Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kavejuru Eliadory Felix
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Primary Question
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda vya kuchakata zao la migomba?
Supplementary Question 1
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imesema itaanzisha kongani ifakapo Julai, 2025, je, programu hii imewekwa kwenye bajeti au Serikali itatumia chanzo gani mahususi kwa ajili ya utekelezaji wa programu hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mpaka sasa kuna hatua gani zilizochukuliwa kuandaa wakulima wa migomba kwa ajili ya kongani?
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Felix Kavejuru kwa kuendelea kufuatilia kuhusiana na uongezaji wathamani mazao ya kilimo katika Mkoa wa Kigoma na hasa Jimbo la Buhigwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kongani tunazozianzisha hapa nchini maeneo yote zinawekwa kwenye bajeti na hili liko kwenye mpango wa bajeti ambayo itasomwa hapa kwa ajili ya mwakani 2025/2026 ambayo Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Selemani Jafo atawasilisha katika Bunge lako Tukufu. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, Serikali tumejipanga na ndiyo maana tumesema tutaanza kutekeleza kwa mwaka huo 2025/2026 kwenda 2030.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hatua ambazo tumechukua kuwaanza wakulima na wadau wote katika hatua za awali. Kwanza kama nilivyosema ndizi au migomba ni zao ambazo linalimwa Tanzania nzima na maeneo mengine. Kupitia Wizara ya Kilimo wamewezeshwa pembejeo na utaalam kupitia Maafisa Ugani ili kuhakikisha wanazalisha kwa tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tayari utaratibu huu tunao kwenye mazao mengine kwa mfano katika Mkoa wa Kigoma kwenye zao la chikichi tayari kuna kongani hizo na zimeonesha kufanya vizuri sana pale Kigoma na yeye ni shahidi. Kwa hiyo, tutatumia module hiyo hiyo kuhakikisha na kwenye zao la ndizi na migomba tunafanya hivyo. Ninakushukuru.
Name
Jonas Van Zeeland
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mvomero
Primary Question
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda vya kuchakata zao la migomba?
Supplementary Question 2
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Mgeta ina wakulima wa mbogamboga na wakulima wa matunda, lakini wamekuwa wakipata hasara kila mwaka kwa sababu ya kukosa soko la uhakika. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kujenga kiwanda kidogo cha kusindika matunda katika Tarafa ya Mgeta? Ahsante. (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri, lakini hasa kwenye sekta hii ya matunda na mbogamboga ambayo maeneo mengi hapa Tanzania tunazalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaongeza thamani ya mazao yote ya kilimo ikiwemo haya ya matunda na mbogamboga. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Tarafa ya Mgeta nao watanufaika na mpango huu na kama nilivyosema tunaanza kongani katika mikoa yote na halmashauri zote ili kuhakikisha kila kwenye mazao haya tunapunguza upotevu baada ya mavuno (post-harvest loses). Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge hata kule Mgeta nako tutafika na tutawasiliana ili tuone namna gani ya kuvutia wawekezaji waje katika jimbo lako. Ninakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved