaba ya Mheshimiwa Neema na Mbunge wa Jimbo pia tunashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo maswali yangu ni mawili. Swali la kwanza; je, ni lini hivyo vipande viwili vilivyobakia yaani upande wa Morogoro na upande wa kuja hadi Njombe Mjini vitaanza pia kutangazwa ili ianze kujengwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; wakati Waziri anajibu swali namba 38 alizungumza kuhusu kipande cha Makete, Kitulo kuelekea Mbeya Barabara ya Isyonje ni kweli mkandarasi amefika na ni kweli mkandarasi ameanza kazi, lakini hivi ninavyozungumza muda huu magari mengi yamekwama barabarani kwa sababu ya hali mbaya ya barabara. Ni yapi maelekezo ya Serikali muda huu kwa mkandarasi aweze kuyanasua na barabara iweze kupitika ili wananchi waendelee na shughuli za kiuchumi?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kujibu swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge. Katika kipindi hiki cha Masika na hasa pale ambapo tunakuwa na ujenzi tunakuwa na hizi barabara za mchepuko kwa maana ya diversions na maeneo mengi kwa sababu barabara inakuwa si imara sana kama barabara yenyewe mvua ikinyesha kubwa ama inaondoa tuta ama inafanya lile eneo lisipitike.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kumwelekeza Meneja wa Mkoa wa Njombe kuhakikisha kwamba anamsimamia mkandarasi ambaye yuko site kukwamua magari yote ambayo yamekwama ili wananchi wasipate hiyo adha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili la vipande vilivyobaki kutangazwa, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Njombe na hasa Mbunge wa Lupembe, sasa hivi tunavyoongea jana zabuni ilifunguliwa ishatangazwa kilometa 42 kutoka Kibena hadi Kijiji kinaitwa Kidegembe kilometa 42 ambayo yalikuwa ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tayari Zabuni imefunguliwa. Kwa hiyo, tunategemea kazi itaanza haraka iwezekanavyo. Ahsante.
Name
Godwin Emmanuel Kunambi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Njombe – Kibena – Madeke - Lupembe kuelekea Mkoa wa Morogoro?
Supplementary Question 2
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara hii ya Morogoro Njombe border kupitia Mlimba kipande cha kutoka Ifakara – Chita, Ifakara – Mbingu – Igima tayari mkandarasi yuko site. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba anijibu kwa nini mkandarasi hajaanza kazi na yuko site huu ni mwaka wa pili? Ahsante.
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunaposema barabara imeanza kujengwa ni kwamba taratibu zile za manunuzi na mkandarasi ameshaenda site tunajua kwamba tayari tumeshaanza mchakato wa kuanza kuijenga na ambacho kinafanyika sasa hivi ni kumlipa advance huyo mkandarasi. Kwa hiyo, kipande cha kwanza tayari ameshalipwa na tunategemea muda si mrefu kipande cha pili mkandarasi atalipwa. Hivi vipande vyote vinavyokamilisha kilometa 100 vianze kujengwa kwa kasi. Ahsante.
Name
Tecla Mohamedi Ungele
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Njombe – Kibena – Madeke - Lupembe kuelekea Mkoa wa Morogoro?
Supplementary Question 3
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Barabara ya kutoka Kiranjeranje – Nanjilinji – kwenda Ruangwa itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, hii Barabara ya Kiranjeranje kwenda Ruangwa tumeshaifanyia usanifu yote. Hata hivyo, hii barabara pia nataka nimjulishe Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba ina mito mingi mikubwa ambayo ilikuwa ni mtihani mkubwa kupita hapa. Tunachoongea sasa hivi madaraja matatu ambayo yako katika barabara hii Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatafuta fedha ambazo kwanza tutahakikisha tunayajenga hayo mdaraja ya kudumu likiwemo Daraja la Mto Mbwemkuru ambalo lilikuwa ni mtihani mvua ikishanyesha hapapitiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tukishakamilisha hayo madaraja sasa ndiyo tutaanza kujenga hiyo barabara yote kwa kiwango cha lami, lakini kwanza wananchi wawe na uwezo wa kupita kwa mwaka mzima. Ahsante.
Name
Issaay Zacharia Paulo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Njombe – Kibena – Madeke - Lupembe kuelekea Mkoa wa Morogoro?
Supplementary Question 4
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mkandarasi wa Kichina anayejenga Barabara ya Mbulu – Garbabi ametelekeza mradi huu kwa zaidi ya mwaka sasa na kwa kuwa barabara hiyo imekuwa kero kubwa sana kwa wananchi wa Mbulu. Je, ni lini Serikali itamrudisha huyu mkandarasi ili akamilishe kazi iliyoko kwenye mkataba wake?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tayari Mheshimiwa Mbunge alishafika ofisini na kutoa hiyo changamoto. Tumeshatoa maelekezo kwa Meneja wa Mkoa wa manyara kuhakikisha kwamba mkandarasi anarudi. Hata kama hajaanza, lakini ana wajibu wa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inapitika kipindi chote na hasa katika kipindi hiki. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati tunatafuta fedha ya kumlipa, lakini ile kazi ya kuhakikisha watu wanapita aifanye kwa sababu ni wajibu kimkataba. Ahsante.
Name
Flatei Gregory Massay
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Njombe – Kibena – Madeke - Lupembe kuelekea Mkoa wa Morogoro?
Supplementary Question 5
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaishukuru Serikali kwa kukubali kujenga Barabara ya Haydom kwenda Labay na kwa kuwa mkandarasi yuko site na hawajamlipa fedha. Je, ni lini watamlipa fedha ili barabara hiyo ianze kujengwa?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu mengine. Wakandarasi wote ambao wameshakwenda site sisi kama Wizara tumeshapeleka hati za madai yao Wizara ya Fedha na wametuhakikishia kwamba muda si mrefu wakandarasi hao watalipwa malipo yao ili waweze kuendelea na kazi ikiwepo na hiyo barabara ya Mheshimiwa Flatei kama alivyouliza. Kwa hiyo, tuna uhakika wakandarasi watalipwa, lakini cha muhimu mkandarasi aendelee kufanyia matengenezo hiyo barabara katika kipindi hiki cha mvua.
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Njombe – Kibena – Madeke - Lupembe kuelekea Mkoa wa Morogoro?
Supplementary Question 6
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Kwa Sadala – Kwale – Lemira kilometa15 Serikali iliahidi mwaka wa fedha huu kufanya upembuzi yakinifu. Ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara hii ya Kwa Sadala – Kwale – Lemira kilometa 15? Ahsante.
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tuliahidi na tunachofanya sasa hivi kwa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Hai, ni kwamba tunavyoongea sasa hivi kazi tunayofanya mwaka huu barabara ilikuwa haijasanifiwa, ni kuifanyia usanifu barabara yote ikiwa ni pamoja na kulijenga lile Daraja la Kikafu Juu ambalo tayari mkandarasi yuko site kulijenga hilo Daraja.
Name
Mrisho Mashaka Gambo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Njombe – Kibena – Madeke - Lupembe kuelekea Mkoa wa Morogoro?
Supplementary Question 7
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Arusha – Kibaya – Kongwa ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami na hasa ukizingatia kwamba Arusha tutanufaika na barabara ya njia nne kutoka Kona ya Mbauda mpaka Kwa Mrombo ambapo tunakwenda kujenga stendi ya kisasa lakini pia na Kona ya Kiserian hadi by pass kule kwenda Fun Retreat. Ujenzi wake utaanza lini?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge wa Arusha Mjini ilikuwa ni sehemu ya zile barabara za EPC+F. Baada ya kufanya mabadiliko ya ujenzi barabara hii itajengwa kilometa70 kuanzia Arusha na barabara zote hizo alizozitaja ni sehemu ya ujenzi wa hiyo Barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyoongea tarehe 11 Februari tulisaini mikataba kwa sababu wakandarasi wa awali ndiyo haohao ambao watajenga. Kwa hiyo, tunategemea na hasa tukijua barabara hizo pia zitahudumia sana mashindano ya AFCON. Tuko makini tutakapokuwa tumekamilisha taratibu zote barabara hiyo itaanza kujengwa kipindi hiki cha mwaka wa fedha. Ahsante.
Name
Seif Khamis Said Gulamali
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manonga
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Njombe – Kibena – Madeke - Lupembe kuelekea Mkoa wa Morogoro?
Supplementary Question 8
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, niwapongeze Simba kwa kufuata nyayo za Yanga; hongereni bado hamjafikia fainali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa niweze kumuuliza swali la nyongeza Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa sasa ni miezi mtano toka tupate mkandarasi wa kujenga Barabara ya Choma – Ziba – Mkinga mpaka Puge. Je, ni lini tutasaini mkataba kwa ajili ya kuanza kwa kazi hiyo ya ujenzi? Ninakushukuru sana.
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaposaini mikataba tunakuwa tumefanya mawasiliano ya karibu na tumeshawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha kwa barabara zote ambazo ziko tayari kuzisaini basi tunavyosaini tuwe na uhakika kwamba zinaenda kuanza kujengwa ikiwa ni pamoja na hii barabara ya Mheshimiwa Gulamali ya Choma kwenda Ziba.